- Mtiririko
- Ufaafu wa Anwani ‘Toba ya Kalia’.
- Dhamira ya Mwandishi
- Maudhui
- Wahusika: Sifa na Umuhimu.
- Mbinu za Uandishi
Toba ya Kalia- Douglas Ogutu.
Mtiririko
Jack anapokea simu ya Kalia, babake Siri, rafikiye mkubwa tangu utotoni.
Ujumbe ni kuwa Siri atakuwa hewani kwenye runinga ya Kikwetu, na ameagiza Jack na wazazi wake (Siri) wawepo.
Anavaa shati alilolainisha kwa kuweka chini ya godoro na suruali ya khaki.
Hali hii ni kwa kuwa anawekeza kujiendeleza kimasomo.
Safarini, Jack anakumbuka baruapepe ya Siri akimweleza angetumia fursa hiyo kupitisha ujumbe aliotaka ulimwengu usikie.
Siri huwasiliana na wazazi wake kupitia skype, na Jack ndiye huwasaidia kuunganisha mitambo, licha ya kuwa amekomea shule ya upili kimasomo.
Wanaketi ukumbini wa mahojiano na kukaribishwa kwa sharubati.
Kiswahili cha binti mtangazaji kinamfurahisha Bi. Mshewa, mkewe Kalia kwani ni mwalimu wa Kiswahili.
Jane Gatoni, mtangazaji, anawakaribisha watazamaji katika kipindi chao, Nyumbani ni Nyumbani na kuwatambulisha wageni, kisha kuwapa fursa kuwasabahi watazamaji.
Picha ya Siri inatokea kwenye kiwambo.
Gatoni anamshukuru kwa kuitikia wito baada ya mchango wake mwingi kupitia facebook na twitter.
Anamwuliza sababu ya ufanisi wake katika Kiswahili akiishi Uchina, na hata kukifundisha huko.
Siri anaeleza kuwa hali hiyo ilichangiwa na tabia za Monika katika riwaya ya Z. burhani ‘Mwisho wa Kosa’, aliyeenda ughaibuni na kuiga kila kitu huko.
Akaahidi moyo wake kuwa mzalendo.
Hata Uchina, kuna waliojifunza lugha hiyo na huizungumza vyema kuliko watu wa nyumbani.
Wanaenda mapumzikoni kwa furaha huku Bi. Mshewa akimwahidi Jack siku yake itafika, kwani shindano la awali wakiwa kidato cha nne lilitoa nafasi kwa mtu mmoja.
Jack anaungulika kwa kupokwa nafasi yake.
Gatoni anamwuliza Siri historia ya ufanisi wake.
Kalia anapatwa na wasiwasi, kwani kuna sehemu isiyofaa kujulikana.
Anaenda msalani kumpigia Siri simu lakini hampati.
Anarejea kupata Siri akiendelea.
Anaeleza mashindano yaliyofadhiliwa na wahandisi wa Uchina, mshindi akiahidiwa ufadhili kufikia uzamifu katika Chuo Kikuu cha Uhandisi.
Shule yao ilitoa miradi bora, Jack akiwa wa kwanza naye wa tatu. Anajuta kumhini Jack bahati yake.
Katika sherehe za kutambua mshindi, Kalia anabadilisha orodha, Siri anapewa ushindi na Jack kupewa nafasi ya tatu.
Wanashiriki chamcha na mawaziri na wazazi wao pamoja na walimu wa shule.
Jack na Kembo, anayechukua nafasi ya pili, wanakabidhiwa hundi za shilingi elfu kumi.
Kembo anawapa wazazi wake, naye Jack anampa Bi. Mshewa amhifadhie.
Urafiki wao ukaendelea na kumaliza kidato cha nne, Jack bado akamshinda Siri kwa pointi tano.
Kwa kukosa wazazi, akaanzisha biashara kwa zile elfu kumi, akilipa nusu ya faida kwa wazaziwe Siri, eti ni shukrani ya malezi.
Siri anakiri wazaziwe wangempeleka shule bila ufadhili.
Waliahidi kumtunza Jack hadi kilele cha masomo yake, lakini alibakia kuuza viatu.
