Kiswahili Paper 2 Questions and Answers - Kenya High Post Mock 2023 Exams

Share via Whatsapp

.Maagizo

 • Jibu maswali yote.
 • Majibu yote yaandikwe kwa lugha ya Kiswahili.


MASWALI

 1. UFAHAMU
  Soma taarifa ifuatayo kasha ujibu maswali.
  Historia ya katiba
  Katiba ni utaratibu wa sheria unaoweka mpango wa jamii kuendesha mambo.Ni muhimu kila raia ajue katiba ya nchi yake.
  Katiba yaweza kuwa imeandikwa au haikuandikwa. Katika jamii za jadi, katiba ilihifadhiwa na kupokezwa kwa mdomo. Mtindo wa kuandika katiba ulianza nchini Marekani mwaka 1787. Ingawa katiba hii imefanyiwa mabadiliko hapa na pale,bado ni ileile. Kenya ilipowekwa chini ya himaya ya Uingereza mwaka 1895, ilianza kutumia katiba ya Uingereza. Baada ya masetla wa kikoloni kujikita, Kenya kuwa koloni. Hii ililazimu pawe na katiba nyingine mwaka 1920. Waafrika waliupinga mfumo huu kwa sababu haukuwahusisha kikamilifu kwenye masuala ya uongozi. Utetezi wa wanasiasa uliilazimisha serikali ya Uingereza kuitisha makongamano mbalimbali kama vile lile la Devonshire na mengine ili kurekebisha katiba. Waafrika hawakuridhika. Wakaendelea kudai katiba mwafaka. Harakati hizi zilileta kuitishwa kwa kongamano la katiba la Lancaster. Lengo lilikuwa kuandika katiba itakayotumiwa nchini hadi leo. Kati ya wajumbe walioenda Uingereza kuandika katiba mwaka 1962 ni pamoja na Tom Mboya, Jean Marie Seroney, Julius Kiano, Jomo Kenyatta, Masinde Muliro, Oginga Odinga, Ronald Ngala, Daniel Arap Moi na James Gichuru. Wengine ni Martin Shikuku, Dennis Akumu, Taita Towett, Abdilahi Nassir, Jeremiah Nyaga na John Keen.
  Katiba ni kitovu cha taifa. Baina ya mambo inayotekeleza ni kuweka utaratibu na kanuni za utawala, kwa mfano, utawala wa kimikoa na serikali za wilaya. Pamoja na haya, katiba hufafanua vyombo vikuu vya serikali ,mamlaka yavyo na mipaka yavyo ya kutenda. Vyombo hivi ni bunge, mahakama, urais, jeshi n.k. Hali kadhalika, katiba hupambanua haki za raia.
  Hii hudumisha demokrasia na huwawezesha wananchi kupata uhuru na haki za kimsingi. Katiba hukinga haki za kila raia, hasa kutokana na udhalimu wa wengi au wenye uwezo mkubwa. Zaidi ya yote, katiba huimarisha asasi za umma ili kudumisha uwajibikaji.
  Katiba huhalalishwa na watawaliwa. Hii hutokea wanaposhirikishwa katika uandishi wake. Kuanzia miaka ya themanini, raia walianza kudai katiba igeuzwe. Mwamko wa kutaka mageuzi ulianza kwa harakati za kubadilisha mfumo wa kisiasa kutoka ule wa chama kimoja hadi ule wa demokrasia ya vyama vingi. Haja ya mfumo mpya wa kisiasa ulilenga kuwashirikisha wananchi katika utawala na kuondoa uimla.
  Harakati zilitia fora miaka ya tisini. Mambo yaliyochochea hali hii ni mengi. Kwanza, katiba iliyokuwa imeandikwa na watu wachache ilikuwa imefanyiwa marekebisho mengi. Marekebisho haya yalimpa rais mamlaka mengi juu ya serikali kuu na vyombo tofauti vya serikali. Pili, viongozi na watu wenye uwezo na utajiri walipuuza katiba. Raia walihisi wanadhulumiwa. Walipinga hali ya wachache waliomzunguka rais kunufaika huku umma ukitengwa. Tatu, kutokana na uongozi uliokuweko wakati huo, wanawake, watoto na walemavu walidhulumiwa na kukosa uwakilishi ufaao.Hatimaye, pakawa na ongezeko la uharibifu wa mazingira, ufisadi na unyakuzi wa mali ya umma kama vile ardhi.
