SEHEMU A: HADITHI FUPI
K.W. Wamitila: Mayai Waziri wa Maradhi na Hadithi Nyingine.
- Eleza nafasi ya usimulizi iliyotumiwa katika hadithi ya “Mkimbizi”. (alama 3)
- Bainisha mifano mitatu ya mbinu rejeshi katika hadithi hii na ueleze umuhimu wa kila mojawapo. (alama 9)
- “Ukimbizi ni kikwazo cha maendeleo.” Thibitisha kauli hii kwa kurejelea hadithi hii. (alama 8)
SEHEMU YA B: RIWAYA
Said A. Mohamed: Utengano
Jibu swali la 2 au la 3- ‘Lo, ama wewe mchawi,….Cheleko … nakuvisha kilemba.’
- Fafanua muktadha wa dondoo hili. (alama 4)
- Andika tamathali mbili za usemi zinazojitokeza katika dondoo hili. (alama 4)
- ‘Wewe mchawi.’ Onyesha jinsi kauli hii inavyomwafiki mzungumziwa kwa kurejelea riwaya. (alama 12)
- “Wanawake katika Utengano ni vyombo vikuu vya ukiukaji wa haki za kibinadamu.”
Thibitisha. (alama 20)
SEHEMU YA C: TAMTHILIA
Kithaka wa Mberia: Kifo Kisimani
Jibu la 4 au la 5 - “Mtukufu Mtemi anafurahia sana … Kama ujuavyo, anapenda sana watoto …Kwa hakika, kama mzazi, hana kifani katika Butangi nzima.”
- Eleza muktadha wa dondoo hili. (alama 4)
- Taja na utoe mfano wa sifa moja ya mzungumzaji inayopatikana katika dondoo hili. (alama 2)
- Fafanua vichocheo vinne vya sifa uliyotaja katika (ii) hapa juu. (alama 2)
- Onyesha jinsi wanyonge katika Kifo Kisimani walichangia katika ukandamizaji wao. (10 marks)
- “Anwani Kifo Kisimani” inaafika tamthilia hii. Thibitisha. (alama 20)
SEHEMU D: USHAIRI
Jibu swali la 6 au la 7. - Soma shairi lifuatalo kisha ujibu maswali.
Said A. Mohamed: Mbele ya Safari
1. Iilipoanza safari, ilianza kwa dhiki
Tulishikana kwa ari, kwenda safari ya haki
Tukawa ni majabari, nyoyo zisitaharuki
Tukajizatiti
2. Njaa ikawa thabiti, na kiu tukamalaki
Nasi tulitia dhati, tusijali kuhiliki,
Ingawa mbele mauti, dhila na mingi mikiki
Tulijizatiti
3. Huu mwisho wa safari, tukaambiwa ni haki
Shangwe kwetu na fahari, utumwa hatuutaki
Kuwa mbele ya safari, juhudi iliyobaki
Tuljizatiti
4. Ile ilikuwa ndoto, mwisho wake mafataki
Nguvu zimechomwa moto, sahala ‘mekuwa dhiki
Wagombania kipato, utashi haukatiki
Na kutabakari
5. Msafara ukasita,kwenye mlima wa haki
Kijasho kinatuita, mlima haupandiki
Basi sote ‘kajipeta, kukikwea kima hiki
Twataka hazina
6. Tukiwa migongo wazi, tukainama kwa shaki
Tukawa ‘chia ukwezi, kialeni wadiriki
Wakapanda bila kazi, kuteremsha miliki
Wakaitapia
7. Wakafikia makazi, ya pumbao na ashiki
Huko wakajibarizi kwenye raha lakilaki
Wakaisahau ngazi, ya umma uliomiliki
Mbele ya safari
8. Na hazina yetu sote, kuishusha hawataki
Wamo wanatema mate, kwa umati halaiki
Imezima nia yote, kiza hakitakasiki
Mbele ya safari- Eleza safari inayorejelewa katika shairi hili. (alama 2)
- Onyesha kinaya cha safari inayozungumziwa. (alama 6)
- Taja na ueleze bahari mbili za ushairi ukizingatia: (alama 4)
- Mizani;
- Vina.
- Andika ubeti wa saba katika lugha nathari. (alama 4)
- Eleza umuhimu wa aina mbili za uhuru wa kishairi zilizotumiwa katika ubeti wa sita. (alama 4)
- Eleza safari inayorejelewa katika shairi hili. (alama 2)
- Soma shairi lifuatalo kisha ujibu maswali
1. Wakati tunywapo chai hapa upenuni
Na kuwatazama watoto wetu
Wakicheza bembea kwa furaha
Tujue kamba ya bembea yetu imeshalika
Na bado Kidogo tutapoomoka
2 Kulikuwa na wakati ulinisukuma juu
Nikaenda zaidi ya nusu duara
Kulikuwa na wakati nilikudaka
Ulipokaribia kuanguka
Na kulikuwa na wakati tulibebeana kwa zamu
Mmoja wima ukisukuma mwingine amekaa
3 Wakati huo, japo tulipaa mbele na nyuma
Tulicheka kwa matumaini yaliyotiwa chumvi
Na Kisha tukaongozana jikoni kupika chajio
Ilikuwa aldhuhuri yetu
4 Sasa tukisubiri ndoto tusizoweza kuzitekeleza tena
Tumalizie machicha ya chai yetu ya jioni
Bila ya kutematema na kwa tabasamu
Na baada ya hapo tujilambe utamuutamu
5 Tukikumbuka siku ilee ya kwanza
Tulipokutana jioni chini ya mwembe
Tukitafuta tawi zuri gumu
La kufunga bembea yetu
Naye mbwa simba akisubiri
6 Lakini kabla hatujaondoka kimyakimya
Kukamilisha duara iliyobaki
Tuhakikishe vikombe vyetu ni safi.
