MASWALI
SEHEMU A: RIWAYA
- Lazima
K. Walibora: Kidagaa Kimemwozea.
"Labda ni suala la mzigo wa mwenzio kanda la usufi."
"... Sijui 'mwenyewe' aliyetajwa ... ni nani. Lakini sharti awe mtu ambaye kwake msiba kwa wengine kwake arusi."- Fafanua muktadha wa dondoo hili. (alama 4)
- Bainisha tamathali mbili za usemi zinazojitokeza katika dondoo hili. (alama 2)
- Jadili jinsi ambavyo hali ya, 'msiba kwa wengine kwake arusi', inavyojitokeza katika Kidagaa Kimemwozea. (alama 14)
SEHEMU B: TAMTHILIA
T.Arege: Mstahiki Meya
Jibu swali la 2 au la 3 - "Waache wagome, watajiponza wenyewe."
- Eleza muktadha wa dondoo hili. (alama 4)
- Dondoo hili linadokeza mojawapo ya mbinu hasi za utawala. Iandike. (alama 2)
- Fafanua mbinu nyingine saba hasi za utawala zilizotumiwa katika tathmilia hii. (alama 14)
- " Ngoja ngoja huumiza matumbo." Thibitisha kauli hii kwa kurejelea tamthilia ya Mstahiki Meya.
SEHEMU C: HADITHI FUPI
K. Walibora na S.A Mohammed: Damu nyeusi na hadithi Nyingine.
Jibu swali la 4 au la 5.
"Maskini, Babu yangu!" (K.Walibora) -
- "Salalaa! Mbona wasirudi kwao waishi maisha ya maana kidogo."
- Eleza muktadha wa dondoo hili. (alama 4)
- Fafanua umuhimu wa mzungumzaji katika hadithii hii. (alama 8)
- "Shangazi wakumbuke watoto. Waonee huruma!"
- Andika tamathali ya usemi inayojitokeza katika kauli hii kwa kurejelea hadithi: "Samaki wa Nchi za Joto." (alama 2)
- Bainisha matumizi mengine matatu ya tamathali hii ya usemi katika hadithi hii. (alama 6)
- "Salalaa! Mbona wasirudi kwao waishi maisha ya maana kidogo."
- "Hutaki kuwaeleza, kuwa meridhika, oo 'ridhika."
Eleza kiyume kinachojitokeza katika maneno yaliyopigiwa mstari kwa kurejelea hadithi hii. (alama 20)
SEHEMU D: USHAIRI
Jibu swali la 6 au swali la 7. - Soma shairi lifuatalo kisha ujibu maswali.
Amiri A.S Andanenga: Sauti ya Kiza- Ngakua na mato, ya kuonea
Ngalisana kito, cha kuchezea
Kilicho kizito, cha kuelea
Kikamuenea, akivae. - Makusudi yangu, ngaliandaa
Ngafinyanga chungu, cha mduwaa
Ngatia vitangu, vinavong'aa
Ili ziwe taa, kwa apikae. - Mkungu wa tano, wa mduwara
Ulo bora mno, kisha imara
Ulo na maono, kuwa ni dira
Kwenye barabara, itindiae. - Ngaomba baraka, kwake Rabana
Punje za nafaka, kila aina
Chunguni kuweka, kwa kulingana
Hajaangu suna, yule alae. - Ngafanya bidii, kwenda mwituni
Sio kutalii kukata kuni
Ya miti mitii, huko jikoni
Isio na kani, ni iwakae. - Kwa yangu mabega, nikathubutu
Ngabeba mafiga, yalo matatu
Bila hata woga, kwenye misitu
Simba tembo chatu, sinitishie. - Miti yenye pindi, na jema umbo
Ngajenga ulindi, mwema wimbowimbo
Fundi aso fundi, penye kiwambo
Moyo wenye tambo, apekechae. - Singaajiri, ngachimba mimi
Kisima kizuri, cha chemichemi
Maji ya fahari, ya uzizimi
Jua la ukami, siyaishae. - Tamati na funga, kwa kuishia
Mato ndo malenga, kanikimbia
Nahofu kutunga, mabeti mia
Asije chukia, ayasomae.
- Eleza ujumbe wa shairi hili. (alama 2)
- Kwa kurejelea ubeti wa pili, eleza umuhimu wa aina mbili za uhuru wa kishairi alioutumia mshairi. (alama 4)
- Andika ubeti wa saba kwa lugha ya nathari.(alama 4)
- Eleza toni ya shairi hili. (alama 2)
- Fafanua aina tatu za urudiaji zilizotumiwa katika shairi hili. (alama 6)
- Bainisha nafsineni katika shairi hili. (alama 2)
- Ngakua na mato, ya kuonea
- Soma shairi lifuatalo kisha ujibu maswali.
T.Arege: Watafuta Riziki- Watafuta riziki, watokwa jasho vijijini
Wakulima shakiki, wakuza chai na mibuni
Vyakula wahakiki, visipungue vinyuani. - Watafuta riziki, wahangaikao mjini
Kutwa kile na hiki, kama watanga na mpini
Japo hawasikiki, hawakosi kujiamini. - Watafuta riziki, wazalendo wa nchi hii
Kamwe hawajidhiki, tama za moyo kutii
Bali huafiki, kupingana na ulaghai. - Watafuta riziki, pato ambalo la halali
Ndoto hazimiki, ya kesho kuwa njema hali
Wiki baada wiki, la haramu jasho hawali.
