Dhamira na Maudhui Katika Chozi la Heri - Mwongozo wa Chozi la Heri

Share via Whatsapp


Dhamira ya mwandishi

Kwa mujibu wa kamusi ya Kiswahili sanifu, neno Dhamira lina maana ya kusudi wazo kuu au ujumbe mkuu wa mwandishi. Dhamira pia ni lengo la mwandishi anapoandika kazi. Kwa hivyo tunapoangazia dhamira ya mwandishi tutajibu swali hili: Je, nia/lengo/kusudi la mwandishi huyu ni gani? Assumpta K. Matei alidhamiria yafuatayo alipokuwa akiandika Riwaya ya Chozi la Heri.

Kuupiga vita ukabila.

Tumepata katika Riwaya ukabila ukiwa chanzo cha migogoro. Watu wengi wameathirika vibaya kwa kuwa watu wa kabila tofauti na lao waliwabagua, kuwaumiza au hata kuwafukuza makwao hata kama walikuwa majirani kwa miaka mingi. Kwa mfano mamake Mwanaheri(Subira) alilazimika kuondoka nyumbani bila hiari na kutengana na familia yake kwa kuwa alibaguliwa, akafitiniwa na hata kulaumiwa kwa asiyoyatenda. Alifanyiwa mambo haya yote kwa kuwa Subira alikuwa ametoka kwenye jamii ya Bamwezi naye babake Mwanaheri alikuwa wa jamii tofauti. Kila mara Subira alikuwa akiitwa na mama mkwe muki yaani "huyo wa kuja". Subira alidhhoofika kiafya kwa kutengwa na aliodhania kuwa wa aila yake. Hatima ya mambo haya ilikuwa ni Subira kujitoa uhai.

Kuvipiga vita 'vita vya baada ya kutawazwa'

Vita vya baada ya kutawazwa vilikuwa sababu ya watu kuacha makwao na kuwa wakimbizi wa ndani kwa ndani. Wahafidhina wengi waliathirika sana. Familia zikatengana na watu wakapoteza wapendwa wao na mali zao walizokuwa wametafuta kwa jasho lao wenyewe. Mwandishi huyu ana nia ya kuwahamasisha raia kujitenga kabisa na machafuko hayo kwani huzaa shida na dhiki kuu.

Kuufichua uozo ulio katika jamii.

Katika Riwaya ya Chozi Ia Heri, mwandishi kupitia kwa wahuslka wake na mtindo wake wa uwasilishaji, amefaulu kuunchu uozo. Uozo ni mambo yote mabaya yanayokinzana na maadlli. Uozo huu ni pamoja na: biashara haramu ya aw kulevya, utekaji nyara wa watoto, kubakwa kwa wasichana, kupashwa tohara kwa wasichana, ndoa za mapema kwa wasichana wadogo, uasherati na uavyaji mimba, matumizi ya mihandarati, Wizi na uporaji wa mali za wenyewe, mauaji ya halaiki, uharibifu wa mazingira, ukabila, ubinafsi wa viongozi, ufisadi nk. Mambo haya yote yamefichuliwa kuwa yapo katika jamii na kuwa hayafai kabisa kwani ni kinyume na maadili ya mwanadamu.

Kuonyesha umuhimu mapenzi katika ndoa na familia.

Mwandishi huyu ameonyesha wazi kuwa taasisi ya ndoa na familia inafaa kujengwa katika mapenzi/upendo. Familia ya Lunga ilisambaratishwa na ubinafsi wa Naomi. Naomi alimwacha mume wake na watoto wao watatu- Umu, Dick na Mwaliko. Wana hawa walipata taabu kwa namna mbalimbali kwani baada ya baba yao kuiaga dunia kijakazi Sauna alipata nafasi ya kuwateka nyara Dick na Mwaliko na kuwauza kwa wateja wake. Watoto hawa walibahatika tu kwa kudura za Mwenyezi wakapata wazazi wengine wenye utu na mapenzi wakawalea na mwishowe wakawa watu wa kutegemewa. Kwa hivyo, tasisi hii ya ndoa inafaa kujikita katika upendo.



