Harubu ya Maisha summary notes - Mwongozo wa Mapamazuko ya Machweo na Hadithi Nyingine

Share via Whatsapp


Harubu ya Maisha - Paul Nganga Mutua

Mtiririko

Utulivu wa mazingira unamsahaulisha msimulizi(Kikwai) mpito wa wakati hadi anapopokea simu ya Mama Mercy(mkewe) akilalamika kuwa mtoto atalala.

Anagundua ni saa nne kasorobo usiku na kufunga kazi na kuondoka ofisini.Hakuna msongamano wa magari.

Anapofika Kenyatta Avenue, anagundua simu inaita.

Ni mamake amepiga.

Haipokei bali anaamua kumpigia akifika nyumbani.

Anapofika nyumbani, analakiwa na malalamishi ya bintiye, Mercy, ya njaa.

Mama Mercy anamwambia kuwa hapendi mambo ya kukopa na ndio maana hakupika, kwani ndani ya nyumba hamna chakula.

Analalamika kuwa alikuja likizo lakini Kikwai hana muda wake.

Kikwai anamweleza kuwa ni hali kazini ilivyo, haimruhusu kuwa naye.

Mercy anashtakia njaa tena na hapo Kikwai anaelekea kwa Vaite.

Anamkopesha unga na mayai mawili.

Kikwai anamlisha Mercy na kuelekea kulala, kwani hataki kula hali mkewe hali.

Mama Mercy analalamikia mapuuza ya Kikwai kwenye malazi.

Kikwa anamweleza kuwa wako katika shughuli za kuandaa vitabu vya kuwasilisha kwa baraza.

Hawajalipwa miezi miwili.

Anaahidi kusema na Bosi siku inayofuata.

Anamwambia aende na Mercy kazini lakini anapinga kuwa hilo haliwezekani.

Anapotega majira ya kuamka kwenye simu, anakumbuka kumpigia mama.

Anapokea na kumweleza hali yao ngumu, akitaka msaada.

Anamweleza kuwa fundi wa nyumba anatishia kutwaa mali yao kufidia malipo yake yaliyochelewa mwezi mzima.

Kikwai anamwomba kuzungumza naye asubiri, anaahidi kuwakumbuka akipokea malipo.

Asubuhi, anaamshwa na kilio cha Mercy ambaye anamshtakia njaa.

Anamwahidi kumnunulia kitu ale, kisha anaamka kujiandaa kwenda kazini.

Anakumbuka awali.

Alikuwa na mshahara mdogo lakini uliwakimu, hadi Mama Mercy alipokuwa mja mzito na kujifungua.

Mercy naye akawa na mataizo yaliyowagharimu, na hata sasa anahitaji vitu vya shule.

Kazini nako mshahara umeanza kucheleweshwa na kufanya mambo kuwa changamano zaidi.

Anapofika kazini, Bosi anampigia simu kumwita ofisini.

Anamwuliza kuhusu mwenzake, Nilakosi, ambaye anaandaa ripoti ya tathmini ya mswada fulani.

Bosi anasema mkataba wake wa miezi miwili huenda ukakatizwa kwa kuwa hali si nzuri.

Anaahidi kutoa jibu kuhusu kadhia ya Nilakosi, ambaye ametishiwa na mpangishaji kumfungia nyumba.

Anaomba advansi, angaa elfu tano alipe kodi.

Anaitwa na Bosi tena, akimtaka aende kwake(Bosi) akampeleke mwanawe aliyeugua hospitali.

Anamweleza kuwa hakuja kwa gari alilokabidhiwa na kampuni kwa kukosa mafuta.

Bosi anakasirishwa na hili na kumtaka kurudi kazini.

Siku inayofuata, Bosi haji. Wanapofunga kazi na Nilakosi, wanatembea.

Anawazia hali ya familia yake. Tatizo lake kubwa ni Mercy, kwani hawezi kuelewa hali.

Langaoni la kuingia kwake, anapata bango la wazazi wanaotafuta kurithi mtoto wa kike.

