Kiswahili Paper 3 Questions and Answers - Mokasa 1 Joint Pre Mocks Exams 2023

Share via Whatsapp

Maagizo

  • Jibu maswali manne pekee.
  • Swali la kwanza ni la lazima.
  • Chagua mengine matatu kutoka sehemu nne zilizobaki yaani: Riwaya, Tamthilia, Hadithi Fupi na Ushairi.
  • Usijibu maswali mawili kutoka katika sehemu moja.
  • Majibu yaandikwe katika kijitabu cha majibu utakachopewa.
  • Hakikisha kuwa kurasa zote zimepigwa chapa sawasawa na kwamba maswali yote yamo.
  • Karatasi hii ina kurasa 8 zilizopigwa chapa.

SEHEMU YA A: FASIHI SIMULIZI

  1. Lazima
    Soma utungo ufuatao kisha ujibu maswali.


    Zimepita siku ayami
    Siku chungu tangu giza lipotanda
    Wakati lipotazama kwa kiwewe na shauku
    Pumzisho kipania, roho kupigania
    Ziraili alipokakamaa aushiyo kufakamia.

    Nilikwita kwa sauti
    Ela mpenzi hukunitika
    Machoyo litunga mbele
    Kumkabili huyu nduli
    Nikabaki kunyongonya
    Jaala kitumainia,
    Mtima kijiinamia
    Hatima kungojea.

    Ya mwisho lipopumua,
    Alfajiri ya kiza kuu
    Nalidhani wanichezea,
    Mizaha yako kawaida
    Lijaribu kupulizia
    Hewa toka langu pafu,
    Tumaini kiniambia pumzi zangu takuhuisha
    Sikujua hizo likuwa juhudi za mfa maji muhebi.

    Macho libaki kutunduiya, tabasamuyo kitaraji
    Kumbe mwenzangu kaniacha!
    Ukiwa ulinivaa, ukungu ukatwandama
    Pa kuegemea sikujua fundo chungu linisakama
    Tabibu alipoingia na kutangaza rasmi mauko.

    Ilikuwa kana kwamba ndo jana lipofunga nikahi,
    Kumbukizi zilinijia kwa chozi teletele
    Japo kifo ni faradhi ndwele hino halieleweki
    Ama jicho la hasidi,
    Limekuangaza jamani?

    Koja hili ninalokuwekea,
    Kando ya kasri hili la shakawa
    Ni hakikisho toka kwangu, nitatamba sana njia
    Kutafuta alotwendea kinyume kutupoka,
    Mauko kutuleteya.
    1.  
      1. Ainisha utungo huu kwa kuzingatia kipengele cha maudhui. (alama 1)
      2. Andika sababu tatu kuthibitisha jibu lako la a(i). (alama 3)
    2. Bainisha sifa mbili za jamii inayosawiriwa wa utungo huu. (alama 2)
    3. Fafanua vipengele vinne vya kimtindo ambavyo vimetumiwa kufanikisha uwasilishaji wa utungo huu. (alama 4)
    4. Tungo za aina hii zinaendelea kufifia katika jamii yako. Fafanua hoja tano utakazotumia kuishawishi jamii yako kukinga dhidi ya hali hii. (alama 5)
    5. Unanuia kutumia mbinu ya kushiriki kufanya utafiti kuhusu tungo za aina hii. Eleza sababu tano za kuchagua mbinu hii. (alama 5)

SEHEMU YA B: RIWAYA

Assumpta Matei:Chozi la Heri

Jibu swali la 2 au la 3

  1. . … alijua kwamba msimamo wake huu ungempalia makaa. Lakini alihiari kupoteza riziki yake ili kuyaokoa maisha ya wanyonge wasio na hatia.
    1. Eleza muktadha wa dondoo hili. (alama 4)
    2. Fafanua sifa za anayerejelewa katika dondoo. (alama 4)
    3. Huku ukirejelea wahusika riwayani, thibitisha kuwa hiari ya wahusika inawafanya kujipalia makaa. (alama 12)
  2. … kisha ninaanza kumsimulia yaliyojiri kana kwamba ni mgeni wa hali hii. Ninajua kwamba simsimulii … bali pia Mamia ya Wahafidhina ambao huenda hawajaishuhudia hali hii.
    1. Eleza muktadha wa dondoo hili. (alama 4)
    2. Eleza umuhimu wa usimulizi wa msemaji katika kujenga riwaya ya Chozi la Heri. (alama16)

SEHEMU YA C: TAMTHILIA

Jibu swali la 4 au la 5

  1. “ Maradhi! Madhila yake hayasemeki. Yakimla mtu humthakilisha. Humwacha hoi hana mbele wala nyuma.Yakitaka huzichezea dawa mwajificho. Dawa zikiingilia huku, maradhi hutokezea pale hali pesa zinakwenda, shughuli zinasimama ... Dunia ina mitihani tosha lakini panapo maradhi sugu, uzito wake haumithiliki.”
    1. Eleza muktadha wa dondoo hili. (alama 4)
    2. Bainisha mbinu nne za kimtindo zilizotumiwa kwenye dondoo. (alama 4)
    3. Huku ukirejelea hadithi, eleza sifa sita za msemaji wa kauli hii. (alama 12)
  2. Sara: Nilipopata harufu ya mahamri nilijua bila shaka kwamba baba yako ameingia jikoni.
    Neema: Mama sijaona baba akipika hivi karibuni.
    Kwa kurejelea nukuu zilizotolewa hapa juu, fafanua usasa na utamaduni vilivyosawiriwa tamthiliani. Kila upande utawe na hoja kumi kumi. (alama 20)

SEHEMU YA D: USHAIRI

  1. Soma shairi lifuatalo kisha ujibu maswali

    Soma waliosoma, masomo wa zama soma,
    Soma hata wangasoma, wasome na kusosoma,
    Soma mwisho watasoma, kusoma kuyosoma,
    Soma somato msoma, wasoma wambe kusoma.

