Aina za Maneno - Sarufi na Matumizi ya Lugha Kiswahili Notes

Share via Whatsapp


Nomino (N)

  • Nomino ni maneno ambayo ni majinaya watu, vitu, hali n.k. Kuna nomino za kawaida na nomino za kipekee miongoni mwa aina nyingine za nomino.

Aina za Nomino

  • Kunazo aina mbalimbali za nomino katika lugha ya Kiswahili.
    • Nomino za Kipekee
    • Nomino za Kawaida
    • Nomino za Jamii/Makundi
    • Nomino za Kitenzi-Jina
    • Nomino za Dhahania
    • Nomino za Wingi

Nomino za Kawaida

  • Haya ni majina ya kawaida yanayoweza kutumiwa kurejelea vitu mbalimbali, watu, wanyama, mahali na kadhalika.
  • Nomino hizi zinaweza kuwa katika umoja au wingi kulingana na ngeli yake. k.m: nyumba, mbuzi, daktari, soko, kalamu, jua

Nomino za Kipekee

  • Haya ni majina maalum ya watu, mahali, bidhaa, kampuni, na kadhalika.
  • Herufi ya kwanza ya nomino hizi huwa ni herufi kubwa.
  • Nomino za kipekee haziwezi kubadilika, na hivyo basi hazina wingi. k.m: Tanzania, Nairobi, Anita, Athi, Kimbo, Easyelimu

Nomino za Jamii

  • Nomino za jamii hurejelea kundi la vitu au wanyama, kwa ujumla. Aghalabu vitu vinavyorejelewa hutokea kwa makundi ya vitu mbili au zaidi. Nomino hizi hutumia wingi tu tunaporejelea makundi zaidi ya moja. k.m: jozi la viatu, umati wa watu, bustani la maua, bunga la wanyama

Nomino za Wingi

  • Nomino hizi hurejelea vitu ambavyo hutokea kwa wingi na haziwezi kuhesabiwa.
  • Vitu kama hivyo hutumia aina nyingine ya vipimo ili kurejelea kiasi chake.
  • Nomino za wingi hazina umoja. k.m: maji, maziwa, changarawe, pesa, nywele

Nomino za Vitenzi Jina

  • Nomino hizi huundwa kutokana na vitenzi kwa kuongeza kiungo KU mwanzoni mwa mzizi wa kitenzi. k.m: kulima, kuongoza, kucheza, kulala

Nomino za Dhahania

  • Haya ni majina ya hali au vitu ambavyo havionekani wale haviwezi kushikika. k.m: upendo, furaha, imani, elimu, ndoto, mawazo, maisha, usingizi


Viwakilishi (W)

  • Viwakilishi vya Nomino ni maneno yanayotumika badala ya nomino. Kiwakilishi hakiwezi kuambatanishwa na nomino inayorejelewa.

Aina za Viwakilishi

  • Viwakilishi vya Nafsi
  • Viwakilishi Viashiria
  • Viwakilishi Visisitizi
  • Viwakilishi vya Sifa
  • Viwakilishi vya Idadi
  • Viwakilishi Viulizi
  • Viwakilishi Vimilikishi
  • Viwakilishi Virejeshi (O-Rejeshi)
  • Viwakilishi Vya A-Unganifu

Viwakilishi vya Nafsi

  • Viwakilishi hivi hutumika kwa niaba ya nafsi kwa umoja na kwa wingi. k.m: mimi, wewe, yeye, sisi, nyinyi, wao
    NAFSI UMOJA  WINGI
    Nafsi ya Kwanza  Mimi Sisi
    Nafsi ya Pili Wewe Ninyi/Nyinyi
    Nafsi ya Tatu Yeye Wao
    k.m.
    - Sisi tuliwatangulia nyinyi kufika hapa.
    - Mimi si mjinga kama vile yeye anavyofikiria

Viwakilishi Viashiria

  • Viwakilishi viashiria (vionyeshi) hutumika badala ya nomino kwa kutumia kuonyesha nomino inayorejelewa bila kuitaja. k.m: huyu, yule, hapa, n.k
    - Hiki hakina maandishi yoyote.
    - Hao hawajui tofauti ya viwakilishi na vivumishi
    - Tumekuja hapa ili kuwaburudisha kwa nyimbo tamu tamu.

