Msiba wa Kujitakia summary notes - Mwongozo wa Mapamazuko ya Machweo na Hadithi Nyingine

Share via Whatsapp


Msiba wa Kujitakia- D. W. Lutomia

Mtiririko wa hadithi

Wakazi wa Matopeni wako katika kipindi kigumu sana cha maisha, taabu zinawaandama kila uchao wala hawana wa kumlilia.

Machoka ni mmoja kati ya Wasakatonge wanaoishi mtaa wa matopeni.

Amefika nyumbani jioni akitoka katika shughuli za kutafuta kibarua ili kupata cha kutia tumboni lakini hajaambulia chochote.

Anaona tofauti kubwa iliyopo kati ya wapiga kura na wale wanaopigiwa kura. 

Hali yake inamkumbusha shairi alilowahi kusoma, la ‘Msiba wa Kujitakia’, ambao kamwe hauna kilio.

Ndio hali waliyo nayo baada ya kuwachagua viongozi wasiojali maslahi yao.

Anakumbuka wakati wa siasa kabla ya uchaguzi.

Serikali inajinaki jinsi ilivyoleta maendeleo huku upinzani nao ukipuuzilia mbali hoja hizo.

Wanatoa ahadi tele za kuboresha maisha ya wakazi wa mtaa huu. 

Machoka anakumbuka kauli ya jirani yake, Zuhura kuwa wanafaa kumchagua mtu wa ukoo wao, awe anafaa au la, tendo ambalo hata Zuhura mwenyewe anajutia.

Tofauti kati ya uteuzi wao wa viongoziuliwafanya kuzua uadui, lakini sasa dhiki inawaleta pamoja.

‘Mtu wake’ aliyechagua Zuhura hawafai kitu.

Bidhaa zinapanda bei na maisha kuwa magumu.

Anagundua kosa lake. 

Wakati wa uchaguzi, jimbo la Matopeni linageuzwa ngome ya watu fulani.

Wananchi wanarauka mapema kwenda kupiga kura kwa matumaini kuwa viongozi hao wataboresha maisha yao.

Hata hivyo, wanawatelekeza.

Zuhura anakumbuka akimweleza Machoka walivyokosea kwa kumchagua kiongozi kwa kuwa ni wa ukoo wao, au kutokana na vizawadi vidogo vidogo walivyopatiwa na visenti vya kununulia pombe.

Hali inazidi kuwa ngumu kwa wakazi wa Matopeni.

Udhalimu unazidi, huku mapato yao madogo yakimegwa na ushuru.

Fumo Matata ni mpinzani mkuu wa Sugu Junior.

Anawakumbusha wapiga kura kukoma kupigia viongozi kura kwa kuwa ni wa ukoo wao kwani hali hiyo inawaathiri.

Kauli yake haitiliwi maanani.

Fumo mwenyewe anawania kiti hiki kwa mara ya tatu mfululizo. 

Ni miaka arobaini na mitatu tangu jimbo la Matopeni likombolewe kutoka kwa walowezi kwa uongozi wa Sugu Senior, babake Sugu Junior.

Zuzu Matata, babake Fumo Matata alipendelewa na wakoloni kuongoza lakini akakataa akiwataka kumwachilia kwanza Mzee Sugu Senior kutoka gerezani. 

Alipoachiliwa, akawa na umaarufu kumshinda na kutwaa uongozi kwa shuruti za wazee wa jamii yake.

Hali hii ikazua uhasama kati yao hadi Zuzu Matata alipofariki bila kuongoza jimbo hili.

Mwanawe pia anazidi kupambana kutimiza ndoto hiyo.

Ni familia hizi mbili tu zinazozozania uongozi wa Matopeni. 

Fumo Matata anapigiwa upatu kushinda ila mambo yanabadilika.

Matokeo yanapokuja, Sugu Junior ameshinda licha ya Fumo kuwa na wafuasi wengi na kupiga kampeni ya kupigiwa mfano.

Yasemekana kuwa upigaji kura si hoja, kwani katika kuzihesabu, mambo huenda kombo na wananchi kulimbikiziwa viongozi wasiowataka. 

Fumo Matata anapata ujumbe kutoka kwa mwandani wake, Kahindi Mlalama, akimpongeza kwa ‘ushindi’.

Hata hivyo, anamwonya kuwa ushindi huo huenda usione jua, lakini siku zijazo uchaguziutakuwa huru na wa haki, bali si wa kulimbikiziwa viongozi madikteta na wakoloni mamboleo.

Vipimo vya uongozi vitategemea sera na tajriba bali si ukoo, umaarufu au utajiri. 

Kiwanjani Mamboleo, shughuli ya kumwapisha Sugu Junior inaandaliwa.

Saa tatu asubuhi, watu washafika huku wanahabari wakinasa matukio yanayopeperushwa moja kwa moja.

Wapo viongozi wa majimbo mengine, mawaziri, wabunge na viongozi tofauti serikalini.