    Soma ya leo msoma, soma siwache wasoma,
    Soma akiliyo choma, kisomo cha waliosoma,
    Soma hata wangasoma, mizomo haitachoma
    Soma somato msoma, wasoma wambe kasoma.

    Soma ja samaki shoma, kusoma kuno kushoma,
    Soma wa jana mshoma, bado kitu hajashoma,
    Soma kuno ndo kusoma, kushoma bila kuchoma,
    Soma somato msoma, wasoma wambe kasoma.

    Soma waseme wasoma, ya kwamba hawajasoma,
    Soma wakusome soma, mbwa wapi yuno msoma?
    Soma wakisoma soma, washindwe yako kusoma,
    Soma somato msoma, wasoma wambe kasoma.

    Soma ya kusomea soma, yasosomwa pia soma,
    Soma masomo kuchoma, masomo yaseme 'soma'!
    Soma siwe ja mzoma, kuzoma siyo kusoma,
    Soma somato msoma, wasoma wambe kasoma.

    Soma walimwengu soma, visomo vyao kusoma,
    Soma kusomoa soma, kushomashoma kusoma,
    Soma kusoma msoma, kisichosomwa kusoma,
    Soma somato msoma, wasoma wambe kasoma.

    Soma hata ungasoma, jua bado hujasoma,
    Soma kuna walosoma, kwao utakuwa joma,
    Soma msomaji soma, hakuna tama kusoma,
    Soma somato msoma, wasoma wambe kasoma.
    (Hamisi Babusa)

    Maswali
    1. Eleza mbinu alizotumia mshairi ili kukidhi mahitaji ya kiarudhi. (alama 2)
    2. Fafanua bahari katika shairi hili kwa kuzingatia vigezo vifuatavyo: (alama 3)
      1. Idadi ya vipande
      2. Mpangilio wa maneno
      3. Mpangilio wa vina
    3. Chambua ubeti ya nne kiarudhi. (alama 3)
    4. Bainisha vipengele vya kimtindo katika shairi hili. (alama 2)
    5. Fafanua aina zozote tatu za urudiaji katika shairi hili. (alama 3)
    6. Andika ubeti wa mwisho kwa lugha nathari. (alama 4)
    7. Eleza toni katika shairi hili. (alama 1)
    8. Fafanua maana ya maneno yafuatayo kama yalivyotumika katika shairi hili. (alama 2)
      1. Zoma
      2. Tama

SEHEMU YA E: HADITI FUPI

Rachel Wangari: Fadhila za Punda

  1.  “Nisikuone tena ofisini mwangu, mwanamke wewe. Kuja kuniaibisha, wapinzani wangu waseme nimeshindwa kumdhibiti mke wangu, sembuse kaunti nzima!”
    1. Bainisha muktadha wa dondoo hili. (alama 4)
    2. Eleza toni katika muktadha huu. (alama 2)
    3. Asasi ya ndoa imo hatarini. Jadili ukweli wa kauli hii kwa kurejelea mandhari ya dondoo hili. (alama 4)
    4. Jadili namna mbinu zifuatazo zilivyotumiwa na mwandishi wa hadithi Msiba wa Kujitakia. (alama 10)
      1. Kinaya
      2. Mbinu rejeshi

        Clara Momanyi: Mapambazuko ya Machweo
  2. “…umeniita tukae hapa kando ya barabara kwa nini lakini?
    1. Weka dondoo hili katika muktadha wake. (alama 4)
    2. Eleza sifa zozote nne za Mzee Makucha. (alama 4)
    3. Fafanua changamoto zinazowakumba msemaji na msemewa pamoja na wenzao katika hadithi hii ya Mapambazuko ya Machweo”. (alama 6)
    4. Jadili visababishi vyovyote sita vya matatizo yanayowakumba wahusika katika hadithi ya Harubu ya Maisha. (alama 6)

