- UFAHAMU
Soma kifungu kifuatacho kisha ujibu maswali. (Alama 15)
Ziara ya wanafunzi wa Chama cha Mazingira kutoka shule ya Faidi ilikuwa ya kuvutia. Mara tu walipofika kwenye lango la uwanja wa maonyesho, walikaribishwa kwa ngoma za kitamaduni. Vilevile, vikundi tofauti vya muziki vilipishana kuwalaki wageni kwa miondoko yao. "Haya, mmejionea, mwacha mila ni mtumwa," alisema mwalimu Mkala akiwaelekeza wanafunzi wake kwenye sehemu nyingine za maonyesho. Huko ndani walijionea mengi. Waliona vielelezo na kupewa maelezo kuhusu mbinu mpya za kilimo. Mbinu hizo zilikuwa na azma moja; kuhifadhi mazingira. Uhifadhi wa maji, miti na wanyamapori ni baadhi ya mambo yaliyotiliwa mkazo. Wanafunzi nao walibaini kuwa viumbe hutangamana na kutegemeana. Lena, mwenyekiti wa Chama cha Mazingira alivutiwa na sehemu ya maonyesho iliyohusu mbinu za kisasa za ufugaji. Alistaajabishwa na maelezo kuhusu ufugaji wa wadudu. "Lo! Wanafuga konokono; tena wanaliwa?" Lena alimuuliza mwalimu wake kwa sauti ya chini.
"Naam, wadudu wanaofugwa na wanaoliwa ni wengi. Huu ni mwanzo tu, hatujafikia kwenye kibanda cha kumbikumbi na chenene. Waandalizi wa maonyesho haya walitangaza kuwa kibanda hicho kitakuwepo." Mwalimu alimjibu Lena. Baada ya kukamilisha ziara yao, wanafunzi walikuwa wameshiba kwa mafunzo na maelezo mapya ya namna ya kuhifadhi mazingira na kuzalisha chakula.
"Natumai mmejifunza mengi ambayo yatawafaa na kuwafaidi wengine. Utamu wa elimu ni kuelimishana. Najua mtaipanda mbegu ya maarifa mliyopewa leo istawi na kuzaa matunda." Mwalimu Mkala aliwaambia wanafunzi wake. Basi lao liliposhika baraste kuu, Lena alizama kwenye mawazo. Mara wazo lilimjia. Aliona kwamba kuna uwezekano wa kikundi cha Wanarika katika kijiji chao kuanzisha mradi wa kufuga wadudu.
"Sofi, unaonaje tukianzisha mradi wa kufuga vipepeo kijijini mwetu wakati wa likizo?" Lena alimuuliza rafiki yake.
"Lena, mradi wa vipepeo unahitaji kundi kubwa la watu ili ufanikiwe. Utahitaji ushirikiano wa wanakijiji wote. Je, utaweza?" Sofi alimuuliza Lena. "Utaweza Lena, Sofi asikuvunje moyo. Unachohitaji ni nia na ari ya kutimiza maono yako." Mwalimu Mkala alimhimiza Lena. Ushauri wa Mwalimu Mkala ulimpa Lena mshawasha wa kuanzisha mradi huo. Wakati wa likizo, Lena aliwaarifu baadhi vijana katika kijiji chao kuhusu wazo lake. Pendekezo hili lilipokelewa kwa hisia tofauti. Waliovutiwa walikuwa wengi. Walilikumbatia pendekezo hilo likawa si wazo la Lena tena bali lao.
Papo hapo, vijana walianza mchakato wa kuhakikisha mradi wao umefaulu. Lena alimwalika Chifu wa eneo lao katika mojawapo ya mikutano yao. Chifu aliwaelekeza kuhusu namna ya kupata leseni. Kisha, akawatengea sehemu ya uwanja wa umma palipo na bustani ili kufanyia shughuli zao. Kwenye bustani mlikuwa na vipepeo wachache. Vijana waliimarisha mazingira ya pale kwa kupanda miti ya kiasili na bustani za maua ili kuwavutia vipepeo zaidi. Vipepeo walizaana. Kukawa na vipepeo wa rangi anuwai na maumbile mbalimbali. Vijana walisakura kwenye mtandao na kupata maarifa zaidi kuhusu maisha ya vipepeo na namna ya kuwatunza. Polepole, mradi wao ulianza kuzaa matunda. Picha na video za vipepeo wa kupendeza walizoweka kwenye mitandao ya kijamii ziliwavutia wengi. Aidha, Lena na viongozi wenzake walialikwa kwenye kituo maarufu cha runinga kuelezea zaidi kuhusu mradi wao.
