Kiswahili Paper 3 Pre Mock Questions and Answers - Mokasa I Joint Examination July 2021

Share via Whatsapp

Maagizo

  1. Andika jina lako na nambari yako ya mtihani katika nafasi ulizoachiwa hapo juu.
  2. Tia sahihi yako kisha uandike tarehe ya mtihani katika nafasi ulizoachiwa hapo juu.
  3. Jibu maswali manne pekee.
  4. Swali la kwanza ni la lazima.
  5. Maswali hayo mengine yachaguliwe kutoka sehemu nne zilizobaki: yaani; Riwaya, Ushairi  na Fasihi simulizi
  6. Majibu yote lazima yaandikwe kwa lugha ya Kiswahili.
  7. Majibu yote sharti yaandikwe kwenye nafasi ulizoachiwa katika kijitabu hiki cha maswali.
  8. Karatasi hii ina kurasa 5 zilizopigwa chapa.
  9. Watahiniwa ni lazima wahakikishe kwamba kurasa zote za karatasi hii zimepigwa chapa sawasawa na kuwa maswali yote yamo.

Kwa matumizi ya mtahini pekee

Swali

Upeo

Alama

1

20

 

2

20

 

3

20

 

4

20

 

5

20

 

6

20

 

7

20

 

Jumla

80

 


MASWALI

SEHEMU A: RIWAYA
Asumpta Matei: Chozi la Heri

  1. Lazima
    Kipi kinachowavuta raia kuhamia ughaibuni? Angeuliza nafsi yake pale ambapo mzigo wa simanzi na ukiwa ulipokilemea kifua chake.  Je, ni huo mshahara mnono unaowageuza kuwa watumwa wa kufanya kazi kidindia ati kwa kudai kuwa nchi za ughaibuni ni twenty-four-hour economies?
    1. Eleza muktadha wa dondoo hili  (Alama 4)
    2. Huku ukitolea mifano maridhawa, fafanua mbinu nne za kimtindo zinazojitikeza katika dondoo hili (Alama 4)
    3. Eleza changamoto inayomkumba msemaji katika dondoo hili(Alama 2)
    4. Fafanua jinsi maudhui yanayojitokeza katika dondoo hili yameshughulikiwa kwingineko riwayani. (Alama 4)
    5. Fafanua umuhimu wa mandhari katika kuijenga riwaya hii kwa kurejelea Msitu wa Mamba (Alama 8)

SEHEMU B : TAMTHILIA
Pauline Kea : Kigogo
Jibu swali la 2 au la 3

  1. Ama ale hizo falsafa zake! Udongo haubishani na mfinyanzi. 
    1. Eleza muktadha wa dondoo hili (Alama 4)
    2. Tambua na ueleze tamathali mbili za usemi katika dondoo hili (Alama 4)
    3. Eleza umuhimu wa msemaji katika kuijenga tamthilia hii kwa hoja zozote nne (Alama 4)
    4. Eleza maudhui manne yanayojitokeza katika dondoo hili (Alama 8)
  2.                                      
    1. Jimbo la Sagamoyo limetawaliwa na uozo mwingi. Tetea kauli hii. (Alama 10)
    2. Eleza mbinu zifuatazo za kimtindo jinsi zilivyotumika katika tamthilia ya Kigogo :
      1. Kinaya (Alama 5)
      2. Jazanda (Alama 5)

SEHEMU C : USHAIRI
Jibu swali la 4 au la 5

  1. Soma shairi linalofuata kisha ujibu maswali:

Nakumbuka kwa dhiki Mto Monyara
Tuliochelea kukaribia kingo zake
Tukatulia kwanza; ukakamavu kujihamia
Kwa kunyenyekea wingi wa yake maji
Yaliyojiendea utadhani yamesimama.

Ni katika mto huu
Ambapo samaki wakubwa tulivua
Maguo kuyatakasa japo kwa kuunyemelea

Na walevi stadi wakachelea kuuvuka
Ulipofura na kupita kwa kiburi
Kwa kushiba maji yake
Yaliyofanya mawimbi madogo.

Ni hapa ambapo marehemu nyanya
Mkono alinishika na njia kuniongoza
Juu la ulalo wa miti
Vikapu vyetu hewani vikielea;
Mimi nikishika change kwa mkono mmoja
Naye akikiachilia chake kujishikisha kichwani
Masafa baina yetu na mtambo
Uliokwenda kwa nguvu za maji
Tuliyapunguza kwa kila hatua tulopiga.

Ni katika mto huu ambapo
Samaki tuliowavua tuliwapasua na kuwasafisha
Na hivyo kuuficha umaskini wetu
Ulotuzuia kununua mnofu wa bucha
Ni hapa ambapo wanawake walifika
Mawe ya kusagia kupata
Ni katika mtu huu ambapo
Waumini walifika kutakaswa kwa ubatizo
Baada ya ulevi, usinzi na kufuru nyinginezo.

Ni hapa ambapo ilisimuliwa kuwa
Hata wachawi walifika kufanya vitimbi vyao
Baada ya utawala wa jua kumezwa na nguvu za giza
Sasa Monyara niloijua haipo tena
Zimebaki kingo zilizokaukiana
Kama uso wa mrembo aliyekosa mafuta
Siku ayami.

Mti huu ambapo pembeni mwake
Watoto walipashwa tohara
Maji yake yakishangia, umekonda
Na mbavu zake nje kutoa
Na sasa vitoto vikembe vinazikanyaga
Vikijiendea zao kusaga mahindi
Juu mlimani
Katika mtambo wa Kizungu
Usioisha kulalamika
Nao wanawake hawaji tena
Kutafuta mawe ya kusagia wimbi
Imebaki njia ya walevi warejeao nyumbani
Nayo miti iliyosimama wima ukingoni
Iliisha kuanguka kwa kuleweshwa na pumzi za walevi
Wasioisha kupita hapa. 

Maswali: 

  1.                          
    1. Hili ni shairi la aina gani? (alama 1)
    2. Thibitisha jibu lako katika (i)  (alama 2)
  2. Bainisha tamathali tatu za usemi zilizotumiwa katika shairi hili. (alama 3)
  3. Linganisha sifa za zamani na za sasa za Mto Monyara. (alama 3)
  4. Andika mifano miwili ya mistari mishata katika shairi hili.  (alama 2)
  5. Eleza muundo wa shairi hili.   (alama 4)
  6. Huku ukitolea mifano, bainisha uhuru wa kishairi zilizotumiwa na mshairi. (alama 2)
  7. Bainisha nafsineni katika shairi hili.(alama 1)
  8. Fafanua toni ya shairi hili. (alama 2)
  1. Soma shairi lifuatalo kisha ujibu maswali

Tusitake kusimama, bila kwanza kutambaa,
Au dede kuwa hima, kabula hatujakaa,
Tutakapo kuchutama, kuinama inafaa,
Tujihimu kujinyima, makubwa kutoyavaa.

