Kiswahili Paper 2 - 2021 KCSE Prediction Questions and Answers Set 1

Share via Whatsapp

Maagizo

Jibu maswali yote

 

 1. UFAHAMU ALAMA 15

  Shule yangu ya upili

  Majio yangu katika shule hii ya upili hayakutokea kwa bahati nasibu bali kwa mipango kabambe niliyoianza tangu nikiwa shule ya vichekechea. Nikiwa sitetereki hata kwa wazazi wangu waliponisihi nijiunge na shule nyingine za karibu nikawa sisikii la mwadhini wala la mteka maji msikitini. Nikawa na ragba ya mkanja nikingoja siku ya kujiunga na shule yenyewe. Kweli majuto ni mjukuu na huja kinyume.

  Nilizaliwa katika aila yenye nafasi iliyotopea na kubobea katika ukwasi uliodhihirika kutokana na mitaa tulikoselelea kwa muda kabla ya baba kuaamua kununua nyumba yake mwenyewe huko upande wa Karen hivyo tukagura kutoka Runda. Wakati wa likizo tukawa tunaruka hadi pwani ambako mama yangu alikuwa amemiliki jumba lililokuwa katika ufuo wa bahari lililojengwa katika kipande kisichopungua ekari tatu alilotunukiwa wakati wa nikahi yao na wakwe wa baba yangu.

  Wavyele wangu wakawa wanaendesha magari meusi ya kifahari ingawa sikuwahi kumwona mama akichangamka kuendesha magari yake ya maana, kila macheo ya siku za kazi gari lililoendeshwa na dereva ambaye alimstahi mama hadi akawa anamfungulia mlango wa gari na kuufunga baada ya mama kujitoma katika tumbo la gari lilimjia na kumrejesha kwa wakati. Nikajiunga na shule ya msingi ya kibinafsi ambako nilishughulikiwa kama kikembe. Wengi wa wale tuliosoma nao walikuwa wa tabaka langu na walikuwa wametoka katika kila sehemu nchini Kenya.

  Hayawi hayawi huwa na siku ya kuripoti ikafika. Alfajiri, dereva mmoja akatumwa kwenda hadi Kisumu ili atulaki na kutusafirisha kutoka uwanja wa ndege hadi shule ya upili ambayo ilikuwa yangu ya rohoni. Nasi tukaelekea hadi uwanja wa ndege ili turuke hadi Kisumu. Safari yetu kutoka kitongoji cha kifahari hadi Airport ilikuwa njema, safari yetu tulipoabiri ndege ilikuwa bila bughudha, safari yetu kutoka Kisumu mjini haikuwa na kasoro na tulienda kulingana na mpango. Safari yetu ilikuwa mufti hadi tulipofika katika lango la shule ya kitaifa! Tulipotia ozi tu!!....jamani......jamani nikafa moyo. Labda mama aliweza kubaini mabadiliko ya hisia zangu, nilitamauka, nikawa mchege na kusema kweli niliyoyaona sikuamini. Mvua iliyokuwa imepasua hapo awali ilikuwa imeacha vitua vya maji kwenye vijia vya kutembea vilivyochakaa na kubomoka bila yeyote kujali kuvikarabati. Majengo yalikuwa makongwe yaliyojengwa miaka mia moja iliyopita na yalistahili kuitwa makafadhi badala ya pahali pa kumkaribishia mwanafunzi aliyepita kwa alama mia nne na thelathini na tano. Asiye na wake ana Mungu, nikapiga moyo konde lazima nisajiliwe katika shule ya ndoto langu. Ningewezaje kughairi wazo langu baada ya siku hizo zote za maandalizi tena mbele ya wanuna walioniona kama kielelezo chao tangu walipozaliwa. Nikasajiliwa!

