Kiswahili Paper 3 Questions and Answers - Kenya High Post Mock 2023 Exams

Share via Whatsapp

Maagizo

 •  Jibu maswali manne pekee
 • Swali la kwanza ni la lazima
 • Maswali hayo mengine matatu yachaguliwa kutoka sehemu nne zilizobaki, yaani: Riwaya, Tamthilia, Fasihi simulizi na Hadithi Fupi
 • Usijibu maswali mawili kutoka sehemu moja
 • Majibu yote lazima yaandikwe kwa lugha ya Kiswahili


MASWALI

SEHEMU A: USHAIRI
Swali la lazima.

 1. Soma shairi lifuatalo kisha ujibu maswali. (alama 20)
  Mbio hizino twendazo, twendapi mbio hizino?
  Mbio zisizo viuzo, ni mbio za mashindano!
  Mbio za mfululizo, mbele zina mgongano
  Mbio hazina vigezo, twaendapi mwendo huno?

  Mbio zina matatizo, pasipo maelewamo
  Mbio kwenye mtelezo, watu hugwa na miguno
  Mbio hazileti tuzo, mbona huu mwandamano
  Mbio ni njia ambazo, twenende mwendo mnono.

  Mbio nguo uvaazo, hufichi hata kiuno
  Mbio jicho mlegezo, ajaye ni tangamano
  Mbio chini kwa mlazo, huogopi kisonono?
  Mbio watoa pumbazo, kila rijali ni vuno.

  Mbio hazino mchezo, huhitaji mshikano
  Mbio zenye mwelekezo, zendwazo kwa maagano
  Mbio ziwe mjalizo, hatua kwa mfwatano
  Mbio siwe mfukuzo, ukenda mwendo wa sono.

  Mbio bora zifaazo, sizo za mafarakano
  Mbio tena kwa tangazo, tuanze sawa pambano
  Mbio si kwenye pambizo, sote ndani mfwatano
  Mbio si maangamizo, mwendo ukawa mbano.

  Mbio si nyimbo zimbwazo, midomoni kwa maneno
  Mbio ni sera ambazo, mepangwa kwa mlingano
  Mbio ziwe mageuzo, maisha yawe manono
  Mbio si mlimbikizo, ni uchoyo mwendo huno.

  Mbio rijali mwendazo, kila saa mchuwano
  Mbio banati si hizo, kuridhi haja za ngono
  Mbio dada uigazo, usilingane na pono
  Mbio huweki vikwazo, mwendo utakata kano.

  Mbio kwao hamnazo, musosikia maneno
  Mbio mali mzo mzo, zilizo mrundikano
  Mbio wachache wanazo, wengi wana misinono
  Mbio bora ni chagizo, mwendo uso na mibano.

  Mbio zangu maagizo, kwa weledi wa maneno
  Mbio zenye mahimizo, kuleta utangamano
  Mbio za maendelezo, sare bila utengano
  Mbio si za mchuchuzo, mwendo uso na mfano.
  Maswali.
  1. Eleza aina ya ushairi huu. (alama 1)
  2. Shairi hili linaangazia nyendo ainati. Thibitisha nyendo hizi kwa kutoa mifano sita kutoka kwenye shairi. (alama 3)
  3. Fafanua umuhimu wa aina mbili za urudiaji zilizotumiwa katika shairi hili. (alama 3)
  4. Bainisha nafsineni katika shairi hili. (alama 2)
  5. Eleza kwa kutoa mfano, mbinu mbili ambazo mshairi ametumia kutosheleza mahitaji ya kiarudhi. (alama 3)
  6. Shairi hili ni la mkondo gani? Thibitisha. (alama 2)
  7. Eleza toni ya mshairi. (alama 1)
  8. Eleza umuhimu wa maswali ya balagha yaliyotumika. (alama 2)
  9. Eleza ujumbe unaojitokeza katika ubeti wa mwisho. (alama 2)
  10. Eleza msamiati wa maneno yafuatayo kama yalivyotumiwa katika ushairi. (alama 1)
  11. Rijali
  12. Mbano

SEHEMU B: CHOZI LA HERI (ASSUMPTA MATEI)