- Fafanua sifa tano za watu wanaozungumziwa katika shairi hili. (alama 5)
- Bainisha umuhimu wa tamathali tatu za usemi zilizotumiwa katika shairi hili. (alama 6)
- Eleza kwa kutoa mifano, mbinu tatu mshairi ametumia kutosheleza mahitaji ya kiarudhi. (alama 6)
- Ainisha shairi hili kwa kuzingatia vigezo vifuatavyo: (alama 3)
- idadi ya mishororo katika ubeti
- mpangilio wa vina
- mpangilio wa maneno
SEHEMU E: FASIHI SIMULIZI.
- Watafuta riziki, watokwa jasho vijijini
- Soma hadithi hii kisha ujibu maswali.
Basi Mulungu akamtuma kinyonga duniani kumpasha binadamu ujumbe ufuatao: "Maisha yako hayatakuwa na mwisho, hata ukifa utafufuka."
Kinyonga akaondoka kama mshenga apelekaye posa. Akatambaa polepole, moyoni amejawa na hofu ya kuiharibu ardhi ya wenyewe. Hata alipowafikia binadamu machweo ya usiku wa saba baada ya kupashwa ujumbe, alimpata mnana keshaubatilisha ujumbe huo; ameisha kumwambia binadamu kuwa akifa atatokomea kama mizizi ya msubili. Huo ndio ukawa mwanzo wa mauti.- Andika aina ya hadithi hii. (alama 2)
- Fafanua umuhimu wa aina hii ya hadithi katika jamii. (alama 10)
- Eleza majukumu manne ya fomyula ya kumalizia katika ngano. (alama 8)
- Soma hadithi hii kisha ujibu maswali.
Mwongozo wa Kusahisha
-
-
- Kauli ya kwanza ni ya Amani kwa Imani.
- Kauli ya pili ni ya Imani.
- Anamwambia Amani.
- Anamhadithia Amani kuhusu kadhia iliyompata; kupigwa kwa mama yake, kufa kwa mama yake, na kuchomewa nyumba, kisha kukashifu hali ya wanakijiji cha Baraka kutotenda lolote kumtetea.
- Wamo kibandani mwa Amani.
- Imani anashangaa ni nani aliyewatuma askari kutekeleza matendo haya ya kinyama.4 x 1 = 4
Tanbihi
Dondoo limetolewa uk. 58.
-
- Kinaya - mtu kufurahia msiba wa wengine.
- Tanakuzi - msiba na arusi ni vinyume - kuonyesha uovu/ugumu wa moyo.
- Sitiari
- msiba - matatizo
- arusi - furaha
- mzigo wa mwenzio kanda la usufi - kudunisha matatizo ya wengine.
- msiba kwa wengine kwake harusi - kufurahia matatizo ya wengine.
- Methali, “Mzigo wa mwenzio ni kanda la usufi”, imedokezwa na kauli, ‘Mzigo wa mwenzio kanda la usufi.’2 x 1 = 2
-
- Raia wa Baraka, badala ya kumpoza Imani kwa kuchomewa nyumba, wanaogopa hata kuonekana wakizungumza naye, wanaaendelea tu na shughuli zao.
- Viongozi wanawadhulumu hata wasio na chochote. Nasaba Bora anawadhulumu akina Imani shamba lao na kujifaidi kwalo.
- Nasaba Bora anamuua Chichiri Hamadi ili kunyakua mali yake.
- Baadaye Yusufu anasingiziwa mauaji haya na anafungwa.
- Nasaba Bora anampagaza Amani malezi ya Uhuru huku akijua mtoto si wa Amani. Hata anamtarajia Amani kuendelea na kazi yake ya uchungaji pamoja na ulezi huu.
- Nasaba Bora anashirikiana kimapenzi na msichana mchanga - Lowela - bila kujali mustakabali wake.
- Nasaba Bora anakitupa kitoto chake mlangoni pa Amani ili kujitoa lawamani bila kuwazia afya yacho.
- Nasaba Bora anamwachia mkewe upweke huku akitafuta raha kwa wasichana wadogo kama vile Lowela.
- Nasaba Bora anampiga Amani kikatili kwa shutuma zisizo na ithibati na kumtupa; anachojali ni kulipiza kisasi tu.
- Fao anamwendea kinyume mwanafunzi wake kwa kuhusiana naye kimapenzi bila kujali unyonge wake kama mwanafunzi. Anapomtunga mimba anaondoka bila kujali hali ya mtoto na mama yake.
- Michelle anakataa posa ya Majununi hata baada ya Majununi kujikalifu kujenga jumba ili kutimiza masharti yake.
- Majisifu anamwibia Amani mswada na kujifaidi kwao, hajali yatakayompata Amani.
- Majisifu, badala ya kuhudhuria madarasa, anaingilia ulevi bila kujali maendeleo ya wanafunzi wake.
- Wenzake Amani chuoni wanamsingizia uchochezi na kumfanya kufungwa na kukatiza masomo yake.
- Nasaba Bora anawafungia Amani na Imani kwa madai kwamba wamekiua kitoto japo kimekufa kwa kichomi. Askari kuwabeza Amani na Imani.