Hakulalama, japo Siri anaumika.
Anamwomba msamaha Jack na pia kwa ajili ya wazazi wake.
Amepata kazi, na anatoa mshahara wa mwaka wa kwanza kufadhili elimu ya chuo kikuu ya Jack.
Anawataka watatazamaji wasidhulumu mayatima na maskini.
Bi. Mshewa anamwomba msamaha Jack kwa yote waliyomtendea.
Kalia anamsifia Siri kwa ujasiri na kumwomba Jack msamaha, akiahidi kushughulikia masomo yake.
Jack anafurahi kuwa atarudi masomoni.
Anamshukuru Siri na kuwasamehe wazazi wake.
Anawashukuru kwa kumwezesha kuanzisha biashara, iliyomfunza mengi.
Bi. Gatoni anatamatisha kipindi na kuwaaga.
Njiani, kila mmoja yuko huru, huku wakichagua vyuo Jack angeweza kusomea.
Ufaafu wa Anwani ‘Toba ya Kalia’.
Toba’ ni majuto yanayotokana na kutenda maovu.
Hivyo basi, mada hii inarejelea majuto ya Kalia kutokana na maovu aliyotenda.
Ndilo tukio kuu katika hadithi hii.
Siri anampa Jack ujumbe kuwa amewaalika pamoja na wazazi wake katika kipindi cha Nyumbani ni Nyumbani kwenye runinga ya Kikwetu.
Anamwambia kwamba ana ujumbe muhimu ambao angependa ulimwengu ujue, lakini asimwambie babake.
Sababu ni kuwa unahusu uovu wa Kalia.
Siri anapoulizwa kuhusu safari ya mafanikio yake, Kalia anaenda msalani kumjulisha kuwa kuna sehemu ya historia hiyo isiyofaa kusikika na yeyote.
Hii ni sehemu aliyompoka Jack haki.
Hataki kukiri makosa yake na kuomba toba, hadi muda unapofika.
Siri anasimulia Jack alivyoshinda katika mashindano na kutwaa fursa ya kusomea Uchina, lakini Kalia akampoka nafasi hiyo na kumwekea mwanawe, Siri, aliye huko wakati huu.
Anajuta sana kwa hilo, na anamwomba Jack msamaha, na pia kwa ajili ya wazazi wake.
Jack anawasamehe.
Kalia anaomba msamaha pia kutokana na kitendo chake.
Kuonyesha toba yake ni ya dhati, anaahidi kuyashughulikia masomo ya Jack hadi atakapo.
Kando na hayo, matendo ya Kalia yanastahili toba, kwani anamchukulia Jack nafasi hiyo, licha ya kuwa na uwezo wa kumsomesha Siri bila msaada. Anayepokwa nafasi hiyo ni yatima!
Si hayo tu, Kalia aliahidi kumsomesha hadi atakapo baada ya wazazi wake kuaga.
Jack anapoanzisha biashara ya viatu, anaanza kuimarika na hapo wazazi wa Siri wanaanza kudai nusu ya faida yake, eti ni zawadi ya malezi.
Hata hivyo, Jack anawasamehe wala hana kinyongo.
Anaikubali toba ya Kalia.
Kitendo cha Siri kwa Kalia ni toba.
Anamwanika kwenye runinga ya Kikwetu kutokana na matendo yake ya awali.
Kisa cha Jack kinamwuma kiasi cha kutovumilia na kuamua kuuambia ulimwengu.
Hawezi kuvumilia zaidi.
Dhamira ya Mwandishi
Anadhihirisha umuhimu wa mahusiano ya kimataifa katika kuendeleza nchi za Kiafrika.
Anawasilisha teknolojia na umuhimu wake, hasa katika mawasiliano.
Anadhihirisha nafasi na umuhimu wa urafiki katika maisha.
Kutoa ushauri kwa wale wanaowatesa mayatima na maskini kukomesha tabia hiyo.
Anawasilisha viongozi wanaotumia nyadhifa zao kujinufaisha kwa jasho la wengine.
Anawasilisha umuhimu wa kukiri makosa na kuomba msamaha.
Maudhui
Elimu.
Jack na Siri wanasoma katika shule moja ya upili ambayo ni maarufu nchini.
