Kiswahili Paper 2 Questions and Answers - 2021 KCSE Eldoret Diocese Mock Exams

Share via Whatsapp

Maswali

MAAGIZO

  • Jibu maswali yote.
  •  Majibu yote lazima yaandikwe kwa lugha ya Kiswahili.

 

  1. Ufahamu (Alama 15)
    Soma makala haya kwa uangalifu kisha ujibu maswali yanayofuata.

    Asubuhi hiyo kabla ya mrauko wa watu wengi kama ilivyokuwa ada ya wanakijiji cha Kaulizeni, Kabibi alimrausha mumewe Mzee Mori kwa lengo la kumpeleka kwenye zahanati ya pale pao – heko kwa mfumo mpya wa kiutawala uliotokana na kuanza kutekelezwa kwa katiba iliyoasisi ugatuzi na hapo kuwezesha taasisi zitoazo huduma nyingi muhimu kuletwa karibu na wananchi. Miaka michache iliyopita, wangehitajika kutumia zaidi ya saa nne kufikia kituo cha matibabu kilichokuwa karibu nao. Aidha, wangetakiwa kutumia matwana ambayo haikuwa rahisi kukodeshwa kutoka kwa mwenyewe kwa sababu ya zile barabara zilizoogopa kusakafiwa kutokana na utepetevu wa viongozi wao katika siku zilizotangulia. Chepkwony hakupenda kutesa gari lake kwa kuliruhusu kupitia barabara hizo ambazo ubovu wake ulitia fora. Magenge yaliyosongamana barabarani na mawe yaliyosimama wima ni kama yanapiga saluti yalikuwa tayari kuhujumu vigari vya wachochole kama yeye. Licha ya hofu hii, mara mojamoja alijitolea na kuwanusuru wanakijiji waliochungulia kaburi na akina wajawazito ambao siku zao zilikuwa zimetimia. Aghalabu, ubovu wa barabara hizi ulihakikisha kwamba wengi wao walitua mizigo yao kabla ya kuwasili katika Zahanati ya Nusura.

    Leo hii, imewachukua dakika ishirini hivi, mwendo wa miguu na lau wangepata pikipiki, au ‘nduthi’ kama vijana wanavyoziita kwa kilugha legevu chao, ingewachukua chini ya dakika tatu kukamilisha safari hii. Mambo yametengenea kwelikweli. Ule mgao wa serikali ya kaunti kutoka kwa hazina kuu ya serikali ya kitaifa ulitumiwa kwa uwajibikaji mkubwa na gavana wao kwa ushirikiano na mwakilishi wa kata hiyo kwenye bunge la kaunti. Na hii sio natija ya pekee iliyopatikana kutokana na mabadiliko haya ya kisiasa. Kabla siku ya leo, ilimbidi mkazi yeyote wa Kijiji cha Kaulizeni ajiandae vyema kabla ya kuenda zahanatini kwa matibabu kwa chamcha kilicholiwa asubuhi au kupakiwa kwenye mifuko ya sandarusi kabla ya kupigwa marufuku na shirika linalodhibiti ubora wa mazingira maarufu kama NEMA, ili kiliwe huko ukisubiri kuhudumiwa. Ama kweli milolongo iliyopangwa kuingia katika kila sehemu hapo zahanatini ilikuwa mirefu: si pa usajili, si pa uchunguzi wa daktari, si pa malipo, si maabarani, si pa dawa na hata msalani foleni ilikuwapo si hoja kwamba uchafu uliokuwepo ulitosha kumfanya mja apoteze haja ya kuzuru huko ghafla.

    Ilisemekana kwamba wafanyakazi wa hapo zahanatini ndio walisababisha chelewesho hili na kufanya foleni kurefuka katika kila idara. Mathalani, madaktari walisemekana kuingia kazini saa nne hivi baada ya kupitia kliniki zao za kibinafsi na kuondoka kabla ya saa tisa. Maafisa wa usajili nao walificha majalada maksudi ili kubembeleza kadhongo kutoka kwa wagonjwa kabla kuanzisha usajili wao. Wale wanaohusika na dawa walizoea kuwambia wagonjwa kuwa dawa zilikuwa zimeisha na kuwaelekeza kwenye maduka ya wauza dawa karibu sana na zahanati yenyewe. Halafu ukifika huko na kununua dawa, unapigwa na butwaa kuona dawa ulizouziwa zikiwa na nembo ya serikali. Hakika waso haya wana mji wao. Sikuelewa ni kwa nini udokozi wa namna hii ulifanywa hadharani mchana wa Mungu.