Sherehe bila shaka imegharimu mamilioni ya pesa za watoaushuru kama kina Machoka na Zuhura. 

Yasemekana serikali ndiyo imegharamia nauli ya ndege ya viongozi wa majimbo mengine kutokana nao kutilia shaka ushindi wake.

Sherehe kama hii iliandaliwa tena miaka arobaini na mitatu iliyopita baada ya Sugu Senior kuachiliwa huru.Watu washaanza kufika.

Sugu Junior ndiye anatarajiwa kufika wa mwisho baada ya wageni wengine.

Zuhura ni mmoja wa wananchi waliofika kushuhudia. Uwanja umegawa pande mbili, kwa viongozi na kwa wananchi.

Upande wa viongozi una hema, viti vizuri na soda na maji huku wananchi wakipigwa na miale mikali ya jua. 

Muda unasonga, na kufikia saa sita, viongozi waalikwa hawajafika ila wachache tu.

Hata viongozi wa majimbo jirani waliolipiwa nauli hawajafika.

Watu wameanza kuchoka lakini mfawidhi anawatuliza.

Hatimaye Sugu anafika chini ya ulinzi mkali.

Anapigwa na butwaa kuona hali ilivyo.

Jioni hiyo, mada kuu katika vyombo vya habari ni taarifa ya viongozi kususia sherehe za kuapishwa kwa Sugu Junior. 

Ufaafu wa anwani ‘Msiba wa Kujitakia’

Msiba ni tukio linalosababisha huzuni tele na kilio kingi kwa wahusika.

Msiba wa kujitakia ni sehemu ya methali inayosema kuwa ‘Msiba wa kujitakia hauna kilio’.

Mada hii basi inarejelea matatizo yanayomkumba mtu kutokana na matendo yake mwenyewe.  

Machoka anapitia hali ngumu kimaisha. Ametoka kutafuta kibarua lakini hajaambulia chochote, hata cha kutia tumboni.

Wakazi wengine wa jimbo hili pia wanapitia hali ngumu kama hiyo.

Hali yao ni Msiba wa Kujitakia, kwa kuwa wanfanya uchaguzi bila kuzingatia vigezo vinavyofaa kupata kiongozi anayefaa.  

Machoka anakumbuka shairi la Malenga Mteule alilowahi kusoma mahali fulani.

Shairi hili linahusu msiba wa kujitakia. Kibwagizo chake ni ‘Msiba wa kujitakiya, kweli hauna kiliyo’.

Linaoana na hali ilivyo katika jimbo la Matopeni. Linaongelea visanga vilivyojaa nchini watu wakifilisika.

Mtunzi anamwomba Rabana awafungue macho ili waweze kuona.Kauli ya Zuhura ni ithibati kuwa hali yao ni msiba wa kujitakia.

Anamwambia Machoka kuwa wanafaa kumchagua kiongozi wa ukoo wao hata kama hafai kwa kuwa ni mtu wao.

Sasa hivi, Zuhura anajutia uamuzi wake huo kutokana na dhiki inayomkumba. 

Ugomvi kati ya Zuhura na Machoka ni msiba wa kujitakia.

Wanatofautiana kwa kuwa wana misimamo tofauti katika uchaguzi wa viongoiz.

Ajabu ni kuwa baada ya uchaguzi, dhiki inawaleta pamoja kwani viongozi wenyewe hawawajibiki kwa vyovyote vile.

Wakazi wa Matopeni wanaruhusu jimbo lao kugeuzwa ngome ya watu fulani wanaowania uongozi.

Wanarauka asubuhi na mapema na kustahimili jua la mchana ili kuwapigia kura viongozi, ambao baadaye wanawapuuza na kutojali matatatizo yao.

Zuhura anakiri kuwa walikosea kwa kumchagua kiongozi kwa kuwa aliwanunulia vijizawadi vidogo vidogo.

Anasema kuwa yanayowakumba ni zao la kumchagua kiongozi kutumia matumbo badala ya akili.

Wao ni msiba wa kujitakia.

Fumo Matata anawakumbusha wakazi wa Matopeni kuwa si busara kuwachagua viongozi kwa kuzingatia koo, kwani hali hiyo inaendeleza uongozi mbaya.

Hata hivyo, wanampuuza na kumteua Sugu Junior kuwa kiongozi.

Wanazidi kutaabika kutokana na mapuuza yao hata baada ya kuonywa.  

Zuzu Matata kukosa uongozi wa Matopeni ni msiba wa kujitakia.

Anapendekezwa na walowezi kutwaa uongozi lakini anasisitiza kuwa lazima Sugu Senior kwanza aachiliwe kutoka gerezani.

Anapoachiliwa, anakuwa maarufu kumliko na kutwaa uongozi. Anakosa fursa nyingine ya kutwaa uongozi huo na kubakia kuwa mpinzani wake hadi kifo chake. 

Wananchi wanakubali kukandamizwa.

Wanatengewa upande wa kiwanja wanapoadhibiwa na jua huku viongozi wakitengewa upande wenye hema na kuongezewa vinywaji na ulinzi.

