- Mtiririko
- Ufaafu wa Anwani ‘Nilitamani’
- Dhamira ya Mwandishi
- Maudhui.
- Wahusika: Sifa na Umuhimu
- Mbinu za Uandishi
Nilitamani- Phibbian Muthama.
Mtiririko
Tumaini(Msimulizi) yuko katika hali ya kutanga huku njaa imemzidi, kwani hajala tangu jana ila chai rangi aliyokunywa usiku, ila ana matumaini ya maisha bora.
Ameondoka kwa Nina awali, anayemkaribisha katika nchi hii ya Wabongo na kuishi naye kama mwanawe kwa muda.
Tumaini alimwacha mwanawe wa pekee na bibi yake, Farida.
Nina anamtembeza, kumtunza na kumshauri kuepukana na Wabongo.
Sasa anagundua alimwonea gere Nina kutokana na majaliwa ya mume mzuri na mali.
Naye anatamani kuishi maisha mazuri kama Nina.
Aliona hafai kugharamiwa na Nina, akaondoka kwake.
Yuko kwenye stendi anapowaza haya.
Anaamua kwenda Kariokoo kusaka kazi yoyote ya kumpa hela.
Anasimamisha gari na kondakta anakubali kumbeba bure baada ya kumdanganya amepoteza kipochi chake.
Anashuka sokoni Kariokoo na kuanza kupitapita maduka ya Wahindi.
Anahofia kuwa watamtambua kwa Kiswahili chake na sura ya ugeni, lakini ana imani.
Machozi yanamtoka kwani hana wa kumwauni na hataki kumsumbua Nina.
Anaona ofisi za mabasi ya Tahmeed, anayoyajua tangu Kenya na kwenda hapo.
Anampata kaka mmoja anayemfaa kwa shilingi elfu tano za Tanzania na kumpa nambari ya simu, akimwahidi kumjuvya akipata kazi.
Ananunua chakula na kumnunulia rafikiye, Jenifa matembele.
Baada ya wiki tatu, anampigia jamaa huyu simu lakini hapatikani.
Anabaki kumtegemea Mungu tu. Anaona Jenifa hana tabasamu tena, labda sababu yake kuwa kupe.
Hataki kumsumbua Nina amsaidie japo anahitaji.
Anawaza kurudi Kenya, lakini anaona hawezi kurudi mikono mitupu.
Anaanza sasa kutaka, sio kutamani.
Anataka maisha mema na mume mzuri.
Jumamosi moja, Nina anampigia simu kumjulia hali, kisha kwa hiari akamtumia pesa kiasi.
Siku hizi hali nyumbani, anamdanganya Jenifa amekula alikokuwa kumpunguzia gharama.
Anaamua kubarizi Coco Beach. Anaketi ufuoni kwenye pareo akiangalia bahari, baada ya kununua mihogo na soda.
Anasikia mlio wa gari, na kando yake anasimama mwanamume mmoja.
Anamwona kama aliyemtamani awe wake.
Sura yake inamvutia na anaamua kumsikiza.
Mwanamume anadai kuwa aliwahi kumwona Westlands, nchini Kenya.
Mwanamume yule anamwalika chamcha na kumshika mkono.
Wanaondoka wakizungumza, na hapo anajua jina lake ni Romeo.
Tumaini anamwona kuwa mumewe anayetarajia kwa uzuri wake.
Romeo naye anashtakia mapenzi kwake.
Wanaelekea asikojua, ila tu anakisia ni kwenye migahawa mikubwa.
Anamweleza atakavyomfanya tajiri kwa kumiliki mali yake tele.
Kuwa Mbongo hakumfanyi kughairi nia ya kuolewa naye.
Ndani ya gari, hisia zinazidi kumsisimka Tumaini.
Wanatabasamu wote. Romeo anampapasa na kumzulia msisimko mkubwa.
Anamwita na kumwambia kwambe yeye(Romeo) si mtu wa kawaida, tena atakuwa mke wake katika dunia yao mpya.
Alikoingia hawezi kutoka. Sauti yake ni nzito na kali.
Tumaini anaanza kujuta.
Anasikia simu ya Romeo ikiita na kusikia kwamba damu yake inatakikana! Romeo napoongea kwenye simu, Tumaini anafaulu kujifungua mkanda.
Anajaribu kufungua mlango lakini umetiwa ufunguo.
Anapita juu ya Romeo na kuponyoka mbio. Anakata misitu bila kujua aendako.
Anatamani sasa kuwa nyumbani Kenya.
Alitamani kupata mume mzuri, lakini si kwa njia hii.
Vyote alivyotamani vimemponyoka.
Ufaafu wa Anwani ‘Nilitamani’
Ina maana ya kuwa ‘nilitaka sana’.
Hali hii ya kutamani ndiyo inamzonga msimulizi tangu mwanzo hadi mwisho.