    Kwenye maabara kulisemekana kwamba kemikali maalum za kutumiwa kupima maradhi hazikuweko hivi kwamba matokeo ya uchunguzi yalionyesha kwamba kila mgonjwa alikuwa na aina ile ile ya ugonjwa. Maarufu miongoni mwa maradhi yaliyodhihirishwa maabarani ilikuwa malaria na homa ya matumbo. Sasa haikuwa ajabu mtu kutilia shaka uchunguzi uliofanywa katika maabara haya. Matokeo haya yalitolewa baada ya kipindi kirefu cha kusubiri kwa wastani saa mbili na nusu! Usishangae kwamba wakati wa kipindi hiki cha kusubiri, wangeonekana wakiwa katika harakati kama wahandisi wanaokarabati mtambo maalum wa tarakilishi mara wanakoroga, mara wanamimina majimaji vyomboni au wanakonyeza macho kutazama miujiza waliyotambua wao pekee yao kama wanajimu wanaozuru anga za juu. Wale wa idara ya malipo walikuwa maarufu kwa kuwambia wateja wao kwamba hawakuwa na hela za kuwarejeshea kama mabaki yao; wakawa na masalio ambayo, kama kawaida kidogo kidogo hujaza kibaba, yalizalisha maelfu ya pesa katika kipindi kifupi na kunenepesha mifuko yao.

    Gavana wa gatuzi hili alifagilia mbali uchafu huu wote. Mori alihudumiwa katika kipindi cha chini ya saa moja baada ya ugonjwa wake kupatikana. Ugonjwa wake ulikuwa ni mwiba wa kujidunga ambapo mhasiriwa hastahili kuambiwa pole. Ukaidi wao uliwafanya kukataa kulala chini ya vyandalua vya kuwazuia wadudu wasababishao maradhi haya sugu kwa kuongozwa na imani potofu eti vyandalua huzuia usingizi. Usisahau kwamba vilitolewa bure kwa kila mkazi wa gatuzi hili kupitia mapango maalum wa rais wa taifa mojawapo la ulimwengu lenye ustawi mkubwa wa viwanda. La kuchekesha zaidi ni kuviona vyandalua walivyopewa vikiwa vimetumiwa kuzingira vitalu vilivyopandwa mboga. Hiki ndicho kinaya kilichozuliwa na Mori na mkewe hata wakawa windo rahisi kwa mbu.

    Maswali
    1. Orodhesha hoja tatu zinazoonyesha maendeleo yaliyotokana na ugatuzi kulingana na makala. (alama 3)
    2. Kabla ya ugatuzi, wafanyakazi wa vituo vya afya walikuwa wanawanyanyasa wagonjwa. Taja makosa matano yaliyofanywa na wafanyakazi mbalimbali wa vituo vya afya. (alama 5)
    3. Wataje viongozi wawili wa kuchaguliwa wanaozungumziwa na msimulizi. (alama 2)
    4. Nakili neno moja kutoka aya ya pili lenye maana sawa na plastiki. (alama 1)
    5. Taja jina la ugonjwa aliokuwa anaugua Mzee Mori. (alama 1)
    6. Eleza maana ya maneno yafuatayo kama yalivyotumiwa kifunguni. (alama 3)
      1. kuhujumu …………………………………………………………………………………….
      2. chamcha ………………………………………………………………………………………
      3. unapigwa na butwaa ………………………………………………………………………….

  2. Ufupisho (Alama 15)
    Soma makala kisha ujibu maswali yanayofuata.

    Kilimo ni moja kati ya shughuli muhimu sana zinazotekelezwa na binadamu katika vizazi vyote na hujishughulisha na upanzi wa mimea na ufugaji wa wanyama. Maisha ya binadamu katika nyanja zote hutegemea kilimo hivi kwamba endapo harakati za kilimo zitasitishwa, bila shaka maisha ya binadamu yatafikia kikomo. Chakula na mavazi ya binadamu hupatikana kutokana na shughuli hii muhimu na imekuwepo maishani mwa binadamu kwa karne nyingi. Wataalamu wa historia husema kwamba kilimo kilianza wakati ambapo ustaarabu wa binadamu ulianza kustawi yaani kadri binadamu alivyoanza kukumbatia ustaarabu ndivyo kilimo kilianza kustawi hali kadhalika. Kabla ya kustawi kwa kilimo, binadamu wa kwanza aliishi maisha ya kulumbata wanyama akikusanya miti, majani, maganda, mizizi na matunda kwa ajili ya kujikimu maishani mwake. Katika kipindi hiki mtindo huu wa kupata chakula na mavazi ya binadamu ulikuwa mwafaka mradi hakuweza kutindikiwa na chochote.

