Kenya Certificate Of Secondary Education(KCSE 2013) Kiswahili Karatasi ya Kwanza with Marking Scheme

Share via Whatsapp

Kiswahili Paper 1 (102/1)

  1. Lazima:
    Wewe ni meneja katika kampuni ya Jitihada ambapo pamekuwa na visa nya ukiukaji wa maadili ya kikazi. Waandikie wafanyakazi memo kuwaonya dhidi ya jambo hili.
  2. "Rununu(simutamba) imeleta athari mbaya katika jamii." Jadili.
  3. Andika kisa kitakachodhihirisha maana ya methali: Usitukane wakunga na uzazi ungalipo.
  4. Tunga kisa kinachoanza kwa maneno yafuatayo:
    Moyo wangu ulidunda kwa matarajio makuu...


MARKING SCHEME

  1. Huu ni utungo amilifu. Vipengele viwili vikuu vya utungo wa aina hii vishughulikiwe:
    1. Maudhui;
    2. Muundo.
  1. Muundo wa memo
    Mtahiniwa azingatie muundo wa juu (sura) wa memo.
    Vipengele vifuatavyo vya kimsingi vizingatiwe.
    1. Nembo na anwani ya Kampuni ya Jitihada. Iandikwe juu, katikati mwa karatasi wala si juu pambizoni kama ilivyo katika barua rasmi ya kawaida . Anwani inaweza kujumuisha mahali, mtaa, barabara au jengo ambamo kampuni ya Jitihada inapatikana.
      Kwa mfano: Mtaa wa Viwandani, Barabara ya Tungama, n.k; anwani ya barua pepe, tovuti na kipepesi (faksi).
    2. Nambari ya marejeleo/kumbukumbu ya marejeleo. Kwa mfano:
      Kumb./ Rej. JIT/ JUMLA/NIDHAMU/2013/2
    3. Tarehe - inaweza kuandikwa pambizoni kwenye mstari mmoja na nambari ya kumbukumbu.
    4. Mtajo
      1. Kutoka Kwa: Meneja
      2. Kwa: Wafanyakazi wote
    5. Mada/Kuhusu: Ukiukaji wa maadili ya kikazi
      Au
      Mada: Onyo kuhusu ukiukaji wa maadili ya kikazi
    6. Utangulizi
      Mtahiniwa atangulize kiini cha memo. Kwa mfano: mtindo ufuatao unaweza
      kufuatwa:
      Ripoti zilizowasilishwa katika afisi hii na wakuu wa vitengo mbalimbali zimebainisha
      kudorora kwa maadili ya kikazi ..., n.k
    7. Mwili: Hapa ndipo hoja zitakapojadiliwa.
      Hoja zipangwe ki - aya.
    8. Hitimisho (kimuundo)
      Mtahiniwa ahitimishe utungo wake.
      Hapa anaweza kujumuisha hatua ambazo zitachukuliwa kwa atakayeendelea kukiuka
      maadili ya kikazi.
    9. Kimalizio Muundo wa mwisho wa memo udhihirike kama ifuatayo:
      1. sahihi
      2. jina
      3. cheo (si lazima) kwa vile ametaja tayari.
      4. Nakala kwa, kwa mfano,
        1. Mkurugenzi
        2. Wakuu wa vitengo
          (Nakala si lazima)
  2. Maudhui
    Mtahiniwa aibue hoja zinazohusiana na kutozingatia nidhamu kazini. Baadhi yazo ni:
    1. Kuchelewa kazini
    2. Kuondoka mapema
    3. Kuzembea kazi/kutofikia malengo
    4. Matumizi mabaya ya rasilimali za kampuni
    5. Mahusiano yasiyoruhusiwa, kwa mfano ya kimapenzi
    6. Mawasiliano yasiyofaa, kwa mfano yanayoeneza kashfa dhidi ya wafanyakazi wengine au viongozi
    7. Mavazi yasiyo na staha
    8. Kudai malipo ghushi
    9. Kutoa siri za kampuni
    10. Kuhusika katika biashara/shughuli inayoendelezwa na kampuni ya Jitihada
    11. Mapendeleo kazini, kwa mfano kuhusiana na utoaji wa nafasi za kujiendeleza
    12. Utoaji na upokeaji wa rushwa
    13. Kutoheshimu /kutozingatia haki za wafanyakazi wenye mahitaji maalum
    14. Kushusha hadhi ya kampuni kupitia mwenendo wako
    15. Kutumia muda wa kampuni kujiendeleza masomoni bila kufidia.
    16. Matumizi mabaya ya vileo
    17. Kutoa zabuni kwa njia ya mapendeleo
    18. Kutowaheshimu wakuu wako/kudhalilisha hadhi ya wakuu
    19. Kukosa kuwajibikia makosa pale yanapotokea
    20. Kuendeleza dhuluma ya kimapenzi
    21. Kutumia mali ya kampuni bila idhini kujiendeleza
      Hitimisho (kuhusiana na mada)
      Hitimisho inaweza kujumuisha hatua ya kinidhamu kulingana na sera za kampuni, k.v onyo, kusimamishwa kazi kwa muda na kufutwa. Mtahiniwa anaweza pia kuwahimiza wafanyakazi kuzingatia maadili ya kikazi (bila kutoa onyo) ili kufanikisha utendakazi na maendeleo ya kampuni.