Viwakilishi Visisitizi

  • Husisitiza nomino inayowakilishwa kwa kurudiarudia kiashiria chake. k.m: yuyu huyu, wawa hawa, kiki hiki, papo hapo, mumu humu,
    Zizi hizi ndizo zilizovunjika wiki jana
    - Yule yule aliyekamatwa juzi, ameiba tena.

Viwakilishi vya Sifa

  • Husimama badala ya nomino kwa kurejelea sifa yake. k.m: '-eupe, -zuri, -tamu, -embamba, -rembo, safi'
    - Vyekundu vimehamishwa
    - Warembo wamewasili.
    - Kitamu kitaliwa kwanza.

Viwakilishi vya Idadi

  • Hutumika kusimama badala ya nomino kwa kurejelea idadi yake.
    • Idadi Kamili- hutumia nambari kuelezea idadi ya nomino. k.m: 'saba, mmoja, ishirini'
      - Wawili wamepigwa risasi polisi leo jioni.
      - Alimpatia mtoto wake hamsini kununua chakula
    • Idadi Isiyodhihirika- huelezea kiasi cha nomino kwa ujumla, bila kutaja idadi kamili k.m: 'chache, nyingi, kadhaa, kidogo, wastani'
      - Tutazungumza na wachache kabla ya kuanzisha maonyesho yetu.
      - Kadhaa zimeripotiwa kupotea.

Viwakilishi Viulizi

  • Viwakilishi viulizi hutumika kwa niaba ya nomino katika kuulizia swali.
  • Baadhi ya viwakilishi viulizi huchukua viambishi vya ngeli k.m: ' -ngapi?, -pi?'
    - Vingapi vinahitajika? - kuulizia idadi
    - Zipi zimepotea?
  • Kunavyo viwakilishi viulizi vingine ambavyo havichukui viambishi vyovyote. k.m: 'wapi?, gani?, nini?, vipi?'
    - Gani imefunga bao hilo?
    - Wapi hapana majimaji?
    - Yule mvulana alikupatia nini?
    - Uliongea naye vipi? - kuulizia namna

Viwakilishi Vimilikishi

  • Viwakilishi hivi hurejelea nomino kwa kutumia vimilikishi. k.m: '-angu, -ako, -ake, -etu, -enu, -ao '
    - Kwetu hakuna stima.
    - Lake limekucha.
    - Zao zimeharibika tena

Viwakilishi Virejeshi (O-Rejeshi)

  • Hutumia O-rejeshi ama amba- kurejelea kusimamia nomino k.m: 'ambaye, ambao, ambalo, ambacho, huyo, yule'
    - Ambalo lilipotea limepatikana.
    - Ambaye hana mwana, aeleke jiwe

Viwakilishi Vya A-Unganifu

  • Huwakilishi nomino kwa kutaja kinachomiliki nomino hiyo. Huundwa kwa kuambatanisha kiambishi cha nafsi/ngeli pamoja na kiambishi -a cha a-unganifu, kisha nomino nyingine
    k.m: 'cha, la, kwa, za, ya'
    - Cha mlevi huliwa na mgema
    - Za watoto zitahifadhiwa.


Vitenzi (T)

  • Vitenzi ni maneno yanayosimamia kitendo. Kila kitenzi huwa na shina la kitenzi (sehemu ndogo zaidi ya kitenzi ambayo ndiyo huwakilisha tendo hilo). Shina la kitenzi huambatanishwa na viambishi ili kutoa maana iliyokusudiwa kama vile mtendaji, mtendewa, wakati kitendo kinafanyika na pia kauli ya kitenzi hicho.

