A. KUSOMA UFAHAMU (alama 15)
Soma makala yafuatayo kisha ujibu maswali yanayofuata.
Mihadarati ni kitu chochote ambacho huleta madhara kwenye mwili kinapotumiwa. Dawa hizi za kulevya zinaweza zikazoeleka zinapotumiwa kwa muda mrefu. Hali hiyo ya kutegemea dawa za kulevya inajulikana kama uraibu. Mifano ya mihadarati ni kama vile mandraksi, hashishi, gundi, mairungi, kokeini, marijuana, bangi, sigara na pombe. Mihadarati huingizwa mwilini kwa kutumia mbinu mbalimbali mathalani kumeza, kunywa, kunusa, kudungwa, kuchanganywa na chakula na kadhalika. Bila shaka, dawa hizi zina madhara chungu nzima kwa mtumiaji, jamii na taifa kwa jumla.
Naam, mihadarati imewasababishia watumiaji matatizo kwa sababu wao hutumia pesa nyingi kununua dawa hizi. Wanavyoendelea kuzitumia ndivyo pesa zao zinavyozidi kupungua na hatimaye wanakuwa maskini. Dawa hizi pia husababisha maradhi mengi. Kwa mfano, sigara husababisha saratani ya midomo, koo na mapafu. Tujuavyo maradhi haya hufanya mtumiaji akonde na kubaki akiwa karibu kufa. Navyo vileo kama pombe husababisha saratani ya ini, shinikizo la damu na mshtuko wa moyo. Hali ikiwa mbaya, wengine hurukwa na akili na kuwa wendawazimu.
Vilevile, si ajabu kuwaona vijana wengi wakijiingiza katika utumiaji wa pombe. Wengine wao hulazimika kuanza uhalifu kama wizi au unyang'anyi ili waweze kupata pesa za kununulia dawa hizi. Haya huwafanya wengi wao kupigwa na watu au kutiwa mbaroni. Idadi kubwa ya vijana vilevile hulazimika kuacha masomo yao. Hakuna anayeweza kuendelea na masomo vizuri ikiwa anatumia dawa za kulevya. Isitoshe, ingawa ajali haina kinga, wakati mwingine ajali nyingi zinaweza kuepukika. Ikumbukwe kuwa, ajali nyingi husababishwa na madereva waliolewa au wapitanjia walevi. Ajali kama hizi huwasababishia wengi ulemavu ambao hawakuzaliwa nao au wakati mwingine kifo cha kujitakia wenyewe.
Halikadhalika, ulevi na uraibu wa vileo hivi hufanya familia kuharibika. Ikiwa wazazi wote au mmoja anashiriki ulevi kupita kiasi, familia haiwezi kuishi vizuri. Watoto watakosa mwelekeo na kielelezo maishani. Watakosa malezi mema na kwa hivyo kupotoka kimaadili. Maisha yao yatakuwa ovyo na kukosa maana. Licha ya hayo, waliooana nao huachana. Ni vigumu sana kwa mtu yeyote kuvumilia visanga na vitimbi vya anayeitumia mihadarati kila wakati. Mtu anayeshinda vilabuni akinywa pombe hatunzi familia yake ipasavyo. Ni mara ngapi umesikia wanaume ambao wameshindwa kudumisha ndoa zao? Kweli, anasa hunasa. Aidha, siku hizi si jambo la ajabu kuwaona kina mama wajawazito wakishiriki ulevi wa kila aina. Kunena waziwazi, jambo hili huhatarisha maisha ya mtoto aliye tumboni. Mimba nayo inaweza kuharibika au mtoto kuzaliwa akiwa na kasoro chungu nzima. Mbona utese malaika kama huyo bila sababu?
