Mapamazuko ya Machweo summary notes - Mwongozo wa Mapamazuko ya Machweo na Hadithi Nyingine

Share via Whatsapp


Mapambazuko ya Machweo - Clara Momanyi

Mtiririko.

Mzee Makucha na Mzee Makutwa ni marafiki, ambao wamestaafu na umri wao umesonga.

Hata hivyo, urafiki wao uliokolea awali sasa umepungua, umebaki tu ule wa kujuliana hali.

Mzee Makutwa anaonekana akizurura mtaani na gari lake baada ya kustaafu, wala hakuna ajuaye shughuli zake, hata Mzee Makucha.

Anaonekana tu kila mara akiwabeba vijana garini, wala haijulikani anawapeleka wapi.

Mkewe Makucha, Bi Macheo anamsaili mumewe kuhusiana na hili lakini hapati taarifa yoyote.

Makutwa anajinaki kuwa hawezi kuishi maisha ya kutaabika hata kama amestaafu.

Bi. Macheo anamshauri mumewe akomeshe urafiki na Mzee Makutwa, lakini mumewe anamweleza kuwa urafiki uliobaki kati yao ni wa salamu tu.

Mzee Makucha anauza vitafunio kwenye makutano ya barabara baada ya kustaafu kutoka kazi yake alipopigwa kalamu.

Anafanya kazi na shirika la reli lakini linasambaratika baada yake kuachishwa kazi, hivyo juhudi zake kwenda mahakamani ni bure.

Akiwa kazini kwake(kuuza vitafunio), anashangazwa na kazi anayofanya Makutwa, ambaye anatangamana na vijana kila uchao wala hana hata muda wa kuwasabahi wazee wenzake.

Mzee Makutwa anafika katika kazi ya Mzee Makucha na kutapakaza vumbi kwenye vitafunio vyake kwa gari lake akilipiga breki.

Anamkejeli Makucha, akimwambia kuwa anafaa kujipumzisha nyumbani na kazi hiyo kuachia vijana.

Lakini Makucha anamsisitizia kuwa yuko sawa nayo, kuliko yeye anayezurura mitaani na vijana.

Anamdhihaki kuhusu bintiye aliyetoroshwa na Mhindi, huku akimkumbusha afurahie maisha licha ya matatizo.

Mashaka ya Makucha kuhusu kazi afanyayo Makutwa yanazidi.

Vijana wawili, Dai na Sai wananunua kashata kwa Makucha na kuelezana kuhusu taabu za maisha baada ya kufuzu na kukosa kazi.

Wanaamua kujaribu bahati yao na gari la probox linalozunguka likikusanya vijana.

Makucha anajua bila shaka ni gari la Makutwa.

Gari linapofika wanalipungia mkono na kuingia.

Linaendeshwa na kijana sasa hivi, sio Makutwa.

Makucha anamwita mkewe kuchukua vitu vyake na kuchukua teksi kulifuata gari lile.

Wanasafiri hadi wanapoingia kwenye mgodi wa kisiri uliofichwa katika mazingira makavu.

Anaingia kwenye mgodi na kushuhudia jinsi vijana wanavyodhalilishwa humo kwa kazi ya kutafuta madini.

Anarudi tena na kuwadanganya walinzi kuwa anamtaka Mzee Makutwa, ambaye huku anaitwa Mzee Mamboleo.

Anawaaga akidai atamfuatilia nyumbani.

Anarudi mjini Kazakamba na kuripoti polisi, ambao wanaandamana naye hadi kwenye lile pango.

Wanamkuta Mzee Makutwa akikagua mgodi.

Anatokomea pangoni na kupotelea humo, hadi polisi wanapomrushia vitoza machozi.

Anatoka akikohoa na kufungwa.

Anamlaumu Mzee Makucha kwa kumwendea kinyume, lakini naye anamwambia haki ndio muhimu.

Hatimaye anatupwa korokoroni kwa kosa la jinai.

Mzee Makucha anapokea zawadi ya hundi ya pesa kutoka kwa tajiri mmoja anayeendeleza miradi ya maendeleo kwa vijana.

Anayaona haya kama mapambazuko mapya, licha ya maisha yake kuwa katika machweo.

Ufaafu wa anwani 'Mapambazuko ya Machweo'.

Mapambazuko ni wakati wa asubuhi inapoingia na jua kuchomoza.

Machweo nao ni wakati wa jua kutua na giza kuingia. Mada hii inaweza kufasiriwa kuwili; mapambazuko yanayotokea wakati wa machweo, au mapumbazuko yaliyo katika machweo.

