Kiswahili Paper 2 Questions and Answers - Nginda Girls Mock Examination 2023

Share via Whatsapp

Maagizo

  • Jibu maswali yote.
  • Majibu yote yaandikwe katika lugha ya Kiswahili


MASWALI 

  1. UFAHAMU (ALAMA 15)
    Soma makala yafuatayo kisha ujibu maswali yatakayofuata
    Baada ya biashara ya utumwa kupigwa marufuku katika karne ya kumi na tisa kule Marekani,watu weusi na wa rangi waliendelea kukabiliwa na dhuluma za kila namna. Walidhalilishwa na kuchukuliwa kama binadamu wa hadhi ya chini kuliko weupe. Sheria zilitumika kuweka mipaka ya maingiliano kati ya raia wa nchi moja. Weusi wangepatikana popote palipotengwa weupe wangechukuliwa hatua za kisheria.
    Katika usafiri wa umma, Mmarekani Mweusi alitakiwa kisheria kumpisha kiti Mmarekani mweupe ndani ya chombo cha usafiri. Aliyevunja sheria hii alitiwa mbaroni au kuhukumiwa kifungo pamoja na faini. Halikadhalika, alihatarisha maisha yake kwani angevamiwa na makundi ya wakereketwa kama vile ku klax klan (kkk); kundi ambalo lilitetea vikali udumishaji wa ubaguzi wa rangi.
    Hii ndiyo iliyomchosha mwanamke, Mmarekani Mweusi Rosa Lee Parks. Akajifunga kibwebwe kukaidi sheria dhalimu na kupigania mabadiliko ya jamii. Akakamia mabadiliko yaliyolenga kuleta usawa wa kijamii na haki kwa wote bila kubaguliwa.
    Mwanamke huyu aliyepewa lakabu ya ‘Mama wa Mapigano ya Haki za Kimsingi’ ni wa asili ya watumwa waliotwaliwa kutoka Afrika kwenda kutumikishwa na weupe katika mashamba yao kule Marekani. Alizaliwa Februari 14 mwaka 1913 huko Tuskegee, jimbo la Alabama. Masomo yake ya awali yalikwamizwa na maradhi pamoja na umaskini uliokabili familia yake. Hata hivyo baada ya ndoa yake na Raymond parks, manamo 1932, bwanake alimhimiza kwenda shuleni.
    Elimu aliyoipata Rosa pamoja na ushawishi wa mumewe ulimfungua macho kuhusu ubaguzi wa rangi katika jamii yake. Alijiunga na kundi la wanaharakati waliokuwa wakiwatetea watu weusi, pamoja na Suriama. Rosa alichukizwa na ubaguzi uliotamalaki katika jamii yake. Alikirihiwa na sheria zilizoigawa jamii katika msingi wa rangi huku zikimtukuza mtu mweupe na kumtweza mweusi.
    Kilele cha kuudhika kwa Rosa kilikuwa pale Desemba mosi 1955 akiwa ndani ya basi, abiria mweupe alitokeza na kumwamuru Rosa ampishe kiti alichokuwa amekalia. Miguu ya Rosa ilikuwa inauma. Hakuona ni kwa nini asimame ampishe abiria mwenzake ambaye alikuwa amelipa nauli sawa na yake. Rosa alikuwa amechoka na vitimbi vya kubaguliwa na kuchukuliwa kama mwananchi wa hadhi ya chini. Alikataa katakata kumpisha abiria huyu kiti.
    Rosa alijua fika kuwa tendo lake la maasi lingempeleka kuhukumiwa jela, kutozwa faini, kutishwa, kuumizwa au kuuliwa na makundi ya wakereketwa weupe. Lakini yote haya aliyaweka pembeni ili atetee haki na usawa katika jamii.
    Kwa uasi huo, Rosa alikuwa amekiuka sheria. Alitiwa mbaroni na kuhukumiwa kifungo na faini ya dola nne za Kimarekani; kiasi kilichokuwa kikubwa sana wakati huo. Hukumu hii ikazua maandamano dhidi ya sheria za ubaguzi. Umma ukiongozwa na kasisi wa Kibaptisti Martin Luther King uliungana na Rosa kutetea haki na usawa. Umma ukagomea mabasi kwa muda wa siku 381 huko Montgomery, Alabama. Migomo hii, pamoja na maandamano yakaishurutisha serikali kuanza juhudi za kuleta usawa na haki kwa wote Marekani. Juhudi hizo zilizoanzishwa na kuasi kwa Rosa zikafikia upeo wake mwaka 1964. Mwaka huo, serikali ya kitaifa ya Marekani ikapitisha sheria iliyopiga marufuku ubaguzi wa rangi.