    Baadaye dharura ya kuwa na utaratibu tegemevu wa kujipatia maslahi ya binadamu ikatokea kwa sababu ya kuendelea kuongezeka kwa idadi ya watu, pakawa na haja ya kulainisha mfumo wa uzalishaji wa chakula na kutimiza mahitaji mengine ya kibinadamu. Matokeo ya juhudi hizi yalianzisha shughuli ya uvuvi, uwindaji wa wanyama na ndege na ukusanyaji wa vyakula mbalimbali na kuvihifadhi. Harakati za kusaka chakula kwa wingi zikashadidi katika kila janibu za ulimwengu. Hii ilifuatiwa na kuanza kufuga wanyama waliozalisha bidhaa kama vile maziwa, nyama, ngozi na mayoya yaliyotumiwa kutengeneza mavazi. Wanyama waliofugwa hivi, baada ya miongo fulani, wakaanza kutumiwa mashambani kufanya kazi ya kusaidia kuandaa mashamba kwa minajili ya kuzalisha vyakula.

    Ustaarabu ulipoimarika zaidi kutokana na mpito wa wakati, mahitaji ya chakula kilichozalishwa kupitia kilimo yakawa makubwa kushinda chakula kilichokuwepo kwa ajili ya kuyakimu mahitaji ya binadamu katika kipindi hicho cha kizazi cha binadamu. Jambo hili lilisababisha haja ya kubuni mbinu mpya na bora zaidi za uzalishaji wa chakula kutokana na matumizi ya ardhi.Aghalabu katika baadhi ya sehemu, uzalishaji ulizuiwa na hali ngumu ya hewa kwa sababu ya mvua isiyotegemewa, ama ichelewe au ipotee kabisa na kusababisha kiangazi kilichonyausha na kukausha mimea mashambani. Mimea mashambani inaachwa ikisononeka kutokana na uhaba au ukosefu kabisa kabisa wa maji. Ili kukabiliana na changamoto hii ya hali ya hewa, mitaro mikubwa ilichimbwa kutoka maeneo ya maji kama vile mabwawa, mito ya kudumu, maziwa na vidimbwi ili kuelekeza maji mashambani na kuwezesha mimea kustawi ipandwapo. Huu ulikuwa mwanzo wa kilimo cha kunyunyizia maji mashambani. Mtindo huu ulistawi zaidi nchini Misri Kaskazini mwa Bara la Afrika kwa sababu ya kuwepo kwa Jito la Nile. Mbali na kutumia mtindo wa kunyunyizia maji mashambani ili kuimarisha uzalishaji, haja ilizuka ya kuimarisha aina ya mbegu zilizopandwa ili kuongeza kiwango cha mazao ambayo yangepatikana hata katika eneo dogo. Kadhalika, mbegu zilizoimarishwa hivi zilikuwa na uwezo wa kuhimili hali ngumu ya hewa kama kiangazi, magonjwa na wadudu waharibifu. Hizi zilikuwa baadhi ya hatari zilizokumba mimea na kudunisha kiwango cha mazao yanayotoka kwenye mashamba. uzalishaji.

