Alama za Uakifishaji - Sarufi na Matumizi ya Lugha Kiswahili Notes

Share via Whatsapp


Utangulizi

 • Kunazo alama kadhaa zinazotumika kuakifisha maneno na sentensi za Kiswahili.


Alama ya Kikomo au Kituo Kikuu (.)

 1. Kuonyesha mwisho wa sentensi.
  1. Huu ndio mwisho wa sentensi hii.
  2. Kioo kimevunjika
 2. Katika kufupisha maneno
  1. U.N, K.B.C, Y.C.S, N.Y.S
  2. Dkt. Maktaba, Bw. Msumari
 3. Kuonyesha Saa 
  1. Misa ilianza saa 4.30 za asubuhi.
  2. Hivi sasa ni saa 10.20.
 4. Katika hesabu kuonyesha sehemu isiyo nzima
  1. Ukigawa tatu mara mbili, utapata 1.5
  2. Mtoto huyo ana uzani wa kilo 8.27
 5. Kuonyesha senti katika pesa
  1. Bei yake ni shilingi 12.50.
  2. Karo ya shule mwaka huu ni 80,000.00


Alama ya Kituo, Kipumuo au Koma (,)

 1. Kuorodhesha vitu zaidi ya mbili
  1. Nimenunua simu, saa, redio na viatu.
  2. Kina mama waliimba, wakapiga ngoma na kunengua viuno vyao.
 2. Kugawanya mawazo katika sentensi.
  1. Baada ya sala za jioni, Mzee Makosa alitoka nje na kuwasha sigara yake.
  2. Nilipomwuliza kama alimjua binti yule, aliniangalia tu na kucheka
  3. Ingawa kitabu hiki ni kizito, sina budi kukibeba.
 3. Kutoa maelezo zaidi.
  1. Shabiba, mmojawapo ya wanawake wajawazito, amejifungua mtoto wa kike.
  2. Shati hili, ingawa nalichukia, nitalivalia tu.
 4. Katika tarakimu, kugawa elfu.
  1. Shilingi 209, 408, 000 ziliporwa na serikali.
  2. Dawa hiyo iliua takribani mbu 61, 247.


Alama ya Dukuduku (…)

 1. Hutumika kuonyesha kuwa maneno yameachwa ya kutangulia, kati au ya mwisho. Yaweza kuachwa kwa kuwa makali
  - Nyani haoni…
 2. kukatizwa usemi/kauli
  AMINA: Mama ni…
  MAMA: Kwanza watoka wapi usiku huu?
 3. maneno yanaendelea
  - Alimwambia ajihadhari anapovuka barabara…


Alama ya Kinukuu (' na ")

 1. Kunukuu usemi halisi
  1. "Ukitaka kufua dafu," mama akamwambia mwanawe, "lazima utie bidii."
  2. Alimtazama kisha akamwuliza, "Unadhani nimechanganyikiwa kama wewe?"
 2. Kunukuu kichwa cha kazi ya sanaa k.v kitabu, wimbo, kipindi n.k
  1. Saumu na Neema ni wahusika katika riwaya "Hamu ya Sumu Tamu".
  2. Rose Muhando ndiye aliyeimba "Mteule Uwe Macho".
 3. Kuonyesha maneno yasiyo ya Kiswahili unapochanganya ndimi katika sentensi
  1. Huyu ndiye mchezaji "number one"
  2. Amesema "keyboard" ya "computer" yake haifanyi kazi..
 4. Kuonyesha maneno yanayowakilisha maana tofauti na maana yake ya kawaida au kinaya.
  1. Lesi alipoenda kwenye 'maktaba' alipata mimba.
  2. Rais wetu 'mtukufu' amewatisha mawaziri wake.
  3. Moto ulioteketeza shule hiyo ulitokana na kusudi la wanafunzi la 'kumshtua' mwalimu wao.
 5. Kuonyesha herufi iliyoachwa nje au kufupisha maneno katika ushairi hasa kwa kusudi la kutosheleza idadi ya mizani
  1. 'takufuata popote wendapo,
  2. 'liapo ya mgambo, lazima kuna jambo
 6. Katika maendelezo ya sauti ya ung'on'g'o (ng')
  1. Ng'ombe wa Ng'ang'a wanang'ang'ania nini?
  2. King'ang'i anapenda kunung'unika ovyo ovyo.