    Bi Rosa Lee Parks, aliyekufa akiwa na umri wa miaka 92, ni kielezo cha nguvu fiche za wanawake ambazo zinaweza zikatumika kutetea hadhi, haki na usawa wa wote waliokandamizwa. Atakumbukwa kama mtu aliyepigania binadamu kuwa huru na kupewa hadhi kama binadamu bila kubaguliwa. Alikuwa amechoshwa na unyanyasaji na kufedheheshwa. Silaha pekee aliyokuwa nayo ni uasi kwa njia ya amani. Silaha iliyotokeza kuwa na nguvu zaidi kuliko mtutu wa bunduki. Hili ni funzo kwa watu waliobaguliwa, hasa wanawake kote duniani wanaoendelea kukandamizwa na tamaduni zinazotukuza ubabe wa kiume. Bila shaka hao wanaweza kumwiga Rosa na kubadilisha hali zao kama alivyoweza Rosa.
    Maswali 
    1. Biashara ya utumwa ilipigwa marufuku lini kule Marekani? (alama1)
    2. Kwa nini Rosa Parks alipewa lakabu ya “Mama wa Mapigano ya Haki za Kimsingi” (alama 2)
    3. Fafanua dhuluma ambazo Wamarekani Weusi walikabiliana nazo kulingana na taarifa hii. (alama 4)
    4.  
      1. Onyesha matokeo ya matendo ya Rosa kwa jamii ya Wamarekani na ulimwengu mzima. (alama 2)
      2. Ni funzo gani unalolipata kutokana na maisha ya Rosa? (alama 1)
    5. Je,ni kweli kuwa silaha aliyokuwa nayo Rosa Parks ilikuwa na nguvu kuliko mtutu wa bunduki? Tetea jibu lako. (alama 2) 
    6. Eleza maana ya maneno yafuatayo kama yalivyotumika katika taarifa (alama 3)
      1. Nguvu fiche
      2. Wakereketwa
      3. Ubabe wa kiume
  2. UFUPISHO (ALAMA 15)
    Sisi vijana wa Kenya inatupasa tuwajibike kufanya kazi kwa bidii na kwa dhati ya mioyo yetu ili tuweze kupata ufanisi na uwezekano wa kuinua nchi yetu changa katika kiwango cha juu. Tukumbuke, “Ajizi ni nyumba ya njaa”. Kwa hivyo basi haifai kulaza damu ikiwa matatizo nchini mwetu yametunzonga. Lazima tufanye kazi kwa busara, adabu njema na jitihada kwa moyo mmoja. Sharti tutilie maanani zaidi elimu ya vijana na watu wazima, kilimo, uchumi na amani katika nchi yetu. Tunahitaji taifa lenye watu walioelimika kwani bila elimu itakuwa vigumu sana kuweza kutekeleza mipango mbalimbali ya maendeleo. Tupende tusipende lazima tuzidishe mazao mashambani kwani kila kukicha idadi ya watu inaongezeka. Ni sharti tuweze kujitosheleza katika vyakula. Zaidi ya hayo pia lazima tujishughulishe na biashara ambapo kwa sasa ni Wakenya wachache sana ambao wanatambua umuhimu wa biashara. Wengi ni wale wenye mawazo ya kwamba lazima kila mmoja aajiriwe maishani. Yatupasa tujitahidi kuleta uchumi katika mikono ya wananchi wa Kenya badala ya kuwaachia wengine ambao hawahusiki.
    Mafunzo tunayopata majumbani, shuleni na hata katika jamii, lazima yatuwezeshe kutambua mbinu za kupitia. Tunahitaji elimu tambuzi ambayo itamfanya Mwanakenya kujua wajibu wake katika jamii. Tumesinywa na elimu pumbao; inayotupumbaza na kutufanya tusiwe mbele. Sisi vijana tukiwa viongozi wa siku zijazo tuwe kielelezo chema kwa wengine. Watu lazima washirikiane na kufikiria kwamba wao ni wamoja, “utengano ni uvundo”. Lugha ya taifa ndicho chombo pekee ambacho kinatuunganisha na kuweza kutuwasilishia mapendekezo, mawaidha na hisia zetu. Kukosa ndiko kibinadamu, wakati tunapokosea ,lazima tukubali tumekosea na kufanya masahihisho mara moja kwani, “usipoziba ufa utajenga ukuta”. Tusikasirike kwa sababu tumesahihishwa makosa yetu na mwenzetu. Lazima tujitoe mhanga na kupigania nchi yetu tukiwa wazalendo halisi.
