Tuesday, 11 July 2023 07:23

Kiswahili Questions and Answers - Class 8 Mid Term 2 Exams 2023 Set 4

Share via Whatsapp

Soma vifungu vifuatavyo. Vina nafasi 1 mpaka 15. Kwa kila pengo umepewa majibu manne, Chagua jibu lifaalo zaidi.

__1__ wa mali haujawahi kuwa katika kiwango __2__ hapa nchini Kenya. __3__ mitatu hivi iliyopita, yaani takriban miaka thelathini hivi iliyopita wezi walikuwa wakivunja mabenki na kwa wakati __4__, __5__ ambao ulikuwa ni kuwaibia watu kwa lazima na kuwaumiza kwa silaha. Wazembe hawa __6__ viongozi wa dini ndio waliochukua nafasi za majambazi hawa sugu.
"Viongozi hawa wanaowaghilibu __7__ wauze mali yao na kuwapelekea hela zote kwa kuwa dunia imefika ukingoni ndio wanaopigiwa mfano wa methali, __8__ kwa kuwa hawana stadi inayohitajika.

   A   B   C   D 
1.   Uchoyo   Uchu   Tamaa   Shauku 
2.  kilichofika   uliofikia   kitakachotimia   kisichotimia 
3.  Misimu  Miaka   Miongo   Darzeni 
4.  ingine  wengine   kwengine   mwingine 
5.  wezi wa mabavu   wizi wa kimabavu   ulaghai wa hiari   uchopozi wa siri  
6.  wanaojiita  waliohitimu kuwa   kusomea   kufanywa kama 
7.  waamini  wafugaji   waumini   wanachama 
8.  ndugu ni kufaana si kufanana   akufaaye kwa dhiki ndiye rafiki  mwana wa ndugu kirugu, mjukuu mtu wa mbali kichwa cha kuku hakistahili kilemba

 

Mwalimu Kijuba __9__mwalimu wangu wa kwanza wa lugha ya Kiswahili.Alinitoa matongo machoni na __10__ masikioni kuhusu lugha hii akhiyari. Mwanzo alinifahamisha kuwa ina sauti 11___. Aidha, alinifunza kuwa sauti hizi zimegawanywa katika sehemu mbili; yaani __12__ na sighuna. __13__ ,nilijuzwa kuwa kuna __14__ kadhaa za lugha kama vile __15__ methali, istiara, tashbihi, misemo, tanakali za sauti na nyingine nyingi.

   A   B   C   D 
 9.   ndiye aliyekuwa   ndio aliyekuwa   ndiye ambao alikuwa   siye aliyekuwa 
 10.   masuo  ukongo   uchafu   nta 
 11.  salasini  thalathini  thelathini   ishirini na tano 
 12.  ghuna  alfabeti  vokali   konsonati 
 13.  Mintarafu  Isitoshe   Maadamu   Seuze 
 14.   tamadhali  mapambo   maneno   tamthali 
 15.  ;  :   ,   . 

 