Anamwazia Mercy, jinsi anavyotaabika kumkimu na uhusiano wake na Mama Mercy ulivyoathirika vibaya.

Anapofika, anajulishwa kuwa Mercy alishindwa kula ugali wenye ladha na harufu ya mafutataa, alibahatika tu na ndizi mbili kutoka kwa shangazi yake aliyewatembelea.

Anamtembelea Bishop wake, ambaye anamsaidia kwa chakula cha siku hiyo.

Kikwai anafika ofisini.

Anapata arafa ya Nilakosi kuwa hatafika kazini kwani hali ni ngumu.

Bosi anaingia ofisini na kumpigia simu afike humo mara moja.

Anataka amweleze sababu ya kutofika kazini na gari la kampuni.

Anapokea simu na kueleza kuwa mwanawe yuko salama.

Kikwai anamweleza kuwa alikosa pesa.

Bosi anadai kuwa Kikwai anaweka pesa mbele ya maslahi ya kazi.

Anamwagiza amwone mhasibu kupokea mshahara wake kisha arejeshe vitu vya kampuni.

Anapitia duka la Tuskys na kununua chakula na vitu vya kutumia na kwenda nyumbani.

Baada ya kuandaa chakula na kula, anapumzika kidogo, kisha kuchukua kipakatalishi kuipiga msasa tawasifu kazi.

Mercy anaingia na mara hii kushtakia shibe.

Ufaafu wa anwani 'Harubu ya Maisha'.

Harubu ina maana ya taabu anayopata mtu.

Maisha yamejaa harubu katika hadithi hii.

Simu ya Mama Mercy ndiyo inamtoa Kikwai ofisini, huku akilalamika kuwa mtoto atalala.

Ni wazi kwamba mambo si mazuri upande huo.

Anapofika, anapata kuwa Mama Mercy hajapika kwa kuwa hataki kukopa.

Mercy anamshtakia njaa mfululizo.

Mama Mercy anamzidishia Kikwai harubu kwa malalamishi yake kila mara.

Analalamika kuwa Kikwai anamtelekeza na kuwa hawajibikii wajibu wake.

Anasema kuwa yeye alikuja likizo hali mambo yako hivyo, hawapati muda wa kuwa pamoja.

Hata anamtaka mumewe aandamane na Mercy kazini.

Kikwai analazimika kulala njaa kwa kuwa mkewe hajala.

Haoni haja ya kula mkewe akiwa humo humo hali yeye hali. Isitoshe, chakula chenyewe kina ladha ya mafutataa.

Wanaendelea kuzozana kwenye kitanda.

Kikwai anapokumbuka kumpigia mamake, anampasha taarifa ya harubu walio nayo, angaa awasaidie.

Anamweleza kuwa fundi wa nyumba anatishia kutwaa mbuzi wao ili awauze ajilipe deni ambalo limecheleweshwa karibu mwezi mzima.

Hii ni harubu nyingine kwa upande wa Kikwai, kwani hana la kuwafaa, ila anaahidi kumtumia hela mwisho wa mwezi akipata mshahara.

Kikwai anaamshwa na kilio cha Mercy asubuhi, ambaye analalamikia njaa.

Anajiandaa kwenda kazini huku akikumbuka harubu alizokuja nazo Mercy.

Mahitaji mengi, mara mafua na meno, mara atie punje za mahindi sikioni au puani na kulazimu kiadi na daktari, hadi sasa anapohitaji sare za shule, kalamu, madaftari, karo na mengine.

Kazini, Nilakosi pia ana harubu yake.

Mkataba wake wa miezi miwili unafupishwa kuwa mmoja, na pia anapata matatizo ya nyumba.

Mpangishaji wake anatisha kumfungia nyumba kwa kuwa hajalipa kodi, anadhani anataka kumlaghai.

Japo Bosi anatoa ahadi kutoa jibu, hafanyi hivyo.

Bosi analalamika kuwa Kikwai hafai kuacha gari la kampuni, ilhali hana pesa za kulitia mafuta.