Tusitake kuenenda, guu lisipokomaa,
Tujizonge na mikanda, inapochagiza njaa,
Na mazuri tukipenda, ni lazima kuyandaa,
Tujiase kujipinda, kujepusha na balaa.

Tusitake uvulana, au sifa kuzagaa,
Tushikiye nyonga sana, tunuiyapo kupaa,
Kama uwezo hapana, tutolee dagaa,
Tujiase hicho kina, maji yanapojaa.

Tusitake vya wenzetu, walochuma kwa hadaa,
Wanaofyatua vitu, na kisha vikosambaa,
Uwezo hatuna katu, umaskini fazaa,
Tujihimu kula vyetu, siendekeze tamaa.

Mtaka kuiga watu, hufata kubwa rubaa,
Vyao vijaile kwetu, vifaa vingi vifaa,
Tunamezwa na machatu, tusibakishe dhiraa,
Tujihimu kilo chetu, hata kama twapagaa.

(Mohamed, S.A)

Maswali:

  1. Eleza ujumbe wa mshairi katika shairi hili. (alama 5)
  2. Ainisha shairi hili kwa kuzingatia vigezo vifuatavyo:  (alama 4)
    1. Idadi ya vipande katika kila mshororo
    2. Idadi ya mishororo katika kila ubeti
    3. Mpangilio wa maneno katika kila ubeti
    4. Mpangilio wa vina katika beti
  3. Andika ubeti wa tano kwa lugha nathari.(alama 4)
  4. Andika aina mbili za urudiaji zilizotumiwa katika shairi hili. (alama 2)
  5. Bainisha aina tatu za uhuru wa kishairi zilizotumiwa katika shairi hili. (alama 4)
  6. Eleza maana ya maneno yafuatayo jinsi yalivyotumiwa: (alama 2)
    1. Makubwa kutoyavaa
    2. Tushikiye nyonga

SEHEMU D : HADITHI FUPI
K. Walibora na S.A. Mohamed: Damu Nyeusi na Hadithi Nyingine
Shibe Inatumaliza : Salma Omar Hamad

  1. “ Kwa hakika … wanajituma na kujitutumua kwa uzalendo wa taifa lao.”
    1. Eleza muktadha wa dondoo hili. (alama 4)
    2. Taja na kufafanua sifa zozote nne za warejelewa kwenye dondoo hili. (alama 4)
    3. Onyesha kinaya kinachojitokeza kwenye dondoo hili ukirejelea hadithi nzima. (alama 12)

Mame Bakari: Mohammed Khelef Ghassany

  1. “Hapo tena ilimjia ile picha chafu ambayo haijabanduka mpaka leo tokea wakati ule ilipoanza. Aliendelea kuliona lile janadume asilolijua likimvamia na kumbaka ghafla.Kisha likambamiza ardhini na ardhi ikashuhudia ukatili na udhalimu ule. Hadi sasa maskioni mwake anasikia miguno na mingurumo ya lile dubwana la janadume.”
    1. Fafnua toni inayojitokeza kwenye dondoo hili. (alama 2)
    2. Huku ukitoa mifano, bainisha mbinu tatu za kimtindo zinazojitokeza kwenye dondoo.  (alama 6)
    3. Onyesha athari za ukatili uliotajwa kwenye dondoo. (alama 12)

SEHEMU E : FASIHI SIMULIZI

Kijiji chavuma vishindo,
Vya ngoma na nyimbo.

Kwenye vilima vya kata,
Na mabonde kuliko na mito,
Wamama wanalitafuna,
Watoto na vijana wanaliimba, jina,
Jina la nguli Amali wa Jamali. Jamadali kamili.

Ukoo wake wa mashujaa,
Babuze walisifika sana,
Mikuki na mishale walifua,
Kuihami jamii na riaka,
Na hata magao ya kujisitiri, pindi lijapo pambano.

Leo yeye atamba,
Shujaa wa nguvu za tembo,
Mwamba anayepigana bila silaha yoyote,
Angurumapo mahasimu wanazirai, wanavaa lebasi ya woga hasa,
Wasiwasi unawakumbatia.
Angurumapo simba mcheza nani?
Anapotisha Amali wa Jamali atasimama nani?

Zawadi za kole za nazi,
Na mashuke ya mtama,
Zamiminika kwake kutoka kusini na kaskazini,
Kwa kujuhudi za kuwarejesha mitamba na mafahari,
Kutoka mbali walikotekwa,
Mazizi sasa yana uhai,
Miroromo sasa inasikika tena.

Wengine wanaleta vishazi vya samaki,
Kumtunuku,
Huyu mja mwenye nemsi zisizo na ndweo.

Akida wetu,
Atamvisha taji la ngozi ya duma,
Yenye kipembe cha kifaru,
Atamvisha nguo ya ngozi ya simba.

Maswali:

  1. Tambua kipera cha utungo huu na utoe sababu ya jibu lako. (Al 2)
  2. Ni sifa gani hukibainisha kipera ulichotaja hapo juu? (Al 5)
  3. Eleza dhima za kipera hiki katika jamii. (Al 5)
  4. Jamii iliyoakisiwa kwenye utungo huu huendeleza shughuli gani za kiuchumi? (Al 4)
  5. Fafanua mtindo katika kifungu hiki. (Al 4)


MOKASA MWONGOZO

102/3: Mwongozo wa usahihishaji

  1. Eleza muktadha wa dondoo hili  (Alama 4)
    Haya ni mawazo ya Kiriri akiwa nyumbani kwake kabla ya kifo chake. Alikuwa anasumbuka kwa kuachwa na jamaa yake. Alikuwa ameachwa na mkewe ,Annette na wanawe ambao sasa walikuwa ughaibuni na walikataa kurudi nchini alikokuwa Kiriri hata baada yake kuwarai. 
  2. Huku ukitolea mifano maridhawa, fafanua mbinu nne za kifasihi zinazojitikeza katika dondoo hili  (Alama 4)
    Maswali ya balagha/mubalagha -Kipi kinachowavuta kuhamia ughaibuni?
                -.....nchi za ughaibuni ni    twenty-four-hour economies?
    Sitiari -mzigo wa simanzi kurejelea huzuni aliokuwa nao Kiriri kwa kuachwa na jamaa yake. 
    Mshahara mnono-kurejelea mshahara mkubwa. 
    Uhaishaji/tashihisi- mzigo wa simanzi ulipokilemea kifua chake. 
    Kuchanganya ndimi- twenty-four-hour economies.  (4×1=4)
  3. Eleza changamoto inayomkumba msemaji katika dondoo hili (Alama 2)
    Ukiwa/upweke- Kiriri aliachwa na mkewe Annette na wanawe ambao sasa walikuwa ughaibuni.
  4. Fafanua jinsi maudhui yanayojitokeza katika dondoo hili yameshughulikiwa kwingineko riwayani. (Alama 4)
    Maudhui ya upweke/ukiwa
    • Lunga anaachwa na mkewe
    • Umu anachwa na kijakazi 
    • Umu anaachwa na watoto wao wakembe ;Dick na mwaliko waliouzwa na kijakazi. 
    • Umu anaachwa na babake,Lunga anapoaga dunia hata baada ya Mamake kumwacha babake alipokuwa akilala. 
    • Ridhaa anaachwa na mwanawe Tila,Mkewe ,Terry na pia mkaza mwanawe na mjukuwe. 
    • Selume anaondoka nyumbani kwa katika Msitu wa Heri baada ya kushutumiwa na jamii ya mumewe. 
    • Mwangemi anawapoteza Mkewe na mwanawe. Hata anapokuwa katika nyumba yake kando ya bahari,anawawaza.   (Hoja 4×1)

