Thursday, 14 April 2022 07:46

Kiswahili Questions and Answers - Class 8 End of Term 1 Exams 2022

Share via Whatsapp

MASWALI

Soma vifungu vifuatavyo. Vina nafasi 1 mpaka 15. Kwa kila nafasi umepewa majibu manne hapo. Jaza kila pengo kwa jawabu lifaalo zaidi.

Bahili hakujua__ 1___ ya ukarimu __ 2 _siku _ 3 _ na ya kumfika. Yeye alikuwa_ 4 watu wanaosadiki kuwa kwa lolote ambalo __5 _mtu yeyote, hawana budi 6. malipo. Watu hawa hujitetea kwa methali isemayo, _ 7__'. Siku hiyo alipoteza nauli yake alipokuwa akirejea nyumbani. Juhudi zake za kuomba msaada hazikufua dafu. Basi __ 8hadi chengoni huku amechoka tiki.

  1.      
    1. thamani
    2. dhamani
    3. umuhimu
    4. sababu
  2.      
    1. tangu
    2. hata
    3. wala
    4. hadi
  3.      
    1. aliofikwa
    2. aliyefikwa
    3. alipofikwa
    4. alivyofikwa
  4.      
    1. baadhi ya
    2. mithili ya
    3. kati ya
    4. miongoni ya
  5.      
    1. wanalomtendea
    2. wanamtendea
    3. wamtendealo
    4. wakimtendea
  6.      
    1. kumtoza
    2. kumtolesha
    3. kumtoesha
    4. kutozwa
  7.      
    1. Jaza ya hisani ni hisani
    2. Lisilo budi hubidi
    3. Tenda wema nenda zako
    4. Mkono mtupu haurambwi
  8.      
    1. akaenda joshi
    2. akapiga milundi
    3. akatia mrija
    4. akapiga vijembe

Ni jambo la kusikitisha kuwaona vijana wakiingilia starehe    9     .Jambo hili limechangia _ 10_ kwa maadili katika jamii. __11___vijana hata wanaoingilia uhalifu__12__starehe hizi. Wengine nao huzurura mithili ya    14     wakitafuta wenzao watakaowanunulia vileo.__15___ na hali hii huenda tukakipoteza kizazi cha kesho.

  1.      
    1. wasiozimudu
    2. wasioimudu
    3. wasizozimudu
    4. wasivyozimudu
  2.      
    1. kuzorota
    2. kufilisika
    3. kuimarika
    4. kutekelezwa
  3.      
    1. kuko
    2. iko
    3. раро
    4. wapo
  4.        
    1. japo
    2. ili
    3. bali
    4. ila
  5.      
    1. kugharimia
    2. kugharimu
    3. kugharamia
    4. kugharamisha
  6.      
    1. dira
    2. mwewe
    3. mbwakoko
    4. pakashume
  7.        
    1. Tukienda
    2. Mkiendelea
    3. Wakiendeleza
    4. Tukiendelea

Kuanzia swali la 16 mpaka 30, jibu kila swali kulingana na maagizo uliyopewa.

