KCSE 2018 Kiswahili Paper 1 with Marking Scheme

Share via Whatsapp

QUESTIONS

 1. Lazima
  Wewe ni katibu wa chama cha Walinda Mazingira Wasio na Mipaka shuleni mwenu. Andika kumbukumbu za mkutano uliofanyika kujadili suala la uharibifu wa mazingira katika eneo lenu
 2. Udanganyifu katika mitihani haumwathiri mwanafunzi tu, bali pia jamii yake." Fafanua
 3. Tunga kisa kitakachodhihirisha maana ya methali ifuatayo:
  Mti mkuu ukigwa, wana wa ndege huyumba.
 4. Tunga kisa kinachoanza kwa kauli ifuatayo:
  "Waja husema kuwa subira huvuta heri hii yangu inazidi kuvuta machungu kila kuchapo. Hii heri itapatikana lini?" Tuama alijisemea kwa masikitiko.

MARKING SCHEME

 1. Hii ni insha ya kumbukumbu. Vipengele vya: 
  1. Kimuundo vya utungo wa aina hii vidhihirike kama ifuatavyo: 
   1. Kichwa: Kionyeshe :
    1. Kundi linalokutana
    2. Mahali pa mkutano 
    3. Tarehe ya mkutano 
    4. Wakati wa mkutano
   2. Waliohudhuria - vyeo na nyadhifa zidhihirishwe.
   3. Waliotuma udhuru
   4. Ambao hawakuhudhuria
   5. Waalikwa / katika mahudhurio/waliohudhuria, bali si wanachama (si lazima).
   6. Ajenda za mkutano
   7. Kumbukumbu zenyewe:
    1. Utangulizi
    2. Wasilisho la mwenyekiti
    3. Kusomwa na kuthibitishwa kwa kumbukumbu za mkutano uliopita/uliotangulia
    4. Yaliyoibuka kutokana na kumbukumbu hizo 
    5. Masuala yanayojadiliwa leo / masuala mapya (kulingana na ajenda).
   8. Masuala mengineyo
   9. Hitimisho:
    1. sahihi, jina la Mwenyekiti na tarehe
    2. sahihi, jina la Katibu na tarehe
  2. Maudhui
   1. Mtahiniwa adhihirishe majadiliano na uamuzi uliofikiwa na wanachama kuhusu hali ya uhabirifu wa mazingira shuleni na katika ujirani wa shule/eneo lao/mtaa.
   2. Madhara (hatima) ya uharibifu huu yajitokeze.
    Zifuatazo ni baadhi ya hoja:
    1. Utupaji taka ovyo wa wanafunzi - umesababisha hali kama vile kuambulia magonjwa kama vile pepopunda kutokana na kukatwa na vigae vya chupa.
    2. Ukataji wa misitu kwenye ujirani ambayo ingepunguza madhara ya upepo mkali.
    3. Kuacha miti na magugu kujiotea ovyo karibu na majengo ya shule; hiudhoofisha usalama kwani vichaka vinaweza kuwa makao mufti ya majangili na wanyama/wadudu kama vile mbu.
    4. Viwanda kwenye ujirani wa shule kuelekeza taka shuleni; matokeo yakiwa magonjwa ya aina mbalimbali.
    5. Mioshi kutoka mabiwi ya taka yanayochomewa karibu na shule.
    6. Kelele kutoka kwenye magari yanayopita karibu na shule; zinavuruga utulivu madarasani.
    7. Maeneo ambayo yanaweza kutumiwa kupandia vyakula kutumiwa kwa ujenzi, hivyo kutishia kutojitosheleza kwa chakula.
    8. Majengo yaliyosongamana kwenye ujirani wa shule kuwa hatari wakati wa janga kama vile janga la moto.
    9. Upuliziaji dawa mimea kwenye mashamba jirani; dawa hizi zinaweza kuwadhuru baadhi ya wanafunzi ikiwa upuliziaji haudhibitiwi.
    10. Kuelekeza taka kwenye mito/mto ulio karibu na shule huchafua maji yanayoweza, kutumiwa na wanafunzi. Taka hizi huua wanyama wa majini.
     Tanbihi
     Hii ni kumbukumbu, si ripoti sharti majadiliano yadhihirike na uamuzi uliofikiwa kuonyeshwa.
 2. Utungo uonyeshe madhara ya kudanganya katika mitihani, kwa mwanafunzi na kwa jamii yake. Hoja zifuatazo zijadiliwe: 
  1. Udanganyifu husababisha kupata alama ambazo hazilingani na kiwango cha utambuzi cha mwanafunzi. 
  2. Huenda mwanafunzi akapatwa na wasiwasi na hivyo kutofanya vyema. 
  3. Hupalilia upujufu wa maadili hasa unapokuwa na mazoea. 
  4. Humletea mwanafunzi fedheha/hushusha hadhi ya mwanafunzi. 
  5. Hushusha hadhi ya shule. 
  6. Huvifanya vyeti vya nchi/vilivyotuzwa na mabaraza ya mitihani nchini kutothaminiwa kutoaminika kimataifa.
  7. Wanafunzi wanaweza kukosa nafasi katika vyuo vya kimataifa kutokana na sifa mbaya ya mitihani nchini mwao.
  8. Udanganyifu unapogunduliwa mwanafunzi hupoteza matokeo. 
  9. Mwanafunzi kuwa mzigo kwa wazazi kulazimika kulipa karo tena ili arudie.
  10. Wazazi kufedheheka. 
