Kila Mchezea Wembe summary notes - Mwongozo wa Mapamazuko ya Machweo na Hadithi Nyingine

Share via Whatsapp


Kila Mchezea Wembe- Pauline Kea Kyovi

Mtiririko

Hadithi ni barua kutoka Hospitali ya Uhai ni Neema inayoandikiwa Emmi na mpenziwe, Tembo.

Nia kuu ni kuomba msamaha huku akimweleza mwenziwe yaliyomsibu, akikiri makosa yake.

Bado yuko kitandani, japo ameimarika kidogo. Anaweza kusema kwa kulazimisha na chakula kinapita kooni, ila hajadiriki kuona.

Maisha humo ni mazito upande mmoja na mepesi upande mwingine.

Ni mazito kutokana na upweke na kejeli za wanaopita huko, ambao wanasema watafariki tu kama hao wengine.

Ni mepesi kutokana na marafiki wa hospitalini kama muuguzi Nasir, anayemhudumia kwa utu, na Bwana Salim, mwathiriwa mwenzake anayempa tumaini kila uchao.

Hata ndiye anamtia shime na kumsaidia kuandika barua.

Salim ameimarika haraka, anafikiri sababu ya mapenzi kutoka kwa aila yake ambao wanamiminika kumwona.

Yeye(Tembo) amevunja muamala na watu sababu ya ulevi, hata wazazi wake.

Kaka na dada pia wanamtema baada ya kuleta vurugu katika mazishi ya mpwake.

Anatamani angeweza kusema siku ya mwisho ya Emmi kumtembelea, na anakumbuka malalamishi yake aliyosikia kwa mbali.

Anashangaa kwa nini hakubadili mienendo, kuacha pombe, tamaa na anasa licha ya kumwonya, kuitelekeza familia, kutowapa heshima licha ya kuonywa na majirani.

Anamwona alivyojiponza, huku akimwomba talaka.

Hata yuko radhi kuwalea wana. Tembo alisikia hayo tu, akatamani amwombe radhi lakini bila mafanikio.

Anamwomba akivumilie kisa chake wanavyovumilia Salim, anayekiandika, na Mwanaheri, shemejiye ambaye ako tayari kupeleka barua hiyo kwa Emmi. 

Siku ya maangamizi, aliamshwa saa nne na mkewe kuamsha kinywa.

Baada ya kumaliza kiamsha kinywa saa sita, aliondoka bila kuaga mkewe, aliyekuwa jikoni akichoma mahamri.

Alielekea mtindini, akapata walevi wamejaa japo mazingira ni mabovu.

Walikunywa kwa kikoa.

Ghafla, Moshi akaanguka na kuanza kufafaruka.

Kila mtu akatoroka.

Alipata taarifa Moshi alifia hapo hapo, na mama pima yu korokoroni. 

Licha ya kujua pombe ya mama pima ni haramu, waliinywa sumu hiyo kwa hiari.

Pombe hiyo ndiyo imempofusha na labda kumfanya hanithi.

Uchunguzi umedhihirisha ilitiwa dawa ya kuhifadhia maiti.

Mapipa hayo pia yalipatikana vitu kama panya wa kuoza, nyoka wafu, sodo na nguo za ndani. 

Tembo na wengine walielekea kuzima kiu kwingine.

Waliburudika kwa pombe ya watu wa kima cha chini na kuingia jukwaani.

Msichana aliyejiremba alimjia Tembo na kumrai wacheze naye akakubali. 

Aligutushwa na sauti nyembamba ikimwamsha huku akitikiswatikiswa.

Akajipata na mwanamke aliyezeeka, mwenye sura ya kutisha.

Hakuwa na mguu mmoja, tena kichwani kulikuwa vinyoya vyeupe vya kuhesabu.

Walikuwa kwenye chumba cha udongo kilichoezekwa kwa mabati machakavu yenye matundu.

Aliwaza jinsi ya kujiopoa lakini hakuwa na namna.

Akasaili sababu yake kuwa hapo.

Angeelika, au Anji kama alivyojiita akamwambia walikuja pamoja baada ya dance, tena yuko kwenye safe hands. 

Alidai malipo kwa Tembo kwa ajili ya huduma aliyompa.

Aligundua amejifunga kanga.

Akaendea suruali yake iliyoanikwa kwenye kamba, akatoa pochi, lakini halikuwa chochote.

Akaunti ya simu pia haikuwa na kitu.

Akachimbua kwenye soksi na kumtolea Anji salio la mshahara wake na kumpa.

Aliondoka na kutembea kwa miguu hadi nyumbani.

Baada ya kufika nyumbani, mkewe alimwamkua na kumwandalia kiamsha kinywa.

Anatamani mkewe angemwuliza atokako wasawazishe mambo.

Kwa kuhofia matokeo, aliamua kunyamaza.

Anaamini unyende wa mkewe baada yake kuvua mavazi na kulala ndio ulimwokoa.

Alipousikia, alijaribu kuinuka lakini akakosa nguvu.

Emmi akaja ameshika nguo zake, alama za midomo Tembo hajui zilifikaje hapo.

Mkewe aligundua hali yake ilihitaji dharura ya matibabu. Anamshukuru kwa kujasirika kuokoa maisha yake.