Fauka ya hayo, waja wengi hudanganyika kuwa watumiapo dawa hizi watasahau shida zao. Kujidanganya huku huwa ni kwa muda mfupi. Mara wanapokumbuka hujikuta na shida nyingi zaidi au wakati mwingine kujiletea aibu isiyo na mfano. Kando na hayo, uchumi pia huharibika kwani wanaotumia mihadarati hawafanyi kazi kwa bidii. Kwa hivyo, hawachangii kuleta maendeleo. Serikali nayo hutumia hela nyingi kwa matibabu ya wagonjwa na kuanzisha vituo vya ushauri nasaha. Isitoshe, fedha ambazo zingetumiwa na mtu binafsi kuanzisha biashara hutumika kununua vileo. Kumbuka kinga na kinga ndipo moto uwakapo. Ama kweli mihadarati ina athari tele. Enyi vijana, msiwe bendera ya kufuata upepo. Jiepusheni na janga hili linalotukodolea macho likiwa tayari kutumeza wazimawazima. Zingatieni ya wahenga kuwa
kinga ni bora kuliko tiba.
- Kifungu kinaeleza kuwa dawa za kulevya zinapotumika kwa muda mrefu husababisha nini? (alama 1)
- Kifungu kinaeleza kuwa dawa za kulevya husababisha madhara kwa _________________ na ________________(alama 1)
- Ni kweli kuwa mihadarati husababisha umaskini. Eleza njia mbili zinazofanya mihadarati isababishe umaskini. (alama 2)
- Mtu mwenye mazoea ya kunywa pombe anaweza akaambukizwa ugonjwa gani? (alama 1)
- Eleza maana ya nahau 'kutiwa mbaroni' jinsi ilivyotumika katika kifungu. (alama 1)
- Andika madhara mawili ya matumizi ya dawa za kulevya kulingana na aya ya tatu. (alama 1)
- Mwandishi angetumia neno gani jingine. lenye maana sawa na 'familia'? (alama 1)
- Watoto huathirika vipi iwapo wazazi wao ni watumiaji wa dawa za kulevya? (alama 1)
- Kulingana na kifungu, kwa nini mwanamke mjamzito anashauriwa kujiepusha na matumizi ya dawa za kulevya? (alama 1)
- Matumizi ya dawa za kulevya hurudisha nyuma utendakazi kazini. Eleza kauli hii. (alama 1)
- Eleza maana ya neno 'uraibu' jinsi lilivyotumika katika kifungu. (alama 1)
- Andika faida moja inayoweza kupatikana kwa serikali ikiwa kila mkenya atajiepusha na matumizi ya dawa za kulevya.
(alama 1) - Methali 'kinga na kinga ndipo moto uwakapo' inatoa funzo gani? (alama 1)
- Andika mada inayofaa kwa kifungu hiki. (alama 1)
B. UFUPISHO (alama 5)
- Soma kifungu kifuatacho kisa ukifupishe kwa maneno hamsini.
Juma alionekana akiwa amekaa chini ya mti. Hiyo haikuwa siku yake ya kwanza kuonekana akiwa katika hali hiyo. Alikuwa amekaa hivyo kwa takriban wiki mbili mtawalia. Alikula kwa nadra sana. Hakucheka wala kucheza na wanafunzi wenzake. Hakuonakana uwanjani akifanya mazoezi kama ilivyokuwa desturi yake hapo awali. Naima, aliyekuwa rafiki yake wa chanda na pete, aliingiwa na wasiwasi. Alimwuliza iwapo alikuwa na shida. Hata hivyo, Juma alisisitiza kuwa hakuwa na tatizo lolote. Naima aliuliza wanafunzi walioishi karibu na nyumbani kwa akina Mrisi lakini nao hawakuwa na mwao.
Siku moja wakati wa wikendi, Naima alienda kuongea na kaka wa Juma. Hapo ndipo alipobaini tatizo kuu. Kumbe alilemewa na hisia za huzuni baada ya kutofanya vyema katika mchezo wa kandanda. Baadhi ya wanafunzi wakiongozwa na Moira - walimcheka sana. Naima alichukua hatua ya kuzungumza na Juma. Alimshauri kuwa ni vyema akabiliane na hisia za huzuni na kuzidhibiti. Aidha, alizungumza na kundi la Moira. Aliwashika sikio na kuwaonya dhidi ya hulka za aina hiyo. Vijana hao walitamani sana mwalimu wao wa darasa asijue. Mwalimu wa darasa alikuwa simba; hakupenda tabia zisizokuza umoja na ushirikiano.
