Kiswahili Paper 2 Questions and Answers - Mokasa 1 Joint Pre Mock Exams 2023

Share via Whatsapp
Maagizo
  • Jibu maswali yote
  • Maswali yote ni sharti yaandikwe kwa lugha ya kiswahili
  1. UFAHAMU   (alama 15)
    Soma makala yafuatayo kwa makini kisa ujibu maswali yanayofuata.


    ‘Hamjambo wananchi? Ni fursa kubwa kwangu kusimama hapa kwa niaba ya wachukuzi, makuli, wakulima, waashi, masonara na wengine wote wanaokandamizwa ili kufaamishana kwamba tumeamidi kugoma kuanzia kesho kutwa. Madhila yanayotusakama hayaitaji mtaalamu ili kutuchambulia. Watoto wetu wamebaki nyumbani tangu kufunuliwa kwa shule kwa sababu ya kukosa kutimiza mahitaji ya kimsingi kwa ajili ya masomo yao. Aina haja kukumbushana kuhusu adha za wenye nyumba kwa sababu ya kulimbikiziwa kodi pasi na kujali maslahi ya wapangaji. Si hanikizo la uvundo, si mrundiko wa taka, si maji taka yaliyovavagaa, si ukuukuu wa majengo na rangi zinazoning’inia, si maji ya kubahatisha  ilmuradi hali si hali hapa. Malalamishi yetu ama yanaangukia masikio yenye nta au yaliyozibwa kwa komango. Mwisho wa mwezi hawachelewi kunyoosha mkono kudai kodi. Alfajiri unasikia mgongo mlangoni mradi mwezi umeisha;  hawajali kwamba hujalipwa na una kibaba cha kuikimu aila yako. Milungula waliyolishwa wakuu wa kutetea maslahi ya wapangaji katika wizara ya nyumba ilifanya kazi yake barabara – hawajali, bali ukubali yote yasemwayo na wenye nyumba. Ni dhahiri kwamba tumetekwa kikamilifu – mbele simba, mgongoni fisi’.

    Bahati alitongoa hoja zake akisikizwa kwa makini na wenzake, kisha akaendelea:

    ‘Kule mashambani wakulima wanalazimishwa kupeleka mifugo yao kupigwa sindano maalum eti kuzuia magonjwa ambayo hawaambiwa. Ni wazi kwetu kwamba mifugo wakipigwa sindano watakufa. Hapana anayejua faida ya ng’ombe kupigwa sindano maana ng’ombe wetu wamekuwa wakiumbwa na kjiponea bila hiyo chanjo yao. Wanataka wawapige ng’ombe sindano tu ikiwa watakufa au kupona, si hoja kwao. Tumejifunza kutoka kwa majirani zetu kwamba upigaji sindano ng’ombe umeteketeza ng’ombe. Ni lazima wafugaji wachukue tahadhari katika jambo kama hili kabla ya kuharibikiwa kabisa. Kumbuka wakati ule walipotaka kujenga uwanja wa ndege waliwafurusha wakulima kutoka katika ardhi yao na kuvunja nyumba zao. Madai yao yalikuwa kwamba wenye ardhi walipewa fidia. Hatujui ndege zinazoruka na kutua zina maslahi gani kwetu kama sio zile kelele za kuudhi masikio na kubughudhi usingizi wa wanetu?’

    Mzee Gae, licha ya umri wake, alitafakari mtimani mwake kuhusu mawazo fyongo ya namna hii yaliyomdondoka Bahati kutoka kinywani bila simile. Labda kuhusu yale malalamishi ya kwanza kulikuwa na nafuu ya kukubaliana nayo lakini haya ya chanjo na uwanja wa ndege yalikuwa na taksiri hasa. Lau yangetoka kinywani mwa mzee kama yeye, msamaha ungeweza kufikiriwa. Mzee hangeweza kutabiri kama miaka iendeleavyo ndivyo binadamu anaimarika au anasambaratika kimawazo. Akiwa angali mawazoni hivi, Simali hivi, naye akadakiza usemi wa Bahati kwa hotuba yake fupi:

    ‘ Heri waache tulime mashamba yetu, ndege zibaki huko huko angani au kule zitokako!’
    Stahamala za Mzee Gae zikafika mwisho sasa akaja juu kwa ukakamavu wa ghafla na kuanza …

