KCSE 2017 Kiswahili Paper 2 with Marking Scheme

Share via Whatsapp
  1. UFAHAMU: (Alama 15)

    Soma kifungu kifuatacho kisha ujibu maswali.

    "Asante baba, asante mama," akasema Bahati jioni moja baada ya chajio, “Sijui ilitokeaje kukawa na watu wanaothamini binadamu wenye mahitaji maalumu katika jamii hii. Sitawauliza mlichofanya kunikinga na hukumu ya ukoo ya kuniangamiza, hayo mtakuja kunihadithia siku moja. Ila nataka mjue kwamba kuishi na ulemavu wa aina yoyote ile kuna dhiki kuu. Niliyokabiliana nayo baada ya uamuzi wenu wa kunipeleka shuleni hayawezi kutoshea hata chapisho la kurasa elfu. Si kudhihakiwa na miale ya jua; ngozi yangu inashindwa kuuhimili ukali wake, si kutengwa na marika, si kulazimika kusoma hati za kawaida hadi pale serikali ilipoanzisha sera ya kuhakikisha kwamba matini zote za kiusomi zimeandikwa pia kwa hati ambazo zinaweza kusomwa na wenye changamoto kama yangu, si kubaguliwa kazini....” Bahati alitua, akawatazama wazazi wake kama anayetaka kuona taathira ya maneno yake kisha akaendalea,

    “Msinione kama aliyekosa hisani, ila nataka niwaambie kwamba hata uamuzi wenu wa kunitafutia mlinzi kuandamana nami hadi shuleni ulinitia kwenye ngome zaidi. Nilijihisi kama niliyedhulumiwa zaidi katika kule kulindwa! Najua mlikuwa mnachelea kwamba ningekuwa windo rahisi kwa walanguzi wa binadamu ambao wanaamini kwamba viungo vyetu sisi ni dawa ya kutibia ndwele mbalimbali. Hata hivyo, katika kipindi chote hicho nilitamani kwamba mngenifunza mbinu za kujilinda mimi binafsi. Amini usiamini hata nilitamani kwamba ningetekwa nyara, nijadiliane na watesi wangu kuliko kupokwa nafasi ya kubuni mikakati ya kujihakikishia usalama".

    “Mwanangu Bahati," alisema mume wangu, "binadamu hawi jagina kwa kuzifuata tamaduni za jamii yake bila kuzichunguza. Haidhuru kwamba ilichukua muda kuyang'amua haya. La muhimu ni kwamba umeweza kuishi kama ndugu zako".

    Nilimtazama mume wangu kwa macho yaliyokuwa yamepofushwa na dimbwi la machozi. Moyo uliituma akili yangu kurudi nyuma kule -e-e-e- kwenye miereka ya baada ya kuzaliwa kwa Bahati. Asubuhi hiyo ya kipupwe nilishika ujia ulioelekea kwenye msitu uliokuwa karibu na boma la Mzee Kedi, baba mkwe wangu; mgongoni nimeifungia mbeleko ambayo ilikisitiri kitoto changu. Nilitazama nyuma, nikaiona nyumba ambayo mimi na mume wangu tulikuwa tumechanga bia kuijenga.

    "Haya yote nayaacha,” nilijiambia, "nayaacha na mengine mengi. Nawaacha mabinti wangu wawili, namwacha mume wangu, naiacha kazi yangu, nayaacha maisha yangu. Wala sijuti kwa kuyaacha haya yote. Sina cha kujutia kwani imebidi kuondoka. Jamii yangu imenitema; mimi na mwanangu. Haina nafasi ya mwanangu, kwa hivyo nami nimeamua kwamba haina nafasi yangu kwa vile imesema huu ni mzigo wangu. Ikiwa ukoo umeamua kuwa hatima ya mwanangu huyu ni kuwa kitoweo cha fisi, basi na tuwe sote karamu ya fisi,” nilitamatisha kauli yangu kisha nikayarudisha nyuma tena mawazo yangu.

    Nilikumbuka sauti ya muuguzi hospitalini siku ambayo nilijikopoa, “Pongezi Tamasha, Mungu amekutunukia kipusa”. Nilikifunua kitoto changu kilichokuwa kimefunikwa gubigubi, nikakitazama viguu, vikono, uso...kisha, Mungu wangu!' ikanitoka.