Kwanza, anaondoka kwao Kenya hadi nchi ya Wabongo kwa kutamani maisha mazuri.
Licha ya mengi yanayomkumba, ana matumaini makuu kuwa atapata maisha bora.
Tumaini anaishi na Nina ambaye anamtunza vizuri kama mwanawe.
Anamkidhia mahitaji yake yote.
Anaona jinsi Nina alivyobarikiwa kwa mume mzuri na utajiri mwingi.
Anatamani kuwa na milki kama hiyo ya Nina.
Ndiyo mara ya kwanza anagundua kwamba alimwonea gere.
Anapohama kwa Nina, Tumaini ana matumaini ya maisha mazuri.
Anaazimia kutafuta kibarua cha aina yoyote, almuradi aweze kutia tonge kinywani.
Kwenye stendi alipo, anaamua kupanda basi kuelekea Kariokoo, akitamani kutafuta kibarua huko angaa apate hela kiasi.
Tumaini anapatana na kaka mmoja kwenye ofisi ya mabasi ya Tahmeed, ambaye anamwahidi kumtafutia kazi na kumpa nambari yake ya simu.
Tamaa ya kupata kazi inamtuma kumpigia baada ya wiki, lakini anamkosa.
Anabaki kutamani tu.
Mambo yanazidi kuwa magumu kwake, lakini anabakia na matumaini kwamba ipo siku.
Anatamani pia kumtua Jenifa mzigo wa utegemezi, lakini hana namna.
Anaona kwamba hana raha, na anakisia ni kwa sababu anatumia vitu vyake bure bilashi.
Anahofia pia kumkopa Nina japo ana uhitaji.
Kutamani kwake kunamtuma kumlilia Mungu, akiahidi kumtumikia milele akimpa ajira. Hakuna ibada inayompita.
Tumaini anatamani kurudi nyumbani lakini hana namna.
Anashangaa jinsi bibi yake atampokea, na mwanawe Radhi.
Hawezi kuwarudia hivyo tu.
Anaamua heri kufia huku ugenini.
Anazidi kutumaini kila uchao, na sasa anapanda ngazi kutoka kutumaini na kuanza kutaka.
Anataka yaliyo mema na mazuri, maisha matamu.
Kutamani kwake kunajisisitiza kwa ushairi mawazoni.
Anatamani kuwa na kasri afurahie, kazi ajikimu, na gari la kifahari.
Anatamani kupata mume mwema wa ndoa, wapate watoto wema waadilike kwa dini, maisha yawe mepesi na kumpa burudani.
Tumaini anatumiwa pesa kiasi na rafikiye Nina na kuamua kwenda kubarizi Coco Beach.
Anakutana na Romeo, mwanamume mtanashati ambaye anamshtakia mapenzi.
Kwa tamaa yake, anamwona kama mwanamume aliyemwaza kwenye lile shairi lake.
Wanaandamana huku akijidai kumpeleka katika mgahawa mmoja mkubwa.
Romeo na Tumaini wanavutana katika mapenzi kama sumaku.
Hata hivyo, anagundua jinsi kutamani kwake kulivyomwingiza matatani.
Romeo anamwambia sasa atakuwa mke wake katika dunia yake mpya, kwani yeye si binadamu halisi.
Anagundua hatari aliyoko anaposikia Romeo akiitishwa damu yake.
Anaponyoka na kuchana mbuga mbio.
Anapasua misitu na kutoroka, asijue aendako.
Japo alitamani kupata mume, si kwa njia hiyo.
Anatamani kuwa nyumbani kwao Kenya ikiwezekana.
Anakumbuka vyote alivyotamani bila mafanikio, ila tu mitihani inayomzonga.
Alitamani lakini hajaweza.
Dhamira ya Mwandishi
Anawasilisha matatizo yanayowakumba raia wanaoazimia kujaribisha maisha katika nchi za kigeni.
Anadhihirisha hatari ya kuwa na tamaa kupita kiasi.
Anaonyesha umuhimu wa kuthamini nyumbani, hata kukawa vipi kwani bado ni nyumbani.
Anawasilisha matatizo yanayowakumba vijana katika harakati za kutafuta riziki.
Anasawiri dini na nafasi na umuhimu wake katika kujenga na kuendeleza jamii.
Anaonyesha ulaghai wa kimapenzi na hatari zake kwa wahasiriwa.
Maudhui.
Tamaa.
Tumaini ana tamaa sana katika maisha yake.
Anatamani maisha mazuri na kuamua kuondoka kwao Kenya kwenda nchi ya Wabongo kufuatilia maisha hayo.
Anatamani kuwa na mali kama Nina, anatamani kuishi kwa raha teletele na pia kupata kazi nzuri.
Tumaini anapanda kutoka kiwango cha kutamani na kuanza kutaka.