Dhana hizi, mapambazuko na machweo pia zimetumiwa kwa maana nyingine.

Mapambazuko yanawakilisha wakati wa ujana, huku machweo yakiwakilisha uzee.

Pia, mapambazuko yanaashiria mwangaza(fanaka) huku machweo yakiashiria giza(taabu/mashaka).

Makutwa anawashangaza wengi kwa kuwa anashinda na vijana kila wakati licha ya kuwa ni mzee.

Hashirikiani na wazee wenzake hata kidogo.

Anaonekana kama ujana wake umeingia akiwa mzee, yaani mapambazuko yake yanamjia akiwa katika machweo.

Mzee Makucha anafanya biashara ya kuuza vitafunio.

Japo Mzee Makutwa anamkejeli, yeye anaiona kuwa ndio tumaini lake baada ya kufutwa kazi kwenye shirika la reli.

Machweo yanaingia kwa kuachishwa kazi, na anaiona biashara hii kuwa mapambazuko yake.

Binti yake Makucha, Riziki, anaolewa na kigogo Mhindi baada ya kushindwa kuvumilia dhiki.

Kutokana na machweo ya umaskini, anaonelea ndoa hiyo kama mapambazuko kwake.

Mzee Makucha anamweleza Mzee Makutwa kuwa siku moja, jua la macheo(Mapambazuko) litambishia mlango japo anaelekea machweo.

Yaani, ipo siku atafanikiwa licha ya uzee wake.

Sai na Dai wanaeleza taabu ya maisha yao.

Ni miongoni mwa vijana waliohitimu kutoka chuo kikuu na kukosa kazi.

Wanazurura tu mitaani. Wako karibu kukata tamaa.

Machweo yameanza kuwaingilia katika maisha hali bado wako wakati wa mapambazuko.

Wanaona shughuli za probox ya Makutwa kama nafuu ya pekee, yaani mapambazuko ya kuwatoa katika machweo waliyomo.

Mzee Makucha anapofuata gari la Makutwa kwa teksi, linawaongoza hadi kwenye mgodi mkubwa, ambapo vijana na watoto wadogo wanafanya kazi ya kusaka vito vya thamani.

Wanapata taabu nyingi, na wengi wao wanakosa hata fursa ya masomo.

Machweo yameshaingia katika maisha yao hali wako katika mapambazuko.

Mzee Makutwa amewatesa vijana wengi kwa kuwaingiza katika machweo ya kumfanyia kazi ya kinyama ya kusaka vito.

Hawana imani ya maisha bora. Kukamatwa kwake na polisi ni mapambazuko ya machweo, kwani uovu wake unafikia kikomo.

Mzee Makucha anapata zawadi ya hundi kutoka kwa tajiri mmoja anayeendeleza miradi ya kuwainua vijana kimaendeleo.

Amekuwa akiishi kwa taabu kwa kuuza vitafunio kando ya barabara.

Haya ni mapambazuko(mafanikio) ambayo yanamwangukia katika machweo ya maisha yake(uzee na taabu).

Dhamira ya Mwandishi

Kuelimisha kuhusiana na nafasi ya vijana katika kujenga na kuendeleza jamii

Anawasilisha hali ya maisha na pandashuka zinazohusika, pamoja na juhudi za waja kujikimu.

Anadhihirisha namna biashara haramu zinavyoathiri jamii vibaya.

Anawasilisha mgogoro wa kiumri kati ya vijana na wazee unavyoathiri jamii.

Anatoa tumaini kwa wanajamii wenye bidii kuwa siku moja mafanikio yao yatafika.

Anaonya watenda maovu kuwa siku yao ya kunaswa itafika.

Maudhui

Migogoro

Mzee Makucha na Mzee Makutwa wako katika mgogoro baada ya kustaafu.

Makucha anafanya kazi ya kuuza vitafunio kando ya barabara hali Makutwa hajulikani kazi anayofanya.

Anaonekana tu akizurura huku na huko na gari lake.

Anaiona kazi ya Makucha kama ya kujiumbua lakini Makucha anaiona kuwa asili ya riziki yake. Anapopita na kumrushia vumbi, Makucha hafurahii tendo hili. Isitoshe, anamdhihaki Makucha kuhusiana na kazi yake na pia sababu ya bintiye Riziki aliyeolewa na Mhindi.

Bi. Macheo pia anajipata katika mgogoro na mumewe kuhusiana na Makutwa.

Hapendi jinsi Makutwa anavyomfanyia stihizai mumewe, na kila mara anamtaka kukomesha urafiki kati yao.