Maudhui.

Maudhui ni jumla ya mawazo yote yanayozungumzwa pamoja na mtazamo wa mwandishi juu ya mawazo hayo. Hujumuisha mawazo na mafunzo tofauti yaliyomsukuma

1. Maudhui ya migogoro

Migogoro ni mivutano na mikinzano mbalimbali katika kazi ya fasihi. Migogoro huweza kuwa kati ya wahusika, familia zao, matabaka tofauti, nyadhifa mbalimbali, kiuchumi, nafasi katika jamii au hata kisiasa. Aina za migogoro katika riwaya hii.

  1. Kuna mgogoro kwenye familia ya Mzee Mwimo Msubili, kwa sababu familia yake ilikuwa kubwa na hakuitosheleza kwa chakula. Uk 9,"Wingi wa vinywa vya kulishwa ulizua uhasama, migogoro na hata uhitaji mkubwa "
  2. Mgogoro wa kijamii unajitokeza baada ya mkoloni kupuuza sera za Mwafrika. Uk 10,"Hatua ya mkoloni ya kupuuza sera za Mwafrika za umiliki wa ardhi na kuamua kujumuisha pamoja ardhi iliyomilikiwa na mtu binafsi na kuuidhinisha umiliki huu kwa hatimiliki, ilivuruga mshikamano wa kijamii "
  3. Kulijitokeza mgogoro shuleni wakati Ridhaa aliitwa 'mfuata mvua',na kutengwa na wenzake. Walimwona kama mwizi. Uk 10,"Wewe ni mfuata mvua. Hatutaki kucheza nawe. Umekuja hapa kutushinda katika mitihani yote. Wewe ndiwe unayetuibia kalamu zetu "
  4. Ridhaa alijipata katika hali ya mgogoro na nafsi yake. Uk 12,"Miguu yake sasa ilianza kulalamika pole pole parafujo za mwili wake zililegea, akaketi juu ya ya wapenzi wake. Baada ya muda wa mvutano, wa hisla na mawazo, usingizi ulimwiba.
  5. Kulikuwa na mgogoro uliosababishwa na wanasiasa, juu ya nani atakaye kuwa kiongozi wa jamii, kati ya mwanamke mwananume. Uk 19,"MijadaIa hii ilizua na kukuza migogoro isiyomithilika "
  6. Mgogoro mwingine ulijitokeza kati ya raia na wanapolisi, wakiwa katika harakati zao za kuweka amani. Uk 19,"Mchezo wa polisi kukimbizana na raia ulianza katika mchezo huo mamia ya roho zisizo na hatia zilisalimu amri chini ya pambaja za risasi na mapigo ya rungu, vitoa machozi navyo vikafanya kazi barabara.
  7. Nyamvula anajikuta katika mgogoro wa nafsi yake, wakati ambapo imani yake inakinzana na kazi ya kuwa askari. Uk 62,"Kulingana na Nyamvula, kuwa askari wa vita kulikinzana na imani yake, hasa kwa vile Nyamvula alisema ni born again. Mwangeka alimsisitizia kuwa kulinda usalama si sawa na kuua " Katika ukurasa wa 38 Tila anaitaja migogoro kadha katika Tamthilia ya Hussein. Tamthilia hii ya Mashetani ninayorejelewa ina migogoro mingi sana kama: migogoro ya kisiasa, kiuchumi, na pia ya kijamii.
    "Tila: Nadhani umesahau baba. Suala hili ulisema limeshughulikiwa katika kazi za kifasihi kama vile Mashetani, ile tamthilia ya Hussein inayoisawiri migogoro ya kisiasa, kiuchumi na kijamii ya baada ya ukoloni lsitoshe, mwalimu alitaka tu kuonyesha kwamba upo uhusiano kati ya mfumo wa kiuchumi na mfumo wa kisiasa alituambia kwamba mfumo wa kiuchumi hudhibitiana na mfumo wa kisiasa. Utawala huteuliwa makusudi kuendeleza mfumo uliopo wa kiuchumi kwa maslahi ya watawala na tabaka ambalo linazimiliki nyenzo za uzalishaji mali "