Walipofika shuleni, Naima alimwelekeza Juma hadi kwa mwalimu wao wa ushauri nasaha. Walimsimulia yaliyojiri tangu awali hadi aheri. Juma alieleza jinsi alivyoshindwa kukabiliana na hisia za huzuni na aibu. Mwalimu alimfafanulia kuwa ni muhimu kukabiliana na hisia zinazotokana na kushindwa. Aidha, alieleza kuwa hisia zitokanazo na ushindi au ufanisi zinafaa kukabiliwa kwa njia inayofaa. Kaka wa Juma alipongezwa sana na mwalimu kwa kueleza tatizo la Juma. Naima naye alipewa shukrani na mwalimu kwa kuwa rafiki wa kweli. Wawili hao waliitwa mbele ya wanafunzi wenzao na kupongezwa kwa kuwa na tabia za kuwajali na kuwafaa wenzao. Moira na wenzake nao walionywa dhidi ya kuwacheka wenzao wanaokumbwa na changamoto.
Ufupisho uwe aya moja, uhusu mambo makuu katika kifungu na kuakifishwa kwa njia inayofaa.
C. MATUMIZI YA LUGHA (alama 40)
Kuanzia nambari ya 16 -50, jibu swali kulingana na maagizo.
- Zifuatazo ni nomino za kawaida isipokuwa; (alama 1) kitana, nyumba, maji, gari
- Andika kipengele kimoja cha kuzingatia wakati wa kusikiliza mazungumzo. (alama 1)
- Tumia nomino ifuatayo kutunga sentensi. (alama 1) Kenya
- Andika kipengele kimoja cha kuzingatia wakati wa kujibu mazungumzo. (alama 1)
- Kijana kwenye mchoro ufuatao anafanya nini? (alama 1)
- Eleza maana ya usafi wa kibinafsi. (alama 1)
- Alama ifuatayo ya kuakifisha inaitwaje? (alama 1)
- Andika matumizi mawili ya herufi kubwa. (alama 2)
- Akifisha sentensi ifuatayo. (alama 2) njeri na omari watazuru mji wa mombasa siku ya alhamisi
- Andika mifano miwili ya nomino za pekee. (alama 1)
- Pigia mstari nomino ya makundi kwenye sentensi ifuatayo. (alama 1)
Mtoto huyo aliona thurea ya nyota angani, siku ya Alhamisi. - Andika mifano miwili ya nomino za kawaida. (alama 1)
- Tunga sentensi ukitumia nomino ifuatayo. (alama 1) furaha
- Chagua nomino ambayo haifai kuwa kwenye kundi lifuatalo. (alama 1) [kalamu, mwalimu, Disemba]
- Pigia mistari sauti zinazokaribiana kwenye jozi ifuatayo ya maneno. (alama 1) thamini dhamini
- Jina lingine la nomino za makundi ni gani? (alama 1)
- Andika mifano miwili ya msamiati unaohusu lishe bora. (alama 1)
- Tumia nomino ifuatayo kutunga sentensi. (alama 1) mswaki
- Eleza umuhimu wowote wa barua ya kirafiki ya kutoa mwaliko. (alama 1)
- Kamilisha nomino zifuatazo kwa usahihi. (alama 1)
- Kicha cha
- Umati wa
- Andika mifano miwili ya nomino za dhahania. (alama 1
- Eleza maana ya fasihi. (alama 1)
- Taja tanzu mbili za fasihi. (alama 2)
- Ushairi simulizi, mazungumzo, maigizo na semi ni mifano ya utanzu gani wa fasihi? (alama 1)
- Novela, riwaya, tamthilia na hadithi fupi ni mifano ya utanzu gani wa fasihi? (alama 1)
- Eleza maana ya novela. (alama 1)
- Andika sifa mbili za novela. (alama 2)
- Andika mifano miwili ya nomino za wingi. (alama 1)
- Kusoma, kuimba na kutembea ni mifano ya aina gani za nomino? (alama 1)
- Tunga sentensi ukitumia nomino ifuatayo. (alama 1) unga
- Tumia nomino ifuatayo kutunga sentensi. (alama 1) kuimba
- Andika sifa yoyote moja ya fasihi simulizi. (alama 1)
- Nomino 'maradhi' hupatikana katika ngeli gani? (alama 1)
- Andika katika wingi. (alama 1)
Sahani yake imewekwa ndani ya kabati. - Rekebisha sentensi ifuatayo. (alama 2) Pale nyumbani kuna wageni wenye wanasikiliza wimbo.