 1.  “Sasa huu ni mji mpya kwake.Ametengana nao kwa muda sasa …”
  1. Ejeza muktadha wa dondoo hili (alama.4)
  2. Ni masaibu yapi yaliyomkumba mrejelewa alipofika tu mjini? (alama.5)
  3. Fafanua sifa za mhusika anayerejelewa (alama 5)
  4. Eleza umuhimu wa mrejelewa (alama 6)
 2. Tathmini jinsi mwandishi wa riwaya ya Chozi La Heri alivyofaulu katika matumizi ya Taswira na majazi (alama 20)

SEHEMU C. TAMTHILIA
T. Arege: Bembea ya Maisha
Jibu swali la 4 au la 5

 1. ."... wakati mwingine mwindaji huwa mwindwa. Hata kijijini wanaishi watu . Watu hao hawakumbwi na dhiki kiasi hiki. Ya nini kung'ang'ana kuyatafuta maisha kama kwamba hayapiti? Maisha ni mshumaa uso mkesha! Ukijiachia sana peupe hata upepo unaweza kuuzima kabla ya kulika hadi nchani.”
  Maswali
  1.  Eleza muktadha wa dondoo hili. (alama. 4)
  2. Bainisha toni katika kauli hili (alama. 2)
  3.  Eleza vipengele vinne vya kimtindo alivyotumia msemaji kufanikisha uwasilishaji wa ujumbe. (alama. 4)
  4. Eleza umuhimu wa msemaji katika kuendeleza ploti ya tamthilia hii. (alama 10)
   au
 2.  
  1. Fafanua umuhimu wa mazungumzo kati ya Luka, Beni na Yona katika kujenga tamthilia ya “Bembea ya Maisha” (alama 10)
  2. "Bembea inapolika na kukatika haiwi mwisho wa michezo.Huungwa na mchezo kuanza tena." Thibitisha ukweli wa kauli hii kwa kutolea mifano mwafaka tamthiliani. (alama. 10)

SEHEMU YA D: HADITHI FUPI: MAPAMBAZUKO YA MACHWEO NA HADITHI NYINGINE.

 1.  “Yu wapi kirukanjia wako? Wajua yuko wapi? Uliacha mbachao kwa msala upitao. Atakutunza nani, maana kwako fadhila za punda ni mashuzi!”
  1. Yaweke maneno haya katika muktadha wake. (alama 4)
  2. Taja mbinu mbili za lugha zilizotumika katika dondoo hili. (alama 2)
  3. Bainisha toni ya dondoo. (alama 1)
  4. Fafanua sifa zozote tatu za mzungumziwa. (alama 3)
  5. Kwa kurejelea hadithi “Fadhila za punda” onyesha ukweli wa kauli kuwa fadhila za punda ni mashuzi kwa mifano mwafaka. (alama 10)
   Au
 2. Huku ukirejelea hadithi zifuatazo tano jadili maudhui ya migogoro kwa kutoa mifano maridhawa. (alama 20)
  1. Fadhila za punda
  2. Msiba wa kujitakia
  3. Mapambazuko ya machweo
  4. Harubu ya maisha
 3. SEHEMU E : FASIHI SIMULIZI
  1. Miviga ni nini ? (alama 2)
  2. Fafanua sifa zozote sita za miviga. (alama 12)
  3. Miviga ina majukumu yapi katika jamii ? (alama 6)