  1. Chagua sentensi iliyotumia kielezi cha kutilia mkazo kwa usahihi.
    1. Wao ni marafiki wa kufa kupona.
    2. Kamau ni rafiki yangu wa toka nitoke.
    3. Tumeuenzi utamaduni wetu tangu asili na jadi.
    4. Waombolezaji walilia kwa shangwe na hoihoi.
  2. Nyuzi ni wingi wa uzi aidha ni
    1. kasi ya mawimbi baharini.
    2. vipimo vya joto.
    3. viwango vya mvua iliyonyesha.
    4. Makadirio ya masafa ardhini.
  3. Tambua sentensi iliyotumia ji ya hali.
    1. Mtoto alijichafua akicheza.
    2. Mwimbaji yule ni maarufu sana. 
    3. Utunzaji wa mazingira ni wajibu wetu sote.
    4. Jigari hilo ni la mjoba wake.
  4. Ukitaka kupima usawa wa ukuta utatumia kifaa kipi?
    1. Timanzi
    2. Patasi.
    3. Jiriwa.
    4. Pimamaji.
  5. ______ ni zao zima la mmea uzaao ndizi. 
    1. Chane 
    2. Mgomba 
    3. Kipeto
    4. Mkungu
  6. Andika wingi wa sentensi ifuatayo:
    Hukujua kuwa angeniuliza swali kama hilo.
    1. Hawakujua kuwa mngewauliza maswali kama hayo.
    2. Hamkujua kuwa wangeniuliza maswali kama hiyo. 
    3. Hamkujua kuwa wangetuuliza maswali kama hayo. 
    4. Hawakujua kuwa mngetuuliza maswali kama hayo. 
  7. Akifisha sentensi ifuatayo.
    Mwalimu aliwauliza mnafanya nini hapa. 
    1. Mwalimu alitaka kujua walichokuwa wakifanya hapo? 
    2. Mwalimu aliwauliza, "Mnafanya nini hapa?" 
    3. Mwalimu aliwauliza, "mnafanya nini hapa?"
    4. Mwalimu aliwauliza, "Mnafanya nini hapo?
  8. Ainisha maneno yaliyoangaziwa katika sentensi ifuatayo. Timu hii ni hodari kuliko ile. 
    1. Kivumishi, kielezi, kiwakilishi. 
    2. Kivumishi, kihusishi, kivumishi. 
    3. Kivumishi, kiunganishi, kielezi.
    4. Kiwakilishi, kihusishi, kivumishi.
  9. Kinyume cha methali:
    Mtoto akililia wembe mpe ni
    1. Mpanda ngazi hushuka.
    2. Mtoto umleavyo ndivyo akuavyo.
    3. Mchagua jembe si mkulima.
    4. Pilipili usiyoila yakuwashiani?
  10. Kati ya vyombo hivi vya muziki, kipi cha asili?
    1. Gitaa.
    2. Fidla.
    3. Tarumbeta.
    4. Siwa.
  11. Mimi ni mvulana. Jina langu ni Tito. Nina dada mmoja anayeitwa Asha. Kila tunapoonana sisi huitana
    1. kaka.
    2. mpwa.
    3. umbu.
    4. mnuna.
  12. Mzigo huu ni nanga ukiubeba kidogo tu unalowa jasho chapachapa. Sentensi hii imetumia tamathali gani za uscmi?
    1. nahau, tashbihi.
    2. Sitiari, tanakali za sauti.
    3. Chuku, milio.
    4. Sitiari, nahau.
  13. Zawadi anayopewa mtu kwa kupata kitu kilichopotea huitwaje?
    1. Fichuo.
    2. Arbuni.
    3. Koto.
    4. Kiangazamacho.
  14. Mkutano ulimalizika wakati wa jua la utosi.Je huu ni wakati gani?
    1. Adhuhuri.
    2. Macheo.
    3. Machweo.
    4. Asubuhi.
  15. Chagua kikundi cha sifa zisizochukua viambishingeli.
    1. imara, halali, dhaifu, laini.
    2. bora, safi, chafu, gani.
    3. tele, refu, embamba, kali.
    4. tajiri, tano, gumu, kadhaa.