Alama ya Kiulizi (?)

 1. Kuulizia swali
  1. Je, utamtembelea lini?
  2. Ariana anaishi wapi?
 2. Kuonyesha pengo lililoachwa wazi
  1. Ndama ni mwana wa ng'ombe ilhali ___?___ ni mtoto wa mbuzi.
  2. __?__ mpokee mke wako, __?__, siku ya leo umepata jiko.


Alama ya Hisi (!)

 1. Kuonyesha hisia kama vile hasira, mshangao, furaha n.k
  1. Lo! Ukistaajabu ya Musa utaona ya Firauni.
  2. Pepo nyeusi! Shindwa! Chomeka! Kwenda kuzimu!
 2. Kuigiza Tanakali za Sauti
  1. Amejikwaa sasa ameanguka pu!
  2. Moyo ulidunda ndu! ndu!


Alama ya Nukta-Mbili au Koloni (:)

 1. Kutanguliza orodha
  1. Harusi hiyo ilihudhuriwa na watu wa wengi: wake kwa waume; wadogo kwa wakubwa; wazee kwa vijana.
  2. Kuna aina kadhaa za vivumishi: vivumishi vya sifa, vivumishi vya idadi, vivumishi viwakilishi na kadhalika
 2. Kuelezea sababu au kuonyesha matokeo ya kitu.
  1. Saumu a lipoingia chumbani alipigwa na butwaa: mamake alikuwa amekufa.
  2. Baba alinipatia zawadi nzuri sana: nilirukaruka kwa furaha.
 3. Kuonyesha saa
  1. Wimbo huo unachukua dakika 4:45.
  2. Aliingia saa 5:1 5
 4. Kunukuu ukurasa wa Bibilia
  1. Padre alisoma Luka 2:1-6
  2. Katika kitabu cha Mwanzo 5: 2-7, Bibilia inasema...
 5. Kuonyesha maneno ya msemaji katika tamthilia au mchezo wa kuigiza
  1. Mzee Mwanyati: Unafikiria mimi ni nyanyako?
  2. Kadogo: (akitetemeka) Tafadhali naomba unisamehe.
 6. Kuonyesha mada katika barua au kumbukumbu za mkutano
  1. KUH: Ombi Lako la Kujiuzulu.
  2. RE: Barua ya tarehe 3/2/1 999.
 7. Katika kumbukumbu za mkutano
  1. KUM: 2/321 /2000 Mbinu Mpya za Kunyamazisha Raia
  2. Ajenda 2: Kusomwa kwa kumbukumbu za mkutano uliotangulia


Alama ya Nukta-Kituo au Semi Koloni (;)

 1. Kuorodhesha vitu hasa vinapokuwa na zaidi ya neno moja
  1. Harusi hiyo ilihudhuriwa na watu wa wengi: wake kwa waume; wadogo kwa wakubwa; wazee kwa vijana.
  2. Wakati wa likizo tulitembelea sehemu kadhaa: Mombasa, Kenya; Dodoma, Tanzania; Kampala, Uganda na tukamalizia hapa Nairobi, Kenya.
 2. Kuunganisha vishazi huru viwili au kuonyesha mawazo mawili.
  1. Tuliwasili darasani tukiwa tumechelewa; mwalimu alitukaribisha kwa kiboko.
  2. Usiwe na wasiwasi; nitakuwa pamoja nawe siku zote.


Alama ya Kistari Kifupi (-)

 1. Kuunganisha maneno mawili
  1. Mbwa-koko aliuma mwana-haramu.
  2. Nawatuma kama wana-kondoo miongoni mwa mbwamwitu.
 2.  Kuonyesha hadi, au mpaka
  1. Bei imepanda kutoka shilingi 20 - 30
  2. Tutasoma kitabu cha Matendo 2: 3 - 7
 3. Kama alama ya kupunguza au kutoa katika Hesabu
  1. 9 - 7 = 2
  2. 4 - 5 = -1
 4. Kuonyesha neno ambalo halijakamilika litaendelezwa katika msitari ufuatao
  1. Ukitaka twende kwetu nyumbani nitakupeleka ukamwone mamangu.
  2. Kuna migumo kumi na mitatu katika Bustani la Kuzimu.
 5. Kuonyesha tarehe
  1. Watu wengi walikufa tarehe 07-08-1 998.
  2. Marehemu alikufa tarehe 06-06-2006