Kutoka swali la 16 mpaka 30, chagua jibu sahihi

  1. Andika wingi wa sentensi ifuatayo
    Uta ule aliokujengea umekatika
    1. Ukuta ile alizokujengea imekatika
    2. Nyuta zile mlizowajengea zimekatika
    3. Kuta zile mlizowajengea zimekatika
    4. Nyuta zile waliowajengea zimekatika
  2. Neno 'mhadhara' lina silabi ngapi?
    1. Nne
    2. Sita
    3. Nane
    4. Tatu
  3. Ni sentensi gani iliyotumia kwa' kuonyesha sababu?
    1. Wafanyakazi walinufaika kwa bidii zao
    2. Kutafuta kwa mapana na marefu kutakupeleka mbali
    3. Kuimba kwa furaha kulituchangamsha
    4. Wageni walikula wali kwa mchuzi wa kuku
  4. Bainisha aina za maneno yaliyopigiwa mstari katika sentensi ifuatayo.
    Wanafunzi wako ni bora kuliko wetu,
    1. Kivumishi, kitenzi, kiwakilishi
    2. Kiwakilishi, kivumishi, kielezi
    3. Kivumishi, kiunganishi, kiwakilishi
    4. Kiwakilishi, kitenzi, kivumishi
  5. Akisami 4/7 kwa maneno ni
    1. tusui nne
    2. tusui saba
    3. thuluthi saba
    4. subui nne
  6. Maneno yafuatayo yanafuatana vipi katika kamusi?
    1. nungu
    2. nungunungu
    3. nung'unika
    4. nung'uniko
      1. (ii), (iii), (iv), (i)
      2. (iii), (ii), (i), (iv)
      3. (i), (ii), (iii), (iv)
      4. (iv), (iii), (ii), (i)
  7. Tambua sentensi iliyoakifishwa ipasavyo
    1. Wanafunzi wote- wale waliohusika - walitumwa nyumbani.
    2. Kanisa hilo lilifungwa! tutajiunga na jingine.
    3. Mtoto (aliyeugua) alipelekwa (hospitalini).
    4. Ewaa! ameumwa na joka kubwa.
  8. Chagua sentensi ambayo haikuendelezwa sahihi kimantiki
    1. Amejipaka mafuta usoni mwake
    2. Wanafunzi wengi waliwahi shambani
    3. Mabata wanapenda kuchezea vidimbwini
    4. Ajali nyingi zinaweza kukingika
  9. Kamilisha methali ifuatayo
    Mla nawe hafi nawe _________________________
    1. usizaliwa naye
    2. ila mzaliwa nawe
    3. kuliko mzaliwa nawe
    4. kama mzaliwa naye
  10. Ndege ni kwa kiota kama vile konokono ni kwa
    1. kizimba
    2. zizi
    3. shimo
    4. kombe
  11. Ni nini maana ya 'kula njama'?
    1. Kufanya mkutano wa siri wenye nia mbaya
    2. Kula nyama nyingi na kushiba sana
    3. Kushiriki katika mkutano wa hadhara
    4. Kuzeeka au kuishi miaka mingi
  12. Tunapata jina gani kutokana na kitenzi 'andika'?
    1. Andikwa
    2. Andikisha
    3. Mwandishi
    4. Andikiana
  13. Tambua mchezo ufuatao
    'Wachezaji huruhusiwa kuukamata mpira kwa mikono na kukimbia nao, na mpira wenyewe ni wa umbo la duaradufu'
    1. Raga
    2. Gozi
    3. Soka
    4. Gori
  14. Ni sentensi ipi inayoonyesha matumizi sahihi ya kiambishi -po- cha wakati?
    1. Alipotoka sipajui
    2. Tunapoishi ni pema
    3. Nilipomwona nilifurahi
    4. Wapo wanaosoma vizuri
  15. Chagua maelezo sahihi
    1. Kishaufu huvaliwa shingoni
    2. Hazama huvaliwa puani
    3. Kikero huvaliwa sikioni
    4. Shemere huvaliwa mguuni

Soma kifungu kifuatacho kisha ujibu maswali 31-40

Ujio wa teknolojia umeiwezesha dunia kufanya mambo kwa haraka na wepesi mno. Dunia imedogoshwa na kuwa kama kijiji kidogo kwa kuwa; mazungumzo, midahalo, mawasiliano, sayansi na teknolojia, mikutano na mihadhara vinaweza kufanywa bila kuzingatia kitalifa chochote. Hata hivyo, uvumbuzi huu wa kisayansi unaonekana kuwapunja watoto na vijana wadogo ambao hawaelewi mitambo ya teknolojia ililetwa kwa mintarafu gani. Utawaona watoto wadogo hawana muda wa kucheza ila utawapata wamegandana na rununu au tarakilishi wakicheza michezo ya wazungu isiyoisaidia miili yao katika ukuaji.