Wanakubali kukaa siku nzima wakimsubiri kiongozi wao huku wakiumizwa na jua hilo. 

Sugu anakosa washirika katika hafla ya kuapishwa, licha ya kuwalipia nauli ya ndege viongozi wa majimbo jirani.

Huu ni msiba wa kujitakia, kwani hatilii maanani maslahi ya wananchi.

Anataka kuwatumbuiza viongozi kutoka nje kwa fedha za walipa ushuru. Hali hii pia inatokana na ushindi wake anaopata kupitia mlango wa nyuma.  

Dhamira ya Mwandishi

Kuwaonya wapiga kura dhidi ya kuwachagua viongozi kwa kutegemea misingi ya kikabila na zawadi wanazowapa na badala yake kutumia vigezo muhimu kama uwajibikaji na kujali maslahi yao. 

Anadhamiria kuwatoa matongo wananchi wanaozozana kwa sababu ya misimamo yao tofauti kuhusu viongozi kwani mwisho wa siku ndio wanaobaki katika taabu, na hatimaye dhiki yao itawaleta pamoja tena.

Kuwakanya viongozi wanaotwaa uongozi kupitia mlango wa nyuma na kuendeleza ukoloni mamboleo na udikteta kwamba siku yao ya kulipia maovu hayo itafika.

Kudhihirisha hali halisi inayowakumba Waafrika na binadamu kwa jumla kutokana na maamuzi yao wenyewe.

Anasawiri utofauti uliopo katika jamii nyingi kutokana na toafuti za kiuchumi kati ya watu.  

Maudhui

Utabaka

Jamii ya jimbo la Matopeni imegawanywa katika makundi mawili makuu kwa kutegemea hali ya kiuchumi.

Kuna wenye hadhi na kina yakhe kwa kutegemea hadhi yao katika jamii.

Wananchi ambao ndio wapiga kura na watozwa ushuru wako katika kundi la chini linalohangaikia maisha kila uchao. 

Maisha kati ya makundi haya mawili tunaambiwa kuwa yametengana kama mbingu na ardhi.

Baada ya ahadi za uongo, viongozi wanatwaa nyadhifa zao na kujiendea kuishi kwa fahari. 

Zuhura na Machoka wanalazimika kurejelea uhusiano wao mzuri baada ya uchaguzi.

Tunaambiwa kuwa dhiki ndiyo inayorejesha uhusiano wao ambao unavurugwa awali na misimamo yao inayokinzana kuhusiana na viongozi wanaopendelea.

Wanagundua kuwa wako katika kundi moja kijamii, kundi la wasakatonge wala viongozi wanaopigania hata hawayajali maslahi yao. 

Utabaka pia unadhihirika katika safu ya uongozi.

Inavyooonekana, ni kana kwamba kuna wale waliozaliwa kuongoza huku wengine wakiwa wafuasi.

Katika jimbo la Matopeni, Sugu Junior na Fumo Matata ndio wanaozozania nafasi ya kuongoza.

Nafasi hizi wanaridhi kutoka kwa wazazi wao.

Sugu Senior, babake Sugu Junior ndiye alikuwa kiongozi wa matopeni baada ya walowezi kuondoka, hali Zuzu Matata, babake Fumo Matata akiwa mpinzani wake.

Yashangaza kuwa ni familia hizo mbili tu zinazozozania uongozi hadi sasa. 

Hali ya utabaka pia inaonekana katika mkutano wa kumwapisha Sugu Junior.

Kiwanja kimegawanywa mara mbili. Kuna upande uliotengewa wenye ulwa katika jamii kama mawaziri, viongozi wa serikali na viongozi wa majimbo jirani.

Upande huu umewekwa hema la kuwazuia jua, kuna vinywaji na walinzi pia.

Upande wa pili ni ule wa raia wa kawaida.

Huko, jua linawateketeza inavyofaa. Isitoshe, wanalazimika kufika mapema kusubiri kiongozi wao, ambaye anafaa kuwasili mwisho wa wote.

Anapofika, yuko na walinzi wanaoimarisha usalama wake, tena anafika saa sita. 

Usaliti 

Jimbo la Matopeni linadhihirisha usaliti wa viongozi waliochaguliwa kwa matumaini ya kuboresha maisha ya wananchi.

Wakati wa kupiga kampeni, wanatoa ahadi si haba ambazo wanaahidi kutimiza pindi tu wakiingia mamlakani.

Wanaaahidi kuimarisha sekta ya afya, kutengeneza barabara, kuimarisha ukulima, elimu na kuwapa kina mama mikopo ya kuanzisha biashara pamoja na ajira kwa vijana.

Hata hivyo, wanasahau ahadi hizi zote wanapoingia mamlakani na kuwatelekeza wananchi waliowachagua.  

Zuhura na Machoka wanasaliti demokrasia, jimbo lao na kujisaliti wenyewe wanapochagua viongozi wasiofaa.

