Kiswahili Paper 3 Questions and Answers - Moi Kabarak High School Mock 2020/2021

Share via Whatsapp

Maagizo

  • Jibu maswali manne pekee.
  • Swali la kwanza ni la lazima.
  • Maswali hayo mengine yachaguliwe kutoka sehemu nne zilizobaki; yaani Riwaya, Hadithi Fupi, Ushairi na Fasihi Simulizi.
  • Usijibu maswali mawili kutoka sehemu moja.
  • Majibu yote ni lazima yaandikwe kwa lugha ya Kiswahili.

SEHEMU A: USHAIRI

  1. Lazima
    Soma shairi lifuatalo kisha ujibu maswali

    MVUNJA JASHO
    Kila mvunja jasho,
    Maishaye ya kesho,
    Si ya utajirisho,
    Achumacho ni posho,
    Mbaya wake mwisho,
    Lazima suluhisho,
         Lakini kwa vitisho.

    Wachimba migodi,
    Kwa juhudi,
    Bila yoyote kedi,
    Au na ukaidi,
    Na nyuma hawarudi,
    Kwa kuwa ni weredi,
          Lakini hafaidi.

    Wachimba mafuta,
    Watu waso matata,
    Huwa wanatafuta,
    Ardhini kuvuta,
    Na wakisha yapata,
    Wenyewe huwaita,
         Lakini kipato 'ta!

    Wavuvi baharini,
    Maisha yahatarini,
    Wakiwa safarini,
    Dhoruba na tufani,
    Samaki kwa matani,
    Yavuliwayo pwani,
         Lakini bei chini.

    Wakulima shambani,
    Majembe mikononi,
    Wao wa kilimoni,
    Asubuhi na jioni,
    Mazao kila fani,
    Vuno kuwa sokoni,
         Lakini pato duni.

    Nao wafanyakazi,
    Hutumia ujuzi,
    Kuchapa sana kazi,
    Wao wanienzi,
    Kwa huba na mapenzi,
    Bila ya ubazazi,
         Lakini malofa.

    Lazima waungane,
    Wanyonge washikane,
    Washirikiane,
    Dhuluma waikane,
    Lazima wapambane,
    Na wasaidiane,
          Lakini bila hofu.

    Maofisi balaa,
    Rushwa imezagaa,
    Uoza ulojaa,
    Hakuna manufaa,
    Tumepigwa butwaa,
    Na wengi kushangaa,
            Lakini twateswa.

    Maswali
    1. Huku ukitoa mifano mitatu, bainisha jinsi hali ya kinyume inavyojitokeza kwenye
      shairi hili. (alama 3)
    2. Mshairi amelipa shairi hili sura gani?   (alama 4)
    3. Ni vipi mshairi anaizindua jamii yake? Onyesha.      (alama 4)
    4. Uandike ubeti wa tano kwa lugha ya nathari.    (alama 4)
    5. Huku ukitoa mifano, onyesha umuhimu wa ukiukaji wa miundo ya kisarufi kwenye ubeti wa tatu. (alama 3)
    6. Eleza maana ya msamiati huu kama ulivyotumiwa kwenye shairi. (alama 2)
      1. Kedi
      2. Malofa

        SEHEMU YA B: RIWAYA
        A. MATEI: Chozi la Heri
        Jibu swali la 2 au la 3 

  2. “Vipi binadamu anavyoweza kuyazoa maji yaliyomwagika?"
    1. Eleza muktadha wa dondoo hili.   (alama 4)
    2. Taja na kufafanua tamathali ya usemi iliyotumiwa kwenye dondoo hili. (alama 4)
    3. Onyesha jinsi baadhi ya wanajamii katika jumuiya ya Chozi la Heri
      walivyomwagikiwa na maji.  (alama12)
  3. “ Haidhuru kuwa huenda wimbo huu unawaghasi waliolala. Atakalo mwimbaji huyu ni kutakasa hisia zake." Bainisha jinsi mrejelewa alivyotakasa hisia kwa kutumia wimbo wake kwa mifano mwafaka. (alama 20)

    SEHEMU YA C:TAMTHILIA
    P. Kea: Kigogo
    Jibu swali la 4 au la 5 

  4. “Sitaki kazi za uchafu hapa Sagamoyo."
    1. Eleza muktadha wa dondoo hili.   (alama 4)
    2. Kwa hoja kumi na sita, onyesha jinsi kazi za uchafu zinavyoendelezwa kwenye jimbo la Sagamoyo."
      (alama 16)
  5. Onyesha uhusiano uliopo baina ya wahusika hawa na maudhui ya hadithi. (alama 20)
    1. Majoka
    2. Tunu

      SEHEMU YA D: Hadithi Fupi
      A. Chokocho na Dumu Kayanda: Tumbo Lisiloshiba na Hadithi Nyingine
      Jibu swali la 6 au la 7 