  Sikujua, hakika sikujua, sikujua shule ya upili ya kitaifa yaweza kuwa hivi. Kweli mwanafunzi aweza kukosa viatu na hata kushindwa kununua rangi ya kupaka viatu hivyo iwapo amenunuliwa na wahisani? Nilimlaumu nina maana hakunieleza kuwa mtu anaweza kula chakula ambacho mbwa wetu hawezi hata kukiangalia. Nilipoingia katika ukumbi wa chakula nilihisi kitefutefu nusura nichafukwe na moyo, makapi ya mboga na uchafu usioelezeka ulinikumba, kisha nikapewa kisahani cha plastiki na kupakuliwa kipande cha ugali ambacho bado kilikuwa na unga na kuachiwa hiari ya kukila au kukitupa. Wenzangu wakawa wanakirambatia chakula kwa kasi huku mmoja wao alipoona jinsi nilivyokiangalia changu akanihisi nimpe chote na kukimaliza fyu. Wote walikuwa na furaha kemkem na kuajabia utukufu wa shule iliyotukuka ya kitaifa ila mimi.

  Baada ya mlo ‘rojo rojo’, tukaelekea darasani nilikopigwa na mghuma mkubwa. Tulikuwa wanafunzi hamsini na watano katika darasa moja tu! Mwalimu mmoja akaja na kutukaribisha shuleni kisha akatuarifu kuwa atakuwa mwalimu wa darasa letu. Nilipomsikia akinena nusura niishiwe na stahamala, kimombo chake kilinishangaza, hasa matamshi yake yalipungukiwa na kudhirisha athari za lugha ya asili. Nilihisi kana kwamba ningemrekebisha lakini sikudhubutu.

  Tukafululiza hadi bweni na nikajilaza kitandani chembamba huku mwingine nisiyemjua lakini asiyejua kuwa kuna nguo maalum za kulala akalala uchi katika ghorofa ya juu ya kitanda chetu. Mgeni njoo mwenyeji apone maana baada ya muda wadudu ambao sikuwahi kuwaona aushini mwangu wakanza kunishambulia. Nikaamka baada ya kumnasa mmoja wa wadudu hawa na kuuliza mmoja wa wenzangu ni wepi wadudu hawa na kwa kutojali hata kidogo, akanieleza kuwa hawana neno bali ni kunguni tu, sikujua na kwa kweli mama hakuniambia kuwa kuna wadudu wanaotafuna mtu na hunuka fye! Sikulala kwa hofu huku wenzangu wakiforota kwa njia ya kunighasi. Sikuwahi kudhani kuwa watu wengi wanaweza kulala chumba kimoja huku changu kikiwa na hamamu na vifaa vyote muhimu kikibaki bila mtu!

  Tulisomeshwa na walimu wasiojali kana kwamba tunaelewa au la. Hawakushughulika iwapo tulifanya kazi za ziada au la, ndio, hakujali chochote. Kilichonishangaza ni kuwa wanafunzi waliojiunga nasi kutoka shule za umma wenye alama duni waliwapenda na kuelewa haraka walichosomeshwa na hawakujali matamshi yao, labda hawakuyatambua.

  Hatimaye tukafanya mtihani wa mwisho wa muhula wa kwanza. Nilishangaa ghaya iliponibainikia kuwa aliyetuongoza alikuwa ghulamu mmoja mshamba niliyempuuza tu mvulana kutoka kijijini ambacho singetambua katika ramani ya nchi ambaye hata vitu vya kimsingi vilimpiga chenga. Nikafanya uchunguzi nikatambua mwenzangu alikuwa na alama mia mbili hamsini na tatu akitoka katika darasa la nane, nilifanikiwa kuwa nambari mia mbili hamsini na tatu kwa jumla ya wanafunzi mia tatu! Tulipofunga kwa likizo ya Pasaka nikaamua kuchukua hatua nyingine sitawahi kuhama kutoka shule hii ya upili wala kuwa zaidi ya nambari kumi! 

  Maswali

  1. Thibitisha kauli kuwa msimulizi ana msimamo dhabiti (alama 2)
  2. Tofautisha jinsi mwandishi alivyofunzwa katika shule ya kibinafsi na shule ya upili. (alama 3)
  3. Taja mambo matatu yanayotuonyesha kuwa msimulizi alilelewa katika aila ya kikabaila kulingana na aya ya pili.    (alama 3)
  4. Andika masuala matatu yaliyomshangaza katika shule ya upili (alama 3)
  5. Andika tamathali mbili zilizotumika katika kifungu. (alama 2)
  6. Eleza maana ya msamiati huu kama ulivyotumika katika kifungu.        (alama 3)
   1. alimstahi 
   2. kughairi 
   3. kunighasi 
 1. UFUPISHO ALAMA 15
  Soma makala yafuatayo kisha ujibu maswali                                                       

