Kiswahili Paper 3 Questions and Answers - KCSE 2020 Past Papers

Share via Whatsapp

Maagizo

  • Jibu maswali manne pekee.
  • Swali la kwanza ni la lazima.
  • Maswali hayo mengine matatu yachaguliwe kutoka sehemu nne zilizobaki; yaani:
    Riwaya, Tamthilia, Ushairi na Fasihi Simulizi.
  • Usijibu maswali mawili kutoka sehemu moja.
  • Majibu yote lazima yaandikwe kwa lugha ya Kiswahili.

SEHEMU A: HADITHI FUPI
A. Chokocho Na D. Kayanda:
Tumbo Lisiloshiba na Hadithi Nyingine

  1. Lazima
    D. Kayanda: "Mwalimu Mstaafu"
    1. "Naomba radhi mfawidhi ... lakini nadhani ni jambo la busara kutokitia mchanga kitumbua .. . "
      1. Eleza muktadha wa dondoo hili .          (alama 4)
      2. Bainisha toni ya dondoo hili.                (alama 2)
      3. Kwa kurejelea hadithi hii jadili kwa kutoa hoja kumi namna mhusika Jairo alivyokitia kitumbua mchanga. (alama 10)
    2. Bainisha vipengele vya kimtindo katika dondoo lifuatalo: (alama 4) 
      "Alijaaliwa mvi nyeupe zilizojianika kwenye kichwa chake kidogo kilichosimama jadidi kwenye shingo yake nyembamba. Alijaaliwa mvi kwa vile zilikuja mapema wakati akiwa bado ana umri wa miaka thelathini. Watu wakasema hekima hiyo kutabasuri huko. Kwa hiyo, hakujisumbua kujipaka rangi nyeusi kuung'ang'ania ujana uliotishia kumwondoka mapema ... mvi zimemkaa kwa haiba kama theluji ... "

SEHEMU B: RIWAYA
A. Matei: Chozi la Heri
Jibu swali la 2 au la 3

  1.  
    1. "Mara moyo unaanza kumwenda mbio na vipapasio vya akili yake kusimama wima. Anajihisi kama anayetarajia kuanza kinyang'anyiro kikali cha upiganaji masumbwi. Kwa mbali anasikia mbisho hafifu ... Anatoka nje kwenda kuitikia mbisho huu ... Mara anasikia moyo wake ukimwambia, "Yako ya arobaini imefika," ...
      1. Eleza muktadha wa dondoo hili.   (alama 4)
      2. Jadili aina mbili za taswira katika dondoo hili.     (alama 2)
      3. Bainisha vipengele vingine vinne vya kimtindo katika dondoo hili.        (alama 4)
    2. Jadili umuhimu wa mandhari katika kuijenga riwaya hii kwa kurejelea kituo cha afya cha Mwanzo Mpya. (alama 10)
  2.   
    1. Changanua mtindo katika kifungo kifuatacho:
      Wakati kama huu Mwangeka angejitanua kifua na kusema. "Mimi ni mwana wa mhunzi, na bila shaka wa mhunzi asiposana huvuvia. Babangu hakuna linalomshinda katika uwanja wa upasuaji. Ni kama yule mbabe wa kivita aliyepigana na Akavi kuwakokoa mifugo wa ukoo wetu kutokana na kutekwa na jamaa hawa ambao siku hizo wakiamini ndio waliotunukiwa na Manani jukumu la kuwamiliki ng'ombe wote. Baba huniambia kuwa mara nyingi huwafufua maiti katika chumba cha wagonjwa mahututi, akawatoa kwenye mashine na kuwarejeshea uhai, jamaa zao wakitazama hivi hivi! Hilo usilione dogo. Tet! Baba si tofauti na huyo Fumo Liyongo tuliokuwa tukihadithiwa na nyanya. Ati bwana huyu angeweza kuinua tani ngapi vile za chuma?"
    2. Kwa kurejelea kisa kinachosimuliwa kuhusu Mwangeka,Mwangemi na babu yao,jadili mchango wa familia katika kuendeleza desturi za kijamii. (alama 12)

SEHEMU C: TAMTHILIA
P.Kea: Kigogo
Jibu swali la 4 au la 5

  1.  "Nilijua ninapoanza, nilijua ninawapunja, nilijua ninawadhuru... lakini nilimezwa na tamaa"
    1. Eleza muktadha wa dondoo hili.     (alama 4)
    2. Bainisha vipengele viwili vya kimtindo katika dondoo hili.  (alama 4)
    3. Fafanua umuhimu wa mzungumzaji katika kuvijenga vipengele vifuatavyo vya tamthilia hii.
      1. Ploti
      2. Maudhui
  2.  
    1. Jadili mchango wa wasomi katika hali ya maisha ya Wanasagamoyo (alama 10)
    2. Fafanua umuhimu wa mazungumzo kati ya Majoka na Daktari katika kujenga tamthilia ya Kigogo.  (alama 10)

SEHEMU D: USHAIRI
Jibu swali la 6 au la 7

  1. Soma shairi lifuatalo kisha ujibu maswali.

    Mruka juu kipungu, hurejea ardhini
    Yasemwa tangu tangu, zamani hizo zamani
    Ukweli jua mchungu, hili mja ubaini
    Mpanda ngazi jamani, hakwei ili kushuka.

    Muhali hili nasema, mpanda ngazi kushuka
    Utabaki kutazama, kama ataporomoka
    Hapo juu kagandama, kileleni amefika
    Mpanda ngazi jamani, kurudi chini hawezi.