MARKING SCHEME

  1. FASIHI
    1.  
      1. Ainisha utungo huu kwa kuzingatia kipengele cha maudhui. (alama 1)
        Mbolezi 1×1=01
      2. Andika sababu tatu kuthibitisha jibu lako la a(i). (alama 3)
        1. Lugha hisishi – inaibua hisia nzito za huzuni
        2. Anataja Ziraili – Malaika wa kifo
        3. Toni ya huzuni – anasema alivaliwa na ukiwa
        4. Unataja sifa nzuri za marehemu
        5. Anazungumza moja kwa moja na marehemu
        6. Inaonyesha nguvu za Muumba – kifo na faradhi
        7. Inaonyesha Imani kuhusu chano cha kifo (za kwanza 3×1=03)
    2. Bainisha sifa mbili za jamii inayosawiriwa wa utungo huu. (alama 2)
      1. Washirikina – anasema atabaki kusaka aliyesababisha ndwele ya mpenziwe
      2. Wanaamini katika nguvu za majaliwa – kifo ni faradhi (za kwanza 2×1=02)
    3. Fafanua vipengele vinne vya kimtindo ambavyo vimetumiwa kufanikisha uwasilishaji wa utungo huu.    (alama 4)
      1. Ritifaa – mpenzi anazungumza na aliyekufa kama kwamba yu pale.
      2. Taswira – wimbo mzima umejaa picha ya huzuni/ukiwa
      3. Nidaa/siyahi – kumbe mwenzangu kaniacha!
      4. Tashihisi/uhaishaji/uhuishi – ukiwa ulinivaa
      5. Mbinu rejeshi/ kisengere nyuma – mwimbaji anakumbuka siku ya kufunga ndoa
      6. Sitiatri – kifo kinalinganishwa moja kwa moja na nduli
      7. Nahau – funga nikahi – ndoa
      8. Balagha – ama jicho la hasidi limekuangamiza jamani?    (Za kwanza 4×1=04)
    4. Tungo za aina hii zinaendelea kufifia katika jamii yako. Fafanua hoja tano utakazotumia kuishawishi jamii yako kukinga dhidi ya hali hii.      (alama 5)
      1. Kuufanyia utafiti nyimbo za mbolezi
      2. Kuzihifadhi nyimbo hizi kwenye vitabu na kanda za sauti
      3. Kufundisha nyimbo hizi katika jamii
      4. Kuwasilishwa kupitia vyombo vya Habari
      5. Kuzitumia katika uwasilishaji wa tanzu zingine – hadithi
      6. Kuwarithisha vijana
      7. Kutumiwa kuwasilisha tanzu za fasii andishi kama vile riwaya, tamthilia na haithi fupi (za kwanza 5×1=05)
    5. Unanuia kutumia mbinu ya kushiriki kufanya utafiti kuhusu tungo za aina hii. Eleza sababu tano za kuchagua mbinu hii.                  (alama 5)
      1. Mtafiti anapata habari za kutegemewa zaidi kwa vile anashiriki katika uwasilishaji wenyewe.
      2. Anaweza kuuliza maswali hapo hapo na kusaidiwa kupata hoja
      3. Anaweza kupatasifa kama vile za sauti ambazao hawezi kupata kupitia hojaji
      4. Ni njia ya kufidia wale wahojiwa ambao wana changamoto za kujieleza
      5. Mtafiti anapata taathira ya moja kwa moja kuhusu wimbo husika
      6. Mtafiti anaweza kutumia fursa hii kujenga uhusiano wa karibu na wanajamii husika na kupata habari za kutegemewa 
      7. Mtafiti anapata picha halisi ya aina, sifa na amajukumu ya wimbo wenyewe
      8. Ni njia ya kukinga dhidi ya kupotea au kufisidiwa kwa data au habari kwa sababu mtafiti anazikusanya papo hapo
        (Za kwanza 6×1=06
  2. . … alijua kwamba msimamo wake huu ungempalia makaa. Lakini alihiari kupoteza riziki yake ili kuyaokoa maisha ya wanyonge wasio na hatia.
    1. Eleza muktadha wa dondoo hili. (alama 4)
      1. Ni maelezo ya mwandishi.
      2. Anamrejelea Lunga
      3. Lunga alikuwa mkulima katika Msitu wa Mamba baada ya kutaafishwa mapema.
      4. Mwandishi anasimulia kuhusu msimamo wa Lunga kutokubali kuidhini uuzaji wa mahindi yenye sumu.    4 x 1 = 4
    2. Fafanua sifa za anayerejelewa katika dondoo. (alama 4)
      1. Mwenye bidii– alikuwa amesomea kilimo ambapo baadaye aliaajiriwa kama Afisa wa Kilimo Nyanjani.
      2. Mhifadhi mazingira – Aliasisi Chama cha Watunza Mazingira Wasio na Mipaka akiwa shuleni. Mwandishi anasema kuwa, Lunga Kiriri alikuwa amrijeshi wa uhifadhi wa mazingira.
      3. Mwenye bidii – Baada ya kustaafishwa anafanya kazi ya ukulima kwa bidii hadi anaitwa kwa jina la msimbo Mkulima Namba Wani.
      4. Mwenye msimamo thabiti – licha ya rai za wakubwa anapinga tendo la kuwapa raia mahindi yaliyoharibika.
      5. Mtetezi wa haki – anahiari kupoteza riziki yake ili kuyaokoa maisha ya wanyonge wasio na hatia.
      6. Mwenye tamaa – awali alikuwa na nia ya kumwondoa babake katika Msitu wa Mamba lakini anapoona uzuri wa zao la mahindi katika shamba la babake anapatwa na uchu unaolemaza uadilifu wake. Anatamani kulima maekari na maekari zaidi katika Msitu wa Mamba ili kukuza mimea ya kuuza.
      7. Mwenye mapenzi – Lunga alijisabilia kwa hali na mali kumridhia na kumpendeza mkewe (uk. 81).
      8. Ametamauka – Baada ya kuachwa na mkewe, Lunga aliingiwa na kihoro kilichomsababishia uwele wa shinikizo la damu. Hatimaye anafariki.
      9. Mwenye kuandamwa na mikosi – Lunga anakumbana na mikosi mbalimbali kama vile kuachishwa kazi, kuachwa na mkewe na kufukuzwa kutoka Msitu wa Mamba.
      10. Mwenye imani/huruma – anahiari kupoteza kazi yake ili kuyaokoa maisha ya wanyonge wasio na hatia.
      11. Mlumbi – kila Ijumaa alipokuwa shuleni, angewahutubia wenzake kwenye gwaride kuhusu uhifadhi wa mazingira.
        Zozote 4 x 1 = 4
    3. Huku ukirejelea wahusika riwayani, thibitisha kuwa hiari ya wahusika inawafanya kujipalia makaa. (alama 12)
      1. Lunga kupinga uuzaji wa mahindi yaliyoagizwa kutoka ughaibu kwa kuwa yalikuwa yameharibika. Hali hiyo inasababishwa Lunga kustaafishwa mapema kama mkurugenzi katika Shirika la Maghala na Fanaka.
      2. Makaa kujaribu kuwaokoa waliochomeka kutokana na lori la mafuta waliyokuwa wakipora kushika moto. Tendo la makaa kujaribu kuwaokoa wahasiriwa wa moto linasababisha kifo chake baada ya kuteketea pia.