Anamtaka pia kwenda kwake kupeleka mtoto wake hospitalini kwa gari hilo.

Siku inayofuata, haji kazini. Kikwai na Nilakosi wanalazimika kutembea kwani hawana hela za kupanda gari.

Tatizo kuu la Kikwai ni Mercy ambaye hawezi kuelewa hali ilivyo.

Kikwai anafika nyumbani na kuambiwa kuwa Mercy alikataa kula ugali wenye ladha ya mafutataa.

Alibahatika tu kupata ndizi mbili kutoka kwa shangazi yake aliyekuja kuwatembelea.

Yanapomzidia, anaamua kwenda kwa Bishop ambaye anawaauni kwa chakula cha siku hiyo.

Nilakosi anazidiwa na kushindwa kabisa kufika ofisini.

Kikwai anapofika anapata wito wa Bosi kufika ofisini mwake.

Bosi analalamika kuwa anajali pesa kuliko kampuni, eti sababu haji kwa gari la kampuni kwa kukosa pesa za mafuta.

Hivyo, anaafutwa kazi na kulipwa mshahara anaodai. Huu unaondokea kuwa mwisho wa harubu ya maisha, lakini ukawa mwanzo wa nyingine.

Analazimika kuishughulikia tawasifu kazi yake ili kuanza kusaka ajira mpya.

Maudhui

Kazi

Kikwai anatia kila juhudi katika kazi yake ili kujipa riziki.

Anapopigiwa simu na mkewe, bado yuko ofisini akiendelea na kazi, saa nne kasorobo.

Anapopanda kitandani, anamweleza mkewe hali ilivyo kazini.

Anamwambia kuwa wanaandaa vitabu vya kuwasilishwa kwenye wizara.

Haikosi anafanya kazi katika kampuni ya uchapishaji. Isitoshe, anamweleza kuwa hawajalipwa mshahara kwa miezi miwili sasa.

Anatega majira ya kuamka kwenye simu ili awahi kazini. Anapoamshwa na kilio cha mwanawe, halali tena bali anajiandaa kwenda kazini.

Anakumbuka awali jinsi kazi ilivyomkimu na mkewe, licha ya mshahara kuwa mdogo.

Baadaye anakuja Mercy na mahitaji yake yanayonyonya pesa vilivyo.

Isitoshe, kazini nako mishahara inaanza kucheleweshwa. Hali hii inasababisha matatizo ya kutoelewana kati yake na mkewe.

Kazini, yupo Nilakosi anayefanya kazi kwa kandarasi(contract) ambayo inatarajiwa kuisha baada ya miezi miwili.

Hata hivyo, inpunguzwa hadi mwezi mmoja kutokana na upungufu wa mauzo.

Kwa sasa, yuko katika harakati za kuandaa ripoti ya tathmini ya riwaya fulani aliyofanya.

Kazi hii ndiyo inamkidhia mahitaji an kutokana na kuchelewa mshahara, anaanza kutishiwa kufungiwa nyumba kwa kuwa hajalipa kodi.

Bosi anawahangaisha wafanyakazi vilivyo.

Anaahidi kutoa jibu la suala la Nilakosi lakini hasemi lolote.

Pia, anamtaka Kikwai kwenda kwake kumpelekea mwanawe hospitali akidai magari ya kampuni ni ya dharura kama hizo.

Anakosa kufika kazini siku inayofuata.

Nilakosi na Kikwai wanalazimika kusafiri kwa miguu kwani hawana hela.

Siku inayofuata, Nilakosi anashindwa kufika kazini, hali ni ngumu.

Kikwai naye anaitwa na Bosi na kupigwa kalamu kwa kisingizio cha kuthamini pesa Zaidi ya kampuni kwa kuwa haji na gari la kampuni, sababu hana pesa za kulitia mafuta.

Analipwa mshahara wake na kuagizwa kurudisha mali ya kampuni.

Maisha lazima yaendelee.