2. Umasikini

Umaskini ni ukata. Ni hali ya kukosa fedhamali nk. Tunapata kuwa waafrika wanajikuta katika hali ya umasikini;

  1. Uk 7,"Waafrika waliobahatika kuwa na makao yao binafsi walipata sehemu ambazo hazingeweza kutoa mazao yenyewe; na bila shaka hali yao iliweza kutabirika; kuvyazwa kwa tabaka la wakulima wadogowadogo, maskini, wasio na ardhi " Uk 25,"Nyinyi ndio vikaragosi wanaotumiwa na wasaliti wa nia zetu kuendelea kutudidimiza kwenye lindi hili la ukata "
  2.  Ridhaa pia anajikuta kwenye lindi la umaskini baada ya mali yake yote kuchomwa, ikiwemo familia yake. Uk 1,"Ridhaa alisimama kwa maumivu makali, mikono kairudisha nyuma ya mgongo wake uliopinda kwa uchungu. Macho yake yaliyotanda ukungu alikuwa kayatunga juu angani, akitazama wingu la moshi lililojikokota kwa Kedi na mbwembwe; wingu lililomwonyesha na kumkumbusha ukiwa aliozaliwa nao na ambao alihofia kuwa angeishi na kuzikwa nao"
  3. Tunapata pia kuwa watu wengi wanaiaga dunia wakijaribu kujikomboa kutokana na hali hii ya ukata, wanapoenda kuchota mafuta kwenye lori ambalo limebingirika kisa na maana alienda kuwaokoa watu ambao walikuwa wakipora mafuta kutoka kwenye lori, ambalo lilikuwa limebingiria lnasemekana kuwa umaskini uliwasukuma watu hawa kuchukua kisichokuwa haki yao!"

3. Ushirikina

Hii ni hali au tabia ya watu kuamini mambo ya utamaduni ambayo mara nyingi, yanajihusisha na uchawi.

  1. Ridhaa anaposikia milio ya bundi, anaamini kuwa milio hii ina maana iliyofichika. Uk 1,"Anakumbuka mlio wa kereng'ende na bundi usiku wa kuamkia siku hii ya kiyama. Milio hii ndiyo iliyomtia kiwewe zaidi kwani bundi hawakuwa wageni wa kikaida katika janibu hizi " Uk 2,"Ninashangaa ni vipi daktari mzima hapo ulipo unajishughulisha na mambo ya ushirikina.

4. Ndoa

Haya ni maafikiano rasmi baina ya mume na mke ili waweze kuishi pamoja.

  1. Kuna ndoa kati ya Ridhaa na Terry. akamgeukia mumewe tena na kusema, ...laiti Ridhaa angalijua kwamba hii ndiyo mara yake ya mwisho kuzungumza na mpenzi mkewe. Tunapata kuwa Ridhaa ana mwoa Terry, uk ll "Baadaye aliamua kuasi ukapera, akapata mke, Terry "
  2. Mwangeka alikuta na Lily Nyamvula katika Chuo kikuu na kumwoa. Walibarikiwa na mtoto mmoja kwa jina Becky. Ndoa hii haikudumu kwani Lily na Becky waliangamia kwenye janga la moto.
  3. Baada ya ndoa ya mwanzo kusambaratika, Mwangeka alimwoa Apondi. Walibarikiwa na mwana wa kiume kwa jina Ridhaa.
  4. Mwangemi alimwoa mwanamke kwa jina Neema. Hawakufaulu kupata mwana wao kindakindaki japo walipanga mwana wao kwa jina Mwaliko.
  5. Kangata alikuwa na mke wake kwa jina Ndarine. Walibarikiwa na wana wafuatao. Lunga Kiriri, Lucia Kiriri na Akelo Kiriri. Lucia Kiriri — Kangata-,-alikuwa ameolewa katika ukoo wa Waombwe ambao awali walikuwa maadui sugu wa ukoo wa Anyamvua. Ndoa hii ilipata pingamizi sana kutoka kwa ukoo mzima lakini kutokana na Msimamo imara wa Kangata ndoa hii ilisimama. Watu wa ukoo wa kina Kangata walishangaa ni kwa nini mwana wao akaozwa kwa watu ambao huvaa nguo ndani nje na pia huzaa majoka ya mdimu ambayo ni machoyo kupindukia.
  6. Kaizari alikuwa na mke kwa jina Subira. Walibarikawa na mabinti wawili, Lime na Mwanaheri.
  7. Lunga alikuwa na mke kwa jina Naomi. Walikuwa na wana watatu, Umu, Dick na Mwaliko. Ndoa hii haikudumu kwani Naomi alimwacha Lunga na kwenda mjini alikokuwa shangingi kwelikweli.
  8. Pete na Fungo- tunaelezwa kuwa Pete alipoingia darasa Ia saba alipashwa tohara nao wajombake wakapokea posa na baadaye mahari kutoka kwa buda mmoja kwa jina Fungo aliyemuoa kama bibi wa nne. Ndoa hii haikudumu kwani Pete alihiari kumwacha baba huyu.