      Tanbihi
      1. Kwa vile hili ni onyo, mtahiniwa anahitajika kutumia lugha yenye toni kali au inayohimiza nidhamu kazini.
      2. Mtahiniwa anaweza kufafanua kosa na hapohapo akataja hatua ya kinidhamu.
      3. Kaida nyingine zote za usahihishaji wa karatasi hii zizingatiwe.
  1. Hii ni insha ya mjadala. Ifuate kanuni za mjadala ambapo patakuwa na hoja za kuunga mkono na za kupinga.
    Kuunga mkono
    1. Hatari za kuangamia kwa lugha ambazo hazitumiki kwa wingi katika mawasiliano ya simu tamba
    2. Kupalilia uraibu wa matumizi ya rununu, vijana kujizika katika matumizi ya rununu kiasi cha kufifilisha utendaji wao kielimu
    3. Kuchipuka na kustawi kwa aina mpya na nyeti za uhalifu kama vile utapeli 
    4. Kuporomoka kwa misingi ya familia, ikiwa mume/mke atamdhibiti mwenzake kwa kutaka kusoma ujumbe wake mfupi au kuchunguza nani wanaompigia mwenzake simu, mtafaruku unaweza kuzuka. Pia jamaa nyingi huhiari kupigania simu badala ya kuonana ana kwa ana, hivyo kupujua mshikamano wa kifamilia
    5. Kuvuruga lugha/sarufi. Watu wamezoea kuandika kwa ufupi.
    6. Kudanganya katika mtihani, hivyo kupujua thamani ya mitihani.
    7. Kuzorota kwa maadili, k.v kuharibia mtu sifa kupitia ‘facebook’, kudanganya moja kwa moja pale ulipo n.k.
    8. Kudhalilisha ubunifu/wizi wa kiusomi. Baadhi ya watu hutumia simu kuiba mawazo ya wengine.
    9. Wizi wa ubunifu wa kazi za kisanii ambazo hazijapewa hakimiliki
    10. Kurahisisha uporaji na unyakuzi wa malighafi za mataifa yanayoendelea kupitia kwa mtandao
    11. Upujufu wa maadili, vijana kutazama filamu chafu.