    ‘Simali unasahau jambo moja. Mgala muue lakini haki yake usimhini. Angatua unayoikejeli imetufaa si haba. Lile gonjwa sugu liliplipuka na kuzua taharuki, madaktari na wauguzi walifikishwa hapa haraka kwa ndege kupitia angatua hiyo. Vyakula vya msaada kwa walioathirika na njaa iliyozuka miaka mitano iliyopita, vilisafirishwa haraka kwa sababu ya kuwepo kwa miundomsingi huu. Wakati wa mafuriko yam waka jana daraja la kutuunganisha na mji mkuu lilisombwa na maji ikawa vigumu kupata mahitaji ya kila siku. Kama sio uwanja huu, nusura yetu ingetoka wapi? Mwanao aliyekuwa mtahiniwa wa mwaka jana hapa petu anaelewa jinsi uwanja huu ulivyomfaa yeye na watahiniwa wenzake vinginevyo katarasi za mitihani zingebaki huko huko kashani. Mengi yaliyowezeshwa na kuwepo kwa uwanja huu yanaonekana sio nuruni  tu bali hata penye giza totoro. Ni kweli kwamba kujengwa kwa uwanja huu kulitatiza malisho na uzalishaji wa mazao ya kilimo lakini kama ilivyo ada shughuli huvunja nyngine. Binadamu yu mbioni kufanya uvumbuzi usiku na mchana ili maisha yake nay a vizazi vya usoni yawe bora zaidi. Anapovumbua kitu kilicho bora kuliko kile alicho nacho, hana budi kuvunja ili kujenga! Si lazima mbegu izikwe ndipo imee?

    ‘Ni kweli kwamba amani haipatikani ila kwa ncha ya upanga. Hata hivyo, amani ijayo kwa njia hii ina gharama kubwa na huwaachia majeraha mengi wahusika kisha makovu yake hudumu milele. Majuto na chuki hukalia viti vya mioyo ya wahusika bila kubanduka. Makuruhu tunayokumbana nayo jinsi Bahati alivyochmbua mwanzoni yanadhihirika na kupinga kuwepo kwake ni hujuma kwa jamii yetu. Lakini katika ulimwengu wa sasa, kunazo mbinu mbadala za kuyasuluhisha. Ulimwengu mzima umesheheni visa vya mizozo baina ya jamii mbalimbali lakini wangwana hufanya vikao vya kimataifa kama njia ya kukumbatia umuhimu wa mashauriano mahali pa kushika zana za vita. Kumbuka hata sasa kuna zana bora sana za kivita zilizobuniwa lakini hakuna taifa lililo na haraka ya kuzitumia kero zinapozuka. Mgomo hautasuluhisha migogoro yetu vyema. Heri tung’ang’anie mazungumzo kwa kuwatuma wajumbe wetu kwa wakuu wetu. Hata hivyo, wajumbe wasijihasiri kwa kupinga swala la chanjo ya ng’ombe dhihi ya maradhi ya miguu na midomo ambayo yamefagia mifugo katika taifa jirani. Maneno hayo!’

    Akatamatisha Mzee Gae na kuketi akitazamwa kwa meno na Bahati na Simali na wote waliokuwa pale. Avuliwapo nguo, muungwana huchutama.

    Maswali
    1. … “tumetekwa kikamilifumbele simba, mgongo fisi”. Kwa kuzingatia hali ya wapangaji, rejelea mifano minne kuthibitisha ufaafu wa kauli hii. (alama 4)
    2. Kwa mifano miwili kwenye makala, thibitisha kinaya katika hotuba ya Bahati au kinachotokea mashambani. (alama 2)
    3. ‘Mgala muue lakini haki yake usimhini’. Kwa kurejelea kifungu, thibitisha kauli hii kwa hoja nne. (alama 4)
    4. Thibitisha kwamba walimwengu wa sasa wanatawaliwa na hekima zaidi ya nguvu katika kusuluhisha migogoro. (alama 2)
    5. Andika visawe vya maneno haya: (alama 3)
      1. Tumeamidi ……………………………………………………………………………..
      2. Yaliyovavagaa …………………………………………………………………………
      3. Walijihasiri ……………………………………………………………………………
  2. UFUPISHO (ALAMA 15)
    Soma kifungu kifutacho kisha ujibu maswali yanayofuata