Soma kifungu kifuatacho kisha ujibu maswali 31 – 40
Hivi karibuni, nchi ya Kenya iliingia katika hesabu ya zile nchi ambazo zimewahi kudungwa na mwiba wa vita vya wenyewe kwa wenyewe. Japo vita hivi vilisababishwa na uchaguzi wa mwaka Elfu mbili na saba, vilituonyesha namna tulivyogawanyika katika misingi ya kikabila. Kuna mengi ambayo tunaweza kufanya ili kuuziba ufa huu ambao umetugawanya.
Kwanza tunaweza kuhimiza matumizi ya lugha ya taifa katika nyanja zote za maisha badala ya watu kutumia lugha zao za mama. Vilevile, viongozi waache ukabila na wawe na mtazamo wa kitaifa. Wamechangia sana kuchochea hisia za kikabila badala ya kuwaunganisha Wakenya. Maeneobunge mengine yamegawika katika misingi ya kikabila na hata kupewa majina ya kikabila. Pia inafaa kila Mkenya ahubiri umoja wa kitaifa.
Shule zetu za upili zimekuwa vyungu vya kuchemshia ukabila. Isipokuwa shule za kitaifa ambazo huchukua wanafunzi kutoka maeneo yote nchini, shule za magatuzi almaarufu kaunti na zile za wilaya huchukua asilimia sabini ya wanafunzi kutoka maeneo ya karibu. Hivyo basi utapata mwanafunzi amesomea eneo hilo kutoka shule ya msingi mpaka kidato cha nne. Wanafunzi kama hawa hutumia lugha za mama na kwa hivyo hawachangii katika utaifa. Itafaa vilevile iwapo kutakuwa na ugavi sawa na rasilimali. Ilivyo sasa ni kuwa maeneo mengine yana maendeleo ya hali ya juu na mengine hayana hata chakula. Jambo hili linaleta uhasama wa kimaeneo.
Tunaweza vilevile kuwa na siku ya utamaduni ambapo tuna maonyesho ya kitamaduni. Kwa kuonyesha utamaduni wa kila kabila nchini, tutafurahia tamaduni anuwai tulizo nazo na kuzichukulia kuwa kitegauchumi kuliko kuwa sababu ya vita.
Makundi haramu pia yanaleta ukabila. Wakati wa vita vilivyozuka hapa nchini, kila kabila lilikuwa na kundi lake la kulipigania. Kulikuwa na uhalifu mkubwa uliosababishwa na makundi haya yafaa kupigwa marufuku.
Nafasi za kazi nazo ziwaendee wale waliohitimu na wala si kutolewa kwa misingi ya kikabila. Vilevile, iwapo viongozi watakuwa mifano mizuri watasaidia sana viongozi waache matamshi kama vile, “kabila letu linaonewa," au "Ndugu zangu tunamalizwa.” Iwapo watakuwa na mitazamo ya kitaifa, basi watasaidia sana kuleta mtagusano katika nchi hii.
Wananchi wenyewe waelewe kitu kimoja, kuwa makabila nchini Kenya ni mawili - matajiri na maskini. Kwa mfano, hata baada ya kuwachonganisha Wakenya viongozi wetu huonekana wakila na kucheka pamoja. Sisi wananchi tumebaki na kinyongo lakini wao ni marafiki baada ya kututumia na kupata walichotaka, madaraka.
Vyombo vya habari vinapaswa kuarifa, kuelimisha, kuburudisha na kuyafichua maovu. Hata hivyo, kuzuka kwa idhaa za kikabila kimechangia kuvuruga umoja. Viongozi hutumia vyombo hivi kuhubiri chuki kwa watu wa makabila yao. Mambo ya aina hii hudhoofisha juhudi za kulinganisha taifa.
Hakika, ni vyema tufikirie kuhusu wajibu wetu katika maendeleo yetu binafsi na ya taifa letu. Chombo hakiendi ila kwa kafi. Tukijijenga, taifa zima tutapiga hatua kubwa pia. Badala ya kutumia juhudi zetu kuzozana kwa misingi ya kikabila, ni vyema tushikane mikono ili tusonge mbele pamoja.

