Soma vifungu vifuatavyo. Vina nafasi 1 mpaka 15. Kwa kila nafasi umepewa majibu manne. Chagua jibu lifaalo zaidi kati ya yale uliyopewa.
Dereva mwangalifu ___1___ kuwa amezingatia sheria za barabarani. ___2___ magari ___3___ yanatakiwa kutimiza kanuni mbalimbali ili yakubaliwe kutoa huduma___4___ usafiri. Madereva wanapaswa___5___ ___6___ magari hayo. Abiria nao wasinyamaze katu madereva___7___ utaratibu ufaao. Ili kuepuka maafa ___8___kila mmoja atahadhari kwani ___9___.
A | B | C | D | |
1. | huhakikishia | huhakikisha | huhakishiwa | huhakikishiana |
2. | Maadamu | Lau | Mathalani | Japo |
3. | sote | zote | mote | yote |
4. | za | kwa | mwa | wa |
5. | kukaa tutwe | kukaaa doria | kukaa ange | kukaa tayari |
6. | wanavyoyaendesha | wanapoyaendesha | wanakoyaendesha | wanazoyaendesha |
7. | wakikiuka | wangekiuka | wamekiuka | wakakiuka |
8. | inatubidi | inakubidi | inawabidi | inambidi |
9. | mwenye macho haambiwi tazama. | kinga ni bora kuliko tiba. | hakuna marefu yasiyo na ncha. | usilolijua ni usuku wa kiza. |
Mchezo ___10___ wa kabumbu yaani wa ___11___ huchezwa kote ulimwenguni. Ni mchezo ___12___ tija kwa ___13___ taifa lake. Huchukua dakika tisini.___14___ timu zinazocheza hazijafungana bao, huongezewa muda wa___15___ kupata mshindi.
A | B | C | D | |
10. | maarufu | stadi | hodari | bingwa |
11. | soka | voliboli | vikapu | raga |
12. | kwenye | wenye | penye | mwenye |
13. | analochezea | anayochezea | anayechezea | anakochezea |
14. | Hadi | Ingawa | Hata | Iwapo |
15. | kiasi | halafu | ziada | awali |
Kutoka swali la 16 mpaka 30, chagua jibu sahihi.
- Nomino zilizopigiwa mstari katika sentensi ifuatayo ni za aina gani?
Rembo alinunuliwa manukato katokana na usafi wake.- wingi, dhahania
- kawaida, pekee
- dhahania, kawaida
- pekee, wingi.
- Chagua wingi wa sentensi ifuatayo.
Daktari aliyemtibu ametuzwa na shirika hilo.- Madaktari waliomtibu wametuzwa na mashirika hayo.
- Madaktari waliowatibu wametuzwa na mashirika hayo.
- Madaktari waliowatibu wametuzwa na shirika hilo.
- Madaktari waliomtibu ametuzwa na shirika hilo.
- Matumizi ya -po- katika sentensi ifuatayo ni:
Mwema alipofika tuchezeapo, alimpata katibu wa chama chetu.- mahali, wakati
- wakati, mahali
- mazoea, masharti
- masharti, mazoea.
- Chagua sentensi yenye kivumishi cha pekee.
- Mkulima atawafuga ng'ombe wale shambani mwake.
- Mwanafunzi amenunua vitabu vinne vya Kiswahili.
- Hatibu mwenyewe aliwashauri vijana kuhusu masomo.
- Mvuvi ambaye anasifika sana anaitwa Pato.
- Sarafu huanguka sakafuni tang! ilhali moto huzimika:
- pu!
- ndi!
- fyu!
- zii!
- Ni sentensi ipi inayoonyesha kuwa tukio moja linategemea lingine?
- Tina alimpikia chakula kitamu akafurahi.
- Balo angali analima tangu asubuhi.
- Tesi na bintiye wameamua kwenda sokoni.
- Mose alikuwa ameibuka mshindi katika uogeleaji.
- Matumizi ya kwa katika sentensi ifuatayo.
'Kanusu alisoma kwa bidii akapata themanini kwa mia,' ni:- jinsi, sehemu ya kitu kizima.
- sababu, sehemu ya kitu kizima.
- umilikaji, sehemu ya kitu kizima.
- kulinganisha, sehemu ya kitu kizima.
- Chagua jibu lisilo sahihi.
- chura kiluwiluwi
- njiwa-kipura
- kipepeo - kisuse
- papa - kinengwe.
- Chagua jibu lifaalo kujaza pengo katika sentensi ifuatayo.