  6. Mame Bakari- (Mohammed Khelef Ghassary)
    “Haikuwa stahiki yake kubebeshwa mzigo kama ule.”
    1. Fafanua muktadha wa dondoo hili. (alama 4)
    2. Taja na kueleza tamathali iliyotumiwa kwenye dondoo hili.  (alama 4)
    3. Onyesha jinsi mrejelewa alivyoathirika kwa kubebeshwa mzigo.  (alama 12)
  7.  
    1. Mwalimu Mstaafu- (Dumu Kayanda)
      "Hiari na mukhitari ni juu yako. Lakini yeye kafika nyumbani.”
      Eleza mawazo makuu ambayo mwandishi wa hadithi hii anayoibua kabla na baada ya kutolewa kwa usemi huu.     (alama 10)
    2. Ndoto ya Mashaka- (Ali Abdulla Ali)
      Anwani "Ndoto ya Mashaka” inaakisi barabara yaliyomo kwenye hadithi. Fafanua.     (alama 10)

      SEHEMU YA E: FASIHI SIMULIZI
    1. Kwa kutumia vipengele vitano, onyesha maingiliano yaliyopo baina ya fasihi simulizi na fasihi andishi. 
      (alama 5)
    2. Ni mambo gani huchangia kubadilika kwa kazi za fasihi simulizi?   (alama 10)
    3. Zitaje changamoto zozote tano za miviga katika jamii yoyote ile.       (alama 5)


Marking Scheme

  1. Lazima

    Maswali
    1. Huku ukitoa mifano mitatu, bainisha jinsi hali ya kinyume inavyojitokeza kwenye shairi hili.   (alama 3)
      • Anafanya kazi kwa bidii lakini anapata posho tu
      • Wachimba migodi hawafaidi
      • Wachimba mafuta wakiyapata huwafaa wengine
      • Wakulima huzalisha mazao mengi lakini wakiyauza hawapati faida.
      • Wavuvi huvumilia hatari za baharini lakini bei ya vuo lao huwa chini.
      • Wafanyakazi kwa ujumla huwa hawafaidi
        (Hoja za kwanza 3x1=3)
    2. Fafanua sura ya shairi hili.   (alama 4)
      • Shairi lina beti nane
      • Shairi lina mgao mmoja kwenye mishororo yake
      • Kila ubeti una vina tofauti isipokuwa ubeti wa nne na tano
      • Kila mshororo una mizani saba
      • Shairi halina kibwagizo
      • Shairi lina anwani: Mvunja Jasho
        (Zozote 4x1=4)
    3. Ni kwa njia gani mshairi anawazindua walengwa wake? (alama 4)
      • Anawashauri waungane- wanyonge washirikiane ili waikatae dhuluma - ubeti wa saba
      • Anapinga hali ya kuwa na rushwa ofisini- anasema rushwa haina manufaa
        (Hoja 2x2=4)
    4. Uandike ubeti wa tano kwa lugha ya nathari.  (alama 4)
      • Wakulima hufanya kazi kwa bidii shambani la
      • Huwa shambani kuanzia asubuhi hadi jioni
      • Wao huzalisha mazao ya kila aina
      • Wayapelekapo sokoni, malipo huwa duni
        (Hoja 4x1=4)
    5. Huku ukitoa mifano, onyesha umuhimu wa ukiukaji wa miundo ya kisarufi kwenye ubeti wa tatu. (alama 3)
      • Inkisari- waso- wasio
                          'ta- hata
      • Mazida- aridhini- ardhini
        Idhini zote mbili zimetumiwa kuleta urari wa mizani
        (Kutaja idhini 2x1=2, Kueleza sababu 1x1=1)
    6. Eleza maana ya msamiati huu kama ulivyotumiwa kwenye shairi. (alama 2)
      1. Kedi- hila/kiburi/majivuno
      2. Malofa- maskini/ mtu asiye na chochote
        (2x1=2)

        SEHEMU YA B: RIWAYA
        A. MATEI: Chozi la Heri
        Jibu swali la 2 au la 3 