(E. Kezilahabi)- Fafanua maana ya kijuujuu na maana ya kitamathali ya shairi hili. (alama 6)
- Bainisha matumizi ya vipengele vifuatavyo katika shairi: (alama 6)
- usimulizi;
- usambamba ;
- taswira.
- Tambulisha mzungumzaji (nafsi-neni) katika shairi hili.( alama 2)
- Fafanua toni ya shairi hili.( alama 4)
- Eleza maana ya mshororo : “Tuhakikishe vikombe vyetu ni safi.” (alama 2)
SEHEMU E: FASIHI SIMULIZI
- Fafanua maana ya kijuujuu na maana ya kitamathali ya shairi hili. (alama 6)
- Huku ukitoa mifano, fafanua majukumu matano ya nyimbo. (alama 10)
- “Mwimbaji ana nafasi muhimu katika kufanikisha uwasilishaji wa wimbo.” Thibitisha (alama 10)
- Huku ukitoa mifano, fafanua majukumu matano ya nyimbo. (alama 10)
MARKING SCHEME
-
-
- Hadithi hii inasimuliwa katika nafsi ya kwanza. Usimulizi huu unafanywa na mhusika mtoto/kijana.
- Msimulizi ni mhusika mmojawapo wa hadithini.
- Kuna matumizi ya mofu (ni) na (tu) za nafsi ya kwanza.
kutaja - alama 1
maelezo - alama 2
Jumla - alama 3
- Mifano mitatu ya mbinu rejeshi na umuhimu wayo.
- Maelezo ya Msimulizi kuhusu usiku ambao babake na watu wengine walizungumza kuhusu mzozo baina ya Wahutu na Watutsi. Babake aliuma kidole. Aidha tunaelezwa kuwa Msimulizi ambaye ni Mhutu alicheza na watoto wengine waliokuwa Watutsi bila kuona tofauti.
Hapa mbinu rejeshi inaonyesha kuwa:- Watoto hawakuhusika na tofauti za kikabila.
- Watu wazima ndio wenye kuhusika na tofauti za kikabila.
- Mzozo baina ya Wahutu na Watutsi ni jambo lililopangiwa kikamilifu.
- Vita huwatia wasiwasi hata watu wazima.
- Pia mbinu rejeshi inaibua maudhui ya ubaguzi, na uzalendo.
kutaja - alama 1
umuhimu 2 x 1 = 2
Jumla - alama 3
- Msimulizi anakumbuka kuhusu maisha yao shuleni ambapo alisoma na Jesse: UK 119 Umuhimu wake:
- Kuonyesha kuwa msimulizi na Jesse walikuwa na uhusiano mzuri.
- Wote walikuwa hodari katika masomo ya lugha (Kinyarwanda (Jesse)
Kifaransa (Msimulizi) (maudhui ya bidii) - Athari ya ukimbizi - wanaachishwa masomo.
kutaja - alama 1
umuhimu - 1 x 2= 2
Jumla - alama 3
- Msimulizi anawaza kuhusu wema wa Jesse baada ya Jesse kufa. UK 122
Anakumbuka uhusiano wao mwema wakiwa shuleni Rugifare.
Umuhimu wake:- inaonyesha uhusiano wa kidugu baina yao.
- imani ya Jesse
- anamletea msimulizi njugu shuleni.
- kuonyesha mshikamano wa kijamii - wanacheza pamoja.
- kuonyesha dhiki ya kisaikolojia inayosababishwa na ukimbizi.
kutaja - alama 1
umuhimu - 1 x 2= 2
Jumla - alama 3
- Msimulizi akiwa safarini kuelekea ng'ambo anakumbuka maneno ya Savalanga, anakumbuka kilio cha uchungu cha mamake na hali iliyomfanya kuwa mkimbizi.(UK 124)
- Msimulizi anakumbuka sura ya mama na ndugu zake akiwa Betinga (UK 122).
Umuhimu wake:- Kuonyesha dhiki ya kisakolojia inayochechewa na vita.
- Kuonyesha maafa yanayosababishwa na vita.
Umuhimu - inaonyesha uzalendo wa Msimulizi. Anakumbuka kwao, anawazia wasia wa Savalanga.
- inafumbata maudhui ya ujenzi wa jamii mpya kwa kutarajia kutimiza aliyoambiwa na Savalanga.
kutaja - alama 1
umuhimu - alama2
Jumla - alama 3
Tanbihi- Mtahiniwa aonyeshe alipo sasa na kusimulia tukio la nyuma.