    “Dadangu, unastahili kumshukuru Mungu,” akasema muuguzi, "wapo wanawake, mimi mwenyewe nikiwemo, ambao hawajawahi kuambulia ujauzito, sikwambii hata kupoteza mimba. Huyu wako ni kiumbe kamili, kasoro yake i kwenye ngozi tu, na hii ni hali ambayo unaweza kukabiliana nayo. Hapa unionapo nimelazimika kumpa mume wangu talaka, mwenyewe alienda kortini akaiomba. Anadai kwamba hatusikilizani. Ila najua kiini cha haya yote ni kutoshika kizazi".

    Nilimtazama huyo muuguzi kana kwamba hajasema lolote. Nilimwona kama anayeuona mzigo wangu kuwa kanda la usufi. Huenda huyu muuguzi hakujua kwamba katika jamii yangu watoto wa aina hii ni kama pacha, huaminiwa kuwa nuksi kwa ukoo mzima, kwa hivyo hutupwa. Muuguzi huyu hakujua pia kwamba tayari nilikuwa na watoto wawili wa kike na huo tayari ulikuwa mzigo mkubwa kwangu kwani ilibidi kumhakikishia mavyaa kila mara kwamba hawa pia walikuwa watoto.

    Moyo ulinipa kukumbuka jitimai iliyojiandika usoni mwa mume wangu asubuhi hiyo alipokuja hospitalini. Alikitazama kitoto chetu kana kwamba anaona mzuka. Alinyamaza kwa muda, akashusha pumzi, kisha akanishika kwenye bega na kuondoka kwenye wodi. Machozi yalivunja kingo zake huko yanakohifadhiwa, nikalia kama mfiwa. Mume wangu alirudi tena baada ya siku mbili; anakuja kunipeleka nyumbani.

    "Mke wangu, naomba msamaha kwa kutokuja kuwatazama kwa siku mbili. Ilibidi nishauriane na ukoo kuhusu tanzia hii. Inavyoonekana ni kwamba msimamo wa baba na wazee wengine ni ule ule. Wanasema ukoo wa Baulanga haujawahi kupata mtoto wa aina hii, kwamba kumhifadhi mwana huyu kutakuwa kuupaka masizi ukoo. Wahenga hawatakubali tendo hili. Sijui nitakutetea vipi. Nimo kwenye njia panda," mume wangu alikamlisha uzungumzi wake na kuelekea kwenye afisi ya mhasibu kukamilisha viviga vya kutuondoa hospitalini.

    "Huna haja ya kunitetea. Sijafanya kosa lolote. Nililofanya ni kujaliwa kiumbe ambaye anaonekana kuwa punguani kwa misingi ya jamii yako. Nitakilinda kitoto hiki hata kifoni," nilimwambia mume wangu mawazoni.
    1. “Kufanikiwa kwa watu wenye mahitaji maalumu kunategemea jamii." Thibitisha kwa kutoa hoja sita kutoka aya tatu za kwanza.  (alama 6)
    2. Kwa kurejelea aya ya nne hadi ya saba, onyesha jinsi unyanyasaji wa kijinsia unavyoendelezwa katika jamii hii,(alama 3)
    3. "Msimulizi anahimiza uwajibikaji." Thibitisha kwa kutoa hoja nne kutoka aya tatu za mwisho.  (alama 4)
    4.  
      1. Andika kisawe cha, 'hisani' kwa mujibu wa taarifa.   (alama 1)
      2. Eleza maana ya 'kuupaka masizi' kulingana na taarifa.  (alama 1)
  2. UFUPISHO:   (Alama 15)

    Soma kifungu kifuatacho kisha ujibu maswali.

    Moja kati ya mambo ambayo yamerahisisha maisha ya binadamu ni maendeleo ya kisayansi na kiteknolojia. Siku hizi shughuli nyingi ambazo zilichukua muda mrefu kutekelezwa zinachukua muda mfupi sana. Tuchukue kwa mfano shughuli za usafiri na utendaji kazi. Siku hizi zipo mashine ambazo zinafanya kazi kuwa nyepesi mno. Kwa mfano, katika ukulima. kuna mashine za kulima, kuvuna na hata kupura nafaka. Magari nayo yamerahisisha usafiri na upashanaji habari. Safari ambayo awali ilichukua siku mbili au tatu, siku hizi inachukua siku moja au hata saa chache tu kwa sababu ya kuwepo kwa magari ya kisasa