Wanatamatisha elimu ya kidato cha nne pamoja, na Jack anampiku Siri kwa pointi tano.
Inawawezesha kushiriki katika shindano linaloandaliwa na wahandisi kutoka Uchina na kuibuka katika nafasi tatu za kwanza.
Mashindano hayo yanamwezesha Siri kupata fursa ya kuendeleza elimu yake Uchina, japo ni Jack anayestahili nafasi hiyo.
Jack anaandaa kazi ya kupigiwa mfano na hata fomyula zake zinaingizwa kwenye vitabu, japo kwa jina la Siri.
Jack pia akiwa Uchina anaendeleza elimu ya lugha ya Kiswahili kwa wakazi wa huko, na anasema kwamba baadhi yao wanapata umilisi hata kuliko wazungumzaji wa nchi yake ya nyumbani.
Anaimarisha ujuzi wake wa lugha kwa kusoma riwaya mbili, tamthilia mbili na diwani ya amashairi kila mwezi.
Jack anapokamilisha masomo yake ya shule ya upili, anakosa namna ya kuendelea kwa kuwa wazazi wake waliaga.
Anaanza biashara ya kuuza nguo lakini baada ya Siri kuanika matendo ya Kalia hewani, hali inabadilika.
Anapata nafasi ya kujiunga na chuo kikuu kwa ufadhili wa Kalia.
Kando na hayo, Bi. Mshewa pia ameelika hadi kuwa mwalimu wa Kiswahili, sawa na Bi. Gatoni, mtangazaji na mwendeshaji wa kipindi cha Nyumbani ni Nyumbani katika runinga ya Kikwetu.
Teknolojia na Mawasiliano.
Hadithi inadhihirisha maendeleo ya teknohama katika jamii.
Jack anapokea simu kutoka kwa Kalia, kumweleza kuhusu mwaliko wa Siri katika mahojiano kwenye runinga ya Kikwetu.
Wakiwa njiani, Jack anakumbuka baruapepe aliyotumiwa na Siri kumfahamisha kuwa kuna siri alitaka kusema.
Tunaambiwa kwamba Siri huwasiliana na wzazi wake kupitia skype, na Jack ndiye huwaunganishia mitambo kuhakikisha mawasiliano yanafaulu vizuri.
Wanapatana naye vyema akiwa Uchina.
Ukumbi wa mahojiano unadhihirisha hali ya teknolojia na mawasiliano kwa uwazi.
Jack anaketi karibu na mtangazaji, huku mkabala mwa mtangazaji mna kiwambo kikubwa kama ukuta.
Hapa ndipo picha ya Siri inatokea wakati wa mahojiano na wanaendesha shughuli nzima bila matatizo.
Kalia anapohisi hatari ya Siri kutaja yasiyofaa, anaelekea msalani kumkumbusha kuhusu hayo.
Hata hivyo, mawasiliano hayakamiliki kwani simu ya Siri haipatikani kwa wakati huo.
Ndoa
Ndoa katika hadithi hii ni kati ya Kalia na Bi. Mshewa, wazazi wake Siri.
Yaelekea kwamba ndoa yao ina fanaka, kwani wanaonekana kupatana na kuelewana katika masuala mengi.
Wanakubaliana katika tendo la kumpoka Jack nafasi yake na pia kukubaliana wakati wa kuomba msamaha kwa hayo.
Wamejaliwa mwana ambaye ni Siri, na ambaye wanashirikiana ipasavyo katika malezi yake.
Ulaghai
Kalia anatumia ulaghai kumtwalia mwanawe nafasi ya kusomea Uchina.
Jack anatokea kuwa na kazi bora na kuchukua nafasi ya kwanza katika mashindano.
Ndiye ana haki ya kwenda Uchina kwa ajili ya masomo ya juu.
Hata hivyo, Kalia anabadilisha matokeo kumweka Siri nafasi ya Jack.
Bi. Mshewa anapoona biashara ya Jack imeimarika, anamwamrisha kutoa nusu ya faida yake kwao, eti ni shukrani ya malezi, hali hawajamsaidia kwa lolote.