Aina za Vitenzi

  • Vitenzi Halisi
  • Vitenzi Vikuu
  • Vitenzi Visaidizi
  • Vitenzi Vishirikishi
  • Vitenzi Sambamba

Vitenzi Halisi

  • Hivi ni vitenzi vinavyorejelea kitendo moja kwa moja. Vitenzi halisi vinapoambatanishwa na vitenzi vidogo katika sentensi, huitwa vitenzi vikuu. k.m: soma, kula, sikiza
    - Waziri Mwasimba aliwasili jana kutoka ng'ambo.
    - Kawira atapikia wageni.
    - Funga mlango wa dirisha.

Vitenzi Vikuu

  • Hivi ndivyo vitenzi ambavyo hubeba maana kuu ya kitendo pasi kuchukua viambishi awali na tamati kama ilivyo  katika vitenzi halisi.
  • Aghalabu vitenzi hivi hufungamanishwa na kiambishi 'ku' kwa mfano Cheza, Lima, kula, soma,  lia, amka,  piga, Ondoka, safiri, lala.

Mifano katika sentensi

  1. Wanafunzi waliamua kusoma kwa bidii.
  2. Baba amehitimisha safari yake.
  3. Mtoto alitaka kula samaki jana jioni
  4. Jua kali anapenda kuimba nyimbo za mapenzi

Vitenzi Visaidizi

  • Vitenzi visaidizi hutangulia vitenzi halisi (vitenzi vikuu) katika sentensi ili kuleta maana inayokusudiwa kulingana na wakati au hali. k.m: -kuwa, -ngali,
    - Jua lilikuwa limewaka sana.
    - Bi Safina angali analala

Vitenzi Vishirikishi

  • Vitenzi vishirikishi hutumika kuelezea hali iliyopo au mazingira. Kuna aina mbili za vitenzi vishirikishi:
    1. Vitenzi Vishirikishi Vipungufu - havichukua viambishi vyovyote. k.m: ni, si, yu, tu, ngali, japo
      1. Mwalimu wetu angali hajatuzwa zawadi.
      2. Nuru ya fasihi ni kitabu kizuri cha kudurusu.
      3. Ogala si kocha mzuri kama Kimanzi
    2. Vitenzi Vishirikishi Vikamilifu - huchukua viambishi vya nafsi au ngeli. Vitenzi hivi vinaweza kusimama peke yake au vinaweza kufuatiliwa na vitenzi vikuu. k.m: ndiye, ndio, ndipo
      - Sanita ndiye mkurugenzi wa kampuni
      - Huku ndiko kulikoibiwa

Vitenzi Sambamba

  • Hivi ni vitenzi ambavyo hutumiwa viwili au zaidi kwa pamoja iii kutoa maana moja kwa ukamilifu. Yamkini huwa vitenzi visaidizi. Vitenzi hivi vyote vinapotumika huwa vimechukua viambishi vya wakati kwa mfano;
    1. Wanafunzi waliweza kuona wanyamapori wengi.
    2. Hatujaenda kumwona mgonj wa hospitalini.
    3. Yusufu aliweza kuftindisha kabla ya kustaafu.
    4. Mama hai aenda kumtembelea tanRu atoke marekani.
    5. Atapaswa kusoma makala hayo aliyoyandika

Muundo wa Vitenzi

  • Kwa kuzingatia muundo wa vitenzi, tunaweza kuweka vitenzi katika aina zifuatazo:
    1. Vitenzi vya Silabi Moja
    2. Vitenzi vya Kigeni
    3. Vitenzi vya Kibantu

Vitenzi vya Silabi Moja

  • Hivi ni vitenzi vyenye silabi moja pekee. Ili kuleta maana kamili, vitenzi hivi huambatanishwa na kiungo KU- katika kauli ya kutenda. Kama vitenzi vingine, vitenzi vya silabi moja vinaweza kunyambuliwa. k.m: soma, kula, sikiza
    1. -cha - kucha - jua linapochomoza asubuhi k.m kumekucha
    2. -fa - kufa - kuacha kupumua, kupoteza uhai k.m amekufa
    3. -ja- kuja - fika mahali hapa k.m nimekuja
    4. -la- kula - kutia chakula mdomoni k.m anakula
    5. -nya- kunya - kutoa mabaki ya chakula toka tumboni k.m mtoto amekunya
    6. -nywa- kunywa - kutia kinywaji kama vile maji au maziwa mdomoni k.m ninakunywa uji
    7. -pa- kupa - kumkabithi/kumpatia mtu kitu k.m amenipa pesa
    8. -pwa- kupwa - kujaa hadi pomoni - k.m kisima kimekupwa maji
    9. -twa- kutwa - jua linapozama magharibi na usiku kuingia k.m kumekutwa
    10. -wa- kuwa - kutokea katika hali au mahali fulani k.m alikuwa