    Katika sekta ya elimu, maendeleo makubwa yameshuhudiwa. Siku hizi mwalimu anaweza kuhuisha somo lake kwa kutumia tarakilishi. Vipindi mbalimbali vimenaswa na kuhifahiwa kwenye kompyuta. Itokeapo kwamba mwalimu wa darasa atakosa kuhudhuria somo. wanafunzi wanaweza kufunzwa na mwalimu wa kompyuta. Shughuli za utafiti nazo zimefaidika mno kutokana na uvumbuzi wa kiteknolojia. Wasomi na wanafunzi wanaweza kupata matini mbalimbali za rejea kupitia kwenye mtandao. Hili linasaidia kufidia upungufu wa vitabu vya kikaida. Hali kadhalika, maendeleo ya kiteknolojia yamerahisisha shughuli za usajili vyuoni na hata shuleni. Wanafunzi wanaweza kujisajili na hata kulipia kozi mbalimbali kupitia kwenye mtandao. Hali hii inaokoa muda ambao watahiniwa na wanaafunzi wangepanga foleni vyuoni, na hata katika taasisi zinazotoa mitihani, ili kujisajili kadhalika, teknolojia imesaidia katika kuhakikisha usalama wa alama za wanafunzi. Wataalamu wa teknolojia wameweza kuweka mikakati ambayo itahakikisha kwamba mabadiliko yoyote ya alama yanaweza kufuatiliwa kupitia kwenye mtandao.

    Upande wa matibabu nao haujaachwa nyuma. Utafiti kuhusu tiba za kukabiliana na magonjwa sugu unafanywa kupitia kwenye mtandao wa intaneti. Pia, kuna mitambo ya kuchunguzia viini vya magonjwa mbalimbali na kutoa matokeo hapo hapo. Hali hii husaidia kumpa mgonjwa matibabu yafaayo wakati ufaao, hivyo kuokoa maisha yake. Madaktari pia wanaweza kufanya udodosi hapo hapo kwa kubofya tu tarakilishi.

    Yumkini manufaa zaidi ya maendeleo ya kisayansi na kiteknolojia yamepatikana kwenye uwanja wa biashara na uchumi kwa jumla. Ni dhahiri kwamba siku hizi ubadilishanaji wa bidhaa na huduma umekuwa rahisi mno. Kwa mfano, mfanyabiashara anaweza kuuza na kununua bidhaa zake kutoka nga'mbo akiwa hapo hapo kiwandani au afisini mwake. Hali hii imefanikishwa hata zaidi na uvumbuzi wa simutamba; kifaa kidogo lakini chenye akili kama ya bindamu. Kifaa hiki huwa na huduma ya intaneti ambayo humwezesha muuzaji kumtumia mnunuzi picha ya bidhaa aitakayo akiwa popote pale. Kifaa hiki pia ni muhimu katika kuendeleza huduma za benki. Je, unajua kwamba unaweza kutoa na kuhifadhi fedha kwenye akaunti yako kwa sekunde mbili au tatu ukiwa hapo hapo sebuleni mwako? Unajua pia unaweza hata kuomba na kupokea mkopo kupitia simu yako ya mkononi? Huduma hii ya simutamba pia humwezesha mtu kuwatumia pesa jamaa zake bila kulazimika kwenda benki au posta kuzituma. Mtu anaweza hata kuhifadhi laki moja kwenye simu na kuzituma pesa hizo kulingana na matilaba yake. Kadhalika mtu anaweza kulipia huduma kama vile za umeme, maji, matibabu na hata karo kupitia kifaa hicho hicho.

    Ni dhahiri kwamba uvumbuzi wa kisayansi na kiteknolojia umeiletea jamii natija kubwa, Hata hivyo, hakuna mchele usiokuwa na ndume. Maendeleo haya yameandamana na changamoto anuwai kuwepo kwa mtandao wa intaneti kumewafanya baadhi ya wanajamii kutumia muda wao mwingi kwenye mtandao, mara nyingine kwa nia ya kujiburudisha tu au kuzungumza na marafiki. Hili linapalilia kuzorota kwa maadili ya kikazi. Aidha, kuna baadhi ya watu ambao wanatumia mtandao kuwatusi na kuwadhalilisha wengine kwa namna mbalimbali. Wengine huingilia uhuru wa kibinafsi wa wenzao kwa kuangaza mahusiano yao ya kimapenzi. Hali kadhalika, kuna wanajamii ambao hutumia mtandao kuwatisha wengine. Baadhi hutumia mtandao kuwatapeli wengine. Pengine hata wewe umewahi kupigiwa simu ukaambiwa umeshinda milioni moja, ukaanguka kwenye mtego huo, na baadaye hata ukapoteza kiasi fulani cha fedha ukifuata milioni ambayo haipo!