    Usisahau kwamba uvumbuzi wa viwanda ulipozuka kule Ulaya, vifaa bora vya kutumia katika kilimo vilivumbuliwa. Vifaa hivi vilikuwa kama vile plau na tingatinga na vilisaidia sana kuandaa konde kwa njia bora zaidi na tena kwa kipindi kifupi. Hatua hii iliimarisha mchakato mzima wa kuendeleza kilimo kwa manufaa ya binadamu. Kwa kweli akili ni mali na si mali tu bali ni mali ya aina yake. Ni dhahiri kwamba mti hauwezi ukaenda pasipo na nyenzo.
    1. Fupisha aya mbili za kwanza ukitumia kati ya 70 na 80. (alama 6)
      Matayarisho
      Nakala Safi
    2. Kwa maneno 80 hadi 90 kuandika hoja muhimu katika aya ya tatu na ya nne. (alama 9)
      Matayarisho
      Nakala Safi
  3. Matumizi ya Lugha (Alama 40)
    1. Taja na ainisha konsonanti zilizo katika neno ‘ng’ata’ ukizingatia ala za kutamkia. (alama 1)
    2. Toa mifano minne ya maneno yenye irabu tatu pekee katika Kiswahili sanifu. (alama 2)
    3. Onyesha silabi zenye kutiliwa mkazo wakati wa kutamka maneno yafuatayo: (alama 1)
      1. ombea ………………………………………….
      2. hakimu ……………………………
    4. Eleza maana mbili tofauti katika sentensi: (alama 2)
      Dumu na mwanawe Bor ni waimbaji hodari.
    5. Tunga sentensi mojamoja ukitumia kivumishi cha pekee - ingineo ukianza kwa maneno yafuatayo: (alama 3)
      1. sisimizi:
      2. mkanda:
      3. kuchoka:
    6. Andika muundo wa sentensi hii kwa kutumia msitari. (alama 2)
      Mgogoro huo ulimalizika leo kwa mapatano.
    7. Ainisha mofimu katika neno ‘iue’. (alama 2)
    8. Onyesha kisha uainishe nomino katika sentensi hii: (alama 3)
      Kipakatalishi cha Wangila kina kasi kubwa.
    9. Akifisha sentensi hii: (alama 3)
      umeanza kusoma tamthilia ya kigogo kigogo alimuuliza kangogo.
    10. Kanusha:
      1. Wanafunzi wengi wameenda kucheza kandanda katika shule jirani. (alama 1)
      2. Tukianza safari yetu asubuhi tutachelewa kikaoni. (alama 2)
    11. Andika kwa kinyume:
      Wananchi wengi walihudhuria mkutano ndani ya uga wa Kitaifa. (alama 2)
    12. Geuza katika umoja au wingi kulingana na maagizo ndani ya mabano mwishoni mwa kila sentensi.
      1. Idara mpya iliundwa na mkurugenzi wa kampuni hiyo. (wingi) (alama 1)
      2. Vyungu vya kupikia vimesahaulika na wapishi. (umoja) (alama 1)
    13. Tunga sentensi zilizo na miundo ifuatayo:
      1. S - KN (W+V) + KT (T+E) (alama 2)
      2. S - KN (N)+ KT (T) (alama 1)
    14. Andika sentensi hii ukitumia maneno yenye maana sawa na yale yaliyopigiwa mistari. (alama 2)
      Banati alishusha beramu saa kumi na mbili jioni.
    15. Kwa kutumia sentensi moja, tofautisha vitate vifuatavyo: sima, zima (alama 2)
    16. Ni methali gani inayolengwa na maelezo yafuatayo? (alama 1)
      Panapokuwa na juhudi katika jambo lolote hata likiwa gumu, hatimaye ufanisi hupatikana.
    17. Tumia nahau ‘ng’oa nanga’ katika sentensi ili kudhihirisha maana yake. (alama 1)
    18. Jaza pengo kwa vihisishi mwafaka. (alama 3)
      Unapotaka kupishwa hutumia neno ………………………………. na ……………………….. ni tamko la kuagana mnapoachana na mtu usiku kama ambavyo ……………………………. hutumiwa unapomwomba mtu msamaha kwa kumkosea.
  4. Isimujamii (Alama 10)
    Andika sifa kumi za lugha utakayotumia ukipata fursa kutangaza mchezo wa kandanda. (alama 10)