"Je, mradi wenu unawafaidi vipi?" Mwanahabari aliwauliza akina Lena. "Mradi wetu una faida kochokocho. Kwa mfano, mazao shambani yameimarika kutokana na vipepeo kusambaza mbegu kwenye maua ya mimea. Nyuki pia wameongezeka. Watu wametundika mizinga kwenye miti ya kiasili na wengine tayari wanarina asali. Faida ni nyingi ila hazionekani kwa macho," alieleza Lena huku akitabasamu. Wenzake pia walitoa michango yao.Habari ya kijiji chao zilienea kwa kasi ya moto wa nyikani. Kijiji kikapata jina jipya - Kijiji cha Vipepeo. Isitoshe, Lena na wenzake walipata ufadhili wa kuendeleza masomo yanayohusiana na mradi wao na suala zima la mazingira. Vilevile, walipokea mialiko ya kitaifa na ya kimataifa ili kuzungumzia mradi wao.
Kijiji chao nacho kilifaidi si haba. Viongozi walishikana na kujenga kituo kikubwa cha kulea na kutafitia vipepeo. Watalii waliozuru kijiji chao ili kujionea vipepeo na kuwafanyia utafiti walitozwa ada. Ada hii ilidunduizwa na kuwekwa katika hazina ya kuendeleza miradi ya kijiji chao. Sura ya kijiji ilibadilika, barabara, hospitali na shule zikajengwa na zilizokuwepo zikaimarishwa.- Eleza jinsi Mwalimu Mkala alivyowafaa wanafunzi kwa mujibu wa kifungu. (alama 2)
- "Wanafunzi nao walibaini kuwa viumbe hutangamana na kutegemeana." Thibitisha kauli hii kwa kurejelea hoja tano kutoka kwenye kifungu (alama 5)
- Wanachama wa Chama cha Mazingira walipanda mbegu ya maarifa, ikastawi na kuzaa matunda. Fafanua kauli hii kwa mujibu wa kifungu (alama3)
- Andika mambo mawili yanayoonyesha kuwa Lena ni mkakamavu. (alama 2)
- Eleza maana ya: (alama 2)
- mchakato
- kasi ya moto wa nyikani
- Kipe kifungu hiki anwani mwafaka. (alama 1)
- UFUPISHO
Soma kifungu kifuatacho kisha ujibu maswali. (Alama 15)
Vijana wanapomaliza kozi fulani, matarajio yao ni kupata ajira. Kati ya vijana wanaohitimu katika vyuo, shule za sekondari na za msingi ni wachache sana wanaopata ajira. Hili linatokana na tatizo kuu la ukofesu wa ajira nchini Kenya na ulimwenguni kwa jumla. Ikumbukwe kwamba kati ya watu kumi humu nchini, saba ni vijana walio chini ya miaka thelathini na mitano. Hii ina maana kwamba nafasi za ajira ni chache ikilinganishwa na idadi ya vijana.
Japo serikali imewekeza katika maswala ya vijana, ajira kwa vijana ingali tatizo linalohitaji suluhisho la kudumu. Tafiti zinaonyesha kwamba uhaba wa ajira husababishwa na mambo anuwai. Ilivyo sasa ni kuwa, maarifa aliyo nayo mtu ndiyo huchangia katika kuajiriwa kwake. Hata hivyo, wapo wale ambao hawapati ujuzi na maarifa ya kutosha kwa sababu ya kukosa makini wakati wa mafunzo. Vilevile, inawawia vijana vigumu kupata ajira ama kwa kuwa hawakukamilisha kozi fulani au hawakupata ujuzi wa kuwawezesha kuajiriwa. Si ajabu kupata vijana ambao wanapata ajira ila wanakosa kuwajibika na hivyo kuachishwa kazi. Hawa utapata wanachelewa kufika kazini, wanakosa kukamilisha kazi walizopangiwa, wanakosa kufika kazini bila idhini, na hata kukosa kushirikiana na wenzao.