    Kurudi chini hawezi, hili jambo muhali
    Ameotesha makwezi, apania kwenda mbali
    Angani ndio makazi, kuanisi kila hali
    Mpanda ngazi jamani, kushuka chini haramu.

    Kushuka chini haramu, hili bado nakariri
    Twabaki kumhukumu, mkwezi huyu mahiri
    Usingoje kwa hamumu, zapita nyingi dahari
    Mpanda ngazi jamani, amebaki kileleni.

    Amebaki kileleni, hukohuko anaketi
    Daima yu furahani, hapati shida katiti
    Walo chini mashakani, walia zao nyakati
    Mpanda ngazi jamani, amepanda akapanda.

    Amepanda akapanda, walio chini wa chini
    Umpinge ukipenda, ila hili libaini
    Mpanda ngazi kapanda, harudi tena badani
    Mpanda gazi jamani, hatashuka kwa hiari .

    Hatashuka kwa hiari, jinsi anavyoanisi
    Wala haoni hatari, katu hana wasiwasi
    Anaishi kwa fahari, ni nyofu yake nafasi
    Mpanda gazi jamani, hakwei ili kushuka

    Hakwei ili kushuka, kuacha yake makao
    Ameshika kwa hakika, mashiko penye mafao
    Amepanga kaka kaka, kuchuma mengi mazao
    Mpanda ngazi jamani, kuija chini hashuki.

    Kuija chini hashuki, mti ungaporomoka
    Tumpige kwa mikuki, ngawiraye kumpoka
    Atahapa haki haki, si halali kwa hakika
    Mpanda ngazi jamani, harudi katu harudi.

    Harudi katu harudi, kurudi chini tulipo
    Apigwe pigo ja radi, atabaki papo hapo
    Bado azidi kaidi, kuapa kila kiapo
    Mpanda ngazi jamani, hakwei ili kushuka.
                                                                 (Kitula K.)

    1. Fafanua, kwa hoja sita mtazamo wa nafsineni kuhusu mpanda ngazi kwa mujibu wa shairi hili. (alama 6)
    2. Eleza aina nne za taswira zinazojitokeza katika shairi hili.   (alama 4)
    3. Bainisha aina tatu za urudiaji zilizotumiwa katika shairi hili.  (alama 3)
    4. Huku ukitoa mifano, onyesha mbinu mbili ambazo mshairi ametumia kutosheleza mahitaji ya kiarudhi. (alama 2)
    5. Bainisha mbinu zifuatazo za kimtindo katika shairi hili:      (alama 3)
      1. Tanakuzi
      2. Chuku
      3. Sitiari
    6. Eleza muundo wa ubeti wa tisa na kumi.        (alamu 2)

  2. Soma Shairi lifuatalo kisha ujibu maswali.

    U wapi ujana wangu, na madhubuti ya nia?
    Niko hapa peke yangu, ujana umepotea
    Umeanacha na machungu, mambo niliyozoea
    Kuwa na uwezo wangu, leo hayawezi kuwa
    Afya ya ujana wangu, nayo imeshika njia,
    Siku za ujana wangu, nazo sizioni pia,
    Nadhari sasa si yangu, tazama hii dunia!

    U wapi ujana wangu, ubingwa na mazoea?
    Ndugu za jamaa zangu, na watu niliojua,
    Wamehama ulimwengu, ni pweke nimebakia
    Nguvu wanazo wenzangu, sasa wanazitumia
    Nikishikacho si changu, ajabu hii dunia.
    Hutia kizunguzungu, wakati wa kuchungua
    Kama hukumbuki Mungu, kufuruni utakuwa.

    U wapi ujana wangu, na maringo ya tabia?
    Hamna kinywani mwangu, jino lililobakia,
    Na laini gumu kwangu, sina cha kutafunia
    Kitamu sasa kichungu, hata kama ni halua
    Kama ningefungwa pingu, sina la kufurahia
    Katika maisha yangu, nimebaki na fadhaa
    Kama fumbo ulimwengu, na watu wazuzuliwa.
                                                                          (S. Robert)

    1. Bainisha kwa hoja tano kinyume kinavyojitokeza katika shairi hili.    (alama 5)
    2. Eleza muundo wa shairi hili.  (alama 4)
    3. Eleza aina nne za taswira katika shairi hili.   (alama 4)
    4. Onyesha mifano ya mbinu zifuatazo katika shairi hili:    (alama 4)
      1. Kweli kinzani
      2. Tashihisi
      3. Tasfida
      4. Usambamba
    5. Bainisha nafsineni katika shairi hili.   (alama 1)
    6. Eleza toni ya shairi hili.     (alama 2)

SEHEMU E: FASIHI SIMULIZI

  1. Soma ufungo ufutao kisha ujibu maswali.

    Zamani sana Sungura na Fisi walikuwa marafiki wa kufa kuzikana. Mjukuu wangu sijui kama umewahi kuuwazia urafiki wa aina hii, ule wa mmoja wao akijikwaa dole anayeuhisi uchungu wenyewe ni mwenzake.

    Siku moja walialikwa karamuni na Tumbili. Marafiki hawa waliafikiana waandamane asubuhi na mapema. Hata hivyo, Fisi alipofika nyumbani kwake moyo wake ulimrai."Ndugu, wewe unajua mambo ya akutanguliaye chanoni hukuzidi tonge na atanguliaye kisimani hunywa maji maenge? Itakuwaje umngojee Sungura na hali kimo chake ndicho hicho? Hata akafika amechelewa atakula shibe yake, wewe unahitaji kutwa nzima kulijaza tumbo lako kuza. Wewe jihimu mapema, huyu mwenzako atakufuata."