      3. Sauna na Bi Kangara kushiriki biashara ya utekaji nyara wa watoto. Tendo hilo linasababisha Sauna kukamatwa na polisi.
      4. Mamake Sauna kumlazimisha Sauna kuavya mimba. Tendo hilo linamfanya Sauna kutoroka nyumbani kwao.
      5. Zohali kushiriki mapenzi shuleni. Kutokana na tendo hilo, Zohali anapata ujauzito na baadaye kufukuzwa shule.
      6. Zohali kutoroka nyumbani kwao. Zohali anapotoroka nyumbani kwa kufanyishwa kazi nyingi anaishia kupata matatizo chungu nzima mjini.
      7. Terry kupuuza hofu ya Ridhaa kwa kuona kama ushirikina. Baadaye Terry anateketea hadi kufa baada ya kuchomwa na kedi
      8. Selume kumuunga mkono Mwekevu. Kutokana na Selume kuhiari kumuunga mkono Mwekevu anaonewa na wakwe zake hivyo hatimaye kutoroka kwake.
      9. Selume kutoroka kwake kwa kuwa wakwe zake walimshutumu kwa kumuunga mkono Mwekevu kunamfanya yeye kutenganishwa na mwanawe Sara.
      10. Tindi anapuuza ushauri wa mamake kurejea nyumbani kabla ya saa kumi na moja magharibi. Mapuuza hayo yanasababishwa kuuawa kwa Lemi hivyo Tindi kujuta.
      11. Ridhaa kununua kiwanja katika eneo lililotengewa upanuzi wa barabara. Hali hiyo inamsababishia hasara baada ya majumba yake kubomolewa.
      12. Naomi kutoroka ndoa yake. Tendo hilo linamfanya Naomi kujuta kwa kutenganishwa na wanawe.
      13. Tuama kupashwa tohara. Tendo hili linamletea Tuama shida kwa kuwa anatokwa na damu nyingi.
      14. Kipanga kunywa kangara. Kipanga ananusurika kifo kilichowaua watu sabini na baadaye Kipanga analazwa katika hospitali ya Mwanzo Mpya.
      15. Mwangeka na Mwangemi kumtania Mwimo Msubili. Kutokana na tendo hilo wao wanaadhibiwa vikali.
      16. Mwangeka na Tila wanaigiza mazishi ya ndugu ya Dede, na baadaye  Mwangeka kuadhibiwa na baba yao, Ridhaa
      17. Pete kushiriki ulevi. Kutokana na ulevi, Pete anabakwa na mwanamume anayempachika mimba.
      18. Fumba kushiriki mapenzi na mwanafunzi wake, Rehema. Hali hiyo inasababishwa Fumba kusimamishwa kazi kwa muda.
        Zozote 12 x  1 = 12
  3. … kisha ninaanza kumsimulia yaliyojiri kana kwamba ni mgeni wa hali hii. Ninajua kwamba simsimulii … bali pia Mamia ya Wahafidhina ambao huenda hawajaishuhudia hali hii.
    1. Eleza muktadha wa dondoo hili. (alama 4)
      1. Msemaji ni Kaizari
      2. Alikuwa akimrejelea Ridhaa
      3. Walikuwa katika Msitu wa Mamba.
      4. Kaizari alikuwa anaanza kumsimulia Riadhaa kuhusu chanzo cha vita vya wenyewe kwa wenyewe na matokeo yake.
        4 x 1 = 4
    2. Eleza umuhimu wa usimulizi wa msemaji katika kujenga riwaya ya Chozi la Heri. (alama 16)
      1. Kuonyesha chanzo cha vita. Wahafidhina wanapigana wenyewe kwa wenyewe kwa sababu kiongozi mwanamke alikuwa amechaguliwa.
      2. Kubainisha desturi za wahafidhina – Kaizari anasema kuwa kulingana na desturi za Wahafidhina mwanamke hakufaa kuiongoza jamii hiyo.
      3. Kuonyesha ubaguzi dhidi ya wanaume katika jamii ya Wafadhina. Kaizari anasimulia jinsi Tetei alivyoeleza jinsi mwanamke alivyotetewa katika vyombo vya habari huku mwanaume akipuuzwa.
      4. Kuonyesha kuwa Mwekevu alikweka juhudi ili kuchaguliwa. Kupitia usimulizi wa Kaizari. Tunaelezwa kuwa Mwekevu alijitosa, akaomba kura kama walivyofanya wapinzani wake.
      5. Kubainisha washiriki wa vita. Kwa mujibu wa Kaizari walioshiriki katika vita vya wenyewe kwa wenyewe walikuwa wafuasi wa Mwekevu na wale wa mpinzani wake.
      6. Kuonyesha jinsi siasa zinavyoweza kuwatenganisha wanajamii. Kwa mujibu wa usimulizi wa Kaizari, waliopigana walikuwa wafuasi wa Mwekevu na mpinzani wake ambao awali waliishi kama majirani na kushirikiana katika shughuli anuwai
      7. Vita vilisababisha vifo na uharibifu wa mali. Kaizari anasema kuwa, katika mchezo wa polisi na raia kukimbizana mamia ya roho zisizo na hatia zilisalimu amri.
      8. Kuonyesha kuwa Wahafidhina walihama kwao/ kuwa wakimbizi kutokana na vita. Kaizari anadai kuwa, misafara kwa misafara ya watu walihama kwao bila kujua waendako.
      9. Kubainisha ubakaji uliotendewa Lime na Mwanaheri. Kundi la mabarobaro linawabaka Lime na Mwanaheri mbele ya Kaizari, baba yao.
      10. Kubainisha elimu duni vyuoni. Kijana aliyevalia shati lililoandikwa ‘Hitman’ analalamika kuhusu elimu wanayopata chuoni kwa kuwa ni ya nadharia tu.
      11. Kuonyesha unafiki wa wanasiasa - Kijana aliyevalia shati lililoandikwa ‘Hitman’ anaeleza jinsi wanasiasa wanavyowapa vijana ahadi za kazi ila baada ya kuchaguliwa wanawapuuza vijana hao.
      12. Kuonyesha ufisadi katika shughuli za uchaguzi - Kijana aliyevalia shati lililoandikwa ‘Hitman’ anaeleza jinsi walivyotumiwa na wanasiasa kuwadanganya ajuza kupiga kura visivyo.
      13. Kubainisha wema wa Tulia – Tulia, jiraniye Kaizari alienda kuwaokoa kwa kuwaambia watoke kama bado walikuwa wanathamini uhai wao. Aidha, anamsaidia Kaizari kufunganya na kumsindikiza hadi njia panda.
      14. Kuonyesha changamoto zilizowakumba wakimbizi katika Msitu wa Mamba kama vile kukosa makazi, vyakula, magonjwa na ukosefu wa misala.
      15. Kuonyesha jinsi vita vilivyosambaratisha familia. Selume analazimika kutoroka kwake kwa kuwa wakwe zake walimshutumu kwa kumuunga mkono Mwekevu.
      16. Kubainisha umuhimu wa mashirika kidini katika kuwasaidia wakimbizi. Selume anawaeleza kina Kaizari kuwa, misikiti na makanisa yalikuwa yamekusanya magunia ya vyakula kuwalisha wahasiriwa wa vita. Zozote 16 x 1 = 16