Mwongozo wa Kusahihisha

  1. Ufahamu (alama 15)
    1. Maendeleo yaliyotokana na ugatuzi
      1. Huduma muhimu zimeletwa karibu na watu/wananchi.
      2. Barabara zimeimarishwa.
      3. Huduma zahanatini zimeimarika.
        (3 x 1= 3)
    2. Makosa ya wafanyikazi katika vituo vya afya
      1. Madaktari waliingia kazini wakiwa wamechelewa.
      2. Maafisa sajili walificha majalada maksudi/walidai kadhongo kabla ya kutoa majalada.
      3. Maafisa wa dawa waliuza/waliiba dawa za serikali na kuwauzia wagonjwa.
      4. Maafisa maabara walikosa kemikali za kupima magonjwa.
      5. Maafisa wa maabara walichelewesha matokeo ya uchunguzi wa magonjwa. (saa mbili u nusu)
      6. Maafisa wa maabara hawakuwarejeshea wagonjwa mabaki ya hela baada ya malipo.
        (5 x 1= 5)
    3. Viongozi wa kuchaguliwa kwenye makala
      1. gavana
      2. mwakilishi wa kata
        (2 x 1= 2)
    4. Neno moja la maana ‘plastiki’
      1. sandarusi
        (1 x 1= 1)
    5.  Jina la ugonjwa wa Mzee Mori
      1. malaria
        (1 x 1= 1)
    6. Maana ya maneno
      1. kuhujumu – kuharibu, kudhuru
      2.  chamcha – chakula cha mchana
      3. unapigwa na butwaa – unashangaa, unapatwa na mshangao
        (3 x 1= 3)
  2. Ufupisho (alama 15)
    1. Hoja katika aya mbili za kwanza
      1. Kilimo ni moja kati ya shughuli za binadamu.
      2. Hujishughulisha na upanzi wa mimea na ufugaji wa mifugo.
      3. Maisha ya binadamu hutegemea kilimo.
      4. Kilimo kimekuwa maishani mwa binadamu kwa karne nyingi.
      5. Kilimo kilianza ustaarabu ulipostawi.
      6. Kabla ya kilimo binadamu aliishi maisha ya kukusanya.
      7. Dharura ya kuwa na utaratibu tegemevu ikatokana na kuongezeka kwa idadi ya watu.
      8. Harakati za kusaka chakula zikashadidi kote.
      9. Hii ilifuatiwa na kufuga wanyama kwa ajili ya bidhaa zao.
      10. Baada ya miongo wanyama wakatumiwa mashambani kufanya kazi.
        (hoja 8 x 1 = 8)
    2. Hoja muhimu katika aya ya tatu na ya nne
      1. Ustaarabu ulipoimarika mahitaji ya chakula yakawa makubwa.
      2. Ilibidi kubuni mbinu mpya na bora za uzalishaji wa chakula.
      3.  Katika baadhi ya sehemu, uzalishaji ulizuiwa na hali ngumu ya hewa.
      4. Ili kukabaliana na hali hii, mitaro ilichimbwa kutoka maeneo ya maji na kuelekeza maji mashambani.
      5. Haja ilizuka ya kuimarisha aina ya mbegu zilizopandwa.
      6. Uvumbuzi wa viwanda ulipotokea vifaa bora vya kilimo vilivumbuliwa.
      7. Hatua hii iliimarisha na kuendeleza kilimo kwa manufaa ya binadamu.
        (hoja 6 x 1 = 6)
        a) - 8
        b) - 6
        Ut – 1
        Jumla - 15
  3. Matumizi ya Lugha (alama 40)
    1. Kutaja na kuainisha konsonanti katika nenop ‘ng’ata’ kwa mujibu wa ala za kutamkia
      1. /ng’/ - kaakaa laini, /t/ - ufizi/ masine
        (2 x ½ = 1)
    2. Maneno yanayoundwa kwa irabu tatu pekee
      1. aua
      2. aoa
      3. eua 
      4. iue 
      5. uue
        (4 x ½ = 2)
    3. Silabi zenye shada
      1. ombea ii. hakimu (2 x 1 = 2)
    4. Maana mbili za sentensi
      1. Bor ni mwanawe Dumu.
      2. Mwana ni wa Bor.
        (2 x 1 = 2)
    5. Kutunga sentensi kuanzia nomino na kivumishi cha pekee ‘-ingineo’
      1. Sisimizi mwingineo atakuuma. / Sisimizi wengineo watakuuma. (ngeli ya a – wa umoja na wingi)
      2. Mkanda mwingineo umekatika.
      3. Kuchoka kwingineko kutanilemea.
        (3 x 1 = 3)
    6. Kuandika muundo wa sentensi katika msitari
      1. Mgogoro huo ulimalizika leo kwa mapatano
        S- KN(N+V) + KT(T+E+H+N)
        (2x1 = 2)