    Asubuhi na mapema Fisi alishika tariki ... guu mosi, guu pili... guu mosi, guu pili ... hadi kwa Tumbili  Harufu nzuri ya mapochopocho ilihanikiza hewa; harufu ambayo ilimfanya Fisi kuchezesha midomo yake hivi na mate kudondoka ndo ndo ndo! Fisi alifika karamuni na kuchukua nafasi katika viti vya mbele asije akapitwa na chochote.

    Nyuma kule Sungura alipitia kwa Fisi lakini hakumpata.

    "Lo, kiumbe huyu!'' Sungura alimwuliza Fisi kimoyomoyo, "utaacha lini tabia hii ya usaliti?" "Lazima nikukomeshe!"

    Sungura alipofika karamuni alikaa kule nyuma akiwazia la kufanya. Fisi ambaye hakuwa na mwao na yaliyokuwa akilini mwa Sungura alimwendea na kumwambia. "Ndugu yangu, mtu huhifadhi akipatacho. Sijui kama nitawahi kuambulia shibe ya aina hii. Je, waonaje tukichukua baadhi ya vyakula hivi tupeleke nyumbani?"

    Sungura alimwambia. "Hamna haja kujidhalilisha. Njia mufti ya kuhakikisha hutaona njaa tena ni kuhifadhi kilicho tumboni. Basi nitatumia ujuzi wangu wa utabibu kukusaidia kukitunza chakula tumboni. Fisi alikubali haraka.

    Fisi alilia kwa maumivu makali lakini alipofikiria kuhusu kile chakula slivumilia huku mwili mzima unamtetema. Sungura alikamilisha rnpango wake na kutwaa tabasamu la ushindi.

    Basi mjukuu wangu, Sungura aliutwaa uzi na sindano ambayo alikuwa kahifadhi kwenye kijaluba akaanza kuupitisha ule uzi polepole kwenye msamba wa fisi. Fisi alilia kwa maumivu makali lakini alipofikiria kuhusu kile chakula alivumilia huku mwili mzima unatetema. Sungura alikamilisha mpango wake na kutwaa tabasamu la ushindi.

    Baada ya muda, Fisi alirejea kubugia sahani za vyakula na mifupa bila kufanya nadhari. Polepole, maumbile yalianza kudai haki, naye akatanabahi kwamba Sungura alikuwa kamnyima uwezo wa kuyatosheleza maumbile haja. Aliangaza macho huku na kule, asimwone Sungura. Alijikokota mithili ya ng'ombe anayechungulia kaburi hadi kwa Sungura.

    Alimsihi Sungura amwondolee udhia huu lakini Sungura alikataa katakata, akamwambia "Jikune ujipatapo.'' Na kweli Fisi alijikuna ajipatapo. Kabla Sungura hajafumba jicho, alisikia kilio cha kite, kisha mpasuko mkubwa Sungura aliangua cheko kubwa la stihizai na kumsukuma Fisi kutoka nyumbani kwake huku amefunika mianzi yake ya pua kwa viganja. Huo ukawa mwisho wa urafiki wa Sungura na Fisi. Tangu wakati huo, Fisi yumo mbioni kumtafuta Sungura iii amwadhibu.

    Hadithi yangu imeishia hapo. Naomba ng'ombe wangu wafaidi nyasi za kijani na wako wafe kwa kiangazi.
    1. Onyesha kwa nini hii ni ngano ya usuli. (alama 2)
    2. Fafanua vipengele kumi vya kimtindo ambavyo fanani ametumia kufanikisha uwasilishaji wake. (alama 10)
    3. Eleza umuhimu wa fomyula ya mwisho katika ngano hii. (alama 3)
    4. Wewe ni kati ya wanaotambiwa ngano ya aina hii. Fafanua mambo matano ambayo wewe na wenzako mnaweza kuchangia wakati wa utambaji. (alama 5)


 



 



 



 



 



 



MWONGOZO WA KUSAHIHISHA

  1.  
    1.  