- Wauguzi hospitali wanakosa kukitibu kitoto, wanasema ni sikukuu, hawafanyi kazi, na kusababisha kifo chacho, huku wakiendelea na shughuli zao.
- Serikali inawatelekeza wazalendo, kama vile Matuko Weye, hata anafungiwa anaposema ukweli kuwahusu viongozi.
- Nasaba Bora anamtaliki mkewe kwa shutuma ambazo hata hajathibitisha, licha ya kwamba mkewe amekuwa mwaminifu kwake. Yeye Nasaba Bora anaendelea na uhusiano wake na Lowela.
- Serikali inawatelekeza wachezaji kama vile Makweche katika umaskini na ugonjwa hata baada ya kuiletea nchi sifa. Makweche anaishia kukatwa mguu.
- Askari wanampiga mamake Imani machoni pake bila kujali dhiki ya kisaikolojia wanayomsababishia. Baadaye Mama Imani anakufa kwa maumivu haya.
- Oscar Kambona, baada ya kuuawa kwa mama yake, anaondoka bila kuaga, anamwachia Imani ukiwa.
- Wahudumu katika zahanati hawamshughulikii DJ. DJ analazimika kuondoka hospitali kutafuta matibabu kwingine.
- Serikali, badala ya kufadhili elimu ya maskini, inatumia pesa hizi kudhamini elimu ya wanaojiweza kama vile Fao. Fao anapelekwa kusomea ng’ambo.
- Nasaba Bora anawashurutisha raia kuchangia elimu ya mwanawe - Madhubuti, hajali hali yao duni kiuchumi. Madhubuti anakwenda kusomea Urusi.
- Majisifu anawadharau wanawe wenye mahitaji maalum. Anamwachia mkewe ulezi bila kujali dhiki anazomsababishia. Hawapeleki wanawe shuleni au kwa uangalizi maalum.
- Nasaba Bora, badala ya kuwahudumia raia katika afisi za Wizara ya Ardhi anaficha faili na kuwalazimisha kutoa hongo ili kuhudumiwa.
- Nasaba Bora hajali afya ya majibwa yake, hayachanji.
- Nasaba Bora anawafuta wafanyakazi wake kiholela, hata kwa kunadhifisha maskani yake, hajali watapata wapi riziki.
- DJ kuumwa na jibwa na mtemi hajali.
- Mtemi kumpita mama anayejifungulia njiani huku mvua ikinyesha. Hajali kumsaidia hata anaponasihiwa na mkewe.
- Wazungu kunyakua mashamba ya Waafrika.
- Wazungu kuwakataza Waafrika kufuga na kupanda baadhi ya mimea.
- Mashaka kuwabeza watoto walemavu wa Majisifu.
- Majisifu anaposhindwa kutoa mhadhara wanafunzi wanamcheka /wanamkejeli.
Tanbihi- Mtahiniwa anaweza kuonyesha:
Tendo la kikatili linaloelekezwa kwa mhusika au kundi fulani, kwa faida ya anayetenda tendo hilo,
Au
Aonyeshe hali ya mapuuza au dhuluma inayosababisha kuhasirika kwa mwingine. - Si lazima anayetenda tendo hilo la kikatili afaidike moja kwa moja. Mtahiniwa anaweza kujadili tu namna mhusika anavyomdhulumu mwingine bila kujali, au kuwazia uchungu anaomsababishia.7 x 2 = 14
- Mtahiniwa anaweza kuonyesha:
-
-
-
- Ni maneno ya Diwani I.
- Anamwaambia Meya, Diwani II na Diwani III.
- Wamo ofisini mwa Meya.
- Meya amewaita ili kutafuta njia ya kuwadhibiti watu ambao anadai wamechochewa na baadhi ya madiwani kulalamikia hali ya Baraza kushindwa kutimiza majukumu yake.
- Meya anawauliza wafanye nini, ndipo wanaanza kutoa maoni, na Diwani I kusema haya.4 x 1
Tanbihi
Dondoo limetolewa Uk. 21.
- Matumizi ya vitisho. Diwani I anasema watakaogoma watafutwa.
Au
Kuwanyanyasa/kuwaangamiza wanaotetea haki - Diwani anataka kuwadhibiti wafanyakazi kwa kuwafuta. -
- Hila/udanganyifu/unafiki. Meya anamwambia Siki kwamba ana akili, ndio maana watu wakamchagua, Meya anaahidi dawa ambazo hazimo, ili watu watulie.
- Uteuzi wa washauri ambao ni vibarakala wa Meya. Diwani I anasema kwamba jukumu lao ni kuhakikisha wamelilinda Baraza la Mstahiki Meya, kwamba wanalipwa kwa sababu hii.
-
- Propaganda - kuwatangazia kujitolea kwa Baraza kutetea demokrasia, na hali sivyo.
- Mashindano kupeperushwa moja kwa moja kupitia vyombo vya habari ili kuibua hisia za uzalendo.
- Uundaji wa kamati za kuhudumu (za madiwani).
Madiwani wenye ushawishi mkubwa wanateuliwa kuongoza kamati hizi ili kusiwe na upinzani. Meya hajali pesa zitakazotumiwa kuendesha kamati hizi. - Hongo/vishawishi. Meya anaidhinisha nyongeza ya mishahara ya madiwani na kutotozwa kodi kwao ili wamuunge mkono.