Vitenzi vya Kigeni

  • Hivi ni vitenzi vyenye asili kutoka kwa lugha nyingine badala ya Kibantu. Baadhi ya lugha hizo ni Kiarabu, Kizungu, Kireno, Kihispania n.k.
  • Vitenzi hivi havifuatilii muundo wa kawaida wa vitenzi vya Kiswahili ambavyo huishia kwa sauti -a. Badala yake, vitenzi hivi huishia kwa sauti nyingine kama vile -e, i, -o, na u k.m: haribu, tubu, shukuru, salimu, thamini, amini, samehe, baleghe

Vitenzi vya Kibantu

  • Hivi ni vitenzi vyenye asili ya Kibantu na ambavyo huishia kwa sauti -a. Kitengo hiki hujumuisha asilimia kubwa zaidi ya vitenzi vya Kiswahili k.m: simama, shika, tembea, beba, soma, lia


Vivumishi (V)

  • Vivumishi au visifa ni maneno yanayotuelezea zaidi kuhusu nomino. Aghalabu vivumishi hutanguliwa na nomino.

Aina za Vivumishi

  • Vivumishi vya Sifa
  • Vivumishi Vimilikishi
  • Vivumishi vya Idadi
  • Vivumishi Visisitizi
  • Vivumishi Viashiria / Vionyeshi
  • Viwakilishi Viulizi
  • Vivumishi Virejeshi
  • Vivumishi vya KI-Mfanano
  • Vivumishi Vya A-Unganifu

Vivumishi vya Sifa

  • Hivi ni vivumishi ambavyo hutoa sifa ya kitu, mtu, mahali, n.k k.m: kizuri, kali, safi, mrembo
    1. Yule mama mweusi hupika chakula kitamu.
    2. Mvulana mkorofi aliadhibiwa na mwalimu kutokana na tabia zake mbaya.
    3. Sauti nzuri humtoa nyoka mkali pangoni

Vivumishi Vimilikishi

  • Vivumishi hivi hutumika kuonyesha nomino inamiliki nyingine. Mizizi ya vivumishi hivi huundwa kulingana na nafsi mbalimbali ( -angu, -ako, -ake, -etu, -enu, -ao). k.m: changu, lako, yake, kwetu, vyenu, zao
    1. Nitatumia talanta zangu kwa manufaa ya taifa letu.
    2. Aliweka kitabu chako sebuleni mwako
    3. Katosha amepata nguo yake miongoni katika sanduku lao.

Vivumishi vya Idadi

  • Hutueleza zaidi kuhusu kiasi, au idadi ya nomino. Kuna aina mbili za vivumishi vya idadi.
    • Idadi Kamili - hutumia nambari kuelezea idadi ya nomino. k.m: tatu, mbili, kumi
      1. Msichana mmoja amewauwa nyoka wawili
      2. Siku kumi zimepita tangu Bi Safina alipojifungua watoto watatu
    •  Idadi Isiyodhihirika - huelezea kiasi cha nomino kwa ujumla, bila kutaja idadi kamili k.m: chache, nyingi, kadhaa, kidogo, wastani
      1. Watu wachache waliohudhuria mazishi ya Kajuta walikula chakula kingi sana.
      2. Baba yao alikuwa mateka kwa miaka kadhaa.