Zuhura anamwambia Machoka kuwa wanafaa kumchagua mtu wao, awe anafaa au la. 

Wanazozana kutokana na misimamo yao inayotofautiana kuhusiana na viongozi wanaotaka.

Ajabu ni kuwa viongozi hao hawawafaidi kwa lolote.

Zuhura anakiri kwamba walikosea kwa kuwachagua viongozi kwa misingi ya kikabila na pia kwa kuwaziba macho kwa vijizawadi vidogovidogo.

Hatimaye wanabaki katika dhiki na kurejesha ujirani wao.

Wahesabu kura pia wanasaliti demokrasia na wapiga kura kwa kuwalimbikiza viongozi wasiotaka.

Tunaambiwa kuwa pale Matopeni kupiga kura na kutopiga ni mamoja kwani uamuzi wa mwananchi hauheshimiwi.

Tunaambiwa kuwa zoezi la kuhesabu kura ndilo muhimu, na kuwa hata wafu hutoka maziarani wakapiga kura na kurejea huko huko.

Ina maana kuwa uamuzi wa wananchi unapuuziliwa mbali na kupatiwa viongozi wasiowafaa. 

Viongozi wa majimbo jirani wanamsaliti Sugu Junior kwa kususia sherehe yake ya kuapishwa, licha yake kugharamia nauli zao za ndege.

Sugu anawasili saa sita, kwani ndiye anatarajiwa kufika wa mwisho kulingana na itifaki.

Anashangaa kuwa ukumbi wa viongozi ukona watu wachache tu, licha ya kuwa amewalipia nauli ya ndege.

Nauli ambayo anawalipia kufuta shauku yao kuwa alipata uongozi kupitia mlango wa nyuma.

Nauli ya pesa za wananchi, wapiga kura, watozwa ushuru.

Ukabila na Unasaba

Wakati wa kampeni, Zuhura anamwambia Machoka kuwa wanastahili kumchagua mtu wao, awe mzuri au mbaya, awe amesoma au la.

Hoja yake ni kuwa wanastahili kuchagua mtu kwa kuwa anatoka kabila lao tu.

Mfumo uu unawaletea matatizo mengi kwani huyo mtu wao hajali maslahi yao hata kidogo.

Anatarajia kuwa serikali ya mtu wao itawafaa lakini wapi, wanabakia katika lindi la umaskini bado.

Zuhura anakiri makosa yake ya kumchagua kiongozi kwa kuwa ni wa kabila lao.

Bado matatizo yanawazidi. Mahitaji yanazidi kuwakaba huku mapato yao yakimegwa na ushuru unaopanda kila uchao. 

Katika mahojiano na Radio Salama iliyopo Matopeni, kiongozi wa upinzani Fumo Matata anawakanya wanannchi dhidi ya mfumo wa kupiga kura kwa kuegemea kwenye misingi ya kijinsia.

Anawaeleza kuwa mfumo huo umepitwa na wakati na bado wataendelea kutaabika chini ya uongozi wa mtu huyo licha ya kuwa wa jamii yao.

Fumo anawaona kama miti ambayo inakubali kuangamizwa na shoka huku ikidhani na mwenzao kwa kuwa mpini wake umetokana nao.

Wananchi wanapuuzilia mbali usemi wake na kuendeleza mtindo huo wa uchaguzi, hali ambayo inawaletea matatizo mengi.

Wanazidi kutaabika.Ni wazi kwamba suala la ukabila lilianza pindi tu baada ya kuondoka kwa walowezi wala si jambo geni.

Tunaambiwa kuwa baada ya walowezi kuondoka, Zuzu Matata anaazimia kuchukua uongozi na kupendekezwa na walowezi.

Hata hivyo, anasisitiza kwamba Mzee Sugu Junior aachiliwa kutoka jela alikofungwa.

Anapoachiliwa, anapata umaarufu kumliko.

Tunaambiwa kuwa Sugu alitwaa uongozi kwa shuruti za wazee wa kabila lake. 

Hali ya unasaba pia inadhihirika katika uongozi wa jimbo la Matopeni.

Mzee Sugu Senior anatwaa uongozi huku Zuzu Matata akiwa mpinzani wake.

Baada yao kufariki, wanao wanachukua nafasi zao katika taifa.

Sugu Junior, mwanawe Sugu Senior, anatwaa uongozi huku Fumo Matata, mwanawe Zuzu Matata akiwa mpinzani wake wa karibu.

Inastaajabisha kuwa ni familia mbili tu ambazo zinazozania uongozi wa Matopeni, ni kana kwamba ndizo zilizaliwa kuongoza na hakuna familia nyingine inayoweza kuchukua uongozi huo. 

Ukoloni

Kuna sura mbili za ukoloni katika hadithi; Ukoloni Mkongwe na Ukoloni Mamboleo.

Tunasimuliwa kuwa wakati fulani huko nyuma, jimbo la Matopeni lilikuwa limetawaliwa na walowezi, lakini hatimaye wakatimuliwa.