Anaanza kushughulikia tawasifu kazi yake ili kutafuta kazi nyingine.

Migogoro Usemi wa Mama Mercy anapompigia simu Kikwai una ladha ya mgogoro.

Anamwuliza sababu ya kutofika hali mtoto aelekea kulala.

Anapofika nyumbani, mgogoro wao unaonekana wazi.

Anamweleza kuwa hajapika kwa kuwa hakutaka kukopa.

Wanapoenda kulala, Mama Mercy analalamika kuwa mumewe hatimizi wajibu wake, na hata kumtaka kuandamana na Mercy kazini.

Mama anamweleza Kikwai mgogoro kati yao nyumbani na fundi wa nyumba. Wamemcheleweshea malipo yake kwa karibu mwezi mzima na sasa anatishia kutwaa mbuzi wao na kuku kuuza ili kujifidia malipo hayo.

Kikwai anagongana na Bosi baada ya kuacha gari la kampuni nyumbani kwa kukosa mafuta.

Bosi anadai kuwa linafaa kuwa katika kampuni kila mara ili kutumika wakati wa dharura.

Mgogoro huu ndio hatimaye unatumika kama kisingizio cha kumwachisha kazi, eti kwa kuwa anathamini pesa zaidi ya maslahi ya kampuni.

Nilakosi pia ana mgogoro na mpangishaji(landlord) wake, kwani mwezi unaisha na hali hajalipa kodi.

Landlord huyu anahofia kuwa Kikwai anataka kumlaghai.

Umenke.

Ni hali ambapo wanawake huwadhulumu wanaume katika jamii; kinyume cha ubabedume.

Hali hii inadhihirishwa na Mama Mercy kwa jinsi anavyomtendea Kikwai, mumewe.

Anampigia simu na kumlazimu kuondoka ofisini akilalamika kuwa mtoto yuko karibu kulala.

Hata anapofika nyumbani, hamlaki kama mume bali anatulia tu kwenye pembe ya kochi.

Kikwai anampata Mama Mercy hajapika kwa kuwa hamna chakula.

Anasema kuwa hapendi mambo ya kukopa.

Kikwai analazimika kwenda kwenye duka mwenyewe kukopa.

Anaporudi nyumbani, anaandaa chakula na kumlisha mwanawe, kasha anaelekea kitandani.

Mama Mercy analalamika kuwa mumewe anawaacha pale na kurudi tena jioni bila chochote.

Hataki kusikiliza kuwa hajalipwa na pia anajaribu awezavyo kukidhi mahitaji yao.

Anamfokea na hatimaye kumtishia kuwa ataenda na Mercy kazini.

Anadai kwamba alikuja likizo ili aweze kujistarehesha.

Hafanyi lolote kumsaidia mumewe kusaka riziki.

Kikwai anaeleza hali ilivyokuwa awali.

Mshahara wake mdogo unawakidhia mahitaji yote, hadi Mama Mercy anapohimili na kujifungua Mercy.

Anayaleta mahitaji mengine yanayomhangaisha Kikwai.

Mama mercy anaathiriwa sana na mabadiliko ya kazini ya kuchelewa kwa mshahara wa mumewe.

Baada ya kulipwa na kuachishwa kazi, anaeleza kuwa anapita kwenye duka na kununua chakula na vitu vya nyumba na kurudi nyumbani.

Ajabu ni kuwa anapofika, bado ndiye anaandaa chakula, wanakula, kisha anaingia kwenye kipakatalishi chake kuipiga msasa tawasifu kazi yake.

Ndoa

Kuna ndoa kati ya Kikwai na Mama Mercy inayodhihirisha misukosuko tele. Wanapooana, mambo yamenyooka kwani mshahara wa Kikwai unawakimu japo ni mdogo.

Kisha Mama Mercy anapata mimba na kujifungua Mercy, anayekuja na mambo yake.

Mafua, meno na kutia punje za mahindi kwenye pua na masikio.

Sasa anahitaji karo, sare, madaftari na kalamu.