Hata hivyo, Makucha haoni neon lolote katika salamu wala haoni haja ya kutozipokea.

Mgogoro kati Makutwa na Makucha unaimarika Makucha anapojua kazi ambayo Makutwa hufanya ya kuwatumikisha vijana katika mgodi kutafuta vito.

Anaamua kumwitia polisi ambao wanaenda kwenye mgodi huo na kumkamata Makutwa.

Makutwa anamlaumu kwa tendo hili huku akimwita rafiki wa uongo, lakini Makucha anamwambia kuwa hawawezi kuwa marafiki na amtazame akihujumu taifa kwa kufyonza nguvu za vijana kiharamu.

Makutwa pia yuko katika mgogoro na sheria.

Anaendesha biashara ya kimagendo ya kuwatumikisha vijana kutafuta vito katika mgodi wake.

Hatimaye, polisi wanapata habari kutoka kwa Makucha na kumwahi katika mgodi huo.

Hatimaye anafungwa jela kwa makosa ya jinai.

Nafasi ya Vijana Katika Jamii.

Vijana wamepatiwa nafasi changamano katika hadithi hii.

Makucha anawachukulia vijana kuwa watumwa.

Anawabeba na kuwapeleka katika mgodi wake kumfanyia kazi ya kutafuta vito vya thamani.

Vijana hawa wanakosa nafasi ya kujiendeleza kielimu na kuyafurahia maisha yao pamoja na kutumikia jamii.

Isitoshe, wanakumbwa na hali ngumu ya kimaisha, kwani huko wanakoishi hakuna hali nzuri.

Hewa si safi na kazi wafanyazo ni za sulubu.

Sai na Dai pia wanawakilisha hali ya vijana wengi katika jamii.

Baada ya kuhitimu kutoka chuo kikuu, hawajapata kazi wala hawana matuamini.

Wanashinda kuzurura mitaani.

Dhiki inapowafika shingoni, wanaamua kujaribu bahati kwa Makutwa, bila kujua wanaelekea kujiuza kwa utumwa.

Hata hivyo, Makucha anawaopoa kabla hawajazama huko.

Makucha anaamini kuwa vijana ndio raslimali kuu ya jamii.

Baada ya kuwaokoa vijana wale kutoka mikononi mwa Makutwa, anawaonea imani.

Anafahamu kuwa wengi wao wanafaa kuwa katika shule wakiandama elimu na hata wengine katika vyuo vikuu. Isitoshe, anapokea zawadi ya hundi ya pesa kutoka kwa tajiri mmoja ambaye anaendeleza miradi ya kimaendeleo kwa vijana.

Bila shaka, anaelewa fika kuwa vijana wana jukumu kubwa katika jamii.

Kazi

Mjini Kazakamba, kila mmoja anajikaza vilivyo kujitafutia riziki kupitia kazi hii au nyingine.

Mzee Makucha kila asubuhi anarauka kuuza bidhaa zake kwenye makutano ya njia akiwa na uhakika wa kunasa wateja wengi iwezekanavyo.

Dhihaka za Mzee Makutwa hazibadilishi mtindo wake wa kujitafutia riziki.

Mkewe naye anachuuza kaimati na vitumbua kwenye veranda ya nyumba yao.

Kabla ya kuanza kuchuuza vitafunio hivi, Mzee Makucha anafanya kazi na shirika la reli ambalo linamtimua kwa ajili ya kupunguza idadi ya wafanyakazi wake.

Baadaye linasambaratika, hivyo anakosa marupurupu yake.

Makutwa naye anafanya kazi kama waziri hadi anapostaafu.

Kazi hii inampa majivuno na anapostaafu, anadharau kazi ya Makucha ya kuuza vitafunio.

Anajigamba na kazi yake anayofanya ambayo haieleweki, kwani anaonekana kila siku akiwabeba vijana huku na huko, wala hakuna ajuaye wanaenda wapi.

Baadaye tunafahamu kuwa ni kazi haramu ya kuwatumikisha kwenye mgodi.

Sai na Dai wanawakilisha vijana wengi wanaopata elimu hadi vyuo vikuu lakini wanakosa kazi.

Vijana hawa wanaishia kuwa wakizurura mitaani na hatimaye kupata kazi za kidhuluma kama ile ya Mzee Makutwa ya mgodi.

Polisi wanafanya kazi yao ya kulinda sheria barabara.

Wanapopashwa habari na Mzee Makucha kuhusiana na nyendo za Mzee Makutwa, wanaandamana naye hadi kwenye mgodi na kumkamata.

Hatimaye, anafikishwa mahakamani na kuhukumiwa kwa kosa la jinai.