Sasa anamhitaji ili kuwa mfano kwa wanaochezea pombe.

Anapojitambua, anataka kujitoa uhai lakini kisa cha Salim cha mhudumu na mkufu kinamghairishia nia.

Tembo amejifunza mengi. Amejua ukatili wa dunia na jinsi inaweza kumtenda mtu.

Hana hanani. Anamwachia mkewe shamba lake.

Hajui iwapo mkewe hajatwaliwa na maharamia.

Licha ya hali yake, anaamini ana thamani mbele ya wampendao wala hatakata tamaa.

Anamwomba Emmi amsaidie, yuko radhi kubadilisha tabia.

Anamwomba mkewe asalimie ndugu na watoto wao, na akiweza awalete awaone, afarijike. Anamalizia kwa kutaja anampenda.  

Ufaafu wa Anwani ‘Kila Mchezea Wembe’  

Ni ufupisho wa msemo ulio kwenye leso ya Bikizee kuwa ‘Kila mchezea wembe hujikata vyanda vyake’.

Ina maana kwamba yeyote ambaye anachezea hatari huathirika kutokana na hatari hiyo. 

Msimulizi yuko hospitalini, hata uwezo wa kuandika hana. Salim ndiye anamsaidia kuandika.

Hana uwezo wa kuona.

Bado mipira mikononi inatona maji japo ya pua ametolewa.

Hana uwezo wa kuona.

Hizi ni ishara za kujikata vyanda baada ya kuchezea wembe kwa kunywa pombe haramu.

Salim pia ni mwathirika mwenzake. 

Tembo anakumbuka wimbo wa watribu, ambao unasema kuwa janga la kujitakia halifanyiwi matanga.

Ni muhimu kutia makini ili kuepuka vitimbi vya dunia.

Maisha yanaweza kukupa fahari sasa, kesho yakakutema.

Wimbo huu unaonya dhidi ya ‘kuchezea wembe’. 

 Tembo pia anachezea wembe kwa kutowaheshimu wanafamilia yake.

Hana ukuruba na wazazi wake.

Dada na kaka zake pia wanamtema anapozusha vurugu kwenye mazishi ya mpwa wake.

Hali hii inamfanya kukosa watu wengi wa kumtembelea.

Anaona kwamba Salim anaimarika vyema kwa kutembelewa na watu wengi wa familia wanaompa tumaini.

Tembo anahisi anastahili pigo hili.

 Tembo anakumbuka malalamishi ya mkewe anapokuja kumwona.

Analalamikia tabia za mumewe ambaye anajitia bingwa wa ulevi, tamaa na anasa, hali ambayo inamletea madhara.

Hata anataka ampe talaka aweze kupumzika.

Yuko katika hatari ya kumpoteza mkewe kwa ‘kuchezea wembe’. 

Moshi anachezea wembe pia kwa kubugia pombe haramu.

Anaanza kufafaruka akiwa huko na hatimaye anaaga hapo hapo.

Mama pima anachezeawembe kwa kushiriki biashara haramu ya kuuza pombe.

Imetiwa dawa ya kuhifadhia maiti na inaleta madhara. Hatimaye anaishia korokoroni. 

Tembo anachezea wembe kwa kukubali kucheza densi na msichana kwenye baa.

Anapogutuka, anajipata chumbani mwake Bikizee wa kutisha, kanga kiunoni.

Analazimika kumpa salio la mshahara wake na kwenda nyumbani kwa miguu.

Emmi pia anachezea wembe kwa kuolewa na mlevi chkari.

Anapitia mengi mikononi mwake.

Analazimika kuwalea watoto peke yake na kumhudumia Tembo anayelewa kila mara na kuwatelekeza.  

Dhamira ya Mwandishi

Kutoa onyo kwa wapiga maji haramu kuhusu madhara yanayoweza kuwakuta.

Anadhihirisha matatizo ya ndoa na malezi yanayosababishwa na ulevi.

Anasawiri umuhimu na nafasi ya matibabu katika kuendeleza uhai kwenye jamii.

Anadhamiria kutoa tumaini kwa walio katika hali tata za kiafya na kijamii kuwa si mwisho wa maisha.

Kudhihirisha umuhimu wa uhusiano/ukuruba mwema na watu wengine, hasa familia.Kuonya kuhusiana na biashara haramu ambayo inaweza kumwangusha mhusika mikononi mwa sheria.

Anadhihirisha nafasi ya mapenzi na ndoa kama asili ya tumaini kwa wahusika. 

Anadhihirisha umuhimu wa kufaana hasa wakati wa dhiki.  

Maudhui

Migogoro

Nia kuu ya Tembo ni kumwomba msamaha mkewe kwa migogoro yao ya awali.

Anakumbuka malalamishi yake mara ya mwisho anapokuja kumwona.

Analalamikia tabia yake ya kupotea kila mara, tena hafanyi lolote kwa ajili ya familia yake.

Hata anamwomba ampe talaka, yuko tayari kuwatunza watoto, kwani amezoea tayari.

Tembo anatamani angepata uwezo wa kumwomba radhi wakati huo.Anakumbuka siku ya maangamizi.

Mkewe anamwamsha mwendo wa saa nne ilia apate staftahi. Anamaliza kuamsha kinywa saa sita.