- Mtahiniwa afafanue kikamilifu mifano yoyote mitatu ili kutuzwa
alama 9
- Maelezo ya Msimulizi kuhusu usiku ambao babake na watu wengine walizungumza kuhusu mzozo baina ya Wahutu na Watutsi. Babake aliuma kidole. Aidha tunaelezwa kuwa Msimulizi ambaye ni Mhutu alicheza na watoto wengine waliokuwa Watutsi bila kuona tofauti.
- Vikwazo vinavyoletwa na ukimbizi.
- Kukatizwa kwa elimu - Jesse na Msimulizi wanaacha masomo yao na kukimbilia usalama. (Athari katika sekta ya elimu).
- Kusambaratika kwa familia. Baba ya Msimulizi anaenda vitani.
- Utegemezi. Wakimbizi wanategemea hifadhi/makao katika nchi nyingine. Wakimbizi wanapiga kambi mpakani/kuwa mzigo kwa majirani.
- Ukosefu wa usalama wa chakula. Wanakula matunda-mwitu na wanyama-mwitu, hata mizoga! Uhamishoni chakula ni haba, wanang'angania chakula.
- Wasiwasi/ ukosefu wa utulivu/ ukosefu wa amani. Kila mara wanahofia kushambuliwa. Hofu inamfanya Msimulizi kujikojolea.
- Vifo vya watu ambao wanachangia maendeleo ya nchi- Jesse/ Savalanga, wakimbizi waliouawa njiani.
- Magonjwa/hali duni ya afya, pale kambini/njiani. Jesse na Savalanga wanakufa kwa ugonjwa.
- Dhiki/athari za kisaikolojia. Msimulizi anasikia milio ya bunduki akilini. - Kutegemea kuelimishwa na jamii nyingine. Msimulizi na wenzake tisa wanapelekwa ng'ambo kusoma.
- Ukosefu wa mshikamano wa kijamii - njiani wanapoulizwa kama wao ni Wahutu au Watutsi wanajawa na woga.
- Hisia za ukiwa - msimulizi anasema walimhurumia Savalanga kwa kupoteza alla yake, hali ambayo inaathiri utulivu wa mtu binafsi.
- Nchi inaachwa bila raia wenye nguvu kuijenga upya. Mzee Savalanga anaonekana kukata tamaa, ndio maana anamuusia msimulizi kurudi nyumbani baada ya vita ili kujenga jamii upya.
- Ukimbizi unaathiri uongozi. Nchi inapoteza vijana kama vile Jesse ambao wangechangia kubadilisha hali ya siasa nchini kwa vile hao hawakutawaliwa na mawazo ya ukabila.
- Makazi duni - njiani na kambini.
(4 x 2 = alama 8)
-
-
-
- Ni maneno ya Farashuu kwa Biti Kocho.
- Wamo nyumbani mwa Farashuu Madongoporomoka.
- Biti Kocho amekuja na Maimuna kumchukua Farashuu ukunga.
- Biti Kocho amemhadithia Farashuu jinsi alivyomtoa Maimuna nyumbani na kumzuga kwa kumtajia mapenzi. Ndipo Farashuu akatamka haya.
(4x 1 = alama 4)
- Sitiari - wewe mchawi - kumlinganisha Biti Kocho moja kwa moja na mchawi. (mchawi - bingwa /haini/mjanja)
- Nahau - nakuvika kilemba (nakupongeza/nakustahi).
- Dhihaka / kinaya - Farashuu kumpongeza Biti Kocho kwa uovu.
(2 x 2 = alama 4)
Tanbihi
Dondoo limetolewa ukurasa 31.
- Uchawi - Ubingwa wa maovu, ulaghai/ujanja/uhaini/ujasiri.
- Biti Kocho anamtoa Maimuna nyumbani kwa ujanja ili kumwonjesha Maimuna mazingira ya uhuru, kusudi Maimuna ashawishike kutoroka.
- Biti Kocho anamchochea Maimuna kuutafuta uhuru. Anamwambia kwamba yeye ni mkubwa si wa kufungwa kama kuku (uk. 27).
- Biti Kocho anakaidi amri ya Maksuudi na kumleta mkunga (Farashuu) kumzalisha Tamima. (Ni bingwa wa ujasiri).
- Anapanga njama kumleta Farashuu ili waweze kulipiza kisasi kwa Maksuudi. (Bingwa wa mikakati ya uovu).
- Yeye na Farashuu wanamtorosha Maimuna na kumtenga na familia yake.
- Ni laghai/mnafiki. Anadai kwamba angalikwenda kumchukua Farashuu lakini anachelea usiku, anataka wa kufuatana naye (Maimuna).
- Anamlaghai Maimuna kuvutiwa na sanamu ya mwanamke na mwanaume ili kumjaza fikira za kutamani mapenzi
- Ni katili. Anajua aliko Maimuna lakini hamwambii Tamima. Hata kengele inapobonyezwa anajidai kwamba labda ni Maimuna na hali anajua siye.
- Anathubutu kumkabili Maksuudi na kumwambia kwamba kumpiga Tamima hakutabadilisha lolote. (Ujasiri).