Anataka maisha mazuri, anataka mume wake waoane na kupata watoto wazuri.
Anapokutana na Romeo akibarizi Coco Beach, anahisi kwamba amepata mume aliyetamani.
Romeo anashtakia mapenzi kwake, naye Tumaini anasalitika.
Anamwona kuwa mtanashati zaidi duniani na kuamua kumkwamilia.
Tamaa ya Tuamaini inamgutua anapomaizi kwamba Romeo si binadamu wa kawaida bali jini.
Anamwambia kuwa ashakuwa mkewe katika dunia yao mpya wala hawezi kutoroka.
Anasikia waziwazi Romeo akiitishwa damu yake.
Anafaulu kuponyoka na kutorokea vichakani.
Tumaini anajutia tamaa yake.
Anakumbuka mambo yote aliyotamani maishani na ambayo hajafanikiwa kuyapata, bali amebakia tu kujipata kwenye mitihani.
Sasa anatamani angekuwa nyumbani kwao Kenya ikiwezekana.
Ametamani vingi, tena sana, lakini hajafanikiwa.
Utabaka.
Tumaini yuko katika tabaka la chini katika jamii.
Anaishi kwa kupapatisha.
Kila siku anahisi afadhali jana kwa jinsi matatizo yanavyomzidi.
Anatamani kupata kazi ili ayaboreshe maisha yake lakini mambo hayawi mazuri hata kidogo.
Mhudumu kwenye ofisi ya Tahmeed anamwahidi kumwitia nafasi ya kazi ikipatikana lakini baadaye anapiga nambari aliyompa na kumkosa.
Anatafuta kazi hapa na pale bila mafanikio.
Anamtegemea rafikiye, Jenifa, ambaye anaonekana kukosa furaha.
Anapofikiri amefanikiwa, anagundua kwamba ndio ameangukia pabaya, kwani anayedhani kuwa atamkweza upeo mwingine anaondokea kuwa hasidi.
Anataka kumtoa kafara na analazimika kutoroka.
Jenifa anaweza kusemekana kwamba yuko katika tabaka la kati.
Si tajiri mkubwa vile, lakini angalau ana uwezo wa kujikimu na kumsaidia Tumaini.
Tumaini anajiona mzigo kwake kwa kumtegemea kwa vitu vya matumizi na kuamua kumtua.
Mara kwa mara anamdanganya amekula ili kumpunguzia mzigo wa kumlisha na kukaa njaa.
Kwa upande mwingine, kuna walio katika tabaka la juu kama Nina na Romeo.
Nina na mumewe wanamiliki mali tele hadi kumtia gere Tumaini.
Anaazimia sana kuwa kama Nina na kumiliki mali aliyo nayo lakini hana namna.
Anamkidhia Tumaini mahitaji yake yote bila matatizo hadi anapoamua mwenyewe kuondoka.
Hata anamtumia Tumaini hela kwa hiari yake, kwani kwake si tatizo.
Romeo anakutana na Tumaini katika mkahawa wa Coco Beach, ambapo anajipumbaza kusahau matatizo yake.
Ana gari aina ya Audi Q5 ambalo ni ishara ya hali yake ya kiuchumi.
Anambeba Tumaini na kumzuga kwa namna atakavyomfanya tajiri na mmiliki wa mali yake tele.
Kazi
Ndiyo nguzo kuu ya kujiendeshea maisha.
Tumaini anataka sana kupata kazi ili aweze kuwa na maisha bora.
Ni moja kati ya sababu zake kuu kuondoka nchini kwao Kenya na kuhamia nchi ya Wabongo.
Anaona kuwa atapata kazi huko na kuyaboresha maisha yake, ya bibi yake na mwanawe.
Akiwa kwenye stendi, Tumaini anaamua kupanda basi kuelekea mjini kutafuta kibarua Kariokoo.
Anaazimia kuwasaidiasaidia matajiri katika kuendesha biashara zao, labda hata awe mesenja.
Hajali kazi atakayofanya, mradi tu aweze kupata hela kidogo za kukidhi mahitaji yake.
Anakutana na jamaa mmoja kwenye ofisi za mabasi ya Tahmeed, ambapo amefika kuulizia kibarua cha aina yoyote.
Kijana yule anampa nambari yake akimwahidi kumpigia akipata nafasi ya kazi.
Baada ya wiki tatu, anaamua kumpigia lakini anamkosa kwenye ile nambari.
Bado ana matumaini ya kupata kazi, na anamwomba Mungu amjalie kila mara.
Urafiki
Tumaini anajaliwa marafiki wawili wa dhati, Nina na Jenifa.
Anapofika nchini mwanzo, ni rafikiye Nina anamweka na kumkidhia mahitaji yake yote kama mwanawe.
Anampa ushauri pia kuepukana na Wabongo, ambao ni wasanii, asije akajipata pabaya.