Umaskini

Mzee Makucha anaanguka kwenye lindi la umaskini baada ya kuachishwa kazi katika shirika la reli bila marupurupu, kwani shirika hilo linasambaratika pia.

Analazimika kuchuuza vitafunio kando ya barabara kujipatia riziki.

Mkewe naye anauza kaimati na vitumbua kwenye veranda ya nyumba yao.

Umaskini unawazidi kiasi kwamba binti yao wa pekee, Riziki, anawatoroka na kuolewa na Mhindi ili kuepuka urumo.

Hata hivyo, umaskini huo unaondoka baada ya kitendo cha kishujaa cha Makucha kinachowaletea hundi ya pesa kutoka kwa tajiri mmoja anayethamini tendo lake.

Vijana maskini wanajipata taabani mikononi mwa Mzee Makutwa.

Anawasomba kwenda kuwafanyisha kazi ya kusaka vito vya thamani katika mgodi wake.

Wanafanya kazi hii katika mazingira mabovu na kufungiwa mle ndani, wasiwe na nafasi ya kutokea.

Uzalendo

Makucha anadhihirisha umuhimu wa uzalendo kupitia tendo lake la kuokoa vijana wanaotumikishwa na Mzee Makutwa.

Anapojua shughuli anazoendesha, anawaendea polisi mara moja kuja kumkamata.

Anawaokoa vijana hao, anaowaona kama amali ya jamii.

Uzalendo wake unathaminiwa na tajiri mmoja anayeendesha miradi ya kuwainua vijana kimaendeleo.

Anamtuza hundi ya pesa kutokana na ushujaa wake.

Tajiri huyu pia anadhihirisha uzalendo kupitia miradi yake ya kujenga taifa, hasa vijana.

Makutwa, kwa upande mwingine, amekosa kabisa uzalendo.

Analipoka taifa nguzo yake muhimu kwa kuwachukua vijana mabarobaro na kwenda kuwatumikisha katika mgodi wake.

Vijana hawa wanafaa kuwa wakiendesha shughuli nyingine muhimu za kujenga jamii.

Ukoloni Mamboleo

Ukoloni huu unaendelezwa na Mzee Makutwa baada ya kustaafu uwaziri.

Makutwa anaonekana akizurura huku na huko na gari lake huku akiwabeba vijana kutoka mitaani wala hakuna anayejua shughuli ambazo anaendeleza wala anakoelekea, hadi Makucha anapofuata gari lake kwa teksi likiendeshwa na kijana mwingine.

Anafika kwenye mgodi wa Makutwa wanakofanya kazi vijana hawa.

Wanateremka bonde ambalo limejificha kabisa, hata miale ya jua haionekani.

Wanaingi a kwenye tambarare kubwa lenye vuduta vya mchanga ambapo vijana kadhaa, ikiwemo watoto wadogo wanafanya kazi.

Wanadondoa vijiwe vidogovidogo vinavyong'aa.

Wanasimamiwa na wanyapara wanaowaamrisha kwa sauti za kutisha. Makucha anapoingia ndani ya pango, anapata taa za vibatari za kuzuia giza lililomo.

Vijana wanachimba madongo ya mchanga na kuyatia ndani ya mikokoteni.

Wamelowa jasho kutokana na upungufu wa hewa ndani ya mgodi huo.

Usiku, wanalala katika mabanda yaliyojengwa kigugu.

Wanaoingia humo hawaruhusiwi kutoka.

Makazi hayo yamezungushiwa ua wa stima na pia yana mabawabu katili na majibwa makubwa ya kuwazuia vijana wale kutoroka.

Makutwa ni kiwakilishi halisi cha 'mkoloni mweusi'.

Maudhui mengine ni kama vile Ndoa, Utabaka, Udhalimu, Malezi, Uwajibikaji, Mabadiliko na Mazingira.

Wahusika: Sifa na Umuhimu.

Mzee Makucha

Ni mwenye bidii.

Baada ya kufutwa kazi, anarauka kila asubuhi kuuza vitafunio kando ya barabara kuhakikisha kuwa amepata riziki.

Ni mpelelezi.

Anashangaa kazi anayofanya mwenzake na kuamua kumpeleleza.

Anasikiliza kwa makini mazungumzo kati ya Dai na Sai wanapotaja gari la Makutwa.

Wanapoingia, anapanda teksi na kuwafuata hadi anapofahamu kazi anayoendeleza Makutwa ya kuwatumikisha vijana kwenye mgodi.

Ni mzalendo.