Hili linamfanya kukosa uwezo wa kujiunga na chuo.
Urafiki
Unadhihirika kupitia kwa Jack na Siri, ambao ni marafiki tangu utotoni.
Wanaanza urafiki huo na unakua hadi kiasi cha watu kuwafikiri kuwa ndugu.
Wanadhihirisha ukweli wa udugu kuwa kufaana sio kufanana, kwani wanafaana katika kila jambo.
Kuna uaminifu kati yao.
Siri anamdokezea Jack kuwa kuna suala kubwa ambalo anatumai kuwasilisha katika mahojiano wanayoenda Jack na wazazi wake.
Anamwambia asidokeze lolote kwa babake, kwani yanafaa kuwa siri.
Ana imani naye kama rafiki kuwa atatunza siri yao, jambo ambalo Jack anatekeleza.
Hata baada ya babake Siri kumlaghai Jack nafasi yake, bado urafiki wao unabakia.
Jack halalamiki na kimya chake kinamwuma Siri hadi kuamua kutoboa ukweli.
Anaposema, hata machozi yanamlengalenga kutokana na uchungu.
Anajitolea kufadhili masomo ya Jack yote kwa mshahara wa mwaka wake wa kwanza kazini.
Kazi
Siri anawaeleza wazazi wake na rafiki yake Jack kuwa amepata kazi.
Amefanikiwa baada ya masomo ya uhandisi nchini Uchina kupitia nafasi aliyotwaliwa na Kalia kwa ulaghai.
Ananuia kutumia kazi hiyo kumfidia Jack kwa kumfadhilia masomo.
Babake Jack pia anafanya kazi kama mmoja wa wanakamati wa Wizara ya Sayansi na Teknolojia nchini.
Yuko katika sherehe za kuwatuza wanafunzi waliofaulu katika shindano. Anatumia nafasi yake hiyo kumfaa mwanawe.
Bi. Mshewa naye anafanya kazi kama mwalimu wa Kiswahili.
Bi. Gatoni naye anatekeleza wajibu wake katika studio, akifanya kazi ya utangazaji.
Ndiye anaendesha kipindi cha Nyumbani ni Nyumbani katika runinga ya Kikwetu.
Jack anapokosa namna ya kuendelea na masomo baada ya wazazi wake kuaga, anatumia elfu kumi alizopatiwa kama tuzo kuanzisha biashara ya kuuza viatu.
Biashara hiyo inamwezesha kukimu mahitaji yake, na pia kuwekeza kwa ajili ya kuendeleza masomo yake.
Maudhui mengine ni pamoja na Dini, Ukatili, Tamaa na Ubinafsi, Udhalimu na Migogoro.
Wahusika: Sifa na Umuhimu.
Jack
Ni msomi.
Anasoma na kuhitimu katika masomo ya shule ya upili.
Anakosa nafasi ya kujiunga na chuo kikuu kwa kukosa hela.
Hata hivyo, anajiandaa kwa kuwekeza, na fursa inapojitokeza, yuko tayari kuendelea.
Ni mwerevu.
Anawasilisha mradi bora zaidi katika mashindano.
Anapata alama tisini na nane.
Siri anaungama kazi ya Jack ilikuwa ya kipekee na hata ilizua fomyula zilizowekwa kwenye vitabu.
Ni rafiki wa dhati.
Urafiki wake na Siri ni wa kipekee.
Wanasaidiana katika kila jambo, hata baadhi wanawafikiri kuwa ndugu.
Hata kuhiniwa fursa yake na kupewa Siri hakuwatenganishi.
Ni msiri.
Anapata baruapepe kutoka kwa siri kumweleza kuwa ananuia kufichua jambo la siri.
Jack hamwambii yeyote.
Anatunza siri hiyo.
Ni mwenye bidii.
Anapoanza biashara ya kuuza viatu, anaimarika mara moja, hadi kumtia tamaa Bi. Mshewa.
Licha ya kutakiwa kulipa nusu ya faida yake, bado anashikilia kazi hiyo vizuri.
Ni mvumilivu.
Anapitia mengi katika maisha yake lakini hakati tamaa. Anafiwa na wazazi wake.