5. Mauti

Hii ni hali ya kuiaga dunia wahusika wengine wanakutana na janga hili la mauti, ilhali wengine walio wakuu hawapatani nalo.

  1. Uk 2;Mamake Ridhaa aliiaga dunia na Ridhaa anakumbuka jinsi mamake alivyokuwa akimwambia "Moyo wa Ridhaa ulipiga kidoko ukataka kumwonya dhidi ya tabia hii ya kike ya kulia Pindi mtu akabiliwapo na vizingiti ambavyo ni kawaida ya maisha, ukamkumbusha maisha maneno ya marehem mama yake siku za urijali wake "
  2. Terry na wana wake wanakumbana na janga la kifo baada ya kuchomwa wakiwa ndani ya nyumba yao. Uk 3,"uuuui!uuuui!jamani tuisaidieni!uuuui!uuuui! Mzee Kedi usituue!sisi tu majirani!maskini wanangu!maskini mume wangu!"
  3. Tunapata pia kuwa Kangata na mkewe Ndarine wanakumbana na mauti. Uk 66; "Miaka mitano imepita. Kangata na mkewe Ndarine wameipa dunia kisogo "
  4. Baada ya Lunga kuachwa na mkewe, alikazana kuwalea watoto wake lakini baadae akaiaga dunia. Uk 82; "Kabla ya mwisho wa mwaka huo, Lunga alifariki na kuwaacha watoto wake mikononi mwa kijakazi wake "

6. Ukoloni mambo leo

Ukoloni mamboleo ni zao la uongozi mbaya. Viongozi waanzilishi wa mataifa yaliyopata uhuru hawakuzua sera na mikakati mwafaka ya kuhakikisha nchi zao zimepata kujisimamia kiuchumi. Katika Chozi la Heri, Waafrika wenyewe wanajifanya wakoloni juu ya waafrika wenzao, ambao wako chini yao kitabaka au kisiasa kwa mfano

  1. katika ukurasa wa 5,mashamba ya Waafrika yananyakuliwa na watu binafsi baada ya wakoloni kwenda, nao waafrika wanawekwa mahali pamoja ili kuishi katika hali ya ujamaa "Lakini baba, wewe siwe uliyeniambia kuwa mashamba ya Theluji nyeusi yalikuwa milki ya wakoloni?na sasa yanamilikiwa na nani? Si mwana wa yule mlowezi maarufu ambaye wewe hunitajia kila mara? Maekari kwa maekari ya mashamba katika eneo la kisiwa bora yanamilikiwa na nani? Si yule myunani aliyewageuza wenyeji kuwa maskwota katika vitovu vya usuli wao?"
  2. Katika ukurasa wa 24 tunapata kuwa vijana wanakufa kwa mitutu ya bunduki wanapojaribu kujikomboa kutokana na ukoloni wa Mwafrika. Walipigania uhuru wa tatu, ambao ni ukombozi kutokana na uongozi wa Mwafrika "Baada ya muda mfupi, vifua vyao vilikabiliana na risasi zilizorashiwa vifua hivyo kama marashi, vifua vikawa havina uwezo dhidi ya Shaba, vijana wakaanguka mmoja baada ya mwingine, wame kufa kifo cha kishujaa, wamejitolea mhanga kupigania uhuru wa tatu"

7. Ukoloni mkongwe

Huu ni ukoloni uliokuwa wa Waingereza, kabla ya Afrika kupata uhuru.