- Anamshutumu Maksuudi kwa ukatili wake. Anamlaumu Maksuudi kwa kumtawisha Maimuna. Anathubutu kumwita Maksuudi mjinga. (uk 51) anapodai kuwa wanawake hawajui siasa.
- Anapoona Tamima ataumizwa zaidi anasimama mbele ya Tamima na kumkinga. / Ana tambo ambalo linamfanya Maksuudi kunywea. Maksuudi anaona kwamba ingawa Biti Kocho ni mwanamke, hana tani yake (52).
- Anamwombea Tamima talaka na kusambaratisha ndoa yake.
- Anahakikisha ya kwamba amemchungachunga Tamima wanapoondoka kwa Maksuudi, anamshauri aende kwao shamba na hata kuhakikisha amepata usafiri (torinkaa) kuelekea huko.
- Ni fisadi. Anamwomba Farashuu shilingi mia mbili kumpa karani wa viwanja hongo amfanyie mpango kupata kiwanja fulani.
- Ni mwenye mbinu za ushawishi/ana uwezo mkuu wa kushawishi. Anatoa maelezo ya kushawishi (wakiwa pale nyumbani kwa Tamima), (wakiwa njiani na Maimuna) kuhusu umuhimu wa kumleta mkunga nyumbani na baadaye utamu wa mapenzi.
(Hoja 6 x 2 = alama 12)
-
-
- Wanawake wanachangia katika kusambaratika kwa asasi ya familia. Kazija, Farashuu, Biti Kocho wanasambaratisha familia ya Maksuudi.
- Wanawake wanamnyima Maimuna na kile kitoto kichanga cha Tamina haki ya malezi. Farashuu anashirikiana na Biti Kocho kumtorosha Maimuna. Biti Kocho anachochea kutalikiwa kwa Tamima ambaye anakiacha kitoto kwa Maksuudi, kitoto kinakufa.
- Wanawake ni vyombo vya uzinifu ambavyo vinasababisha mafarakano katika ndoa. Kuhusiana kwa Kazija na Maksuudi kunamnyima Tamima uwepo/ushirika wa Maksuudi; Tamima anapopata uchungu wa uzazi mumewe hayupo. Wanawake pale Bobea, mfano Maimuna, wanampigania Shoka ambaye hamjali mkewe Selume. Wanawake wanamwingiza Maimuna katika ukahaba. Farashuu anapomtorosha Maimuna anampeleka kwa Mama Jeni (danguroni) ambako anaingilia ukahaba.
- Mama Jeni anawatumia wasichama kama vitega uchumi. Anapanga njama ya kumkutanisha Maimuna na James kwa malipo ya shilingi ishirini. Dora anaishi kwa Mama Jeni akifanya ukahaba, anasema ana deni la kulipa kwa Mama Jeni.
- Farashuu anamnyima Maimuna nafasi ya kukulia katika mazingira ya nyumbani kwao (Liwazoni) kwa kumtorosha.
- Mama Dora anamnyima Dora haki ya malezi kwa kumuuza kwa Mama Jeni.
- Biti Sururu anamwingiza Maimuna katika uuzaji wa pombe pale 'kil mi kwiki'.
- Biti Sururu anamfanya Maimuna kutumia pombe vibaya kwa kumwingiza katika mazingira kunakouzwa pombe. Maimuna analewa hadi kikohozi chake kinachanganya harufu ya damu.
- Mwanasururu anajaribu kumshurutisha Kabi kutenda lisilofaa. Kabi anatoroka na kuishia kugongwa na gari na kupoteza mguu wake.
- Farashuu anamdhalilisha Maimuna mbele ya Kabi kwa kumwita mhuni.
- Wanawake pale pa Mama Jeni wanamsingizia Maimuna wizi na hali siye aliyeiba. Mama Jeni anamfukuza bila hata ithibati kuwa ndiye aliyemwibia.
- Maimuna anapotambua uhuni wa Farashuu na Biti Kocho, na Mama Jeni, badala ya kurudi nyumbani anasema heri aendelee kuishi katika shimo hili badala ya kurudi kwa Tamima. Anamkosesha mama yake mapenzi ya mama na binti.
- Maimuna anamuumbua baba yake pale Rumbalola na kwa Biti Sururu. Anamkana babake na hata kumsababishia kifo kutokana na kihoro cha kukataliwa.
- Kazija anampigisha Mussa kwa babake kwa kuwakutanisha na hata kujaribu kumchochea Maksuudi kumpiga Mussa.
- Udhaifu wa Tamima unamfanya asiweze hata kumtetea Maimuna anaponyimwa elimu rasmi. Anafundishiwa ndani.
- Maimuna anamwibia Ashuru kwa hila na kukiuka haki ya kuheshimu milki ya watu.
- Farashuu anawatumikisha wasichana kwa saa nyingi.
- Kijakazi anamtukana na kumuumbua Maimuna hadharani.
(Hoja 10 x 2 = alama 20)
-
-
-
- Maneno ya Zigu
- Anamwambia Kaloo
- Wamo katika kisima cha Mkomani/Bonde la Ilangi ambamo Kaloo amemfuata Zigu.