    7. Mofimu katika neno: ‘iue’
      • i – ngeli/idadi/wingi/yambwa
      • -u – mzizi
      • - e - kiishio/ uamrishaji
    8. Kuainisha nomino katika sentensi
      • Kipakatalishi cha Wangila kina kasi kubwa.
             kawaida            pekee               dhahania
        (3 x 1 = 3)
    9. Kuakifisha sentensi
      • “Umeanza kusoma Tamthilia ya ‘Kigogo’?” Kigogo alimuuliza Kangogo.
        (Herufi kubwa – 1, alama usemi – 1 na nukuu za kitabu na kiulizi – 1)
    10. Kukanusha sentensi
      • Wanafunzi wengi hawajaenda kucheza kandanda katika shule jirani. (1 x 1 = 1)
      • Tukianza safari yetu asubuhi hatutachelewa kikaoni. Au
      • Tusipoanza safari yetu asubuhi hatutachelewa kikaoni. (1 x 1 = 1)
    11. Kinyume cha sentensi
      • Wananchi wachache walihudhuria mkutano nje ya uga wa Kitaifa. (2 x 1 = 2)
    12.           
      1. wingi: Idara mpya ziliundwa na wakurugenzi wa kampuni hizo. (4 x ½ = 2)
      2. umoja: Chungu cha kupikia kimesahaulika na mpishi. (4 x ½ = 2)
    13. Mifano ya sentensi zenye miundo
      1. S – KN (W + V) + KT (T+E)
        Wale wengine wanatembea haraka.
        (2 x 1 = 2)
      2. S – KN (N) + KT (T)
        Shairi litaimbika.
        (2 x ½ = 1)
    14. Visawe vya maneno katika sentensi
      1. banati – binti, msichana, ii. alishusha – aliteremsha, iii. beramu – bendera kumi na mbili – thenashara (4 x ½ = 2)
    15. Sentensi moja yenye vitate ‘sima’ na ‘zima’.
      • Alizima moto baada ya kula sima. (2 x 1 = 2)
    16. Methali: Panapo juhudi jambo gumu hufanikishwa.
      • Papo kwa papo kamba hukata jiwe.
        (1 x 1 = 1)
    17. Kutumia nahau ‘ng’oa nanga’ katika sentensi kuonyesha maana yake
      • maana – anza shughuli fulani kv kazi au safari
      • mfano: Tuling’oa nanga alfajiri kwenda kumwona mjomba. (1 x 1 = 1)
    18. Kujaza pengo kwa vihisishi
      • Unapotaka kupishwa hutumia neno simile/sumile/hebedari/hela/heria/hebu na alamsiki ni tamko la kuagana mnapoachana na mtu usiku kama ambavyo samahani/kunradhi/kumradhi hutumiwa unapomwomba mtu msamaha kwa kumkosea.(3 x 1 = 3)
  4. Isimujamii
    1. Wachezaji watarejelewa kwa majina yao halisi – Oliech, Mariga, Kadenge
    2. Kuwa na kauli zisizokamalika – Anampa mpira kisha….
    3. Kuwepo kwa takriri- Hatari! Hatari! Mariga! Mariga! Mariga!
    4. Kuwepo kwa vihisishi- aa! la! la! la! laa!
    5. Kuna na chuku - Amefunga bao la kimataifa.
    6. Kuna kuchanganya ndimi- Inakuwa offside.
    7. Kuwepo kwa jazanda - Ngoma inatoka nje.
    8. Tashihisi itatumiwa - Mpira unaenda nje.
    9. Taswira - Arudi nyuma na kuachilia mkwaju kimo cha nyoka.
    10. Sentensi ndefu-X alimpa Y naye akampiga chenga za dharau Z na kukubaliana na kipa kisha kuvuta kwaju zito lililomwacha kipa akiduwaa.
    11. Utohozi - goli, kipa, mpira wa kona
    12. Maswali balagha - Hata kama ni wewe ungezuia bao hilo?
    13. Matumizi ya misimu –
      (Sifa 10 na mifano ambatani x 1 = 10) 
Join our whatsapp group for latest updates

Download Kiswahili Paper 2 Questions and Answers - 2021 KCSE Eldoret Diocese Mock Exams.


Tap Here to Download for 50/-




Why download?

  • ✔ To read offline at any time.
  • ✔ To Print at your convenience
  • ✔ Share Easily with Friends / Students


Get on WhatsApp Download as PDF
.
Subscribe now

access all the content at an affordable rate
or
Buy any individual paper or notes as a pdf via MPESA
and get it sent to you via WhatsApp

 

What does our community say about us?

Join our community on:

  • easyelimu app
  • Telegram
  • facebook page
  • twitter page
  • Pinterest