Ukuaji wa mwili hususan wa mtoto anayekua unahitaji michezo ya aina ainati. Kwa ukweli, michezo ina faida anuwai. Hii ndiyo sababu watoto wengi huhimizwa washiriki katika michezo . Hali ya wanafunzi kujikalia ubwana madarasani huwa na athari zisizokadirika. Usisahau athari zinaweza kuwa hasi au chanya iwapo ni hasi gharama ya kuzidhibiti huwa ya juu sana ukizingatia ukweli kuwa, tuko na mfumko mkubwa wa bei. Shida nyingi ambazo zinamkumba mtu uzeeni husababishwa na kutozingatia hali ya afya njema mtu anapokua. Hii ndiyo maana utawaona watu wakizeeka na kufa mapema kuliko inavyotarajiwa. Watu wa zamani waliishi miaka mingi kwelikweli.

Vijana wa zamani walienzi na kuithamini michezo kama johari. Wavyele wengi walikuwa na kibarua kigumu kuwarudisha wanao nyumbani. Vijana wa zamani walicheza michezo mingi kama vile gungwi, kibe kibatufe, njugwe, kuzungusha tairi kwenye kiuno na hata kuruka kwa kamba. Enzi hizo hungewapata vijana wengi wamejinenepea kama nguruwe.

Ningetaka uwatazame vijana wa kisasa. Utaona idadi kubwa haiendi uwanjani kucheza ila kustarehe tu na kuzizungumzia timu za Uingereza. Utawaona wakijiita wanaManchester, wanaAsenali, wanaChelsie ilhali hawanufaiki na chochote kutokana na timu hizo. Kwao hawatambui kuwa michezo ina manufaa ya kuhusudiwa. Kwanza inajenga misuli na kuimarisha viungo vya mwili. Ni wazi kuwa unaposhiriki michezo unajihisi mwepesi zaidi na unaweza kutekeleza mengi bila kuhisi kuchoka haraka. Pia kwa wale wanaoshiriki michezo katika ngazi za kimataifa hunufaika na mengi. Wao huambulia fedha nyingi zinazowatajirisha haraka. Wengine huajiriwa kama makocha na marefa wa timu za kimaeneo, kitaifa au kimataifa.

Kulaza damu ni wazo la hasara isiyomithilika. Ni dhahiri shahiri kuwa, akili vivu ni karakana ya maovu. Wale wanaojikalia bure bila kufanya kazi yoyote hujipata wakiwazia mabaya. Usisahau, baadhi yao watazama katika matumizi ya dawa za kulevya au wanaswe na mtego wa kimapenzi kabla ya ndoa. Hata hivyo, yule anayeshiriki katika michezo huwa hana nafasi ya kuyawazia mawi. Kila anapotoka uwanjani huwa amechoka tiki na kukosa zihi za kufanya mawi.

Watoto wanaoshiriki michezo mara nyingi huwa na wepesi wa kushika hata wayasomayo. Hii ni kulingana na utafiti wa kisayansi uliofanywa nchini Marekani. Michezo hukuza kumbukumbu za aliyosoma darasani. Usisahau kuwa uwanjani lazima mchezaji awe mmakinifu na anayechemsha bongo na kukuza ubunifu. Mwanafunzi kama huyo huelewa mambo haraka na kwa wepesi. Isitoshe, michezo huchangia kukuza kumbukumbu za aliyesoma darasani. Usisahau kuwa uwanjani lazima mchezaji awe mmakinifu na anayechemsha bongo na kukuza ubunifu. Mwanafunzi kama huyo huelewa mambo haraka na kwa wepesi. Isitoshe, michezo huchangia kukuza nidhamu na umoja. Michezoni pia kuna sheria kali ambazo zinamsaidia mchezaji kujiheshimu na kuwaheshimu wenzake.