Tathmini majibu 

  1. Fafanua umuhimu wa mandhari katika kuijenga riwaya hii kwa kurejelea Msitu wa Mamba (Alama 8)
    • Ukosefu wa vyoo
    • Ukosefu wa malazi/malazi
    • Ukosefu wa chakula
    • Ukosefu wa maji safi
    • Upweke
    • Magonjwa kama vile kipindupindu
    • Uharibifu wa mazingira(Lunga na wakaaji wengine katika Msitu wa Mamba kukata miti ili kuendeleza kilimo. 
    • Ukimbizi wa ndani kwa ndani. 

Hakiki majibu ya mwanafunzi. Awianishe hoja hizo na mandhari. (Hoja 4×1)

KIGOGO
Ama ale hizo falsafa zake! Udongo haubishani na mfinyanzi. 

  1. Eleza muktadha wa dondoo hili (Alama 4)
  2. Tambua na ueleze tamathali mbili za usemi katika dondoo hili (Alama 4)
  3. Eleza umuhimu wa msemaji katika kuijenga tamthilia hii kwa hoja zozote nne (Alama 4)
  4. Eleza maudhui manne yanayojitokeza katika dondoo hili (Alama 8)

MWONGOZO

  1. Eleza muktadha wa dondoo hili (Alama 4)
    • Msemaji-Boza
    • Msemewa- Kombe 
    • Mahali- Soko la Chapakazi
    • Kenga alikuwa amewaletea keki ya uhuru ambayo Sudi alikataa kula hali. 
  2. Tambua na ueleze tamadhali mbili za usemi katika dondoo hili (Alama 4)
    • Nidaa - ama ale hizo falsafa zake !
    • Jazanda -udongo haubishani na mfinyanzi kwa kurejelea kuwa Sudi ni mdogo tu hawezi kubishani na Kigogo. 
  3. Eleza umuhimu wa msemaji katika kuijenga tamthilia hii kwa hoja zozote nne (Alama 4)
    • Ametumiwa Kuonyesha watu wenye tamaa. Anamwunga mkono Majoka kwa lengo la kujifaidi binafsi. Mkewe amepata kandarasi ya kutoka keki. 
    • Ni kielelezo cha vibaraka/vikaragosi. Anaunga mkono utawala mbaya ya Majoka. Anakula keki ya uhuru na kushtumu Sudi kwa kukataa
    • Ametumiwa Kuonyesha watu wapyaro. Anasema Sudi ale falsafa zake. 
    • Ni kielelezo cha watu wenye mabezo/dharau. Anasema Sudi ale falsafa zake. 
    • Ametumiwa Kuonyesha watu wenye vitisho kwa wasiounga mkono viongozi wabaya. Anamtisha Sudi kuwa kupinga Kigogo husababisha maangamizi. 
    • Ametumiwa Kuonyesha watu wapenda anasa. Anakunywa pombe haramu kwa Mamapima. 
    • Ametumiwa kufichua ufisadi. Anarejelea kuwa mkewe alipewa kandarasi ya kuoka keki kwa sababu ya urafiki wake na Husda. 
    • Ametumiwa Kuonyesha mume mwenye mapuuza. Mkewe ana uhusiano wa kimapenzi na Ngurumo na ndipo akapata kandarasi ya kuoka keki. 
    • Ametumiwa Kuonyesha watu wanaowakejeli wanapinga uongozi mbaya. Anawakejeli Sudi na Tiny wanaompinga Majoka na uongozi wake mbaya. 
    • Ametumiwa kumjenga Sudi kama mchongaji stadi. Uchongaji wake ni mbaya ikilinganishwa na Sudi. 
  4. Eleza maudhui manne yanayojitokeza katika dondoo hili (Alama 8)
    • Vitisho. Boza anamtisha Sudi kuwa akimpinga Kigogo ataangamizwa. 
    • Ukaragosi/ubaraka- Boza anaunga mkono utawala wa Majoka. Anakula keki ya uhuru. 
    • Ufisadi. Mkewe Boza anapata kandarasi ya kuoka keki kwa urafiki wake na Husda. 
    • Mabezo/madharau. Boza anamkejeli Sudi kuwa ale falsafa zake. 
    • Udikteta/uimla. Boza anasema kuwa anayempinga Majoka ataangamizwa. 
    • Ubadhirifu wa mali ya umma. Boza anasema Sudi ale falsafa zake kwa sababu yeye mwenyewe alikula keki iliyookwa na mkewe kwa kutumia mali yake ya umma.  

3.a)Jimbo la Sagamoyo limetawaliwa na uozo mwingi. Tetea kauli hii. (Alama 10)