Walikuwa wamemweka kizuizini kiongozi Mzee Sugu Senior lakini Zuzu Matata akampigania hadi kuachiliwa, kisha akachukua uongozi baada ya kuachiliwa kutoka seli.

Hatimaye jimbo la Matopeni likawa huru. 

Hata hivyo, bado ukoloni unaendelezwa na waliotwaa uongozi kutoka kwa walowezi.

Viongozi wa Matopeni hawajali maslahi ya wanyonge wanaowachagua.

Wanapania kujinufaisha tu.

Wanajitenga nao na kujiboreshea maisha huku wapiga kura wakizidi kutaabika.

Wanawatoza ushuru ambao wanatumia vibaya kama vile kulipia nauli ya viongozi majirani kuja katika sherehe za kuapishwa kwa Sugu Junior. 

Ukoloni Mamboleo pia unaonekana kupitia shughuli ya uchaguzi wa viongozi.

Wananchi wanaruhusiwa kupiga kura lakini kura zao hizo hazitiliwi maanani, licha yao kuvumilia jua kali kuteua chaguo lao. Inasikitisha kuwa baada ya hayo yote, bado kura zao hazitiliwi maanani bali wanalimbikiziwa viongozi wasiowataka.

Shughuli ya kupiga kura haitiliwi maanani bali mchakato unaofuata wa kuhesabu kura hukumbwa na tafrani na hatimaye viongozi wasioshinda kuteuliwa, badala ya uteuzi wa wapiga kura kuheshimiwa. 

Hali sawa pia inadhihirika katika sherehe za kumwapisha kiongozi Sugu Junior kiwanjani Mamboleo.

Viongozi wanastahiwa na kupatiwa hadhi ya juu, kinyume na usawa uliopiganiwa wakati wa kuwafukuza wakoloni.

Viongozi wamewekewa hema la kuwasitiri jua na pia kupatiwa vinywaji pamoja na ulinzi wa kipekee, kinyume na wananchi wanaotelekezwa juani.

Isitoshe, Sugu Junior anawasili baadaye baada ya wananchi kumngoja kwa kitambo huku wakiunguzwa na jua. 

Migogoro 

Kuna hali ya mgogoro kati ya viongozi na raia kutokana na hali mbaya ya maisha inayowakumba wananchi.

Tunaambiwa kuwa mzigo wa maisha ambao Wanamatopeni walikuwa wamebebeshwa walikuwa tayari kuutua.

Wanawachagua viongozi ambao wanawatelekeza na kutojali maslahi yao.

Wako tayari kupigania haki zao. 

Zuhura na Machoka pia wanajipata katika mgogoro.

Zuhura anapendekeza kuwa wanafaa kumchagua kiongozi kwa kuwa anatoka katika kabila lao, lakini Machoka ana msimamo wake.

Mgogoro huu unaisha baada ya uchaguzi pale viongozi wao wanapowatelekeza na dhiki yao kuwaleta pamoja.

 Kuna mgogoro kati ya Sugu Junior na Fumo Matata, wawaniaji wakuu wa uongozi katika jimbo la Matopeni.

Fumo amekuwa mpinzani wa Sugu, na sasa anawania uongozi kwa mara ya tatu mfulululizo.

Serikali inasifia maendeleo iliyoleta lakini upinzani unaona hizo kuwa porojo tupu.  

Mgogoro kati ya vinara hawa wawili tunagundua kuwa ulianza kwa wazazi wao, waanzilishi wa jimbo hili.

Zuzu Matata, babake Fumo Matata alikuwa mpinzani sugu wa Mzee Sugu Senior, babake Sugu Junior, alipotwaa uongozi baada ya kuondoka kwa walowezi.

Umaskini

Hali ya umaskini inadhihirika katika makazi ya Machoka, akiwa tu kama mfano wa umma mkubwa wa wakazi wa Matopeni.

Ametoka katika shughuli za kutafuta kibarua lakini hajafanikiwa.

Tumbo linamwuma kwa njaa kwani hajala tangu asubuhi.

Inasemekana kuwa taswira ya chumba chake ingeweza kumliza kipofu.

Zuhura ni mfano mwingine wa hali hii.

Yeye pia anahisi ugumu wa maisha baada ya viongozi kutotimiza ahadi walizotoa wakati wakampeni.

Ushuru nao uko juu na unawakandamiza.

Dhiki inarejesha uhusiani mzuri kati yake na Machoka uliovurugwa na misimamo yao tofauti wakati wa uchaguzi.

Maudhui mengine ni kama vile Ufisadi, Kutowajibika, Udhalimu na Uongozi Mbaya.  

Wahusika: Sifa na Umuhimu

Machoka 

Ni mwenye bidii.

Anarauka asubuhi na mapema kwenda kusaka kibarua ili kukidhi mahitaji yake.

Hakati tamaa hadi jioni anapokosa kabisa.

Ni mkakamavu.

Anaposhikilia lake, habanduki.