    Sisi tukiwa vijana sharti tujishughulishe na kuyaangalia matatizo ya nchi, pia kutafuta njia za kutatua matatizo hayo. Siku zote tutekeleze nidhamu shuleni na majumbani mwetu. Ili watu waweze kuishi maisha bora na kuwa na maendeleo, amani na upendo, lazima tuwe na bidii, ushirikiano mwema na kuchagua viongozi wenye mioyo ya maendeleo. Tukiwa viongozi ambao hawajishughulishi na maendeleo,basi tutabaki nyuma kama mkia siku zote. Bahati mbaya ni kwamba wananchi wengi siku hizi huchagua viongozi wao kwa kufuata ukoo ama kwa utajiri wake. Kwa hivyo basi, tuchagueni viongozi ambao wanatuletea ufanisi badala ya wanaotokana na nasaba kubwa au utajiri.
    Maswali 
    1. Fupisha aya mbili za mwanzo.(Maneno 70-75) ( alama 10,1 ya mtiririko)
    2. Dondoa hoja muhimu katika aya ya mwisho.(Maneno 30-35) (alama 5, 2 za Utiririko)
  3. MATUMIZI YA LUGHA (ALAMA 40)
    1. Taja sauti zifuatazo:
      1. Kikwamizo sighuna cha ufizi (alama 1)
      2. Nusu irabu ya kaakaa gumu (alama 1)
    2. Kwa kutoa mifano , eleza tofauti kati ya silabi wazi na silabi funge. (alama 2)
    3. Ainisha mofimu katika neno: (alama 3)
      Atamnywea
    4. Ainisha vitenzi katika sentensi hii. (alama1)
      Wanafunzi walikuwa wanakariri mashairi
    5.  
      1. Eleza maana ya ngeli. (alama1)
      2. Neno tembo linaweza kuwekwa katika ngeli mbili tofauti, zitaje. (alama 2)
    6. Andika katika hali ya ukubwa wingi (alama 2)
      Mzee huyu ana wake wengi.
    7. Yakinisha sentensi ifuatayo. (alama 2)
      Hawakuwa wakicheza wala kuimba.
    8. Andika kinyume cha sentensi ifuatayo. (alama 1)
      Tabasamu alijenga nyumba ya babu.
    9. Tunga sentensi moja yenye masharti yasiyowezekana. (alama 1)
    10. Andika katika msemo wa taarifa. (alama 2)
      “Nimeenda kumtembelea nyanyangu. Hatujaonana tangu mwezi jana,” mjukuu alisema
    11. Kwa kutoa mifano, eleza matumizi mawili tofauti ya alama ya vifungo. (alama 2)
    12. Tunga sentensi yenye muundo ufuatao. (alama 4)
      KN(N+S ̅) +KT(T+RH+RE)
    13. Tumia ni katika sentensi moja kuleta dhana ya kitenzi na kielezi. (alama 2)
    14. Onyesha aina za shamirisho katika sentensi ifuatayo. (alama 3)
      Watoto wanalipiwa karo kwa hundi na wazazi wao
    15. Eleza maana mbili za sentensi hii. (alama 2 )
      Njoki amkimbilia Fatuma
    16. Tunga sentensi mbili kutofautisha vitate hivi kimaana. (alama 2) 
      1. Landa
      2. Randa
    17. Tumia kirejeshi ‘o’ tamati katika sentensi ifuatayo. (alama 2)
      Cheo ambacho amepewa ni kile ambacho anakitaka.
    18. Iandike sentensi upya kulinga na maagizo. (alama 2)
      Mwanariadha mmoja tu ndiye aliyefuzu katika mbio hizo. (Tumia hakuna na ila)
    19. Mwanafunzi ni kwa mwanagenzi, bendera ni kwa _________________ na _____________ ni kwa hekima. (alama 2)
  4. ISIMU JAMII (ALAMA 10)
    “….watu wa kaunti ya Makueni wamesahaulika kabisa. Ningependa kuelezwa kinagaubaga kama hawa ni Wakenya au la. Order! Order! Mheshimiwa Tata.
    La! Tumekuwa marginalized kwa muda mrefu sana…”
    1. Hii ni sajili gani? (alama 2)
    2. Eleza sifa nane za sajili iliyotajwa. (alama 8)