  • Viongozi huangaisha wanyonge, Ashua anasema,"...na kuhangaishwa na wenye nguvu ndio hewa tunayopumua huko." (uk 2)
  • Wachochole hutumikizwa na viongozi, Kombe, Boza na Sudi wanafanya kazi ya kuchonga vinyago vya mashujaa kwa ajili ya sherehe za uhuru.
  • Viongozi hawajawajibika, kazi yao ni kukusanya tu kodi.Ni jukumu la viongozi kuhakikisha kuwa soko ni safi lakini hawajawajibika kulisafisha. Licha ya wananchi kutoa kodi,soko ni chafu.(uk 2)
  • Viongozi kutangaza kipindi kirefu cha kusheherekea uhuru ni ishara ya uongozi mbaya. Mashujaa wanaenziwa kwa kipindi kirefu ilhali mambo ya kimsingi hayajazingatiwa.Wanasagamoyo wana matakwa mengi kuliko kipindi kirefu cha kusherehekea uhuru.
  • Majoka anafadhili mradi usio na msingi wa kuchonga vinyago huku watu wakiwa na njaa na wao ndio watalipia mradi huo.
  • Viongozi hushawishi wananchi kwa ahadi ili wawaunge mkono. Sudi anashawishiwa na Kenga kuchonga kinyago ili apate malipo mazuri; kuwa mradi huo utabadilisha maisha yake na jina lake lishamiri. Pia atapata tuzo nyingi na likizo ya mwezi mzima ughaibuni na familia yake (uk 11)
  • Aidha viongozi hutumia zawadi kufumba wananchi kuwa wanawajali na kujali hali zao.Kenga anawaletea Sudi, Boza na kombe keki ya uhuru.
  • Kulingana na Sudi, hayo ni makombo na keki kubwa imeliwa kwingineko.
  • Viongozi hawalindi usalama wa wananchi, wananchi wanaishi kwa hofu. Ashua anahofia usalama wao kuwa huenda wakashambuliwa.(uk 15)
  • Migomo inayotokea Sagamoyo na maandamani ni kwa sababu ya uongozi mbaya.Wauguzi wanagoma na pia walimu wakidai haki zao. Wafanyakazi wananyanyaswa.
  • Majoka hajali maslahi ya wanasagamoyo. Anafunga soko ambalo wananchi wanategemea na kupandisha bei ya chakula. Uchumi Sagamoyo unasorota kutokana na soko kufungwa, watu hawana mahali pa kuuzia bidhaa zao.
  • Majoka anafungulia biashara ya ukataji miti bila kujali hali ya anga Sagamoyo, hasara ni kwa maskinii, viongozi wamejichimbia visima. Mito na maziwa yanakauka na mvua isiponyesha, hata maji ya kunywa yatatoka ng`ambo.
  • Majoka hajali kuhusu kifo cha Ngurumo licha ya kuwa mfuasi wake. Anaagiza Ngurumo azikwe kabla ya jua kutua (uk 69)
  • Viongozi hupanga njama ili kuangamiza wapinzani wao;
  • Majoka na Kenga wanapanga njama ya kumtia Ashua ndani.Wanapanga aitwe ofisini mwa Majoka kisha Husda aitwe ili wafumaniane. Ashua anazingiziwa kuzua sogo katika ofisi ya serikali na kutiwa ndani. Husda anafunguliwa baada ya nusu saa.
  • Kifo cha Jabali kilipangwa. Jabali alikuwa mpinzani wa Majoka mwenye wafuasi wengi. Akapangiwa ajali barabarani kisha wafuasi wake wakazimwa na kumfuata jongomeo, chama chake cha mwenge kilimfuata ahera.
  • Tunu anapanga kufanya uchunguzi kuhusu chanzo cha ajali ya Jabali. Majoka anapopata habari hizi, anapanga kuzima uchunguzi huo.
  • Kenga na Majoka wanapanga kuondoa chatu mmoja. Chatu hapa wanarejelea Sudi au Tunu kwa kuwa ndio wanaoongoza mapinduzi. Wanahofia kutolewa uongozini na ili kuzuia hali hii, wanapanga kumwondoa mmoja wao."...chatu mmoja atolewe kafara ili watu wajue usalama upo, wakereketwa waachwe katika hali ya taharuki"
  • Majoka anapanga njama Tunu auliwe, anaumizwa mfupa wa muundi nia yake ikiwa ni kumkomesha asimpinge. Majoka anatumia polisi wake kutekeleza ukatili huo.
  • Katika hotuba ya Tunu anayowahutubia waandamanaji, Sagamoyo kuna uongozi mbaya.Anasema kuwa; pesa za kusafisha soko zimefujwa, soko linafungwa badala ya kusafishwa, haki za wauzaji zimekiukwa.
    1. Viongozi hawasikilizi matakwa ya wananchi. Majoka hana wakati wa kuwasikiliza waandamanaji. Hataki kujua chanzo cha maandamano wala suluhu lake.
    2. Majoka anadhibiti vyombo vya habari Sagamoyo, habari zinazopeperushwa katika runinga ya Mzalendo na picha za watu wengi sokoni wakiongozwa na Tunu zinamfanya Majoka kufunga runinga hiyo ya mzalendo.
  • Viongozi hutumia vitisho. Majoka anatishia Chopi kumwaga unga wake kwa vile polisi hawakuwatawanya waandamanaji, wanasagamoyo wanatishiwa kuhama Sagamoyo kwa juwa sio kwao, wanarushiwa vijikaratasi. (uk 52)
  • Majoka anatumia askari kutawanya raia badala ya kulinda uhuru wao.
  • Viongozi ni waongo. Majoka anatumia uongo ili kumteka Tunu. Anamhaidi jambo la kifahari, kumwoza Ngao Junior akirudi kutoka ng`ambo. viongozi hutendea wananchi ukatili, watu wanaotiwa jela huchapwa na haki zao hukiukwa. Ashua ana majeraha kutokana na kichapo.
  • Viongozi hupanga uvamizi, Sudi anavamiwa (uk 54)
  • Viongozi wamekiuka sheria. Mamapima anadai kuwa anauza pombe haramu kwa kibali kutoka serikali ya Majoka. Ni hatia kuuza pombe haramu lakini viongozi huvunja sheria na kuwapa wauzaji kibali. (uk 61)
  • Sagamoyo hata viongozi hawafuati katiba."...huku ni Sagamoyo, serikali na katiba ni mambo mawili tofauti." (uk 61)
  • Uongozi wa Majoka una ubaguzi, unafaudi wachache tu, wanaomuunga mkono. Asiya bibiye Boza anapata mradi wa kuoka keki mwa vile anauunga uongozi wa Majoka Mkono.
  • Viongozi hujulimbikizia mali. Kuna hoteli ya kifahari Sagamoyo, Majoka and Majoka modern resort.
  • Viongozi ni wanafiki. Majoka amepanga kuficha maovu yake mbele ya wageni. Ukumbi unapambwa na kurembeshwa huku kukiwa na maovu mengi Sagamoyo. Kuna mauaji, unyakuzi, njaa,maziara yamejaa Sagamoyo.
    (HOJA 10)
    KADIRI MAJIBU YA MWANAFUNZI

b) Eleza mbinu zifuatazo za kimtindo jinsi zilivyotumika katika tamthilia ya Kigogo :