- Meya anakabiliana na migomo ya wafanyakazi kikatili (kupigwa). Askari wanawatawanya wafanyakazi waliogoma.
- Dini - Mhubiri anahongwa ili kumuunga mkono.
- Kuunda sheria ambayo inampa Meya mamlaka makubwa yanayomfanya kuongoza kwa mabavu. Mayors Act inampa mamlaka ya kumnyamazisha yeyote anayempinga. Meya ndiye mwenye mamlaka juu ya ugavi wa viwanja vya umma, hivyo anaufisidi uchumi wa Cheneo kwa kujigawia viwanja na kumgawia Bili pia.
- Kuwatenga washauri/viongozi wanaompinga Meya. Maamuzi yanayohusiana na matumizi ya pesa yanatolewa na Meya, Diwani I, Diwani II huku wanamtenga Diwani III ambaye ndiye kinara wa masuala ya fedha. Kwa njia hii Meya anaweza kutoa maamuzi yanayomfaa yeye na vikaragosi wake bila pingamizi.
- Kujilinganisha na mataifa dhaifu kiuchumi ili kuonekana na raia kwamba wameendelea. Meya anasema kwamba Cheneo ni kisiwa chenye amani, huku Siki akimwonya dhidi ya kujilinganisha na chumi dhaifu. 7 x 2 = 14
-
-
- Wagonjwa wanaambiwa wangojee dawa zilizoangizwa, ambazo kwa kweli hazijaagizwa baadhi wanaishia kufa - yule mtoto (Dadavuo).
- Kutoshughulikiwa kwa mishahara duni ya wafanyakazi na kutoboreshwa kwa hali yao ya maisha na utendakazi kunasababisha mgomo wa wafanyakazi.
- Malimbikizo ya mishahara yanawafanya wafanyakazi kukata tamaa, na baadhi yao, kwa mfano Waridi, wanajiuzulu, wengine wanagoma.
- Kutoboreshwa kwa maisha ya wafanyikazi kunawafanya kuishi maisha yasiyo na hadhi. Wanakula makombo (yaliyoharibika) kwa waajiri. (mf. Mama mtoto).
- Wafanyakazi wanakosa vifaa vya kufanyia kazi. Wanadai subira yao imeisha. Mji unaenea uchafu.
- Wafanyakazi wanaposita kuzoa taka mji unarundikana uchafu. Uvundo unaenea hadi afisini mwa Meya.
- Kurundikana kwa uchafu, na tishio la mkurupuko wa magonjwa unawafanya wageni kutozuru Cheneo. Meya anaaibika.
- Meya anapuuza ushauri wa Diwani III kuhusu matumizi ya fedha na kulisababishia Baraza nakisi ya pesa/ Siki kumshauri Meya mara kwa mara na ushauri kupuuzwa.
- Meya anakosa kuona udanganyifu wa Bili, anaishia kusababisha kuibwa kwa fimbo yake mwenyewe ambayo ndiyo kiwakilishi cha umeya.
- Raia wanapuuza umuhimu wa kuwachagua viongozi waadilifu. Wanawachagua viongozi dhalimu na kurithisha uongozi mbaya kwa kuwachagua wabaya wakijua tu ni wabaya.
- Wanataaluma wanakataa kuingia katika siasa (mf. Siki), nchi inakosa huduma yao, uongozi mbaya unaendelezwa zaidi.
- Meya anapuuza mpango wa maendeleo wa miaka kumi (wa mji), akidai wao wanathamini malengo ya kimilenia. Cheneo inashindwa kuzua mipango ya kuzalisha pesa/pato la kuongezea mishahara ya wafanyakazi.
- Meya anakosa kudhibiti tamaa yake, anamruhusu Bili kumshawishi kulipagaza Baraza deni kupitia ile kesi ya mwanakandarasi. Meya anafaidika huku uchumi wa Cheneo ukidorora.
- Meya anashindwa kuurekebisha uongozi wake licha ya ushauri wa Siki na Diwani III. Anaupujua (anaudhoofisha) uongozi wake, na kuishia kung’olewa uongozini.
- Meya anashawishiwa na Diwani I na II kuunda kamati nyingi, hawazii umuhimu wa kamati hizo. Anaishia kuifilisi hazina ya baraza.
- Kutodhibiti mgomo wa wafanyakazi kwa kushughulikia malalamishi yao kunasababisha kutokusanywa kwa kodi, Baraza linapoteza fedha.
- Baraza linashindwa kudhibiti usalama mjini. Askari wameutwaa mji. Wanawafukuza wafanyakazi, wanawafanya watu kukaa tu nyumbani, kutazama matukio yanavyoendelea (Mfano Diwani III).
- Meya anapuuza umuhimu wa madiwani kulipa kodi na kusababisha kuzorota kwa pato la Baraza.
- Meya, badala ya kuzalisha pesa kulipia mishahara, anategemea kuzipata kutoka kwa wafadhili/washirika wao wa kimaendeleo. Hawazi kuwa huu ni mzigo anaovirithisha vizazi vya kesho. Anapalilia hali ya utegemezi.