      Hoja za kupinga

      Rununu zina manufaa chungu nzima kama vile:
    12. Kuleta wanadamu pamoja duniani na hivyo kupunguza tuhuma zinazoelekea kuleta vurugu kwa watu kutofahamiana
    13. Usambazaji wa teknolojia inayorahisisha maisha ya wanadamu kote duniani kupitia kwa huduma zinazotolewa na simu.
    14. Kuendeleza biashara - kubadilishana bidhaa na pesa kupitia mtandao kama vile MPESA.
    15. Hurahisisha huduma za benki. Mtu anaweza kufikia akaunti yake kupitia kwenye rununu.
    16. Huwa na vifaa kama vile vikokotoo vya kurahisisha kufanya hesabu.
    17. Ni chombo cha burudani - vijana hupata michezo mbalimbali.
    18. Huimarisha utafiti. Mtu anaweza kufanya utafiti kupitia kwenye rununu.
    19. Huweza kutumiwa kupigia picha, hivyo kuokoa pesa ambazo zingenunulia kamera au video.
    20. Mtu anaweza kuwasiliana na familia yake kutoka mbali, hivyo kuokoa muda na fedha ambazo angetumia kusafiri.
    21. Mtu anaweza kuhifadhi msahafu(Biblia au Korani) kwenye simu, hivyo kujikuza kiroho kila mara.
    22. Ni njia ya kupata habari kutoka kwenye mashirika ya usambazaji wa habari. Baadhi ya rununu zina redio na hata runinga. Mtu anaweza kusikiliza na kutazama habari hata akiwa safarini.
    23. Hufanikisha kuwanasa matapeli na magaidi. Baadhi ya rununu huonyesha simu ilipopigiwa hivyo kusaidia kudhibiti mitandao ya uhalifu.
    24. Huduma ya simu tamba ni njia ya kujipatia riziki. Wapo raia walioanzisha biashara ya MPESA, na wengine ukarabati wa rununu zilizoharibika. Hili limepunguza makali ya uhaba wa nafasi za kazi nchini.

      Tanbihi
      1. Mtahiniwa anaweza kujadili upande mmoja, kwa mfano, hasara tu. Huyu atahitajika kufafanua kikamilifu angaa hoja 5 ili kukadiriwa vyema kimaudhui.
      2. Wapo watakaosema moja kwa moja kuwa simu tamba imeleta faida tu. Hawa pia wajadili angaa hoja 5 ili kukadiriwa vyema kimaudhui.
      3. Watakaojadili pande zote mbili sharti wafafanue angaa hoja 3 kuunga na 2 kupinga/au 3 kupinga na 2 kuunga, kisha waonyeshe msimamo wao.
      4. Kuna yule atakayejadili pande zote mbile bila kuonyesha msimamo. Huyu ni mtu baki  amepungukiwa kidogo
      5. Kaida nyingine zote za usahihishaji wa karatasi hii zizingatiwe.
  2. Hii ni insha ya methali. Kisa kidhihirishe maana ifuatayo:
    Usimpuuze mtu ambaye alikusaidia awali; au usimpuuze mtu ambaye unahitaji msaada wake ati kwa sababu amekufaa tayari na unahisi kwamba humhitaji tena. Huenda ukamhitaji mtu huyo baadaye.
    Au
    Usivipuuze au usividharau vitu au hali ambayo ilikufaa awali. Huenda ukavihitaji baadaye.
    Kisa kinaweza kudhihirisha hali zifuatazo:
    1. Mhusika ambaye ameishi mahali kwa muda (labda amepewa hifadhi na ndugu au familia) kisha anapofanikiwa anawadharau.
      Kisa kionyeshe hasara / tatizo linalotokana na kupuuza huku. Pengine mhusika anaweza kuhitaji msaada, japo kidogo, wa familia hii na kuona aibu kuomba.
    2. Mwajiriwa ambaye amefanya kazi katika kampuni fulani kwa muda, kisha anapopata kazi kwingine anajiuzulu kwa dharau. Wakati fulani patokee jambo linalomhitaji kupata barua kutoka kwa wakuu wa kampuni hiyo, kisha ahasirike kwa kuona aibu kuomba.
    3. Mwanafunzi ambaye baada ya kukamilisha masomo anatenda mambo kama vile kuwakosea walimu heshima, kuharibu mali ya shule, bila kuwazia kwamba atahitaji barua ya marejeleo kutoka kwa wakuu wa shule. n.k
    4. Mtu ambaye anakitelekeza kifaa chake kikuukuu kwa kununua kipya. Patokee wakati ambapo hicho kipya kimeharibika na hawezi kukitumia kile cha zamani kwa vile hakukitunza.