Ana msimamo wake katika uchaguzi wala kauli ya Zuhura haibadilishi msimamo wake.

Anahiari kukosana naye badala ya kufuata ushawishi wake.

Ni mzalendo.

Siku ya kupiga kura, anaungana na Wanamatopeni wengine kwenda kupiga kura kwa nia ya kumteua kiongozi wao.

Ni mwenye kumbumkumbu.

Anapokinai hali yake, anakumbuka shairi alilowahi kusoma kuhusiana na msiba wa kujitakia lililoandikwa na mshairi mwenye lakabu ya Malenga Mteule.

Umuhimu wa Machoka

Ni kiwakilishi cha mateso wanayopitia raia chini ya utawala mbaya

Ni kielelezo cha bidii na kujituma katika shughuli licha ya matatizo ya maisha.

Anadhihirisha mgawanyiko uliopokatika jamii kwa misingi ya kiuchumi na mamlaka.

Zuhura

Ni mzalendo.

Siku ya kupiga kura, anrauka bukrata na wenzake kwenda kupanga foleni na kusubiri hadi zamu yao kupiga kura ili kumteua kiongozi wao.

Ni mshawishi.

Anamsisitizia Machoka kuwa wanafaa kumchagua kiongozi kutoka kabila lao.

Anapokataa wanazozana.

Ni mkabila.

Ananuia kuteua kiongozi kutoka kabila lake. Hajali iwapo kiongozi huyo ni mzuri au mbaya, amesoma au la.

Ni mvumilivu.

Ni mmoja wa wale wanaosubiri ujio wa Sugu Junior katika sherehe za kuapishwa kwake.

Anaunguzwa na jua na kusubiri, hata hina mikononi na wanja machoni unaanza kuyeyuka lakini anangoja hadi kiongozi anapofika.

Ni mkakamavu.

Anapofanya uamuzi hatetereki.

Anakata kauli kumteua kiongozi kutoka katika kabila lake.

Anangoja hadi kiongozi anapofika katika sherehe za kuapishwa kwa Sugu Junior. 

Umuhimu wa Zuhura.

Anadhihirisha jinsi raia wanavyochangia katika matatizo yanayowakumba kwa kuwachagua wasiofaa.

Ni kiwakilishi cha ukabila na mchano wake katika kuiangusha jamii.Kupitia kwake, mgawanyiko wa kijamii kwa misingi ya kiuchumi unadhihirika.

Ni kiwakilishi cha matatizo wanayopitia raia wa kawaida katika nchi.

Sugu Junior

Ni fisadi.

Anawaacha wananchi waliompa wadhifa kutaabika wala hajali maslahi yao.

Anatwaa uongozi kwa njia za kifisadi kwani siye chaguo la wananchi

Ni mbadhirifu.

Anatumia visivyo hela za jimbo la Matopeni.

Anawalipia nauli viongozi wa majimbo jirani kuja katika sherehe za kuapishwa kwake, sherehe ambazo hata hawaji.

Ni mwenye tamaa.

Ana tamaa ya uongozi. Anatumia kila njia kuhakikisha kuwa ametwaa uongozi japo siye chaguo la wananchi.

Ni mnafiki.

Wakati wa kampeni, anajinasibisha na watu na hata kuwa karibu nao ili kupata kura zao.

Anapopata mamlaka, anajitenga nao kama mbingu na ardhi.

Umuhimu wa Sugu

Ni kiwakilishi cha viongozi wasiojali maslahi ya umma uliowachagua.

Kupitia kwake, hali ya mvutano katika uongozi inadhihirika na jinsi hali hiyo inavyoathiri maendeleo

Ni kiwakilishi cha unafiki wa viongozi wengi katika jamiiNi kiwakilishi cha ukoloni mamboleo katika jamii ya sasa.

Fumo Matata

Ni mkakamavu.

Anapoamua kuwania uongozi, harudi nyuma licha ya kufeli.

Anafeli mara mbili lakini bado yuko debeni kwa mara ya tatu.

Ni mwenye bidii

Anazunguka kote Matopeni akiimarisha kampeni zake na kutwaa wafuasi wengi.

Ni mwenye maono.

Watu wanapendezwa sana na mipango yake aliyoweka ya kuwaboreshea maisha na wako tayari kumchagua kwa ajili hiyo.

Umahimu wa Fumo

Ni kiwakilishi cha viongozi wanaojaribu kwa kila hali kupigania maslahi ya wananchi wanaoteseka.

Kupitia kwake, hali ya ukoloni mamboleo inadhihirika ilivyokita mizizi katika jamiiAnadhihirisha mizozo iliyopo ya uongozi na athari yake katika jamii.

Ni kiwakilishi cha imani na tumaini la usawa wa kijamii katika siku zijazo.  

Mbinu za Uandishi.

Tashbihi 

Maisha kati ya makundi haya mawili, yaani mpiga kura na mpigiwa kura, yametengana kama mbingu na ardhi.

Anasimama pale kama kigingi

Zuhura na Machoka walikuwa kama fahali wawili-hawakai katika zizi moja.