  1. Aya ya kwanza haijaeleza kuwa
    1. teknolojia imekuza michezo chanya ya watoto
    2. teknolojia inawezesha watu kuwasiliana vyema hata wakiwa mbali
    3. wanafunzi wanaweza kupokea mafunzo hata wakiwa mbali
    4. teknolojia imeifanya ulimwengu kuwa kama kata ndogo tu
  2. Ni nani aliyepata hasara kubwa kutokana na teknolojia mpya?
    1. Wanasayansi na wavumbuzi wenyewe
    2. Watu wote wanaotumia vyombo vya teknolojia
    3. Watu wa umri mdogo wasiojua matumizi kamili ya teknolojia
    4. Watu wote wanaohusika na michezo mbalimbali
  3. Michezo aina ainati yaani
    1. michezo inayokuza miili 
    2. michezo ambayo hainufaishi
    3. michezo ambayo haipatikani
    4. michezo ya aina nyingi
  4. Wazee wa kale
    1. hawakuishi miaka mingi ikilinganishwa na sasa
    2. waliishi miaka mingi wakilinganishwa na wale wa kisasa
    3. walitumia mitambo ya teknolojia vyema kuliko wa kisasa
    4. hawakucheza michezo mingi kama ile inayochezwa na vijana wa kisasa
  5. Mtu anaweza kupata athari gani akikaa tu bila kufanya kitu kulingana na aya ya pili?
    1. Kuathiri hali ya kiuchumi ya mtu binafsi
    2. Kuathiri hali ya mapato ya mtu binafsi
    3. Kuhatarisha maisha ya wahasiriwa wote
    4. Kunaathiri hali ya ukuaji wa mwili wake.
  6. Kulingana na kifungu, tunaweza kusema kuwa vijana wa kisasa na wale wa kale ni kama usiku na mchana kwani
    1. vijana wa leo hawathamini michezo
    2. vijana wa leo wanathamini michezo sana
    3. hakuna tofauti hata kidogo kwa kuwa mitazamo yao ni sawa
    4. vijana wa zamani hawakuthamini michezo hata kidogo
  7. Vijana wanaostarehe tu na kushabikia timu za kizungu wanakosa manufaa yafuatayo isipokuwa
    1. kusaidia timu anayeisifia kushinda 
    2. kujenga misuli na kuimarisha viungo vya mwili
    3. kuhisi mwepesi zaidi na bila kuchoka kwa haraka
    4. kupata hela haraka na kutajirika kwa haraka
  8. Michezo katika vijana inafanya nini kulingana na aya ya tano?
    1. Inawafanya kutelekeza afya za miili yao 
    2. Huwasaidia kushabikia timu kubwa za kizungu
    3. Huwasaidia kuepukana na mawi yatakayowahatarisha
    4. Huwafanya kuingilia mihadarati na mapenzi ya haramu
  9. Kulingana na utafiti wa kisayansi uliofanywa Marekani
    1. wachezaji wote huwa werevu
    2. michezo huchangia katika kunoa akili
    3. bora kijana ashiriki michezo atakuwa mwerevu
    4. michezo ndiyo njia ya pekee ya uerevu darasani
  10. Anwani mwafaka katika kifungu hiki inaweza kuwa
    1. Faida za teknolojia ya kisasa 
    2. Madhara ya teknolojia ya kisasa 
    3. Madhara ya michezo mingi
    4. Faida za michezo kwenye afya

Soma kifungu kifuatacho kisha ujibu maswali 41- 50

Katika msitu mkuu ulio upande wa mashariki mwa Afrika palikuwa na wanyama ambao waliongozwa naye bwana Kifaru. Mfalme huyu aliongoza msitu huo kwa kipindi cha miongo isiyopungua miwili. Kifaru alipounyakuwa uongozi huu kutoka kwa utawala wa Simba I, wanyama wote walishangilia kwa hoihoi, vigelegele na nderemo. Hii ni kwa sababu cheo hicho daima kilikuwa cha familia ya simba. Hata hivyo, muda wa mfalme Kifaru ulikuwa umekamilika. Wanyama walikuwa wananoa makali yao ili kwenda debeni tena.