Anaambiwa mkewe anachoma mahamri jikoni lakini anaondoka bila kuaga. Anahofia kujibu maswali kuhusu wapi aendapo. 

Walijipata tena kwenye mgogoro baada yake kurudi nyumbani siku iliyofuata.

Mkewe anamwandalia chamcha, naye anavua mavazi na kujitupa kitandani.

Anasikia ukemi wa mkewe, huku ameshika nguo zake zenye alama za rangi ya midomo.

Anajua ana maswali ya kujibu lakini hali yake hairuhusu.

Mkewe anamshughulikia kupata matibabu. 

Tembo pia anajikuta kwenye mgogoro na Angelica kwenye chumba chake anapogutuka.

Hajui kafikaje humo, tena Bikizee huyu anatakaje. Anatamani kutoroka lakini hana namna.

Anji anadai malipo kwa huduma zake.

Analazimika kuzoa salio la mshahara wake kwenye soksi na kumpa ili kujiopoa.

Anji anasema atampeza lakini Tembo hanuii kuwahi kuonana naye tena.

Analazimika kutembea hadi nyumbani, mwendo wa saa nzima. 

Emmi anapomtembelea pia, analalamikia migogoro ya mumewe.

Anapolewa anarudi nyumbani na maudhi, matusi na vipigo tu.

Analalamika kuwa hawaheshimu yeye na watoto wake, wazazi wala wakwe, na hata majirani.

Tembo pia ana mgogoro na familia yake. Hana ukuruba na wazazi wake.

Dada na kaka zake wanamtema anapozua vurugu kwenye maziara wakati wa mazishi ya mpwa wake.

Hivi, hapati watu wa kumtembelea hospitalini kama rafikiye Salim.Starehe na Anasa. 

Emmi anashangazwa na tabia ya Tembo ya kujistarehesha kwa anasa za pombe.

Anamkumbusha kuwa anasa za dunia hii hawezi kuzimaliza.

Anajitia bingwa wa dunia na kusahau alikotoka, hali ambayo inamletea madhara na kumlaza hospitalini.

Siku ya kisanga kikuu, Tembo anaamshwa na mkewe kunywa staftahi.

Anapomalizia saa sita, anamhepa mkewe na kuelekea kujistarehesha mtindini.

Anawapata wenzake huko na wanakunywa kwa kikoa.

Kila mmoja ana zamu ya kununua pombe.

Hata baada ya kituko cha Moshi, bado Tembo na wenzake wanaelekea kuzima kiu kwingine.

Wanakunywa pombe ya kima cha chini wanayoweza kununua.

Baadaye wanaingia jukwaani kusakata densi.   

Tamaa ya anasa inamfanya kukubali rai ya msichana anayetaka kucheza naye, lakini anamgeuka baadaye.

Kumbe ni Bi. Kizee aliyejipodoa.

Anajipata mikononi mwake, ambapo anajinasua kwa kulipa salio la mshahara wake kwa ajili ya huduma alizopewa.

Mapenzi na Ndoa.

Ndoa kuu katika hadithi hii ni kati ya Tembo na Emmi.

Inakumbwa na misukosuko kadha wa kadha.

Wamejaliwa wana ambao hata Tembo hajui wanakula nini.

Amewatelekeza kabisa.

Mkewe hata anamwomba ampe talaka, yuko tayari kuwalea watoto wao pekee yake. 

Tembo anaamshwa na mkewe asubuhi ya saa nne ili kupata kiamsha kinywa.

Anapomaliza saa sita, anaondoka bila kumuaga, akihofia kuulizwa maswali kuhusu kule anakokwenda.

Hana mapenzi ya dhati kwa mkewe wala hamjali.

Tembo anaporudi nyumbani kutoka kwenye mtindi, anavua nguo na kulala.

Anagutushwa na ukemi wa mkewe. Amebeba nguo zake zenye alama za midomo.

Kabla ya kumsaili, anagundua anahitaji dharura ya matibabu na hapo anamshughulikia mara moja.

Tembo anamshukuru kwa hilo. 

Dhamira kuu ya barua hii ni Tembo kumwomba msamaha mkewe.

Anamwachia shamba lake lenye rutuba.

Anahofia huenda amenyakuliwa na maharamia.

Anahisi kwamba ndiye tu amebaki, akimwomba arejee kwake ili kumpa tumaini.

Anamtaka kuwasalimia nduguze na wanawe, na hata awalete apate kuwaona afarijike.

Anatamatisha kwa kusema anampenda.Ulevi Tembo amezama katika ulevi na ndio unamletea madhara yote aliyo nayo.

Hana uwezo wa kuona.

Yuko hospitalini hali hoi.

Salim pia yuko hospitali hiyo hiyo, ni mwathiriwa mwenzake. 

Anapoamshwa na mkewe, Tembo anakunywa staftahi hadi saa sita kisha kuondoka bila kumuaga mkewe anayechoma mahamri jikoni.

Anahofia maswali ya wapi anaenda kwani anajua anaelekea kwenya anasa za ulevi.

Anapofika huko anawapata wenzake wanaokunywa kwa kikoa, kila mmoja akichangia zamu yake.