  2. “Vipi binadamu anavyoweza kuyazoa maji yaliyomwagika?"   (alama 4)
    1. Eleza muktadha wa dondoo hili.
      • Haya ni maneno ya Mwanaheri
      • Alikuwa akiwaambia Kairu, Zohali na Umu.
      • Walikuwa katika shule ya upili ya Tangamano.
      • Ni baada ya wao kukutana na kusimuliana kuhusu masaibu yaliyowaleta pale.
        (Hoja 4x1=4)
    2. Taja na kufafanua tamathali ya usemi iliyotumiwa kwenye dondoo hili. (alama 4)
      • Jazanda (alama 1)
      • Kuyazoa maji yaliyomwagika (alama 1)
      • Kurekebisha mambo yaliyoharibika au hata kwenda kombo. Hapa Mwanaheri anarejelea masaibu yaliyomfisha mamake. (1x2=2)
        (Kutambua tamathali ni alama 1, kuiandika alama , na kisha maelezo yake ni alama 2)
    3. Onyesha jinsi baadhi ya wanajamii katika jumuiya ya Chozi la Heri walivyomwagikiwa na maji.  (alama 12)
      • Lunga anaachwa na mkewe Naomi hali inayomletea kihoro na maradhi baadaye.
      • Umu na nduguze wanaachwa mayatima wakati Lunga anapofariki. Hali hii inampa kijakazi Sauna upenyu wa kuisambaratisha familia hii kwa kuwatenganisha.
      • Ridhaa anaipoteza aila yake katika kisa cha kuteketezwa isipokuwa Mwangeka aliyenusurika kwa sababu alikuwa nje ya nchi.
      • Mwangeka kumpoteza mkewa na mwanaye katika shambulizi lililowateketeza.
      • Zohali kutungwa mimba katika umri mdogo na kusababisha kukatizwa kwa masomo yake kwa muda na kisha kuteswa na wazazi wake.
      • Waafrika kukatazwa na wakoloni kulima mazao yaletayo fedha huku wakilazimika kufanya vibarua. Baadhi ya vijana wa rika la Tauma wanaaga dunia baada ya kupashwa tohara.
      • Wagonjwa kwenye hospitali za umma kukosa huduma za dawa, ukosefu wa vifaa na mwangaza kutokana na usimamizi mbaya wa hospitali. Wakazi wa Msitu wa Mamba wanaharibikiwa pale wanapofurushwa huku mazao waliyolima yakiibiwa na viongozi.
      • Vijana barobaro wanaotumiwa na wanasiasa kuandamana, wanamiminiwa risasi vifuani na kuuawa na walinzi.
      • Kitoto kilichookotwa na Neema kilimwagikiwa na maji pale kilipotupwa na mamake mzazi badala ya kukilea.
      • Ridhaa kubomolewa nyumba zake kwenye mtaa wa Zari- hakupewa fidia. Wale waliowauzia ardhi hiyo haramu waliingia mitini.
      • Lunga kufutwa kazi na mkurugenzi kwa kupinga mradi wa ununuzi wa mahindi.
      • Lime na Mwanaheri kubakwa na genge la majabazi kadamnasi ya baba yao.
      • Lemi kudhulumiwa na umati wa watu kwa kuchomwa moto baada ya kusingiziwa wizi wa rununu ya mwanamke mmoja.
      • Rehema kudhulumiwa kimapenzi na mwalimu wake Fumba akiwa kidato cha tatu na kutwikwa mimba katika umri mdogo.
      • Selume kutengwa na mumewe kwa misingi ya kikabila - mumewe anaoa mke wa kikwao.
      • Tauma anapashwa tohara hali iliyosababisha yeye kuugua na kulazwa hospitalini.
      • Pete anahatarisha maisha yake anapomeza vidonge vya kukiangamiza kitoto chake kilichokuwa tumboni.
      • Mambo yanawaendea vibaya walevi wakati ambapo watu sabini wanakufa na wengine kunusurika kifo kama vile Kipanga kutokana na unywaji wa pombe haramu.
        (Hoja zozote 12x1=12) Tathmini majibu mengine ya watahiniwa
  3. “Haidhuru kuwa huenda wimbo huu unawaghasi waliolala. Atakalo mwimbaji huyu ni kutakasa hisia zake.” Bainisha jinsi mrejelewa alivyotakasa hisia zake kwenye wimbo wake kwa mifano mwafaka. (alama 20)
    • Ulevi kumpa utulivu uliosababishwa na kuwepo kwa shinikizo kutoka kwa wenye uwezo- Majabali (uk. 129) ulevi kwake ni suluhisho la kuyakimbia matatizo.
    • Kubaguliwa na mahasidi wenye uwezo/tabaka la juu kumbagua.
    • Kuchekwa na matajiri wakiwa kwenye roshani za nyumba zao. Walikuwa wamekula na kushiba (uk. 130) Wanamkejeli kwa kumuita Bwana Dengelua.
    • Watu wanamkejeli tu pasi na kutaka kujua ni nini kilichosababisha uraibu wake wa pombe.
    • Kutwaliwa kwa shamba lao la asili na Bwana Mabavu ambaye anahalalisha wizi huo kwa hatimiliki bandia. Wao walishindwa kumpinga (uk. 131)
    • Ananwonea babake huruma kwa kumenyeka kwa kazi za sulubu ili apate riziki na karo.
    • Yeye alifanya bidii chuoni ili kuivua aila yake kutoka kwenye umaskini. Alipohitimu alikosa kazi.
    • Nafasi za kazi zilitolewa kwa mapendeleo ya kinasaba. (uk. 133)
    • Kazi aliyoipata ni duni – ya kufutia mchozi na mshahara wake ulikuwa mdogo. (uk. 133)
    • Wanapodai nyongeza ya mshahara, mwajiri wao anawarejelea kama 'unskilled labourers' hivyo waridhike na mshahara duni waupatao.
    • Walipoandamana kuomba wafikiriwe kama wataalamu wengine kazini na kutaka wapandishwe cheo, walifukuzwa walikokaa mabandani na kufutwa kazi.
    • Babake Shamsi kufanya kazi ya sulubu hata katika umri wake mpevu bila kuonewa imani na mwajiri wake. (uk. 131)
    • Babake 'anaaga dunia kwa njaa - alilazimika kula vijasumu vilivyomuua.
    • Mfumo duni wa afya- hamna hospitali pale kijijini. Babake alikosa matibabu ya dharura hivyo kuaga dunia.
    • Wanaomcheka kutokana na ulemavu wa mali, bila shaka hata nao yatawafika.
    • Chakula kinapatikana kwa taabu. Shamsi ana matumaini kuwa Bi. Halua ameambulia kibaba cha unga kutokana na ujira mdogo.(uk.135)
    • Kuna watu wanaomsifu kwa kuwa wa kwanza kuhitimu masomoni na hivyo kuwa mwanga wa jamii- hilo halikutimia.
    • Ndoto zake za ujana zimezimwa na watu waliomzidishia umaskini. (uk. 137)
    • Anabahatika hakupofuka wala kufa kutokana na unywaji wa pombe haramu kama wenzake.
    • Wagema kuitia pombe haramu vijasumu ili iive haraka- matokeo yake ni upofu na vifo. Shamsi anawalaumu kwa hilo.
      (Hoja 20x1=20) Tathmini majibu mengine ya wathiniwa