- Kaloo anamwomba Zigu amshukuru Bokono kwa kuamrisha mtoto wa Kaloo kupewa kazi.
- Ndipo Zigu anamwambia Kaloo haya.
(4x 1 = alama 4)
- Mwongo/mdanganyifu/mnafiki.
Anasema kwamba Bokono anapenda watoto sana na hali anajua kwamba Bokono ameidhinisha kuchukuliwa kwa uwanja wa kuchezea watoto.
(kutaja) - 1 (kueleza - 1) (alama 2) - Vichocheo
- kutaka kutambuliwa
- ulimbukeni/usungo
- kutaka kujitambulisha na wakubwa
- woga
- tamaa ya mali/mamlaka/ubinafsi
- kujikomba kwa wakubwa/kutaka kuonekana mwema/mjuzi na Kaloo.
- Udikteta wa Bokono unamfanya kuwa mnafiki ili kufaidika kwaye / asiadhibiwe.
- Hali ya uhitaji Butangi inamfanya yeye na wenzake kutaka kuvutia kwao tu.
(4x 1 = alama 4)
Tanbihi
Dondoo limetolewa uk 89
-
-
- Baadhi wanaendeleza uongozi dhalimu badala ya kuupinga. Kaloo anakwenda uwanjani kuandalia mkutano wa Bokono badala ya kuususia. Gege anafika uwanjani kupiga ala. Washauri wanamsifu Bokono kiongo badala ya kumkosoa.
- Ubinafsi na tamaa unawafanya wengine kutumiwa kama vikaragosi. Gege anamuua Mwelusi ili kufanikisha uongozi wa Bokono.
- Askari II, III na makachero, kwa kujiona kuwa katika kundi sawa na Bokono, wanafuata kanuni kandamizi za gereza na kuishia kuwanyanyasa wanyonge wenzao.
- Askari II, III wanamnyima Mwelusi chakula, Mweke na Talui wanampiga Mwelusi. Askari II na kikosi chake wanamuua mtuhumiwa na kumzika msituni..
- Wanawake wanaridhia kutumiwa kama vyombo vya burudani. Kaloo anashangaa ikiwa hawatamkatikia Mtemi watamkatikia nani?
- Wanyonge wanamwimbia Mtemi nyimbo za kumsifu kiongo badala ya kumkosoa. Wanasema wamshukuru Mungu kwa zawadi adimu (Bokono) na hali anawadhulumu. Wengine wanakwenda Ikuluni kumhakikishia Mtemi uzalendo wao. (mf Kijiji cha Mipashoni Uk. 102)
- Baadhi wanaombea utawala wa Bokono udumu. Askari II anaomba Mungu ampe Bokono maisha marefu ili azidi kumhifadhi na huku anazidi kuwanyanyasa wanyonge.
- Wengine wanataka kurithi/kuendeleza mfumo kandamizi. Askari I anataka kumwangamiza Bokono kwa shoka lakini Atega anamkataza.
- Tanya anapuuza uhasama kati ya Gege na Mwelusi, anamwelekeza Gege kwa Mwelusi, Gege anaishia kumuua Mwelusi/Ingawa Gege ni mnyonge kama Mwelusi anakubali kutumiwa kama chombo cha kumwangamiza Mwelusi.
- Ujasiri wa Mwelusi, badala ya kumfaa unamsababishia kupigwa na Mweke na Talui. Mwelusi anakataa kusema anampenda Bokono, jambo ambalo linawafanya Mweke na Talui kumpiga sana.
- Mwelusi anakataa ushauri wa mamake kuwa aondoke Butangi: anaishia kuuawa kwa amri ya Bokono. (Anapuuza uhasama baina yake na Gege)
- Raia wanaruhusu viongozi wanarithi mfumo kandamizi na kuuendeleza. Uongozi dhalimu umekuwepo tangu enzi za Mtemi Mulima na wengine kama Bokono hawawazii kuubadilisha.
(10 x 1 = alama 10)
-
- Ufaafu wa anwani
- Mtahiniwa abainishe maana ya juu - Kifo cha Mwelusi kinatokea katika Kisima cha Mkomani.
- Maana ya Kiistiari
- Kifo ni sitiari ya mateso/maangamizi/kutofikia malengo au maazimio/ uozo/ tandabelua/ machafuko. Kisima ni sitiari ya nchi/ taifa/ chemchemi ya uhai / hifadhi ya raia.
- Mtahiniwa aonyeshe kinyume cha mambo. Badala ya Kisima/ nchi kuwa chemchemi ya uhai/ fanaka, viongozi wanakuwa watesi wa raia/ wanawaangamiza raia. Hoja zifuatazo zinaweza kuzingatiwa
- Viongozi wanawanyima raia uhuru wa kuchota maji kisimani - wanaruhusiwa kuchota siku tatu tu kwa wiki.
- Viongozi kuwapiga raia kinyama - Mwelusi anapigawa na Mweke na Talui gerezani. Mtuhumiwa anapigwa na Askari II na kikosi chake msituni. Andua na mtoto wa Chendeke wanapigwa
- Wapigania haki kufungwa gerezani - Mwelusi anafungwa kwa madai kuwa ni kiongozi wa Kabakaba/anawachochea raia, yeye na wenzake wa kikundi cha Nuru ya Butangi.