  Waliopigania katiba mpya walikuwa na haja ya katiba ambayo uandikaji wake ungewahusisha Wakenya wote. Mwanzoni, serikali ilipinga wito wa mabadiliko. Lakini mnamo mwaka 2001 iliunda Tume ya Marekebisho ya Katiba ili kutekeleza mahitaji ya wananchi. Tume hii iliwahamasisha na kuwashawishi raia kutoa maoni. Tume iliandaa vikao katika maeneo ya ubunge 210 ambapo wananchi walitoa mapendekezo kuhusu marekebisho ya katiba waliyotaka.
  Katika mapendekezo hayo raia walisisitiza mambo kadhaa. Jambo la kwanza ni utawala mwema na uwajibikaji wa viongozi na maafisa wa umma .Jambo lingine ni kulinda haki za binadamu zikiwemo za wanawake, watoto na walemavu. Raia walidai kanuni za usawa na ulinganifu. Aidha walitilia mkazo mahitaji ya msingi kama chakula, afya nzuri, makao, elimu, usalama, uchumi, na kadhalika.
  Msingi wa mapendekezo hayo yote ni kuwepo na amani ya kitaifa, umoja na uadilifu ili kulinda maslahi ya wananchi wote na taifa.
  Maswali :
  1. Eleza kilichosababisha kongamano la katiba la Lancaster (alama3)
  2. Taja mambo matatu yaliyotiliwa mkazo na raia katika maoni yao kuhusu katiba. (alama3)
  3. Eleza umuhimu wa katiba kwa mujibu wa taarifa. (alama3)
  4. Taja sababu zilizochangia ubadilishaji wa katiba. (alama3)
  5. Eleza maana ya maneno haya kama yalivyotumiwa katika taarifa. (alama3)
   1. Kitovu
   2. Harakati
   3. Hamasisha
 2. UFUPISHO. (ALAMA 15)
  Mwezi jana, Serikali ya kitaifa na zile za kaunti ziliwasilisha makadirio yao ya bajeti, miezi miwili kabla ya mwaka wa kifedha kuisha kama zinavyohitajika na katiba. Serikali hizo zilieleza jinsi zinavyonuia kutumia mabilioni ya pesa kufadhili shughuli zao mwaka ujao wa kifedha wa 2013/2014.
  Serikali ya Rais Uhuru Kenyatta ilisema itatumia shilingi 1.6 Trilioni kufadhili maendeleo na shughuli za sekta na idara zake tofauti. Makadirio haya ambayo yaliwasilishwa na kiongozi wa walio wengi bungeni, Bw Aden Duale. Hata hivyo yalikosa kueleza jambo moja muhimu – jinsi kitita hicho kitakavyopatikana. Nasema hivi kwa sababu kuna habari ambazo zimenipa tumbojoto na wasiwasi mkubwa. Imebainika kuwa kufikia mwishoni mwa Machi mwaka huu, Kenya ilikuwa inadaiwa Shilingi 1.8 Trilioni na wafadhili wa humu nchini na kigeni.
  Kama habari hizi hazijakushtua sitakulaumu kwa sababu huenda ukawa hujui ukubwa wa kiasi hiki cha fedha. Ili uweze kuelewa, nitazigawanya fedha hizi miongoni mwa wakenya milioni 40 ili tujue kila mkenya anadaiwa kiasi gani. Kila mkenya nchini, wakiwemo watoto na wazee wakongwe, anadaiwa Shilingi 45,000 ! Hivyo basi ili deni hili liweze kulipwa, kila mkenya atalazimika kutoa kiasi hicho cha fedha.
  Ni deni ambalo Rais Uhuru Kenyatta alirithi kutoka kwa mtangulizi wake, Rais Mwai Kibaki ambayo utawala wake ulivunja rekodi ya kukopa. Wahenga hawakukosea waliposema dawa ya deni ni kulipa. Deni hili linapaswa kumkosesha usingizi Rais Kenyatta ambaye anapaswa kutafuta njia za kulilipa bila kuathiri uchumi, maendeleo na utekelezaji wa ahadi nyingi alizowapatia wakenya wakati wa kampeni.