Isitoshe, baadhi ya vijana wana mazoea ya kuchagua kazi na kudharau kazi nyingine. Wao hupendelea kazi za ofisini na kupuuza zile zinazodhaniwa kuwa za sulubu. Ukiwauliza wengine watakwambia kwamba lengo lao ni kuwa tajiri kwa haraka bila kujali njia watakazotumia kupata utajiri huo. Pia kuna wale ambao wanawategemea walezi wao kwa kila kitu. Hawa, hawaoni haja ya kujishughulisha katika kutafuta ajira. Vijana wengine wanachelea kuajiriwa kwa kisingizio kwamba watakosa muda wa kujumuika na wenzao katika shughuli za starehe na anasa. Fikiria pia, kuhusu vijana wanaoshinikizwa na wenzao kukataa ajira. Hawa hulaza damu na kujipiga kifua wakidai kuwa si lazima wafanye kazi.
Kwa mujibu wa Malengo Endelevu ya Umoja wa Mataifa (2015); Lengo nambari nane linabainisha haja ya kuwepo kwa ajira zenye staha na manufaa kwa wote. Ajira yenye staha ni ile inayoambatana na maarifa na ujuzi alionao mtu. Hata hivyo, ukosefu wa ajira umewafanya vijana kushiriki shughuli zisizokuwa na thamani. Mathalan, wapo vijana waliohitimu katika taaluma mbalimbali ila wanafanya kazi zisizoambatana na maarifa waliyoyapata. Vijana hawa hufanya kazi katika mazingira magumu na yenye kuhatarisha maisha yao. Wengine wanalazimika kufanya kazi kwa muda mrefu na hivyo kuathiri afya yao. Pia kuna vijana wanaopokea malipo duni yasiyoweza kukidhi mahitaji yao ya kimsingi. Ugumu wa maisha huwafanya baadhi ya vijana kuwa wepesi wa kushawishika kushiriki katika matendo maovu na yenye kukiuka maadili ya kijamii ili wafaidike.
Si ajabu kupata baadhi ya vijana wakiwa na malimbikizi ya madeni kotekote. Wao huishi maisha ya kujifichajificha ili kuepuka wadeni wao. Hali hii huwatia fedheha, kuwakosesha uhuru na huwanyima fursa ya kujiendeleza maishani. Kadhalika, ukosefu wa ajira mara nyingi huweza kusababisha mitafaruku katika familia. Huenda wazazi wakakosa kuelewana wao kwa wao au wakakosa kuelewana na wana wao kwa sababu ya kuwa na misimamo tofauti kuhusu suala la ajira kwa watoto wao. Kutokana na hali kwamba vijana wengi hawapati ajira pindi tu wanapokamilisha kozi maalum, kuna uwezekano wa kudidimia na kusahaulika kwa maarifa waliyokuwa wamepata. Mwishowe, vijana wanaojipata katika mazingira ya aina hii huchushwa na kuchoshwa na makali ya maisha. Hivyo, wanaishia kujitenga na wanajamii ili kuepuka aibu, kusutwa na hata kuelekezewa kidole cha lawama kila mara. Hatima yake ni kushiriki ama katika matumizi ya dawa za kulevya au unywaji wa pombe kupindukia ili kujiliwaza.