_____________ nitamwona, nitampasha habari hizo.- Bali
- Ikiwa
- Angaa
- Halafu
- Safari yangu itaanza siku ya tatu baada ya jana. Je, itaanza lini?
- Mtondo.
- Mtondogoo.
- Kesho.
- Kijoto.
- Chagua usemi wa taarifa wa:
"Mkifika mapema mtauwahi mkutano." Karani alisema.- Karani alisema kuwa wangefika mapema watauwahi mkutano.
- Karani alisema kuwa wakifika mapema, watauwahi mkutano.
- Karani alisema kuwa wangefika mapema wangewahi mkutano.
- Karani alisema kuwa wakifika mapema wangewahi mkutano.
- Ni sentensi ipi iliyoakifishwa ifaavyo?
- Fisi na Sungura ni maadui Sana.
- Fatuma amepika; Chapati, Biriani na kaukau.
- "Karibuni nyumbani wanangu," mama aliwaomba.
- ng'ombe, mbuzi na kondoo watachinjwa leo.
- Sentensi, "Asingalichora vyema, asingalituzwa," ina maana:
- Hakuchora vyema, akatuzwa.
- Alichora vyema, akatuzwa
- Hakuchora vyema, hakutuzwa.
- Alichora vyema, hakutuzwa.
- Chagua jibu lenye nomino za ngeli ya U-U
- uyoga, wema, wizi
- waya, wali, uzi
- uso, ukuta, ugali
- werevu, uji, wino.
- Akisami, 7/9 kwa maneno ni:
- tusui saba
- tusui tisa
- subui tisa
- subui saba.
Soma kifungu kifuatacho kisha ujibu maswali 31 mpaka 40.
Je umewahi kutafakari kuhusu neno mazingira? Ni neno ambalo daima limekuwa vinywani mwa waja. Mazingira ni ile hali au mambo yanayozunguka mtu mahali anapoishi; nchi kavu, angani na hata majini. Manufaa atakayopata binadamu yanategemea namna anavyoyatunza mazingira yake.
Fikiria vile hali ingekuwa bila mito, miti, maziwa, milima, mabonde na hewa safi! Yakini, hali ingekuwa si hali. Tuchukue kwa mfano mito na maziwa, faida zake ni chungu nzima. Maji tunayoyatumia nyumbani, kupikia, kufulia na kunyweshea mifugo na kwa unadhifu wa binadamu hutoka pale. Aidha, shughuli nyingi za viwandani huhitaji maji kwa wingi. Wakulima nao wanafaidika kwa kuwa wanayatumia maji kunyunyizia mimea yao.
Isitoshe, miti ina tija kubwa kwa jamii. Hutumiwa katika ujenzi, kutengeneza dawa, kutupatia chakula na kama hifadhi ya wanyama na ndege. Vilevile, miti huvuta mvua, husafisha hewa na kuzuia mmomonyoko wa udongo na kurembesha mazingira. Ukataji miti kiholela hum- nyima binadamu faida hizi.
Ni dhahiri kwamba mazingira ni uhai na hatuna budi kuyatunza. Mathalan tuyaondoe maji yaliyotuama kwenye vidimbwi kisha tuvizibe. Vyombo vingine kama vile mikebe na vigae ambavyo vimetapakaa nje huweza kuhifadhi maji kunyeshapo na kutuama hivyo kuwa mahali pa mbu kuzalia. Endapo hatutachukua hatua hii, mbu wanaweza kuzaliana humo na kusababisha malaria. Hali kadhalika watu wanaweza kuyanywa na kuambukizwa uwele wa waba. Hatari hizi zinaweza kuzuiwa kwa kutia kemikali kwenye maji hayo ili kuwaangamiza viluwiluwi waliomo. Vyombo ambavyo vinaweza kuweka maji yasiyohitajika visitupwe ovyoovyo.
Hewa safi ni muhimu kwa maisha ya binadamu. Hewa hii inaweza kuharibiwa na moshi utokao kwenye magari mabovu na pia viwandani. Kutokana na uchafuzi wa hewa, uhai wa bi- nadamu huhatarishwa kwani huenda akapatwa na magonjwa anuwai yakiwemo pumu, saratani kifua kikuu na hata yale ya ngozi. Aidha, uchafuzi wa hewa huwa na athari kwa hali ya anga. Kwa mfano safu ya ozoni ikiharibiwa, joto jingi hutokea na huweza kuathiri afya ya binadamu na wanyama. Misimu na majira pia hubadilika jambo ambalo huweza kuathiri kilimo na miundo misingi. Ili kukabiliana na janga hili, magari mabovu yanayotoa moshi mwingi yakarabatiwe au kuondolewa barabarani. Wenye viwanda wanastahili kubuni mikakati kabambe ili kudhibiti gesi na majitaka yatokanayo na shughuli za kuzalisha bidhaa.