Kabla ya uchaguzi ambao ulipania kufanywa mwakani, wanyama wazalendo walianza kutathmini kazi ya kiongozi Kifaru. Baada ya mijadala kwenye vyombo vya habari, ilibainika wazi kuwa kiongozi huyo anayeng'atuka alikuwa ameleta maendeleo si haba. Mwanzo, barabara zilikuwa zimenyoka twa! Pili, alikuwa amefungua vyuo vikuu na vyuo anuwai ambavyo vilifadhiliwa kwa asilimia sabini na tano. Waliojiunga na vyuo hivyo walipata ufadhili vile vile wa karo. Wanyama wengi walikuwa wameelimika kuliko misitu mingine majirani. Wengi walisikika wakisema kuwa pasingekuwa na kifungu kwenye katiba kumzuia, wangemruhusu Kifaru kutawala milele. Hata hivyo, uchumi wao ulikuwa umezorota kwa kuwa alikuwa na madeni mengi yaliyozichukua pesa nyingi za walipa ushuru.

Siku ya uchaguzi ilipowadia, wanyama walimchagua mwana wa simba I ambaye alikuwa ameongoza hapo awali. Wengi walimchagua kwa kusingizia kuwa alikuwa na damu ya uongozi kutoka kwa baba yake. Wengine walimpendelea kwa kuwa alikuwa amesoma hadi kiwango cha uzamifu pale katika chuo kikuu cha Uingereza. "Simba II atatuletea maendeleo ya Uingereza," Nyani walisikika wakimmiminia sifa sufufu. Isitoshe, Simba II alikuwa mkakamavu ajabu. Hata hivyo kuna wale waliopinga wakisema kuwa si vyema wanyama kutoka jamii moja kuongoza milele kwa kuwa wengi wapo, Simba II alitawazwa kuwa mfalme wa tatu wa msitu wa Rosana.

Simba II alishika hatamu za uongozi. Alilitawala pori hilo hivi kwamba wanyama wote walimpenda na kumtii. Hata hivyo, kwa kutamani maendeleo ya pupa, aliwatoza wanyama ushuru mkubwa ajabu. Kila mwanzo wa mwezi, wanyama wote walijumuika kwake ili kulipa ushuru. Wengine walitoka mapangoni, chini ya mawe, miti, viota na kwenye milima na mabonde. Walisimama gwarideni na mfalme angeamua kodi ambayo kila mmoja angelipa. Mfalme huyu aliapa na kutangaza kuwa hakuna hata mmoja ambaye angejaribu kukwepa kulipa ushuru.

Wanyama wengi walilalamikia ushuru wa juu lakini wakalipa ila Mamba. Mwezi ulipokamilika, wanyama wote waliwasili nyumbani kwa simba kulipa ushuru. Kama ilivyokuwa kawaida, Mamba hakuwa miongoni mwao. Wakati huu tabia ya Mamba ilikuwa imemfika mfalme kooni. Hakuwa tayari kupokea vijisababu vyake na alisisitiza kuwa lazima Mamba alipe shilingi milioni kumi kwa kuishi majini. Mfalme Simba II aliamua kumtuma Kiboko akamwite Mamba kwenye kasri. Alilalamika kuwa tabia hiyo ya Mamba ilikuwa sasa kia cha mwili.

Mamba alipofikishiwa ujumbe alisema kuwa alikuwa na mfalme wake majini aliyemlipa ushuru. Mfalme aliposikia hayo, alichemka nyongo. Aliondoka shoti hadi majini. Wakati huo, maji yalikuwa safi na yametulia tuli. Simba alinguruma na kutazama ndani. Mle ndani, alimwona Simba mwingine. Papo hapo, aliruka na kutumbukia majini chupwi! Akazama zi! na kutokomea kabisa.