  Hili halitafanyika kama serikali itatenga fedha nyingi kuwalipa maafisa wake mishahara na marupurupu minono pamoja na kuwapa mabilioni ya pesa kununulia magari ya kifahari. Pengine Rais hajafahamishwa kuwa mwaka ujao wa kifedha serikali itajipata pabaya kwani Halmashauri ya ukusanyaji ushuru nchini (KRA), haitaweza kukusanya kiwango kilichowekewa na serikali baada ya shughuli ya ushuru kutatizwa na hofu iliyotanda wakati wa uchaguzi
  KRA imekusanya shilingi 560 bilioni kufikia mwishoni mwa Machi ilhali ilikuwa imeagizwa kukusanya shilingi 881 bilioni.
  Serikali za kaunti, ambazo zingali changa, zimependekeza kutumia mabilioni ya fedha ambazo hazitaweza kukusanya. Badala yake zimeomba serikali kuu ijaze pengo hilo au zipewe idhini ya kukopa.
  Rais Kenyatta hana budi kuchukua hatua za dharura kuhakikisha kuwa wakenya hawataendelea kuandamwa na madeni maishani mwao.
  Maswali.
  1. Kwa maneno yasiyozidi 70, fupisha aya za kwanza nne. (alama 10, 1 mtiririko)
   Matayarisho
   Jibu
  2. Kwa nini serikali haitaweza kulipa madeni yake? (maneno 40 -50) (alama 5, 1 mtiririko)
   Matayarisho
   Jibu
 3. MATUMIZI YA LUGHA (ALAMA 40)
  1. Eleza sifa mbili mbili za sauti zifuatazo. (alama. 2)
   1. /i/
   2. /o/
  2. Onyesha mahali mkazo unapowekwa kwenye neno ‘Tenganisha’. (alama. 1)
  3. Eleza matumizi manne ya kiimbo. (alama.2)
  4.  
   1. Eleza dhana ya mofimu. (alama. 1)
   2. Huku ukitolea mfano, taja aina mbili za mofimu. (alama. 2)
  5. Ainisha vipengele vya kisarufi katika sentensi hii.
   Aliyekusamehea (alama.3)
  6. Ainisha nomino katika sentensi hii.
   ‘Juma, na jeshi lote walikula chakula cha raha’ (alama.2
  7. Andika kwa udogo wingi. (alama.3)
   ‘Njia hii yetu inapitiwa na mtu mnene.
  8. Bainisha aina za vishazi katika sentensi hii. (alama.2)
   ‘Katiba ambayo inapingwa na wengi haitetei maslahi ya walio wachache’
  9. Onyesha chagizo katika sentensi ifuatayo. (alama. 1)
   ‘Alipiga mpira teke ukaruka juu juu zaidi.’
  10. Changanua sentensi hii kwa kutumia kielelezo cha matawi. (alama.4)
   ”Tulimtembelea mgojwa jana hospitalini“
  11. Tumia kireshi ‘O’ tamati katika sentensi ifuatayo. (alama.2)
   ‘Kalamu ambayo alinunua ni ile ambayo anaipenda.’
  12. Andika sentensi hii katika usemi wa taarifa.
   “Msiposoma kwa bidii wakati huu, mtaanguka mtihani mwaka ujao.”Mwalimu akawaambia wanafunzi wake. (alama.3)
  13. Tunga sentensi ukitumia kitenzi kifuatacho kauli ya kutendeka. (alama.2)
   ‘nywa.’
  14. Eleza matumizi mbalimbali ya “ni” katika sentensi ifuatayo. (alama. 4)
   ‘Nendeni mkamwite Kanini ambaye ni mwanafunzi wangu niliyemwacha maktabani.’
  15. Tunga sentensi moja kuonyesha tofauti ya kimaana kati ya ‘Husuni’ na ‘Huzuni.’ (alama.2)
  16. Tunga sentensi kwa kutumia vihisishi vifuatavyo. (alama. 2)
   1. Alhamdulilahi
   2. Laiti
   3. Eleza maana mbili za sentensi hii. (alama. 2)
    Alinichezea na Baniani
 4. ISIMUJAMII (Alama 10)
  1. Lahaja huainishwa katika makundi mawili. Yataje (alama 2)
  2. Eleza sifa zozote nne za lugha ya taifa. (alama 4)
  3. Tolea ushahidi namna nne kwamba Kiswahili ni lugha ya kimataifa. (alama 4)