Anapojua biashara anayoendeleza Makutwa ya kuwadhulumu vijana, anaamua kuwaita polisi kumkamata na kuwaokoa vijana wale ili waweze kuhudumia taifa.

Ni mjanja.

Anafaulu kuingia katika pango la mgodi licha ya kuwa na walinzi wanaomzuia.

Tunaambiwa kuwa anawachenga na kuingia ndani ya pango.

Ni mwerevu.

Anapowapata walinzi wakiwahangaisha vijana wa teksi aliokuja nao kwa maswali, anawaambia kuwa alikuwa akimtafuta Mzee Makucha na kwa kuwa hajamwona, ataondoka tu.

Hili linawazuia kujua mikakati yake ya kuwaita polisi.

Mwenye hamaki.

Mkewe anapomzungumzia kuhusu Makutwa, anamjibu kwa hasira kuwa ataishia kuwa kidhabu.

Matendo na maneno ya Makutwa anapofika anapouzia na gari yake yanamuudhi, hasa maneno kuhusu binti yake Riziki.

Umuhimu wa Makucha

Ni kielezo cha umuhimu wa uzalendo na utetezi wa haki katika jamii.

Ni kielelezo cha bidii na tumaini katika jamii na jinsi vinavyoweza kuleta mafanikio.

Ni kiwakilishi cha dhiki zinazowakumba wananchi wa kima cha chini kiuchumi.

Kupitia kwake, umuhimu wa ndoa na mchango wake katika kujenga jamii vinadhihirika.

Anadhihirisha aina za migogoro inayopatikana katika jamii.

Makutwa

Ni mwenye dharau.

Anamsemesha Makucha kwa dharau licha ya kuwa anajidai kuwa rafiki yake. Anamkejeli kuhusiana na kazi yake duni ya kuchuuza vitafunio na bintiye mtoro.

Ni mnafiki.

Anajitia urafiki na Makucha lakini hawezi kumfaa.

Makucha anasema kuwa hajawahi kumfaa akiwa waziri, licha yake kumtaka Makucha amsafirishie shehena bila kulipa.

Ni dhalimu.

Anawakusanya vijana na kuwapeleka katika mgodi wake kufanya kazi katika mazingira duni.

Aidha, hawaruhusiwi kuondoka pale.

Wamefungiwa kwa ua wa stima na kuwekewa walinzi wenye mbwa wakali.

Ni katili.

Anapiga gari lake breki na kutapakaza vumbi kwenye vitafunio anavyouza Makucha bila haya.

Hana imani kamwe na vijana anaowatumikisha.

Ni jasiri.

Polisi wanapomjia, anawakimbia na kuingia kwenye mgodi.

Anakataa kabisa kusalimu amri hadi pale wanapomtoa ndani kwa kumrushia vitoza machozi.

Ni mkakamavu.

Baada ya kustaafu kama waziri, anaamua hawezi kuishi maisha ya kimaskini katu.

Anaamua kufanya kazi ya mgodi na kuwatumikisha vijana ili kukimu hali yake ya kiuchumi.

Ni mwenye majivuno.

Anajishaua mbele ya Makucha kuwa yuko kazini na gari lake na kuipuuza kazi yake ya kuuza vitafunio kando ya barabara.

Umuhimu wa Makutwa

Ni kiwakilishi cha marafiki wanafiki ambao wanalenga tu kujifaidi kutokana na marafiki zao bila wao kuwafanyia lolote la haja.

Kupitia kwake, matendo ya kihuni katika jamii yanadhihirika kupita kazi yake ya mgodi

Anadhihirisha jinsi wenye nafasi ya hali hutumia hali ya umaskini miongoni wa vijana kuwakandamiza.

Bi. Macheo

Ni mdadisi.

Anamzungusha mumewe kichwa kwa maswali.

Anamsaili kuhusu rafikiye Makutwa anakopeleka watoto anaowapakia kwenye gari, kwa nini aendeleze urafiki wake naye na kwa nini amkaribishe kwake.

Ni mwenye makini.

Anashuhudia kila tukio baina ya mumewe na Mzee Makutwa.

Anamwona akipakia vijana kwenye gari lake asijue aendako.

Pia, anagundua jinsi Makutwa anavyomdhihaki mumewe.

Ni mshauri.

Anampendekezea mumewe kukomesha uhusiano wake na Makutwa kutokana na shughuli zake zisizoeleweka na pia kwa jinsi anavyomkosea heshima.

Ni mwenye bidii.

Anamsaidia mumewe pakubwa katika kuzumbua riziki.

Anauza kaimati na vitumbua kwenye veranda ya nyumba yao.