  1. Kinaya (Alama 5)
    • Habari zinazotolewa na mjumbe katika rununu ni za kinaya, kuwa wanasagamoyo wasirudishe maendeleo nyuma bali wafurahie ufanisi ambao umepatikana katika kipindi cha miaka tisini baada ya uhuru.
      Ujumbe huu ni kinaya kwa vile Sagamoyo hakuna maendeleo wala ufanisi. Watu wana njaa na wanakosa mambo ya kimsingi kama vile maji, elimu na matakwa mengine mengi.
    • Boza anadai kuwa kulipa kodi ni kujenga nchi na kujitegemea. Kauli hii ni kinaya kwa vile kodi wanayolipa wanasagamoyo haitumiki kujenga nchi kwa vyovyote vile.
    • Sudi anasema kuwa katika kipindi cha mwezi mzima wa uhuru wale mali walizochuna kwa miaka sitini. Ni kinaya kwa kuwa hakuna walichovuna, viongozi hujilimbikizia mali.
    • Boza anamwambia Sudi kuwa wanatia doa kwa kila jambo nzuri. Ni kinaya kwa vile hakuna mambo mazuri ambayo Majoka amefanya Sagamoyo. (uk5)
    • Wanasagamoyo kusheherekea miaka sitini ya uhuru ni kinaya kwani hakuna cha muhimu kusheherekewa, hakuna maendeleo Sagamoyo.
    • Boza anadai kuwa kinyago chake chapendeza na kufanana na shujaa Marara Bin Ngao, ni kinaya kwani kinyago hicho hakifanani na shujaa huyo.
    • Majoka kudai kuwa anamheshimu sudi ni kinaya. Majoka hana heshima kwa raia wake, nia yake ni kutaka Sudi amchongee kinyago. (uk13)
    • Kenga kumwambia Sudi kuwa ipo siku atamtafuta mzee Majoka ni kinaya kwani Sudi hana haja naye.
    • Majoka kudai kuwa takataka za soko zitaaribu sifa nzuri za jimbo la Sagamoyo ni kinaya kwa vile hakuna sifa nzuri Sagamoyo. Viongozi wanaendeleza maovu na hata kupanga mauaji.
    • Kauli ya Husda kuwa Ashua ni kimada wa Majoka ni kinaya kwa vile Ashua hana nia yoyote na Majoka. Amefika kwake kuomba msaada.
    • Ni kinaya kwa polisi Sagamoyo kutawanya waandamanaji. Polisi wanapaswa kulinda na kutetea haki za wananchi.
    • Majoka kusema kuwa Sagamoyo wanajiweza ni kinaya. Watu wana matakwa mengi, ni maskini, wana njaa na hata kupata ufadhili kitoka nje kwa miradi isiyo muhimu.
    • Ni kinaya Kenga anapomwambia Majoka aache moyo wa huruma, kwa sababu Majoka hana hata chembe cha huruma. Anapanga mauaji na kunyanyasa raia.
    • Majoka anaposema kuwa juhudi za Tunu kuandaa migomo hazitamfikisha mahali ni kinaya kwa vile Tunu wanafanikiwa katika maandamano yao na hata kuungwa mkono na wengi.
    • Ni kinaya kwa Ashua kumwambia Sudi kuwa ni kosa lake kutiwa ndani. Kosa ni la Majoka na njama yake ya kutaka kuchongewa kinyago.
    • Ashua anasema kuwa katika jela kuna amani na amechoshwa na Sudi. Ni kinaya kwani Ashua anapata maumivu akiwa jelani.
    • Uvumi unaoenea kuwa Sudi na Ashua ndio wanaowinda roho ya Tunu ni kinaya kwani wote hawa ni wanamapinduzi wanaopigania haki Sagamoyo.
    • Madai ya Ngurumo ni kinaya kuwa tangu soko kufungwa Sagamoyo ni pazuri mno. Eti mauzo ni maradufu ilihali watu hawana mahali pa kuuzia bidhaa zao, kifungwa kwa soko kunawaangaisha raia hata zaidi.
    • Ngurumo kusema kuwa pombe ni starehe ni kinaya kwani watu wanaangamia kutokana na pombe, wengine kuwa vipofu.
    • Watu wengi wanatarajiwa kufika katika uwanja wa ikulu ya Majoka kusherehekea uhuru siku ya sherehe lakini ni kinaya kwa kuwa ni watu kumi tu ambao wanafika
  2. Jazanda (Alama 5)
    • Kinyago cha shujaa anachochonga Sudi kwamba shujaa huyo ni mkubwa kuliko jina lake na urembo wa shujaa huyo ni bora zaidi. Shujaa anayerejelewa hapa ni Tunu, yale ambayo anatendea Sagamoyo ni makuu kuliko jina lake, kutetea haki za wanyonge. (uk10)
    • Husda anamwambia Ashua kuwa hawezi kumtoa bonge kinywani hivi hivi. Bonge ni Majoka bwanake Husda kuwa Ashua hawezi kumnyanganya bwana.
    • Husda kumwita Majoka pwagu, pwagu ni mwizi na Majoka amewaibia wanasagamoyo; ananyakua ardhi, anaiba kodi na kuwalaghai wanasagamoyo. (uk27)
    • Husda anamwambia Ashua kuwa ameshindwa kufuga kuku na kanga hatamweza. Kuku ni mumewe Sudi, na Kanga ni Majoka, kwamba Ashua ameshindwa kumtunza Sudi na Majoka hampati. (uk28)
    • Tunu kuwekewa vidhibitimwendo ni kukomeshwa au kuwekewa vikwazo ili afe moyo kutetea haki za wanasagamoyo.
    • Majoka anasema kuwa hatatumia bomu kuulia mbu. Anamrejelea Tunu kuwa mbu kunaanisha hatatumia nguvu nyingi kumwangamiza. (uk35)
    • Majoka anasema ili kuongoza Sagamoyo ni lazima uwe na ngozi ngumu, kumaanisha ni lazima uwe mkali na mwenye nguvu.
    • Jukwaa kupakwa rangi kwa ajili ya sherehe ya uhuru ni kufunika uozo ulio Sagamoyo.
    • Majoka anaposema salamu zinamgoja Sudi kwake, salamu ni Ashua mkewe aliyendani ya jela.
    • Majoka anamshauri Sudi anawe mikono iwapo anataka kula na watu wazima. Kunawa mikono ni kukubali kuchonga kinyago ndiposa Ashua mkewe aachiliwe.
    • Chopi anamwambia Sudi iwapo shamba limemshinda kulima aseme. Shamba anarejelea Ashua kuwa iwapo Ashua amemshinda kutunza, aseme atunziwe na Majoka.
    • Siafu huwa wengi na si rahisi kuwamaliza. Siafu ni wanasagamoyo ambao ni wengi kuliko Majoka na si rahisi kuwashnda. Hatimaye raia wanamshinda Majoka. (uk52)
    • Tunu anasema kuwa moto umewaka na utateketea wasipouzima. Moto ni harakati za mapinduzi Sagamoyo .Kuteketea nice kumng`oa Majoka mamlakani.
    • Hashima anamwonya Tunu asijipeleke kwenye pango la joka.Pango la joka anarejelea majoka na watu wake ambao ni kati na wauaji.
    • Majoka anadai lazima mtu mmoja atolewe kafara ili watu wajue kuwa kuna usalama Sagamoyo. Chatu anamrejelea Sudi au Tunu ambao ni tishio kwa uongozi wake na kuwatoa kafara ni kuua mmoja wao ili kukomesha maandamano.
    • Majoka anaposema yupo kwenye chombo cha safari ya jongomeo anamaanisha kuwa mwisho wake uko karibu kuondolewa mamlakani.
    • Kinyago cha mke mrembo shujaa anachochonga Sudi kinaashiria Tunu ambaye ni shujaa wa kweli Sagamoyo
    • Husda anafananishwa na chui anayeishi ndani ya ngozi ya kondoo kuashiria kuwa yeye ni mnafiki. Hana mapenzi ya kweli kwa Majoka ila aliolewa naye kwa sababu ya mali.
    • Jazanda ya marubani ambao hawaendesha vyombo vyao vizuri ni viongozi ambao hawaingozi kwa haki. wamejawa na ulaghai na tamaa. (uk80)
    • Babu anamwambia Majoka kuwa hawezi kuelewa mambo kwa vile hajapambua ngozi yake ya zamani. Majoka anapaswa kubadili mienendo yake mbaya.
    • Chombo anachopanda Majoka kinaenda kinyume badala ya kwenda mbele, Majoka hajafanya maendeleo Sagamoyo kwa sababu ya ufisadi na tamaa. (uk81)
    • Kisima kuingiwa na paka maji hayanyweki tena. Sagamoyo ni dhiki tele, hakukaliki kwa kuwa na shida nyingi; soko kufungwa, mauaji kutekelezwa na unyakuzi.