Alama ya Kistari Kirefu (‒)

 1. Kutoa maelezo zaidi
  1. Nilipokutana na Zakido ‒ ambaye aliripotiwa kupotea miaka miwili iliyopita ‒ nilimsalimia lakini hakunitambua.
  2. Hatimaye nimeshinda ‒ baada ya kujaribu kwa masaa matatu.
 2. Kuorodhesha hoja au vitu
  1. Umuhumu wa fasihi simulizi:
   ‒ kuburudisha
   ‒ kuelimisha
   ‒ kuunganisha jamii


Alama ya Mabano au Parandesi ()

 1. Kutoa maelezo zaidi
  1. Z. Anto (aliyeimba Binti Kiziwi) ametoa wimbo mpya.
  2. Shangazi yangu (ambaye ni naibu wa waziri) amenitumia zawadi.
 2. Kutoa neno jingine lenye maana sawa
  1. Dhamira (nia) ya mshairi huyu ni kutushauri tusikimbilie maisha.
  2. Mabanati (wasichana) hao hutembea uchi jijini usiku wa manane.


Alama ya Kinyota (*)

 1. Kuonyesha neno ambalo litaelezewa zaidi chini ya ukurasa(foot note)
  1. Alipopata nafasi ya kuingia shule ya upili ya Starehe*, mwanafunzi huyo alijawa na furaha tele.
                                                                                                     
   *Starehe ni mojawapo ya shule zinazofanya vizuri zaidi barani Afrika.
 2. Kuficha herufi/silabi katika neno ili kupunguza ukali wa maneno yasiyo na nidhamu.
  1. Ra is aliwaita wananchi m**i ya kuku.
  2. Aidha, alisema kwamba nyote ni wapu***vu.


Alama ya Mlazo (/)

 1. Kuonyesha 'au'
  1. Mkutano huo utahutubiwa na Rais/Waziri Mkuu.
  2. Wazungumzaji wengi wa Kiswahili wanatoka Kenya/Tanzania.
 2. Kuonyesha neno au fungu la maneno lenye maana sawa.
  1. Sheila amepewa cheo cha katibu/mwandishi.
  2. Hawa ndio wanaotapatapa ovyo/wasio na mbele wala nyuma.
 3. Katika hesabu kuonyesha kugawanya au akisami.
  1. 5/7 ya siku za juma ni siku za kazi.
  2. 12/6 = 2
 4. Katika tarehe
  1. Shule zilifunguliwa tarehe 08/01 /201 2
  2. Kamati hiyo ilikubaliana kwamba, Mwokozi alizaliwa tarehe 25/12


Alama ya HERUFI KUBWA

 1. Kuanzisha sentensi'
  1. Fisi hula mizoga.
  2. Huu ndio mwanzo wa sentensi hii.
 2. Kuonyesha Nomino za Kipekee
  1. Bi Rangile anatoka Vikwazoni.
  2. Nchi ya Tanzania imebarikiwa na Mlima Kilimanjaro unaowavutia wageni kutoka Ulaya.
 3. Kuonyesha Kichwa au Mada
  1. ALAMA ZA UAKIFISHAJI
  2. UFAHAMU
  3. Njia Tano za Kuua Mbu
 4. Kuonyesha maneno yaliyofupishwa
  1. UKIMWI ni Ukosefu wa Kinga Mwilini.
  2. TUKI ni Taasisi ya Uchunguzi wa Kiswahili
Join our whatsapp group for latest updates

Download Alama za Uakifishaji - Sarufi na Matumizi ya Lugha Kiswahili Notes.


Tap Here to Download for 50/-
Why download?

 • ✔ To read offline at any time.
 • ✔ To Print at your convenience
 • ✔ Share Easily with Friends / Students


Get on WhatsApp Download as PDF
.
Subscribe now

access all the content at an affordable rate
or
Buy any individual paper or notes as a pdf via MPESA
and get it sent to you via WhatsApp

 

What does our community say about us?

Join our community on:

 • easyelimu app
 • Telegram
 • facebook page
 • twitter page
 • Pinterest