  Mwana wa Adamu ni kiumbe cha ajabu! Ni kiumbe kilichopewa uwezo wa kuhodhi na kumiliki kila kitu, kiumbe kilichopewa akili na maarifa fuvu tele ili kutaratibu shughuli na mambo: kiumbe kilichopewa uwezo wa kuwasiliana na kutumia sauti nasibu ili kuwa na urari na muwala; kiumbe kilichopewa uwezo wa kufaidi viumbe wengine kwa njia mbalimbali na jumla jamala; hiki ndicho kiumbe kilichopewa idhini maalum ya kuzaana na kujaza dunia. Huyu ndiye mwana wa mama Hawa ambaye sasa amegeuka ndovu kumla mwanawe.

  Kwa sababu ya bongo alizonazo, binadamu ana uwezo wa kutumia teknolojia kwa manufaa yake na ithibati zipo tele. Binadamu ametumia nyambizi kuzuru chini ya bahari, amefika mwezini, amevumbua magala: amevumbua uyoka: amevumbua tarakilishi na sasa shughuli zake ni za kutandaridhi. Mwenyewe yuasema kuwa dunia yake imekuwa kitongoji katika muumano huu.

  Chambilecho wavyele, akili nyingi huondoa maarifa. Binadamu amekuwa dubwana linalojenga kushoto na kubomoa kulia na tuna sababu ya kulisoza dubwana hili kidole. Rabana ndiye msanii asiye mfanowe kwani aliisawiri murua. Rabuka akaona yote yalikuwa mema na mazuri: akamwambia binadamu,” Haya twende kazi!”

  Viwanda vya binadamu vinatiririsha maji-taka ovyo hadi mitoni, maziwani na baharini na matokeo yamekuwa ni vifo vya viumbe vya majini kama samaki ambavyo ni urithi aliopewa na muumba. Hakuna kiumbe kinachoweza kustahimili maisha bila maji safi. Maji yote sasa yametiwa sumu na binadamu kwa sababu ya ‘maendeleo’ yake. Joshi kutoa katika viwanda vivyo hivyo nalo limehasiri ukanda wa ozone ambao sasa umeruhusu jua kutuhasiri kwa joto kali mno. Siku hizi inasemekana kuwa kuna mvua ya aside inayonyesha katika baadhi ya sehemu za dunia na kuleta madhara makubwa. Labda hata mabahari yamekasirika kwa sababu hivi majuzi katika kile kilichoitwa ‘tsunami’, bahari lilihamia nchi kavu na kusomba maelfu ya binadamu na kuwameza wazima wazima. Vimbunga navyo vimetokea kwa wingi. Wataalamu wanasema kuwa viwango vya miyeyuko vitazidi kwa sababu ya joto na kiwango cha maji kitazidi pia. Binadamu atatorekea wapi?

  Idadi ya binadamu imezidi hadi kiasi asichoweza kukishughulikia kwa sababu anaijaza kiholela kwa sababu anadai kuwa aliruhusiwa kuijaza. Hii ni imani potovu. Anasahau kuwa alipewa ubongo wa kuwaza na kuwazua kabla ya kufanya chochote. Dhiki, maradhi na ufukara zimehamia kwa binadamu na kumtia kiwewe’

  Binadamu amefyeka misitu kwa kutaka makao, mashamba, mbao, makaa, ujenzi wa nyumba na barabara na mahitaji mengine mengi. Wanyama wamefurushwa na wengi kuangamia kwa sababu ya ukosefu chakula na wengine kushindwa kuhimili mabadiliko katika mazingira. Chemichemi za maji zimekauka nalo jangwa limeanza kutuzuru kwa kasi inayotisha. Kazi ya binadamu imekuwa ya kusukia kamba motoni. Itambidi aanze kujenga kwa matofali ya barafu.