  1. Tunapata kuwa mkoloni anapata fursa ya kuendeleza kilimo katika sehemu za mashamba ya Waafrika zilizotoa mazao mengi. Uk 7, "Mustakabali wa ukuaji wetu kiuchumi uligonga mwamba wakati sheria ya mkoloni ilipompa mzungu kibali cha kumiliki mashamba katika sehemu zilizotoa mazao mengi. Ukengeushi wa ardhi ukatiliwa muhuri, umilikajia wa ardhi na Mwafrika katika sehemu hizi ukapigwa marufuku; si mashamba ya chai, si ya kahawa yote yakapata wenyeji wageni dau la mwafrika likagonga jabali.
  2. Katika ukurasa wa 7 tunasoma; "Waafrika waliobahatika kuwa na makao yao binafsi walipata sehemu ambazo hazingeweza kutoa mazao yenyewe; na bila shaka hali yao iliweza kutabirika; kuvyazwa kwa tabaka la wakulima wadogowadogo, maskini, wasio na ardhi. Nadhani unaweza kukisia hali ilivyokuwa kwa familia nyingi za kiafrika. Kama vile baba Msumbili alivyokuwa akisema, jamii yetu iligeuka kuwa hazina kuu ya wafanyakazi ambamo wazungu wangeamua kuchukua vibarua kupalilia mazao yao" Tunaona kuwa wazungu bado waliwatumia waafrika kama wafanyakazi mashambani 'mwao',ambayo walinyakua kutoka kwa waafrika.

8. Utamauishi

Hii ni hali ya wahusika kukata tamaa katika maisha yao au katika jambo fulani.

  1. Wakulima wanakata tamaa baaa ya kutopata waliyotarajia baada ya kupata mazao yao. Uk 6; "Sijui ni kwanini hatujaweza kujisagia kahawa au chai yetu itakuwaje mbegu ziwe zetu, tuchanike kukuza zao lenyewe, kasha tumpelekee mwingine kwenye viwanda vyake, aisage tuuzia hiyo hiyo kahawa na chai kwa bei ya kukatiha

9. Elimu

Haya ni mafunzo yanayotolewa na jamii kwa watu wake. Elimu yaweza kuwa rasmi na kutolewa darasani, au iwe sio rasmi ambayo hutolewa kwenye mazingira ya kawaida yasiyo kuwa ya shuleni au darasani.