SEHEMU YA C: TAMTHILIA

  1. “ Maradhi! Madhila yake hayasemeki. Yakimla mtu humthakilisha. Humwacha hoi hana mbele wala nyuma.Yakitaka huzichezea dawa mwajificho. Dawa zikiingilia  huku, maradhi hutokezea pale hali pesa zinakwenda, shughuli zinasimama ... Dunia ina mitihani tosha lakini panapo maradhi sugu, uzito wake haumithiliki.”
    1.  
      1. Msemaji ni Neema 
      2. Ni uzungumzi nafsia wa Neema.
      3. Alikuwa kwao nyumbani
      4. Anawaza kuhusu maradhi ya mamake ambayo yamemwacha hoi huku wakifukarika kwa gharama ya juu ya matibabu.
        (Hoja zozote 4x1=4)
    2. Mbinu za kimtindo
      1. Siyahi – maradhi!
      2. Uhuishi/tashhisi – maradhi kumla mtu, pesa zinaenda, shughuli zinasimama
      3. Tanakuzi – hana mbele wala nyuma
      4. Msemo – hana mbele wala nyuma
      5. Jazanda – mitihani ( changamoto/matatizo maishani)
      6. Taswira muonjo - yakimla mtu
      7. Taswira mwendo – pesa zinakwenda
      8. Taswira hisi – uzito wake haumithiliki      (Hoja 4x1=4)
    3. Sifa sita za msemaji (Neema)
      1. Mwenye bidii- anafanya kazi ya kuuza tarakilishi kuanzia asubuhi sana hadi jioni.
      2. Mwenye huruma- anapoelezwa na mamake jinsi babake alivyofutwa kazi baada ya kuzamia ulevi, anamhurumia na kutamka”Maskini!” Uk. 19
      3. Mtambuzi- anaelewa kuwa tatizo la ugonjwa wa mamake limesababishwa na ugomvi wa babake. Uk. 24
      4. Mwenye utani- anamtania mamake na kusema amekuwa wakili hodari wa mlevi wake. Uk. 21. Hapa Sara anamtetea mumewe.
      5. Mwenye heshima- mumewe anapomwita anaitika “Bee!” na kuelekea sebuleni alipo. Uk. 25
      6. Mwenye mapenzi ya dhati- anapozungumza na mumewe anamrejelea kama “mume wangu” uk. 25
      7. Mwenye busara- anamweleza mumewe kuwa mwanao Lemi ameimarika kielimu kwa kuongeza alama zake japo alikuwa ameshuka kidogo kwenye nafasi yake katika darasa.
      8. Mnyenyekevu- anapomtaka mumewe amsaidie kugharamia matibabu ya mamake, anasema naye kwa upole sana, “... ninakuomba tu unitilie pondo ili angalau mzigo huu wa mama uwe mwepesi” uk. 39
        (Hoja za kwanza 6x2= 12)
  2. Sara: Nilipopata harufu ya mahamri nilijua bila shaka kwamba baba yako ameingia jikoni.
    Neema: Mama sijaona baba akipika hivi karibuni.
    Kwa kurejelea nukuu zilizotolewa hapa juu, fafanua usasa na utamaduni vilivyosawiriwa tamthiliani. Kila upande uwe na hoja kumi kumi.  (Alama 20)
    Usasa
    1. Wasichana kupata elimu - Neema anapata elimu tofauti na Mamake Sara ambaye utamaduni haukumruhusu msichana kupata elimu.
    2. Kuna matibabu ya kisasa - Sara anapelekwa ambako huduma ni nzuri kuliko hotelini (uk 42)
    3. Kuajiri wafanyakazi wa nyumbani - Neema anawaajiria wazazi wake wafanyakazi wa nyumbani tofauti na kitamaduni ambapo watoto ndio hufanya kazi nyumbani.
    4. Utepetevu wa kizazi cha kisasa - Wafanyakazi wa Mzee Yona na Sara wanapoondoka, Sara anasema kizazi cha sasa hakitaki kufanya kazi.
    5. Elimu kama kigezo cha kuwa kwenye ndoa - Mzee Yona anauliza Neema angepata wapi ndoa kama sio elimu waliyompa.
    6. Thamani ya mtu ni uwezo wake wa kiakili - Kiwa anamwambia Dina kuwa dunia ya leo haithamini kimo, inathamini akili.
    7. Wanawake kumiliki na kuwa na uwezo wa kuendesha gari - Dina anaajabia Neema kuwa na gari na kwamba analiendesha mjini mwenyewe.
    8. Miji ya kisasa - Mijini kuma watu wengi, magari mengi, barabara nyingi na majengo makubwa.