  1. Bila kupoteza maana iliyokusudiwa na mwandishi wa taarifa, fupisha aya ya kwanza.
   (Maneno 40-50)   (alama 5)
  2. Kwa kuzingatia aya 4 za mwisho, eleza mambo muhimu yanayoshughulikiwa na mwandishi
   (maneno 95-105) (alama 8)

 

 

 1. MATUMIZI YA LUGHA. ALAMA 40
  1. Taja sifa mbili bainifu za irabu /u/ (alama 2)
  2. Tunga sentensi kwa kutumia kiwakilishi huru cha nafsi ya tatu umoja.        (alama 2)
  3. Andika umoja wa sentensi zifuatazo. (alama 2)
   1. Wakitaka tuwasamehe waje watuombe radhi kwa waliyotufanyia.
   2. Yaliyosemekana kuwa ni yao yameharibiwa na binamuo
  4. Yakinisha (alama 2)
   Hasikii la mwadhini wala la mteka maji msikitini.
  5. Bainisha shamirisho kipozi na kitondo katika sentensi ifautayo. (alama 2)
   Mama alimpikia mwanawe chakula alichokitamani sana.
  6. Tunga sentnesi moja yenye chagizo ya mahali na ya wakati. (alama 2)
  7. Onyesha mfumo wa sauti katika tungo: Mtumbwini. (alama 2)
  8. Tambulisha vipashio vitatu vya sarufi ya Kiswahili. (alama 3)
  9. Huku ukitoa mfano, eleza mantiki inayopatikana katika kauli ya kutendua. (alama 2)
  10. Taja matumizi manne ya kiambishi "ki". (alama 2)
  11. Eleza maana mbili ya sentensi ifuatayo. (alama 2)
   Jambazi lilimwibia Okoth gari jipya.
  12. Bainisha vishazi huru na vishazi tegemezi katika sentensi ifuatayo. (alama 2)
   Nitaenda maktabani ingawa ninaumwa na kichwa.
  13. Andika katika kauli ya kutendesha (alama 1)
   Ile pombe aliyokunywa Chacha ilimfanya alewe.
  14. Changanua kwa kutumia mtindo wa kielelezo matawi. (alama 4)
   Mtoto ambaye amefika ni ndugu yangu.
  15. Andika kinyume cha sentensi ifautayo. (alama 2)
   Huzuni alisifu nduguye aliyekusanya takataka zote.
  16. Tumia neno 'vibaya' kama:
   1. kivumishi
   2. Kielezi
  17. Tunga sentensi yenye kihuhishi cha 'A' - unganifu katika ngeli ya U - ZI. (alama 1)
  18. Mbwa wetu amekatwa mkia. Geuza katika hali ya ukubwa. (alama 2)
  19. Tunga sentensi moja kutofautisha maana ya maneno haya. (alama 1)
   Mkembe, mkebe
  20. Tumia ngali kutunga sentensi ili kuleta maana ya: (alama 2)
   1. Tendo katika hali ya kuendelea
   2. Tendo kutoweza kufanyika kwa sababu ya wakati kupita
 1. ISIMUJAMII (ALAMA 10)
  1. Kwa nini kulikuwa na haja ya kusanifisha lugha ya Kiswahili. Toa sababu tano. (alama 5)
  2. ….sote tunajua kwamba ni kudura. Makiwa!”
   1. Tambua sajili iliyotumika katika dondoo hili. (alama 1)
   2. Eleza sifa nne za sajili hiyo. (alama 4)

 

 