Anamkidhia haja zote wala halalamiki, hadi Tumaini mwenyewe anapoamua kuondoka.
Nina anampigia simu kumjulia hali.
Tumaini hana nia ya kumjuza kuhusu masaibu anayopitia, wala hawazii kurudi tena kwa Nina.
Hata hivyo, Nina anajitolea kwa hiari yake kumtumia pesa kiasi kwenye simu yake, ambazo anaamua kujiburudisha kwenye mkahawa kando ya bahari.
Baada ya kuagana na Nina, Tumaini anaishi na rafikiye mwingine, Jenifa.
Ndiye anakidhi mahitaji ya nyumba.
Tumaini anahisi ugumu wa kumtegemea kwa kila kitu kwa kuwa hana kazi.
Anahisi kuwa mzigo kwa kutumia chakula, sabuni, mafuta na vitu vingine vyake.
Anaamua kumhadaa mara kwa mara kwamba amekula ili kuepuka hayo.
Anapopata hela kutoka kwa kijana wa mabasi ya Tahmed, anamnunulia Jenifa matembele.
Mazingira
Tumaini anapendezwa na mazingira ya nyumbani kwa Nina anakoishi baada ya kufika nchi ya Wabongo.
Anasema kwamba Nina na mumewe walimiliki mashamba ya misitu, magari ya usafiri na nyumba kama kasri.
Kuna taa za kisasa, madirisha makubwa kama ya benki na miti ya manukato iliyozingira kama vile milangilangi na misumini.
Mazingira ya Coco Beach pia yanaonekana kuwa ya kuvutia sana.
Tumaini ananunua kaukau za muhogo na soda ya pepsi kisha kutandaza leso chini na kukaa kuvinjari.
Ni kwenye ufuo wa bahari na anaketi akiitazama. Inaashiria maisha yasiyokuwa na kikomo.
Romeo naye anapombeba Tumaini, anampeleka hadi kwenye ufuo wa bahari na kumwonyesha baadhi ya mali anayomiliki.
Anamwonyesha majumba ya kifahari karibu na ufuo wa bahari, penye miti iliyoshika rangi ya kijani.
Hata anapopata upenyu wa kutoroka, anakata katikati ya misitu na kukimbilia huko.
Ulaghai
Tumaini anamjulisha konda kwamba anaomba kubebwa bila hela.
Anamdanganya kuwa amepoteza kipochi chake, lakini ukweli ni kuwa hana hela zozote.
Ili kutilia mkazo ulaghai wake, anatumia sauti ya unyenyekevu na kuvaa wasiwasi usoni.
Tumaini anakutana na jamaa kwenye ofisi za mabasi ya Tahmeed, ambaye anamwahidi kumsaidia kupata kazi akipata yoyote mahali.
Anampa nambari na kumwahidi kumpigia. Hata hivyo, Tumaini anapiga nambari hiyo baada ya kama wiki tatu hivi lakini anaambiwa kwamba haitumiki.
Romeo pia anamteka Tumaini kwa ulaghai.
Anajitia kwamba amewahi kukutana naye mtaani Westlands, nchini Kenya.
Hata hivyo, Tumaini anagundua baadaye kuwa kwao ni Zanzibar.
Isitoshe, anamchochea kwa maneno ya mapenzi hadi kumteka mzima, bali ana nia tofauti ya kumtia mtegoni Tumaini.
Anataka kumpeleka katika ulimwengu wake tofauti na huu wa binadamu wa kawaida.
Starehe na Anasa.
Tumaini anapotumiwa hela na Nina, anaamua kwenda kuvinjari kwenye Coco Beach, karibu na ufuo wa bahari.
Ananunua kaukau za muhogo na soda ya pepsi na kuketi kwenye pareo kujiburudisha.
Anatazama maji ya bahari na kuyaona kama maisha yasiyo na mwisho.
Romeo anapokutana na Tumaini, anamteka kwa fikra kuwa anapelekwa katika migahawa mikubwa pale mjini.
Anamwendesha hadi kwenye ufuo wa bahari na kumwonyesha majumba yake mengi pamoja na miti iliyoshika rangi ya kijani.
Ndoa.
Nina na mumewe wanaishi kwa staha na hali ya kumtamanisha yeyote kuwa katika ndoa.
Mume mwenyewe ameumbika vizuri, na pia wanamiliki mali ya aina tofauti ambayo inafanya maisha yao kuwa ya raha mstarehe.
Hata Tumaini anapoishi nao anaanza kuwaonea wivu na kutamani kuwa na mume kama huyo.
Tuamini yuko katika ndoa ya kisaikolojia.
Anatamani sana kupata mume mzuri amwoe, waishi maisha mazuri.
Anajiona akiwa ameolewa, huku wamejaliwa watoto ambao wanawalea kwenye misingi ya kidini na kuwakuza vyema.