      SEHEMU YA C: TAMTHILIA
      P. Kea: Kigogo
      Jibu swali la 4 au la 5 
  4. “Sitaki kazi za uchafu hapa Sagamoyo."
    1. Eleza muktadha wa dondoo hili.  (alama 4)
      • Msemaji ni Majoka .
      • Anamwambia Ashua
      • Walikuwa ofisini mwa Majoka
      • Ashua alikuwa akiomba soko lifunguliwe ili wafanye biashara na wajikimu. Majoka alisema takataka za soko hilo zinaharibu sifa nzuri za jimbo lao.
        (Hoja 4x1=4)
    2. Kwa hoja kumi na sita, onyesha jinsi kazi za uchafu zinavyoendelezwa kwenye jimbo la Sagamoyo."  (alama 16)
      • Kutengeneza sumu ya nyoka
      • Uuzaji wa pombe haramu
      • Kushambuliwa na kujeruhiwa na vikosi vya usalama
      • Kuuwawa kwa wapinzani kwa mfano Jabali
      • Kunyakuliwa kwa ardhi ya soko- Majoka alitaka kujenga hoteli kwenye uwanja wa soko . Ulanguzi wa dawa za kulevya hali inayosababisha wanafunzi kufeli masomoni
      • Kandarasi muhimu kutolewa kwa njia ya mapendeleo- Ngurumo na Asiya kupewa kandarasi ya kuoka keki za kuliwa siku ya sherehe ya uhuru .
      • Ushauri potovu- Kenga kupanga jinsi ya kumwadhibu Sudi kwa kukataa kuchonga kinyago cha Ngao. Aidha alishiriki kupanga mashambulizi ya Tunu.
      • Raia kutishiwa kufurushwa jimboni- Hashima anaeleza kuhusu vijikaratasi vilivyosambazwa vikiwataka wahame Sagamoyo.
      • Bei ya bidhaa kuongezwa maradufu kwenye kioski cha kampuni
      • Kufungwa kwa soko mahali ambapo wachuuzi na wachongaji vinyago hupata riziki
      • Uzinifu- Majoka kumtamani sana Ashua kimapenzi ilhali ana mke. Ngurumo anahusiana kimapenzi na Asiya ambaye ni mkewe Boza.
      • Kudhulumiwa kwa wafanyabiashara- wanasema wanatozwa kodi na kitu juu yake.
      • Matumizi ya hila- Majoka kupanga kuwaongezea walimu na wauguzi pesa huku akipandisha kodi. Kukandamizwa kwa vyombo vya habari, kwa mfano runinga ya Mzalendo kutishiwa kufungwa baada ya kupeperusha taarifa za maandamano.
      • Kumfungia Ashua kizuizini bila hatia.
      • Kutishia kumfuta kazi Kingi bila kujua kazi yake imelindwa kikatiba.
      • Majoka kutoa kibali cha kukatwa kwa miti hali inayosababisha ukame na mazao kupungua.
      • Ubadhirifu wa mali ya umma- Majoka ana magari mengi- mkewe anafika pale kwake ofisini kisha dereva anaagizwa kumpeleka nyumbani kwa gari jingine.
        (Hoja za kwanza 16x1=16) Tathmini majibu mengine ya watahiniwa.
  5. Onyesha uhusiano uliopo baina ya wahusika hawa na maudhui ya hadithi. (alama 20)
    1. Majoka
      • Kielelezo cha viongozi dhalimu- anamuua Jabali, kumjeruhi Tunu, kumfungia Ashua kizuizini, n.k.
      • Ni mfano wa kiongozi mwenye bezo- anamweleza Ashua alikataa uchumba wake sasa amekuwa ombaomba
      • Ni mfano wa kiongozi asiyethamini wanyonge- anawatusi- Alimwita Sudi zebe, Tunu na Sudi makunguru (uk 38) na kuwarejelea wanasagamoyo kama wajinga.