    9. Kazi kuwanyima wazazi nafasi kuonana na watoto wao - Neema hapati muda kuonana na Lemi kwa anapotokea kazini kazini hupata Lemi amelala.
    10. Watoto kusomea shule za bweni - Neema na Bunju wanampeleka Mina shule ya bweni ili apate elimu bora.
    11. Jukumu la kukithi mahitaji ya familia kuwa la mume - Bunju analipa karo ya shule, ananunua mavazi, anamnunulia mkwewe gari na mahitaji mengine.
    12. Baadhi ya wazazi kuishi na watoto wao nyumba moja - Neema anasema kuna wazazi wanaoishi na watoto wao nyumba moja tena ndogo.
    13. Kuishi katika mazingira ya ufinyu - Asna anahiari kuishi chumba kidogo na kuwa na vitu vichache mjini kuliko kuishi kijijini ambapo kuna nafuu ya gharama na kuna nafasi.
    14. Wanaosoma kuhamia mijini - Asna anaona ajabu kurudi kijijini na elimu yake.
    15. Wembamba wa mwili kuthaminiwa kama kigezo cha urembo - Asna anasema kuwa wengi wanang’ang’ania kuwa wembamba kama yeye.
    16. Utabaka wa mitaa wakakoishi watu - Asna anaishi mtaa wa kifahari ambao si kila mtu anaweza kuishi kwa sababu ya gharama ya juu ya kodi.
    17. Wasichana kutotaka kuolewa - Asna anapinga shinikizo za kuingia kwenye ndoa, anayaona kama maisha ya kuzungushwa kichwa na kusababishiwa machozi kila wakati.
    18. Watoto kupelekwa na wazazi nje kama sehemu ya malezi - Lemi anapania kupelekwa out na wazazi wake.
    19. Michezo ya watoto inagharamiwa - Bunju analalamika kuwa michezo ya watoto siku hizi inanunuliwa sio kama zamani (uk 48)
    20. Wazazi kuwasaidia watoto wao kufanya kazi za shuleni - Bunju anaeleza anavyomsaidia Lemi kufanya homework mara nyingi.
    21. Mwanamke kuwa nje ya nyumbani kwake shughuli za kazi - Bunju analalamika kuwa mkewe Neema mara nyingi yuko nje kikazi.
    22. Waraibu wa ulevi kusaidiwa kujirekebisha - Sara na Asna wanazungumzia jinsi enzi ambapo Mzee Yona alizamia ulevi hakukuwa vituo vya kujirekebisha.
    23. Desturi ya wazee kuonja mavuno ya kwanza haitiliwi maanani - Yona anasema sasa mambo hayo hayatiliwi maanani tena licha ya kuwa ilikuwa desturi nzuri.
    24. Kuna dini za kisasa - Dini zimekuja na kuwakengeusha watu na kuwafanya kuziona mila kuwa chafu kwa mujibu wa Yona.
    25. Watoto kutojua asili yao - Watoto hawajui asili yao bali wanakumbatia uzungu anavyosema Luka (uk 58)
    26. Kizazi cha sasa kuwa na mseto wa tamaduni - Kizazi cha sasa kina kila utamaduni na hivyo kupoteza utamaduni wao.
    27. Watu kutojua lugha zao za asili - Wajukuu wa Yona hawajui neno hata moja la lugha yao. Wanaongea Kiswahili na Kiingeraza.
    28. Kutotofautisha wanyama wa nyumbani - Wajukuu wa Yona na wa Beni wanashindwa kuwatofautisha baina ya kondoo, mbuzi na mbwa.
    29. Malezi ya watoto kuachiwa yaya - Wazazi wengi kwa sababu ya shughuli za kikazi wanaachia malezi ya watoto wao yaya.
    30. Thamani ya mtoto wa kike imepanda - Mtoto wa kike ana thamani na nafasi yake katika jamii imepanuka kwa mujibu wa Luka. Wasichana wanawapiku hata baadhi ya wavulana kwa thamani hata kwa wazazi wao . kwa mfano Neema.
    31. Wanafunzi waadhibiwi kwa kiboko - Yona anaeleza kuwa siku hizi huwezi kumnyoosha mtoto kwa kiboko.
    32. Kuna teknolojia ambayo imerahisisha mambo - Usafiri umekuwa wa haraka na wenye raha (uk 64)
    33. Wanaume kuingia jikoni kupika - Mzee Yona anaingi jikoni na kusaidia katika mapishi. (uk 66)
    34. Wanawake wanashindana na wanaume - Neema anasema anawajua wanawake wengi ambao ni hodari katika kazi zao kuliko wanaume.
      Hoja 10 za kwanza