4.

  1.                          
    1. Hili ni shairi la aina gani? (alama 1)
      • Shairi huru
    2. Thibitisha jibu lako katika (i)  (alama 2)
      • Idadi ya mishororo katika kila ubeti inatofautiana
      • Silabi za mwisho katika katika kila mshororo zinatofautiana
      • Idadi ya mizani inatofautiana
  2. Bainisha tamathali tatu za usemi zilizotumiwa katika shairi hili.  (alama 3)
    • Tashibi – zimebaki kingo zilizokaukiana kama uso wa mrembo aliyekosa mafuta kwa siku ayami
    • Tashihisi – ulipofura na kupita kwa kiburi / maji yakishangilia
    • Kisengere nyuma – nakumbuka kwa dhiki mto Monyara
  3. Linganisha sifa za zamani na za sasa za Mto Monyara. (alama 3)
    • Maji yalikuwa mengi zamani ilhali kwa sasa zimebaki kingo zilizokaukiana.
    • Zamani, wanawake walienda kutafuta mawe ya kusagia wimbi ilhali kwa sasa wanawake hawaji tena.
    • Zamani kulikuwa na miti iliyosimama wima ukingoni ilhali kwa sasa miti hiyo iliisha kwa kulewesha pumzi za walevi
  4. Andika mifano miwili ya mistari mishata katika shairi hili. (alama 2)
    • Ni katika mto huu – ambapo samaki wakubwa tulivua
    • Ni hapa ambapo amrehemu nyanya – mkono alinishika na njia kuniongoza
    • Ni katika mto huu – samaki tuliowavua tuliwapasua na kuwasafisha
    • Ni katika mto huu ambapo waumini walifika kutakaswa kwa ubatizo
  5. Eleza muundo wa shairi hili.  (alama 4)
    • Shairi hili lina beti sita
    • Idad ya mishororo katika kila ubeti inatofautiana
    • Idadi ya mizani katika kila mshororo inatofautiana
    • Silabi za mwisho katika kila mshororo zinatofautiana
    • Mshororo wa mwisho katika kila ubeti inatofautina
  6. Huku ukitolea mifano, bainisha uhuru wa kishairi zilizotumiwa na mshairi. (alama 2)
    • Kuboronga sarufi – samaki wakubwa tulivua badala ya tulivua samaki wakubwa
    • Inkisari – tulopiga badala ya tuliopiga
    • Ulotuzuia badala ya uliotuzuia
  7. Bainisha nafsineni katika shairi hili. (alama 1)
    • Mjukuu – ni hapa ambapo marehemu nyanya mkono alinishika na njia kuniongoza.
  8. Fafanua toni ya shairi hili.  (alama 2)
    • Toni ya masikitiko a- anasikitikia Mto Monyara kwa namna ilivyokuwa zamani na hali yake ya sasa

5.

  1. Eleza ujumbe wa mshairi katika shairi hili.  (alama 5)
    • Tusitamani makubwa  / kutoyapapia makubwa
    • Tukipenda mazuri ni lazima kuyaandaa
    • Tusiringe tunaponuia / tunapokusuidia kupaa
    • Tusitake ya wenzetu waliotafuta kwa hadaa
    • Umaskini ni fazaa lakini tujihimu ili tule vyetu wala tusiendekeze tama
  2. Ainisha shairi hili kwa kuzingatia vigezo vifuatavyo:   (alama 4)
    1. Idadi ya vipande katika kila mshororo 
      • Mathnawi – kila mshororo una vipande viwili; ukwapi na utao
    2. Idadi ya mishororo katika kila ubeti
      • Tarbia – kila ubeti ina mishororo minne
    3. Mpangilio wa maneno katika kila ubeti
      • Kikwamba – nenp tusitake limetumiwa mwanzoni mwa beti nne za kwanza   
    4. Mpangilio wa vina katika beti
      • Ukara – vina vya mwisho vinatiririka katika shairi nzima
  3. Andika ubeti wa tano kwa lugha nathari. (alama 4)
    • Anayetaka kuiga watu wengine hufuata rubaa kubwa
    • Vifaa vyao vingi vimejaa kwetu
    • Tnamezwa na machatu kusibakishe dhiraa
    • Tujihimu na kilicho chetu hata kama tunapagaa 
      Iandikwe kwa aya moja
  4. Andika aina mbili za urudiaji zilizotumiwa katika shairi hili.(alama 2)
    • Urudiaji wa sauti – a
    • Urudiaji wa neno – tusitake
  5. Bainisha aina tatu za uhuru wa kishairi zilizotumiwa katika shairi hili.  (alama 3)
    • Tabdila- tunuiyapo badala ya tunuiapo, tushikiye badala ya tushikie
    • Mazida – kuenda badala ya kwenda, kabula badala ya kabla
    • Inkisari – walochuma badala ya waliochuma / walivyovichuma, siendekeze badala ya tusiendekeze, kilo badala ya kilicho, kujepusha badala ya kujiepusha, hufata badala ya hufuata
  6. Eleza maana ya maneno yafuatayo jinsi yalivyotumiwa: (alama 2)
    1. Makubwa kutoyavaa – makubwa kuyatamani / makubwa kutoyapapia
    2. Tushikiye nyonga – turinge / tujivunie