      1.  
        1. Mzungumzaji ni Mwalimu Mustaafu, Mosi.
        2. Anazungumza na hadhira✓ ambayo imekuja kumuaga/mfawidhi
        3. Yuko shuleni✓
        4. Mwalimu mstaafu aligundua baadhi ya wasemaji walibaguliwa.
      2.  
        1. Toni ya kuonya  kutahadharisha - si vizuri kukitia kitumbua mchanga
        2. kunyenyekea/unyenyekevu - Naomba/upole
        3. Masikitio/huzuni.
        4. Kejeli
          (dondoo limetolewa uk.121)
      3.  
        1. Kuwadhalilisha wenzake kama vile Baraka, Festo mshamba na Nangeto anapoonyesha hali yao mbaya ya awali.
        2. Kufichua njama za kifisadi- anasema pesa zilizochangishwa na rais zililiwa na wakora kama vile akina Festo
        3. Anapewa nafasi na Mwalimu Mosi kuhutubu lakini anamuaibisha anasema anafurahia kuondoka kwa Mwalimu Mosi
        4. Kutotambua mchango wa Mwalimu Mosi -anasema Mosi ataondoka shule ipumzike
        5. Anashindwa kustahimili changamoto shuleni. Kim hasomi-uzumbukuku k.m Kim kufeli mtihani.
        6. Anajidhalilisha kwa kusifia✓ suala kama vile utapeli na wizi, hajiamini -  anajiita zumbukuku asiyeweza kuimarika.
        7. Anakosa kuyawajibikia maisha yake. Analaumu✓ Mwalimu Mosi anasema umaskini uwake ulisababishawa na Mwalimu Mstaafu/Kukatazwa kunywa pombe
        8. Anakosa kuwajibikia familia yake. Hatekelezi majukumu yake kama mume na mzazi.
        9. Kutelekeza familia- hakuwahi kupita kwa Mwalimu Mosi kuwajulia hali wanafamilia wake. (uk. 128)
        10. Kumharibia Mwalimu jina kwa kusema kuwa amekioa kitoto chake (uk. 130)
        11. Jairo kutaka kujiua/ kujinyonga /kitanzi/kujitosa majini.
          10 × 1 =10
    2.  
      1. Taswira-uoni-nyeupe, nyembamba
      2. Tashihisi-mvi kujianika
      3. Takriri/urudiaji-Alijaaliwa mvi
      4. Tashbihi-kama theluji
      5. Taashira-mvi-ishara ya hekima
      6. Kinaya-mvi kuashiria busara- kujaliwa mvi mapema
      7. Usimulizi - Kifungu chote ni usimulizi
      8. Chuku/udamisi-mvi kujianika
      9. Mdokezo-kama theluji...
        (dondoo limetolewa uk.120)                  4 × 1=4 
    1.  
      1.  
        1. Haya ni maneno ya msimulizi/mwandishi
        2. Yanamhusu Sauna.
        3. Sauna yumo nyumbani mwa Bi. Kangara.
        4. Anahisi anakabiliwa na hatarifulani ndipo moyo unamwenda mbio
        5. Anapofungua lango anakumbana na polisi ana kwa ana
          (Dondoo limetolewa uk.153)      4×1 =4
      2.  
        1. Taswira hisi - anahisi/kikali
        2. Mwendo - anatoka nje, moyo kumwenda mbio,kusimama.
        3. Usikivu - mbisho hafifu/anasikia
        4. Mguso - vipapasio                              2×1= 2
      3.  
        1. Tashbihi - anajihisi kama anayetarajia kuwa na kinyang'anyiro cha upiganaji masumbwi.
        2. Tashihisi - kusimama kwa vipapasio vya akili/ moyo ukimwambia.
        3. Mdokezo /sehemu wa methali -yake ya arobaini imefika.
        4. Kutumia usimulizi wa wakati uliopo- mara anasikia..
        5. Nahau/msemo - kumwenda mbio.
        6. Taashira - vipapasio, moyo kumwenda mbio
        7. mdokezo wa kauli - hafifu .....imefika
    2.  
      1. Kuonyesha changamoto zinaz kumba hospitali za umma. Selume anshangaa namna alivyoweza kustahili matatizo kama vile ukosefu wa glavu hospitalini.
      2. Kuangazia swala la ufisadi. Dawa zilizotengewa hospitali zinauzwa na wasimamizi wa hospitali. (uk. 140). Ruzuku kutolewa kwa wasiostahili.
      3. Kuonyesha ukosefu wa uwajibikaji wa wasimamizi wa taasisi za umma. Hospitali haijalipa umeme. (uk. 140)
      4. Kuendeleza ploti - kupitia sadfa. kituo kinakamilika wakati ambao Selume anajiuzulu; anapataka kazi, na mkondo wa matukio kubadilika.
      5. Kuonyesha migogoro inayosababishwa na tamaa ya rasilimali. Mgonjwa analemazwa katika mapigano ya kung'ang'ania ardhi. (uk 141).
      6. Kujenga tabia za wahusika. Kwa mfano,utu wa Ridhaa. anaanzisha kituo cha afya na kuwapa ajira Selume na Kaizari.
      7. Kuonyesha athari za matumizi mabaya ya vileo.mwanafunzi anakufa kutokana na pombe haramu. (uk. 142).
      8. Kuonyesha ukengeushi . Wasomi wanashindwa kukabiliana na  matatizo/changamoto wanatumia mbinu hasi ili kujisahaulisha na hali ya duni.(uk 142).
      9. Kuangazia changamoto zinazokumba sekta ya elimu. Halmashauri ya mikopo kutotosheleza mahitaji ya wanafunzi.