Ingawa uhaba wa ajira ni suala linalokumba jamii nyingi, ni muhimu kubaini kuwa zipo njia zinazoweza kutumiwa kukabiliana na hali hii. Vijana wanahitaji kuhamasishwa kuhusu uwezo walio nao katika ujasiriamali ili kuziba pengo la ajira. Aidha wanahitaji kufahamu kuwa si lazima waajiriwe bali wanaweza kujiajiri na hatimaye kuwaajiri vijana wengine. Jambo hili linawezekana iwapo vijana watawezeshwa kwa kupewa nafasi ya kupata mtaji wa kuanzisha au kubuni miradi mbalimbali ya kuwaletea kipato. Vijana wanapopata mitaji hii, wanastahili kupata mafunzo maalum ya namna ya kusimamia miradi hiyo. Vilevile vijana wanaweza kunufaika kutokana na maelekezo watakayopokea kutoka kwa wadau waliobobea katika taaluma maalum. Ni wajibu wa vijana kuungana na kushauriana miongoni mwao ili kujengana. Muhimu zaidi ni kuwa, vijana wana nafasi kubwa katika kuendesha maisha yao; kwani penye nia pana njia.- Fupisha ujumbe wa aya tatu za kwanza kwa maneno 90. (alama 8)
- Kwa maneno 85, eleza masuala ambayo mwandishi anaibua katika aya ya nne na ya tano. (alama 7)
- MATUMIZI YA LUGH (Alama 40)
- Andika irabu zeifa zifuatazo: (alama1)
- mbele ,juu,tandazwa
- nyuma, kati, viringwa
- Banisha silabi inayotiwa shadda katika maneno yafuatayo: (alama 1)
- bingiria
- walimwengu
- Ainisha mofimu katika maneno yafuatayo: (alama 2)
- anavyojenga
- mfariji
- Ainisha vitenzi katika sentensi ifuatayo:
Mkulima yupo shambani anapalilia mimea. (alama 2) - Andika sentensi ifuatayo katika umoja:
Waashi walijenga majumba ya kifahari ya kupendeza.(alama 1) - Andika sentensi ifuatayo upya kwa kufuatamaagizo
Wahandisi walikarabati barabara zote (alama 1)
(Anza kwa: Barabara...) - Tumia nomino ya jamii mbadala ya maneno yaliyopigiwa mstari katika sentensi ifuatayo: (alama 1)
Serikali imeduni mikakati ya kukabiliana na nzige wengi wanaovamia mashamba. - Alama ya mshazari hutumiwa kutenga nambari. Tunga sentensi moja kuonyesha matumizi mengine ya alama ya mshazari. (alama 1)
- Kanusha sentensi ifuatayo: (alama 1)
Wanariadha wameenda uwanjani kufanya mazoezi. - Andika sentensi zifuatazo upya kwa kufuata maagizo.
- Watalii walifika katika mbuga ya Tsavo walikowaona wanyamapori.
(Tumia 'amba") (alama 1) - Mkurugenzi aliwashauri wafanyakazi wajibidiishe kazini.
(Geuza maneno yaliyopigiwa mstari kuwa nomino)
- Watalii walifika katika mbuga ya Tsavo walikowaona wanyamapori.
- Ainisha virai katika sentensi ifuatayo:
Vipepeo wale weupe wanaashiria mvua ya maka inayotarajiwa mwakani. (alama 2) - Bainisha yambwa na chagizo katika sentensi ifuatayo:
Wanakijiji waliwajengea wongwe nyumba kwa mawe. (alama 3) - Andikantens ifuatayo katika hali ya mazoea. (alama 2)
Huduma za afya zilipoboreshwa, viwango vya maambukizi vilipungua. - Andika sentensi ifuatayo katika usemi wa taarifa.
"Watunza mazingira watanadhifisha soko letu kesho." Chifu aliwaambia wafanyabiashara. (alama 2) - Tunga sentensi mbili kuonyesha matumizi mawili ya kiambishi "-ka-" (alama 2)
- Nomino zifuatazo zimo katika ngeli gani? (alama 2)
- bendera
- ujana.
- Andika sentensi ifuatayo katika hali ya udogo.