  11. Baadhi ya wanafunzi hujiua udanganyifu unapogunduliwa.
  12. Hudhoofisha viwango vya elimu kwani baadhi ya walimu hungojea kufunza yale tu yaliyo kwenye mtihani uliosambazwa kwao
  13. Kufutwa kwa baadhi ya walimu wanaoshukiwa kuhusika na udanganyifu.
  14. Wanafunzi waliodanganya kufanya kazi wasizozimudu; hulazimika kubadilisha kozi au kuacha masomo.
  15. Kuvyaza wanataaluma ambao humudu kazi zao.
  16. Kudidimiza ubunifu kwani wanafunzi hungojea kupewa maswali, kuyatafutia majibu ili kukidhi haja ya kupita mtihani tu.
  17. Husababisha uharibifu wa mali; wanafunzi wanaoshindwa kupata maswali ya mtihani awali, huanza kujiingiza katika vitendo vya utovu wa nidhamu kama vile kuchoma shule. 
  18. Huwafanya wanafunzi wanaotia bidii masomoni kuvunjika moyo wanaposhindwa na wale wasiotia bidii.
   Tanbihi
   Sharti mtahiniwa ajadili hoja zinazoonyesha athari kwa mwanafunzi na kwa jamii (kama wazazi, walimu na nchi).
 3. Mtahiniwa atunge kisa kinachodhihirisha maana ifuatayo: Kiongozi/mkuu/mzazi akiondoka/akifa, wale wanaomtegemea/wale anaowaongoza hupatwa na shida/ (huzuni hupungukiwa.
  Au
  Kiongozi/mzazi/mkuu akipotoka wale anaowaongoza/wanaomtegemea hutatizika/hupotoka pia.
  Au
  Mtahiniwa aonyeshe kwamba matatizo/maovu yanayofanywa na kiongozi/mzazi huiathiri jamii/familia yake vibaya.
  Hali zifuatazo zinaweza kujitokeza:
  1. Mzazi afariki, watoto wapate shida kama vile kupokwa urithi.
  2. Wazazi wazozane, mwishowe wa farakane na kuwasababishia watoto matatizo.
  3. Baba/mama apotoke, pengine awe mlevi, watoto wainukio kuwa walevi/wakose mahitaji ya kimsingi.
  4. Kiongozi afanye maamuzi yasiyofaa, pengine kuchukua mikopo kutoka nchi nyingine na kuvipagaza vizazi vya kesho madeni.
  5. Kiranja mkuu wa shule apotoke, awapotoshe wanafunzi wenzake.
  6. Kiongozi/Viongozi waibe mali ya umma na kuwasababishia raia umaskini.
  7. Kiongozi wa kidini apotoke na kuwafanya waumini wapotoke.
   Tanbihi
   Sehemu mbili za methali zijitokeze:
   1. Kugwa/kuanguka/kupotoka/kufa kwa kiongozi/mzazi/mtu anayetegemewa. 
   2. Kuyumba kwa wana/ kuteseka/kuhuzunika/kupotoka kwa wanaomtegemea.
 4. Hii ni insha ya mdokezo.
  Mtahiniwa abuni kisa kinachoafikiana na mwelekeo/toni/mtazamo wa kauli hii. Kisa kidhihirishe machungu anayoyapitia msemaji (Tuama), pengine kutokana na mtu mwingine, ugonjwa au hali mbaya inayomzunguka.
  Yafuatayo yanaweza kudhihirika:
  1. Mhusika ametafuta kazi kwa muda asipate, uvumilivu wake unafikia mwisho.
  2. Mhusika asimulie kisa ambamo pengine amekabiliwa na tatizo la kuwa na watoto walemavu, mmoja baada ya mwingine. Anatarajia apate angaa mmoja mwenye afya nafuu. 
  3. Msimulizi awe na mtafaruku na mwenzake; labda mume au mke. Avumilie hadi kufikia kiwango hiki.
  4. Msimulizi augue ugonjwa, atafute matibabu, ugonjwa uendelee kumwathiri hata baada ya kutumia pesa nyingi.
  5. Mhusika akumbwe na matatizo ya ukosefu wa fedha, atafute njia ya kujiinua asipate.
   Tanbihi
   1. Kisa sharti kidhihirishe hali mbaya/machungu/mahangaiko/changamoto anazopitia Msimulizi/Mhusika (Tuama).
   2. Ajaribu/avumilie hadi kufikia kiwango hiki cha kuvunjikiwa.
   3. Kauli hii inaweza kuwa ndiyo mwisho wa kisa, Msimulizi akaturudisha nyuma kuhadithia yaliyotokea.
   4. Msimulizi/mtahiniwa pia anaweza kuanza kwa kauli hii na kuendeleza kisa kuanzia hapo bila kutumia mbinu rejeshi.
Join our whatsapp group for latest updates

Download KCSE 2018 Kiswahili Paper 1 with Marking Scheme.


Tap Here to Download for 50/-
Why download?

 • ✔ To read offline at any time.
 • ✔ To Print at your convenience
 • ✔ Share Easily with Friends / Students


Get on WhatsApp Download as PDF
.
Subscribe now

access all the content at an affordable rate
or
Buy any individual paper or notes as a pdf via MPESA
and get it sent to you via WhatsApp

 

What does our community say about us?

Join our community on:

 • easyelimu app
 • Telegram
 • facebook page
 • twitter page
 • Pinterest