  1. Ni sahihi kusema kuwa,
    1. Kenya ilijiunga kupigana na mataifa yenye vurugu.
    2. Kenya imehusika tena katika machafuko ya kisiasa.
    3. Kenya imekuwa mojawapo ya nchi zilizoshuhudia machafuko.
    4. Kenya ilikuwa nchi ya kwanza kushuhudia vita vya kikabila.
  2. Vita hivi vinavyozungumziwa,
    1. vilitokea kabla ya uchaguzi mkuu nchini.
    2. vilitokana na tofauti za kikabila zilizojitokeza kisiasa.
    3. vilisababishwa na viongozi wenye maono ya kitaifa.
    4. vilikuwa baina ya makabila makuu na yale madogo.
  3. Umuhimu wa lugha ya kitaifa kulingana na kifungu hiki ni,
    1. kuyaangamiza makabila.
    2. kutambulisha taifa.
    3. kukuza utamaduni.
    4. kuliunganisha taifa.
  4. Shule za upili nazo zimelaumiwa kwa
    1. kutohimiza utangamano wa jamii mbalimbali.
    2. kutoa mafunzo kwa kutumia lugha ya marna.
    3. kupokea wanafunzi kutoka sehemu mbalimbali.
    4. kuwanyima nafasi wanafunzi wa jamii za karibu.
  5. Kuendelea kwa baadhi ya maeneobunge kuliko mengine ni ishara kuwa,
    1. ubaguzi unajitokeza katika ugavi wa rasilimali.
    2. mipaka ya kimaeneo imewekwa kwa misingi va kikabila.
    3. watu wa maeneo haya wana bidii kuliko wenzao.
    4. serikali inazingatia usawa katika ugavi wa rasilimali
  6. Kulingana na aya ya nne,
    1. kuwepo kwa tamaduni mbalimbali kunahujumu umoja wetu.
    2. Maonyesho ya kitamaduni yamechangia ukabila nchini.
    3. tofauti zetu zinaweza kutufaidi badala ya kutugawanya.
    4. kila kabila lina siku ya utamaduni ya kitaifa.
  7. Makundi haramu nchini,
    1. yanasaidia kutetea makabila yao yasinyanyaswe.
    2. mara nyingi hutetea haki za makabila yote.
    3. hayana uhusiano wowote na makundi ya kikabila.
    4. hutekeleza uhalifu kwa visingizio vya kutetea jamii.
  8. Makala haya yameonyesha wazi kuwa,
    1. Viongozi wa kisiasa ni maadui wakubwa.
    2. Viongozi wa kisiasa huwatumia wanyonge kujifaidi.
    3. Nchi hii haina makabila mengi jinsi tunavyofikiria.
    4. Idhaa za kikabila huanzishwa na Wanasiasa nchini.
  9. Methali 'chombo hakiendi ila kwa kafi' ina maana kuwa,
    1. maendeleo hayatapatikana bila watu kuwa na ubinafsi.
    2. juhudi za kuliunganisha taifa nila serikali na viongozi.
    3. taifa haliwezi kuendelea bila mchango wa wananchi.
    4. wananchi hawawezi kuungana bila viongozi wa kisiasa..
  10. Neno mtagusano jinsi lilivyotumika lina maana sawa na,
    1. utangamano.
    2. utengano.
    3. mvurugano.
    4. utamaduni.