Ngoma hizo zimetengenezwa kwa ngozi laini. (alama 2) - Tunga sentensi ukitumia kihisishi kinachoibua hisia kinyume cha matarajio. (alama 1)
- Tunga sentensi yenye muundo ufuatao:
KN(N +5)+ KT(T) + KN(N + ) (alama 3) - Bainisha maana mbili zinazojitokeza katika sentensi ifuatayo: (alama 2)
Jena angalfuata ushauri wa mwelekezi wake angalifaulu - Baraste ni kwa barabara,hekima ni kwa ............... na sihi ni kwa ............ (alama 2)
- Tunga sentensi moja kubainisha maana mbili za neno hema.(alama 2)
- Rafiki yako ana mazoea ya kutoa visababu ili asifanye kazi fulani. Andika methali unayoweza kutumia kumwonya dhidi ya tabia hiyo. (alama 1)
- Andika irabu zeifa zifuatazo: (alama1)
- ISIMUJAMII
Soma makala yafuatayo kisha ujibu maswali. (Alama 10)
"Wateja wetu wameagiza bidhaa tena. Katoni mia mbili ziwe tayari kufikia leo jioni. Kazi ianze mara moja!"- Bainisha sajili ya makala haya kwa kutoa mfano kutoka kwenye makala. (alama 2)
- Fafanua sifa nyingine nane za sajili hii ambazo zingejitokeza katika makala haya. (alama 8)
MARKING SCHEME
- UFAHAMU
-
- Aliandamana na wanafunzi ziarani.
- Aliwaelekeza wanafunzi kwenye sehemu mbalimbali za maonyesho.
- Alimtia moyo Lena.
- Aliwashauri wanafunzi. Hoja 2 x 1=2
-
- uwepo wa vipepeo na nyuki bustanini
- vipepeo kusambaza mbegu na mimea kunawiri
- wadudu kuwa lishe kwa binadamu
- binadamu kurina asali kutoka kwa nyuki
- watalii kuzuru kijiji cha Faidi (Kijiji cha Vipepeo)
- kijiji kunufaika kutokana na ada iliyotozwa Hoja 5 x 1 = 5
-
- Kupata wazo kuwa na wazo la kuanzisha mradi.
- Kuanzisha mradi wa vipepeo.
- Kuendeleza mradi - kuwalea/ kuwatunza vipepeo.
- Kunufaika kutokana na ada -- kufanyiwa kwa utafiti, kufadhiliwa.
- Kijiji kupata umaarufu.
- Miundomsingi kuimarika. Hoja 3 x 1 = 3
-
- Ni kiongozi wa chama cha wanamazingira.
- Alimuuliza mwalimu swali.
- Aliwarai wenzake kuhusu mradi wa ufugaji wa vipepeo.
- Alijibu maswali kwenye runinga. Hoja 2 x 1=2
-
- mpangilio/ utaratibu/mfululizo wa shughuli/mchakacho/mfuatano/ njia ya kufanya jambo
- haraka, wepesi Hoja 2 x 1=2
-
- Ufugaji/ uhifadhi wa vipepeo
- Vipepeo
- Mradi wa vipepeo Hoja 1 x 1=1
-
- UFUPISHO
-
- Matarajio ya vijana ni kupata ajira.
- Vijana wachache wanaohitimu hupata ajira.
- Kuna tatizo la uhaba wa ajira nchini na ulimwenguni kote.
- Serikali imewekeza katika maswala ya vijana.
- Tatizo la ajira kwa vijana linahitaji suluhisho la kudumu.
- Maarifa aliyo nayo mtu ndio huchangia kuajiriwa kwake.
- Wapo wanaokosa ujuzi na maarifa kwa sababu ya kutokuwa makini.
- Vijana wanakosa ajira kwa kutokamilisha kozi fulani.
- Vijana wanakosa ajira kwa kuwa hawakupata ujuzi wa kuwawezesha kuajiriwa.
- Vijana kuachishwa kazi kwa kukosa kuwajibika.
- Baadhi ya vijana huwa na mazoea ya kuchagua kazi.
- Vijana kutamani utajiri wa haraka bila kujali njia watakazotumia kupata utajiri huo. (xiii) Vijana kutegemea walezi kwa kila kitu.