Umuhimu Wake

Ni kiwakilishi cha wanawake wenye bidii na wanaowasaidia waume zao katika shughuli za kuzumbua riziki.

Kupitia kwake, umuhimu wa ndoa katika jamii unabainika na nafasi yake kwa wahusika kujengana.

Anawakilisha changamoto za maisha kwa jumla na jinsi ya kuzikabili.

Anawakilisha nafasi na majukumu ya mwanamke katika ndoa na jamii kwa jumla.

Mbinu za Uandishi

Semi

kujitanua kifua- kujigamba

unayepakwa mafuta kwa mgongo wa chupa- unayehadaiwa/unayedanganywa

wasio na mbele wala nyuma- wasio na lolote la maana, wasio na thamani

alipigwa kalamu- alifutwa kazi

kumpa kisogo- kumwacha, kumtenga

kuponda raha- kujivinjari, kujifarahisha

iliwapiga chenga- iliwazidi maarifa, iliwakwepa

kujiendea shambiro- kujiendea huku na huku ovyoovyo

alitega sikio- alisikiza kwa makini

hoi bin taabani- katika hali mbaya

akiwa na moyo mzito- akiwa na hisia nyingi

Istiara

Sinema hiyo ya kikatili ilijibainisha mbele yao ....

Maajabu ya Firauni ndiyo haya!...

Aliyedhani ni rafikiye kumbe alikuwa mbwamwitu aliyevaa ngozi ya kondoo.

Ndani ya pango, mbio za paka na panya zilishamiri

Kinaya

Mzee Makutwa anasemekana kuwa anashinda tu kujumuika na vijana, hata wazee wenzake hana muda wa kubarizi au kuongea nao.

Makutwa anaposimamisha gari kwenye biashara ya Makucha, anamwambia kuwa hakukusudia kumwudhi.

Tendo la kutapakaza vumbi kwenye bidhaa zake na kejeli kuhusu bintiye ni wazi kwamba ananuia kumwudhi.

Makutwa anamwambia kuwa atawarejesha vijana wale katika kazi hiyo katika uwepo wa askari.

Tayari ana makosa na anaongezea mengine.

Makutwa anamwambia Makucha kuwa alidhani ni rafiki wa dhati.

Ni kinaya kwa kuwa Makutwa mwenyewe si rafiki wa dhati hata kidogo.

Hakumsaidia akiwa waziri na kila mara humkejeli.

Sadfa

Shirika la reli analofanyia kazi Mzee Makucha linamfuta kazi.

Wakati akitafuta haki, shirika lenyewe linasambaratika.

Anakosa hata marupurupu yake.

Mzee Makucha anawazia nyendo za Mzee Makutwa za kuwabeba vijana katika gari lake kila mara.

Wakati huo huo, anashtukia Makutwa mwenyewe amepiga breki mbele yake.

Mzee Makucha anapowazia kazi aliyofanya Makutwa, Sai na Dai wanakuja na kununua kashata kisha kuanza kuzilia hapo.

Wanaanza kuzungumzia gari la Makutwa, na kumtia Makucha shaka zaidi.

Huku vijana hawa wawili wakiendelea kuwasiliana, gari la Makutwa wanalozungumzia linawasili.

Kisadfa, mara hii si Makutwa analiendesha bali kijana machachari. Inakuwa rahisi kwa Makucha kuliandama.

Inasadifu kuwa Mzee Makucha anapofika kwenye mgodi wa Makutwa, mwenyewe hayupo.

Anaweza kufahamu jinsi anavyotesa vijana, na kuwa anatumia jina bandia la Mamboleo.

Mzee Makucha anapowachukua polisi na kwenda nao mgodini, inasadifu kuwa Mzee Makutwa amerudi, na hivyo wanafaulu kumkamata.

Methali

Ujana ni moshi

Jambo usilolijua ni usiku wa giza.

Mwomba Mungu hachoki

Tashbihi

Machungu yaliyompata ni sawa na yale ya kupigiliwa msumari wa moto kwenye kidonda kibichi.

Matarajio yake ya kuwa na maisha mema yakaporomoka kama jabali la barafu juani.

Hawa walikuwa wakidondoa vijiwe vidogovidogo vyenye kung9aa ungedhani walikuwa wakitenga ndume kwenye mchele.

Usiku walilala kwenye mabanda yaliyojengwa kigugu mfano wa mazizi ya ng'ombe.

Alisimama mahali alipokuwa kama sanamu.

Mzee huyo...baada ya kufungwa kama mbuzi anayepelekwa kichinjioni.