    Uvumbuzi wa kiteknolojia umechangia kuendeleza wizi wa kitaaluma. Kuna wasomi katika ngazi mbalimbali ambao hunakili mawazo ya wataalamu moja kwa moja bila hata kutambua mchango wao kwenye marejeleo. Hii ni njia moja ya kudhoofisha fani yenyewe ya utafiti. Kadhalika, mtandao wa intaneti umetumiwa na watu waliopotoka kimaadili kupujua thamani ya mtihani. Baadhi ya watu huchukua sehemu ya mtihani au hata karatasi nzima ya mtihani wakaipiga picha na kuituma kwa wateja wao kupitia kwenye mitandao ya kijamii. Visa vya kigaidi navyo vinaendelezwa kwa ufanifu mkubwa kupitia kwenye mtandao wa intanenti na simu za mkononi. Njama nyingi za ulipuaji wa majengo zimepangwa kupitia simutamba. Vilevile, uvumbuzi wa kiteknolojia unatishia kuteteresha mshikamano wa kifamilia. Siku hizi mzazi anaweza kukaa kwa miezi miwili bila kuonana ana kwa ana na watoto wake, wanazungumza tu kupitia kwenye simu. Hili hutepua ule uhusiano wa kibinafsi kati ya jamaa, na mwishowe huweza kusababisha ukengeushi; watoto na wazazi wakajiona kuwa wageni kwa kila mmoja. Juu ya hayo, huduma zinazopatikana kwenye mtandao zimewafanya vijana kuwa waraibu kiasi cha kutotenga wakati kuyadurusu masomo yao. Hili linawatia kiwewe wakati wa mtihani na yamkini ni mojawapo ya vyanzo vya udanganyifu katika mitihani.

    Maendeleo ya kiteknolojia yamesaidia kuimarisha maisha ya binadamu katika nyanja zote za maisha. Binadamu wameweza hata kupata mafundisho ya kidini moja kwa moja kupitia kwenye simu zao za mkono. Hata hivyo, binadamu ameweza pia kuhasirika kutokana na uvumbuzi huu. Mashine zimetwaa nafasi ya binadamu katika utendakazi, jambo ambalo linapalilia zaidi uhaba wa nafsi za kazi. Ni muhimu binadamu ajitahidi kutumia teknolojia kwa njia endelevu ili kujifaidi.
    1. Fupisha ujumbe wa aya nne za kwanza kwa maneno 90.    (alama 8, 1 ya mtiririko)
    2. Fafanua masuala ambayo ,mwandishi anaibua katika aya tatu za mwisho. ( maneno 70)     
      ( alama 7, 1 ya mtiririko)
  3. MATUMIZI YA LUGHA    (Alama 40)
    1. Andika tofauti moja kati ya sauti zifuatazo:   (alama 2)
      1. /ng / na /gh//
      2. /v/ na /f/
      3. /r/ na /l/
      4. /m/ na /n
    2. Andika maneno yenye miundo ifuatayo:   (alama 2)
      1. konsonanti, konsonanti, konsonanti, irabu, konsonanti, irabu
      2. konsonanti, konsonanti, irabu, konsonanti, irabu
    3. Tunga sentensi mbili kuonyesha matumizi mawili ya kiambishi : 0.  (alama 2)
    4. Andika sentensi zifuatazo upya kulingana na maagizo.   (alama 2)
      1. Mhalifu alisamehewa kwa sababu alinyenyekea.
        (Geuza maneno yaliyopigiwa mstari kuwa nomino.)
      2. Waigizaji wengine wameingia jukwaani.
        (Tumia kivumishi cha idadi chenye kuonyesha nafasi katika orodha.)
    5. Tunga sentensi ukitumia kirai kihusishi kama kielezi.   (alama 1)
    6. Unganisha sentensi zifuatazo kwa viunganishi mwafaka.       (alama 2) 
      1. Kheri aliweza kutujengea hospitali. Atajenga zahanati pia.
      2. Zumari anasomea Uanasheria. Vilevile Maki anasomea Uanasheria
    7. Onyesha miundo miwili ya nomino katika ngeli ya A - WA.   (alama 2)
    8. Tunga sentensi katika wakati uliopo hali isiyodhihirika.     (alama 1)
    9. Andika sentensi ifuatayo katika umoja.   (alama 1)
      Maseremala walilainisha mbao hizo wakatutengenezea meza.
    10. Andika upya sentensi zifuatazo kulingana na maagizo.  (alama 4)
      1. Kaumu amewafanya mifugo wangu wanywe maji.
        (Anza kwa: Mifugo wangu , usitumie, 'amewafanya'.)
      2. Wanakijiji wanaishi karibu na msitu. Wanakijiji hawawavamii wanyama.
        (Unganisha kuunda sentensi ambatano.)
    11. Andika sentensi ifuatayo katika hali ya ukubwa.   (alama 1)
      Ngoma hizo zao ziliibwa na wezi wale.
    12. Tumia 'kwa' katika sentensi kuonyesha:
      1. sehemu ya kitu kizima   (alama 1)
      2. namna tendo lilivyofanyika       (alama 1)
    13. Andika sentensi ifuatayo katika usemi wa taarifa     (alama 2)
      "Kusoma kwa mapana kutapalilia ubunifu wa wanafunzi hawa wenu," mtaalamu akatuambia.
    14. Ainisha vishazi katika sentensi ifuatayo.   (alama 2)
      Viwanda vikianzishwa mashambani idadi ya wanaohamia mjini itapunguzwa.
    15. Tunga sentensi zenye miundo ifuatayo.    (alama 2)
      1. KN (N + RH) + KT (Ts + T)
      2. KN (V+N) + KT (t + v)
    16. Ainisha yambwa katika sentensi ifuatayo.     (alama 2)
      Mhunzi alimfulia mjukuu wake pete ya shaba.
    17. Bainisha maana mbili zinazojitokeza katika sentensi ifuatayo.      (alama 2)
      Bedui alimrushia tufe.
    18. Alama za mtajo hutumiwa kufungia maneno halisi ya msemaji. Tunga sentensi mbili kuonyesha matumizi mengine mawili ya alama za mtajo.     (alama 2)
    19. Andika sentensi ifuatayo upya kwa kutumia kinyume cha maneno yaliyopigiwa mstari.
      Mwanafunzi mkakamavu huzingatia masomo yake.    (alama 1)
    20. Tunga sentensi moja kutofautisha maana ya rithi na ridhi.    (alama 2)
    21. Tunatumia simile tunapotaka mtu atupishe .............. tunapoomba kitu kinusurike, na kefule............. na jambo.(alama 1) 
    22. Andika visawe vya maneno yafuatayo:
      1. doa ..................................
      2. omba ................................
    23. Andika sentensi ifuatayo upya kulingana na maagizo.           (alama 1)
      Maeneo haya yana uyoga.
      (Anza kwa: Uyoga.)
  4. ISIMUJAMII:       (Alama 10)