Mazingira ya nyumbani nayo ni muhimu. Tunafaa kuyatunza kulihali kwani tusipotahadhari tutajilaumu wenyewe. Mabaki ya chakula husababisha uvundo katika nyumba zetu yasipohifad- hiwa vizuri. Zaidi ya hayo, picha tuipatayo katika baadhi ya nyumba inachukiza. Utapata taka zimeenea kote; si maji machafu, si maganda ya ndizi na parachichi, si kaka za mayai, si karatasi na matunda yaliyooza na kuozeana. Ni nani mwingine atakuja kudumisha usafi wa nyumba zetu ila sisi wenyewe? Hatari inayotukodolea macho ni kubwa. Kuna uwezekano kuwa umewahi kuteleza na kuanguka kutokana na kukanyaga ganda la ndizi lililotupwa shelabela. Wa kulaumiwa ni nani? Wahenga walig'onga ndipo waliposema mwiba wa kujichoma hauambiwi pole. Kila mmoja katika familia ana jukumu la kuhakikisha kwamba taka zote za nyumbani zimetupwa kwenye jalala.
Ni wazi kuwa mazingira ni a hidaya ambayo tunapaswa kuithamini lau sivyo tutakuwa chachandu anayejipalia makaa.
- Kwa mujibu wa aya ya kwanza:
- Watu wengi hupendezwa na mazingira yao.
- Mazingira hutawaliwa na hali kavu.
- Anga inaweza kuyaboresha maisha ya binadamu.
- Binadamu atafaidika akiyazingatia yaliyomo katika maeneo anamoishi.
- Aya ya pili imedhihirisha kuwa:
- Maji yana faida zaidi nyumbani kuliko mahali pengine.
- Maisha ya binadamu yatakuwa magumu bila mazingira.
- Kilimo hakihitaji maji mengi kama uzalishaji bidhaa.
- Maziwa yana manufaa mengi zaidi yakilinganishwa na milima.
- Jibu lisilo sahihi kuhusu miti kwa mujibu wa aya ya tatu ni:
- Chombo cha kusafisha hewa na kuchangamsha viumbe.
- Kiungo cha tiba na huwalisha binadamu.
- Pambo la mazingira na hukinga udongo usisombwe.
- Chanzo cha mvua na ni makazi ya viumbe.
- Aya ya nne imebainisha kuwa lazima tuyatunze mazingira ili
- tuepuke kunywa maji machafu.
- tukwepe kutupa toka ovyo.
- tuzuie mbu kuongezeka.
- tuwe na siha njema.
- Kwa mujibu wa kifungu:
- Mbu hupendezwa na maeneo yoyote yaliyo na maji.
- Maji yaliyotiwa dawa hutibu magonjwa yaletwayo na mbu.
- Uharibifu wa hali ya anga huweza kuvuruga shughuli za ukulima.
- Mabadiliko ya hali ya anga huchangia kuwepo kwa hewa safi.
- Jukumu la wenye viwanda katika utunzaji mazingira kulingana na aya ya tano ni:
- Kudhibiti mvuke utokanao na mitambo itumikayo viwandani.
- Kuimarisha harakati za kuzalisha bidhaa za viwandani.
- Kuzua njia zifaazo za kukabiliana na vichafuzi votakavyo viwandani.
- Kushirikiana na wenye magari makuu kuu kuzuia moshi kuchafua mazingira.
- Ni jibu lipi ambalo si ushauri kwa mujibu wa aya ya sita.
- Ni wajibu wa kila mja kunadhifisha mahali anakoishi.
- Chakula kilichosalia kinastahili kutunzwa kwa njia ifaayo.
- Uchafu hutapakaa kote katika baadhi ya nyumba.
- Majaala ya kutupia taka yanapaswa kuwekwa kila mahali.
- Maana ya kauli 'miti ina tija kubwa' ni:
Miti ina- gharama kuu.
- mvuto mkubwa.
- tiba nyingi.
- manufaa mengi.
- Chagua maana ya methali, "Mwiba wa kujichoma hauambiwi pole" kwa mujibu wa kifungu.
- Ukiweka maji machafu nyumbani mwako utajisababishia madhara mengi.
- Ukieneza kaka za mayai na karatasi usitarajie kuhurumiwa.