   MARKING SCHEME

 1. UFAHAMU
  1. Hatetereki anapoishiwa abadilishe wazo kuhusu shule ya ndoto lake.
  2. Uamuzi wa kutohama kutoka shule hii hata baada ya kuona yaliyompata. 2 x 1 = 2
   B: Shule ya binafsi
   • Alitunzwa kama kikembe.
   • Walimu waliomfunza walitamka kimombo kwa njia bora.
    Shule ya upili
   • Matamshi ya walimu yaliathiriwa na lugha ya asili. walimu wasiojali uelewa wa wanafunzi. Wasioshughulika wasipofanya kazi za ziada. zozote 3 x 1 = 3 
    C: Mitaa walikoishi
   • Uamuzi wa kununua nyumba Karen.
   • Kuruka hadi pwani.
   • Mama yake kumiliki jumba katika shamba la ekari.
   • tatu ufuoni. zozote 3 x 1 = 3
    D:
   • Mwanafunzi kukosa viatu.
   • Chakula duni katika shule hii.
   • Idadi ya wanafunzi katika darasa.
   • Kushambuliwa na wadudu.
   • Kuongozwa na mvulana wa alama 253. zozote 3 X 1 = 3
    E:
   • Uhuishi - Tumbo la gari.
   • Misemo - Ragba ya mkanja.
   • Takriri - Sikujua.
   • Methali - Mgeni njoo mwenyeji apone. 2 x 1 = 2
    F:
   • Alimstahi - Heshimu.
   • Kughairi - badilisha.
   • Kunighasi - kunikasirisha. 3 x 1 = 3
    Katika sehemu ya ufahamu adhibu ifuatavyo.
    1/x makosa 6 ya hijai = 3 1/x makosa 6 ya sarufi = Jumla 6
 2. UFUPISHO
  1.  
   1. Binadamu alipewa uwezo wa kumiliki kila kitu.
   2. Binadamu alipewa akili na maarifa ili kupanga mambo yake.
   3. Alipewa uwezo wa kuwasiliana na wenzake kwa kutumia lugha.
   4. Alipewa uwezo wa kufaidika kutokana na mazingira yake.
   5. Alipewa uwezo wa kuza na kujaza dunia. (Yoyote 5x1=5)
  2.  
   1. Binadamu amekuwa dubwana linalojenga na kubomoa.
   2. Viwanda vinachafua maji na kuua viumbe muhimu kwa binadamu.
   3. Moshi kutoka viwandani umedhuru ukanda wa ozone na joto kuzidi duniani.
   4. Idadi ya binadamu imeongezeka zaidi ya uwezo wake.
   5. Maradhi na ufukara yamekuwa matatizo makubwa kwa binadamu.
   6. Binadamu anafyeka misitu yote.
   7. Binadamu amewafurusha na kuwaangamiza baadhi ya wanyama.
   8. Chemichemi za maji zimekauka na kuwa jangwa. (Zozote 8x1=8)
    tanbihi : alama 1 ituzwe kwa mtirirko katika kila swali 
 1. MATUMIZI YA LUGHA: (Alama 40)
  1. Taja sifa mbili bainifu za irabu/u/. (alama 2)
   -irabu ya nyuma - Irabu mviringe/hutamkwa na mdomo ukiwa mviringo. 2x1=2
  2. Tunga sentensi kwa kutumia kiwakilishi huru cha nafsi ya tatu umoja (alama 2)
   -mf :Yeye atasoma kidagaa kimemwozea. (1x2=2
  3. Andika umoja wa sentensi zifuatazo (alama 2) .
   -Akitaka nimsamehe aje aniombe radhi kwa aliyonifanyia. 1x1=1
   - Lililosemekana ni kuwa lake limeharibiwa na binamuye. 1x1=1
  4. Yakinisha. (alama2)
   - Anaskia la mwadhini na lamteka maji msikitini. 1x2=2
  5. Bainisha shamirisho kipozi na kitondo katika sentensi ifuatayo. (alama 2)
   Kitendo-chakula
   kipozi -mwanawe                                           2x1=2
  6. Tunga sentensi moja yenye chagizo ya mahali na ya wakati. (alama 2)
   -mfano: Walienda uwanjani jana jioni                                   1x2=2 (mahali wakati )
  7. Onyesha mfumo wa sauti katika tungo: matumbwini. (alama 2)
   K+KI+KKKI+KI                                                         (4x½=2).
  8. Tambua vipashio vya sarufi ya Kiswahili (alama 3)
   - Sauti - Silabi - Neno – Sentensi (zozote 3 x 1=3
  9. Huku ukitoa mfano, eleza mantiki inayopatikana katika kauli ya kutendua. (alama 2)
   - Vitenzi katika kauli hii huwa na maana ya kinyume k.m funga - fungua fukia-fukua kosa-kosoa 1x2=2
  10. Taja matumizi manne ya kiambishi “ki” (alama 2)