    Soma makala yafuatayo kisha ujibu maswali.

    "Kwa mujibu wa ushahidi uliotolewa mahakama hii imethibitisha bila chembe ya shaka kwamba wewe mshtakiwa, Bi Mlachake Chauchau ndiye ulivepika pombe haramu ambayo ilisababisha vifo vya raia hamsini na kupofuka kwa wengine mia moja. Unahukumiwa kwa kosa la mauaji."
    1. Bainisha sajili ya makala haya kwa kutoa mifano miwili kutoka kwenye makala.      (alama 2)
    2. Fafanua sifa nyingine nane za sajili hii ambazo zingejitokeza katika makala haya.          (alama 8)


MARKING SCHEME

  1. Ufahamu
    1.  
      1. Wazazi wanampeleka Bahati shuleni.
      2. Bahati kupata dhiki ya kisaikolojia kwa kudhihakiwa i
      3. Wazazi kumtafutiaBahati mlinzi wa kumkinga na wateka nyara. 
      4. Bahati na wengine kama yeye kusoma hati za kawaida hapo awali 
      5. Bahati kubaguliwa kazini
      6. Serikali kuhakikisha matini zimeandikwa kwa hati inayoweza kusomwa na walemavu 
      7. Wazazi hawamfunzi Bahati mbinu za kujilinda, hivyo anajihisi mfungwa. 
      8. Walanguzi wa watu kuhatarisha usalama wa watoto wa aina ya Bahati
      9. Ukoo kuamua kuangamiza watoto wenye ulemavu
      10. Bahati kudhihakiwa shuleni/kutengwa na wenzake 
      11. Mama/wazazi kuamua kumhifadhi Bahati