Wazazi wa Kalia wanamdhulumu lakini bado anawaheshimu na kuwapa nusu ya faida yake.
Ni msamehevu.
Anawasamehe wote waliomkosea mwishoni.
Anawaeleza wazazi wa Siri kuwa hana kinyongo nao kabisa.
Umuhimu wa Jack
Ni kiwakilishi cha vijana shupavu walio na akili pevu ya kupambanua mambo.
Anawakilisha madhila yanayowapata yatima katika jamii mikononi mwa wasiowajali.
Kupitia kwake, umuhimu wa urafiki unabainika.
Ni kielezo cha msamaha na upendo kwa waliotukosea.
Ni kielelezo cha bidii na umakinifu katika kutekeleza mambo.
Kupitia kwake, nafasi ya teknolojia na mawasiliano inabainika.
Siri
Ni msiri.
Anamweleza Jack kwa siri kupitia baruapepe kuwa ananuia kutoa ujumbe fiche kwa ulimwengu kwenye mahojiano wanayoenda na wazazi.
Anamwagiza kutunza siri ile, na wazazi wake wanafahamu wakiwa hewani.
Ni msomi.
Anasoma hadi chuo kikuu, ambapo amepata ufadhili wa kusoma hadi shahada ya uzamifu katika Chuo Kikuu cha Uhandisi.
Ni jasiri.
Anatoboa siri kubwa kuhusu ufanisi wake uliopokwa Jack kwenye mahojiano ya runinga bila kitete hata kidogo.
Hata babake anamhongera kwa ujasiri huo.
Ni mzito wa hisia.
Kimya cha Jack kinamchoma moyoni, hadi anapoamua kutoboa ukweli.
Katika masimulizi yake, analengwalengwa na machozi.
Ni mzalendo.
Anaeeza kuwa alichukia tabia za Monica, mhusika wa riwaya ya Z. burhani, ‘Mwisho wa Kosa’, kutokana na kukengeuka kwake.
Anakipigania Kiswahili na kukifunza Uchina.
Ni rafiki wa dhati.
Urafiki wake na Jack ni wa kumpigiwa mfano tangu utotoni. Hata yuko tayari kutoa mshahara wake wa mwaka kumlipia karo ya chuo.
Ni mshauri.
Mwishoni mwa kipindi, anawapa watazamaji wosia kuwa wasiwadhulumu mayatima na maskini.
Umuhimu wa Siri.
Kupitia kwake, nafasi na umuhimu wa urafiki unadhihirika.
Anawakilisha teknolojia na mawasiliano na umuhimu wake katika kuunganisha jamii.
Kupitia kwake, umuhimu na nafasi ya elimu katika kujenga jamii inadhihirika.
Ni kielelezo cha watetezi imara wa haki na ukweli.
Ni kielelezo cha ujasiri katika kutekeleza mambo.
Ni kielelezo cha uzalendo na umuhimu wake katika jamii.
Kupitia kwake, mahusiano ya kimataifa na umuhimu wake katika jamii unadhihirika.
Kalia
Ni laghai.
Anamhini Jack nafasi yake ya kusomea uhandisi Uchina na kumkabidhi mwanawe, Siri.
Anabadilisha orodha na kumweka mwanawe wa kwanza licha ya kuwa alikuwa wa tatu.
Ni mnafiki.
Anatoa ahadi ya kumtunza Jack baada ya wazazi wake kuaga, lakini hatimizi bali anatumia wadhifa wake kumdhulumu.
Ni mwenye tamaa.
Anapoka nafasi ya Jack na kumpa Siri, licha ya kuwa ana uwezo wa kumsomesha bila msaada wowote.
Ni mfadhili.
Anaahidi kusimamia elimu ya Jack hadi atakapo badala ya Siri.
Umuhimu wa Kalia
Ni kiwakilishi cha wanajamii wanaotumia nyadhifa zao kujinufaisha na familia zao.
Anawakilisha nafasi ya mzazi katika malezi ya mwanawe.
Kupitia kwake, madhara ya ulaghai yanadhihirika.
Ni kiwakilishi cha wanajamii wanaowadhulumu mayatima kutokana na hali yao.
Bi. Mshewa.
Ni msomi.