MWONGOZO

 1. .Ushairi
  1. Tarbia (unne): Kila ubeti una mishororo minne. (al 1 x 1 = al 1)
  2.  
   1. Watu wana haraka ya kuiga mavazi mabaya.
   2. Kuna mbio katika kufanya uhuni (ngono)
   3.  Kuna haraka ya kukimbiza mali.
   4. Watu wanawapumbaza vijana na kuwapokonya mali.
   5. Kuna mbio za kusema maneno bila vitendo.
   6. Kuna haraka ya kuangamizana.
   7. Kufanya mambo yasiyo na maana yoyote. (zozote 6 x 1/2 - al 3)
  3.  
   1. Urudiaji wa neno - mbio, mwendo
    Umuhimu : Kutilia mkazo / kusisitiza.
   2. Urudiaji wa vifungu vya maneno : Mbio hizino.
    Umuhimu: Kusisitiza wazo kuu.
   3. Usambamba (urudiaji wa miundo sawa ya sentensi / vishazi / virai: Mfano: Mbio si : Umuhimu - kuchimuza toni ya shairi.
  4. Nafsi neni ni: mshauri (alama 1 x 2 = 2)
  5.  
   1. Tabdila :Sono - soni
    Mfwatano - mfuatano
    Zimetumika kuleta urari wa vina vya utao
   2. Lahaja : hizino, huno
    Kuleta urari wa vina vya utao.
    hugwa - kuanguka - kuleta urari wa mizani.
   3. Inkisari: Twendapi - tunaenda wapi
    Mepangiwa - amepangiwa
    Zendwazo - ziendwazo
    Hutumika kuleta urari wa mizani.
   4. Kufinyanga sarufi / kuboronga sarufi.
    Mbio hizino twendazo - twendazo mbio hizino.
    Hutumika kuleta urari wa vina.
  6. Mkondo wa ushairi:
   1. Kikwamba: Neno mbio linatumika kuanzia kila mshororo wa ubeti fulani.
   2. Mathnawi: Kila mshororo wa kila ubeti umegawika katika pande mbili.
   3. Mtiririko: Vina vya upande wa ukwapi vinafanana (zo) vile vile vya upande wa utao vinafanana (-no)
   4. Sabilia: Shairi lina kituo kinachobadilika badilika katika kila ubeti. Zozote 2 x 1 = al 2
  7. Toni ya mshairi:
   1. Kusuta / kukejeli - banati wanaokimbilia kufanya ngono.
   2. Kuelekeza / kushauri - watu wawe na umoja. Yoyote 1 x 1 = al 1
  8. Umuhimu wa maswali ya balagha:
   Kuibua hisia za nafsi neni za kuemewa } twendapi mbio hizino
   twendapi mwendo huno yoyote 1 x 2 = al 2
  9.  Ujumbe wa mshairi:
   1. Kuwatia watu shime ya kuleta umoja.
   2. Watu wapige mbio katika kuleta umoja na mshikamano / utangamano.
   3. Watu wapige mbio katika kuleta mambo ya faida. Zozote 2 x 1 = al 2
    Tanbihi: Hoja zijadiliwe kwa ukamilifu.
  10. Maana ya maneno.
   1. Rijali - mwanamume mwenye nguvu.
   2. Mbano - nafasi ndogo ; pahali palipofinyika.