MWONGOZO 

  1. UFAHAMU
    1. katika karne ya kumi na tisa. (1x1)
    2.  
      1. alijifunga kibwebwe kukaidi sheria dhalimu
      2. Alipigania mabadiliko ya kijammii yaliyolenga kuleta usawa wa kijamii na haki kwa wote bila kubaguliwa (2x1=2)
    3.  
      1. kumpisha kiti Mmarekai Mweupe ndani ya chombo cha kusafiria.
      2. Kuchukuliwa kama binadamu wa hadhi ya chini
      3. Kutiwa mbaroni
      4. Kuhukumiwa kifungo pamoja na faini
      5. Kutishwa
      6. Kuumizwa
      7.  Kuuliwa na wakereketwa weupe (zozote 4x 1=4)
    4.  
      1. Matokeo
        1. Serikali kuanza juhudi za kuleta usawa na haki kwa wote nchini Marekani
        2. 1964, serikali ya kitaifa ya marekani ikapitisha sheria iliyopiga marufuku ubaguzi wa rangi (2x1=2)
      2. Funzo
        1. Wanawake wana nguvu fiche ambazo zinaweza kutumika kutetea hadhi, haki na usawa wa wote wanaokandamizwa
        2. Binadamu anafaa kukataa kubaguliwa na kuchukuliwa kama mwananchi wa hadhi ya chini
        3. Penye nia pana njia (hoja yoyote 1x1=1)
    5. Ndio
      Ililazimisha serikali kuanza juhudi za kuleta usawa na haki kwa wote ( jibu 1, sababu 1 2x 1=2)
    6.  
      1. Nguvu fiche- nguvu ambazo hazijavumbuliwa/ hazijatambuliwa
      2. wakereketwa - uasi kwa njia ya amani/ watetezi/ wanaharakati/wapiganiaji haki.
      3. ubabe wa dume - taasubi ya kiume, hali ya wanaume kuwadunisha/kuwadharau/ kuwadhalilisha wanawake
  2. UFUPISHO
    1.  
      1. tuwajibike kufanya kazi kwa bidii na dhati ya moyo
      2. haifai kulaza damu ikiwa matatizo nchini mwetu yametuzonga
      3. lazima tufanye kazi kwa busara, adabu njema na jitihada.
      4. tutilie maanani elimu ya vijana na watu wazima, kilimo, uchumi na amani
      5. tuzidishe mazao mashambani ili kujitosheleza kivyakula
      6. Tujishughulishe na biashara
      7. Tujitahidi kuleta uchumi katika mikono ya wananchi
      8. Tuwe na elimu tambuzi na sio elimu pumbao
      9. Vijana wawe kielelezo chema
      10. Watu washirikiane
      11. Tunapokosea tukubali kusahihishwa.
      12. tuwe wazalendo halisi (hoja zozote 9x1=9, ut - 1)
    2.  
      1. Tutekeleze nidhamu.
      2. Waishi maisha bora
      3. wawe na amani na upendo
      4. Tuwe na bidii
      5. Wawe na ushirikiano mwema
      6. Wachague viongozi wenye mioyo ya maendeleo.
      7. Wachague viongozi ambao wataleta ufanisi (hoja zozote 4x 1 =3, ut 1)
  3. MATUMIZI YA LUGHA (ALAMA 40) 
    1.  
      1. /s/
      2. /y/ ( 2x 1)
    2. Silabi wazi ni silabi zinazoishia kwa irabu
      ba, ma
      silabi funge ni silabi zinazoishia kwa konsonanti
      muk- / mu – k -
      dak- / da-k-
      m- ti,
      n-zi,
      (maelezo ½ , mfano ½ 4x ½ = 2)
    3. a - ta - m - nyw - e - a
      a- Nafsi/ngeli/mtenda/kiima/yeye/
      ta - Wakati
      m- Mtendewa/ nafsi /Shamirisho/ yambwa
      nyw - Mzizi/ Shina