Amesoma hadi kiwango cha juu na kuwa mwalimu wa Kiswahili.
Ni mwenye tamaa.
Anakiri kuwa anapoona biashara ya Jack imeanza kuimarika, anapandwa na tamaa na kumtaka kuwa anawapa nusu ya faida yake.
Ni mwenye majivuno.
Anafurahishwa sana na umilisi wa mwanawe katika Kiswahili, na kudai kwamba ni urithi aliomwachia, kwani yeye ni mwalimu wa Kiswahili.
Umuhimu wake
Kupitia kwake, madhara ya tamaa yanadhihirika.Ni kiwakilishi cha ndoa na nafasi yake katika kujenga jamii.
Anawakilisha nafasi ya mzazi katika malezi na makuzi ya mwanawe.
Bi. Gatoni
Ni mwajibikaji.
Anatekeleza wajibu wake kwa umma kama mtangazaji.
Anawakaribisha studioni wageni waalikwa na kuwapa sharubati kisha kuendeleza kipindi.
Ni mwenye umilisi.
Anazungumza kwa ufasaha mkubwa katika kuendesha kipindi kile.
Ni jasiri.
Anasikiliza maneno ya Siri yanayotoa ujumbe mzito.
Anawauliza Kalia na Bi. Mshewa usemi wao kuhusu madai ya mwanao.
Umuhimu wa Bi. Gatoni
Anadhihirisha nafasi ya teknohama katika kujenga na kuendeleza jamii.
Ni kiwakilishi cha uwajibikaji katika utendakazi.
Kupitia kwake, nafasi na umuhimu wa vyombo vya habari katika jamii unadhihirika.
Mbinu za Uandishi
Tashbihi
… na meno meupe mithili ya theluji…
Mkabala… kulikuwa na kiwambo kikubwa kama ukuta.
Tulizidi kufanya kazi kwa pamoja na kupendana kama ndugu wa toka nitoke
.…kuniruhusu kufanya biashara ni kama kuniingiza katika chuo cha maisha.
Majazi Siri. Anaficha sababu kuu ya kuwaita wazazi wake katika mahojiano.
Anamwambia Jack asiwadokezee kuwa ana ujumbe anaotaka kupasha ulimwengu.
Hata hamwambii Jack jambo gani haswa ananuia kusema.Kalia. Ina maana ya kukaa juu ya mtu au kitu.
Hutumika pia kumaanisha kumdhulumu mtu bila hiari yake. Anamkalia Jack kwa kunyakua nafasi yake na kumpa Siri.
Kwenye studio, anataka kumkalia Siri kwa kumwagiza asidokeze yasiyofaa lakini hampati kwenye simu.
Kikwetu.
Jina ya runinga anayohojiwa Siri.
Ni ya kikwetu, kwani inatumia lugha ya Kiswahili, na pia inahoji masuala ya kinyumbani kwa watu wa nyumbani.
Masumbuko.
Jina la pili la Jack. Anasumbuka kwa kuhiniwa nafasi yake ya ufadhili, kushindwa kuendelea na masomo na kulazimishwa kulipa nusu ya faida yake kwa wazazi wa Siri.
Analainisha nguo kwa kuiweka chini ya mto na kuvaa suruali ambayo haijakauka.
Kinaya
Tunaambiwa kuwa Jack ndiye anaenda kwa Kalia kuwaunganishia mitambo kuwasiliana na Siri.
Ajabu ni kuwa licha ya kuwasaidia, hawamjali hata kidogo.Siri anaeleza hali ya kinaya katika riwaya ya Z. burhani, ‘Mwisho wa Kosa’.
Monika, mhusika mkuu, anapelekwa ng’ambo kusoma.
Marejeo yake yanayotarajiwa kuleta furaha yanaleta huzuni.
Waliomsomesha na kumtunza anawaona kama hawana maana na kuwakebehi.
Siri anafundisha watu wa Uchina Kiswahili.
Anasema kuwa baadhi yao wanapata umilisi zaidi ya watu wa nyumbani, waliolelewa na lugha hiyo!
Kalia anaenda msalani kumwambia Siri kuwa kuna sehemu ya ufanisi wake ambayo haifai kujulikana na mtu yeyote, seuze ulimwengu.