      10. Kuonyesha umuhimu wa mshikamano wa kifamilia katika maisha ya watoto. Kipanga anaingilia matumizi mabaya ya vileo kwa kukataliwa na aliyedhani ndiye babake.
      11. Kuonyesha athari za kufuata mila zinazorudisha nyuma maendeleo ya kijamii. Tuama anakasirika kwa kupashwa tohara.
      12. Kuangazia swala la ukiukaji wa haki za watoto. Mama yake Pete kutoshughulika kutambua kwamba binti yake amekua na mahitaji yake yamebadilika.
      13. Kuonyesha jukumu la jamii katika kuwarithisha vijana mbinuishi. mwanzo mpya inawapa vijana kama vile Kipanga huduma za ushauri nasaha unaosaidia kubadilisha tabia.
      14. Kuangazia uozo wa jamii. Uavyaji mimba - Pete anajaribu kuavya mimba.
        5 × 2
  2.  
    1.  
      1. nahau - kujitanua kifua.
      2. Mdokezo wa methali - mimi ni mwana wa mhunzi na bila shaka wa mhunzi asiposana huvuvia
      3. Chuku - Kuinua tani mia moja/ kufufua maiti
      4. Tashbihi/ ulinganishi - kama yule mbabe wa kivita
      5. Balagha - angeweza kuinua tani ngapi vile za chuma?
      6. Taswira - uoni,kuinua, wakitazama
      7. Mbinu rejeshi - hadithi ya Fumo Liyongo na ile ya Akavi
      8. Nidaa/ usihai - tet! hivi hivi! mia moja!
      9. Udokezaji - anadokeza ushujaa wa Liyongo hatujui ni shujaa wa aina gani.
      10. Ubanaji wa matukio - Tukio linalotokea mara nyingi linasimuliwa tu mara moja.
      11. Urudiaji - Baba, babngu.
      12. Utata - matumizi ya maneno hivi hivi yanaweza kurejelea maana zifuatazo
        1. namna
        2. kimchezo
        3. bila kusumbuka
        4. palepale
        5. wakishangaa  ( mifano lazima)
      13. Kutumia usemi halisi na wa taarifa.
      14. Utohozi - mashine, teni
      15. Usimulizi - maelezo yote
      16. Ishara/uigizaji - Hivi hivi
      17. lakabu - Tet!
      18. Ucheshi - Tet!
      19. Ulinganishi/urejeleaji ( si tofauti na Fumo Liyongo)
        ( Dondoo limetolewa uk.181)
         8 × 1 =8
    2.  
      1. Kuendeleza mshikamano/ ushirikiano wa kifamilia. Mwangeka na Mwangemi wanapendana. Wanashiriki shughuli mbalimbali.
      2. Kuangazia historia yakijamii. Mwangeka anataja vita baina ya jamii yake na Akavi ili kuwaokoa mifungo. Kutajwa kwa mashujaa.
      3. Kuendelea tamaduni kama vile utambaji. Nyanya anawahadithia kina Mwangeka kuhusu Fumo Liyongo.
      4. Usuluhishaji migogoro/ kuendeleza shughuli za usuluhishaji wa migogoro katika jamii. Babu Msubili ni jaji wa kienyeji.
      5. Kudhibiti vitendo vya wanajamii/kupitisha na kuendeleza imani ya kijamii. babu hakupenda kukutana na mwanamke asubuhi. Mama ya msimulizi anawakataza kumpelekea uji asubuhi; anawatuma ndugu wake wakiume.
      6. Kudumisha nidhamu. Mwangeka na Mwangemi wanapomwiga Babu wanachapwa na Babu, kisha wanakatazwa chakula.
      7. Kutoa mwongozo kuhusu namna ya kuishi. Mama Mwangeka na Mama Mwangemi wanakilaani kitendo cha kumwiga babu. Wanawaadhibu zaidi ili kukomesha tabia hii.
      8. Kudumisha mahusiano ya kijamii/kiada zinazoongoza mahusiano ya kifamilia. Mwangeka na Mwangemi wanamwiga Babu ili kumkumbusha kwamba anastahili kuwa mtani wao kama ilivyo desturi ya jamii yao.
      9. Kuendeleza shughuli za kijamii, kwa mfano michezo ya watoto na uigizaji.
      10. Kuendeleza imani kuhusu majukumu ya kijinsia katika jamii. Mwangeka anapobeza kuwepo kwa shujaa wa kike ( Mekatilili - Uk. 179).
        Kuonyesha Imani ya kijamii kwamba shujaa wa kivita sharti awe mwanamume. Babu anamkumbusha Mwangema kuwa wanaume hawalali mapema.
      11. Kuendeleza mbinu ya kijadi za urekebishaji tabia/ufunzaji wa maadili. babu anatumia kichapo, ambacho ndicho njia pekee iliyoaminika kumshinikiza mtoto kutii.
      12. Kuhimiza maridhiano. Mwangeka na Mwangemi wanawapa majogoo wao punje za mahindi pamoja na kuwakumbusha asiyekubali kushindwa sii mshindani. ( uk. 183)
      13. Kukuza uzalendo - Kupenda familia yake/ Kujitolea kulinda furaha yake.
        Hoja 12 × 1 =12 
    1.  
      1. Ni maneno ya Asiya/ Mama-pima 
      2. Anawaambia Wanasagamoyo waliokutana sokoni/ Tunu/ Sudi.
      3. Wako kwenye lango kuu sokoni/jukwaani
      4. Pombe yake imemwagwa; anajutia matendo yake ya awali.
        4 × 1=4
        ( Dondoo limetolewa uk.92)
    2.  
      1. Usambamba - Nilijua ninawaponza
                             nilijua ninawapunja