Hata anapokutana na Romeo, mawazo haya ndiyo yanayomsukuma kwake.
Anamwona jinsi alivyo mtanashati na kudondokea kwake.
Romeo anamweleza mapenzi yake kwake na Tumaini anasalitika.
Wanapofika ufuoni, Romeo anamwambia kwamba atakuwa mkewe kwenye dunia mpya, kwani yeye si binadamu wa kawaida.
Japo Tumaini anatamani kupata mume, si kwa njia hiyo.
Anakataa na kutoroka mbio.Maudhui mengine ni pamoja na Mabadiliko, Malezi, Kutowajibika, Umaskini na Dini.
Wahusika: Sifa na Umuhimu
Tumaini
Ni mwenye tamaa.
Anatamani kumiliki mali kama ya Nina.
Anatamani kuwa mtu wa maana katika jamii, na kubadilisha hali yake ya maisha.
Anatamani kuwa na mume mzuri na familia.
Anapokutana na Romeo, tamaa inamwangusha mtegoni, nusura aishie dunia nyingine!
Ni mwenye tumaini.
Licha ya hali ngumu, bado anaona kwamba mambo yatakuwa mazuri.
Anasema kwamba anazidi kutafuta kazi kila uchao, akiamini kwamba siku yake itafika.
Ni mnafiki.
Anapoona mambo yake yameenda kombo, anamgeukia Mungu na kumpa ahadi ya kumtumikia milele iwapo atamfungulia milango.
Anakuwa mtu wa kanisa wala hakuna ibada inayompita.
Ni mwenye utu.
Hataki kuwa mzigo kwa yeyote, na anafanya kila awezalo kutimiza hili.
Baada ya kuishi kwa Nina kwa muda akimtimizia mahitaji yake, anaondoka.
Anamdanganya Jenifa amekula alikokuwa ili kumpunguzia gharama.
Anaposaidiwa hela mjini, anamnunulia matembele.
Ni mwongo/mdanganyifu/mhadaifu/mzandiki.
Anamhadaa kondakta wa basi kwamba kipochi chake kimepotea na kutumia sauti ya unyenyekevu na kuvaa uso wa wasiwasi.
Anamhadaa Jenifa kuwa amekula alikokuwa.
Anamhakikishia Nina kuwa yuko sawa japo matatizo yamemjaa.
Ni mwenye bidii.
Kila uchao anajituma kuhakikisha kwamba maisha yake yanakuwa bora.
Anaazimia kupata angalau hela kidogo kuwaauni bibi yake Farida na mwanawe Radhi.
Anazuru kila sehemu katika harakati za kusaka ajira ya aina yoyote.
Ni mkakamavu.
Anapofanya uamuzi, basi.
Anatoka kwao na kuhamia nchi ya Wabongo ili kusaka maisha mapya.
Japo mambo huko ni magumu mno, anajikakamua na kupambana na hali.
Anahiari kufia huko kuliko kurudi nyumbani mikono mitupu.
Ni mwoga.
Anapofahamu nia haswa ya Romeo kwake, anagutuka kupata kwamba amejitabawalia.
Umuhimu wa Tumaini.
Kupitia kwake, masaibu yanayowakumba raia katika nchi za kigeni yanadhihirika.
Ni kiwakilishi cha bidii na tumaini katika kusaka maisha bora.
Ni kiwakilishi cha matatizo halisi ya maisha hasa kwa maskini.
Kupitia kwake, madhara ya kuwa na tamaa iliyokinai yanabainika wazi.
Ni kielelezo cha utu katika jamii.
Ni kionyeshi cha unafiki wa kidini, ambayo anaikwamia wakati wa matatizo.
Nina
Ni mwenye utu.
Anampokea Tumaini ambaye ni raia wa nchi nyingine kwake na kumkidhia mahitaji yake yote bila lalama.
Anamsaidia kujizoesha maisha yake mapya.
Akiwa kwa Jenifa, anamtumia hela kwa hiari yake mwenyewe.
Ni mshauri.
Anampa Tumaini ushauri dhidi ya Wabongo, ambao wana sifa za kisanii.
Anamwonya ajihadhari nao wasije wakamwacha kwa mataa.
Ni mfadhili.
Tumaini anapoishi kwake, anamfadhili kwa kila kitu wala hapati tatizo lolote hadi anapoondoka.
Hata akiwa kwa Jenifa, anamtumia hela kwenye simu yake aweze kujifaa.
Ni mwenye kujali.
Anamkidhia Tumaini kila kitu na kuhakikisha kwamba ako sawa katika hali zote.
Anamshauri dhidi ya kuwaamini sana Wabongo asije akaingia matatani.
Anamjulia hali mara kwa mara baada ya kuondoka kwake.
Umuhimu wa Nina.