   − Hutumiwa kuonyesha udogo wa nomino k.m kibuzi.
   − Hutumiwa kama kiamishi cha upatanisho wa kisarufi ngeli ya ki-vi.
   − Hutumiwa kufananisha na vielezi vya namna mfano.
   − Hutumika mwanzoni mwa majina ya lugha k.v Kiswahili.( ½x4=2)
  11. Eleza maana mbili ya sentensi ifuatayo (alama 2)
   − Jambazi lilimwaibia Okoth gari jipya.
   − Jambazi liliiba gari likampa Okoth.
   − Jambazi liliiba gari la Okoth. 2x1=2
  12. Bainisha vishazi huru na vishazi tegemezi katika sentensi ifuatayo (alama 2)
   -Nitaenda maktabani- Kishazi huru
   -ingawa ninaumwa na kichwa- Kishazi tegemezi 2x1=2
  13. Andika katika kauli ya kutendesha (alama 1)
   − Ile pombe aliyokunywa Chacha ilimlevya. 1x1=1
  14. Changanua kwa kutumia mtindo wa kielelezo cha matawi. (alama 4)
   KISWNRTE
  15. Andika kinyume cha sentensi ifuatayo. (Alama 2)
   - Huzuni alikashifu nduguye aliyetawanya takataka zote. 1x2=2
  16. Tumia neno “vibaya” kama:
   1. Kivumishi
    Vyombo vibaya vimetupwa    (1x1=1)
   2. Kielezi
    Aliimba wimbo huo vibaya. 1x1=1
  17. Tunga sentensi yenye kihusishi cha ‘a’- unganifu katika ngeli ya U-ZI. (alama 1)
   Ukuta wa nyumba umebomoka. (1x1=1)
  18. Mbwa wetu amekatwa mkia. Geuza katika hali ya ukubwa. (alama 2)
   Jibwa letu limekatwa jikia/kia /Jijibwa letu limekatwa jikia. (1x2=2)
  19. Tunga sentensi moja kutofautisha maana ya maneno haya. (alama 1)
   Mkembe, mkebe
   Sentensi iwe maana ya: mkebe- chombo cha bati kinachotumiwa kuweka vitu vidogo vidogo
   mkembe - mtoto mdogo mwenye umri baina ya mwaka mmoja na miaka sita au kijana aliyebaleghe ambaye hajoa.
  20. Tumia ngali kutunga sentensi ili kuleta maana ya: (alama 2)
   1. tendo kuendelea :Wanafunzi wangali wanacheza uwanjani (1x1=1)
   2. Tendo kutoweza kufanyika kwa sababu ya wakati kupita: Mwalimu angalikuwa na pesa angalienda ulaya. (1x1=1)
 2. ISIMU JAMII
  1. − Kuwepo kwa lahaja nyingi- baadhi yazo hazingeeleweka na kila mtu.
   − Kulikuwa na haja ya kuwa na hati sawa ya kuandika Kiswahili –Kul;ikuwa na hati nyingi kwa mfano ,Kirumi , kilatini na kiarabu.
   − Kulikuwa na haja ya kusawazisha maandishi ya kitaalamu katika kamusi.
   − Haja ya kuwa na lugha moja ya mawasiliano na elimu 
   –kutumika katika kamusi.
   − Haja ya kuwa na lugha moja ya mawasiliano na elimu 
   –kutumika katika mikutano, shuleni, vyuoni n.k (5x1=5)
  2. Sajili ya mazishi /matanga /kilio masikitiko /msiba/ maombolezo/uzikaji.
   Sifa
   − Msamiati maalum kwa mfano makiwa marehemu.
   − Lugha ya kufariji/liwaza
   − Yenye matumaini
   − Matumizi ya vihihisishi oh, wuui,
   − Lugha ya kusitasita
   − Huhusisha sana mambo ya kidini na Mungu na Imani za jamii.
   − Ni lugha ya hasira.
   − Kuchanganya ndimi
   − Inaadaman na viziada lugha
   − Matumizi ya sentensi fupi
   − Matummizi ya sentensi ndefu
   − Imesheheni sifa za m wendazake
   − Matumizi ya lugha isiyozingatia kanuni za kisarufi. Zozote 5x1=5) 
Join our whatsapp group for latest updates

Download Kiswahili Paper 2 - 2021 KCSE Prediction Questions and Answers Set 1.


Tap Here to Download for 50/-
Why download?

 • ✔ To read offline at any time.
 • ✔ To Print at your convenience
 • ✔ Share Easily with Friends / Students


Get on WhatsApp Download as PDF
.
Subscribe now

access all the content at an affordable rate
or
Buy any individual paper or notes as a pdf via MPESA
and get it sent to you via WhatsApp

 

What does our community say about us?

Join our community on:

 • easyelimu app
 • Telegram
 • facebook page
 • twitter page
 • Pinterest