        Tanbihi
        Mtahiniwa anaweza kuangazia dhuluma pekee. Anaweza pia kuangazia utekelezaji wa haki kwa watu wenye mahitaji maalumu pekee. Anaweza pia kuchanganya hoja. Mradi amedondoa hoja sita.
        (6 x 1)    (alama 6)
    2.  
      1. Muuguzi kutalikiwa kwa kutopata mtoto
      2. Watoto wa kike kuonekana kuwa mzigo/si watoto
      3. Kusimangwa na mavyaa - kuwa hajazaa watoto.  
        (3x 1)    (alama 3)
    3.  
      1. Mume kuondoka bila neno kwa mkewe - anakuja kuomba msamaha.
      2. Mume kushauriana na ukoo kuhusu mtoto 
      3. Ukoo kuamua kuangamiza kitoto bila kujali hisia za mama/wazazi
      4. Mume kumjuza mke uamuzi wa ukoo
      5. Mume kulipia gharama ya matibabu
      6. Msimulizi kuamua kukihifadhi kitoto chake
      7. Msimulizi anakashifu mtazamo wa jamii kuhusu watoto wa aina hii.  (aya ya mwisho)
        Tanbihi
        Mtahiniwa anaweza kuonyesha uwajibikaji au hata ukosefu wa uwajibikaji. Anaweza kuchanganya hoja pia.  
        (4x1)     (alama 4)
    4.  
      1. Hisani- fadhila, shukrani  (alama 1)
      2. Kuupaka masizi - kuuharibia sifa/ kuuaibisha    (alama 1)
  2.  
    1.  
      1. Sayansi na teknolojia zimerahisisha maisha ya binadamu.
      2. Mashine zimerahisisha utenda kazi.
      3. Mtu anaweza kusomesha hata bila kuwepo. 
      4. Kuimarisha shughuli za utafiti 
      5. kurahisisha usajili wa wanafunzi na watahiniwa 
      6. Kuimarisha matibabu kupitia utafiti
      7. Kufanya udososi hapo hapo
      8. Kurahisisha ubadilishanaji bidhaa
      9. Kuhifadhi na kutuma pesa xi. Kulipia huduma
        (7x1)      (alama 7)
        Mtiririko- alama 1. Jumla-alama 8
        Tanbihi
        1. Mtahini awe makini kutambua hoja ambazo zimetolewa kama ufafanuzi wa nyingine.
        2. Hizi hazipaswi kutuzwa kama sehemu ya ufupisho wa mtahiniwa.
    2.  
      1. Nafasi ya uvumbuzi wa kisayansi
      2. Kuzorotesha utenda kazi 
      3. Kuingilia uhuru wa kibinafsi 
      4. Kuwatisha wengine
      5. Kuwatusi na kuwadhalilisha wengine 
      6. Kuwatapeli
      7. Wizi wa kitaaluma 
      8. Upujufu wa thamani ya mtihani/ wizi wa mitihani
      9. Visa vya kigaidi kuendelezwa kupitia mtandao
      10. Kumomonyoa mshikamano wa kifamilia-mawasiliano ya simu badala ya ana kwa ana
      11. Vijana kupuuza masomo kwa kuwa waraibu wa mtandao
      12. Binadamu huweza kupata mafundisho ya kidini kupitia mtandao. 
      13. Kupalilia ukosefu wa ajira
      14. Binadamu atumie teknolojia kwa njia endelevu ili kujifaidi.
        (6x1)    (alama 6)
        Mtiririko- alama 1. Jumla alama 7
  3.  
    1. Sauti:
      1.  /ng/ni nazali na/gh/ni kikwamizo.
      2. /v/ ni ghuna na /f/ sighuna. 
      3. /r/ ni kimadende na /l/ ni kitambaza. 
      4. /m/ hutamkiwa midomoni ilhali /n/ ni ya ufizi.
        (4 x ½)   (alama 2)