Vivumishi Visisitizi

  • Husisitiza nomino fulani kwa kurudia rudia kivumishi kiashiria k.m: yuyu huyu, wawa hawa, kiki hiki, papo hapo, mumu humu,
    1. Jahazi lili hili
    2. Wembe ule ule
    3. Ng'ombe wawa hawa

Vivumishi Viashiria/Vionyeshi

  • Vivumishi viashiria hutumika kuonyesha au kuashiria nomino kulingana na mahali.
    Karibu hapa, huyu, hiki, hili, huku, haya, ule, wale, pale
    Mbali kidogo  hapo, huyo, hiyo, hicho
    Mbali zaidi pale, lile, kile
    1. Msichana huyu ni mkubwa kuliko yule
    2. Jani hili la mwembe limekauka
    3. Tupa mpira huo

Vivumishi Viulizi

  • Vivumishi viulizi hutumika kuuliza swali.
  • Baadhi ya vivumishi viulizi huchukua viambishi vya ngeli k.m: -ngapi?, -pi?
    1. Ni walimu wangapi wamefukuzwa? - kuulizia idadi
    2. Je, ni dawati lipi lenye funguo zangu?
  • Kunavyo vivumishi viulizi vingine ambavyo havichukui viambishi vyovyote. k.m: wapi?, gani?, nini?, vipi?
    1. Unazungumza kuhusu kipindi gani?
    2. Je, mmefika mahali wapi? - kuulizia mahali

Vivumishi Virejeshi

  • Hivi ni vivumishi ambavyo hurejelea nomino. Vivumishi hivi vinaweza kuwa vivumishi vya O-rejeshi au vivumishi viashiria vinapotumika kurejelea nomino. k.m: ambaye, ambao, ambalo, ambacho,
    1. Msichana ambaye alikuja ni Sheila
    2. Sauti ambayo uliisikia ilikuwa ya Mzee Kasorogan

Vivumishi vya KI-Mfanano

  • Vivumishi vya KI- ya Mfanano hutumika kulinganisha sifa ya nomino na hali au tabia nyingine. Vivumishi hivi hutanguliwa na nomino, kiunganishi cha A-unganifu na huchukua kiungo KI. k.m: wa kifalme, za kijeshi, ya kitajiri, n.k
    1. Chifu wa Vikwazoni anaishi maisha ya kimasikini
    2. Chali anapenda kusikiliza mziki wa kizungu
    3. Bi Naliza huvulia mavazi ya kifalme.

Vivumishi Vya A-Unganifu

  • Vivumishi hivi hutuelezea zaidi kuhusu nomino kwa kuonyesha kitu kinachomiliki nomino hiyo. Huundwa kwa kuambatanisha kiambishi cha nafsi/ngeli pamoja na kiambishi -a cha a-unganifu, kisha nomino k.m: cha, la, kwa, za, ya
    1. Watoto wa mwalimu mkuu wana tabia nzuri
    2. Chai ya daktari imemwagika


Vielezi (E)

  • Vielezi ni maneno yanayotoa habari zaidi kuhusu kitendo kilivyofanyika. Pia vielezi hutoa habari zaidi kuhusu hali, vivumishi au vielezi vingine.

Aina za Vielezi

  • Vielezi vya Mahali
  • Vielezi vya Wakati
  • Vielezi vya Idadi
  • VIelezi Vya Namna

Vielezi vya Mahali

  • Vielezi vya mahali hutoa habari kuhusu mahali ambapo kitendo kilifanyika. Aghalabu vielezi hivi huundwa kwa kutumia jina la mahali au kwa kuongeza kiungo -NI mwishoni mwa neno linaloashiria mahali. k.m: nyumbani, kazini, shuleni
    1. Mtoto huyo hajatulia nyumbani tangu alipotoka Mombasa.
    2. Msipitie sokoni mkienda kanisani.

Vielezi vya Wakati

  • Huelezea zaidi kuhusu wakati kitendo kipofanyika k.m: jioni, jana, asubuhi, saa saba, mwaka juzi
    1. Mzee Kasorogani amesema kwamba ataoga mwaka ujao
    2. Musa alilazimishwa kuchimba mtaro saa sita usiku
    3. Kisaka na Musa watakutana kesho