  1. Katika ukurasa wa 10; Ridhaa aliungana na vijana wengine kwenda shuleni kupata elimu "Ridhaa alikuwa mmoja wa waathiriwa wa hali hii. Anakumbuka jinsi siku ya kwanza shuleni alivyotengwa na wenzake katika mchezo wao wa kuvuta, mchezo wa kusukuma vifuniko vya chupa ya soda kwa ncha za vidole vyao "Uk 11; "
  2. Ridhaa alipea kwenye anga za elimu, akabisha kwenye milango ya vyuo, akafika kilele cha ufanisi alipohtimu kama daktari "
  3. Mwaliko pia anaendeleza masomo yake hadi akafikia kiwango cha Chuo kikuu. Uk 149; " Hata alipohitimu masomo yake ya kidato cha nne na kujiunga na Chuo kikuu kusomea shahada ya isimu na lugha, Mwangemi na Neema walijua kuwa juhudi zao za malezi hazikuambulia patupu "
  4. Mwangeka anapatikana akienda shuleni kupata Elimu. Tunaambiwa kuwa Jumamosi moja, Mwangeka alikuwa ametoka shuleni, na siku hizo walimu walikuwa wameng'ang'ania kuwafunza Jumamosi wanafunzi waliokaribia 'ICU',kama walivyoliita darasa ala nane (uk 59).Mwangeka anaonekana kuendeleza masomo yake hadi Chuo kikuu na baadae kuajiriwa kazi (uk 62.)
  5. Lunga Kiriri Kangata naye anapata elimu yake, kwani tunapata kumuona kama amri-jeshi wa uhifadhi wa mazingira walipokuwa shuleni. Tunaambiwa kuwa kila Ijumaa wakati wa gwaride, Lunga angehutubia wanafunzi wenzake na walimu kuhusu swala la mazingira (uk 67-68).
  6. Umulkheri pia anaenda kupata elimu yake katika shule. Tunampata mwalimu wake akijaribu kumrejesha Umu darasani wakati fikra zake zinapo ondoka katika shughuli za masomo. Tunapata pia kuwa kwa hali ambayo Umu alikuwa akiishi, mwalimu mkuu wa Shule ya Tangamano, anamsajili kuwa mwanafunzi huko, kwa hisani yake na kwa ushauri wa wizara ya elimu (uk 78).Umulkheri anayaendeleza masomo yake hadi Chuo kikuu, anapoenda ughaibuni kusomea huko (uk 128).
  7. Mhusika Pete pia anatumika katika kuwasilisha maudhui ya elimu, ingawa elimu yake inagonga mwamba baada ya kuozwa kwa mzee mmoja aliyeitwa kuwa katika darasa la saba, wazazi wake walipomuoza kwa mzee huyu.
  8. Baada ya Naomi kuhangaika kwa miaka mingi akiwatafuta watoto wake, anaamua kuanzisha biashara ndogo karibu na Chuo kikuu cha Mbalamwezi, na kazi anayoifanya ni kuwapigia wasomi chapa na kuisarifu miswada yao. Kwa hivyo, tunapata kuwa maudhui haya ya elimu yanajitokeza pia, kwa kuwepo kwa Chuo kikuu (uk 193).

10. Uongozi

Haya ni madaraka anayopewa mtu ya kusimamia au kuongoza shughuli fulani. Anayepewa mamlaka haya anakuwa ndiye kiongozi. Uongozi waweza kuwa mbaya au uongozi mzuri.

  1. Tunapata kuwa watu wanachagua viongozi wanaotaka, na kampeni pia zinafanywa kwa njia ya kutupa vikaratasi ovyo ovyo. Uk 12;"Sasa ameanza kuelewa kwa nini wiki iliyopita vikaratasi vilienezwa kila mahali vikiwatahadharisha kuwa mna gharika baada ya kutawazwa kwa Msumbi ( kiongozi) mpya. "Siku ile baada ya kutawazwa kwa kiongozi mpya, kiongozi ambaye kulingana na desturi za humu mwetu, hakustahili kuiongoza jamii ya Wahafidhina, kisa na maana alikuwa mwanamke, mbingu zilishuka "

11. Mapenzi.

Hii ni hali ya mvuto na upendo alionao mtu kwa mtu mwingine. Pia nia hisia ya upendo anayokuwa nayo mtu kuhusu mtu mwingine.