- Hali ya baadhi ya wanyonge kujiwazia wao wenyewe inafanya hali ya jamii ya wanyonge kutobadilika. Dida anasema kwamba hajali hali ya Meya kuwapeleka watu wake mbali na uvundo wa mji, mradi mameya waendelee kuwepo naye aendelee na kazi yake duni ya kunadhifisha nyumba zao.
- Meya anapuuza umuhimu wa kutumia pesa za umma vyema. Anabadhiri pesa kwa kumpeleka Bili kujistarehesha na kumpeleka mkewe kuzalia ng’ambo.
- Meya, anaendeleza hali duni ya elimu, badala ya kuiboresha, anawapeleka wanawe kusomea ng’ambo.
- Meya anapuuza athari za mgomo wa wafanyakazi/anapuuza umuhimu wa wafanyakazi wa kima cha chini. Anamwambia Diwani III kwamba hata wakigoma, watarudi baada ya siku chache; kwamba mahitaji ya kimsingi yatawasukuma kurudi kazini. Hili linaathiri utendakazi wa Baraza, pia linasababisha kuong’olewa mamlakani kwake.
- Meya anakataa kushughulikia changamoto za leo. Anasema kesho ... na mtondogoo hawatakuwepo, hivyo haina haja kujidhiki. Mtazamo huu wake ndio unaofanya uozo Cheneo kuongezeka, na kuangamia kwa uongozi wake.
- Badala ya Meya kuhifadhi hazina ya Baraza, anaifilisi zaidi kwa kumpa mhubiri sadaka ya elfu mia moja kila mwezi.
- Meya anaongozwa na mtazamo finyu kulifilisi Baraza zaidi kwa kuagiza hata mvinyo wa kuwastareheshea wageni kutoka ng’ambo. Anatumia pesa hizohizo wanazoleta kwa manufaa ya hao hao wageni.
- Meya anapuuza wajibu wake wa kuilinda ardhi ya Cheneo; anajigawia ardhi na kumgawia Bili. Anaendeleza zaidi ukiukaji wa sheria kuhusiana na ugavi wa ardhi.
Tanbihi
Mtahiniwa sharti aonyeshe pande mbili.- Kupuuza/kungojea /kutoshughulikia/kukaidi/kutoona hila, au hasara/kufuja/ kubadhiri.
- Kuhasirika/kuzorotesha hali zaidi/kutofanikiwa/kuangamia kwa uongozi. 10 x 2 = 20
Kutoshughulika/kupuuza/kudhulumu -1
Hasara/athari mbaya - 1
-
-
- Ni maneno ya Babu/Babu Maende/Maende.
- Anamwambia mjukuu wake/msimulizi.
- Wamo mtaa wa Madongo/wamo Kochokocho sehemu iitwayo Madongo.
- Babu ameona hali duni/majengo duni yaliyosongamana hapa, ndipo akasema haya/Babu amewaona wanawake wanaokaanga samaki na kuwauzia wapita njia katika kitongoji hiki duni, ndipo akasema haya.4 x 1 = 4
Tanbihi
Dondoo limetolewa Uk. 78- Anadhihirisha/anahimiza umuhimu wa raia kuendeleza sehemu za mashambani badala ya kujidhiki kwa maisha duni mjini yanayopalilia umaskini zaidi. (Uk. 78)
- Anaonyesha hali ya kukatisha tamaa mjini. (Uk. 78).
- Anaendeleza maudhui ya usaliti. Anasema kwamba alidhani uhuru wa Sakata utaleta manufaa kwa wote, ila sivyo. (Uk. 78).
- Anakashifu ubaguzi kwa misingi ya utabaka/anakashifu utabaka. Anasema Sakata ina makabila mawili tu; maskini na tajiri.
- Ni kielelezo cha wazalendo wanaopinga ukabila. Kila mara aliwazungumzia wanawe kuhusu ukabila Sakata.
- Anadhihirisha na kupinga ufisadi nchini Sakata.
- Anamjuza msimulizi akiwa mchanga kuhusu hali halisi katika jamii yake. Msimulizi alimsikia babu akitaja maneno kama vile uhuru, ukabila, hongo, ufisadi. (Uk. 78).
- Anaendeleza mshikamano wa kijamii kwa kumkubalia mwanawe kuoa mke asiyetoka kwenye jamii yao.
- Ni kielelezo cha mwanajamii mwenye bidii. Hapendi kuiacha mifugo yake kuja mjini, anakuja mjini tu kwa shinikizo la mwanawe.
- Anaonyesha ukiukaji wa haki za kibinadamu. Umati unampiga na kumuua kwa tuhuma kuwa ni mwizi wa watoto.
- Kupitia kwake tunasawiriwa uozo katika jamii ya Sakata. Wizi wa watoto unaendelezwa.
- Anaonyesha madhara/hatima ya ubaguzi wa rangi. Anauawa kwa tuhuma kwamba ameiba mtoto kwa vile mtoto ana rangi tofauti na yake.
- Kupitia kwake tunaona ukakamavu wa msimulizi - anamuuma mama aliyempiga Babu ili kumtetea.8 x 1 = 8
-
- Kinaya
Ni kinaya kwamba mchuuzi anamsihi msimulizi/Christine awakumbuke watoto na kuwaonea huruma na hali Christine amekwisha kuavya mimba.