B : CHOZI LA HERI

 1.  
  1. Haya ni maneno ya mwandishi yakimrejelea Umu(Umulkheri)Umu alikuwa amefika tu asubuhi kwa gari moshi katika jiji la Karaha .Alikuwa ametoka kwao Mlima wa Simba baada ya wanuna wake. kutoroshwa na Sauna kijakazi wao.
  2.  Masaibu yaliyomkumba Umu alipofika tu jijini (al5)
   Alitafunwa na njaa
   Alihisi baridi kali
   Woga mkuu ulimsumbua maana hakulijua jiji vizuri
   Hakujua iwapo angepata msaada na jinsi angeanza Maisha yake upya
   Alihisi upweke mwingi maana hakujua yeyote 5x1
  3. SIFA ZA UMU 9al5)
   •  Mwajibikaji -alienda kuripoti kutoroshwa kwa wanuna wake katika kituo cha polisi
   • Mwenye utu-alimpa kijana ombaomba shilingi 200
   • Msomi alitia bidii masomoni hadi akapata shahada ya uhandisi
   •  Mwenye busara-hata anapogundua na kuhisi kuwa askari walimwuliza maswali ya kijinga(km walivaa mavazi gani ilihali walipotoroshwa hakuwaona) hakuonyesha kuudhika bali aliwajibu kwa unyenyekevu
   • Pia aliamua kutowaambia askari wale kuwa hakuwa na wazazi maana walidhihirisha ukatili mwingi.
   • Mwadilifu-baada ya taswira ya majanadume yakimtumia madanguroni kumpitia akilini aliamua angejidumishia heshima na uadilifu
   • Mcha Mungu-aliandamana na wazazi wake jumapili kwenda kanisani kwa ibada . Pia anawaombea wazazi wao malipo kutoka kwa Mungu kwa ajili ya wema wao
   •  Mwenye Kumbukizi- kibao kilichoandikwa “Church Road “ kilimkumbushsha aliwahi kupitia hapo na kutoa msaada kwa ombaomba Fulani. Pia alikumbuka mamake akikataa kumpa shilingi mia ili ampe ombaomba
   • Mwenye Imani- alimwahidi Dick angewalea baada ya mama yao kutoweka
   • Mwenye mapenzi ya dhati – aliwapenda ndugu zake Dick na Mwaliko sana na alisikitika sana alipowakosa .Aliwapenda wazazi wake Mwangeka na Apondi
   • Mwenye shukrani- anawashukuru wazazi wake wa kupanga kwa kumlea na kumfadhili kwa kila hali.pia kwa kumchukyua Dick Anashukuru Mwangemi kwa kumlea Mwaliko
   • Mtani – anamkosoa mwangeka kuwa alikuwa amesahau kuna mhandisi mwingine katika familia yao(Engineer Umulkheri)
   • Mshauri 5x1
  4. UMUHIMU WA UMU (al5)
   • Ni kielelezo cha Watoto wanaochukua usukani wa kuiongoza familia pindi tu wazazi wanapoondoka
   •  Ni mfano wa Watoto ambao huwa wame wajibika anaulizia wanuna wake kwa majirani na hatimaye anapowakosa anapiga ripoti kwenye kituo cha polisi .
   • Ni kielelezo cha wasichana wanaokata auli kuwa waadilifu maishani.
   • Ni kielelezo cha watu wenye utu tofauti na Naomi anaahidi nduguze kuwa angewalea kwa mikono yake midogo, , ALIMFAA OMBAOMBA
   • Ametumiwa kufunza jamii kuwa na shukrani
   • Ni kielelezo cha vijana ambao wanawezakutumiwa kushauri na kuwaelekeza wengine- aliwashauri Sophie na Dick maishani.
   • Ni kielelezo cha watu ambao hawakati tamaa maishani
   • Ametumika kuwapa tumaini Watoto wanaopitia changamoto maishani kuwa hawatateseka milele km wanaotoka kwa familia zilizovunjika,mayatima kwenye vituo vya mayatima,,wanaorandaranda mitaani 5x1