Payuka alikuwa kilimilimi hivi kwamba lolote alilonasa kwa yeyote awaye yule, sharti angeliwasilisha na kumtaarifu mwingine. Hakujali lilisemwa na nani au kwa nini. Hata mambo ya faragha ya baraza la wazee angeingilia tu, sijui akiwa mgeni wa nani, kisha angeyasambaza hata kwa vibaka na vigoti. Udukizi wa namna hii ulimpelekea kuwa na rabsha baina yake na wote waliomzunguka. Kila aliyemwona akikaribia alijaribu kuyafunika maneno yake hadi apite. Msemo, “funika kombe mwanaharamu apite," ukawa wamlenga yeye.
Waaidha, alikuwa na ulimi wa upanga. Kungalikuwa na mashindano ya kukaripiana, neno la kwanza la payuka lingalimpiga dafrao mpinzani wake hata ajiuzulu mara moja. Alifikiri maisha ni jukwaa la mashindano na kwake yeye aliyekuwa na upyaro wa msimu ndiye angeshinda. Maneno yake yote yalikuwa mfano wa sumu ya joka kali. Naye kwake, hili lilikuwa na hasara pia. Aliuvaa uso usiofurahi, kila wakati umekunja mapeto, midomo imekunjana na uso umejaa makanyanza kama mzee mwenye umri wa miaka mia moja. Mgeni yeyote aliyemwona na kusikia kuwa alikuwa mtoto ambaye hata ubwabwa haujamtoka shingoni alimaka.
Payuka pia alikuwa mcheza shere. Ukweli ukawa neno lisilo na maana kwake. Hakuiona ahadi kuwa deni kazini angeahidi jambo fulani wala asingelitimiza asilani. Mkutanapo angekupiga chenga kukudanganya. Angekupaka mafuta kwa mgongo wa chupa na uridhikapo na kuenda, angeahirisha utekelezaji wa ahadi yenu hadi mtakapokutana tena. Kwa mtendwa, hii ilikuwa dhihaka iliyokithiri.
Uchokochoko wake ulimfanya awe ndumakuwili. Akimwona yeyote akinawiri angejitokeza kama anayeteremea mno na mwenye kusherehekea pamoja na apataye. Hili lingefanya anayelengwa kumfunulia moyo wake wote na kuuacha wazi kwake amchunguze atakavyo. Maadui wangevutwa kwa ulimi. Kuna walioibwa kutapeliwa, kuhujumiwa kwa mioto au kwa namna yoyote ile, wengine waliuawa kutokana na hila zake kumbe alitafuta jinsi ya kufaidika yeye!
Naye avumaye baharini papa kumbe wengine wapo? Ukiua kwa upanga, kwa upanga pia utakufa. Chokochoko za payuka zikawabughudhi vijana wengi kwa muda mrefu, nao wakampangia njama. Wakaitumia njia ile ile aliyotumia kulipizia kisasi - ulimi mtamu. Walijua kuwa yeye alipenda kuutumia ulimi wake kupata sifa. Wakati huo makachero walikuwa wakichunguza kwa kina vyanzo vya visa mbalimbali vya uhalifu kitongojini humo. Wakajua kumsifu kwa kiasi kidogo tu kungemfanya kujisahau na kuelezea siri zake zote
Licha ya kuutumia kuropoka, ulimi wa Payuka pia ulitumiwa kuchapa maji. Siku ya mtego, vijana hao walijifanya karimu kwelikweli, wakamnunulia kileo. Alipokwishauchapa ugimbi, vijana wakaanza kumsifu Payuka kwa ujanja huku wakiwakashifu watu mbalimbali waliojua kuwa walikwishahasiriwa na afriti huyu. Kusikia sifa zake zainuka, alianza kutokwa na maneno shelabela. Alieleza alivyowashusha wote hao kwajinzi mbalimbali - kuna aliowapangia kuuawa, kuibiwa, kuchomewa nyumba na kadhalika.
Wakati huu wote, kachero mmoja alikwishakaribia akiwa na kiredio cha kunasia sauti. Akishaboboka bobobo, makachero wawili wakajitokeza, wakajitambulisha na kumfahamisha Payuka shughuli zao pale. Alipojaribu kujitetea kiredio kikafunguliwa, akayasikia yote aliyosimulia. Akalevuka palepale, akawaangalia vijana wale majirani ambao sasa walikuwa wakitabasamu. “Twende kituoni!” Makachero wakamwamuru. Waliokuwepo wakajisemea nyoyoni, “Kweli heri kujikwaa dole kuliko kujikwaa ulimi”.