      2. Tashhisi - Nilimezwa na tamaa.
      3. Takriri/Uradidi Nilijua/Nilijua
      4. Mdokezo - ...
      5. Chuku - Tamaa meza
        2 × 2
    3.  
      1. Ploti
        1. Kupitia kwake tunaelezwa kuhusu usuli wa utoaji wa kandarasi ya✓ uokaji keki; yeye na Ngurumo walimwandama Husda.
        2. Baadhi ya matukio katika maisha ya wahusika✓ fulani yanaangaziwa katika kibanda chake cha pombe. Ngurumo anasema alisoma na Tunu (uk. 57)
          Tunaonyeshwa kuwa Siti alikuwa mlevi hapo awali. ( uk. 58)
        3. Wimbo✓ anaoimba Mamapima ni kipengele cha ploti. Anautumia kuitetea kazi yake. (uk. 60)
        4. Anajenga mgogoro kati ya wanamabadiliko na wanaotaka hali ibakie hivyo. Tunu anasema amekuja kuwakomboa✓ walevi ilhali Mamapima anasema anaharibiwa biashara.
        5. Matukio kwenye biashara yake yanawezesha kujua nani aliyempiga✓ na kumuumiza Tunu. Ngurumo anaashiria miguu ya Tunu iliyoumia - (uk. 63)
        6. Kuonyesha hatima✓ ya mgogoro baina ya viongozi na wanyonge. Anasema wamemgeuka, wameimwaga pombe.
        7. Kuonyesha mstakabali wa Sagamoyo. Anajuta✓, anaomba msamaha; anaonyesha kuibadili nia/ kueleza uaminifu wake kwa Tunu; anataka kuibusu miguu yake Tunu ( uk. 92)       6 × 1 =6
      2. Maudhui
        1. Anaendelea swala la ufisadi✓.
          Anapewa kandarasi ya kuoka keki kwa kuwa yeye ni rafiki ya Husda
        2. Kuonyesha upujufu wa maadili✓. Anahusiana na Ngurumo kimapenzi.
        3. Kuonyesha ukosefu wa uwajibikaji. Anauza pombe haramu huku akijua ni hatari
        4. Anaangamiza kizazi cha vijana✓. Kwa kuwauzia dawa za kulevya ( Mtu i Mtu ii wameathirika na matumizi ya dawa za kulevya ( uk. 62)
        5. Anaonyesha matumizi mabaya ya cheo✓. Anapewa kibali cha kuuza pombe haramu kwa sababu mumewe ni kikaragosi cha watawala.
        6. Anaonyesha haja ya maridhiano✓. Anajutia matendo yake, anaomba msamaha na kumtambua Tunu (anataka kumbusu).
        7. kuangazia mabadiliko✓. anajutia alivyotenda. Anajiunga na wanaotetea mabadiliko.
        8. Anaendeleza maudhui ya tamaa ✓na ubinafsi. Anauza pombe haramu bila kujali athari zake kwa jamii. kumweka Husda kwapani ili anufaike.
          6 × 1 =6
  3.   
    1. Wasomi 
      1. Wanachangia kuendeleza uchumi✓. Hata wanapokosa ajira, wajiajiri. Sudi anachonga vinyago; Ashua anauza mandazi.
      2. Wanapigania haki za wanyonge. Tunu na Sudi wakiwa chuoni walikuwa viongozi wa harakati✓ za kupigania haki.
      3. Wanawazindua Wanasagamoyo kuhusu haja ya kuwa na uongozi unaozingatia misingi ya kidemokrasia. Tunu na Sudi wanawahamasisha Wanasagamoyo kuhusu haki zao.
      4. Wanaukosoa uongozi. Tunu anamkabili Majoka na kumwambia kwamba Wanasagamoyo wana haki ya kuishi.(uk. 45).
      5. Wanahimiza haja ya kuzingatia maadili ya kijamii. Ashua anaheshimu asasi ya ndoa. Anakataa ushawishi wa Majoka.
      6. Wanachangia kuboresha hali ya utendakazi katika taaluma zao. Walimu wagoma ili kupata mazingira mazuri ya kufanyia kazi.
      7. Wanatoa kielelezo cha uongozi ufaao. Tunu anasema kwamba wanahitaji viongozi wanaofahamu matatizo yao.
      8. Wanafunza kuhusu umuhimu wa familia na malezi. Sudi anamwambia Ashua awafikirie watoto wao. (uk. 48)
      9. Wanaunda na kuimarisha itikadi za kijinsia zinazowawezesha kuleta mabadiliko katika jamii. Licha ya Sudi na Tunu kushukiwa kuwa wapenzi, hawalegezi juhudi zao za kuuhamasisha umma. Sudi anachonga kinyago cha mwanamke.
      10. Kuwakosoa wanyonge ambao wanatumiwa kama vibaraka. Tunu anamuuliza Ngurumo kipi muhimu; dhifa au kufunguliwa kwa soko. Sudi anawatanabahisha kina Boza kuhusu swala la majitaka.
      11. Baadhi yao wanaendeleza ubaguzi wa kijinsia. Ngurumo anasema hawezi kumpa mwanamke kura.
      12. Wanasisitiza umuhimu wa elimu na ustaarabu. Ashua anasema kutoelimika kuna tatizo (uk. 28), naye Husda anasema elimu bila ustaarabu haifai.
      13. Baadhi wanakwamiza juhudi za kupigania haki. Ngurumo anatumiwa na Majoka kumpiga na kumnyamazisha Tunu.
      14. Daktari anatoa huduma za matibabu kuboresha afya za Wanasagamoyo.
        5 × 2
    2.  Majoka na Daktari
      1. Kuendeleza mgogoro wa kinafsia✓. Majoka anasema kuna kilio kikubwa ndani kwa ndani. (uk. 73)
      2. Kuchimuza✓ matukio ya awali; kwa mfano kuuawa kwa Jabali (uk. 73)
      3. Kudokeza hatari✓ iliyomngojea Majoka - mikono yangu imefungwa kwa minyororo (uk. 73)