Majazi

Makutwa.

Ina maana mbili, mchana mzima(kutwa) au kupatikana.

Mzee Makutwa anazurura na gari lake mchana kutwa kwa shughuli ambazo hazieleweki.

Pia, anakutwa katika uhalifu wake na kutiwa ndani.

Makucha.

Ina maana mbili pia, usiku mzima au kupambazuka(kucha), na pia kucha kubwa.

Kila kuchapo, yuko mbioni kunogesha biashara yake.

Pia ana 'Makucha', yaani uwezo mkubwa wa kupata atakacho.

Makucha yake yanadhihirika kupitia bidii zake.

Anatafuta haki anapofutwa kazi na pia kumnasa Makutwa.

Macheo.

Ina maana ya wakati wa jua kuchomoza, ishara ya matumaini.

Ni 'macheo' katika maisha ya mumewe.

Anamsaidia kuzumbua riziki na kumshauri panapohitajika.

Riziki.

Ni bintiye Makucha anayetoroka kuolewa na Mhindi.

Neon hili lina maana ya uwezo wa kujikimu au baraka kutoka kwa Mungu.

Anaamua kusaka riziki yake kupitia kuolewa na Mhindi na pia anapata baraka za mume.

Kazakamba.

Mji wanakoishi kina Makucha. Kila mtu huku amekaza kamba, yaani kujitolea, ili kuboresha maisha.

Kuna wanaochuuza bidhaa na wanaofanya uhuni.

Sai na Dai.

Sai ina maana ya kuudhi au kuwa mshindani.

Dai nalo lina maana ya kutoa maoni au kupendekeza jambo.

Sai anajibu maswali ya Dai kwa ushindani huku naye Dai akimtolea pendekezo la kupanda kwenye gari la Makutwa.

Tashihisi

Maneno ya mkewe yalimtwanga kichwa Mzee Makucha.

Ujana ulikwisha kumpa kisogo lakini alikuwa akiukimbiza.

Alikuwa akiufukuza na kujaribu kuukamata.

Magari hayo yalianza kuteremka kwenye bonde kubwa ambalo lilificha kabisa miale ya jua.

Jazanda

Shirika la reli alilohudumia tangu macheo ya maisha yake.

Tayari alikuwa katika magharibi ya maisha yake

Huu sio wakati wa kujenga kichunguu bali wa kustarehe ndani ya kichunguu.

Heri wewe unayestaladhi katika machweo ambayo sasa ni mapambazuko kwako.

Ukiumwa na nyuki, hauna haja ya kujitwika jukumu la kuharibu mizinga yote ya asali.

Hujui faida ya nyuki ulimwenguni?

Uliamua kurina asali ya nchi.

Magharibi ikamkuta akigaragara kwenye sakafu baridi huku akisubiri kufunguliwa mashtaka.

Mkono wa sheria nao ukamsukuma kuyakabili machweo ya maisha yake kifungoni.

Ingawa nimefikia magharibi ya maisha yangu, sudi hii imenipa tumaini la mapambazuko mapya maishani.

Nahisi kwamba jua la asubuhi limeniangazia miale ya matumaini mapya, hata kama machweo yako karibu!

Dayolojia

Mazungumzo kati ya Makucha na mkewe kuhusiana na urafiki wake na Makutwa.

Mazungumzo kati ya Makutwa na Makucha katika biashara ya Makucha kuhusiana na hali zao na kazi zao.

Mazungumzo kati ya Sai na Dai kuhusiana na maisha na jinsi ya kuishi baada ya kuhitimu wanapokuja kununua kashata kwa Makucha.

Mazungumzo kati ya Makutwa na Makucha kwenye mgodi baada ya Makutwa kukamatwa na polisi.

Uzungumzi Nafsia/Monolojia

Kwa nini niendelee kumstahi mtu asiye na fadhila kama yule? Aliwaza.

''Kazi? Kazi gani hii ya kubebana na vijana mchana kutwa? Maajabu haya!''

Gari aina ya probox? Mzee Makucha aliwaza. Hilo silo la Mzee Makutwa? Ndiye pekee Aliya na gari la aina hiyo hapa mjini. Kwani kipi kinaendelea?

Mzee Makucha.....aliendelea kujismemea, Utumwa mamboleo ndio huu. Ubedui uliogubikwa ndani ya ukawaida wa kisasa ndio huu.

Balagha

''Sasa mtu akija kwako kukujulia hali umfukuze? .... Je, alinisaidia alipokuwa waziri?...''