  1. Chagua jibu lililo sahihi.
    1. Payuka aliyachunguza mambo vizuri kabla ya kuyasambaza.
    2. Wengi walipenda kuzisikiliza chokochoko za Payuka.
    3. Baraza la wazee lilimtumia Payuka kutangaza mambo yake.
    4. Payuka alipenda kuchunguza maneno ili ayasambaze.
  2. Kutokana na hulka ya Payuka,
    1. mara nyingi alivurugana na watu.
    2. alijizolea umaarufu kila mahali.
    3. alipendwa sana na vibaka na vigoli.
    4. alijipata akizungukwa na watu mara nyingi.
  3. 'Neno la kwanza la Payuka lingalimpiga dafrao mpinzani wake hata ajiuzulu mara moja'. Kauli hii imetumia tamathali gani za usemise
    1. sitiari, nahau.
    2. nahau, chuku.
    3. tashihisi, chuku.
    4. tashbihi, kinaya.
  4. Payuka alionekana kuwa mzee kwa sababu ya,
    1. upyoro wake 
    2. kununa mara nyingi. 
    3. kuchukiwa na watu.
    4. maneno mengi aliyojua.
  5. Sifa nyingine ya Payuka iliyojitokeza ni,
    1. kutotimiza ahadi.
    2. kuingiliana na wageni.
    3. kupenda vita.
    4. kuhepa watu wasikutane.
  6. Msemo mwingine wenye maana sawa na, angekupaka mafuta kwa mgongo wa chupa'ni
    1. angekupiga vijembe.
    2. angekuvika kilemba cha ukoka.
    3. angekuonea gere.
    4. angekutia kiwi.
  7. Payuka alijenga uhusiano na wale waliofanikiwa ili,
    1. azijue siri zao na kuwatangazia wengine.
    2. aige nyendo zao na kufanikiwa kama wao.
    3. atangaze siri zao waweze kutiwa mbaroni.
    4. awavute karibu na kupata nafasi ya kuwadhulumu.
  8. Madhara ya ulevi yanayojitokeza katika i kifungu ni,
    1. mtu kushindwa kudhibiti maneno yake.
    2. kunaswa na makachero bila kujitetea ipasavyo.
    3. kutoa siri za wenzetu kwa maadui zao.
    4. kuwafuata hata maadui ili kufaidika.
  9. Payuka hakuweza kujitetea kwa kuwa,
    1. alikuwa mlevi kupindukia.
    2. ushahidi dhidi yake ulikuwa dhahiri.
    3. wenzake walitoa ushahidi dhidi yake.
    4. alishtakiwa kwa mambo ambayo hakuyajua.
  10. Kulingana na kifungu, ni wazo kuwa,
    1. askari walipofika pale walikuja kumchunguza Payuka.
    2. vijana waliomnunulia Payuka pombe walikuwa makachero.
    3. Payuka alikuwa mhusika mkuu kwenye maovu kijijini.
    4. vijana waliomsaliti Payuka walikuwa washirika wake maovuni.


MARKING SCHEME

  1. A
  2. D
  3. C
  4. C
  5. B
  6. A
  7. B
  8. B
  9. C
  10. A
  11. D
  12. B
  13. A
  14. C
  15. D
  16. C
  17. B
  18. C
  19. A
  20. D
  21. C
  22. B
  23. A
  24. B
  25. D
  26. C
  27. B
  28. D
  29. A
  30. A
  31. C
  32. B
  33. D
  34. A
  35. A
  36. C
  37. D
  38. B
  39. C
  40. A
  41. D
  42. A
  43. C
  44. B
  45. A
  46. D
  47. D
  48. A
  49. B
  50. C
Join our whatsapp group for latest updates

Download Kiswahili Questions and Answers - Class 8 End of Term 1 Exams 2022.


Tap Here to Download for 30/-




Why download?

  • ✔ To read offline at any time.
  • ✔ To Print at your convenience
  • ✔ Share Easily with Friends / Students