        Majoka kusema yuko katika safari ya jongomeo
      4. Kuonyesha udhaifu✓ wa uongozi wa Sagamoyo.Majoka anamuuliza Daktari/ Babu kama ndiye rubani wa ombwe hilo. ( uk. 74)
      5. Kujenga sifa✓ za mhusika. Tunasawiriwa tamaa ya Husda inayomfanya kusaha kwenye ndoa ya mateso/ uchungu na furaha/ Majoka ni mwenye taasubi/anaishi na mke huyo
      6. Yaangazia usaliti✓ katika ndoa. Majoka anakiri kuwa anampenda Ashua; hampendi mkewe Husda.
      7. Kuonyesha nafasi ya mwanamke✓ katika jamii; Wanasawiriwa kama wasioweza kutegemewa. Majoka anasema hawashikiki.
      8. Kuonyesha ukosefu wa uwajibikaji wa uongozi✓. Majoka anasema hajashika usukani (uk. 80)
      9. Kuonyesha kuwa Wanasagamoyo wamezinduka. Majoka anasema wanaililia✓ damu yake ( uk.79)
      10. Kuonyesha kwamba Sagamoyo haipigi hatua kimaendeleo✓. ( uk. 81) Chombo kinakwenda kinyume.
      11. Kuonyesha swala la mgongano✓ kati ya utawala wa Babu na ule wa Majoka. Majoka anasema kwamba athari ya chombo cha Babu/kinatikisa chake ( cha Majoka) na kukifanya kutaka kuubadilisha mkondo.
      12. Kumtanabahisa/kumsuta✓ Majoka kuhusu uongozi wake, na kumwonyesha haja ya kubadilika. Babu anasema: Huoni kisima kimeingiwa paka na maji hayanyweki tena?
        5 × 2
  4.  
    1.  
      1. Akipanda harudi chini.
      2. Hawezi kuporomoka/kuanguka.
      3. Amepata mbinu za kuendelea kupanda(ameotesha makwezi)
      4. Makao/mahali pake ni pale juu/mamlakani.
      5. Kushuka kwake si halali/ni haramu.
      6. huhukumiwa ila hubaki huko juu.
      7. Haoni hatari wala wasiwasi.
      8. Amejishikiza penye manufaa.
      9. Amepanga mikakati ya kujipatia pato.
      10. Hata mti ukiporomoka, hashuki.
      11. Akatalia juu hata akipigwa na radi.
      12. Hashuki kwa hiari.
      13. Daima yu furahani.
      14. Hapati shida
        6 × 1
    2.  
      1. Taswira hisi - ukweli jua mchungu/yu furahani.
      2. Taswira uoni - utabaki kutazama.
      3. Taswira mguso - kagandama.
      4. Mwendo - mpanda juu/ ngazi
        4 × 1
    3.  
      1.  Urudiaji silabi/ ngu, ngu, ngu( ubeti 1)
      2. Urudiaji wa neno- tangu, tangu amepanda akapanda.
      3. Urudiaji wa kipande - mpanda ngazi jamani.
      4. Urudiaji wa sauti o u a e
      5. Urudiaji wa mstari/mshororo - mpanda ngazi kushuka
        3 × 1
    4.  
      1. Kufinyanga sarufi/ kubananga lugha - hili mja ubaini - ubaini hili mja, mengi mazao - mazao mengi.
      2. Inkisari - ngawiraye - ngawira yake/ walo -walio/ badani
      3. Tabdila - gazi, atahapa
      4. Mazida - kuija,hamumu
        2 ×1
    5.  
      1. Tanakuzi - mpanda - hushuka, juu- ardhini.
      2. Chuku - mpanda ngazi kubakia pale miaka na dahari/ kushuka chini kuwa haramu.
      3. Sitiari - mapanda ngazi - kiongozi anayepata mamlaka/ kilele kwenye mamlaka/ ufanisi.
    6.  
      1. Mistari/mishororo minne katika ubeti.
      2. Vipande viwili katika mishororo.
      3. Vina vinabadilika kulingana na ubeti.
      4. Mizani 8, u =16 katika mshororo.
      5. Kipande cha mwisho cha ubeti kuanzia ubeti unaofuata.
      6. Zina kimalizio.
      7. Kipande (Ku) kinafanana kwanza.
        2 × 1 
  5.  
    1.  
      1. Alikuwa na uwezo wa kutenda mambo akiwa kijana, sasa hana.
      2. Alikuwa na afya, sasa hana. 
      3. Alikuwa na ushirika wa ndugu na jamaa; sasa hana.
      4. Anachoshika si chake - sasa hamiliki lolote.
      5. Amepoteza baadhi ya viungo alivyokuwa navyo. Sasa hana meno
      6. Vitamu ni vichungu kwake.
      7. Hana la kumfurahisha kama awali.
      8. Vilivyokuwa laini ni vigumu.
    2.  
      1. Shairi lina beti tatu.
      2. Kila beti una mishororo saba.
      3. Kila mshororo una vipande viwili.
      4. Vina vya ndani na vya nje vinatofautiana.
      5. Mizani 8, 8 =16 katika kila mshororo isipokwa mstari wa 3 ubeti wa 1
      6. Kila ubeti unaanza kwa kauli; u wapi ujana wangu
      7. Kila ubeti unajitosheleza/ ujumbe/ kimaudhui.
      8. Kipande cha kwanza kinatoa wazo na cha pili kinakamilisha.
      9. Shairi limetumia mistari kifu/toshelezi.
      10. Kila ubeti kuanza kwa swali la balagha. 
      11. Mshororo wa mwisho haujamalizwa/ kituo/ kiishio/ kina.
        4 × 1
    3.  
      1. Taswira hisi - machungu.
      2.  Taswira uoni -  Tazama hii dunia.