Mama Mercy anaanza kumlalamikia mumewe kila mara baada ya suala la kuchelewa kwa mishahara.

Anamlaumu wala haamini anapomweleza hali ilivyo. Anasusia kupika kwa kuwa hakuna chakula wala hapendi kukopa.

Kikwai analazimika kumshughulikia mtoto wao, Mercy, mwenyewe. Ndoa hii pia inadhihirisha umenke.

Mama Mercy anashinda nyumbani mchana kutwa lakini Kikwai anapotoka kazini, analazimika kuja kupika.

Mama Mercy pia anamfokea kila mara, baada yake kufokewa na Bosi huko kazini.

Malezi

Kikwai na mkewe wanakabiliwa na changamoto kubwa ya kumlea mwana wao, Mercy.

Awali, mambo yako sawa hadi anapozaliwa Mercy.

Anakuja na mahitaji ya hapa na pale ambayo yanamhanagaisha Kikwai.

Mara ana mafua na matatizo ya meno, kasha atie punje za mahindi kwenye pua na masikio na kulazimu miadi na daktari.

Sasa anahitaji sare, karo, madaftari na kalamu. Mama Mercy anamtoa Kikwai ofisini akimweleza kuwa mtoto karibu analala.

Analazimika kuacha kazi kwenda kumshughulikia. Anapofika, anamshtakia njaa.

Analazimika kwenda kukopa chakula na kuja kumpikia.

Anamlisha na kumpeleka kulala. Mercy anamwamsha tena asubuhi kwa kilio kingine cha njaa.

Anamwahidi kumnunulia kitu huku akijiandaa kwenda kazini.

Anaporudi, anaambiwa kuwa alikula ndizi mbili tu kutoka kwa shangazi, baada ya kukataa ugali wenye ladha ya mafutataa.

Kikwai anamkimbilia Bishop kwa msaada wa chakula kulisha familia yake.

Siku inayofuata, anapigwa kalamu, lakini analipwa mshahara wake wa awali. Ananunua chakula kingi na kurejea nyumbani.

Anapikia familia yake na wanapokula, anaanza kuipiga msasa tawasifu kazi, tayari kutafuta ajira nyingine kukidhi mahitaji yao.

Ukengeushi/Mkengeuko

Ni tabia ya Waafrika kufuata maadili ya kimagharibi na kutupilia mbali maadili ya nyumbani.

Unadhihirika kupitia kwa Mama Mercy. Anamfokea mumewe kila mara akilalamikia hali ya maisha licha ya kuwa anajitahidi.

Hata anamtaka kuandamana na Mercy kazini. Isitoshe, mumewe ndiye anapika kila mara hata baada ya kuchanika kutafuta chakula chenyewe.

Haya ni mambo ambayo hayafai kulingana na jamii ya Kiafrika. Anafaa kumheshimu mumewe na kumtumikia. Maudhui mengine ni pamoja na Njaa na Umaskini, Mazingira, Dhiki na Usaliti.

Wahusika: Sifa na Umuhimu.

Kikwai

Ni mwenye bidii.

Anajitoa na kujituma katika kazi yake.

Anagutushwa saa nne kasorobo na simu ya mkewe, bado akiendelea na kazi ofisini mwake.

Hata anapokosa mafuta ya gari, anaamka mapema ili kutembea kwenda kazini.

Ni mwajibikaji.

Anafanya kila linalotarajiwa kutoka kwake, nyumbani na kazini.

Anaikimu familia yake kwa kila hali licha ya ugumu wa maisha uliopo.

Anafika kazini kwa wakati kila siku.

Ni mwenye Imani/tumaini.

Kila mara anaamini kuwa maisha yatakuwa bora.

Anamsisitizia Mama Mercy kuwa hali waliyo nayo ni ya muda tu.

Anapoachishwa kazi, anaanza kuipiga msasa tawasifu kazi yake kwa matumaini ya kupata ajira mpya.

Ni mkakamavu.