Vielezi vya Idadi

  • Vielezi vya idadi hutulezea kitendo kilifanyika mara ngapi
    1. Idadi Kamili
      - Vielezi vya Idadi Kamili hutaja idadi kamili ya mara ngapi kitendo kilifanyika. k.m: mara mbili, siku mbili kwa juma, mara kumi
      1. Gibi alimzaba kofi mara tatu na kisha akakimbia.
      2. Daktari alimwagiza mama huyo achukue dawa mara tatu kwa siku na arudi hospitalini siku mbili kwa mwezi
    2. Idadi Isiyodhihirika
      - Vielezi vya Idadi Isiyodhirika huelezea kiasi ambacho kitendo kilifanyika bila kutaja kiasi kamili k.m: chache, nyingi, kadhaa, kidogo, wastani
      1. Mwizi wa kuku alipigwa mara kadhaa kabla ya kuokolewa na polisi.
      2. Yeye hunipigia simu mara kwa mara

Vielezi vya Namna

  • Huelezea jinsi au namna kitendo kinavyofanyika. Kitendo kinaweza kufanyika kwa namna mbalimbali.
  • Hivyo basi kuna aina mbalimbali za vielezi vya namna:
    1. Vielezi vya Namna Halisi
      - Hutufahamisha jinsi kitendo kinavyofanyika kwa kutumia maneno halisi (bila kuambatanishwa na maneno mengine au viambishi vingine). k.m: vizuri, ovyo, haraka, upesi, vibaya
      1. Kioo cha bibi harusi kilianguka na kuharibika vibaya
      2. Mama alipika chakula upesi
      3. Amepigwa kalamu kwa kufanya kazi kiholela
    2. Vielezi vya Namna Hali
      - Hutufahamisha hali ambayo kitendo kilifanyika. Vielezi hivi hujihusisha na tabia ya kitu/mtendaji wa kitendo k.m: kwa furaha, kwa makini,
      1. Bibi harusi aliingia kanisani kwa madaha
      2. Mtoto alilia kwa maumivu mengi
    3. Vielezi vya Namna Kitumizi/Ala
      - Hutoa habari kuhusu kifaa, ala au mbinu iliyotumiwa kufanya kitendo fulani k.m: kwa kisu, kwa jembe, kwa meno, kwa moto, kwa maji
      1. Mkulima aliangusha mti mkubwa kwa shoka
      2. Mzee huyo alimpiga mke wake kwa bakora kabla ya kuchoma nguo zake kwa makaa
    4. Vielezi Vikariri
      - Husisitiza kitendo kinavyofanyika kwa kutaja kielezi kinachorejelewa mara mbili mfululizo. k.m: haraka haraka, ovyo ovyo, juu juu
      1. Polisi walipoingia, wezi walitawanyika haraka haraka.
      2. Wanafunzi wengi hufanya kazi yao ovyo ovyo
    5. Vielezi vya Ki-Mfanano
      - Vielezi mfanano hutumia KI-mfanano kuelezea kitendo kinavyofanyika kwa kulinganisha. k.m: kitoto, kiungwana,
      1. Babake huongea kiungwana.
      2. Harida hutembea kijeshi
    6. Vielezi Viigizi
      - Vielezi hivi huigiza sauti au mlio wa kitu, kitendo kitendo kilipofanyika kwa kutumia tanakali za sauti k.m: tuli, chubwi, tifu, chururu
      1. Mwanafunzi alitulia tuli mwalimu alipomzaba kofi pa!
      2. Kaswimu aliangusha simu changaraweni tifu na kujitumbukiza majini chubwi
    7. Vielezi vya Vielezi
      - Vielezi hivi hutumika kuelezea kielezi kingine. Hivyo basi, hutanguliwa na kielezi badala ya kitendo k.m: sana, kabisa, hasa, mno
      1. Mamake Kajino alitembea polepole sana.
      2. Chungu kilivunjika vibaya kabisa
    8. Vielezi vya Vivumishi
      - Hutoa habari zaidi kuhusu kivumishi k.m: sana, kabisa, hasa, mno
      1. Yeye ni mrefu sana
      2. Mtoto wake ana tabia nzuri mno


Viunganishi (U)

  • Viunganishi ni maneno yanayoutumika kuunganisha, kulinganisha au kuonyesha uhusiano wa dhana mbili au zaidi.