    2.  
      1. Mfano: mbweha, ngwena, ndwele   ( alama 1/0)
      2. Mfano: ndama, mkate, ngama, ndizi, mkeka    (alama 1/0)
    3. Matumizi ya kiambishi O
      Mifano
      1. Kirejeshi cha nafsi ya tatu wingi - Wafanyakazi walioajiriwa wana bidii. 
      2. Kirejeshi cha ngeli ya U-1 - Umoja
        Mguu uliotibiwa umepona. 
      3. Kirejeshi cha ngeli ya U- ZI - umoja
        Ufa uliozibwa ni huu
      4. Kirejeshi cha ngeli ya U-YA- umoja
        Ugonjwa huu ndio uliotibiwa. 
      5. Kirejeshi cha ngeli ya U-U
        Wema aliotuonyesha ulituvutia. 
      6. Kuonyesha tokeo la kitu/kuonyesha nomino/unominishaji
        1. Mtafiti umetoa toleo jipya la kazi hiyo.
        2. Mti umetoa zao lingine
        3. Mkato huu wa nywele haupendezi
      7. Kuonyesha kinyume
        Mwangi aliuchomoa mkuki ardhini
        (2x1)      (alama 2)
    4.  
      1. Mhalifu alipata (alipewa) msamaha kwa sababu (kwa) unyenyekevu wake.   (alama 1/0)
      2. Waigizaji wa kwanza/wa mwisho wameingia jukwaani.( alama1/0)
    5.  
      1. Mama huyo aliwapenda wanawe kwa dhati. (RH/E) 
      2. Bendera ilikuwa juu ya mlingoti. (RH/E) 
      3. Mkurugenzi aliwasili kabla ya mkutano kuanza (RH/E) 
      4. Kaire ni mrefu kuliko baba yake.(RH/E)
        (alama 1/0)
    6.  
      1.  
        1. (Ikiwa/ Kama) Kheri aliweza kutujengea hospitali sembuse zahanati!
        2. Kheri aliweza kutujengea hospitali kwa hivyo atatujengea zahanati (pia).
          (alama 1/0)
      2. Zumari na Maki wanasomea Uanasheria.    (alama 1/0)
    7. Majibu yafuatayo yanaweza kutolewa:
      1. Nomino zinazoanza kwa 'm' katika umoja na 'wa' katika wingi.
        Mfano: Mbunge - Wabunge
      2. Zinazoanza kwa 'mw' katika umoja na 'wa' katika wingi.
        Mfano: Mwanasheria - Wanasheria
      3. Nomino za pekee zinazotaja watu. Maria ametutembelea
      4. Zinazoanza kwa'ki' katika umoja na 'vy' katika wingi.
        1. Kijana huyu ameheshimika.
          Vijana hawa wameheshimika.
        2. Kiboko angali majini.
          Viboko wangali majini.
      5. Ambazo hazina mianzo maalum ila huchukua viambishi A-WA vya upatanisho wa kisarufi.
        Kwa mfano, simba, kuku, bata, mama, baba.
        Simba huyu amehifadhiwa.
        Simba hawa wamehifadhiwa.
        (2x1)      (alama 2)
        Mtahiniwa atoe mfano ili kutuzwa alama 1 kwa kila jibu.
    8. Kiambishi 'a' cha njeo kitumiwe.
      1. Wanariadha wacheza uwanjani.
      2. Jua lachomoza asubuhi.
      3. Sisi twasoma vitabu.
      4. Mwalimu afundisha darasani.
        (1x1)    (alama 1/0)
    9. Seremala alilainisha ubao huo akanitengenezea meza.  (alama 1/0)
    10.  
      1. Mifugo wangu wamenyweshwa maji na Kaumu.    (alama 2/0)
      2. Wanakijiji wanaishi karibu na misitu lakini ilalbali ilhali hawawavamii wanyama.   (alama 2/0)