SEHEMU C. TAMTHILIA
T. Arege: Bembea ya Maisha
Jibu swali la 4 au la 5

 1.  
  1.  
   1. Msemaji ni Sara
   2.  Msemewa ni Asna
   3.  Walikuwa nyumbani kwa Asna/servant’s quarter.
   4. Sara ana maoni kuwa Asna angehamia kijijini kumsaidia. (4x1=4)
  2. Toni ya kushauri (1x2=2)
  3. Vipengele vya kimtindo:
   1. Methali-mwindaji huwa mwindwa
   2. Swali ya balagha- ya nini kung’ang’ana kuyatafuta maisha kama kwamba hayapiti?
   3. Nidaa- Maisha ni mshumaa uso mkesha!
   4. Jazanda/ sitiari- Maisha ni mshumaa uso mkesha( maisha ni mafupi na hayapo daima)
   5. Mdokezo - …wakati mwingine
   6. Tashihisi / uhuishi - upepo unaweza kuuzima kabla kulika hadi nchani.
   7. kweli kinzani – mwindaji – mwindwa
   8. msemo/nahau - Maisha ni mshumaa uso mkesha! (za kwanza 4x1 = 4)
  4. Umuhimu wa Sara katika kujenga ploti
   1. Sara ametumiwa kuonyesha athari ya migogoro katika ndoa. Maradhi ya moyo anayogangua ni tokeo la mzozano baina yake na mumewe Yona.
   2. Kupitia kwake tunaona alivumilia ndoa yake na kufanya juu chini ili wanawe wapate elimu ili kuboresha mustakabali wao.
   3. Aidha, anahakikisha kuwa binti zake Neema na Asna wanapata elimu.
   4. Ni mfano wa wanawake wenye bidii. Hata akiwa hospitalini, akili yake inafikiria mazao yake aliyoyaacha shambani.
   5. Kupitia mazungumzo baina yake na Asna, yanamsawiri Asna kama kijana aliyekengeuka kiasi cha kutotaka kuingia katika ndoa.
   6. Kupitia kwake tunaelezwa kuhusu usuli wa kutopika. Sara anaeleza kuwa kwa sababu ya ugonjwa wake hangeweza kupika.
   7. Sara alisemwa na kutukanwa na wanajamii kwa sababu ya kuwapata watoto wa kike pekee. Hii ilipelekea Yona kuingilia ulevi.
   8. Baadhi ya matukio katika maisha ya wahusika fulani yanaangaziwa katika nyumba yake. k.m Dina anaangaziwa kama mwenye utu kwani anaenda kumpikia kwa kuwa alikuwa mgonjwa.
   9. Kupitia mazungumzo baina yake na Yona, tunapata kujua kuwa Neema ndiye aliyewasomesha wanuna wake hadi chuo kikuu.
   10. Pia, Sara anatujuza kuwa Neema ndiye aliyewaajiri wafanyakazi nyumbani kwake.
   11. Ametumiwa kuonyesha uwajibikaji wa Neema. Neema anagharamia matibabu ya Sara na pia anampa babake/Yona pesa za kwenda kwa wazee wenzake.
   12. Kupitia kwake tunafahamu kuwa Bunju ndiye aliyemsaidia Neema baada ya kupata ajali na kulipia gharama za hospitali ilhali Bunju hakuwa amemjua Neema.
   13. Kupitia mazungumzo baina yake na Neema na Asna tunapata kujua kuhusu tofauti baina ya hospitali za mjini na kijijini. Huduma za hospitali mjini ni mzuri lakini za kijijini zinalinganishwa na seli na wahudumu hawana mlahaka mwema.
   14. Hatima ya mgogoro baina ya Sara na Yona. Yona anaachana na mila na tamaduni za kutopika kwa Mwanaume.
   15. Anaonyesha jinsi utamaduni ulivyowakandamiza wasichana –Sara anamwambia Asna kuwa siku zao elimu ya wasichana ilifanyiwa bezo na kuwa Sara aliachia darasa la saba.
   16. Kuonyesha mustakabali wa Sara wa kumsamehe,Yona-Yona anamwomba Sara msamaha kwa kuwa hakujua upeo wa ugonjwa wa moyo. (zozote 10x1=10)
 2.  
  1.  
   1. Yanaonyesha sifa ya Luka kuwa ni mkarimu -anawakaribisha wenzake kwake nyumbani kwa chakula cha mchana na kinywaji..
   2. Kuonyesha mila na utamaduni - Luka anadokeza kuwa kitendo cha kula pamoja kwa wazee kilikuwa kinafanywa na wazee wao kwani mavuno ya kwanza huonjwa na wazee na kutoa baraka. (uk. 58)