Anamsisitizia Mama Mercy kuwa anashughulika kila mara ili kuboresha maisha yao.

Anakataa katakata kuandamana na Mercy kazini.

Anapitia dhiki nyingi lakini anazikabili kwa ukakamavu.

Umuhimu wa Kikwai

Ni kiwakilishi cha mashaka ya maisha kwa jumla, hasa kwa watu wanaoishi mijini.

Ni kielelezo cha bidii katika utendakazi na umuhimu wake katika maisha.

Ni kiwakilishi cha dhuluma za kindoa zinazotekelezwa dhidi ya mwanamume.

Ni kielelezo cha mwanandoa na mlezi mzuri na nafasi yake katika kuimarisha maisha ya familia yake.

Mama Mercy

Ni mbishi.

Kila mara anazozana na mumewe kuhusiana na suala la kazi.

Japo Kikwai anamweleza kuwa hali iko hivyo, hataki kumwelewa.

Ni mkakamavu.

Anapofanya uamuzi, harudi nyuma.

Anakosa kupika kwa kuwa hataki mambo ya mikopo.

Anamzoza mumewe na hata kumtishia kuwa ataenda na Mercy kazini.

Ni mwenye mapuuza.

Anampigia mumewe simu na kumweleza bintiye yuko karibu kulala.

Hajapika wala kumlisha mtoto.

Kikwai anapofika, amejikunyata kochini wala hata hamsabahi.

Amekengeuka.

Anamtelekeza mumewe na kumgombeza kila mara.

Mumewe anatoka kazini na kuja kupika yeye akiwepo tu wala hajali chochote.

Ni mstaarabu.

Anahiari kutopika badala ya kukopa.

Pia, Vaite anamwambia Kikwai kuwa amemkopesha kwa heshima ya mkewe, ambaye si mmbea kama wanawake wengine pale.

Umuhimu wake

Kupitia kwake, matatizo ya ndoa yanadhihirika wazi.

Ni kiwakilishi cha wanawake wa kisasa wanaowatumikisha waume zao bila shukrani

Ni kielelzo cha wanawake wanaojiheshimu, ambao hawajihusishi na umbea wa mitaani.

Ni kiwakilishi cha migogoro katika jamii

Bosi

Ni dhalimu.

Anawahangaisha wafanyakazi wake ikiwemo Kikwai na Nilakosi.

Anamtaka Kikwai kwenda kwake kupeleka mwanawe hospitali akidai ni dharura.

Suala hilo halihusiani na kampuni.

Anamfuta kazi kwa kisingizio cha kuthamini pesa zaidi ya kampuni.

Ni mbishi.

Anadai kuwa kwa vyovyote vile, Kikwai anafaa kuja kazini kwa gari la kampuni, licha yake kumweleza matatizo anayopata kuhusu mafuta.

Hatimaye, anatumia hilo kumfuta kazi.

Ni mwenye mapuuza.

Haoni sababu ya Kikwai ya kutofika kazini na gari la kampuni licha ya kuwa hana pesa.

Anamfuta kazi bila habari, wala hajali atakakokwenda.

Ni mbinafsi.

Anajali maslahi yake tu.

Kila mara anamwitaita Kikwai ofisini kumpa majukumu lakini hajali maslahi yao.

Anamtaka akampeleke mwanawe hospitalini.

Anaahidi kuangazia suala la Nilakosi ila siku inayofuata haji kazini.

Ni mwenye dharau.

Anamwambia Kikwai kuwa anathamini pesa zaidi ya kampuni, na hivyo anataka kumpumzisha kwa kumwachisha kazi, ili asiwe na bughudha ya kufanya kazi na kucheleweshwa mshahahara.

Umuhimu wa Bosi

Ni kiwakilishi cha udhalimu unaotekelezwa katika sehemu za kazi

Anadhihirisha baadhi ya migogoro inayoshuhudiwa katika jamii.

Kupitia kwake, uhusiano kati ya kazi an familia unadhihirika.

Nilakosi.

Ni mwenye bidii.