Maisha ya Wanamatopeni yalikuwa kama mchezo wa karata, hawajui leo wala kesho.Wanamatopeni walipotathmini hali zao, walijifananisha na panya walionaswa kwenye mtego wa uhitaji.

Fumo aliona hali ya Matopeni kama kisa cha msitu na shoka.Wakishapata walichokitaka, walijitenga na umma kama wagonjwa wa ukoma.

Semi

zimegonga mwamba- zimekosa kufanikiwa kukodoa macho- kufungua macho yotendoto iliyozikwa katika kaburi la sahau- iliyosahaulika vinywa wazi- wameachama, kwa mshangaokula halafa- kuapa/kuapishwa wakipiga doria- wakiimarisha ulinzi

Methali

Punda akichoka, mzigo huutua. Lisilobudi hubidiWajinga ndio waliwao

Mzigo wa mwenzio ni kanda la usufi

Ukistaajabu ya Musa, hujayaona ya Firauni

Subira huvuta heri.

Majazi

Machoka-mhusika huyu amechoshwa na maisha ya umaskini.

Ametoka kutafuta kibarua mchana kutwa huku amechoka.

Yuko tayari kutua mzigo aliotwishwa, ambao umemchosha.

Zuhura- ni sayari ya pili kutoka kwenye jua.

Anajiona kuwa karibu na jua(uongozi), eti kwa sababu kiongozi anatoka kabila lake.

Yuko kwenye mstari wa mbele kupiga kura na pia katika sherehe za kuapishwa kwa Sugu Junior. 

Matopeni-ni jimbo la watu wanaong’ang’ania maisha yao.

Kumejaa tope la umaskini, ujinga, unyanyaswaji na ukabila, miongoni mwa mengine.

Sugu Senior.

Sugu ina maana ya ‘siyoweza kubadilika kwa urahisi’, au ‘siyosikia dawa’.

Mzee Sugu anatwaa uongozi na kuushikilia bila kutetereshwa na upinzani wa Zuzu Matata.

Senior ni kuwa ndiye mkubwa kati ya Sugu wawili kwenye hadithi.

Sugu Junior.

Mwanawe Sugu senior anayeendeleza ubabe wa babake dhidi ya mpinzani wake, Fumo Matata.Zuzu Matata.

Zuzu ina maana ya mjinga. Anapigania Sugu Senior kutolewa seli, na anapotolewa, anamnyang’ama uongozi.

Hili linamletea matatizo mengi(Matata) hadi anapokufa bila kuonja ladha ya uongozi.

Fumo Matata.

Ni mwanawe Zuzu Matata.

Fumo ni aina ya mkuki unaotiwa kwenye upande mmoja wa mpini, au kiongozi wa kijadi.

Ni mkuki wa Matopeni wa kuboresha maisha lakini hapati fursa hiyo.

Pia ni kiongozi kwa kuwa anachaguliwa na raia lakini anapokwa nafasi yake.

Mamboleo.

Ni uwanja anaofaa kuapishwa Sugu Junior.

Hii ni shughuli ya kileo.

Pia, viongozi wanafanya mambo kileo wanaposusia sherehe hizo.

Wamechoshwa na wizi wa kura.

Kinaya

Wakati wa kampeni, serikali inajigamba ilivyoleta maendeleo.

Ukweli ni kuwa haijaleta maendeleo yoyote.

Zuhura anamwambia Machoka kuwa wanafaa kumchagua mtu wao, awe mzuri au mbaya.

Ajabu ni kuwa wao ndio wanateseka chini ya uongozi huo.

Zuzu Matata anampigania Mzee Sugu Senior kutolewa seli.

Kinaya ni kuwa anapotoka, anapata umaarufu kumshinda na kutwaa uongozi.

Wanaishia kuwa wapinzani badala ya kushirikiana.

Tunaambiwa kuwa pale Matopeni kupiga kura na kutopiga ni mamoja kwani uamuzi wa mpiga kura hauheshimiwi.

Sasa kuna haja gani ya zoezi hilo basi?

Shughuli muhimu ya kidemokrasia inageuzwa kuwa mzaha.

Uwanjani Mamboleo, sehemu ya viongozi imeimarishwa kwa hema, viti, vinywaji na ulinzi.

Wananchi wanatelekezwa kwenye jua, hali ndio watoa ushuru.

Viongozi wa majimbo jirani wanasusia sherehe za kuapishwa kwa Sugu Junior hata baada yake kugharamia nauli yao ya ndege.

Kisengerenyuma/Mbinu Rejeshi

Machoka anapokinai matatizo ya maisha, anakumbuka shairi alilowahi kusoma la Malenga Mteule.

Machoka pia anakumbuka mambo yalivyokuwa wakati wa kampeni.

Anakumbuka ahadi ambazo walipatiwa, jinsi serikali ilivyojisifia kuleta maendeleo huku upinzani ukikejeli kauli hiyo.   