      Utamaduni
      1. Mke kutegemewa kwa mapishi nyumbani -Yona anamtarajia Sara kumpikia licha ya kuwa Sara amelemewa na maradhi.
      2. Wazazi kuwategemea wanao uzeeni - Yona anashikilia msimamo kuwa Neema ana jukumu la kumshughulikia mamake kwa kuwa walimlea awasaidie uzeeni.
      3. Mtoto wa kwanza kwenye familia kutegemewa na wadogo zake - Neema analazimika kuwaeleimisha wanuna zake hadi chuo kikuu. Yona anasema, “Fimbo ya mzee hurithi mtoto wa kwanza” uk 2
      4. Mtoto wa kiume kutarajiwa kuwarithi wazazi wake - Wanakijiji wanauliza ardhi ya Yona atarithi nani kwa kuwa hana mtoto wa kiume. 
      5. Wanaokosa wato kusemwa - Sara na Yona wanasemwa na wanakijiji kwa kukosa watoto.
      6. Kukosa mtoto wa kiume kuonekana kama kasoro -  Sara na Yona wanasimangwa kwa kukosa mtoto wa kiume.
      7. Kuoa zaidi ya mke mmoja - Watu walimtaka mzee Yona kuoa mke mwingine amzalie watoto wa kiume (uk 9)
      8. Kutukuzwa kwa watu kwenda nje ya ndoa - Mzee Yona anashinikizwa aende nje ya ndoa iliapate mtoto wa kiume atakayekuwa mrithi wake na kuendeleza ukoo(uk 10)
      9. Kupiga mke - Mzee Yona alipokuwa mlevi alimpiga mkewe Sara hadi akapoteza fahamu.
      10. Wanaume kutojali hali za wake zao - Mzee Yona anaonekana kutojali hali ya ugonjwa wa mkewe Sara, Sara anasema ni desturi ya wanaume (uk 13)
      11. Kazi zote za nyumbani kulimbikiziwa wanawake - Wanaume hawasaidii katika chochote, Sara anasema mila na desturi zimefanya hali iwe hivyo.
      12. Wanaume kuwa watepetevu - Dina anasema wanaume hawawezi kusaida kupiga makasia chombo kinapopungukiwa upepo; hawawezi kusadia hata wakati wake zao wamepungukiwa na nguvu za kazi.
      13. Jamii kukosoa mume kusaidia kazi za jikoni - Mwanamme anayesaidia jikoni anaokena kushuka hadhi (uk 14)
      14. Wazazi kutolala kwa wakwe zao - Sara anaondoka kwa Neema kwa kuwa hawezi kulala kwa mwanawe aliyeolewa.
      15. Kuolewa kama jambo la lazima - Sara anamshinikiza Asna kuolewa kwa kuwa anatamani kununuliwa leso na mume wa bintiye.
      16. Watoto wa kike kunyimwa elimu - Sara anasema siku zao elimu ya wasichana ilifanyiwa bezo, jambo liliofanya aachie masomo darsa la sita.
      17. Utegemezi wa familia- Anayefaulu katika familia anatarajiwa kutoa msaada kwa familia yake. Neema analemewa na mahitaji mengi kwa sababu ya jadi aliyotokea.
      18. Mtazamo kuhusu kazi za nyumbani -Sara anapinga kauli ya Asna kwamba babake Mzee Yona babake hawezi kushindwa kuteka maji; wanajiji wangeliona hilo kama ajabu.
      19. Elimu ya kunga za ndoa - Kunga za ndoa zilizingatiwa katika utamaduni ila katika usasa hazifundishwi. Asna anasema shuleni hawafundishi kunga za ndoa.
      20. Wazee kushiriki dhifa pamoja baada ya mavuno - Mzee Yona na wandani wake wanashiriki mlo na kunywa pamoja nyumbani kwa Luka.
      21. Kusaidiana kwa mke na mume ni mwiko - Sara anasema Yona akifanya kazi za nyumbani sana watu watamcheka.
      22. Wasichana wanapewa mafunzo ya unyago - Sara alipewa mafunzo ya unyago na nyanya yake yaliyojumuisha malezi na kudumisha heshima kwa mume. (uk 67)
        Hoja 10 za kwanza