      • Ni kielelezo cha viongozi wanaowatishia raia- anaposikia Tunu anaongoza maandamano, anatoa vitisho kwake kuwa atawafundisha mambo ambayo hakufundishwa nyumbani.
      • Ni kielelezo cha cha kiongozi mnafiki- Husda ni mkewe ila hampendi na anampenda Ashua.
      • Ni mtu asiyewajali wengine- Anaendeleza ubinafsi. Anatumia cheo chake kujinufaisha kwa mfano kwa kunyakua ardhi ya umma.
      • Anaendeleza maudhui ya uzinifu- licha ya kuwa ana mke, anamtongoza Ashua ambaye ni mkewe Sudi.
      • Ni mfano wa kiongozi mjinga ambaye anakubali ushauri potovu kutoka kwa vibaraka wake kama vile Kenga. Hatambui kuwa wanampotosha.
      • Ni mfano wa viongozi ambao hawawathamini wanawake- (uk. 27) anasema wanawake ni wanawake tu. Anamweleza Husda, "Shut up woman!" Anamwita mkewe "woman" kama mtu asiyefahamu jina lake.
      • Anaendeleza usaliti- anamsaliti babake Tunu na kumuua ingawa walikuwa marafiki . Anawasaliti wananchi kwa kulifunga soko.
      • Anawakilisha kundi la viongozi wanaopata madaraka kutokana na uhusiano wa kinasaba na viongozi watangulizi.
      • Ni mfano wa kiongozi jeuri- Kwenye ndoto, babu yake anajaribu kumnasihi kutenda mema lakini anapuuza.
        (Hoja 10x1=10)
    2. Tunu
      • Ni kielelezo cha vijana wazalendo wanaopigania haki za jamii yao. Anashirikiana na Sudi kupigania wanyonge.
      • Ni mfano wa vijana wenye msimamo dhabiti- anakataa kuozwa kwa Ngao kwa vile hautaki uhusiano na ukoo unaowanyanyasa raia.
      • Ni kielelezo cha raia jasiri- Anamkabili Majoka bila woga na hata kumwita muuaji (uk 47) 
      • Anaendeleza maudhui ya utu- anawahurumia wanoa Sudi na Ashua. Anapendekeza wapelekwe kwao ambako mamake angewatunza.
      • Anaendeleza maudhui ya uadilifu- Yeye hapendi ulevi. Hajihusishi kimapenzi na Sudi kinyume na tetesi za watu.
      • Ni mfano wa vijana wanaofanya bidii masomoni na kufaulu. Anasoma na kuhitimu na shahada ya uzamili na kisha uzamifu katika sheria.
      • Ametumiwa na mwandishi kuonyesa umuhimi wa msamaha na maridhiano. Mwishoni mwa mchezo, Mamapima anaomba msamaha na Ashua anamsamehe.
      • Anaonyesha dhima ya ukakamavu pale anapohutubia umma kwenye lango la soko bila kuogopa Majoka na walinzi wake.
      • Ametumiwa kama njia ya kuhamasisha umma dhidi ya kuwachagua viongozi fisadi ambao hawaonei fahari maendeleo ya jamii yao.
      • Ni mfano wa mzalendo kamili katika jamii licha ya kuumizwa na wahuni, aliendelea kupigania haki za wanyonge kwa kutumia kigari cha magurudumu.
      • Ametumiwa na mwandishi kuwahimiza watu kutenda mambo kwa busara - anapinga wazo la Majoka kuwatenganisha na Sudi pale ofisini.
      • Mwandishi amemtumia kusuta uongozi wa jamii yake ambao hauthamini elimu ya kisasa. Majoka na Kenga walikashifu juhudi zake za kupata elimu. Aidha uongozi huu unashindwa kubuni nafasi za kazi kwa vijana waliohitimu.
        (Hoja 10x1=10)