      3. Taswira mguso - laini, gumu, nikishikacho si changu
      4. Taswira muonjo - kitamu, kichungu.
      5. Taswira mwendo - nayo imeshika njia.
        4 × 1
    4.  
      1. Kweli kizani - kitamu sasa kichungu/laini sasa ngumu.
      2. Tashhisi- afya imeshika njia
      3. Tasfida - wamehama ulimwengu
      4. Usambamba- afya ya ujana wangu
                            siku ya ujana wangu.
        4 × 1
    5. Nafsineni - mzee/mtu aliyekonga  ( 1 × 1)
    6. Toni ya majuto/machungu/kukata tamaa/kutamauka - U wapi ujana wangu?     1 × 2
  6.  
    1.  
      1. Inaonyesha mwisho wa urafiki baina ya Sungura na Fisi -huo ukawa mwisho wa urafiki wa Sungura na Fisi. 1 × 2
    2.  
      1. Fanani kuzungumza moja kwa moja na hadhira -mjukuu wangu..
      2. Matumizi ya chuku - mtu kujikwaa na mwingine kuwa ndiye anayehisi uchungu.
        Kuhitaji kutwa kujaza tumbo.
      3. Tashihisi- Moyo wa fisi unamrai.
      4. Methali- atanguliaye kisimani hunywa maji maenge/jikune ujipatapo.
      5. Nahau - alishika tariki
      6. Urudiaji/takriri/uradidi -guu mosi, guu pili
      7. Ritifaa- Sungura anazungumza na Fisi na ilhali Fisi hayupo.
      8. Tasfida- uwezo wa kuyatosheleza maumbile haja - badala ya - kwenda haja kubwa.
      9. Kuigiza - alijikokota hivi...
      10. Swali la balagha - Itakuwaje ...?
                                - Utaacha lini...?
      11. Ucheshi - kicheko cha Sungura.
      12. Tanakali za sauti ndo ndo ndo!
      13. Taswira - Fisi akilia/Akishona
      14. Mtambaji kuhoji hali/ upenyezi wa mtambaji - sijui kama mjukuu wangu...
      15. Kuchanganya sauti ya usimulizi baina ya nafsi ya tatu hadi ya pili kupunguza masafa ujumi kati ya fanani na hadhira.
      16. Kuchanganya nyakati ( uliopita na sasa) ili kupunguza masafa ujumi.
      17. Kinaya - Mtu kujikwaa na mwingine ndiye anahisi uchungu
      18. Stihizahi/ kejeli/dhihaka - Sungura akicheka.
      19. Msemo- Kataa katakata
      20. Nidaa/Usihai -Lo! Kiumbe huyu!
      21. Uzungumzi nafsia - utaacha lini tabia hii ya usaliti
      22. Tashbihi - alijikokota mithili ya ng'ombe...
      23. Usimulizi - Ndugu wewe unajua...
      24. Taharuki - Hali ya kutaka kujua kitakachomtokea.
      25. Dayalojia - Kati ya Sungura na Fisi
    3.  
      1. Kuashiria mwisho wa usimulizi.
      2. Kuiondoa hadhira kwenye ulimwengu wa fantasia hadi ulimwengu halisi.
      3. Kuwapa kitulizo wasikilizaji/ kuwaondolea watu mwemeo wa matukio ya hadithini.
      4. Kuonyesha mwisho wa mgogoro wa hadithini – unaashiria mwisho wa urafiki wa fisi na sungura.
      5. Kusawiri jamii ya fanani- ni wafugaji- anazungumza kuhusu ng’ombe.
      6. Kuchochea wengine ili waweze kutamba hadithi.
      7. Kusawiri mandhari ya jamii ya fanani.
      8. Kuonyesha funzo la hadithi.
      9. Kujua hatima ya tama ya fisi.
      10. Kupisha shugli inayofuata.
      11. Kupisha mtambaji anayefuata.
      12. Kujenga taharuki.
        3 × 1
    4.  
      1. Kushiriki kwa kupiga makofi.
      2. Kushiriki kwa kuimba nyimbo.
      3. Kuigiza baadhi ya matukio/ matendo ya wahusika/ kuhusisha utambaji.
      4. Kuuliza maswali.
      5. Kutoa mifano.
      6. Hisia /ishara wanazoonyesha usoni huweza kumfanya abadilishe uwasilishaji.
      7. Kutoa – majibu kwa methali na vitendawili iwapo ngano itamalizikia kwa mtambaji kuwategea vitendawili.
      8. Kutoa mifano ya baadhi ya wahusika wa hadithini kutoka jamii zao iwapo wataulizwa.
      9. Wanaweza kuchukua nafasi ya kuitamba upya ngano hiyo.
      10. Kutoa funzo katika hadithi.
      11. Kudikia.
      12. Kucheka/ kulia.
      13. Kujibu maswali.
      14. Kunyamaza na kusikiliza kwa makini ili...
Join our whatsapp group for latest updates

Download Kiswahili Paper 3 Questions and Answers - KCSE 2020 Past Papers.


Tap Here to Download for 50/-




Why download?

  • ✔ To read offline at any time.
  • ✔ To Print at your convenience
  • ✔ Share Easily with Friends / Students


Get on WhatsApp Download as PDF
.
Subscribe now

access all the content at an affordable rate
or
Buy any individual paper or notes as a pdf via MPESA
and get it sent to you via WhatsApp

 

What does our community say about us?

Join our community on:

  • easyelimu app
  • Telegram
  • facebook page
  • twitter page
  • Pinterest