- Sera mbovu za uongozi kutumia propaganda. Batu anamwambia Mwelusi awatangazie raia kuwa uchochezi unaletwa na majirani na hali sivyo.
- Unyakuzi wa mali ya umma - Mgawa ardhi anachukua uwanja wa kuchezea watoto na kumpa Askari Mkuu. Bokono ananyakua Bonde la Ilangi.
- Viongozi wanaharibu mazingira wanalima na kulisha wapendapo, hivyo kuumomonyoa udongo.
- Viongozi kuwatelekeza raia katika njaa. Mwelusi anasema Butangi imejaa njaa.
- Viongozi kutowahakikishia raia usalama. Batu anawalipa wahuni kuwashambulia Balusi na kusababisha uharibifu wa mali.
- Viongozi kuwatenga raia badala ya kuwaunganisha. Batu anapowalipa wahuni kuwashambulia Balusi Batuitui wanasingiziwa ili kuzua chuki baina yao na kuupujua mshikamano wao.
- Maandamano ya raia kupinga uongozi dhalimu. Balusi wanaandamana. Hili lasababisha taharuki kwa uongozi / uongozi unalipiza kwa kushambulia.
- Washauri wa Bokono wanaudhoofisha uongozi wake. Badala ya kumshauri aache uongozi mbaya wanamsifu kiongo. Wanasema yeye ni mwenye busara.
- Gege anausaliti udugu wake na Mwelusi, anamuua Mwelusi.
- Maandamano ya mwisho ya raia wakiongozwa na Atega yanamng'oa Bokono mamlakani, hivyo kuuangamiza (kuuua) uongozi wake. (Mapinduzi)
- Badala ya Bokono kupevuka kimawazo anarudi nyuma. Nyalwe anamwigiza Bokono akirudi nyuma kutoka utuuzima, makamo, ujana, utoto hadi anapokuwa kijusi kwenye mji wa mama yake.
- Uozo - Bokono anadhaniwa kuwa na hawara aliyepigwa na Nyalwe. Zigu anamwambia Kaloo kuwa jicho la Mtemi limemwona. Askari III anajaribu kumshika Andua kifuani.
- Ufisadi - ugavi usiofaa wa mali ya umma. Mgawa ardhi kumpa Askari mkuu uwanja wa kuchezea watoto. Bokono anaidhinisha haya. Bokono anampa mtoto wa Kaloo kazi kwa sababu Kaloo ni kikaragosi wa Bokano.
- Unafiki wa viongozi, Batu anajidai kuwa rafiki wa Tanya ili Tanya amwelekeze aliko Mwelusi. Batu anajidai anamjali Mwelusi pale gerezani. Mweke na Talui kujidai wanamstahi Gege, Mweke anamwahidi Gege kuozwa Alida, huku akijua si kweli.
- Mauaji - Mtuhumiwa kuuawa na kuzikwa msituni, Mwelusi kuuawa na Gege.
- Chuki ya ndugu - Gege anamwonea Mwelusi wivu. Badala ya kwenda kumtazama gerezani anatengeneza ala.
- Dhiki ya kisaikolojia - Wasiwasi unamfanya Tanya kuwa na jinamizi. - Ukosefu wa umoja miongoni mwa vijana. Badala ya Gege kujiunga na akina Mwelusi, anawapinga na kusema wanamchukia Bokono.
- Sheria baraza la hukumu na vyombo vingine vya dola kama vile polisi wanalinda maslahi ya Bokono badala ya umma.
- Uongozi kutolipia huduma. Mbutwe halipwi kwa kutengeneza viti vya kutumiwa na mkutano wa Bokono.
- Asasi za kurekebishia sheria zinapunza haki za wafungwa Mwelusi ananyimwa chakula na fursa ya kutembelewa na jamaa.
(10 x 2 = alama 20)
Kumbuka: Lazima hoja mojawapo iwe ile maana ya kijujujuu.
-
- Ni safari ya kupigania uhuru/ safari ya kutafuta haki/ safari au harakati za kujiendeleza kiuchumi. Anasema walishikana kwenye safari ya haki, walisita kwenye mlima wa haki. Anataja kuteremsha miliki.
Kutaja - alama 1
Kueleza - alama - Maelezo ya (maana ya) kinaya yawepo.
- Kinyume cha matarajio, (viongozi) wachache waliofika kileleni walijawa na uchoyo, wakaamua kujinufaisha. (alama 1)
- Walijitengenezea makazi ya raha, wakajinyakulia vyeo wakakaa kufurahika/huku wakiwasahau waliowakweza mamlakani.
- Wakawa ndio pekee waliofaidi matunda ya uhuru ambayo yalikuwa yamepiganiwa na wote.
- Viongozi wamefika hadi kuwadhuru raia waliowapa hivyo vyeo - Wanawatemea mate.
- Raia kupigania uhuru na baadaye kutofaidika kwao.