        SEHEMU YA D: Hadithi Fupi
        A. Chokocho na Dumu Kayanda: Tumbo Lisiloshiba na Hadithi Nyingine
        Jibu swali la 6 au la 7
  6. Mame Bakari- (Mohammed Khelef Ghassary)
    “ Haikuwa stahiki yake kubebeshwa mzigo kama ule.“
    1. Fafanua muktadha wa dondoo hili.  (alama 4)
      • Maelezo ya mwandishi/msimulizi
      • Ni kumhusu Sara.
      • Sara alikuwa amebakwa na janadume moja alipokuwa akirejea jioni moja kwa masomo ya ziada.
      • Hali hii ilimsababishia huzuni na kilio cha siku nyingi kwa kuwa jitu lile liliyabadilisha maisha yake milele.
        (Hoja 4x1=4)
    2. Taja na kueleza tamathali iliyotumiwa kwenye dondoo hili. (alama 4)
      • Jazanda (alama 1)
      • Kubebeshwa mzigo (alama 1)
      • Maana- kuathirika kutokana na ujauzito wa mapema/ mateso kutokana na ujauzito. (alama
    3. Onyesha jinsi mrejelewa alivyoathirika kwa kubebeshwa mzigo. (alama 12)
      • Kujeruhiwa- baada ya kubakwa, Sara alijeruhiwa vibaya na damu nyingi kuvuja (uk. 67).
      • Maisha yake kuingiliwa na kuharibiwa kabisa kwa kutiwa mimba
      • Kuvunjiwa ujanajike wake na utu wake.
      • Kunyimwa furaha- maisha yake kutawaliwa na kilio siku zote. Anazongwa na mawazo mengi yanayomliza (uk. 67).
      • Mawazo ya kutengwa, kusutwa, na kukashifiwa na jamii yake yalimsumbua sana.
      • Aliona kuwa angelaaniwa na kila mtu wa karibu na wa kando (uk. 48) (jamaa zake na jamii kwa ujumla)
      • Mawazo ya kupigwa na kufukuzwa nyumbani na babake yalimtia wasiwasi sana.
      • Hali ya kutoaminiwa na wazazi endapo angewaeleza ukweli kuhusu kubakwa kwake. Aliona kuwa wazazi wake hawangemwamini kwa kushtakia unyama aliotendewa njiani. Badala ayake wangemlaumu kwa kushindwa kujitunza (uk 48)
      • Kukatiziwa masomo yake- aliwazia jinsi angefukuzwa skuli (uk. 48)
      • Kejeli- mwalimu mkuu angemkejeli kwa kumweleza kuwa ile ilikuwa ni skuli ya wanafunzi sio ya wazazi na kuwa hawafundishi wanawake pale wanafundisha wasichana.
      • Kutengwa na wanafunzi wenzake ambao anasema wangelimsusuika na kumtenga kama mgonjwa wa ukoma. (uk.49)
      • Kuingiwa na wazo la kujitoa uhai ambalo baadaye alilikataa.
      • Kuingiwa na wazo la kuavya mimba ambalo licha ya kukiangamiza kitoto chake, lingeweza kuyatia maisha yake katika hatari. Aliwazia kukimbia kwao kama njia ya kujisalimisha na dhuluma na shutuma za babake.
        (Hoja 12x1=12) 
  7.  
    1. Mwalimu Mstaafu- (Dumu Kayanda)
      “Hiari na mukhitari ni juu yako. Lakini yeye kafika nyumbani”. Eleza mambo makuu ambayo mwandishi anayaibua kabla na baada ya kutolewa kwa usemi huu.  (alama 10)
      • Utu- Jamii ya Mwalimu Mstaafu kumzawadi Mwalimu Mosi alimiminiwa sifa na waliohutubu kwenye sherehe ya kumuaga.
      • Ubaguzi-Wanyonge hawakupewa nafasi ya kuhutubu kwenye sherehe ya kumuaga Mwalimu Mosi. Aidha hawakutengewa mahali maalum pa kukaa kama wastaarabu walioketi kwenye hema.
      • Utabaka- Kuna watu matajiri katika jamii hii. Kwa mfano, wanafunzi wa zamani wa Mwalimu Mosi wanaendesha magari ya kifahari. Kuna watu maskini walitamauka kama vile Jairo anayeingia jukwaani na mavazi yaliyochanikachanika (uk.121)
      • Unafiki. Kati ya wale waliotoa hotuba kumhusu Mwalimu Mosi, wote walimsifia sana. Walimuona kama mtu kamilifu asiye na taksiri (uk. 126) walimuona kama Mungu.