    Mataifa yanayoendelea  yameathirika pakubwa na mabadiliko ya tabianchi. Hali hii imesababisha misimu mirefu ya kiangazi ambayo hatimaye yamesabisha ukame katika mataifa haya. Nchi nyingi pembeni mwa Afrika zenye maeneo kame yameitisha msaada wa dharura kwani jinamizi hili limesabisha maafa si haba. Taswira katika mataifa haya ni ya kutisha. Taarifa katika vyombo vya habari zimeonyesha mamia ya watu waliokufa kwa sababu ya ukosefu wa vyakula. Wengi wamekuwa watoto wachanga na wazee wasiojiweza. Watoto wamekuwa wakikumbwa na utapiamlo,kwani hata wakiambulia chakula hakitakuwa chenye madini mbalimbali yanayohiyajika mwilini. Utapigwa na butwaa vilevile unapoona watu waliokonda na kudhhofika kiafya.  Huwa tayari wamefika mwisho na kupoteza matumaini huku wakichungulia kifo,yao imekuwa kusubiri misaada kutoka mashirika ya kiserikali na yasiyo ya kiserikali.

    Maji katika nyakati kama hizi za kiangazi huwa nadra kupatikana. Watu wengi hulazimika kutembea kwa kilomita nyingi angalau kupata hata kiasi kidogo cha maji. Hata baada ya kubahatika,hupanga foleni ndefu kwani watu hutegemea sehemu moja kupata maji. Hii ni kwa sababu mito mingi hunyauka na hata visima ambavyo ni vichache pia hunyauka. Maji mengine yanayopatikana huwa machafu. Kwa kuwa wakaazi hawana hiari,huishia kunywa na kuyatumia maji haya nyumbani. Hatima yake ni magonjwa yanatokana na maji machafu. Magonjwa hayo ni vile kama kipindupindu,homa ya matumbo miongoni mwa mengine. Ikumbukwe kuwa,hali katika zahanati za vijijini ni duni. Kando na haya, zahanati ni chache na zilizotengana mithili ya ardhi na mbingu. Watu wengi huaga dunia katika harakati za kutafuta huduma za matibabu ama hata kwa kukosa huduma hizo kabisa. Maelfu  ya mifugo pia wamekuwa wakifa nyakati za kiangazi. Hii ni kwa kukosa lishe na pia maji. Hasara hii inatokea huku wenyeji wakikosa chakula. Mifugo wanaosalia huwa wamekondeana kama wamiliki wao. Hata kuuza ni balaa. Hali hii imekuwa si hali kwa muda sasa. Ni muhimu jambo hili liangaziwe kwa lengo la kupata suluhu ya kudumu.

    Baada ya miezi mingi ya kiangazi,mvua inazuka kwa fujo. Maeneo yaleyale yanaripoti mafuriko. Msaada wa kibinadamu unaanza kuitishwa tena. Vifo vya watu na mifugo vinaanza kushuhudiwa. Maji yaliyokuwa nadra sasa yanapatikana kwa wingi kupita kiasi. Je, serikali za nchi hizi zina mipango madhubuti? Kuitisha misaada nyakati zote mbili hushangaza. Ni muhimu kuzingatia ujenzi wa mabwawa. Huu utakusanya maji yote ambayo yangesabisha maafa na kuhifadhi kwa minajili ya kutumika nyakati za kiangazi. Isitoshe,maji yayo hayo yanaweza kunyunyiziwa mimea na hivyo kuchangia pakubwa katika uzalishaji wa vyakula. Bila shaka,vifo vinavyotokana na uhaba wa vyakula vitapunguzwa na hatimaye kuzikwa katika kaburi la sahau.