- Kutofikia maazimio ya kiuchumi. Hawapati milki waliopigania
- Safari ya haki na hali ubaguzi unajitokeza.
(5 x 1 = alama 5)
(- kueleza kinaya/ kujitokeza kwa kinaya - alama 1)
Jumla - 6
-
- Msuko - Mshororo wa mwisho una mizani chache kuliko mingine/ umefupishawa.
- Ukara - Vina vya kati ndani vinabadilikabadilika. Vya nje/ mwisho vinatiririka.
(2 x 2 = alama 4)
(Kutaja - 1, Kueleza - 1)
- Mfano:
Wawakilishi/viongozi walijikuta katika hali nzuri sana za maisha na tamaa ya kujinufaisha ikazidi. Walishiriki starehe za kila aina. Katika hali hii walisahau wananchi/ raia waliowakweza katika nafasi hizo (waliowapa nafasi hizo) za uongozi, na ambao ndio waliokuwa na nyenzo za kuwafanya kufikia hali hii yao (viongozi) ya sasa.
(alama 4) -
- Inkisari tukawa'chia - kutosheleza idadi ya mizani.
- Kufinyanga sarufi/kuboronga sarufi/kubanaanga lugha/miundo ngeu ya kisintaksia.
- Kialeni wadiriki - wadiriki kileleni - kuleta urari wa vina.
- Tabdila-shaki - badala ya shake - kuleta urari wa vina.
- Lugha chakavu/msamiati kikale.
- Kialeni - Kileleni
- Kulipa shairi mapigo ya kimuziki
- Kulipa shairi upeke wa kiutanza.
(kutaja - alama 1, maelezo, alama 1)
(2 x 2 = alama 4)
- Ni safari ya kupigania uhuru/ safari ya kutafuta haki/ safari au harakati za kujiendeleza kiuchumi. Anasema walishikana kwenye safari ya haki, walisita kwenye mlima wa haki. Anataja kuteremsha miliki.
-
-
- Maana ya Kijujuu.
- Ni chai ya jioni.
- Inanywewa na mume na mke huku wakiwatazama watoto wakicheza bembea.
- Chai inakaribia kumalizika.
- Mzungumzaji anamtaka mwenzake wahakikishe wameviacha vikombe vyao vikiwa safi.(3 x 1 = alama
- Maana ya kitamathali.
- Shairi ni sitiari ya maisha yao ambayo yanakaribia kumalizika. Wameanza kuzeeka.
- Bembea - Sitiari ya maisha yao ya ndoa/ safari yao ya maisha/ chai ya jioni (Ushirika/uwepo wao katika siku za mwisho au maisha yanavyokaribia kuisha.
- Waliyopitia katika maisha yao ya ndoa - chamgamoto na furaha (kulikuwa na wakati lipokudaka ulipokaribia kuanguka).
- Maazimio ambayo hawakufikia - (sasa tukisubiri ndoto tusizoweza kuzitekeleza tena.
- Mume/mke anamtaka wamalizie siku zilizobaki vyema.
- Anamkumbusha siku walipokutana mara ya kwanza wakijaribu kujenga urafiki/ kuchumbiana.
(3 x 1 = alama 3)
- Maana ya Kijujuu.
-
- Usimulizi.
- Nafsineni inasimulia wakati walipokuwa wakicheza bembea/jinsi walivyofurahia maisha pamoja kwa matumaini.
- Anasimulia siku walipokutana.
Mfano - 1 x 2 (alama 2)
- Usambamba.
Huu ni urudiaji wa muundo sawa/ huo huo wa mshororo/sentensi.
Mfano:- kulikuwa na wakati ulinisukuma juu.
- kulikuwa na wakati nilikudaka.
Mifano - 2 x 1 (alama 2)
- Taswira
- Pana picha ya watu wanaokunywa chai na watoto wanaocheza bembea.
- Picha ya wenzi wa ndoa wenye furaha/wenye ushirikiano/wanaoongozana jikoni kupika.
- Picha ya watu wakitafuta tawi la kufungia bembea, na mbwa akiwasubiri.
- Picha ya nafsineni/mshirika katika ndoa anayemwambia mwenzake kwa masikitiko) maisha yao karibu yanafikia kikomo.
Mifano - 2 x 1 (alama 2)
- Usimulizi.
- Nafsineni - ni mzuugumzaji au msimulizi katika kazi ya kifasihi. Nafsineni katika shairi hili ni mwenzi katika ndoa (mume au mke). Anasimulia walivyokutana, anataja watoto wao.
(kutaja - 1, Kueleza - 1)
(alama 2) -
- Toni ya mchanganyiko wa furaha matumaini na masikitiko/huzuni (alama 1)
Mifano:- Mzungumzaji anasimulia maisha yao ya furaha; kucheza bembea, kupika pamoja... (
- Hata hivyo anaonyesha haya karibu yatafikia kikomo, anasema wamalizie chai yao ya jioni.
- Kuna maazimio yasiyofikiwa - anasema wanasubiri ndoto wasizoweza kuzitekeleza tena.
- Anakumbuka kwa furaha na masikitiko siku yao ya kwanza kukutana.
- Ana matumaini ya kumalizia machicha (masalio) ya chai yao.