1 x 2 = 1
Kutaja 1
Maelezo 1
AU
Kejeli/stihizai/dhihaka
Mchuuzi anamdhihaki Christine kwa kumwomba awaonee watoto huruma na hali Christine ameavya mimba. -
- Ni kinaya kwamba wavuvi wanasagika kuvua na faida inamwendea Peter.
- Ni kinaya kwamba Diogracias anawadharau akina Christine na hali ni Waafrika wenzake. Anawazungumzia Kiganda ili kuwadhalilisha.
- Christine anadai kwamba ameokoka na hali anahusiana kimapenzi na Peter.
- Dorothy, ambaye anasema ameokoka hamwambii Christine moja kwa moja akome kuhusiana kimapenzi na Peter.
- Ni kinaya kwamba Peter ana mazoea ya kulalamikia hali duni Afrika na hali yeye anatoka kwenye tabaka duni huko kwao.
- Muuguzi Margaret na Miriam, badala ya kumkataza Christine kuavya mimba, wanamwacha tu aavye.
- Mchuuzi anamtaka Christine kuwanunulia watoto peremende na hali Christine ameavya mtoto wake. Hii ni njia ya kuukejeli ukatili wa Christine.
- Peter, badala ya kuhuzunika kwa tendo la uavyaji mimba, anatabasamu tu, na baadaye kumuuliza Christine iwapo anataka pesa.
Tanbihi
Hoja kuhusu kejeli zinaweza kuingiliana na kinaya, mradi mtahiniwa aonyeshe kauli inavyodhamiriwa kumuumiza anayelengwa.3 x 2 = 6
- Kinaya
-
-
- Jamila hajaridhika - Duni analewa kupindukia - hata lakabu yake - Duni inahalalishwa na ulevi huu.
- Hajaridhika kwa kuaibishwa na Duni anaporudi kijijini akiimba na kuwaghasi wakazi wa mtaa wa Sebleni.
- Ukaidi na dharau ya Duni hairidhishi. Anakanywa na wanakijiji dhidi ya ‘taarabu - njia’ lakini anakataa.
- Wanasebleni wamemtoa Duni maanani, wanamwona kuwa hana thamani mbele ya madebe ya taka. Hili haliwezi kuridhisha.
- Jamila anatiwa wasiwasi na tabia ya Duni. Pamoja na umri wake mbichi anamsubiri Duni usiku kwenye roshani.
- Duni anamliza Jamila. Jamila hata anatamani ingekuwa mara ya mwisho kusikia wimbo wa Duni. Duni hajutii matendo yake mabaya kwa mke wake.
- Duni anampiga Jamila na hata kumpa majeraha na makovu ya mwili.
- Duni anamtusi na kumsimbulila Jamila.
- Jamila hajaridhika kwani ana mgogoro wa nafsi. Anawaza ikiwa aufuate ushauri wa wanaomnasihi kutoka kwenye ndoa yenye utesi au abaki. Anaamua kutousaliti moyo wake. /Hata Salim, shangazi wanamsihi atoroke.
- Hisia/matukio ya Duni hayawezi kutabirika. Jamila anapojaribu kumsaidia anamwambia amwache, hahitaji msaada; inabidi Jamila akubali kuwa Duni hahitaji msaada; anaweza kila kitu.
- Duni anamhangaisha Jamila kwa kumtaka Jamila kuleta chakula haraka japo kwa kweli Duni hakili chakula hicho.
- Duni amemuumbua Jamila. Tunaambiwa Jamila hana tena lile busu la Zamani, anaonekana mwenye simanzi hata akiwa usingizini.
- Jamila ana dhiki ya kisaikolojia. Usingizi wake ni wa machovu.
- Jamila anaishi kwa hofu ya kuchelea kuvunjika kwa ndoa yake na Duni. Anatumainia kuwa siku moja Duni atabadilika.
- Duni anarudi nyumbani usiku mkuu saa saba unusu/kuchelewa.
- Duni anawatusi wakazi wa mtaa wake, hivyo tabia hii haiwezi kumridhisha mkewe.
- Duni anamwaibisha Jamila hata kwa majirani; majirani wanasikia matusi anayomwaiwa na mumewe.
- Jamila analazimika kujitia bashasha pale Duni anaporejea akiwa mlevi ili kumridhia mumewe.
- Duni analala akiwa amevaa nguo alizoshindia ulevini.
- Maneno ya Duni ya kinyume yanamsumbua Jamila. Anamwambia awaambie watu ameridhika na hali hajaridhika. Hata Duni mwenyewe anasema kwamba penzi lina miujiza, kuonyesha kwamba yeye ana udhaifu mkubwa na hata Jamila ana udhaifu kwa kuishi naye. (Uk. 57).10 x 2 = 20
-
-
- Shairi linazungumzia tatizo la upofu.
Mf. ngakua na mato. - Kwamba mtu aliyepatwa na tatizo la upofu huwa hawezi kufanya mambo ambayo zamani aliyamudu bila tatizo.
AU
Nafsineni inasikitikia hali yake ya kutomudu kujifanyia mambo kwa sababu ya upofu.
1 x 2 = 2
Kutaja - 1
Mfano - 1
- Shairi linazungumzia tatizo la upofu.