      • Ufisadi- Rais alipokuja kuchangisha pesa kwenye shule ya upili ya Wangwani, pesa hizo zililiwa na wakora. (uk. 122)
      • Anasa- Jairo hunywa pombe na kulewa sana. Hata anatembea bila viatu kutokana na ulevi wake.
      • Ubabedume/taasubi ya kiume- Mwanamke kufuata amri ya mumewe bila ya kukaidi- mkewe Jairo anakubali kutolewa kwake na kukabidhiwa Mwalimu Mosi kama zawadi pasi na kupinga. Anasema, “Ni amri ya mume. Ndivyo nilivyolelewa na kufundishwa. Sharti nimutii mume wangu.” (uk. 127) Baadaye
      • Ushirikiano - Mkewe Jairo kujumuika pamoja na Bi. Sera katika kazi zote shambani na hata nyumbani. Walikuwa na mlahaka mwema.
      • Utu - Mwalimu Mosi analazimika kuikimu familia ya Jairo. Kwa mfano, kuwaelimisha wanawe. 
      • Umbeya - Watu kumwambia Jairo kuwa Mwalimu mosi alitorokea mjini na bintiye Sabina ili kumfanya mkewe (uk, 128-129). Hizi zilikuwa ni tuhuma tu kwa sababu Mwalimu Mosi alimpeleka kwenye shule ya bweni naye akarejea nyumbani anakoendelea kuuguzwa.
      • Ukatili- Jairo kwenda kwa Mwalimu Mosi akiwa na nia ya kumuua kwa kumtorosha bintiye na kumfanya mkewe. (uk. 129-130)
        (Hoja 5x2=10)
    2. Ndoto ya Mashaka- (Ali Abdulla Ali)
      Anwani "Ndoto ya Mashaka” inaakisi barabara yaliyomo kwenye hadithi. Fafanua. (alama 10)
      • Ukosefu wa lishe- makuzi ya Mashaka yalikuwa ya tikiti maji na tango ya kuponea umande (uk. 70)
      • Mashaka kuachwa yatima baada ya mamake kufa muda mfupi baada ya yeye kuzaliwa. Vilevile, babake aliaga dunia baadaye kidogo. Ililazimu Mashaka kuielewa na Biti Kidege- mwanamke mzee, maskini na tena mgonjwa.
      • Kushiriki katika ajira katika umri mdogo- Mashaka alifanya kazi za kibarua ili kujikimu binafsi pamoja na mlezi wake Biti Kidege.
      • Mashaka kusoma kwa taabu hadi akamaliza chumba cha nane. Punde tu baada ya kukamilisha masoma yake ya msingi, mamake mlezi akaaga dunia.
      • Mashaka kufungishwa ndoa ya lazima na Mzee Rubeya kwa kusubuhiana na bintiye Waridi. (uk. 74) Mzee Rubeya alifanya hivi ili kujiondolea aibu na baada ya hapo akamahia Yemeni. Hii ilikuwa ni ndoa ya kimaskini kwa sababu ilikosa harusi.
      • Kuishi katika makazi duni- baada ya kuoana na Waridi, waliendelea kuishi kwenye chumba kile kile kibovu- paa lilikuwa ni la madebe na lilivuja wakati wa mvua.
      • Kuishi kwenye mazingira ya uchafu- pale kwao hapakuwa na vyoo, mifereji ya maji taka ilitema uchafu wake kwenye mito na uvundo ulikirihi. Mambo yalikuwa mabaya zaidi wakati wa mafuriko. (uk. 75)
      • Kuzaa idadi kubwa ya watoto- (watoto saba)- nafasi ya kuwahifadhi haikutosha. Binti zao walibanana na mama yao kwenye chumba hicho usiku na wavulana walilala jikoni mwa Chakupewa kama nyau.
      • Mashaka kufanya kazi duni – alikuwa mlinzi wa usiku. Aidha hakuwa na nafsi ya kutosha kushiriki kikamilifu malezi ya watoto wao.
      • Mshahara duni- Mashaka anasema mshahara ulikuwa ni mkia wa mbuzi (uk. 76) Haungemwezesha kununua vitu vingi.
      • Waridi kumtoroka Mashaka- Aliondoka pasi na kuaga. Mashaka anaporejea kutoka kazini, anawakosa nyumbani na hata baada ya kuwatafuta anaambulia patupu. (uk 76)
      • Mashaka kutamauka- Hata baada ya kuachwa na mkewe, alikuwa na matumaini kuwa mambo yangekuwa mazuri. Anasubiri hadi anakata tamaa.(uk. 79)
        (Hoja 10x1=10)