Ajabu ni kuwa jambo hilo ndilo sababu kuu ya mahojiano haya.
Siri anapanga kulisema kwa ulimwengu.
Kalia anampoka Jack nafasi ya kujiunga na chuo kikuu Uchina na kumpa Siri.
Ajabu ni kuwa ana uwezo wa kumsomesha Siri bila msaada, na anayepokwa nafasi hiyo ni yatima!
Isitoshe, alitoa ahadi ya kumkimu baada ya wazazi wake kufariki.
Bi. Mshewa anamwagiza Jack kutoa nusu ya faida yake kwao, eti ni shukran ya malezi.
Ajabu ni kuwa hawajamlea kwa vyovyote, kwani walimhini fursa yake na kutogharamia masomo yake ya juu.
Semi
kuzungumza moja kwa moja- kwa kuonana, bila kupitia kwa mtu mwingine.
akapiga funda la sharubati- akatia kiasi mdomoni na kumeza.
kupasua mbarika- kusema ukweli wa jambo lenye uzito.
alimkazia macho- alimwangalia bila kupesa.
kazi ya Jack ilikuwa ya kupigiwa mfano- yenye ubora wa kipekee.
alikuwa na kibarua kigumu- alikuwa katika hali ngumu.
Methali
Udugu ni kufaana, sio kufanana.
Liwalo na liweLisilobudi hubidi.
Chuku
Urafiki wao ulifana kiasi cha wao kujulikana na watu wengi kama ndugu.
Makochi… yalipendeza mno kiasi cha kijana huyu kutoamini alifaa kuketi hapo.
Kuchanganya Ndimi
.… Siri huwasiliana na wazazi wake kwa njia ya skype.
Upande wa kushoto…, kulikuwa na nembo ya skype.
Ni kutokana na mchango wako kupitia twitter na facebook…
“Nani hapo nchini asiyetambua Masu footwear?”
Tashihisi
Akachukua shati la kipekee… Lilikuwa limetii amri ya kunyooka baada ya kulaliwa……usifanye hivyo mbele ya macho na masikio ya dunia nzima.
Hata hivyo, kimya chake hunihukumu mno.
Taswira
Urefu wa kimo rangi ya maji ya kunde na meno meupe mithili ya theluji ni baadhi ya sifa za Siri.
Ukumbi wa mahojiano ulikuwa mtulivu na ulisheheni usafi asiowahi kuona Jack.
Makochi yenye rangi ya manjano yalipendeza… bwana Kalia na mkewe, Bi. Mshewa, waliketi kwenye kochi lililowasitiri vyema.
Jack aliketi kwenye jingine karibu na alipokuwa mtangazaji.
Mkabala na alipokuwa mtangazaji, kulikuwa na kiwambo kikubwa kama ukuta…
Upande wa kushoto pembeni mwa kiwambo hicho, kulikuwa na nembo ya skype.
Maswali Balagha
“Nani hapo nchini asiyetambua Masu footwear?”
Mtangazaji alikuwa na kibarua kigumu. Angesema nini?
Uzungumzi Nafsia
Huenda huu ndio wakati wa kupasua mbarika! Siri, usifanye hivyo mbele ya macho na masikio ya dunia nzima, aliwaza Jack.
Hadithi ndani ya Hadithi
Jack anasimulia kuhusu hadithi ya Monika katika riwaya ya Z. Burhani , ‘Mwisho wa Kosa’. Anaeleza alivyochukizwa na tabia ya Monika kuwakebehi watu waliomfaa katika masomo baada ya kurejea kutoka ng’ambo.
Ndiyo inampa motisha ya kuenzi asili yake, na kufundisha Kiswahili Uchina.
Mbinu nyingine ni kama Mahojiano, Nidaa na Utohozi.
Download Toba ya Kalia summary notes - Mwongozo wa Mapamazuko ya Machweo na Hadithi Nyingine.
Tap Here to Download for 50/-
Get on WhatsApp for 50/-
Why download?
- ✔ To read offline at any time.
- ✔ To Print at your convenience
- ✔ Share Easily with Friends / Students