Anakumbuka pia kauli ya jirani yake Zuhura kuwa wanafaa kumchagua mtu wao, awe mzuri au mbaya, amesoma au la.

Anakumbuka hali ya suitafahamu kati yake na Zuhura huyo kutokana na misimamo yao hiyo, hali iliyoyeyushwa na dhiki baada ya uchaguzi.

Tunarejeshwa kwa historia ya Matopeni baada ya kutwaa uhuru, huku Mzee Sugui Senior akiingia mamlakani baada ya kupiganiwa na Zuzu Matata kutolewa seli, upinzani wao katika safu ya uongozi hadi kufariki kwa Zuzu Matata bila kuonja ladha ya uongozi.

Takriri

Anawaza juu ya maisha yake.

Maisha ya wasakatonge. Maisha ya wanaojiita ‘pangu pakavu’.

Maisha ya wapiga kura. Maisha ambayo ni tofauti sana na maisha ya waliowapigia kura.

Maisha kati ya makundi haya mawili…“Wetu ni wetu, hata akiwa mbaya ni wetu… Awe amesoma au hajasoma, angali wetu.”

Leo hii amebaki kujuta. Kujuta ghaya ya kujuta! Tayari alikuwa amekwishafanya kosa.

Kosa ambalo lilikuwa la kujitakia.

Hivyo ndivyo ari yake Zuzu Matata ya kuiongoza Matopeni ilivyogeuka kuwa ndoto.

Ndoto inayosemekana ilizua uhasama mkubwa kati ya viongozi hawa wawili.

Ndoto iliyomfanya Zuzu Matata kuwa mpinzani… Ndoto anayozidi kuiota akiwa mle kaburini.

Ndoto iliyozikwa katika kaburi la sahau. Ila kesho…kesho…kesho yote haya yatakuwa marehemu…Zuhura amechukua nafasi yake kwenye sehemu ya pili…, sehemu ambapo jua kali lilipenyeza miale…,sehemu ya wapiga kura… “Subira…subira…subira…ndugu zangu.”

Tashihisi

Machoka anabaki kukodoa macho huku maonevu yakiihukumu nafsi yake.

Kongole kwa ‘ushindi’ wako, ingawa ushindi huo huenda usione jua!Ukumbini, viti vinamkodolea macho.

Hadithi ndani ya Hadithi

Tunasimuliwa kisa cha msitu na shoka.

Miti katika msitu iliangamizwa na makali ya shoka huku ikifurahia eti kwa kuwa mpini wa shoka ulitokana na mmoja wao.

Ilidhani shoka ni mwenzao. Kisa hiki kinafananishwa na Wanamatopeni wanaomchagua kiongozi kwa misingi ya kikabila ila anawadhulumu wakidhani ni mmoja wao. 

Chuku

Taswira ya chumba chake ingeweza kumliza kipofu.Hata hina aliyokuwa amejiremba Zuhura mikononi na wanja aliokuwa amejipaka imekwishaanza kudondoka kwa makali ya jua. 

Ulinzi mkali ambao ungemzuia hata nzi kupita karibu naye!

Kejeli

Mzigo wa maisha haukuwatisha wala kuwakosesha usingizi viongozi wao Ndoto anayozidi kuiota akiwa mle kaburini!

Pale Matopeni, siku hizi hata wafu hupiga kura na kurejea maziarani!Sherehe hii bila shaka imeigharimu serikali mabilioni ya pesa.

Pesa za walipaushuru, kina yakhe kama Machoka na Zuhura.Zuhura amechukua nafasi yake kwenye sehemu ya pili, palipoandaliwa kwa ajili ya watu kama yeye, sehemu ambapo jua kali lilipenyeza miale yake ya ghadhabu, sehemu ya wapiga kura, watozwa ushuru!

KojaTunaahidi kutengeneza barabara, kuimarisha sekta ya afya, kuinua kina mama wetu kwa kuwapa mikopo ya kuanzisha biashara……kaka, ndoto haifi ila vizingiti haviishi daima; kulimbikiziwa viongozi, udikteta, ukoloni mamboleo

…Mizani ya ubora wa kiongozi haitakuwa kabila lako, ukoo wako, familia yako, nani unayemjua, una hela ngapi…

Mbinu nyingine ni pamoja na Ushairi, Tabaini, Mdokezo, Maswali Balagha, Nidaa, Kuchanganya Ndimi, Tanakali, Lakabu na Ujumbe wa Simu.

Join our whatsapp group for latest updates

Download Msiba wa Kujitakia summary notes - Mwongozo wa Mapamazuko ya Machweo na Hadithi Nyingine.


Tap Here to Download for 50/-




Why download?

  • ✔ To read offline at any time.
  • ✔ To Print at your convenience
  • ✔ Share Easily with Friends / Students


Get on WhatsApp Download as PDF
.
Subscribe now

access all the content at an affordable rate
or
Buy any individual paper or notes as a pdf via MPESA
and get it sent to you via WhatsApp

 

What does our community say about us?