    Kuchimba visima vingi na kueneza nguvu za umeme pia kutaimarisha uwepo wa maji ya kunywesha mifugo na kutumika katika shughuli za nyumbani. Ni muhimu kumfundisha mtu kuvua samaki kuliko kumpa samaki kila wakati. Wananchi wafundishwe njia mwafaka za kuendeleza kilimo chenye kipato kikubwa. Huku kutawafanya kuzalisha kiwango kikubwa cha chakula. Kando na kuwafundisha ni kuwahimiza watu walio katika maeneo kame kupanda mimea inayoweza kustahimili angalau muda mrefu wa kiangazi ili isinyauke haraka. Serikali pia ziangazie upya bei ya pembejeo. Mbolea na mbegu zimekuwa bei ghali katika siku za hivi majuzi. Gharama hii imewavunja moyo wakulima wa maeneo ya nyanda za juu na yenye mashamba yenye uwezo wa kuzalisha vyakula vya kulisha maeneno mengine. Kwa sababu hii,kumekuwa hata na uhaba wa vyakula katika maghala ya serikali.

    Kichwa kibaya cha ufisadi hakijakosa kupata mgao wake wa lawama katika suala hili pana la ukame na mabadiliko ya tabianchi. Viongozi wenye ushawishi serikalini wameishia kufuja pesa zinazotengewa ujenzi wa mabwawa,upunguzaji wa bei ya pembejeo na hata usambazaji wazo. Ni lazima umma na serikali ijizatiti katika vita dhidi ya ufisadi ili kuweza kuukomesha. Serikali pia iweze kuimarisha miundo msingi katika maeneno mbalimbali kwani hali duni ya miundo msingi imechangia. Barabara duni zimezuia usambazaji wa pembejeo na mavuno mashambani huku watu wakikosa chakula kicho hicho baadaye.

    Ni lazima wafugaji wapate kuelewa kuwa mifugo wengi bila mipango ni hasara. Waweze kuwa na mifugo wanaoweza kuwashughulikia ili kupunguza hasara za vifo vyao wakati wa kiangazi. Wafugaji na serikali pia washirikiane kuanzisha au kuimarisha bima ya mifugo ili wafugaji wapate fidia wakati mgumu wa kiangazi na ukame. Kando na hilo,watafiti waimarisha mbegu ya mifugo wanaozaliwa kwani hili litaimarisha kipato chao. Kwa kweli,suala la madhara ya mabadiliko ya tabianchi linaweza kukabiliwa kwa kupanda miti mingi. Serikali na wananchi wapande miti katika mashamba ya serikali na ya watu binafsi. Wabinafsi wenye tabia ya kukata miti misituni ovyoovyo,hata katika chemichemi ya mito lazima wakomeshwe kwa kukabiliwa kisheria. Sheria zilizomo zitiwe shime ili kufanikisha vita hivi. Serikali, wananchi,mashirika ya kiserikali na yasiyo ya kiserikali,miungano ya kimaeneo,kibara na kimataifa ikivalia njuga mabadiliko ya tabianchi na madhara yake, tutakuwa na sababu ya kutabasamu.