  1. Ridhaa alimpenda sana mkewe Terry na wana wake. "Polepole parafujo za mwili wake zililegea, akaketi juu ya ma. jivu-la, juu ya miili ya wapenzi wake "
  2. Tunapata kuwa kuna mapenzi kati ya Mwangeka na baba yake Ridhaa. Haya ni mapenzi ya mzazi kwa mwanawe, Ridhaa alimpenda sana mwanawe Mwangeka kwani ndiye pekee tu aliweza kuepukana na janga Ia mauti kwa familia yote yake Ridhaa. Mapenzi haya yanadhihirika wakati Ridhaa anamlaki mwanawe kwenye uwanja wa ndege anapokuwa akirudi nyumbani kutoka ughaibuni. Wanaonekana wakikumbatiana kwa muda na Mwangeka kujitupa kifuani mwa babake, - na wanashikana kukutu. Pia wanazungumza kimoyoyo kuhusu jinsi maisha yao yamekuwa; kwa kweli haya ni mazungumzo ya wapendanao (uk 46- 47).
  3. Maudhui ya mapenzi pia yanajitokeza kati ya Billy na sally. Sally alikuwa msichana ambaye Billy alichumbia kwao, na kisha akamleta katika nchi hii ya kiafrika ili kumuonyesha mahali wangeweza kuishi baada ya kufunga akida. Kwa bahati mbaya, Billy anasalitiwa na mpenzi wake sally na kuambiwa kuwa jumba lenyewe ni kama kiota cha ndege, mahali ambapo yeye hawezi akaishi hata kuwe vipi (uk 80).
  4. Tunapata pia kuna mapenzi kati ya Subira na wanawe Mwanaheri na Lime. Hili linajidhihirisha baada ya Subira kumwandikia barua mpenzi mwanawe Mwanaheri. Haya ni mapenzi ya uzazi lakini Subira anawasaliti wanawe (uk 95.)
  5. Pia kuna mapenzi kati ya Umulkheri na wazazi wapya wa kupanga, Mwangeka na mkewe Apondi anaowapata baadae. Mwangeka na Apondi wanampenda sana Umu ni kusema kuwa ni baraka za Mungu za kumfidia mwana wao aliyeaga dunia. Umulkheri naye anawapenda sana hawa wazazi wake wapya kwani waliweza kumlipia hafi karo. Pia waliweza kumponya uchungu aliokuwa nao moyoni wa kuachwa na wazazi wake (uk 117-118)
  6. Kuna mapenzi yanayojidhihirisha katika familia hii ya Mwangeka na Apondi, kwa wana wao. Wakati umulkheri anafikiwa na wakati wa kwenda kuyaendeleza masomo yake ughaibuni, wanamsidikisha hadi kwenye uwanja wa ndege. Mapenzi makali yanajidhihirisha wakati kila mmoja wao analia machozi kwa kuachana na Umu alipokuwa akiliabiri ndege Tumaini (uk 128).
  7. Kuna mapenzi kati ya Mwaliko na wazazi wake wa kupanga ambao ni Bwana Mwangemi na Bii Neema, ambao hawakuwa na uwezo wa kukilea kizazi chao, na hatimaye wakaamua kumpanga mwana huyu ili awe wao rasmi. Hawa wawili wanampenda sana Mwaliko, naye Mwaliko anawapenda kama wazazi wake halisi (uk 166-167).
  8. Naomi anawapenda sana wana wake ingawa alikuwa amewasaliti kwa kuwaacha wakiwa wachanga. Ameishi kuwatafuta walikopotelea kwa miaka mingi, lakini mwishowe, anawapata wana wake bado wako hai na wamejiendeleza sana kimaisha na kimasomo. Anawaomba msamaha huku akiwa na uchungu mwingi rohoni mwake. Wana wake wanamsamehe mwishowe kwa mapenzi waliyokuwa mamayao (uk 192-193)

12. Teknolojia

Haya ni maarifa ya sayansi na matumizi yake katika mitambo, vyombo na zana katika viwanda, kilimo, ufundi, au njia za mawasiliano.

  1. Kuna matumizi ya vyombo vya habari (runinga) ambavyo ni mazao ya teknolojia mpya. Uk 12; "Katika fikra zake ambazo tangu hapo zilikuwa macho, alikumbuka taarifa ya habari kupitia kwenye runinga, taarifa ambayo japo ilitangazwa miaka minne iliyopita, ilikuwa kana kwamba anaisikiliza sasa "
  2. Katika ukurasa wa 49 tunapata haya; "Nilipoona yaliyotokea humu kupitia kwa runinga, na mitandao mingine ya kijami; ubadhilifu wa mali, uchomaji wa watu kama makaa, msongamano na magonjwa katika kambi, kasha barua meme iliyonijuza kuhusu msiba uliotupata, niliingiwa na kihoro kisicho na kifani " Matumizi ya runinga na mitandao ya kijamii na pia matumizi ya barua meme, ni uvumbuzi wa teknolojia katika mawasiliano.

13. Ufeministi/taasubi ya kiume

Hii ni hali ambapo mwanamke anajidhalilisha ama anadhalilishwa katika jamii. Mwanamke hapewi nafasi katika jamii, ama anajiona kuwa kiumbe dhaifu mwenye hana uwezo.