Hadithi Fupi

  1. Shibe Inatumaliza
    1.                                    
      • Haya ni maneno ya msimulizi
      • Ni kuwahusu Sasa na Mbura
      • Hawa walikuwa ni mawaziri wa wizara moja ya Mipango na Mipangilio
      • Msimulizi anawasuta kwa kutowajibika na kuendeleza ufisadi katika wizara waliyokuwa waniendesha.(1x4=4)
  2. Sifa nne za warejelewa
    • Fisadi- kitendo chao cha kupanga foleni mara kadhaa kinaonyesha jinsi wanvyofakamia mali ya umma.
    • Wenye tamaa- wanakaa upenuni wakisubiri awamu yao kwa hamu kisha kula kwa tamaa kubwa. Wanapopata nafasi ya kupakua, wanakifagia chakula mara moja na kutunga foleni mara kadha.
    • Wenye mapuuza- msimulizi anasema hakuna wakifanyacho. Wanapuuza wajibu wao kama mawaziri.
    • Wanafiki- wanahalalisha ulaji wao kwa kusema wanakula kwa niaba ya wenzao ilhali ni wao binafsi wanaofaidi.
    • Dhalimu- wana maoni kuwa wanakula kwa niaba ya wengine. Ni miongoni mwa wachache wanaofaidi raslimali za umma bila kujali wengi waoteseka. Hawataki wengine wale.(1x4=4)
  3. Kinaya kinavyojitokeza kwenye dondoo. (alama 12)
    • Mzee mambo hana kazi maalum- yeye ni waziri kivuli wa wizara zote (uk. 35)
    • Anakiri hana kazi hata moja. (uk.37)
    • Mzee Mambo hana kazi maaalum ingawa anapokea mshahara- anasema wapo wasemao yupo kwa ajili ya kuongeza idadi ya walaji karamuni. (uk. 37)
    • Mzee Mambo hujivika uchamungu na kunukuu sehemu za Kurani ili kuonyesha uongofu wake kama aliyeneemeshwa na Mungu ilhali  amejitajirisha kwa wizi wa mali ya umma.
    • Kwa Mzee Mambo kinachoangaliwa ni mtu kwenda kazini lakini si kufanya kazi yenyewe.(uk.37)
    • Mzee Mambo hapokei mshahara kama wengine. Vyeo vyake vinamruhusu kupakua mshahara atakavyo.
    • Mzee Mambo anaandaa sherehe kubwa ya kibinafsi inayotangazwa moja kwa moja na televisheni ya taifa. Hiki ni inyume cha matarajio kwa vile ni ubadhirifu wa mali ya umma.
    • Sasa na Mbura ni mawaziri katika wizara moja na hakuna wakifanyacho katika wizara hiyo.
    • Sasa na Mbura wanaendeleza ufisadi kwa hiari yao wenyewe au kwa kuamriwa na wengine. Hiki ni kinyume cha mambo kwa sababu wantarajiwa kuwa waadilifu.
    • Ni kinaya kuwa mali na raslimali za umma zinatumiwa ovyo kwenye sherehe ya Mzee Mambo. Kwa mfano, magari ya serikali. (uk. 38-39)
    • Ni kinyume cha matarajio kuwa viongozi ambao wanatarajiwa kutumia raslimali za umma kwa faida ya umma wanazifuja na kujinufaisha binafsi. Mfano ni waalikwa kwenye sherehe ya Mzee Mambo kula kwa pupa. (uk. 30-40)
    • Ni kinaya kwa waporaji wa mali ya umma kuwakejeli wanyonge na kuonyesha hawajali jinsi wanatumia hila kuiba. Mfano ni kwenye wimbo wa ‘Sijali Lawama’ (uk. 43)
    • Ni kinaya kuwa serikali inawaruhusu wachache kama DJ na wenzake kuchota mabilioni ya fedha za umma kwenye sherehe ya kibinafsi ya Mzee Mambo.
    • Ni kinyume cha matarajio kuwa dawa zinazofaa kutumiwa kuwatibu wagonjwa zinaporwa na wachache kama DJ na kuwa mtaji kwenye maduka yao ya kuuzia dawa. Maskini wanalazimika kuzilipia.
    • Viongozo wanapata huduma za kimsingi kama vile maji, umeme na matibabu bila kulipia chochote huku wanyonge wakilazimika kulipia.
    • Wachache wa tabaka la juu wanaendeleza wizi wa mali ya umma kila siku. Wanasema, “kila leo tunakula” (uk. 44) Ni kinyime cha matarajio kuwa wanaapa kuendelea na ulaji wa mali ya umma bila kujali.
    • Ni kinaya kuwa watu wanavutiwa na bidhaa kutoka nje ambazo ni duni. Kwa mfano mchele wa basmati na kupuuza vitu asilia, bora na vyenye manufaa zaidi kama vile mchele wa Mbeya.(12x1=12)
  1. Mame Bakari
    1. Fafanua toni. (alama 2)
      • Uchungu/hasira- mrejelewa anakumbuka kwa uchungu unyama aliotendewa.
      • Dharau- Aliyembaka Sara kurejelewa kama ‘janadune’ na ‘dubwana lla janadume’
      • Masikitiko- Mrejelewa anaishi na masikitiko kuwa maisha yake yamekwishavurugika kwa kubakwa na kupachikwa mimba.(1x2=2)
    2. Mbinu tatu za kimtindo. (alama 6)
      • Mbinu rejeshi- kifungu kizima kinarejelea matukio yaliyofanyika awali
      • Taswira- kutokana na maelezoo kifunguni, tunaweza kuona picha kamili akilini ya jinsi Sara alivyodhulumiwa.
      • Uhuishi/Tashhisi- ardhi ikashuhudia ukatili na udhalimu ule
      • Kejeli- mbakaji kurejelewa kama ‘janadume’ na ‘dubwana  la janadume’(3x2=6)
    3. Athari za ukatili aliotendewa Sara. (alama 12)
      • Mzongo wa mawazo- kitumbo cha Sara kilimzushia ukiwa na udhaifu kwenye fikira zake  (uk.46)
      • Kupoteza fahamu- Sara alibakwa na kupoteza fahamu- anazindukana baada ya kama nusu saa hivi. (uk.47)
      • Kukashifiwa- Sara anapopata fahamu anajikuta akiwa amelala chali, amekshifika kwa kuwa uchi. (uk. 47)
      • Kujeruhiwa- Baada ya kubakwa anajeruhiwa- anapozindukana anatambua kuwepo kwa umajimaji mwekundu unaopita.
      • Maisha ya Sara yanaingiliwa na kuharibiwa kwa kupachikwa mimba na kulazimika kuilea katika umri mdogo.