- Vijana kuchelea kuajiriwa kwa kuhofia kukosa muda wa kujumuika na wenzao. (xv) Kuwepo kwa vijana wanaoshinikizwa na wenzao kukataa ajira. Hoja 8 x 1 = 8
-
- Pana haja ya kuwa na ajira zenye staha na manufaa kwa wote.
- Ukosefu wa ajira umewafanya vijana kushiriki katika shughuli zisizokuwa na thamani
- Wapo vijana wanaofanya kazi zisizoambatana na maarifa waliyo nayo.
- Vijana hufanya kazi katika mazingira magumu na yenye kuhatarisha maisha yao.
- Vijana hufanya kazi kwa muda mrefu na kuathiri afya yao
- Kuna vijana waliopokea malipo duni.
- Vijana kushawishika kwa wepesi na kushiriki katika maovu.
- Vijana huwa na malimbikizi ya madeni.
- Ukosefu wa ajira huchangia kuwepo kwa mitafaruku katika familia.
- Kuna uwezekano wa kudidimia na kusahaulika kwa maarifa.
- Vijana huchushwa na kuchoshwa na makali ya maisha.
- Vijana hujitenga na wanajamii.
- Vijana hushiriki katika matumizi ya dawa za kulevya na unywaji wa pombe kupinduki ili kujiliwaza.
Hoja 6x 1 = alama 6
Mtiririko alama 1
-
- MATUMIZI YA LUGHA
-
- /i/
- /o/
-
- bi-ngi-ri'-a au bi-ngi-ri-a
- wa-li-mwe'-ngu au wa-li-mwe-ngu
-
- a-nafsi ya tatu/ mtenda/ngeli/kiambishi cha kiima/ umoja/ idadi
na - wakati uliopo
vyo-kirejeshi/ namna/jinsi
jeng - mzizi
a-kiishio/kauli ya kutenda - m-kiambishi ngeli/ umoja/ mtenda/ idadi/kiima fariji - mzizi
- a-nafsi ya tatu/ mtenda/ngeli/kiambishi cha kiima/ umoja/ idadi
- yupo - kitenzi kishirikishi 1/0
anapalilia - kitenzi halisi 1/0 - Mwashi alijenga jumba la kifahari la kupendeza. 1/0
- Barabara zote zilikarabatiwa na wahandisi baada ya mafuriko.
Barabara zote zilikarabatiwa baada ya mafuriko na wahandisi. 1/0 - Serikali imebuni mikakati ya kukabiliana na wingu la nzige wanaovamia/ linalovamia mashamba. 1/0
- Sentensi ibainishe mojawapo ya matumizi yafuatayo:
- Kuleta maana ya ama/au.
- Kalamu/karatasi inahitajika.
- Kuonyesha maneno yenye maana sawa.
- Watalii waliona ndovu/ tembo mbugani.
- Katika kuandika akisami.
- 1/7 1/0
- Kuleta maana ya ama/au.
- Wanariadha hawajaenda uwanjani kufanya mazoezi. 1/0
-
- Watalii walifika katika mbuga ya Tsavo ambako waliwaona wanyamapori. 1/0
- Mkurugenzi aliwapa ushauri wafanyakazi watie/ kutia bidii kazini. Mkurugenzi alitoa ushauri kwa wafanyakazi watie/ kutia bidii kazini. 2/0
-
- KN
- Vipepeo wale weupe
- Mvua ya masika
- KT
- Wanaashiria mvua ya masika inayotarajiwa mwakani
- inayotarajiwa mwakani
- KV
- wale weupe 4 x ½ = 2
- KN
- Wakongwe-yambwa tendewa/ kitondo
nyumba yambwa tendwa/ kipozi
mawe- yambwa ala/ kitumizi
kwa mawe - chagizo
Majibu yoyote mawili 2x1=2 - Huduma za afya zinapoboreshwa viwango vya maambukizi hupungua.
au
Huduma za afya ziboreshwapo viwango vya maambukizi hupungua. 2/0 - Chifu aliwaambia wafanyabiashara kwamba/ kuwa watunza mazingira wangenadhifisha soko lao siku ambayo ingefuata.