        SEHEMU YA E: FASIHI SIMULIZI
  8.  
    1. Kwa kutumia vipengele vitano, onyesha maingiliano yaliyopo baina ya fasihi simulizi na fasihi andishi.(alama 5)
      • Maudhui- fasihi andishi hujenga maudhui yake kutokana na yale ya fasihi simulizi.
      • Utendaji- kazi za fasihi simulizi zina utendaji. Tamthilia kama kazi ya fasihi andishi ina utendaji pia.
      • Lugha- fasihi simulizi na fasihi andishi hutumia lugha kama nyenzo kuu yakupitisha mafunzo yake.
      • Usimulizi- usimulizi hutumiwa katika fasihi simulizi kuelezea na kusimulia visa. Fasihi andishi huwasilisha ujumbe wake kwa njia ya masimulizi.
      • Dhamira- kazi za fasihi simulizi huwa na dhamira mahususi kama vile kuelimisha, kuadilisha, kuendeleza utamaduni n.k. Fasihi andishi kwa upande wake huwa na dhamira zizo hizo.
      • Fani- mbinu kuu za kuwasilisha maudhui (ploti, wahusika, lugha n.k.) huweza kubainika wazi katika fasihi simulizi sawa na ilivyo katika kazi za fasihi andishi.
        (Hoja za kwanza 5x1=5)
    2. Ni mambo gani ambayo huchangia kubadilika kwa kazi za fasihi simulizi? (alama 10)
      • Hadhira- fanani kulazimika kubadilisha mtindo wa uwasilishaji ili kukidhi mahitaji ya hadhira yake.
      • Fanani- kila fanani ana mtindo wake tofauti wa uwasilishaji. Kwa mfano matumizi ya mbinu ya ufaraguzi miongoni mwa fanani mbalimbali.
      • Teknolojia- mambo ya zamani kubadilika kutokana na athari za teknolojia ya kisasa hasa taknohama.
      • Wakati- kadri wakati unavyoendelea kupita, ndivyo mambo mengi katika maisha ya jamii huweza kubadilika. Mambo hayo huweza kuleta athari ya mabadiliko katika sanaa ya jamii.
      • Mazingira- kuhama kwa watu katika eneo fulani kunaweza kuwanyima mahali mahususi pa kuwasilishia kazi fulani. Kwa mfano miviga.
      • Video- kazi za kisanaa zilizorekodiwa hutofautiana na zile za kuwasilishwa moja kwa moja kutokana na kuathiriwa kwa sauti na picha wakati wa kurekodi.
      • Uhamaji na uhamiaji- kuingiliana kwa tamaduni mbalimbali kunaweza kuathiri jinsi kazi fulani ilivyokuwa tangu mwanzo iwapo kutakuwa na kukopa baadhi ya vipengele vya sanaa ya jamii moja na kuvijumuisha na vya jamii nyingine.
      • Maandalizi- fasihi simulizi inapohifadhiwa kwa maandishi huwa si ya mdomo tena bali ni ya kusomwa.
      • Ukengeushi wa jamii- watu wanaacha utamaduni wao na hivyo baadi ya vipera vya fasihi simulizi huweza kutoweka au vikawa vinajitokeza kwa nadra sana, Kwa ujumla sanaa husika huathirika kutoka na hili. Utafiti- watu kujijazia kile wasichokijua bila ya kwenda nyanjani ilipo jamii husika ili kupata taarifa kamili.
        (Hoja zozote 10x1=10)
    3. Zitaje changamoto zozote tano za miviga katika jamii yoyote ile.  (alama 5)
      • Vifo- upashaji tohara kwa vijana unaweza kusababisha uvujaji wa damu nyingi na mwishowe vifo.
      • Kusababisha magonjwa hatari ya kuambukiza mfano kupitia tohara
      • Husababisha hofu miongoni mwa sehemu ya jamii kwa mfano katika sherehe za kufukuza mapepo.
      • Baadhi huweza kukiuka haki za binadamu mfano tohara kwa wasichana.
      • Baadhi huharibu mazingira- sherehe zinazohusu utoaji wa kelele mfano nyimbo mbalimbali zikiimbiwa mahali pasipofaa, zinaweza kusababisha kelele ambayo itachafua mazingira hayo.
      • Kukinzana na malengo ya kitaifa na kidini mfano tohara kwa wasichana ni marufuku nchini. Shughuli ya maapizo huenda kinyume na mafundisho ya kidini. nk.
      • Hugharimu pesa na raslimali nyingi mfano harusi
      • Baadhi huhusisha imani za kishirikina ambazo zinaweza kuleta uhasama katika jamii. Mfano maapizo.
        (Hoja za kwanza 5x1=5)
Join our whatsapp group for latest updates

Download Kiswahili Paper 3 Questions and Answers - Moi Kabarak High School Mock 2020/2021.


Tap Here to Download for 50/-




Why download?

  • ✔ To read offline at any time.
  • ✔ To Print at your convenience
  • ✔ Share Easily with Friends / Students


Get on WhatsApp Download as PDF
.
Subscribe now

access all the content at an affordable rate
or
Buy any individual paper or notes as a pdf via MPESA
and get it sent to you via WhatsApp

 

What does our community say about us?

Join our community on:

  • easyelimu app
  • Telegram
  • facebook page
  • twitter page
  • Pinterest