Aina za Viunganishi

  • Zifuatazo ni aina mbalimbali za viunganishi kulingana na matumizi yake

Kuonyesha Umilikaji

A-Unganifu Kiatu cha Mzee Sakarani kimepasuka.
KWA (umilikaji wa mahali) Mbinguni kwa Baba kuna makao mengi.

Kujumuisha

na Baba, mama na watoto huunda familia kamili.
pamoja na Mwizi aliiba runinga pamoja na redio
fauka ya, licha ya Fauka ya mapigo yote, Kafa alikatakatwa kwa kisu.
zaidi ya, juu ya Unataka nini tena zaidi ya mema yote niliyokutendea?
pia, vilevile Alimpiga mkewe na bintiye vilevile
mbali na Mbali na hayo nitakujengea nyumba ya kifahari.
aidha Keti akitoka shuleni atapika. Aidha atampelekea nyanya sukuma wiki.
wala (kukanusha) Ndege wa angani hawalimi wala hawapandi.

Kutofautisha

lakini, ila Ongea nayeilausimwambie mipango yetu.
bila Tasha aliondoka bila kusema lolote.
bali Sitawaacha kama mayatima bali nitawatumia msaidizi.
kinyume na, tofauti na Jana kulinyesha kinyume na utabiri wa hali ya hewa.
ingawa, ingawaje Nitamtembelea ingawa sijui nitamwambia nini.
japo, ijapokuwa Nakuomba upokee nilichokileta japo ni kidogo sana.
ilhali Fungo zimepotea ilhali zilikuwa zimewekwa vizuri.
minghairi ya Waliendelea kutenda dhambi minghairi ya kuhubiriwa kanisani.
dhidi ya Vita dhidi ya gonjwa hilo vingali vinaendelea.

Kuonyesha Sababu

ili Hanna aliumizwa ili asikumbuke aliyoyaona.
kwa, kwa vile Emili alinyamaza kwa vile kugombana na rafikize.
kwa maana, kwa
kuwa
Aria alipigwa na butwaa kwa maana mpenzi wake aligeuka kuwa mwalimu wake.
kwani Melisa alijificha kwani hakutaka kuonekana na Spensa.
kwa minanjili ya Chali alitembea mwendo huo wote kwa minanjili ya kuongea na Katosha.
maadam Wanawake katika familia hiyo hawali maini maadam mama mkongwe alilaani maini
katika familia hiyo.
madhali Madhali sote tuko hapa, tunaweza kuanzisha mkutano mapema

Kuonyesha Matokeo

basi, hivyo basi Umekula ng'ombe mzima, hivyo basi huna budi kumalizia mkia.
kwa hivyo Alipatikana na makosa ya kumnajisi bintiye, kwa hivyo akahukumiwa miaka kumi gerezani.
ndiposa Mama Kelele alipenda kuongea sana, ndiposa wakamkata midomo.

Kulinganisha

kama, sawa na Kunywa pombe ni kama kujichimbia kaburi mwenyewe.
kulingana na Mwalimu Makunza hafanyi kazi kulingana na maadili ya shuleni.
kuliko, zaidi ya Talia ni mfupi kuliko Nuru
vile Mganga Daimoni hutibu vile alivyofunzwa na Mganga Kuzimu.

Kuonyesha Kitu kimoja kama sehemu ya kingine

kati ya Vitatu kati ya vitabu hivi vimepigwa marufuku.
miongoni mwa Miongoni mwa walioachiliwa, ni Ngiri na Mende.
baadhi ya Baadhi ya wasichana kutoka Vikwazoni hawaheshimu miili yao.
mojawapo Mojawapo ya maembe uliyochuma yameoza.

Kuonyesha Kitu kufanyika baada ya kingine

kisha Soma mfano huu kisha usome sentensi ifuatayo.
halafu Alichukua kisu halafu akatokomea gizani.

Kuonyesha Kitu kufanyika badala ya kingine

badala ya Mapepo yalimchukua Shakawa badala ya bintiye
kwa niaba ya Mama Roga alitoa hotuba kwa niaba ya mumewe.