    Maswali
    1. Fupisha aya  za kwanza kwa maneno 80-90. (Alama 6,1 utiririko)
      Matayarisho
      Nakala safi
    2. Eleza hatua za kukabiliana na madhara ya ukame na mabadiliko ya tabia nchi kwa maneno 100-110 . (Alama 9,1 utiririko)
      Matayarisho
      Nakala safi
  3. LUGHA ( alama 40)
    1. Andika neno lenye sifa zifuatazo: Kipasuo kwamizo hafifu cha kaakaa gumu, irabu ya chini kati, kipasuo hafifu cha kaakaa laini, irabu ya mbele juu. (al. 2)
    2. Dhihirisha dhima ya viambishi katika kitenzi ukupigao. (al. 2)
    3. Itunge sentensi sahihi ukitumia kihusishi kimoja cha mtendaji. (al. 1)
    4. Lugha ukamilishwa kwa ushirika wa vijenzi vyake vidogo vidogo. Vitaje. (al. 2)
    5. Tumia neno maudhui katika sentensi ili kudhihirisha upatanisho wa kisarufi. (al. 2)
    6. Tunga sentensi kudhihirisha wakati ujao hali timilifu. (al. 2)
    7. Akifisha kifungu kifwatacho: nimekuwa nikisisitiza umoja wa afrika daniel moi 1924 2020     (al. 4)
    8. Geuza katika usemi halisi: Askari jela alimuuliza kendi kama alidhani hapo ni kwao. Alimwamuru aende kwake mara moja.     (al. 2)
    9. Bainisha maana mbili ya sentensi hii: Umu alimwandikisha mkewe.  (al. 2)
    10. Changanua kwa matawi:  Watu ambao wana mali hawatoi zaka zao.  (al. 4)
    11. Eleza matumizi ya neno wale katika sentensi hii: Wale walioiba ni mabanati wale ambao waliambiwa wale kabla ya kitendo hicho.
      (al. 3)
    12. Ainisha virai vilivyopigiwa mstari katika sentensi ifuatayo: Yule mtiifu atatuzwa kesho jioni na mwalimu mkuu (al. 2)
    13. Bainisha aina ya yambwa na chagizo katika sentensi:Binti yake Kimani aliozwa Luka kwa harusi mwezi uliopita.  (al. 2)
    14. Amrisha kwa kutumia kitenzi nywa katika nafsi ya pili (al. 1)
    15. Tunga sentensi moja kuonyesha maana mbili za neno chupa (al. 2)
    16. Tumia neno sembuse katika hali  kanushi kutunga sentensi (al. 2)
    17. Neno sema ni kitenzi, libadili liwe kielezi kwa kutungia sentensi. (al. 2)
    18. Andika katika ukubwa wingi: Kitoto hiki kinalia kwa sababu hakijala mkate. (al. 2)
    19. Tunasema ng’ang’ana kukutu,vunjika ……………………..pelekwa ………………….….(al. 1)
  4. ISIMUJAMII        (alama 10)
    1. Eleza sifa zozote tano zinazotambulisha sajili ya mazungumzo. (alama 5)
    2. Andika sifa tano za kimtindo utakazotumia ukipata fursa ya kutangaza mchezo wa kandanda shuleni.     (alama 5)