Mazingira wanapolewa yanatia kinyaa lakini kwao si hoja. 

Pombe inasababisha mauti ya Moshi.

Wakiendelea kunywa, anaanguka ghafla na kuanza kurusharusha miguu na kugaragara chini huku povu likimtoka.

Hatimaye anafariki hapo hapo.

Inagunduliwa kuwa pombe waliyokunywa ilitiwa dawa ya kuhifadhia maiti, tena ilikuwa na maajabu kama panya wa kuoza, nyoka wafu, sodo na nguo za ndani.

Tembo anakiri kwamba pombe hiyo, ambayo inapatiwa majina kama chang’aa, tear gas, moshi na mengine ni sumu, ambayo wanatoa pesa zao kuinunua, tena kwa hiari yao.

Hana huruma kwa mama pima aliyetupwa korokoroni.

Anaiona kuwa stahiki yake. Licha ya kisanga cha Moshi, bado kiu ya pombe haiwaruhusu kupata hofu.

Tembo anaandamana na wenzake kuzima kiu yao kwingine.

Huko, wanalewa na kuanza kucheza densi.

Anaanguka mtegoni wa Angelica, ambaye anamfyonza salio lake la mshahara kwa huduma za chumbani.

Kutokana na ulevi, hata hagundui kwamba nguo zake zina alama ya midomo, wala hajui zilifikaje huko.

Anapomsikia mkewe akipiga ukwenzi, ndio kwanza anagundua, na anajua ana maswali ya kujibu.

Hata hivyo, mkewe anagundua anahitaji dharura ya matibabu na kumsshughulikia.

Haoni, magoti hayana nguvu, mishipa ya damu nayo inazizima.

Tembo anasema waliolala bila kuamshwa hawajaamka hadi leo, wengi wamefukiwa. 

Majuto

Tembo anapoandika barua hii, yuko katika hali ya majuto makuu.

Anakiri kwamba yeye ni mkosa na yuko tayari kuomba radhi, wala hana la kujitetea.

Hajabanduka kitandani, hana uwezo wa kuona, bado anapigania uhai wake.

Anayahisi maisha kuwa mazito kwa kukosa imani kwa watu wanaopita huko na kudai kuwa watajifia kama wenzao tu.

Anajuta pia kwa kukosa uhusiano mzuri na familia yake.

Hapatani na mama wala baba yake, kutokana na utepetevu wake anapochapa mtindi.

Kaka na dada zake pia wanamtema anapozua vurugu kwenye maziara wakati wa mazishi ya mpwa wake.

Anaona aibu anapokumbuka haya.

Anahisi alistahili pigo hili. 

Anajutia ulevi wake.

Anamwambia Emmi kwamba alikunywa sumu.

Ndilo jina analoweza kuita pombe hiyo haramu.

Licha ya kufahamu ni haramu, bado wananunua na kuinywa pombe hiyo, tena kwa hiari yao.

Ndiyo inamwangusha katika hali aliyo.

Anajuta pia anapojipata kwenye chumba cha Angelica.

Hajui alivyofika hapo, kwani alikuwa amelewa kabisa.

Anatamani kutoroka lakini hawezi.

Anajiokoa kwa kumpa salio la mshahara wake aliohifadhi kwenye soksi.

Analazimika kurudi nyumbani kwa miguu. 

Anajutia kufumbiwa kinywa na mke wake anapofika nyumbani.

Anahisi kwamba ingekuwa afadhali kama angempa kisa hiki wakati huo, labda wangeweza kusawazisha mambo.

Kwa kuhofia hatima yake, yeye alihiari kufumba kinywa.

Ulaghai

Mamapima anawalaghai wanywaji wa pombe yake.

Anawaandalia pombe na kuitia dawa ya kuhifadhia maiti.

Haijatajwa kwa nia gani.

Pia kunapatikana kwenye mapipa yake panya wa kuoza, nyoka wafu, sodo na suruali za ndani.

Inasababisha kifo cha Moshi na wengine na kumpofusha tembo. 

Angelica pia anamlaghai Tembo.

Anamwomba wacheze densi lakini baadaye, Tembo anagutuka kwenye makazi yake, huku amefungwa kanga kiunoni.

Pochi lake halina hata ndururu. Analazimika kumlipa Anji kwa salio la mshahara wake alilohifadhi kwenye soksi.

Pia, anaingia jukwaani huku amejiremba vilivyo ili kuficha sura yake ya kutisha.

Maudhui mengine ni kama vile Ufuska, Sheria, Uwajibikaji, Usaliti na Mauti/Kifo.  

Wahusika: Sifa na Umuhimu.

Tembo 

Ni mlevi.

Anaelekea kwenye mtindi kila mara na kumpuuza mkewe na wanawe.

Ulevi ndio hatimaye unamlaza hospitalini na kumpofusha.

Hata anahofia umempoka ujogoo wake.

Ni mgomvi.

Anapolewa, anagombana na kila mtu na kuvuruga mahusiano yake na watu.

Wazazi wake washamtema kitambo.

Dada na kaka zake walimtema baada ya kuzua vurugu kwenye mazishi ya mpwa wake.

Anagombana pia na mkewe na majirani. 

Ni mvivu.