   3. Yanachimuza ukengeushi - Beni anasema kuwa tatizo la watu siku hizi ni kuzitupa mila zao kabisa. (uk.58) Wajukuu wa Yona hawafahamu lugha yao ya asili. (uk-59)
   4. Yanadhihirisha mchango wa dini - Yona anaeleza dini,imechangia watu kuona mila kuwa chafu. (uk.58)
   5. Yanaonyesha mabadiliko katika malezi - Yona anaambia wazee wenzake kwa malezi kule mjini yameachiwa kina yaya. (uk.59)
   6. Yanaonyesha jinsi mila na tamaduni zilikuwa kandamizi kwani hazikuruhusu mtoto wa kike kuenda shule au kuridhi kitu – kulingana na Luka.(u.k 60)
   7. Yanadhihirisha jinsi hao kina Luka walivyomshinikiza Yona kuoa mke mwingine apate mtoto wa kiume.(u.k 60)
   8. Yonadhihirisha sifa za Beni jinsi ana wivu kwa watoto wa Yona kwani hataki Luka awataje katika mazungumzo yake.
   9. Yanachimuza ufanisi wa watoto wa Yona – Luka anasema walikuwa nyota ya jaha. Neema anarudi kijijini akiwa na gari.
   10. Yonaonyesha thamani ya mtoto wa kike ilivyopanda na nafasi yake kupanuka kwani zamani walikuwa wakiwategemea waume zao laikini sasa hali ni tofauti(u.k.60)
   11. Yonaonyesha maudhui ya uhafidhina – Luka anamuona Neema kama si wao tena baada ya kuolewa.
   12. Yanachimuza hekima ya Luka – Luka anamuuliza Beni kuwa lipi muhimu kati ya tiba au mtu kuja kumpikia mwenzake? (uk.61)
   13. Yanaonyesha sifa za Yona hapo awali kuwa alikuwa mualimu mwenye bidii - Yona anasema angefika kazini majira ya alfajiri, kiboko mkononi, siku nzima kazi tu, aliweza kufunga vitabu kwenye baskeli kwenda kuvisahihisha wikendi. (uk. 62)
   14. Yanadhihirisha mabadiliko katika nyanja ya elimu - Yona anasema siku hizi huwezi tena kumnyoosha mtoto kwa kiboko. (uk.62)
   15. Yanachimuza athari za pombe - jinsi pombe ilivyomfanyaYona kuwa mtumwa akashindwa kuishi bila kulewa (uk62)
   16. Yanaonyesha uvumilivu au stahamala za Sara wakati Yona alipokuwa mlevi. Yona anasema Sara alimsaidia kulea na kusomesha watoto na kwamba bila yeye chombo kingezama. (uk-62)
   17. Yanaonyesha jinsi Yona alivyoanza kutumia tembo alipokuwa chuoni. Wenzake walimpa mvinyo kumrai kuonja. (uk. 62)
   18. Yanadhihirisha uongo wa Beni- kuwa mtoto wake ni fundi wa mitambo na wala si injinia. (uk. 63)
   19. Yanaendeleza ploti- tunatambulishwa kuwa Luka,Beni na Yona ni marafiki na walishiriki vileo pamoja. (zozote 10x1=10)
  2.  
   1. Neema nusura apoteze uhai wake katika ajali Lakini Bunju akamnusuru kwa kumpeleka hospitalini.
   2. Neema na Bunju baada ya kugombana kuhusu mchango wake Bunju katika matibabu ya Sara, Neema anaamua kumuelewa Bunju hivyo ndoa yao kuendelea vyema.
   3. Baada ya changamoto ya kutopata watoto iliyoyumbisha ndoa baina ya Sara na Yona, hatimaye walijaliwa watoto watatu.
   4. Maradhi ya moyo yalipomlemea Sara kiasi cha kukata tamaa na maisha, Neema anajitolea kuhakikisha mamaye amepata matibabu murua hivyo kumrejeshea matumaini.
   5. Japo Yona na Sara walikosa mwana wa kiume na kusimangwa na wanajamii, mabinti zao wanakuwa wembe masomoni hivyo kuwapa furaha katika ndoa yao.
   6. Neema alipoonekana kukata tamaa kutokana na kile alichokiona kuwa ni ubahili wa Bunju, Sara alimpa wasia uliompa nguvu zaidi katika ndoa yake.
   7. Yona baada ya kugundua kuwa ulevi wake unaangamiza familia yake, anaapa kutolewa tena na kumhudumia mkewe Sara.