MWONGOZO

 1. UFAHAMU
  MASWALI
  1. Eleza kilichosababisha kongamano la katiba la Lancaster (alama3)
   • Waafrika hawakua wamehusushwa katika katiba ya mwaka wa 1920.
   • Waafrika walitaka kuhusika katika masuala ya uongozi.
   • Utetezi wa wanasiasa ulilazimu serikali ya uingereza kuitisha kongamano.
  2. Taja mambo matatu yaliyotiliwa-mkazo na raia katika maoni yao kuhusu katiba. (alama3)
   • Utawala mwema na uwajibikaji wa viongozi.
   • Kulinda haki za binadamu zikiwemo za wanawake, watoto na walemavu.
   • Kanuni za usawa na ulinganifu.
  3. Eleza umuhimu wa katiba kwa mujibu wataarifa. (alama3)
   • kuweka utaratibu na kanuni za utawala mf utawala wa kimikoa.
   • Hufafanua vyombo vikuu vya serikali, mamlaka yavyo na mipaka yavyo ya kutenda.
   • Hupambanua haki za raia.
  4. Taja sababu zilizochangia ubadilishaji wa katiba. (alama 3)
   • Katiba iliyokuwa imeandikwa na watu wachache ilikuwa imefanyiwa marekebisho mengi.
   • Viongozi na watu wenye uwezo na utajiri walipuuza katiba.
   • Kutokana na uongozi uliokuweko wakati huo, watoto na watoto na walemavu walidhulumiwa na kukosa uwakilishi ufaao.
  5. Eleza maana ya maneno yafuatayo kama yalivyotumika katika taarifa. (alama 3)
   • Kitovu : Chenye maana na umuhimu.
   • Harakati : Shughuli za kufanya jambo fulani.
   • Hamasisha : Kufanya jambo lieleweke na kukubalika.
 2. UFUPISHO
   • Serikali kuwasilisha ajeti.
   • Kueleza jinsi mabilioni yaliyotumiwa.
   • Serikali kusema itatumia shilingi 1.6 trilioni kwa maendeleo.
   • Makadirio kuwasilishwa na kiongozi wa walio wengi bungeni.
   • Kukosa kueleza jinsi ya kupata kitita hicho.
   • Habari hizi kunipa wasiwasi.
   • Kenya kudaiwa shilingi 1.8 trilioni na wafadhili.
   • Kutolaumu wale wasioelewa ukubwa wa deni hili.
   • Kugawanya deni hili kwa wakenya wote.
   • Kila mkenya kudaiwa shilingi 45,000
   • Deni kumkosesha usingizi Rais.
   • Kutafuta njia ya kulipa bila kuathiri uchumi.
    (Zozote 9x1= 9, 1 ya mtiririko)
  1.  
   1. Serikali kutenga fedha nyingi kuwalipa wafanyikazi.
   2. KRA kutokusanya kiwango kinachohitajika.
   3. Ukusanyaji wa ushuru kukatizwa na hofu wakati wa uchaguzi.
   4. Serikali za kaunti kupendekeza kutumia mabilioni ambayo hawana
    (4x1 = 4, 1 ya mtiririko)
 3. MATUMIZI YA LUGHA (Alama 40)
  1.  
   /i/ - Irabu ya mbele ya ulimi/hutamkiwa mbele ya ulimi.
   • Inapotamkwa midomo hutandaza.
    /o/ - Irabu ya nyuma ya ulimi / hutamkiwa nyuma ya ulimi.
   • Inapotamkwa midomo huviringa. ( ½ x 4 = Al 2)
  2. Tenga‘nisha/ tenganisha/ Tenganisha n.k (1x 1= Al. 1)
  3.  
   • Kutolea rai/wazo
   • Kuuliza swali.
   • Kuonyesha amri/kuamrisha.
   • Kuonyesha mshangao. ( ½ x 4 = Al.2)
  4.  
   1. Mofimu – Ni sehemu ndogo sana ya neno inayowasilisha maana/ kipashio kidogo cha lugha/amilifu katika umbo la neno ambacho hakiwezi kugawanywa zaidi. (1 x 1 = Al.1)
   2. Mofimu funge/tegemezi/ Ambata
    Mifano
    m-tu, m-to, m-levi
    uzee – ka-ji, uzee-ni
    m-gonjwa, mwana-maji, n.k
    • Mofimu huru
     Mifano – Zawadi, dirisha, meli, tunda, shavu, mama, samaki, njia, bata, miwani. ( ½ x 4= Al. 2)