Kuonyesha Uwezekano

labda, pengine Sina pesa leo, labda uje kesho.
ama, au Ama Anita au Katosha anaweza kuja.
huenda Huenda kesho ikifika, Mungu atende miujiza.

Kuonyesha Masharti

bora, muradi Sitakuuliza bora tu usichelewe.
ikiwa, iwapo Ikiwa huna jambo muhimu la kusema, nyamaza.


Vihusishi (H)

  • Vihusishi ni maneno yanayotuarifu zaidi kuhusu uhusiano wa nomino na mazingira yake.

Aina za Vihusishi

  • Vihusishi vya Mahali
  • Vihusishi vya Wakati

Vihusishi vya Mahali

mbele ya, nyuma ya Kuna mzoga nyuma ya jengo hilo.
chini ya, juu ya Joto lilipozidi, watoto waliketi chini ya mti ule.
kando ya Kando ya mito ya Babeli ndipo tulipoketi.
karibu na, mbali na Fisi aliambiwa asile mifupa karibu namtoto yule.

Vihusishi vya Wakati

kabla ya Ni vizuri kusali kabla ya kula chakula.
baada ya Watoto safi hupiga meno mswaki baada ya kila mlo.


Vihisishi (I)

  • Vihisishi ni maneno yanayotumika kuonyesha hisia kama vile hasira, furaha, mshangao, kusifia, kushangilia n.k. Vihisishi hutambulishwa katika sentensi kwa kuambatanishwa na alama ya mshangao (!).
  • Kihisishi kimoja kinaweza kutumika kutoa hisia tofauti kulingana na muktadha.

Mifano ya Vihisishi

  • Ifuatayo ni baadhi ya mifano ya maneno yanayotumika kuonyesha hisia. Hata hivyo, maneno mengine yoyote yanaweza kutumika kama vihisishi, kulingana na mukhtadha. k.v Potelea mbali!
Kihisishi Mfano katika Sentensi Hisia
Lo! Lo! Maajabu ya Musa haya! mshangao
Salaale!,
Masalaale!
Salaale! Angalia watu wote hawa waliofika mahali hapa! mshangao
Kumbe! Nilidhani wewe ni rafiki yangu. Kumbe! mshangao
Po! Sijawahi kuona kijana mjeuri kama wewe. Po! hasira
Ng'o! Omba msamaha utakavyo, lakini unachoka bure. Ng'o! kiburi
Hata! Bwanake hakumwachia chochote! Hata! kusifia, kupuuza
Akh!, Aka! Mtoto mpumbavu huyu! Akh! hasira,
kukashifu
Ah! Ah! Sikuyaamini macho yangu. mshangao
Ala! Ala! Umefika tayari! mshangao
Haha! Haha! Umenivunja mbavu, bwana! kicheko
Ehee!, Enhe! Enhe! Endelea, ninaipenda sana hadithi hiyo! kuitikia
Hmmm! Hmmm! Chakula kitamu hicho! kuitikia, kusifia
Ebo! Ebo! Tabia gani hiyo. kukashifu,
hasira
Kefule! Kefule! Umenifedhehesha sana. hasira
Wee! Katamu alinegua kiuno na kucheza kwa madaha. Wee! Wavulana
wakaduwaa.
kusifia
La!, Hasha! La! Sitaki kusikiliza upuuzi wako tena. kukataa
Hoyeee! Wamama wote, hoyee! Hoyee! kushangilia
Huraa! Huraa! Tumeshinda. kushangilia
Join our whatsapp group for latest updates

Download Aina za Maneno - Sarufi na Matumizi ya Lugha Kiswahili Notes.


Tap Here to Download for 50/-




Why download?

  • ✔ To read offline at any time.
  • ✔ To Print at your convenience
  • ✔ Share Easily with Friends / Students


Get on WhatsApp Download as PDF
.
Subscribe now

access all the content at an affordable rate
or
Buy any individual paper or notes as a pdf via MPESA
and get it sent to you via WhatsApp

 

What does our community say about us?

Join our community on:

  • easyelimu app
  • Telegram
  • facebook page
  • twitter page
  • Pinterest