- Ukitupa taka ovyo hufai kusaidiwa upatapo hasara.
- Ukikanyaga maganda ya matunda utajiumiza wewe mwenyewe.
- Kauli "tutakuwa chachandu anayejipalia makaa' imetumia tamathali gani ya usemi?
- sitiari.
- methali.
- nahau.
- tashbihi.
Soma kifungu kifuatacho kisha ujibu maswali 41 mpaka 50.
"Ngomeni washuke! Ngomeni washuke!"Sauti ya utingo ilihanikiza kote kuwahimiza abiria ambao walikuwa wamejaa pomoni kwenye daladala hii kushuka. Sauti hii ndiyo iliyoniamsha kwenye usingizi mzito. Sikujua nilikuwa nimelala kwa muda gani. Nililokumbuka ni kwamba mara tu baada ya kuhakikisha kwamba nimekihifadhi kirununu changu kibindoni, usingizi uliniiba, nikalala bila hata kuwazia kwamba nilikuwa mwana genzi wa safari. Licha ya kwamba hii ndiyo iliyokuwa mara yangu ya kwanza kuondoka nyumbani peke yangu, ilikuwa pia mara yangu ya kwanza kwenda jijini. Hakika jiji la Tugawane nilikuwa nasikia habari kulihusu ama kutoka kwa marafiki wangu wachache waliobahatika kuwa na jamaa huko, au kupitia magazeti ambayo hayakuchelewa kuandika visa vya kuchangamsha, kushangaza na kuhuzunisha kuhusu jiji hili.
"Ndugu, umelala sana," alisema abiria aliyekuwa ameketi karibu nami, akanitazama tena kisha akaendelea, "Unaenda wapi huku Tugawane? Naona tunakaribia kufika kituo cha mwisho. Hawa wakishuka, tunastahili kujitayarisha kwani tukifika kwenye kituo cha mabasi cha Hamaniko sote tutahitajika kushuka".
Maneno ya abiria mwenzangu yalinitanabahisha kwamba kwa kweli sikujua nilikokuwa naelekea. Sikujua kwa sababu baba yangu aliniambia tu kwamba ami yangu angenipokea huko kituoni. Sikuona haja ya kukumbuka jina la mtaa nilikokuwa naenda kwani baba aliniandikia nambari ya ami, nikaihifadhi kwenye kirununu changu, japo kwa kweli alinitajia jina lenyewe. Nilijua kwamba ningempata ami kituoni na kama ningechelewa, ningempigia simu.
"Sijui ninakoenda," nilimwambia abiria mwenzangu; ami yangu atakuja kunipokea kituoni. Kesho atanipeleka chuoni, Mwenge." Abiria mwenzangu aliniangalia akatikisa kichwa kisha akanitazama tena kana kwamba ananiambia, "Utafungaje safari bila kujua uendako kisha unalala? Naona ubwabwa wa shingo haujakutoka. Nakuhurumia kwa yatakayokupata."
Hatimaye gari lilipunguza mwendo na kupinda kuelekea kituo cha Hamaniko. Kibarabara kilichoelekea huko, kilikuwa kimeshiba kikatapika. Si maelfu ya magari, na rukwama zilizosheheni mizigo ya wachuuzi wa vyakula, si matusi ya mahamali waliotaka kupishwa, si wauzaji wa vipande vya matunda vilivyofungwa kwa karatasi za plastiki... Hata sauti nene ya utingo ilipotangaza, "Shukeni haraka! Tulikuwa tumechukua saa mbili ushei kusafiri masafa ya kilomita tano tu. Mara tu utingo alipotoa tangazo abiria mwenzangu alikurupuka na kushuka haraka bila kunipa hata kwaheri. Niliinuka nikaingiza kiganja changu kibindoni ambamo nilikuwa nimekihifadhi kirununu changu. "Mungu wangu!" Nilisema kwa sauti ya jitimai iliyomshtua hata utingo. "Nini kijana?" Aliuliza utingo. "Sioni rununu yangu," nilimwambia huku nikizuia kilio. "Humo ndimo nilimokuwa nimehifadhi nambari ya simu ya ami yangu. Ami anakuja kunipokea kituoni," Nilimweleza utingo zaidi.
"Basi wewe shuka. Utamsubiri ami yako huko kwenye ubao huo," alisema kisha akajiondokea bila hata kuniuliza kama namjua mwingine yeyote katika jiji hili.