      e - Kauli
      a- Kiishio/kauli ya kutenda (lazima atenge viambishi) (6x ½ =3)
    4.  
      1. walikuwa- kitenzi kisaidizi/ (Ts)
      2. wanakariri- kitenzi kikuu (T) (2 x1)
        au
        walikuwa wanakariri - kitenzi sambamba ( 1)
    5.  
      1. Ni uainishaji/upangangaji( makundi ya nomino) wa nomino kutegemea sifa zinazofanana kisarufi (1x1= 1)
      2. A-WA
        I-I (2x1 = 2)
    6. Majizee haya yana majanajike mengi (2/0)
    7. Walikuwa wakicheza na kuimba
      walikuwa wanacheza na kuimba. ( yoyote 2/0)
    8. Tabasamu alibomoa/jengua nyumba ya babu ( 1/0)
    9. Tanbihi - mwanafunzi atumie kiambishi ngali/ngeli katika senstensi ( 1x 1)
    10. Mjukuu alisema kuwa/kwamba alikuwa ameenda kumtembelea nyanyake kwani/kwa sababu/ kwa kuwa hawakuwa wameonana tangu mwezi uliotangulia (alama 1x2=2)
    11.  
      • Kutoa maelezo zaidi kuhusu neno/maneno yaliyotangulia
      • hutumiwa katika mahojiano/mazungumzo au
      • hutumiwa katika mahojiano/mazungumzo au maandishi ya kitamthilia kufungia ufafanuzi 2x1=2
    12. Mwalimu aliyefika jana alitembea kando ya barabara haraka sana.
      KN N S KT - T KH KE (KN – 2/0, KT 2/0=4)
    13. Mtoto aliyefika shuleni ni mkorofi sana ( kadiria majibu ya mtahiniwa 2X1=2)
    14. karo –sh.kipozi
      Hundi –sh. Ala
      Watoto- sh.kitondo (3 x 1 = 3)
    15.  
      • alikimbia kwa niaba ya Fatuma/ alikimbia kwa sababu ya Fatuma
      • alimlaki Fatuma
      • Alikimbia kuelekea kwa Fatuma ( za kwanza 2 x 1= 2)
    16. Landa – fanana
      Randa - kifaa cha seremala cha kulainisha mbao ( 2x 1=2)
    17. zurura ovyo ovyo
      1. apewacho
      2. akitatakacho (2x1=2)
    18. Hakuna mwanariadha aliyefuzu mbio hizo ila mmoja. (2/0)
    19. bendera – beramu
      hekima – busara ( 2x 1)
  4. SEHEMU YA D : ISIMU-JAMII
    1. sajili ya bunge 1x2=2 
    2.  
      1. Hutumia lugha ya kingereza au Kiswahili/ ku
      2. Hutumia lugha yenye ucheshi
      3. Msamiati wa heshima na adabu hutumiwa
      4. Msamiati maalum kuhusu bunge hutumiwa vipengele muhimu katika katiba hurejelewa ili kuunga mkono jambo Fulani
      5. lugha rasmi/sanifu
      6. kauli ndefundefu
      7. usemi halisi
      8. kurejelea vifungu vya sheria ya bunge na katiba ya taifa
      9. lugha ya majibizano (za kwanza 8x1) (lazima atolee mfano ama aeleze)
Join our whatsapp group for latest updates

Download Kiswahili Paper 2 Questions and Answers - Nginda Girls Mock Examination 2023.


Tap Here to Download for 50/-




Why download?

  • ✔ To read offline at any time.
  • ✔ To Print at your convenience
  • ✔ Share Easily with Friends / Students


Get on WhatsApp Download as PDF
.
Subscribe now

access all the content at an affordable rate
or
Buy any individual paper or notes as a pdf via MPESA
and get it sent to you via WhatsApp

 

What does our community say about us?