   8. Yona na Beni walipotofautiana kuhusu watoto wao,Luka anafaulu kutuliza hali na wazee hawa kuendelea na sherehe zao.
   9. Baada ya kumsababishia mkewe maradhi ya moyo,Yona anamwomba Sara msamaha kwa kuwa hakujua upeo wa ugonjwa wa moyo.
   10. Mgogoro baina ya Sara na Neema kuhusu Yona unaisha Neema anapogundua upendo wa Yona Kwao anapoacha utamaduni wa kutopika chakula.
   11. Mgogoro baina ya Sara na Yona unaisha. Yona anapoachana na mila na tamaduni za kutopika kwa mwanaume.
   12. Tatizo la Sara la kushindwa kumpikia mkewe linasuluhishwa na jiraniye Dina anapokuja kumsaidia.
    (zozote 10 x 1=10)
   13. SEHEMU YA B: HADITHI FUPI: MAPAMBAZUKO YA MACHWEO NA HADITHI NYINGINE.
 3. “Yu wapi kirukanjia wako? Wajua yuko wapi? Uliacha mbachao kwa msala upitao. Atakutunza nani, maana kwako fadhila za punda ni mashuzi!”
  1. Yaweke maneno haya katika muktadha wake.
   • Ni maneno ya mamake Luka.
   • Anamwambia Luka.
   • Yumo katika hospitali (Luka).
   • Ni baada ya gavana Luka kuhusika kwa ajali na yule kirukanjia wake akakosa kuja kumwona baada ya kumsaliti Lilia alipokuwa gavana.
    Zozote 4x1=4
  2. Taja mbinu mbili za lugha zilizotumika katika dondoo hili.
   • Methali – usiache mbachao kwa msala upitao.
   • Swali la balagha – yu wapi kirukanjia wako?
   • Takriri - …wapi…wapi
   • Nidaa - …mashuzi! 2x1=2
  3. Bainisha toni ya dondoo.
   • Huzuni, Majuto, uchungu.
   • Dhihaka,dharau 1x1=1
    Umuhimu wa toni ni kuonyesha hisia za mzungumzaji.
  4. Fafanua sifa zozote tatu za mzungumziwa.
   • Mwenye bidii.
   • Ni laghai.
   • Msaliti.
   • Mzinzi.
   • Ni katili.
   • Mnafiki.
   • Ni msomi.
   • Mwenye dharau. Zozote 3x1=3
  5. Kwa kurejelea hadithi “Fadhila za punda” onyesha ukweli wa kauli kuwa fadhila za punda ni mashuzi kwa mifano mwafaka.
   • Luka anaachiwa kanisa na pastor Lee Imani baadaye anauza kanisa ili awanie gavana.
   • Lilia anampenda Luka na anamshawishi babake akubali kuwabariki lakini Luka anamsaliti Lilia anapokuwa gavana kwa kumpiga makofi na teke la tumbo.
   • Luka anamsaliti pastor Lee baada ya kumkubali na kufadhili elimu, baadaye anakuwa na uhusiano na mtoto wake anayemtesa baadaye.
   • Luka anawasaliti waumini kwa kuuza kanisa na kuingia siasani.
   • Luka anamtendea uovu mkewe anapokosa kuandamana naye kwenye kampeni na kumtusi kuwa amenona kama nguruwe na kwamba wanawake ni wengi.
   • Luka anawasaliti wananchi waliomchagua kwa kutotimiza ahadi alizowatolea wakati wa kampeni.
   • Luka anamsaliti mkewe kwa kuwa na uhusiano ka kiruka njia.
   • Kirukanjia anamsaliti Luka kwa kukosa kumtembelea hospitalini baada ya kujulishwa na daktari huenda asiweze kutembea tena licha ya kuwa na uhusiano wa kimapenzi naye.
   • Lilia anamsaliti babake kwa kuacha kazi ya meneja wa benki baada ya babake kumsomesha na kupata kazi ili awe akipokea wageni wa Luka.
   • Lilia anamsaliti babake kwa kushinikiza aolewe na Luka, ingawa babake hakutaka.
   • Lee anamsaliti Lilia kwa kumrithisha Luka Kanisa 10x1=10
    Au
 4. Huku ukirejelea hadithi zozote tano jadili maudhui ya migogoro kwa kutoa mifano maridhawa.
  1. Fadhila za punda
   1. Lilia na Luka wana mgogoro unaosababisha vita k.m anapojitazama kwenye kioo anaona kovu shavuni na donda.
   2. Mapenzi ya Lilia na Luka yanaleta mgogoro kati ya Lilia na babake-hapendi uhusiano ule.
   3. Kuna mgogoro wa kinafsia kwa babake Lilia anayemshuku Luka kuwa na uhusiano na mwanawe Lilia.