Ni kiwakilishi cha utu na ubinadamu katika jamii.Kupitia kwake, nafasi ya mwanamke katika jamii inadhihirika.
Ni kiwakilishi cha utabaka na mipaka yake katika jamii.
Jenifa
Ni mfadhili.
Anamkidhia Tumaini mahitaji yake yote anapoondoka kwa Nina.
Tumaini anasema kuwa labda anamkera kwa kutumia vitu vyake kama sabuni, mafuta na vitu vingine vidogovidogo.
Ni mwenye shukrani.
Anamshukuru Tumaini anapotoka mjini na kumletea matembele.
Anamshukuru kwa hilo japo dogo tu.
Ni rafiki wa dhati.
Anamsaidia Tumaini katika maisha kama rafiki yake.
Anamlisha na kuishi naye kwake.
Umuhimu wa Jenifa
Ni kiwakilishi cha urafiki wa dhati wa kufaana katika dhiki.
Ni kielelezo cha utu na ubinadamu katika jamii.
Kupitia kwake, tunajifunza kuwa na shukrani hata kwa ajili ya vitu vidogo.
Romeo
Ni laghai.
Anamhadaa Tumaini kwa kisingizio cha mahaba, lakini ukweli ni kwamba anataka kumtumia kwa matambiko yake.
Anamteka kwa ahadi nzito nzito zinazomfumba macho Tumaini.
Ni katili.
Anamlazimisha Tumaini kuwa mkewe wa kipepo.
Anamwambia kuwa ameshaingia katika ulimwengu huo na hawezi kutoka.
Wenzake wanampigia simu kudai damu ya Tumaini.
Umuhimu wa Romeo
Kupitia kwake, ulaghai wa kimapenzi unadhihirika na hatari zake.
Ni kiwakilishi cha uongo na utapeli katika jamii.
Ni kiwakilishi cha madhabahu ya kipepo yanayotumiwa kujilimbikiza utajiri.
Mbinu za Uandishi
Tashbihi
…viwanda na nyumba yao ya kuishi kama kasri la sultan vile
.…madirisha makubwa kama ya benki…
Nilitaka niufukuze ukata niliozaliwa nao.
Niliuona kama laana.
Mweupe, macho yake ya wastani meupe kama theluji lakini malegevu.
Ngozi yake imetepekwa kama jejeta.
Tukaridhiana.
Niliona kama mwezi umechukua nafasi ya jua kuniangazia mwanga.
Siku niliyopata mume bila kutafuta, kama miujiza.
Tukawa kama pacha wa huba.Maisha hapa ni tofauti na nilikoishi mimi.
Maisha kama peponi.
Nikamwangalia usoni, anametameta kama ana lulu ndani yake…
Nilivyovitamani vyote nikavilaani.
Niliona kama ndoto.
Tashihisi
Mara mawazo yanijia akilini na kuizonga nafsi
……kuona miji tofautitofauti na kujua jinsi nitakavyotakabaliana na hali ya maisha katika nchi hii.
Tabasamu nzuri iliyoficha pua yake ya kubabatana
.…maisha yanikubali nami niyakubali, tukubaliane na tufaane
.…nikaona bora niondoke nami nikapambane na maisha ya mjini.
Pale nikawa napita maduka ya Wahindi, nikawa nasema na moyo wangu.
Jua …linafifia na kuleta rangi ya manjano na nyekundu. Machweo yanabisha.
Maswali yalikuwa yanasema na akili yangu.
Tukafuata barabara kuu safi, sikumbuki ilikuwa inatuelekeza wapi
… Maisha yalionekana kupumua hewa safi.
Maswali Balagha
Nifanyeje mimi mgeni?
Lakini nifanye nini?
Nilipata tabu sana.
Lakini ningesemaje huko kwetu nirudipo?
Ningerudi na nini hasa?
Pesa gani, mali gani au na nani?
Bibi angenipokeaje?
Na mwanangu mpendwa je?
Radhi wangu? Sijui.Maisha ni kuishi leo.
Wa kesho aishile?
Nikaanza kuvuta taswira ya maisha mapya, nifanyeje nipate nitakacho?
Mbona mitihani inanizonga namna hii?
Majazi
Kigamboni. Ina maana ya vitani. Ni sehemu anakoishi Tumaini. Yuko vitani dhidi ya dhiki, njaa na umaskini.
Tumaini. Ni kuwa imani kuwa jambo litatokea. Ana tumaini katika maisha yake. Hakati tamaa kamwe. Ana tumaini la maisha mema, kupata kazi, mume na familia nzuri.
Nina. Lina maana ya mama. Anamkidhia Tumaini kama mama. Pia ina maana ya umiliki. Ana mali tele, mume mzuri na utu pia.
Romeo. Ni mhusika wa sinema ya kimapenzi ya Romeo and Juliet. Ameshamiri mapenzi motomoto kwa Tumaini, japo ni ya bandia.