  5. A – kiambishi cha nafsi ya tatu umoja/ kiambishi cha ngeli ya A – WA.
   Li – kiambishi cha wakati uliopita.
   ye – kiambishi cha urejeshi
   ku- kiambishi cha mtendewa
   samehe – mzizi/ shina
   a – kiishio/kimalizio (6 x ½ = Al. 3)
  6. Juma - Nomino ya kipekee
   Jeshi – Nomino ya jamii
   Chakula – Nomino ya kawaida
   Raha – Nomino ya dhahania. (4 x ½ = Al. 2)
  7. Vijia hivi vyetu vinapitiwa na vijitu vinene. (6 x ½ = Al. 3)
  8. Vishazi
   Katiba ambayo inapingwa na wengi – Kishazi tegemezi.
   (Katiba) haitetei masilahi ya walio wachache – Kishazi huru. (2 x 1 = Al. 2)
  9. Chagizo – juu juu zaidi (1 x 1 = Al. 1)
  10. Tulimtembelea mgonjwa jana hospitalini.
   Au
   (8x ½ =al.4)
  11. Kalamua ainunuayo ni ile aipendayo. (2x 1 = Al. 2)
  12. Mwalimu aliwaambia wanafunzi wake kwamba wasingesoma kwa bidii wakati huo.
   • wangeanguka  mtihani mwaka ambao ungefuata. (6 x ½ = Al. 3)
  13. Kutendeka – nyweka
   (Mwalimu akadirie sentensi. (1 x 2 = Al. 2)
  14. Nendeni – amri/vai/wingi
   ni – kitenzi kishirikishi (kipungufu)
   niliyemwacha – Nafsi ya kwanza umoja / nafsi ambati.
   Maktabani – Kielezi cha mahali. (4 x 1 = Al. 4)
  15. Husuni na huzuni
   Husuni – ngome, gereza
   Huzuni – majonzi, masikitiko
   (Sharti yatumiwe katika sentensi moja. Mwalimu akadirie majibu ya wnafunzi)
   (2 x 1 = Al. 2)
  16.  
   1. Alhamdulilahi – Shukrani / Furaha.
    Mfano: Alhamdulilahi ! Sikutarajia mwanangu angepita mtihani huo vizuri hivyo.
    Alhamdulilahi ! Mgonjwa wetu amepona.
   2. Laiti – majuto
    Mfano: Laiti ningejua/ningelijua singempa/singelimpa usaidizi. (2 x 1 = Al.2)
  17.  
   1. Alicheza kwa niaba yangu na Baniani
   2. Mimi pamoja na Baniani tulichezewa. (2 x 1 = Al. 2)
 4. ISIMUJAMII
  1.  
   1. Kijamii
   2. Kijiografia/kimaeneo
    (2 x 1=2)
  2. Huwa na wazungumzaji wengi.
   Huwa ni lugha ya kwanza ya kikundi cha watu inayokiwezesha kikundi husika kupokezana utamaduni.
   Huwa na muundo wakiisimu unaofanana na ule wa baadhi ya lugha za watu wa nchi husika.
   Lazima iwe mojawapo wa lugha asilia.
   (4 x 1=4)
  3. Kiswahili kinazungumzwa na watu wa Afrika Mashariki na Kati.
   Kiswahili hufundishwa katika shule za Kenya, Uganda na Tanzania.
   Kiswahili hufundishwa katika vyuo vya Afrika Mashariki, Marekani na Ujerumani.
   Hutumika katika mikutano ya kimataifa kama vile Umoja wa Afrika.
   Kiswahili hutangazwa katika idhaa za Kimataifa kama vile B.B.C, Redio China na Idhaa ya Kijerumani.
   Kwa sasa hutumika katika mtandao.
   (Zozote 4 x 1=4)
   Kukosoa – h -4 x ½ =2
   s- 4 x ½ =2
Join our whatsapp group for latest updates

Download Kiswahili Paper 2 Questions and Answers - Kenya High Post Mock 2023 Exams.


Tap Here to Download for 50/-
Why download?

 • ✔ To read offline at any time.
 • ✔ To Print at your convenience
 • ✔ Share Easily with Friends / Students


Get on WhatsApp Download as PDF
.
Subscribe now

access all the content at an affordable rate
or
Buy any individual paper or notes as a pdf via MPESA
and get it sent to you via WhatsApp

 

What does our community say about us?