''Sasa mbona wamkaribisha humu mwako nyumbani kila anapobisha? Anapokukebehi na kututafishi hapa mbona unamvumilia?... Mbona hunielewi?''

Kwa nini niendelee kumstahi mtu asiye na fadhila kama yule?

''Huchoki kukaa hapa ukichuuza akali ya vitu kama hivyo?''

''Aliolewa au alitoroshwa? Mbona unaniuliza swali unalojua jibu?''

''Kazi? Kazi gani hii ya kubebana na vijana mchana kutwa?''

Hilo silo la Mzee Makutwa? ...... Kwani kipi kinaendelea?''

''Kwa nini nisilipie? Mnadhani mashaibu kama sisi ni mafukara hohehahe hatuna hata pesa mfukoni?''

Taswira

.....alishtukia kumwona Mzee Makutwa amepiga breki karibu na pahali alipoketi.

Vumbi la hudhurungi lilitapakaa na kutulia juu ya vitanufaji alivyokuwa akichuuza.

Mzee Makutwa alitamka na kuondoka kwa kasi huku akitifua vumbi liliofunika gari lake na kufanya wingu kubwa hewani.

Gari la probox liliacha barabara kuu na kupenya kwenye barabara ndogo ya mchanga... lilifuata taratibu kutokana na mashimo yaliyowatatiza madereva hao... walijikuta wanaingia ndani ya gongo la mwitu.

Kulikuwa na miti mikubwa iliyofanya kivuli pande zote ungedhani jua la kutwa limewasili.

Magari hayo sasa yalianza kuteremka kwenye bonde kubwa ambalo lilificha kabisa miale ya jua.

Mteremko ulikuwa mkali& Walikaribia mahali ambapo palikuwa na tambarare kubwa lililopambwa kwa viduta vidogovidogo vya mchanga.

Upande wa kulia wa tambarare hilo, kulikuwa na umati mkubwa wa vijana waliokuwa wakiupepeta mchanga na kuugawa mafungu....walikuwa wakidondoa vijiwe vidogovidogo vyenye kung'aa .....Walisimamiwa na wanyapara waliokuwa wakiwaamrisha kwa sauti za kutisha.

Humo pangoni, mlikuwa na taa za vibatari zilizowekwa kandokando ya njia ili kuondoa utusitusi uliokuwa mle.

Mzee huyo alipishana na vijana..... wakichimba madongo ya mchanga na kuyatia ndani ya mkokoteni.

Walikuwa wameloa jasho kutokana na uhaba wa hewa mle ndani.

Mavulia waliyovaa ni yale yaliyouzwa majiani..... Usiku walilala humo katika mabanda yaliyojengwa kigugu..... Ua wa stima uliozungushiwa makazi haya pamoja na mabawabu katili wenye majibwa makubwa....

Taharuki

Kazi ya Makutwa inatia kila mmoja taharuki.

Anaonekana kila mara akibeba vijana mitaani kuelekea kusikojulikana.

Hata hana muda wa kuzungumza na kukaa na wazee wenzake.

Tunashangaa kipi hasa kinachomweka ukaribu na vijana, hadi hatimaye tunapojua biashara anayofanya.

Bintiye Makucha, Riziki, anashindwa kuvumilia umaskini na kuolewa na Mhindi.

Hatujaambiwa hali ya maisha anayokumbana nayo huko.

Makucha anasikiliza mazungumzo ya Sai na Dai na kujua wanasubiri gari la Makutwa waende nalo.

Hapo hamu yake ya kujua inazidi. Anapanda teksi na kuwafuata. Hamu ya kujua afanyalo Makutwa inapanda.

Mazingira wanayopita Makucha wanapofuata gari la Makutwa yanatia taharuki.

Wanaingia kwenye gongo la mwitu na kupitia barabara yenye mashimo kisha kupata tambarare kubwa.

Tuna hamu ya kujua mambo yanayoendelea huku.

Mbinu nyingine ni pamoja na Kuchanganya ndimi, Nidaa, Takriri, Mbinu Rejeshi, Chuku, Utohozi, kejeli na Koja.

Join our whatsapp group for latest updates

Download Mapamazuko ya Machweo summary notes - Mwongozo wa Mapamazuko ya Machweo na Hadithi Nyingine.


Tap Here to Download for 50/-
Why download?

  • ✔ To read offline at any time.
  • ✔ To Print at your convenience
  • ✔ Share Easily with Friends / Students


Get on WhatsApp Download as PDF
.
Subscribe now

access all the content at an affordable rate
or
Buy any individual paper or notes as a pdf via MPESA
and get it sent to you via WhatsApp

 

What does our community say about us?