Siku ya maangamizi, mkewe anaelekea kumwamsha kwa ajili ya kiamsha kinywa mwendo wa saa nne.

Anamaliza kuamsha kinywa mwendo wa saa sita mchana.

Ni asiyewajibika.

Anawatelekeza mkewe na wanawe wala hata hajui walacho.

Mkewe anapomtembelea hospitali, anashangaa vipi anajidai kuwa na watoto hali hajui walacho.

Hawajibikii matendo yake, jambo linalomletea mikasa.

Ni mwenye majuto.

Anajutia matendo yake ya awali, ambayo yanamwathiri pakubwa.

Anajutia uhusiano wake mbaya na familia yake, anajutia madhila yake kwa mkewe na kumwomba msamaha.

Ni mpenda anasa.

Anapoamshwa na mkewe na kupata kiamsha kinywa, anaondoka kwenda kuvinjari kwenye mtindi.

Anamhepa mkewe kuepuka maswali.

Hata baada ya kisanga cha Moshi, bado wanaelekea mahali pengine kukata kiu.

Wanalewa na kuingia ukumbini kusakata densi. 

Umuhimu wa Tembo. 

Kupitia kwake, madhara ya ulevi yanadhihirika.

Ni kiwakilishi cha wanaume wanaopuuza familia zao na kujizika katika ulevi na anasa.

Ni kielezo cha watu wanaokiri makosa yao na kuomba msamaha wanapokosa.

Kupitia kwake, nafasi na umuhimu wa ndoa katika jamii unadhihirika.

Kupitia kwake, nafasi ya matibabu katika kusaidia wanajamii inadhihirika.

Emmi

Ni mvumilivu.

Anavumilia vituko vingi vya mumewe bila lalamalalama.

Kila mara, mumewe ni mlevi kupindukia wala hawajali.

Analazimika kutunza watoto wao peke yake lakini anavumilia.

 Ni mwajibikaji.

Anatekeleza wajibu wake.

Siku ya maangamizi, Tembo anakumbuka ndiye alimwamsha, tayari kamwandalia kiamsha kinywa.

Akiondoka, Emmi alikuwa jikoni akichoma mahamri.

Ndiye analea watoto mumewe anapozama kwenye pombe.

Anapogundua hali ya mumewe, anamshughulikia kwa dharura.

Ni mwenye utu.

Licha ya matendo yote ya mumewe, bado anamshughulikia kama mkewe.

Anamlisha na kumtafutia matibabu na hata anapokuwa hospitalini, anakuja kumtembelea. 

Ni mlezi mwema.

Anasema kuwa mumewe hata hajui walacho au kuvaa wana anaowaita wake.

Yeye amewalea kwa kila hali, na hata yuko tayari kuwalea iwapo atampa talaka.

Ni mwenye mapenzi ya dhati.

Anampenda mumewe licha ya kuwa mlevi.

Anamshughulikia kila anapohitajika kufanya hivyo.

Anamtembelea hospitalini hali yake ikiwa taabani.

Umuhimu wa Emmi

Kupitia kwake, matatizo ya ndoa yanadhihirika.

Ni kielelezo cha wanawake walezi wema wanaojali wanao waume zao wanapozamia ulevi.

Ni kiwakilishi cha nafasi ya mwanamke katika jamii. 

Ni kielelezo cha uvumilivu katika maisha licha ya magumu mengi.

Ni kiwakilishi cha migogoro katika jamii.

Salim

Ni mshauri.

Anamsimulia Tembo kisa cha waumini na mkufu, ambacho kinampa tumaini jipya katika maisha.

Anamwambia kuwa hali yake sio mwisho wa maisha na kumwonyesha sababu ya kutokata tamaa.

Ni mwenye utu.

Anamsaidia Tembo kila anapohitajika.

Hata barua ya kumpa mkewe, ndiye anamwandikia kwani yeye ameshapofuka.

Ni mfadhili.

Anamsaidia Tembo kila mara anapohitaji msaada wake.

Anamsaidia kwa ushauri na pia kuandika barua.

Ni mlevi.

Tembo anaeleza kuwa Salim ni mwathiriwa mwenzake.

Hata yeye alidhurika kutokana na pombe haramu.

Ni mwenye imani.

Licha ya yote yaliyowakumba, bado anayaona maisha kwa mtazamo mzuri.

Anaamini kuwa si mwisho wa maisha, imani ambayo anamjaza mwenzake, Tembo.

Umuhimu wa Salim

Ni kielelzo cha tumaini na imani katika maisha.

Anawakilisha nafasi ya matibabu katika kujenga jamii.Kupitia kwake, umuhimu wa kutokata tamaa licha ya matatizo unadhihirika.

Angalica/Anji/Angel/Bikizee

Ni tapeli.

Anamlazimisha Tembo kulipia huduma zake, ambazo hakuagiza.

Anampeleka kwake bila idhini yake na kumlazimisha kumlipa.

Ni mzinzi.

Anamweleza Tembo kuwa yeye hatoi huduma za ubwete.

Tembo anapoamka, amefungwa kanga kiunoni, na suruali yake kuanikwa kwenye kamba.

Ni wazi kuwa ni mambo anayofanya Anji kila mara.

Ni mhadaifu.