MARKING SCHEME

  1.  
    1. … “tumetekwa kikamilifu – mbele simba, mgongo fisi”. Kwa kuzingatia hali ya wapangaji, rejelea mifano minne kuthibitisha ufaafu wa kauli hii. (alama 4)
      1. Kuna uvundo uliohanikiza katika nyumba za wapangaji
      2. Kuna taka zilizorundikana kwenye makazi ya wapangaji
      3. Kuna adha/kero ya majitaka makazini mwa wapangaji
      4. Majengo ya wapangaji ni makuukuu
      5. Majengo hayo yamebambuka rangi
      6. Hakuna mai katika nyumba hizo
      7. Wapangaji wanalimbikiziwa kodi ghali  (za kwanza 4×1=4)
    2. Kwa mifano miwili kwenye makala, thibitisha kinaya katika hotuba ya Bahati au kinachotokea mashambani. (alama 2)
      1. Mifugo wakipigwa sindano wanakufa/ ng’ombe wanaumwa na kujiponea bila chanjo
      2. Ujenzi wa uwanja wa ndege kwa kuwafurusha wakulima kutoka ardhi yao na kuvunja nyumba zao / uwanja wa ndege una manufaa  kuliko zaraa /  kilimo ilhali ardhi walipewa fidia (za kwanza 2×1=2)
    3. ‘Mgala muue lakini haki yake usimhini’. Kwa kurejelea kifungu, thibitisha kauli hii kwa hoja nne. (alama 4)
      1. Uwanja wa ndege ulisaidia madaktari na wauguzi kufika haraka kutatua ugonjwa sugu.
      2. Vyakula vya msaada kwa waathiriwa wa njaa vilifikishwa haraka.
      3. Mahitaji ya kila siku yalifikishwa kwani daraja la kuunga mji mkuu wa mashambani lilikuwa limesombwa
      4. Mitihani ilifikishwa kwa wanafunzi (za kwanza 4×1=4)
    4. Thibitisha kwamba walimwengu wa sasa wanatawaliwa na hekima zaidi ya nguvu katika kusuluhisha migogoro. (alama 2)
      • Wanafanya vikao vya mashauriano kunapokuwa na mizozo badala ya kupigana vita / sasa kuna zana bora za kivita zilizobuniwa lakini hakuna aliye na haraka ya kuzitumia kero zinapozuka   (1×2=2)
    5. Andika visawe vya maneno haya: (alama 3)
      1. Tumeamidi – tumeamua/ tumeazimia/ tumepania 
      2. Yaliyovavagaa  - yaliyotapakaa/ yaliyoenea/ yaliyosambaa
      3. Walijihasiri  - walijiumiza/ walijiharibu/ walijiangamiza/ walijitesa/ -dhuru, -vinja, - chongea
        (Adumishe kauli)
  2.  
    1. Fupisha aya  za kwanza kwa maneno 90-100. (Alama 6,1utiririko)
      1. Mataifa yanayoendelea yameathirika pakubwa na mabadiliko ya tabianchi na madhara ukame.
      2. Nchi nyingi pembeni mwa Afrika zenye maeneo kame yameitisha msaada wa dharura.
      3. Mamia ya watu wamekufa kwa sababu ya ukosefu wa vyakula.
      4. Watu pia wamedhoofika kiafya kwa sababu ya uhaba wa vyakula.
      5. Kiangazi kimesababisha uhaba wa maji. 
      6. Watu wanalazimika kutembea kilomita nyingi angalau kupata hata kiasi kidogo cha maji.
      7. Maji mengine yanayopatikana huwa machafu na hivyo kusababisha magonjwa. 
      8. Watu wanaaga dunia kwa kukosa huduma za matibabu. 
      9. Mifugo wengi hufa kwa kukosa maji na vyakula kwa sababu ya ukame.
    2. Eleza hatua za kukabiliana na madhara ya ukame na mabadiliko ya tabianchi. (Alama 9,1 utiririko)
      NJIA YA KUKABILIANA YA MADHARA YA MABADILIKO YA TABIANCHI NA UKAME.
      1. ujenzi wa mabwawa kwa ajili ya unyunyiziaji wa maji
      2. uchimbaji wa visima
      3. kupunguza bei ya pembejeo na mbolea
      4. wananchi wafundishwe njia mwafaka za kuendeleza kilimo chenye kipato kikubwa cha chakula.
      5. wakulima wahimizwe kupanda mimea inayoweza kustahimili angalau muda mrefu wa kiangazi
      6. ufisadi ukabiliwe vikali
      7. lazima wafugaji wafuge mifugo wanaoweza kuwashughulikia ili kupunguza hasara
      8. wafugaji na serikali washirikiane kuanzisha au kuimarisha bima ya mifugo ili wafugaji wapate fidia wakati mgumu wa kiangazi.
      9. serikali na wananchi wapande miti katika mashamba ya serikali na ya watu binafsi.
      10. ukataji wa miti ukomeshwe kwa kuwachukulia hatua za kisheria wanaohusika.
  3. MATUMIZI YA LUGHA
    1. Andika neno lenye sifa zifuatazo (al. 2)
      Kipasuo kwamizo hafifu cha kaakaa gumu, irabu ya chini kati, kipasuo hafifu cha kaakaa laini, irabu ya mbele juu
      Chaki         2/0
    2. Dhihirisha dhima ya viambishi katika kitenzi ukupigao. (al. 2)
      u-ngeli
      ku -nafsi
      a kiishio
      o kirejeshi
      4x1/2
    3. Itunge sentensi sahihi ukitumia kihusishi kimoja cha mtendaji. (al. 1)