-
- Kuonyesha mfuatano wa matukio au vitendo, kwa mfano: Mkulima alipanda mbegu, akapakilia, akavuna, akauza.
- Kuonyesha kitendo kimoja kinasababishwa na kingine, kwa mfano:
Alitia bidii masomoni akatuzwa. - Kuonyesha nia au matarajio ya kufanyika kwa jambo fulani, kwa mfano: Nitakutuma sokoni ukaninunulie mboga.
- Kuleta wazo la kuamrisha kwa mfano:
Kaondoe uchafu wote uani! (amri) - Kuleta wazo la rai, kwa mfano:
Kamhudumie mteja wetu. (rai) - Katika usemi halisi, kwa mfano:
"Nitakuja kesho." Mama akasema. 2 x 1 = 2
-
- bendera - I-ZI 1/0
- ujana-U-U au U 1/0
- Vigoma/vijigoma hivyo vimetengenezwa kwa vigozi/ vijigozi laini.
au
Vigoma/vijigoma hivyo vimetengenezwa kwa kigozi/ vijiigozi laini - Watahiniwa watumie vihisishi kama vile: kumbe!, Lo!, Eti!, Ati!, Salaala!, Salaale!, Aa!, Aha!, Hivyo!, Afanalek!, Mungu wangu! 1/0
- _
KN(N+S)+KT(T) + KN (N+V)
Madereva waliopata mafunzo wamepokea leseni mpya. 3/0 -
- Jena hakufuata ushauri wa mwelekezi wake hivyo hakufaulu.
- Jena hana nafasi ya kufuata ushauri wa mwelekezi wake ili afaulu kwa sababu kitendo kimefanyika. 2x1 2
- busara 1/0
ombi/ bembeleza/nasihi/ sairi/ rai 1/0 - Watahiniwa watunge sentensi moja tu kubainisha maana mbili za neno hema.
hema - kibanda cha chadarua
hema- tokwa na pumzi kwa nguvu
Kwa mfano: Wanariadha waliokimbia na kuhema walipumzika ndani ya hema. 2/0 - Mchagua jembe si mkulima. 1/0
-
- ISIMUJAMII
- Biashara/ viwandani/ sokoni
- Matumizi ya msamiati maalum wa biashara. K.m. wateja, bidhaa
- Matumizi ya lugha ya kuamrisha. K.m. Kazi ianze mara Moja!
Kubainisha alama 1
Mfano alama 1
-
- Matumizi ya lugha ya unyenyekevu. Kwa Mfano, wafanyikazi wanapozungumza na meneja.
- Matumizi ya kauli fupifupi/ lugha ya mkato. Kwa mfano, kazi ianze mara moja.
- Matumizi ya misimu kutegemea shughuli katika biashara husika. Kwa mfano, tunza wira.
- Kuchanganya ndimi/ msimbo/ lugha.
- Kuhamisha msimbo/kubadili msimbo/ kugeuza msimbo.
- Matumizi ya lugha rasmi hususan mikutanoni.
- Kurudiwarudiwa kwa kauli/ matumizi ya lugha yenye uradidi.
- Matumizi ya lugha isiyo sanifu.
- Matumizi ya lugha ya ishara ili kupunguza mawasiliano ya mazungumzo.
- Matumizi ya lafudhi.
- Matumizi ya maswali na majibu/udadisi.
- Matumizi ya maswali ya balagha.
- Lugha ya utani.
- Maelezo/matimizi ya sentensi ndefu
- Matumizi ya tamathali za usemi. 8x1
Kutaja - 1⁄2
Mfano - 1⁄2
- Biashara/ viwandani/ sokoni
Join our whatsapp group for latest updates
Tap Here to Download for 50/-
Get on WhatsApp for 50/-
Download KISWAHILI Paper 2 Questions and Answers - KCSE 2022 Past Papers.
Tap Here to Download for 50/-
Get on WhatsApp for 50/-
Why download?
- ✔ To read offline at any time.
- ✔ To Print at your convenience
- ✔ Share Easily with Friends / Students