  1. Kulingana na aya ya kwanza;
    1. wanyama walikuwa hawaamini mwanzoni iwapo kuna mnyama mwingine atakayeongoza isipokuwa Simba
    2. aliyeongoza zaidi ya miongo miwili alikuwa ni mfalme Simba
    3. baada ya uongozi wa Kifaru, Simba II alichukua ushukani
    4. kipindi cha mfalme Kifaru hakikuwa kimekamilika
  2. ...wananoa makali ili kwenda debeni..." Kwenda debeni ni nini kulingana na kifungu?
    1. Kuingia kwenye debe
    2. Kumpokea kiongozi mpya
    3. Kwenda kupiga kura
    4. Kuagana na kiongozi wao
  3. Kura zilitarajiwa kupigwa;
    1. mwaka huo
    2. baada ya mwongo mmoja
    3. mwaka uliotangulia
    4. mwaka ambao ungefuata
  4. Kifaru alikuwa amefanya mema yafuatayo ila:
    1. kutengeneza miundombinu kama vile baraste nzuri
    2. kujenga vyuo vikuu na vyuo anuwai ili wanyama wasome
    3. kufadhili ujenzi wa vyuo kwa asilimia mia moja
    4. aliwatawala wanyama vyema hadi wakatamani aendelee
  5. Ni kwa nini haingewezekana Kifaru kuendelea kutawala kwa mintarafu ya wanyama?
    1. Katiba yao haikuruhusu viongozi kutawala milele
    2. Kifaru alitoka familia ambayo haikutarajiwa kuongoza
    3. Uchumi ulikuwa umedorora katika uongozi wa Kifaru
    4. Uongozi wa Kifaru ulikuwa umekopa madeni kupita kiasi
  6. Simba II alikuwa na kiwango gani cha elimu?
    1. Shahada iliyo chini ya shahada ya uzamili
    2. Shahada aipatayo mtu baada ya shahada ya uzamili
    3. Ni shahada mtu apatayo baada ya ile ya astashahada
    4. Ni cheti cha juu zaidi katika kisomo cha duniani
  7. Unafikiri ni kwa nini Simba II alitawazwa kuwa mfalme ilhali wengine walimpinga?
    1. Kiongozi aliyetangulia alikuwa amedororesha uchumi
    2. Kuna wachache walioupenda ukakamavu wake
    3. Simba II alikuwa na kiwango cha juu cha elimu
    4. Simba II alipata ushindi kwa wingi wa kura
  8. "...tabia hiyo ya Mamba ilikuwa sasa kia cha mwili" ina maana kuwa;
    1. yalikuwa mazoea ya Mamba kutolipa ushuru
    2. Mamba alimdharau mfalme
    3. ilikuwa tabia ya Mamba kulalamika
    4. Mamba alikuwa na hasira
  9. Si kweli kusema kuwa
    1. Mamba alilipa ushuru tu baada ya mwaka mmoja
    2. wanyama wote hawakufurahia ushuru waliotozwa
    3. wanyama wote ila Mamba walilipa ushuru
    4. Mamba alitozwa faini ya kutolipa ushuru
  10. Unafikiri alichokiona mfalme majini ni nini?
    1. Mamba aliyedinda kulipa ushuru
    2. Mfalme mgeni wa majini
    3. Mnyama wa majini aliyefanana na Simba
    4. Kivuli cha mfalme Simba II

INSHA

Umepewa dakika 40 kuandika insha yako.

Andika insha isiyopungua ukurasa mmoja na nusu ukianza kwa kifungu ulichopewa.

Tulianza safari yetu alfajiri na mapema. kwa kuwa siku njema huonekana asubuhi, safari hiyo ilitarajiwa kuwa .....................................

MARKING SCHEME

  1. B
  2. A
  3. C
  4. D
  5. B
  6. A
  7. C
  8. D
  9. A
  10. D
  11. C
  12. A
  13. B
  14. D
  15. B
  16. D
  17. A
  18. A
  19. B
  20. D
  21. C
  22. A
  23. A
  24. B
  25. D
  26. A
  27. C
  28. A
  29. C
  30. B
  31. A
  32. C
  33. D
  34. B
  35. D
  36. A
  37. A
  38. C
  39. B
  40. D
  41. A
  42. C
  43. D
  44. C
  45. A
  46. B
  47. D
  48. A
  49. B
  50. D

 

 

Join our whatsapp group for latest updates

Download Kiswahili Questions and Answers - Class 8 Mid Term 2 Exams 2023 Set 4.


Tap Here to Download for 30/-




Why download?

  • ✔ To read offline at any time.
  • ✔ To Print at your convenience
  • ✔ Share Easily with Friends / Students