"Maskini ami asipokuja sijui nitafanya nini," nilijisemea, "Kumbe, mwenzangu huyu alijua aliyotenda? Kumbe ndiyo maana akaondoka bila kunijulia la heri wala la shari?"
- Kulingana na aya ya kwanza:
- Msimulizi alikumbuka alikuwa na kirununu onda kibindoni aliposikia sauti ya utingo ikitangaza washuke.
- Utingo alizungumza kwa sauti nzito ili msimulizi na abiria wasikie aliyosema.
- Hii ndiyo mara ya kwanza kwa msimulizi kusikia habari za yale yanayoendelea mjini.
- Baadhi ya habari alizo nazo msimulizi kuhusu Tugawane zinatoka kwenye vyombo vya habari.
- Aya ya kwanza imeonyesha kwamba:
- Utingo wa daladala za Tugawane walikuwa na mazoea ya kujaza abiria.
- Abiria alilala kwa sababu mizigo yake ilikuwa salama kwenye gari.
- Awali msimulizi alikuwa akiandamana na jamaa kila mara alipotoka nyumbani.
- Ngomeni kulikuwa na watu waliowahuzunisha na kuwashangaza wengine kwa maneno yao.
- Chagua jibu sahihi kulingana na kifungu.
- Abiria mwenzake msimulizi alimwamsha ili msimulizi ajue anakoenda.
- Kituo cha mabasi cha Hamaniko kilikuwa hatua chache kutoka Ngomeni.
- Baba ya msimulizi alikuwa amemtajia mahali ambapo alikuwa anaenda.
- Rununu ilihifadhiwa kibindoni kwani ilikuwa inahitajika mwishoni mwa safari.
- Msimulizi amekosa uwajibikaji kwani:
- Alimwambia mwenzake anakoishi bila kuwaza kuwa ni mgeni kwake.
- Alipuuza maelekezo aliyopewa na baba yake kwa kutegemea kirununu.
- Alitarajia kufika chuoni Mwenge bila kujua njia ya huko.
- Alisahau kwamba alikuwa ameketi kando ya abiria ambaye alihitaji simu.
- Kauli, 'Utafungaje safari bila kujua uendako kisha unalala?" inaonyesha hasa kwamba abiria
- anamhuzunikia msimulizi kwa kushikwa na usingizi.
- anamlaumu msimulizi kwa kukosa makini.
- anamtahadharisha msimulizi kuhusu hatari ya safari za ugenini.
- anachukizwa na ukosefu wa kumbukumbu ya msimulizi.
- Chagua matatizo yanayoukumba mji wa Tugawane kwa mujibu wa aya ya tano.
- Wachuuzi wengi, ukosefu wa heshima.
- Kelele nyingi, wizi kituoni.
- Uchafuzi wa mazingira, msongamano wa magari.
- Barabara zenye mashimo, ukatili garini.
- Ushirikiano wa kifamilia unahimizwa katika kifungu kwani:
- Baba aliandika nambari ya simu kumtambulisha msimulizi.
- Baba alijua kwamba msimulizi akipoteza simu ami atamngojea Ngomeni amwelekeze.
- Ami alifahamu kwamba msimulizi atampigia simu gari likichelewa ili tampokee.
- Ami alichukua nafasi ya baba ya kumpeleka msimulizi Chuoni.
- Kulingana na kifungu, utingo
- alikosa kutilia maanani hali ambayo ingemkumba msimulizi.
- alijua kwamba abiria alikuwa mwizi.
- alichukizwa na kelele ya msimulizi.
- alifahamu mahali ambapo ami huwangojea wageni wake.
- Kauli, "Maskini, ami asipokuja sijui nitafanya nini; inamaanisha kwamba msimulizi
- anajihurumia kwa yale ambayo yatamfika.
- anashangazwa na kuchelewa kwa ami yake.
- anajilaumu kwa kuzungumza na abiria mwenzake.
- anasikitishwa na mazingira mageni mjini.
- Chagua kisawe cha, 'ilihanikiza' kulingana na kifungu.
- Ilisikilizwa
- Ilitangazwa
- Ilienea
- Ilivutia.
INSHA
Umepewa dakika 40 kuanndika insha yako.
Andika insha itakayomalizika kwa maneno yafuatayo.
Ni wazi kuwa kufanikiwa kwangu maishani kulitokana na ushirikiano huo.
Download Kiswahili Questions - KCPE 2023 Past Papers.
Tap Here to Download for 30/-
Get on WhatsApp for 30/-
Why download?
- ✔ To read offline at any time.
- ✔ To Print at your convenience
- ✔ Share Easily with Friends / Students