Radhi. Ina maana ya neema au baraka. Ni baraka kwa Tumaini kama mwana. Pia ina maana ya msamaha. Tumaini hataki kumrudia mkono mtupu. Anafaa lolote la radhi.
Istiara
Nilihisi nimefika, kwamba nina ufunguo wa maisha niliyoyahitaji… na hapa nilihitaji mlango wa kufungua tu.
Ngao yangu ni imani tu.
Nilivuta subira, japo ulikuwa mtihani mgumu sana.
Nilipanda ngazi kutoka kutamani na kuanza kutaka.
Ile bahari iliashiria maisha yasiyokuwa na mwisho…
Kifua nacho ni cha ngao.
Kila nikimtazama Romeo nampata naye ananitazama.
Tumekua sumaku.
Semi
kusaka tonge- kusaka cha kujikimu kimaisha.
nikaze kamba- nitie bidii na kupambana, nisikate tamaa.
nikakata kauli- nikaamua.
Sikukata tamaa- sikuacha kuwa na matumaini.
bure bilashi- bure kabisa, bila sababu yoyote.
Niume jongoo kwa meno- nifanye jambo nisilopenda, linalotia kinyaa.
Nikashika njia- nikaanza safari.
Moja kwa moja- bila kupinda au kubadilika.
kupiga gumzo- kuzungumza.
Nikakimbia mguu niponye- Nikakimbia kasi sana kuepuka hatari.
Kinaya
Tumaini anasema kwamba Nina alimkirimia kama mama yake kwa kila kitu.
Hata hivyo, anaamua kuondoka kwake, japo hana pa kuishi na kuishi kwa rafiki yake Jenifa.
Ni ajabu kuwa anachoka kufadhiliwa hali hana hanani.
Tumaini anasadiki kwamba alimwonea gere Nina.
Haya ni licha ya roho ya utu ya Nina, ambaye anamkidhia haja zake zote.
Tumaini anapopata hela kutoka kwa Nina, anaamua kwenda kudanganya moyo Coco Beach.
Ananunua kaukau za mihogo na soda ya pepsi na kuketi akitazama bahari.
Anavinjari kama mwenye vyake hali anateseka.
Tumaini anasema kwamba hapendi kusema na wageni lakini Romeo anaonekana kuwa mwungwana.
Tunagundua baadaye kwamba si mwungwana hata kidogo.
Sura yake pia ni kinyume cha uhalisia wake.
Tumaini anaiona Jumamosi hii anayokutana na Romeo kuwa ya fanaka maishani mwake.
Hata hivyo, ni matata zaidi ambayo inamletea mikononi mwa Romeo.
Takriri
Sina namna ila nina matumaini. Matumaini ya kuyaishinda maisha… naona mwanga mpya, ukurasa mpya na matumaini kuzidi.
Alinifunza mambo ainaaina…Niende mjini Kariokoo kusaka kazi hata kama ni kuwasaidiasaidia matajiri…
Nisingejali, almuradi nipate hela kidogo.
Nipate kula. Nipate afua… niipate riziki yangu.
Nahitaji chakula, nahitaji nauli kurudi Kigamboni, nahitaji ajira.
Kila kitu nahitaji.“…nifanye chochote nisife njaa, nisife wakati natamani…
Nisaidie kakangu, ni…sa…i…di…e.”
Ni nadra kumpata mwanamke wa namna yake mjini siku hizi, nadra sana.
Ni miezi sita tangu nigurie hii nchi, sina ajira, sina kibarua, sina hata kibanda. Maisha yalikuwa yashachukua mkondo mpya.
Mkondo wa shida na dhiki.
Nilimpenda na kumpenda zaidi kila hatua.
Nikakimbia mguu niponye.
Nilikimbia nisijue niendako. Nikakimbia.
Taharuki
Mwanzoni, tunabaki kujiuliza maswali kadhaa kuhusu msimulizi.
Ni nani, yuko wapi na anasumbuka kwa nini. Haya yanatanzuka taratibu masimulizi yanavyozidi.
Tumaini anatuambia kuwa ana mwana, Radhi, ambaye amemwacha kwa bibi yake, Farida.
Hatujajuzwa kuhusu wazazi wake, na mazingira aliyopata huyo mtoto, kwani ni wazi kuwa hana mume.
Jenifa ni rafiki ya Tumaini ambaye anamkidhia mahitaji yake ya kimsingi.
Hatujaelezwa zaidi kumhusu, hususan usuli wake wala kazi anayofanya.
Tumaini anafikiri kwamba Romeo ni Mkenya, lakini anagundua baadaye kwamba asili yake ni Zanzibar.
Romeo awali anamwambia kwamba alimwona Westlands, jijini Nairobi.
Hatujui iwapo ni ukweli aliwahi kumwona au amejua ni Mkenya tu kwa mbinu nyingine.