Anafanya kazi yake kwa bidii.

Amemaliza kutathmini riwaya, yuko katika harakati za kuandaa ripoti.

Ni mwajibikaji.

Anatimiza wajibu wake kama mfanyakazi wa kampuni na kuwasili kazini hali inaporuhusu.

Umuhimu wa Nilakosi Anadhihirisha hali ya mazingira ya kazi na uhusiano baina ya wafanyakazi unavyofaa kuwa.

Kupitia kwake, taabu za maisha, hasa ya mjini zinabainika.

Bishop

Ni mfadhili.

Anamkaribisha Kikwai kwake na kumsaidia kwa chakula.

Ni mcha Mungu.

Ni mhubiri, na pia anamsisitizia Kikwai kuwa Bwana amekuwa mwaminifu.

Ni mwaminifu.

Kikwai anakumbuka akisema kuwa kwake chakula hakiwezi kukosa. Anapomwendea kwa msaada wa chakula, hakika anakipata.

Ni mwenye utu.

Anamsaidia Kikwai kwa chakula na hata kukataa rai yake ya kumfanyia kazi.

Umuhimu Wake

Kupitia kwake, nafasi ya dini katika jamii inabainika.

Ni kiwakilishi cha utu katika jamii.

Anasaidia kuonyesha uzito wa dhiki zinazomkumba Kikwai katika maisha yake.

Mbinu za Uandishi

Balagha

''Saa ngapi? Si wajua mtoto angali anakusubiri?...''

Lakini mtu anawezaje kula chakula mkewe akiwa na njaa, tena hapo hapo katika chumba kimoja?

''Sasa unataka nifanye nini?... Na mishahara? Sasa miezi miwili imetimia...''

''Hivi, kwani huko kazini wanasemaje? Si karibuni itatimia miezi miwili; miezi miwili bila malipo! Wanafikiri mnakula nini?''

Sasa kuna hili jipya la kucheleweshwa mishahara. Kisa na maana?...... Ukosefu wa hiyo nafuu kazini umemwathiri Mama Mercy....... Au pengine alikuwa anatii kanuni ya maisha ya mabadiliko?

''Aah, brother! Mpaka unifanyie kazi?...''

''Hilo linahusu nini wajibu wako? Tuseme wewe uliamua kususia kuja na gari kama njia ya kuonyesha kuchoshwa kwako na hali ya sasa?... Unatoa mfano gani kwa wenzako kazini?''

Uzungumzi Nafsia

Nitampigia nikifika nyumbani

Kama hatanikopesha huyu Vaite leo, basi nitaona moto, .... Amejuaje hilo?

Atapokea simu majira kama haya?

Hapatakalika hapa,

Si aliwahi kunieleza kuwa hapo kwake hapawezi kukosa chakula? Hapo ndipo ilipo riziki yangu leo.

Kuchanganya Ndimi

Barabara ya Waiyaki Way haina msongamano& ilinichukua dakika chache kuyafikia makutano ya Uhuru Highway na Kenyatta Avenue.

''Hili, Mama Mercy, ni kile tunaita bad coincidence.....''

Kesho nitasema na Bosi. Akiwa katika mood nzuri huenda akanipa kitu kidogo

''...........katika hali kama hii, it is virtually unsustainable kuwa na wafanyakazi wengi. Contract yake inaisha lini?''

''Landlord anatishia kumfungia nyumba..........''

''Nashukuru.....eeh. He’s now stable. Out of danger.....absolutely. Yes........ asante sana......''

Dayolojia

Mazungumzo kati ya Kikwai na mkewe kabla Mercy hajawakatiza kuhusu suala la upishi.

Kikwai anapomsaili, mkewe anamweleza kuwa hakupika kwani hakuna chakula na hapendi kukopa.

Mazungumzo kati ya Kikwai na mkewe, Mama Mercy, akimweleza jinsi hali ilivyo ngumu, na kuwa anafaa kuvulia, mambo yatakuwa mazuri.