         Tanbihi
        Sentensi sharti iwe na vishazi viwili huru. Kimoja kikiwa kitegemezi, basi hiyo haitakuwa ambatano, hata kama atakuwa ametumia kiunganishi ambatani kama vile "lakini' na 'ila.'
    11. Magoma hayo yao yaliibwa na majizi yale.   alama 1/0
    12.  
      1.  
        1. Watoto watatu kwa kumi hupata chanjo hiyo.
        2. Wengine walipata tisa kwa kumi katika tamrini hiyo.
          alama 1/0
      2.  
        1. Sara alifanya kazi kwa bidi.
        2. Polisi waliandamana moja kwa moja hadi kituoni.
        3. Mchinjaji alikata nyama kwa kisu.
          alama 1/0

          Tanbihi
          Hata pale 'kwa' inapotumiwa kuonyesha ala/kitumizi, huonyesha pia jinsi tendo lilivyofanyika.
    13. Mtaalamu alituambia kwamba kusoma kwa mapana kungepalilia ubunifu wa wanafunzi haowetu.
      alama 2/0
    14.  
      1. Viwanda vikianzishwa mashambani - kishazi kitegemezi
      2. Idadi ya wanaohamia mjini- kishazi kitegemezi
      3. Itapunguzwa - kishazi huru
        2 x 1 = 2
    15.  
      1.  
        1. Umati wa watu ulikuwa ukimshangilia.
        2. Kisu cha baba kinahitaji kunolewa.
          alama 1/0
      2.  
        1. Mwenye duka angali mwaminifu.
        2. Yule dalali alikuwa shupavu. 
        3. Huyu mtoto ni mtiifu.
        4. Lenye mpini lilikuwa lake.
          alama 1/0
    16. Mjukuu wake -yambwa tendewa (kitondo)
      Pete ya shaba-yambwa tendwa (kipozi)
      2 x 1 = 2
      Tanbihi   
      Ikumbukwe kwamba sharti yambwa kamili ijitokeze. Kwa mfano, mnjukku anayerejelewa ni wake, hivyo yambwa tendewa itakuwamjukuuwake wala si mjukuun tu.
    17.  
      1. Alirusha tufe kwa niaba ya mhusika huyo.
      2. Alirusha tufe kuelekea kwa mhusika huyo.
      3. Alirusha tufe ya mhusika huyo.
      4. Alimrusha mhusika huyo kwa sababu ya tufe.
    18. Matumizi yafuatayo yajitokeze: 
      1. Kufungia neno la kigeni-"mukimo"
      2. Kuonyesha neno lina maana nyingine na unayomaanisha, k.m. binamu kumaanisha  "mpenzi.
      3. Kufungia anwani- "Pendo la Karaha"
      4. Kuonyesha neno halijakubaliwa katika lugha unayoandikia/unayozungumza.
        2x 1 = 2
    19. Mkakamavu-mzembe/mvivu/mnyonge/goigoi/mtepetevu/dhaifu huzingatia - hupuuza/ hutelekeza
      2 x ½ = 2
      Maana zifuatazo zijitokeze
    20. Rithi - kupata mali/maarifa au ujuzi kutoka kwa mtu/makala fulani
      Ridhi - kukubali au kupendezwa na jambo/kutoa ruhusa jambo litendeke.     alama 2/0
      Tanbihi
      Kwa vile tunatahini matumizi ya maneno haya, anaweza kuvinyambua vitenzi, mradi ile maana ya kimsingi inajitokeza.
    21.  
      1. hamadi
      2. tunapoudhika/tunapokasirishwa
        2 x ½ = 1
    22.  
      1. doa-dosari, kosa, hitilafu, ila, baka.
      2. omba-rai, sihi, sali
    23.  
      1. Uyoga hupatikana kwenye maeneo haya.
      2. Uyoga hupatikana katika maeneo haya.
      3. Uyoga upo kwenye maeneo haya.
      4. alama 1/0
  4.  
    1. Sajili ya mahakamani/sajili ya kisheria
      1. Matumizi ya sentensi ndefu -- sentensi ya kwanza inatakriban maneno 30. 
      2. Msamiati maalum wa kisheria kama vile 'ushahidi','mahakama', 'unahukumiwa'... 
      3. kuzungumza na mshukiwa moja kwa moja- wewe mshukiwa 
      4. Kutoa hukumu
        Kutaja- Alama 1.
        Mfano- Alama 1
    2. Baadhi ya hoja:
      1. Matumizi ya lugha chakavu/kikale 
      2. Kunukuu vifungu vya sheria ili kuondoa shaka. 
      3. Kuzingatia urasmi kwa kiasi kikubwa
      4. Urudiaji unaonuiwa kuweka wazo wazi/kusisitiza 
      5. Msamiati wa kawaida hupewa/huwa na maana maalum. Kwa mfano unaposema, "Learned Friend", kumaanisha mwanasheria.
      6. Lugha ya kuhoji/kudadisi, hasa pale mshukiwa/shahidi anapohojiwa.
      7. Sheria za kisarufi huzingatiwa kwa kiasi kikubwa ili kukinga dhidi ya kupotosha maana
      8. Wakati mwingine sheria hizi huweza kuvunjwa ili kukidhi haja ya mawasiliano, hasa pale mshukiwa hajasoma/haelewi lugha rasmi au lugha sanifu.
      9. Kauli fupifupi hasa wakati wa kuhoji.
      10. Upashanaji zamu kwa kawaida hudhibitiwa na kiongozi wa mashtaka
      11. Kuchanganya au kubadilisha msimbo huweza kutokea.
      12. Lugha ya kushawishi, hasa pale wakili anapotoa utetezi (xv) Toni kali pale hakimu anapotoa hukumu.
        8 x 1 = 8
        Tanbihi
        Ufafanuzi/ mifano itolewe ili kutuzwa alama 1.
Join our whatsapp group for latest updates

Download KCSE 2017 Kiswahili Paper 2 with Marking Scheme.


Tap Here to Download for 50/-




Why download?

  • ✔ To read offline at any time.
  • ✔ To Print at your convenience
  • ✔ Share Easily with Friends / Students


Get on WhatsApp Download as PDF
.
Subscribe now

access all the content at an affordable rate
or
Buy any individual paper or notes as a pdf via MPESA
and get it sent to you via WhatsApp

 

What does our community say about us?

Join our community on:

  • easyelimu app
  • Telegram
  • facebook page
  • twitter page
  • Pinterest