      • Sara anavunjiwa ujanajike na utu wake- Ujauzito wa kulazimishwa ulikuwa umemharibia maisha yake kabisa. (uk.47)
      • Anakabiliwa na aibu  na kudunishwa na wengine – kitendo cha kubebeshwa mzigo kingemsababishia dhiki,aibu na uduni kutoka kwa watu.
      • Kutengwa- aliwazia atakavyotengwa, kusutwa, kukashifiwa na kulaaniwa na jamaa zake pamoja na watu wa kando.
      • Kukanwa na wazazi- nyumbani, anamwona babake akimchinja la sivyo  kumfukuza kwao.
      • Woga/aibu- alihofia au kuona aibu kuelezea tukio la kubakwa kwa wazazi wake. Babake hangefahamu aliloambiwa wala kukubali ukweli wa mambo. (uk. 48)
      • Kufukuzwa nyumbani- Sara aliona akikunjiwakunjiwa matambara yake na kutupiwa nje.
      • Kukejeliwa na kufukuzwa shuleni- Sara alifikiria jinsi skuli itakavyomtazama baada ya tukio lile. Aliwazia kejeli za mwalimu mkuu na hakuona la haki ambalo angetendewa ila kufukuzwa shuleni. (uk. 49)
      • Wazo la kujitoa uhai- mawazo mengi yalimjia na kila moja lilitafuta suluhisho lake. Aliwahi kuwazia kujitoa uhai lakini wazo hilo akalikataza likome hata kumpitikia akilini. (uk. 50)
      • Wazo la kutoa mimba lilikuwa limemjia ingawa alikwishalikana tangu mwanzo
      • Kulipa kisasi- Sara na rafikiye Sarina wanapanga kulipa kisasi dhidi ya mwanamume aliyembaka Sara. Wanasitisha wazo hilo hadi wakati mwafaka. (uk. 52)
      • Kilio- Sara alikabiliwa na kilio cha siku nyingi alipowazia alivyobakwa usiku na yatakayompata miezi mingi ijayo.
      • Kutoroka nyumbani- Sara alitoroka nyumbani kwao na kuhmia nyumbani kwa kina Sarina. Huko aliweza kupata matibabu kutoka kwa Beluwa dadake Sarina aliyekuwa daktari wa uzazi.
      • Gharama- wazazi wake walilazimika kuyafadhili matibabu ya Sara alipopachikwa mimba.Walifanya hivyo kisiri pasi na kumjuza Sara.(12x1=12)
  1. Fasihi simulizi
    1. Tambua kipera cha utungo huu na utoe sababu ya jibu lako. (Al 2)
      • Kipera cha utungo ni sifo.
      • Utungo huu unatoa sifa za mtu ambaye anaisaidia jamii yake kuwarejesha mifugo waliokuwa wametekwa.
    2. Ni sifa gani hukibainisha kipera ulichotaja hapo juu? (Al 5)
      • Huwasifu watu ambao wamefanya matendo ya kupigiwa mfano.
      • Huwa na matumizi ya sitiari na jazanda kutoa taswira ya ujasiri, uhodari na upekee wa wanaosifiwa.
      • Hujikita katika muktadha maalum k.v jandoni kuwasifu watahariwa, katika sherehe ya kumtawaza kiongozi.
      • Huimbwa na mtu binafsi au kundi la watu.
      • Huweza kuibwa na mtu binafsi kwa nia ya kujifu.
      • Huakisi thamani ya jamii inayohusika.
      • Huwa na matumizi mapana chuku kumsifu mhusika.  
    3. Eleza dhima za kipera hiki katika jamii. (Al 5)
      • Huyasifu matendo mazuri ya watu mashuhuri katika jamii.
      • Huyataja mafanikio yaliyofikiwa na jamii kwa mchango wa watu maarufu katika jamii.
      • Hukuza uzalendo kwa kuwafanya wanajamii kuonea fahari jamii na mashujaa wake.
      • Ni namna ya kuhifadhi historia ya jamii kwa kuyakumbuka matukio ya kishujaankatika jamii.
      • Huakisi mtazamo wa jamii kuhusu mambo kama vile ujasiri, usaliti n.k
      • Ni njia ya kutambua mchango wa watu tofauti katika kuboresha maslahi ya jamii yao.
      • Huwaburudisha wanajamii na kuwasisimua wakati wa sherehe kuwatawaza viongozi, kuwatuza mashujaa n.k
    4. Jamii iliyoakisiwa kwenye utungo huu huendeleza shughuli gani za kiuchumi? (Al 4)
      • Uhunzi – Walifua mikuki, mishale na ngao.
      • Kilimo cha nazi – shujaa anatuzwa kole za nazi.
      • Kilomo cha nafaka – shujaa anatuzwa mashuke ya mtama.
      • Ufugaji wa ngombe – anawarejesha mitamba na fahari waliotekwa.
      • Uvuvi – anatuzwa vishazi vya samaki.
      • Uwindaji – shujaa anavishwa taji la ngozi ya duma, kipembe cha kifaru na nguo ya ngozi ya simba.
    5. Fafanua mtindo katika kifungu hiki. (Al 4)
      • Taswira – Kuna taswira ya vilima na hata mabonde yenye mito katika eneo rejelewa.
      • Mbinu rejeshi – wimbo huu unaturejesha nyuma kwa enzi babuze shujaa.
      • Tashbihi – shujaa wa nguvu za tembo.
      • Sitiari / jazanda – shujaa anerejelewa kama mwamba.
      • Chuku – anayepigana bila silaha yoyote , Angurumapo mahasimu wanazirai
      • Uhaishaji – wasiwasi unawakumbatia
      • Methali – angurumapo simba mcheza nani?

Maswali ya balagha – angurumapo simba mcheza nani? , Anapotisha Amali wa Jamali atasimama nani?

Join our whatsapp group for latest updates

Download Kiswahili Paper 3 Pre Mock Questions and Answers - Mokasa I Joint Examination July 2021.


Tap Here to Download for 50/-




Why download?

  • ✔ To read offline at any time.
  • ✔ To Print at your convenience
  • ✔ Share Easily with Friends / Students


Get on WhatsApp Download as PDF
.
Subscribe now

access all the content at an affordable rate
or
Buy any individual paper or notes as a pdf via MPESA
and get it sent to you via WhatsApp

 

What does our community say about us?

Join our community on:

  • easyelimu app
  • Telegram
  • facebook page
  • twitter page
  • Pinterest