Ni vigumu hata kuamini msichana Tembo anayeona kwenye klabu ni yule yule anayepata kwenye chumba kile.

Wa klabuni ni maridadi, tena aliyejiremba, lakini anayejikuta naye chumbani ni bikizee mwenye sura ya kutisha.

Ni mkakamavu.

Hampi Tembo upenu wowote wa kutoroka.

Anashikilia msimamo wake kuwa lazima amlipe.

Hatimaye, anampa salio la mshahara wake alilohifadhi kwenye soksi.

Umuhimu wa Angelica

Kupitia kwake, ukware katika jamii unadhihirika.

Ni kiwakilishi cha wanawake matapeli wanaowafyonza wanaume pesa kwa kutumia ujanja.

Anadhihirisha madhara ya ulevi kwa jinsi anavyoutumia kumnasa Tembo.  

Anadhihirisha nafasi ya mwanamke katika jamii.  

Mbinu za Uandishi.  

Barua.

Hadithi hii imeandikwa kama barua kutoka kwa Tembo, aliye kwenye Hospitali ya Uhai ni Neema, kwa mkewe Emmi kwa ajili ya kumwomba msamaha.

Tashihisi

Baada ya hapo, akili yangu haikunakili kingine zaidi.

Usiku nao ukawa waingia na kwenyewe kwanyunyuza.

Nimetambua kuwa dunia ni danganyifu. Inaweza ikakutia ugani ikucheze… ikakunyonyoa na kukuacha watetema. Ikakurarua ukawa tambara. Ikakufyonza ukabakia tepwetepwe. Ikakupora kila chote chakwako…

Japo maisha yangu yamekanyagwa na kutiwa najisi na tamaa yangu mwenyewe na ghiliba za ulimwengu…

Istiara

Naomba nikuite mpenzi…bado wewe ndiwe waridi la moyo wangu.

Naona heri kukiri makosa na kufanya toba kuliko kuwa mpishi mzembe wa kusingizia moshi apikapo mashendea.Wingu la hofu, kutamauka, kushindwa na kujiuzulu linapoipamba mbingu yangu, ndiye anihimizaye.

Mamapima naye yu korokoroni… Ziraili wao, watoaji roho za watu.

Nilikunywa sumu, Emmi.Msuko wa filamu yangu hiyo ukaendelea kukunjuka aliposhuka kitandani bi kizee huyo.

Niliogopa kusema kitu labda nichokoze mzinga nishindwe kuyakabili makombora nitakayotupiwa.

Tashbihi

Kila siku saa ikiwadia utawaona kafurika wodi.

Ni kama mchwa kichunguuni wanavyokizingira kitanda chake.

Tena kwa mbali kama ambaye niko katika njozi lakini kweli nilisikia malalamishi yako.

Jamaa mmoja almaarufu Moshi alianguka…viputoputo vya hewa vinamtoka kinywani na kufanya povu kama la sabuni ya unga iliyotiwa maji.

Anarusha mateke kama mwenye kuingiwa kifafa.

Anafurukuta kama kuku anayetiwa bismilahi.

Watu wakatawanyika kama siafu waliomwagiwa jivu la moto.

Rangi ni za kila nui na kila mahali… Kifani chake ni tausi. Kumbe kucheza na pombe ni sawa na kucheza na moto.

Tena meno yake ni rangi ya kahawia, utadhani hutafuna matawi kama twiga.Hivi kichwani hakuwa na nywele, ni vinyoyanyoya vichache tu tena vyeupe kama chokaa.

Anakwenda kwa kurukaruka kama kijizimwi kuelekea pembeni.Inaweza ikakutia ugani ikucheze kama mpira.

Semi na Nahau

Niliponea chupuchupu- niliponea kibahati. yafisha moyo- yakosesha tumaini.

Ana moyo mkubwa- ana utu.

aliyenitia shime- aliyenihimiza, alinishinikiza.

namwonea ghere- namhusudu, namwonea wivu.

kupiga mafunda- kumeza kitu kiowevu.

kukutia macho- kukuona.

nikutake radhi- nikuombe msamaha.

atafanya juu chini- atafanya kila awezalo kutimiza jambo.

kufungua kinywa- kula chakula cha asubuhi, kustaftahi.

nilishika tariki- nilishika njia, nilianza safari.

moja kwa moja- kufululiza, bila kupinda popote.

kiguu niponye- kuondoka mbio sababu ya woga au hofu.

Maji ya kwake tuliyachapa kwa hiari- pombe yake tulikunywa kwa kujitakia.

kusakata rhumba- kucheza ngoma.

nivunje kimya- niongee, nimalize kimya.

sikujua alfa wala omega zake- sikujua chochote kuzihusu.

sina sinani- sina chochote.

Maswali Balagha

“Jamani mume wangu, hivi wewe huwezi kurekebisha tabia zako?... Hakuna starehe nyingine uliyoona ila kunywa pombe?...”  “Wajitapa una mke na watoto usiojua walacho wala wavaacho?... Majirani na marafiki wamekuusia mara ngapi uirekebishe tabia yako hii, uniheshimu mimi na watoto? Wazazi na wakwe zako pia uwape heshima? Waonaje sasa yaliyokufika kwa huko kujigeuza chachandu wa kujipalia makaa mwenyewe? Hivi wewe kumbe hukumbuki ulikotoka?...”