-
- Inkisari - imetumika ili kudumisha ulinganifu wa mizani.
Mifano:
ngaliandaa - ningaliandaa
ngafinyanga - ningalifinyanga/ningefinyanga
ngatia - ningetia
Tabdila - imetumiwa ili kuleta urari wa vina
mduwaa - mduara
apikae - apikaye
vinavong’aa - vinavyong’aa
kuupa utungo mahadhi ya kishairi
2 x 2 = 4
Kutaja - 1
Sababu - 1
- Inkisari - imetumika ili kudumisha ulinganifu wa mizani.
- Ningetumia miti iliyopinda (iliyokatika) na yenye umbo zuri kutengenezea kijiti (ulindi). Ningekipekechea kijiti hiki kwenye tundu la wimbombo mwema/mzuri kupekechea moto kwa ufundi/umahiri mkuu kiwamboni. Ningekuwa bingwa/ ningekuwa na moyo mahiri/shupavu (katika upekechaji) na kupekecha moto/ Ningekuwa fundi stadi katika upekechaji wa moto.4 x 1 = 4
Tanbihi- Wimbombo - kipande cha mti kilichotobolewa tundu, na kinachotumiwa kupekechea moto.
- Ulindi - Ni kijiti kinachopekechwa kwenye wimbombo ili kutoa moto.
- Toni ya huzuni/toni ya kuomboleza/ya masikitiko.
Mshairi anahuzunishwa na analalamikia hali yake ya upofu isiyomruhusu kujifanyia mambo mengi.
Kutaja - 1
Maelezo - 1 -
- Urudiaji wa sauti/silabi.
Kwa mfano ubeti wa kwanza: to, to, to / a, a, a
Mstari wa mwisho wa kila ubeti - e - Urudiaji wa maneno, kwa mfano, ulo - ubeti wa 3.
- Usambamba/urudiaji wa vishazi/urudiaji wa miundo sawa ya mistari. kwa mfano, ngalisana kito, cha kuchezea ngafinyanga chungu, cha mduwaa
3 x 2 = 6
Kutaja - alama 1
mfano - alama 1
- Urudiaji wa sauti/silabi.
- Nafsineni ni kipofu/mtu asiyeona. Ubeti I anasema, ‘ngakua na mato!’Ubeti 9 anasema, ‘mato ndo malenga kanikimbia’.
Alama2
Kutaja - alama 1
mfano - alama 1
-
-
-
- Hodari wa kufanya kazi/wenye bidii/hodari.
- Wenye kujiamini
- Waliopuuzwa/hawana makubwa (hawasikiki)
- Hawana tamaa
- Wenye kupinga ulaghai
- Wenye matumaini/ndoto haizimiki.
- Hawahini/huwapa watu haki yao.
- Wanahakikisha kuwa jamii imejitosheleza kwa chakula/hawatulii hadi wapate.
- Wazalendo5 x 1 = 5
- Tashbihi - kama watanga na mipini - kuonyesha jinsi walivyojitolea.
- Tashihisi/uhaishaji
Tamaa za moyo kutii, kupigana na ulaghai. Hapa tamaa za moyo na ulaghai vimepewa uwezo wa kutenda. Binadamu anasawiriwa kama aliye chini ya mamlaka ya tamaa za moyo ambazo ndizo zinazotiiwa. Pia ulaghai unapewa uwezo wa kukabiliana ana kwa ana na binadamu. Imetumiwa kuonyesha ugumu uliopo wa kujitenga na tamaa na ulaghai. - Nahau/msemo - ndoto haizimiki. Hawapotezi tumaini, kuonyesha hali ya kutokata tamaa
La haramu jasho hawali - Kuonyesha hawafaidiki kwa wasichokifanyia kazi. - Hisi mseto.
Ndoto haizimiki, na jasho hawali.
Hapa tendo au jambo linalohusiana na kuona (haizimiki) linahusishwa na jambo au hisi ya kuonja/muonjo (kula - jasho hawali). - Taswira.
‘Kutwa kile na hiki, kama watanga na njia - kuonyesha watu wanaoshughulika kufanya kazi kuiendeleza nchi. - Sitiari/jazanda - ndoto haizimiki - hawapotezi tumaini - kuonyesha kujibidiisha kwa watafuta riziki.
3 x 2 = 6
Kutaja - 1
umuhimu - 1
-
- Mazida - vinyuani badala ya vinywani - ili kutosheleza mahitaji ya idadi ya mizani.
- Kufinyanga sarufi//kuboronga lugha/miundo ngeu/ukiushi wa kisintaksia/ ukiushi wa kimuundo.
Mifano- Tamaa za moyo kutii, badala ya, Kutii tamaa za moyo.
- La haramu jasho hawali - badala ya, ‘hawali jasho la haramu’.
- Ya kesho kuwa hali njema, badala ya, ya hali kesho kuwa njema. Imetumiwa ili kupata urari wa vina.
- Udondoshaji wa maneno, mfano,
- Pato ambalo la halali - badala ya, Pato ambalo ni la halali.
- Wiki baada wiki - Wiki baada ya wiki.
Umetumiwa ili kutosheleza idadi ya mizani / kupunguza idadi ya mizani.
3 x 2 = 6
Kutaja - 1
Mfano - 1
-
- Tathlitha - Mishororo mitatu katika kila ubeti.