      Tanbihi
      1. Kisa kinahitajika kuonyesha hali mbili: kudharau na kuathirika.
      2. Wale ambao wataonyesha kudharau bila kuathirika watakuwa wamepungukiwa tu kimaudhui, hawajapotoka. Wakadiriwe ipasavyo kulingana na vigezo vya kutathminia (mwongozo wa kudumu).
      3. Wale ambao wataandika kisa kisichohusiana kabisa na methali ndio watakaokuwa wamepotoka kimaudhui. Hawa wawekwe katika kitengo kilichopendekezwa na vigezo vya kutathminia (mwongozo wa kudumu).
      4. Watahini wawe makini zaidi. Mtahiniwa anaweza kudokeza athari kwa neno, kirai kimoja, au sentensi tu.
        Athari pia inaweza kudokezwa kama tahadhari na mhusika mwingine katika hadithi, akamwambia yule anayedharau vitu au watu waliomfaa.
  3. Maneno kiini katika swali hili ni kudunda na matarajio. Hali inayodhihirika katika mdokezo huu ni wasiwasi au taharuki.
    Kisa kidhihirishe:
    1. Mhusika anayetarajia jambo.
    2. Jambo ambalo linatarajiwa - kwa mfano:
      1. kutangazwa kwa matokeo ya mtihani
      2. matokeo ya mashindano
      3. uchunguzi wa kiafya
      4. kukutana na rafiki ambaye mmetengana kwa muda
      5. majibu kwa rai au swali, kwa mfano: ombi la posa au ndoa
      6. tangazo la kizuizi cha ndoa kwenye harusi yake kanisani au msikitini
      7. kutawazwa kama kiongozi wa dini kama vile kasisi
      8. kuwasili katika nchi ngeni
      9. mwanzo wa safari kwenda nchi ngeni
      10. mwanzo wa mashindano au mbio fulani; mhusika anangojea kupulizwa kwa kipenga
      11. siku ya kwanza katika kidato cha kwanza, mhusika anangojea kuingia kwenye afisi kusajiliwa
    3. Baada ya kuandika kauli hii ya mwanzo:
      1. Mtahiniwa anaweza kurudi nyuma (kutumia mbinu rejeshi), akasimulia kisa hadi akafikia hali ambayo anatarajia jambo hili. Kwa mfano, mbinu rejeshi inaweza kuonyesha uchumba, pingamizi, kisha arusi ambapo anahofia kuwa huenda pakatokea mtu akaipinga ndoa hii. Anaweza pia kusimulia maisha yake shuleni, kufanya mtihani na sasa anatarajia kutangazwa kwa matokeo.
      2. Mtahiniwa anaweza kuandika kauli ya kuanzia, kisha akafululiza moja kwa moja kusimulia yaliyotokea baada ya jambo analotarajia msimulizi. Kwa mfano: anaweza kutangazwa kuwa mwanafunzi bora zaidi; kisha asimulie kuhusu maisha yake baada ya hayo.
      3. Msimulizi anaweza kuwa aliyohofia, kwa mfano, kupingwa kwa ndoa yake yametokea, upeo wa chini au mporomoko wa maisha yake ukatokea. Kisha asimulie masaibu yake hadi anapofikia hatua ya kujiokoa au kudidimia zaidi katika majonzi, n.k

        Tanbihi
        1. Mtahiniwa atakuwa amepotoka kimaudhui pale tu kitakosa kuoana na kianzio, hivyo kuandika yasiyohusiana na swali.
        2. Mtahiniwa akikosa kuanza kwa kauli aliyopewa lakini kisa chake kioane na kiini cha swali, atakuwa hajapotoka kimaudhui, amepungukiwa kimtindo. Akadiriwe kulingana na masimulizi yake.
        3. Atakayekosa kuanza kwa kauli hii, na kisa kisioane na kiini cha swali atakuwa amejitungia swali.
        4. Kwa vyovyote vile lazima pawe na jambo linalotarajiwa, na ambalo linaweza kuathiri mkondo wa usimulizi, ukaelekea nyuma au mbele. Mtahini asitarajie tu mbinu rejeshi.
        5. Kaida zote za usahihishaji wa karatasi hii zizingatiwe.
Join our whatsapp group for latest updates

Download Kenya Certificate Of Secondary Education(KCSE 2013) Kiswahili Karatasi ya Kwanza with Marking Scheme.


Tap Here to Download for 50/-




Why download?

  • ✔ To read offline at any time.
  • ✔ To Print at your convenience
  • ✔ Share Easily with Friends / Students


Get on WhatsApp Download as PDF
.
Subscribe now

access all the content at an affordable rate
or
Buy any individual paper or notes as a pdf via MPESA
and get it sent to you via WhatsApp

 

What does our community say about us?

Join our community on:

  • easyelimu app
  • Telegram
  • facebook page
  • twitter page
  • Pinterest