(3 x 1 = alama 3)
- Toni ya mchanganyiko wa furaha matumaini na masikitiko/huzuni (alama 1)
-
- Kutenda mema
- Kurekebisha yaliyo kombo katika maisha/ uhusiano wao na wanajamii wenzao uwe wa kuridhisha.
- Kukamilisha/ kutimiza waliyoazimia kutimiza.
(Hoja 1 x 2 = alama 2)
-
-
-
- Nyimbo huhifadhi historia ya jamii, kwa mfano, nyimbo za sifa, nyimbo za siasa, nyimbo za vita.
- Huhifadhi na kupitisha utamaduni k.v. mbolezi hubeba utamaduni wa jamii kuhusu kifo, mazishi.
- Kuliwaza - k.v. mbolezi.
- Kuonyesha ustadi/ ubora wa jamii - wimbo bora/ mwema huonyesha ubora wa msanii.
- Kuhamasisha, kwa mfano nyimbo za kisiasa huhamasisha kupinga udhalimu.
- Kuelimisha - nyimbo za kazi (hodiya) hufunza maarifa ya kazi kama vile ukulima na usasi.
- Hukuza utangamano - Nyimbo za kazi, watu wanapoimba pamoja hujihisi kuwa kundi moja.
- Ni njia ya kutakasa hisia. Nyimbo za mapenzi na mbolezi hutumiwa kutoa hisia za moyoni.
- Huadilisha - Nyimbo hufumbata maadili ya kijamii na kidini. Kwa mfano nyimbo za kidini, bembelezi na hata mbolezi.
- Kukashifu tabia hasi - K.v. nyimbo za jandoni (nyiso) kukashifu woga.
- Kusifu tabia chang - K,v, sito
- Hukuza uzalendo - Wimbo wa taifa, nyimbo za kisiasa/huhimiza raia kujitoa mhanga kwa nchi.
- Kuimarisha ubunifu - Kadiri mtu anavyoimba ndivyo anavyonoa stadi za utunzi na uimbaji.
- Ni nyenzo ya burudani. Takriban aina zote za nyimbo hulenga kuburudisha tumbuizo.
- Hurithisha sanaa yenyewe ya uimbaji na utunzi wa nyimbo kwa vizazi kwa kuziimba kutoka kizazi hadi kingine.
- Hutumiwa katika vipera vingine kama vile ngano kuhuisha hadhira.
(5 x 2 = alama 10)
Tanbihi
Mtahiniwa sharti atoe mifano ya aina za nyimbo zinazotekeleza majukumu aliyotaja.
- Ili kufanikisha uwasilishaji wa wimbo, mwimbaji anahitaji:
- kuwa na sauti ya kuvutia ili kuvuta makini ya hadhira/kuiwezesha hadhira kupata ujumbe, kuihuisha kupata ujumbe.
- kuihusisha hadhira, kwa mfano, kupitia kwa kupiga makofi ili kukinga dhidi ya ukinaifu.
- kutumia udramatishaji/ uigizaji ili kusisitiza ujumbe/ kuufanya wimbo kuvutia/ kuifanya hadhira kukumbuka.
- kuelewa hadhira ili kuubuni wimbo upya/ kutumia mtindo ufaao kuuwasilisha.
- kuuelewa utamaduni wa hadhira ili kukinga dhidi ya kutumia maneno/ishara zinazokinzana na utamaduni huo.
- Kutumia viziada lugha kama vile ishara za uso na kidatu kusisitiza ujumbe.
- Awe mkakamavu ili awasilishe wimbo bila kuogopa hata kama unashirikisha masuala ambayo ni mwiko/nyeti.
- Aelewe lugha ya hadhira ili aweze kuitumia kufanikisha uimbaji wake.
- Awe mbunifu wa kuweza kuubuni wimbo upya kulingana na hadhira. Wimbo wa watoto uhusishe nyenzo kama vile mchezo wa sauti na maneno
- Awe mfaraguzi ili kuuimba wimbo kwa mahadhi tofauti tofauti ili adumishe mvuto.
- Ahusishe masuala ibuka/ masuala yanayoiathiri jamii wakati huo ili kupitisha maadili yafaayo.
- Awe na kumbukumbu nzuri ili aweze kuzirithisha nyimbo kama alivyoimbiwa (kifani na kimandhui) bila kubadilisha sana.
- Avae maleba yanayoafikiana na wimbo anaowasilisha ili kurahisisha uelewa wa ujumbe.
- Abadilishe toni kulingana na ujumbe anaopitisha ili kuibua taathira ifaayo kwa msikilizaji.
- Kutumia ala kwa njia mwafaka ili kukuza mvuto wa utungo wake.
Tanbihi
Mtahiniwa lazima atoe ufafanuzi toshelevu/unaoridhisha ili kutuzwa alama 2 kwa hoja.
(5 x 2 = alama 10)
-
Download KCSE 2012 Kiswahili Paper 3 with Marking Scheme.
Tap Here to Download for 50/-
Get on WhatsApp for 50/-
Why download?
- ✔ To read offline at any time.
- ✔ To Print at your convenience
- ✔ Share Easily with Friends / Students