Inatuonyesha ugumu anaopitia Kikwai, migogoro na matatizo ya ndoa.

Kuna mazungumzo kati ya Kikwai na bintiye, Mercy, anapomwamsha asubuhi kwa kilio.

Anamshatakia kuwa analia sababu ya njaa, naye anamwahidi kumnunulia kitu ale.

Dayolojia hii inatuonyesha matatizo ya malezi na dhiki za maisha ya Kikwai.

Mazungumzo kati ya Kikwai na Bosi kuhusu Nilakosi na kandarasi yake inayokamilika, na pia kuhusiana na gari la kampuni, anapomtaka aende nalo kupeleka mwanawe hospitali, hali ameliacha nyumbani.

Inaonyesha migogoro, udhalimu na matatizo ya kazini.

Mazungumzo kati ya Kikwai na Bishop anapoenda kumwomba msaada wa chakula, wakijuliana hali na Bishop kumkidhia haja.

Yanaonyesha nafasi ya dini katika jamii na umuhimu wa utu.

Mazungumzo kati ya Bosi na Kikwai anapomfuta kazi, akilalamikia mazoea yake ya kuacha gari la kampuni nyumbani.

Anasema kuwa atamwondolea taabu ya kucheleweshwa mshahara kwa kumwachisha kazi.

Yanadhihirisha migogoro na udhalimu kazini.

Semi na Nahau

nikajikaza kiume- nikajikaza kabisa

kuchapa kazi- kufanya kazi kwa bidii

kuuponda wa fisi- kutembea kwa miguu

shingo upande- bila kupenda, kwa kujilazimisha au kulazimishwa tu.

Aliyekula kiapo- aliyeapa, aliyetoa ahadi

Mikono mitupu- bila chochote

Sina budi- inanibidi, sina lingine

Kinaya

Mama Mercy anampigia Kikwai simu kulalamikia mwana yuaelekea kulala.

Amehiari kumweka Mercy na njaa hadi babake arudi, badala ya kukopa.

Bosi anamwambia Kikwai kuwa gari la kampuni linafaa kuwepo kwa ajili ya dharura kama inayomkumba ya mwanawe kuwa mgonjwa.

Ukweli ni kuwa hii ni shughuli ya kibinafsi.

Bosi anamwambia Kikwai kuwa haoni kwa nini haji kwa gari la kampuni, licha yake kumweleza kuwa hana pesa za mafuta.

Anadai kuwa anathamini pesa zaidi ya kampuni, pesa ambazo hata hana!

Bosi anamwambia Kikwai atamwondolea taabu kwa kumwachisha kazi ili asikumbwe na suala la kucheleweshwa mshahara.

Ukweli ni kuwa anamweka katika taabu ya kutafuta kazi nyingine.

Tashihisi

Tuweze kusukuma siku& Kwa sababu nisiyoweza kubaini, uliniparamia mpapo wa moyo nikisubiri simu kupokelewa upande wa pili.

Methali

Kila msiba huandamana na mwenziwe.

Istiara

Niliipokea kwa kasi ya mama anayechupa nje ya nyumba kumfuata mtoto mtundu asiyefahamu hatari iliyoko barabarani anakokimbilia.

Na kuongeza msumari wa moto kwenye kidonda kibichi, chakula kina harufu na muonjo wa mafutataa.

Mbinu nyingine zilizotumika ni kama vile Utohozi, Mdokezo, Takriri, Sadfa, Nidaa na Koja.

Join our whatsapp group for latest updates

Download Harubu ya Maisha summary notes - Mwongozo wa Mapamazuko ya Machweo na Hadithi Nyingine.


Tap Here to Download for 50/-




Why download?

  • ✔ To read offline at any time.
  • ✔ To Print at your convenience
  • ✔ Share Easily with Friends / Students


Get on WhatsApp Download as PDF
.
Subscribe now

access all the content at an affordable rate
or
Buy any individual paper or notes as a pdf via MPESA
and get it sent to you via WhatsApp

 

What does our community say about us?