- Ukara - Vina vya kati / ndani vinafanana katika shairi zima, vya nje vinatofautiana
- Kikwamba - kila ubeti unaanza kwa kirai / maneno, “Watafuta riziki”. 3 x 1
-
-
-
- Kisasili / kisasili cha usuli.
Inazungumzia asili ya kifo.
alama 2 -
- Hutumiwa kuelezea chanzo cha mazoea ya kidini/kijamii. Kwa mfano asili ya dhehebu fulani, asili ya kifo.
- Ni tungo zinazohalalisha baadhi ya desturi na imani za kidini za jamii.
- Ni kitambulisho cha jamii. Kila jamii ina kisasili au visasili vyake vinavyohusu imani zayo.
- Hurithisha imani, desturi, na historia ya jamii kwa kuvitamba kwa vizazi mbalimbali.
- Ni nyenzo ya kuadilisha. Kila kisasili huwa na adili. Kwa mfano, kisasili cha hapo juu kinafunza haja ya kutandarukia mambo.
- Huimarisha utangamano wa kijamii. Watu wanapokuja pamoja kutambiana hujihisi kuwa kundi moja, hivyo umoja kujengeka zaidi.
- Hadithi hizi hutumiwa kupunguza athari za baadhi ya mambo ya kimaumbile au misiba inayompata binadamu. Kwa mfano, kisasili kuhusu chanzo cha kifo hunuiwa kuwapunguzia wanajamii mwemeo wa huzuni, binadamu hulazimika kuwaza kuwa kifo kilihalalishwa na matendo ya binadamu mwenyewe, hivyo hakiepukiki.
- Huburudisha. Watu wanapotambiwa huburudika na kuliwazika.
- Utambaji wa visasili hurithisha fani yenyewe ya utambaji kwa vizazi mbalimbali.
- Hukuza ubunifu. Kadiri mtu anavyotamba, ndivyo anavyopalilia kipawa cha kubuni mitindo ya kuisimulia hadithi.
- Hukuza ukakamavu wa kuzungumza hadharani. Kadiri mtu anavyotamba ndivyo anavyopalilia ujasiri wa kuzungumza hadharani.
- Ni njia ya kudhibiti matendo hasi ya wanajamii. Baadhi ya visasili huhadithia maeneo matakatifu kama vile madhabahu, na hata mibuyu.
Watu huelekezwa kuheshimu mahali hapa. - Hutumiwa kupitisha muda. Watu hushiriki vikao vya utambaji wakingojea shughuli nyingine kama vile kuiva kwa chakula.
- Kukuza lugha.
5 x 2 = 10
Kutaja - 1
Kufafanua / Kutoa mifano - 1
Tanbihi- Mtahiniwa lazima afafanue hoja ili kupata alama 2.
Kutaja, kwa mfano, ‘visasili huburudisha,’ bila kuelezea vipi, hakutoshi. Mtahiniwa huyu atuzwe alama 1. - Visasili ni tofauti na ngano za usuli. Ngano za usuli hazihusiani na imani za kidini. Atakayesema kwamba utungo huu ni ngano ya usuli apate 0 kote kote, (i) na (ii).
- Mtahiniwa lazima afafanue hoja ili kupata alama 2.
- Kisasili / kisasili cha usuli.
- Fomyula ya kumalizia
- Huonyesha kumalizika kwa ngano, hivyo kufunga muktadha wa ulimwengu wa usimulizi/ulimwengu usio halisia.
- Hapa ndipo fanani hutangaza Adili au funzo la usimulizi wake. Kwa mfano, mtambaji anaweza kusema, “mwenye kujaribu kuokoa maisha ya binadamu mwenzake na afuatwe na utajiri, na mwenye kuyaangamiza agubikwe na umaskini”, ili kuonya dhidi ya kumdhulumu mwenzako maisha.
- Baadhi huwapa wasikilizaji changamoto ya kuwa watambaji bora, hivyo kurithisha stadi bora za utambaji.
- Humpisha mtambaji anayefuata. Anaweza kuashiriwa kwa kauli fulani au kwa kupewa changamoto.
- Huitoa hadhira kwenye ulimwengu wa ubunifu na kuaingiza kwenye ulimwengu halisia, hivyo kupunguza makini yao.
- Hupisha shughuli inayofuata, (kwa mfano utegaji wa vitendawili) iwapo shughuli ya utambaji imekwisha.
- Hutuliza hadhira, pengine kwa kuipa suluhisho kwa mgogoro uliopo kwenye ngano. Kwa mfano, inaweza kuonyesha kuuawa kwa zimwi na kurejeshwa kwa usalama katika jamii fulani.
- Hutia mshawasha wa kusikiliza ngano nyingine; pengine kupitia taharuki ambayo huenda ikaibuliwa na fanani, au kukatizwa kwa msuko wa ngano yenyewe.
4 x 2 = 8
Kutaja - 1
Kueleza - 1
-
Download KCSE 2014 Kiswahili Paper 3 Questions with Marking Scheme.
Tap Here to Download for 50/-
Get on WhatsApp for 50/-
Why download?
- ✔ To read offline at any time.
- ✔ To Print at your convenience
- ✔ Share Easily with Friends / Students