      Mfano; Rais alipokelewa na mwenyeji wake kwa taadhima 2/0
    4. Lugha ukamilishwa kwa ushirika wa vijenzi vyake vidogo vidogo. Vitaje. (al. 2)
      Sauti-silabi-neno-sentensi 4x1/2
    5. Tumia neno maudhui katika sentensi ili kudhihirisha upatanisho wa kisarufi. (al. 2)
      Maudhui hayo yanajitokeza vyema riwayani  2/0
      Ngeli ya YA
    6. Tunga sentensi kudhihirisha wakati ujao hali timilifu. (al. 2)
      Atakuwa amemaliza kazi yake tutakapowasili 2/0
    7. Akifisha kifungu kifwatacho: (al. 4)
      nimekuwa nikisisitiza umoja wa afrika daniel moi 1924 2020
      “Nimekuwa nikisisitiza umoja wa Afrika.”- Daniel Moi (1924-2020)   8x1/2
    8. Geuza katika usemi halisi. (alama 2)
      Askari JELA alimuuliza Kendi kama alidhnani hapo ni kwao. Alimwamuru aende kwake mara moja.
      Askari jela alimuuliza Kendi, “Unadhani hapa ni kwenu? Kuja kwangu mara moja.”
    9. Bainisha maana mbili ya sentensi hii. (alama 2)
      Umu alimwandikisha mtoto.
      Alimfanya mtoto kuandika
      Alimwajiri/kusajili
    10. Changanua kwa matawi (alama 4) S
      Watu ambao wana mali hawatoi zaka zao
      F4SwaDMokMP12023Q3
    11. Eleza matumizi ya neno wale katika sentensi hii. (alama 3)
      Wale walioiba ni mabanati wale ambao waliambiwa wale kabla ya kitendo hicho
      Wale walioiba ni mabanati wale ambao waliambiwa wale kabla ya kitendo hicho.
      1 – kiwakilishi
      2 – kivumishi
      3 - kitenzi
    12. Ainisha virai vilivyopigiwa mstari katika sentensi ifuatayo (alama 2)
      Yule mtiifu atatuzwa kesho jioni na mwalimu mkuu.
      Yule mtiifu- RN
      Kesho jioni- RE
    13. Bainisha aina za yambwa na chagizo (alama 2)
      Binti yake  Kimani  aliozwa  Luka kwa arusi mwezi uliopita.
      • Binti yake Kimani- Yambwa tendwa
      • Mwezi uliopita- chagizo ya wakati
    14. Amrisha kwa kutumia kitenzi nywa katika nafsi ya pili. (Alama 1)
      Wewe unywe!
    15. Tunga sentensi kuonyesha maana mbili za neno chupa (al. 2)
      • Chombo cha kutilia vitu viowevu
      • Ruka kutoka juu hadi chini
      • Nahau-vunja chupa,kamata chupa
      • Fuko lililomo tumboni mwa mwanamke ambamo mtoto hukaa
      • Ruka kutoka tawi moja hadi jingne afanyavyo nyani
    16. Tumia neno sembuse katika hali ya kinyume kutunga sentensi (al. 2)
      Hakumla kuku sembuse ng’ombe.
    17. Neno sema ni kitenzi, libadili liwe kielezi kwa kutungia sentensi. (al. 2)
      Sisi tunaelewa anavyosema
      Wanafunzi wanafurahia anavyosema mambo
    18. Andika katika ukubwa wingi (al. 2)
      Kitoto hiki kinalia kwa sababu hakijala mkate.
      Matoto haya yanalia kwa sababu hayajala makate au
      Majitoto haya yanalia kwa sababu hayajala majikate
    19. Tunasema ng’ang’ana kukutu, vunjika kacha pelekwa marshi marshi/ mkikimkiki(al. 1)
  4. ISIMU-JAMII                                                                                                 (alama 10)
    1. Eleza sifa zozote tano zinazotambulisha Sajili ya mazungumzo. (alama 5)
      1. Kuzungumza kwa zamu
      2. Kukatizana kauli
      3. Msamiati maalum kutegemea mada
      4. Lugha husishi – ninakualika
      5. Matumizi ya ishara nyuso (masolugha)
      6. Matumizi ya viziada lugha kusisitiza mada.    ( za kwanza 5×1=05)
    2. Andika sifa tano za kimtindo utakazotumia ukipata fursa ya kutangaza mchezo wa kandanda shuleni. (alama 5)
      1. Kuchanganaya ndimi
      2. Msamiati maalum wa michezo
      3. Utohozi wa maneno
      4. Matumizi ya lakabu
      5. Uradidi wa maneno
      6. Sitiari  - yeye ni nyani
      7. Chuku – kimo cha kuku
      8. Sentensi fupi fupi.     ( za kwanza 5×1=05)
        (Maelezo au mifano ibainike katika majibu ya mwanafunzi ili atuzwe)
Join our whatsapp group for latest updates

Download Kiswahili Paper 2 Questions and Answers - Mokasa 1 Joint Pre Mock Exams 2023.


Tap Here to Download for 50/-




Why download?

  • ✔ To read offline at any time.
  • ✔ To Print at your convenience
  • ✔ Share Easily with Friends / Students


Get on WhatsApp Download as PDF
.
Subscribe now

access all the content at an affordable rate
or
Buy any individual paper or notes as a pdf via MPESA
and get it sent to you via WhatsApp

 

What does our community say about us?