“Je, ni vipi tutoe pesa za jasho letu wenyewe tununue mauti? Jambo la starehe ligeuke kuwa maombolezo…”Tangu lini mtu kahifadhiwa ali hai? Nisemeje mimi kama si mazingira haya? Nikashika mfukoni mwa suruali, lakini wapi?  

Majazi

Hospitali ya Uhai ni Neema.

Ndipo wanapelekwa Tembo na Salim baada ya kuponea kutokana na pombe haramu.

Uhai kwao ni neema. Madaktari wanafanya wawezalo kuwasaidia.

Wameponea baada ya kubugia pombe iliyowaua wengi.

Tembo. Ina maana ya pombe.

Tembo ni mlevi kupindukia.

Pia ina maana ya ndovu.

Anajiona mwenye nguvu kama ndovu kabla ya upofu kumtuliza. 

Moshi. Wingu linalotokana na moto.

Hutoweka na kupotea bila kurudi.

Moshi anaanguka na kufariki papo hapo, anatoweka kama moshi.

Pia ni jina la aina ya pombe haramu, inayomwua Moshi mwenyewe.

Mwanaheri. Ni mwana mwenye heri.

Tembo anasema kuwa amejaliwa maumbile mazuri na akili pevu.

Pia, ana utu kwani anamwahidi Tembo kuhakikisha barua yake imefika.Zawadi na Riziki.

Wanawe Tembo. Zawadi ni tuzo, kitu anachopatiwa mtu kwa jambo zuri alilofanya.

Ni tuzo la ndoa yao. Riziki ni baraka au mafanikio kutoka kwa Mungu.

Mwana huyo ni riziki yao.

Pia humaanisha mapato ya kumwezesha mtu kuishi.

Anamtia mamake shime kutafuta riziki, ana riziki, yaani mahitaji yake yanakidhiwa.

Majengo. Sehemu anayoishi Angelica. Majengo ni wingi wa jingo, yenye maana ya banda au nyumba ya aina yoyote.

Kuna jengo analoishi Anji, na haikosi kuna majengo mengine.  

Methali

Kuvunjika kwa mwiko si mwisho wa upishi. asiye na mwana aeleke jiwe.

Kila mchezea wembe hujikata vyanda vyake.

Zimwi linijualo, halingenila kunimaliza(zimwi likujualo halikuli likakwisha) Asiyesikia la mkuu huvunjika guu.

Majuto kweli ni mjukuu huja kinyume.

Kinaya

Tembo anaeleza kuwa alizua zogo kwenye maziara wakati wa mazishi ya mtoto wa dadake.

Ni kinaya kwake kuzua rabsha katika maziara wakati watu wanaomboleza.

Tembo anasema kuwa walikunywa pombe ya Mamapima kwa hiari, tena kwa pesa zao.

Ni kinaya kuwa wanatoa pesa na kuzitumia kujidhuru kwa kupiga maji haramu yanayowaletea madhara.

Baada ya kisanga cha Moshi, ni kinaya kuwa bado Tembo na wenzake wanaelekea kuzima kiu ya pombe kwingine.

Badala ya kujifunza kutokana na tukio hilo, haliwapigi mshipa.

Mamapima anasemekana kuwa alitia pombe dawa ya kuhifadhia maiti.

Ni kinaya kuitia dawa hiyo kwa pombe itakayonywewa na watu walio hai. 

Ulinganuzi kati ya Angelica wa klabuni na wa chumbani unadhihirisha kinaya.

Wanapokutana na Tembo, amejiremba kwa marangi na maleba, anapendeza kweli.

Anapogutuka kibandani mwake, anakabiliana na Bi. Kizee mwenye sura ya kutisha.

Angelica anasema kuwa watu wanamwita Angel, yenye maana ya malaika.

Sura yake hata hivyo, ni kinyume cha jina hilo.

Pia, anamwambia Tembo kuwa yuko katika safe hands.

Hata hivyo, anamtapeli pesa zake, na pia mwonekano wake unatisha.

Tembo anapoondoka, Anji anamwambia kuwa anatumai watakutana hivi karibuni.

Ukweli ni kuwa Tembo wala yeyote yule hawezi tamani kukutana naye tena. 

Tembo anatamatisha barua yake kwa kumtaka mkewe awalete wanawe awaone.

Ajabu ni kuwa tayari amepofuka, wala hana uwezo wa kuwaona.

Kejeli

Nafahamu fika kuwa ulistahili na unastahili maisha mazuri kuliko yale uliyoishi katika uhusiano wetu huu wa bahati nasibu.

“Hawa hawawezi kupona, watakufa tu hatimaye.

”“Wajitapa una mke na watoto usiojua walacho wala wavaacho?”

Hivi sisi ni mizuka tu hatukustahili kuwa hospitalini bali kuzimu.

Kiumbe huyo angeitwa binadamu tu kwa kukosekana istilahi nyingine ya kuafiki sifa zake za kimaumbile.

Ama kwa kweli nilikuwa kwenye mikono ‘salama’ si haba.“pengine tukutane ahera, mwanga we!”

Takriri

Mimi sina neno kwa kuwa sina neno tu.