MARKING SCHEME
- uraibu au hali ya kuzoea dawa za kulevya
- mtumiaji, jamii, taifa
- dawa za kulevya hununuliwa kwa pesa nyingi, wanaotumia dawa za kulevya huwa hawafanyi kazi kwa bidii, serkall hutumia pesa za maendeleo kuwahudumia walioathiriwa
- saratani ya ini, shinikizo la damu, mshtuko wa moyo
- kushikwa na polisi
- husababisha uhalifu (wizi, unyang'anyi). kupigwa au kutiwa mbaroni, kuacha masomo, husababisha ajali
- ayali, aila, ahali
- familia huharibika, watoto hukosa mwelekeo na kilelezo, watoto hukosa malezi mema na kupotoka
- mihadarati huhatarisha maisha ya mtoto allye tumboni, mimba huweza kuharibika, mtoto huweza kuzaliwa akiwa na kasoro
- Wanaotumia mihadarati haafanyi kazi kwa bidii
- ni hali ya kutegemea dawa za kulevya
- serikali haitatumia pesa nyingi kwa matibabu ya wagonjwa au kuanzisha vituo vya ushauri nasaha.
- ni vyema tushirikiane tunapokabiliana na mihadarati
- athari za mihadarati, mihadarati, dawa za kulevya (tathmini mada yoyote inayoafiki)
- Ufupisho ujumuishe habari kuu, uwe kwa aya moja, utumie alama za kuakifisha na viunganishi mwafaka
- maji
- kuepuka vizuizi vya mazungumzo, kusikiliza kwa makini, kumtazama mzungumzaji ana kwa ana na kadhalika
- tathmini usahihi wa sentensi
- ubadilishanall zamu unaofaa, kutumia lugha ya adabu, kujikita kwenye kiini cha mazungumzo na kadhalika
- anapenga kamasi
- ni njia za kudumisha usafi wa mtu anayerejelewa
- kitone, kikomo, kitone
- Hutumika mwanzoni mwa sentensi kuanzisha nomino maalum, katika akronimu na ufupisho
- Njeri na Omari watazuru mil wa Mombasa siku ya Alhamisi.
- Tathmini mifano hiyo kama vile Ijumaa, Nairobi na kadhalika
- thurea ya nyota
- Tathmini mifano hiyo kama vile kalamu, darasa na kadhalika
- Tathmini sentensi hiyo
- Disemba
- tha, dha
- nomino za jamii
- Tathmini msamiati huo kama vile vitamini, matunda, mboga, maji na kadhalika
- Tathmini sentenai hiyo
- hudumisha uhusiano bora, husaidia kutoa mwaliko na kadhalika
- kicha cha funguo/mboga, umati wa watu
- Tathmini mifano hiyo kama vile furaha, amani na kadhalika
- Fasihi ni somo linalohusiana na tungo za sanaa kama vile tamthilia na riwaya.
- fasihi andishi na fasihi simulizi
- fasihi simulizi
- fasihi andishi
- Novela ni utungo ullo mrefu kuliko hadithi fupi lakini mfupi kwa riwaya, huweza kusomwa kwa kikao kimoja
- Huwa na wahusika wachache, huwa na maudhui machache, huwa na mandhari machache na kadhalika
- Tathmini mifano hiyo kama vile maji. unga, sukari na kadhalika
- vitenzijina
- Tathmini sentensi hiyo
- Tathmini sentensi hiyo
- huwasilishwa kwa maneno ya mdomo, ni mali ya jamii, huhifadhiwa kwenye ubongo na kadhalika
- Ngeli ya YA-YA
- Sahani zao zimewekwa ndani ya makabati.
- Nyumbani pale pana wageni ambao wanasikiliza wimbo/ Nyumbani kule kuna wageni ambao wanasikiliza wimbo.
Download Kiswahili Questions and Answers - Grade 7 End Term 1 Exams 2023 Set 1.
Tap Here to Download for 30/-
Get on WhatsApp for 30/-
Why download?
- ✔ To read offline at any time.
- ✔ To Print at your convenience
- ✔ Share Easily with Friends / Students