   4. Luka kumvamia mkewe na kumvuta nywele kumwelekeza kwenye chumba cha kulala, ambapo anampiga ngumi na mateke.
   5. Luka anamtawisha Lilia na hata kumlazimisha kuandamana naye kwenye kampeni na hii inawafanya wakosane – Luka anamwambia wanawake ni wengi.
  2. Msiba wa kujitakia
   1. Kati ya viongozi na raia ambao wako tayari kupigania haki zao-hawapewi huduma na viongozi.
   2. Zuhura na Machoka-Zuhura angependa kumchagua kiongozi kwa misingi ya kikabila kinyume na Machoka.
   3. Sugu Junior na Fumo Matata – Fumo anaona dai la serikali kwamba kuna maendeleo ni porojo tu.
   4. Mgogoro kati ya tume ya uchaguzi na wananchi.
   5. Mgogoro wa ushindi wa Sugu Junior dhidi ya Fumo matata.
   6. Kati yam zee Sugu Senior na Zuzu Matata; ambapo mzee Sugu senior alitwaa uongozi baada ya kuondoka kwa wakoloni.
  3. Mapambazuko ya machweo
   1. Mzee Makutwa kumtifulia mzee Makucha vumbi na kumdhihaki kuhusiana na kazi yake.
   2. Bi Macheo anajikuta katika mgogoro na mumewe kwa vile hapendi jinsi mzee Makutwa anavyomfanyia stihizai mumewe.
   3. Mzee Makucha anakuza mgogoro anapomwitia polisi mzee Makutwa kwa kuwahujumu vijana.
   4. Mzee Makutwa ana mgogoro na sheria kwa vile anaendesha biashara haramu.
   5. Migogoro kati ya vijana waliosoma na serikali kwa mfano Sai alidai kuwa vijana wanaachiwa kazi za hadhi ya chini.
   6. Mzee Makutwa na polisi wakijaribu kumwingiza pangoni.
   7. Mzee Makucha na shirika la reli-kukataa kumlipa pesa.
  4. Harubu ya maisha
   1. Mama Mercy amtaka mumewe aeleze sababu ya kutofika ilhali motto anaelekea kulala. Mama Mercy analalamika kuwa mumewe hatimizi wajibu wake.
   2. Familia ya Kikwai ina mgogoro na fundi wa nyumba hajalipwa kwa mwezi mzima.
   3. Kikwai anagongana na Bosi kwa kuacha gari nyumbani kwa kukosa mafuta.
   4. Nilakosi ana mgogoro wa mpangishaji wake kwa vile hajamlipa na mwezi unaenda kuisha.
   5. Kikwai kutoleta chakula.
   6. Kikwai kufika amechelewa.
   7. Mercy kulalamikia njaa na upweke.
 5.  
  1. Miviga ni sherehe maalum za kitamaduni zinazoambatanishwa na nyimbo na ngoma
  2. Sifa za miviga
   • huambatana na utamaduni
   • huongozwa na watu maalum
   • hufanywa mahali maalum - mwituni
   • hufanywa kwa utaratibu maalum
   • kuna kula kiapo
   • hufanywa wakati maalum - kutawazwa viongozi, harusi, mazishi
   • huambatana na mawaidha
   • kuna kutolewa kafara zozote 6 x 2 = 12
    kutaja - 1, kueleza - 1
  3.  
   • Huburudisha
   • huelimisha
   • huelekeza
   • hukuza mila na desturi
   • huhifadhi historia ya jamii
   • hutambulisha jamii
   • huandaa wanajamii kukabiliana na hali ngumu
   • njia ya kupitisha maadili kutoka kizazi kimoja hadi kingine
   • huonyesha imani za kidini za kijamii
   • huonyesha matarajio ya wanajamii zozote 6 x 1 = 6
Join our whatsapp group for latest updates

Download Kiswahili Paper 3 Questions and Answers - Kenya High Post Mock 2023 Exams.


Tap Here to Download for 50/-
Why download?

 • ✔ To read offline at any time.
 • ✔ To Print at your convenience
 • ✔ Share Easily with Friends / Students


Get on WhatsApp Download as PDF
.
Subscribe now

access all the content at an affordable rate
or
Buy any individual paper or notes as a pdf via MPESA
and get it sent to you via WhatsApp

 

What does our community say about us?