Sina neno la kusema, sina neno la kujitetea wala neno la kulipia deni la neno unalonidai.Mepesi kwa kuwa nimefanya marafiki humu humu hospitalini.

Orodha huwa ndefundefu.Niliogopa ungetaka maelezo marefumarefu ya kulikoni,…  

Emmi… nastahili kuadhibiwa hata zaidi na zaidi.Naomba uje unipunguzie dhiki, Emmi.

Naomba uje unitoe kwenye lindi hili la majaribu , Emmi. Naomba nafasi ya mwisho moyoni mwako, Emmi.

Njoo unipoze roho, Emmi. Njoo, ewe faraja yangu, njoo…

Chuku

Akili nyepesi masomoni yenye kunata mafunzo kuliko sumaku.

Hali yangu ni kun faya kun.

Ninatamani ahera ningali mzima.

Sijapata kumwona adinasi wa kutisha kama huyo.

Laiti ungemwona, Emmi! Ungefikiri kuwa mbingu zimeteremka na kushusha viumbe kutoka mwezini au labda Mirihi imekosa falaki na kushuka duniani kumleta Bi. Kizee huyu.

Kiumbe huyo angeitwa binadamu tu kwa kukosa istilahi nyingine ya kuafiki sifa zake za kimaumbile.

Tuliite ghofu la mtu.

Mifupa yahesabika.

Mishipa ya damu imechungulia kwenye ngozi yake chakavu iliyokunjana kama ya ndovu.

Anapocheka ndio kabisa utataka ardhi ikumeze. Anafanya maji kukujaa tumboni. Kwanza meno ni ya kuhesabu.

Tena meno yake ni rangi ya kahawia…

Harufu inayomtoka kinywani ni ya panya wa kuvunda.Kama sura mbaya ingalikuwa ugonjwa, kinyanya hiki kingeishi kwenye chumba cha wagonjwa mahututi.

Kijumba ni cha udongo, kimeezekwa kwa mabati mabovu na kilango kina mianya ya kutosha kupita ngamia.

Na ndio maana ya kutamani mbingu ianguke na kunimeza mara moja.

Dakika yoyote ile damu ingenikauka mwilini kwa woga.

Tayari viungo vilikwisha nilegea.

Nahisi mchanganyiko wa kichefuchefu na kizunguzungu.

Mwendo huo wa saa moja ulinichukua robo saa.

Nimetambua kuwa dunia ni danganyifu. Inaweza… Ikakunyonyoa ikakuacha watetema.

Ikakurarua ukawa tambara. Ikakufyonza ukabakia tepwetepwe.

Ikakupora kila chote cha kwako kwenye hazina.

Koja

Niliogopa ungetaka maelezo marefumarefu ya kulikoni, wendapi, warudi lini… Kuna wa kumi, wa tano, wa mkopo, almuradi…Pana harufu ya uvundo, mikojo ya walevi, matope, fujo, yaani mchanganyiko maalum.

Eti moshi, chang’aa, tear gas, sijui nini.Rangi ni za kila nui na kila mahali: mdomoni, mashavuni, nyusini, kopeni na nyweleni halikadhalika.Kuchanganya Ndimi“Sweetheart, amka!“

''I’m Angelica, huku wananiita Angel au Anji…”

 “Ondoa wasiwasi mhibaka, you are in very safe hands. Usiulize maswali. It’s okay. Tulikuja sote jana baada ya dance, umesahau hivi?”

“Kama uonavyo, nyumba hii inahitaji maintenance…”

“Thank you. U mteja wa kipekee…”

Tabaini

Si panya wa kuoza, si nyoka wafu, si sodo na nguo za ndani. 

Hadithi Ndani ya Hadithi.

Kisa ambacho Salim anamsimulia Tembo. Hadithi ya mhudumu na mkufu anaoulizia waumini kama wanautaka, kisha wanaukimbilia hata baada ya kuuangusha, kuuvyoga huku akiusagasaga kwa kiatu na kuutemea mate.

Hadithi hii inampa tumaini Tembo na kumwonyesha thamani ya maisha licha ya matukio yanayomkumba.  

Kisengerenyuma/Mbinu Rejeshi

Matukio yote yanasimuliwa kwa mbinu rejeshi.

Tembo anamwandikia barua mkewe akiwa hospitalini kumsimulia yaliyomkumba katika shughuli za ulevi. 

Ushairi.

Tembo anamkumbusha mkewe ushairi(Wimbo) wa watribu wa umuhimu wa kuchunga mtima.

Lau angefuata nasaha za wimbo huu, basi haya hayangemkumba.Mbinu zaidi ni kama vile Nidaa,Utohozi, Jazanda na Mdokezo.   

Join our whatsapp group for latest updates

Download Kila Mchezea Wembe summary notes - Mwongozo wa Mapamazuko ya Machweo na Hadithi Nyingine.


Tap Here to Download for 50/-
Why download?

  • ✔ To read offline at any time.
  • ✔ To Print at your convenience
  • ✔ Share Easily with Friends / Students


Get on WhatsApp Download as PDF
.
Subscribe now

access all the content at an affordable rate
or
Buy any individual paper or notes as a pdf via MPESA
and get it sent to you via WhatsApp

 

What does our community say about us?