Tumaini mwenyewe anakana japo tunajua ni Mkenya.
Tumaini anapogundua nia ya Romeo, anafaulu kuponyoka kutoka garini mwake na kuyoyomea vichakani.
Hatujui hatima yake ni gani.tunabaki na maswali tele.
Je, atajua vipi njia ya kurudi Kigamboni?
Ataendelea kusaka ajira au atahiari kurudi Kenya?
Tuseme hatarudi nyumbani, Jenifa atachukua hatua gani?
Na je, Romeo aliyemtoroka atamfuata au labda kumnasa kwa mbinu ya giza?
Tamaa ya Tumaini itafika kikomo au ataendelea tu kutamani? Na maswali mengi mengine.
Methali
Maskini hachoki, na akichoka keshapata.
Usiende kwa wenzako mikono mitupu kwani hairambwi.(mkono mtupu haurambwi) Maisha ni kuishi leo, wa kesho aishile?
Chuku
Napunguza mwendo kwa kuishiwa na nguvu, tumbo limebanana na mgongo, usiseme njaa.…kidevu kimenyolewa vizuri utadhani kimechongwa na kuacha uso kung’aa.…na sasa kakutana na mwanamume mtanashati zaidi duniani.Romeo akaanza kunipapasa taratibu.
Nikahisi msisimko wa aina yake, kama mizuka inanipanda vile.
Nikamwangalia usoni, anametameta… mara anageuka mweupe, mara mwekundu!
Taswira
Taswira ya mume wa Nina; …alivyokuwa na mume mzuri, mrefu kiasi, si mweusi si mweupe.
Tabasamu nzuri iliyoficha pua ya kubabatana. Asiyekonda wala kuwa mnene.
Miguu iliyojaa vizuri na kulainishwa na weusi wa malaika…T
aswira ya Tumaini pale Coco Beach; ufuoni nikanunua kaukau za muhogo na soda ya pepsi.
Nikatandaza pareo yangu, nikakaa nikiangalia bahari… ile bahari iliashiria maisha yasiyokuwa na mwisho…
Taswira ya Romeo; Alikuwa wa asili ya Kiarabu. Mweupe, macho yake ya wastani meupe kama theluji ila malegevu.
Uso wenye umbo la embe dodo, kidevu kimenyolewa vizuri utadhani kimechongwa nakuacha uso kung’aa.
Nywele za singa zinanukia udi hasa.
Mwili wote unanukia riha ibura ya uturi. Mikono imechongeka vizuri kwa misuli ya wastani.
Kifua nacho ni cha ngao. Usiseme maguu manene yaliyoketi vizuri kwenye kaptura lake la buluu.
Pale Romeo anapompeleka Tumaini; …Romeo aliegesha gari, akaanza kunionyesha majumba ya kifahari kwenye ufuo wa bahari, penye miti iliyoshika rangi yake ya kijani.
Kuchanganya Ndimi
Romeo na Tumaini wanapokutana katika Coco Beach, wanazungumza kwa lugha ya Kizungu.
Mara ninaona Booking Office ya mabasi yaitwayo Tahmeed…Nikashika njia mpaka Coco Beach.
Tukapiga selfie… Tukatifua vumbi la beach na kuondoka.
Nakumbuka tu akiambiwa, “We need her blood, faster!”
Kisengerenyuma/ Mbinu Rejeshi
Tumaini anakumbuka maisha yake ya tangu utotoni akiwa kwenye stendi alikoketi.
Anakumbuka alivyotoka kwao Kenya, alivyoishi na Nina kwa muda akimkidhia mahitaji yake na baadaye kuhamia kwa rafikiye Jenifa.
Tumaini anapotembea mjini Kariokoo, anaona ofisi za mabasi ya Tahmeed.
Anasema kuwa aliyajua mabasi haya tangu Kenya.
Koja
Ni miezi sita tangu nigurie hii nchi, sina ajira, sina kibarua, sina hata kibanda.
Chakula, sabuni ya kuoga, mafuta na vitu vingine vidogovidogo.
Niliisubiri sana siku hii. Inifae, inikubali, iniridhie, inifanikishe mimi.
Tabaini
Alinifunza mambo ainaina; si upishi, si kuishi na watu kwa wema na kunitoa usungo.
Misimu
Bora uhai!- kauli ya kujipurukusha kutokana na dhiki. Konda- kondakta, anayekusanya nauli garini.
Mbinu nyingine ni pamoja na Mdokezo, Kejeli, Lahaja na Nidaa.
Download Nilitamani summary notes - Mwongozo wa Mapamazuko ya Machweo na Hadithi Nyingine.
Tap Here to Download for 50/-
Get on WhatsApp for 50/-
Why download?
- ✔ To read offline at any time.
- ✔ To Print at your convenience
- ✔ Share Easily with Friends / Students