Rachel Wangari: Fadhila za Punda

  1. “Nisikuone tena ofisini mwangu, mwanamke wewe. Kuja kuniaibisha, wapinzani wangu waseme nimeshindwa kumdhibiti mke wangu, sembuse kaunti nzima!”                                                       
    1. Bainisha muktadha wa dondoo hili.    (alama 4)
      1. Ni maneno ya Luka
      2. Anamwambia Lilia
      3. Wako nyumbani
      4. Ni baada ya Lilia kumtembelea Luka ofisini na anapomsubiri Luka anarudi ofisini akiwa na mwanamke mwingine.
    2. Eleza toni katika muktadha huu.                                                                               (alama 2)
      Toni ya hasira na ghadhabu – Luka amekasirika baada ya Lilia kumtembelea na kumfumania akiwa na mwanamke.
      (1x2= 2) Aeleze ndipo atuzwe 2
    3. Asasi ya ndoa imo hatarini. Jadili ukweli wa kauli hii kwa kurejelea mandhari ya dondoo hili.                    (alama 4)
      1. Ndoa imekumbwa na dhuluma – Luka anamdhulumu Lilia kwa kumpokeza kofi linalomfanya kuona vimulimuli.
      2. Imekumbwa na taasubi za kiume – Luka anamwambia Lilia kwamba hawaheshimu wageni wake na kidomodomo chake.
      3. Imekumbwa na vitisho
      4. Imekumbwa  na dharau
      5. Imekosa kuheshimiana
      6. Uasherati/ mahusiano nje ya ndoa    (zozote 4x1= 4)
    4. Jadili namna mbinu zifuatazo zilivyotumiwa na mwandishi wa hadithi Msiba wa Kujitakia. (alama 10)
      1. Kinaya
        1. Zuhura anabaki kujuta ghaya ya kujuta baada ya serikali ya ‘mtu wetu’ kukosa kutimiza ahadi ilhali yeye na wenzake waliwachagua hao viongozi.
        2. Ni kinaya kwamba wanasiasa walitoa ahadi nyingi kwa wapiga kura alkini hakuzitimiza.
        3. Ni kinaya Jimbo la Matopeni liligeuzwa ngome ya watu fulani ambao ni wenye ushawishi mkubwa serikalini ilhali jimbo hili ni la Wanamatopeni wote waliowachagulia viongozi.
        4. Ni kinaya kwa baadhi ya Wanamatopeni kama vile Zuhura kulalamika kwamba walichagua kiongozi kwa kununuliwa khanga, sukari, unga na mafuta ilhali hakusikiliza onyo la Machoka la kuchagua viongozi bora wala si kwa kigezo cha kikabila.
        5. Ni kinaya kwa Zuzu Matata kumwachia Mzee Sugu Junior kutawazwa uongozi wa Matopeni ambapo baada ya miaka anajaribu kuliongoza eneo hilo lakini hapati nafasi ya kuwa kiongozi.
        6. Ni kinaya kwamba katika Jimbo la Matopeni kupiga kura si hoja, hoja ni kuhesabu kura.  (zozote 5x1= 5)
      2. Mbinu rejeshi
        1. Machoka anakumbuka na kukariri shairi alilowahi kulisoma kimyakimya
        2. Kupitia mbinu rejeshi, tunapata kujua kwamba Jimbo la Matopeni lilikombolewa kutoka mikono ya walowezi.
        3. Mbinu rejeshi imebainisha viongozi wa awali wa Jimbo la Matopeni kama vile, Mzee Sugu Senior
        4. Kupitia mbinu rejeshi tunabainishiwa kuwa uongozi wa Jimbo la Matopeni limekuwa liking’ang’aniwa na familia mbili – Mzee Sugu Senior na hayati Zuzu Matata
        5. Zuhura anakumbuka namna yeye na wenzake walipanga foleni ndefu kwenye vituo vya kupiga kura.
        6. Kupitia mbinu rejeshi inabainika kuwa Zuzu Matata alifaa kuchukua kiti cha uongozi lakini alikataa mwenyewe.
          (zozote 5x1= 05)

Clara Momanyi: Mapambazuko ya Machweo

  1. “…umeniita tukae hapa kando ya barabara kwa nini lakini?
    1. Weka dondoo hili katika muktadha wake. (alama 4)
      1. Ni kauli ya Dai
      2. Anamwambia Sai
      3. Ni kando ya barabara
      4. Dai anamwuliza Sai swali kwa sababu ya kukosa kazi ya kufanya na hakuwa anaona matumaini       ( 4×1=04)
    2. Eleza sifa zozote nne za Mzee Macheo. (alama 4)
      1. Mtambuzi – anatambua kwamba Mzee Makutwa alikuwa anawatumia vijana vibaya
      2. Mdadizi
      3. Aliyewajibika
      4. Mwenye mapenzi ya dhati     (za kwanza 4×1=04)
    3. Fafanua changamoto zinazowakumba msemaji na msemewa pamoja na wenzao katika hadithi hii ya Mapambazuko ya Machweo”. (alama 6)
      1. Ukosefu wa ajira
      2. Ndoa za mapema – Riziki kuoleka angali na umri mchanga
      3. Msongo wa mawazo – Dai na Sai wanajiona kama masazo wa miji
      4. Hali ngumu ya maisha
      5. Kufanya kazi katika mgodi
      6. Kukosa elimu hata ya darasa la kwanza
      7. Kutoruhusiwa kutoka nje mgodini
      8. Kulala katika mazingira duni – wanalala mabandani
      9. Kushindwa kupata namna ya kujiokoa mgodini kutokana n au wa stim ana mabawabu katili     (zozote 6×1=06)
    4. Jadili visababishi vyovyote sita vya matatizo yanayowakumba wahusika katika hadithi ya Harubu ya Maisha. (alama 8)
      1. Kuchelewa kwa mshahara
      2. Deni - Fundi anamsababisia Mama Kikwai na Kikwai wasiwasi
      3. Njaa
      4. Maonjwa
      5. Majeraha
      6. Kazi nyingi
      7. Kutovumiliana katika ndoa
      8. Simu      (zozote 6×1=06)
Join our whatsapp group for latest updates

Download Kiswahili Paper 3 Questions and Answers - Mokasa 1 Joint Pre Mocks Exams 2023.


Tap Here to Download for 50/-




Why download?

  • ✔ To read offline at any time.
  • ✔ To Print at your convenience
  • ✔ Share Easily with Friends / Students


Get on WhatsApp Download as PDF
.
Subscribe now

access all the content at an affordable rate
or
Buy any individual paper or notes as a pdf via MPESA
and get it sent to you via WhatsApp

 

What does our community say about us?