  1. Katika ukurasa wa 16 tunasoma; "Siku ile baada ya kutawazwa kwa kiongozi mpya, kiongozi ambaye kulingana na desturi za humu mwetu, hakustahili kuiongoza jamii ya wahafidhi 82 na, kisa na maana, alikuwa mwanamke.
  2. Katika ukurasa wa 3;"Huku ni kujiumbua hasa. Unyonge haukuumbiwa majimbi; ulitunukiwa makoo " Bibi alikuwa akimwelezea Ridhaa kuwa unyonge haukuumbiwa 'majimbi'ambao ni wanaume, bali uliumbiwa 'makoo',yaani wanawake. Hivyo basi tunapata kuona kuwa jamii pia iliwadhalilisha wanawake tangu zamani.
  3. Katika ukurasa wa 8; "Mzee mwenye wake na wana wengi alihesabiwa kuwa mkwasi kwelikweli basi wake hawa hawakuchelea kutimiza amri ya maumbile, wakapania kuujaza ulimwengu " Tunapata kuwa wanawake wanadhalilishwa kwa kuonekana kana kwamba jukumu lao kuu katka jamii ni kuijaza dunia au kuzaa wana. Mwanamke hapewi nyadhifa za umuhimu katika jamii ila tu kazi yake ni kuoleka na kujaaliwa na wana wengi awezavyo.
  4. Katika ukurasa wa 45;"Viongozi wengi wa awali walibwagwa chini na vijana chipukizi. La kuhuzunisha ni kwamba wengi walishindwa kabisa kukubali ushinde, hasa yule ambaye alikuwa anagombea kilele cha uongozi. Kulingana naye, nafasi hii iliumbiwa mwanamume, na kupewa mwanamke ni maonevu yasiyovumilika "Katika hali hii, jamii haikukubali wanawake kuwa viongozi, bali cheo hiki cha uongozi kilikuwa cha jinsia ya uanaume.
  5. Katika ukurasa wa 149; "Maisha yangu na Fugo yalikuwa kama ya ng' ombe aliyetiwa shemere na kufungwa nira pamoja na punda ambaye anakaidi kusonga. Ule unene wake, lile kituzi lililotoka kwenye makwapa yake makuza na kufudikiza kote chumbani, ule wivu wa mke mwenzangu wa pili, kule kukemewa na kuchekwa na watoto wa mke wa kwanza yote yalininyong' onyeza na kuniumbua. Nilichukia jaala aliyonipa mama kwa kujali maslahi yake tu, nilichukia nguvu ya maumbile iliyoniweka kwenye jinsia ya kike, nilichukia kitoto nilichohimili kwenye mji wangu hata miezi tisa ilipotimia na kupata salama, niliamua kwamba kwa mzee Fungo hakuniweki tena. Na unadhani anakwenda wapi? Utawezaje kujitunza wewe na mtoto wako na hali bibi yako ndiye huyo, hana hanani, na wazazi wako walafi walikuuza kwangu ili wapate pesa za kuwasomesha ndugu wako watano wa kiume?Aliuliza Fungo " -tukio hili linatuonyesha wazi jinsi mwanamke amedhalilishwa katika jamii. Kwanza, mamake mtoto huyu msichana anamwoza kwa mzee mwenye wake wawili, (Mzee Fungo),ili aweze kupata pesa za kuwalipia vijana wake karo ya shule. Msichana anaonekana kutokuwa na umuhimu ya kupelekwa shuleni ili kupata elimu, ilhali yeye mwenyewe aliazimia kuendeleza masomo yake. Maazimio yake ya elimu yanagonga mwamba baada ya kuozwa ka mzee Fungo ambaye anamtesa na mwishowe kumtaliki na kitoto kichanga. Msichana huyu mchanga pia anapitia machungu kwenye ndoa yake kwa kuchekwa na kudharauliwa na wake wenza'- na wana wao.
  6. Katika ukurasa wa 154;"Mlaani shetani' Sauna aliuambia moyo wake, 'unajua kuwa mimi sikuumbiwa ujalaana, walimwengu ndio walinifinyanga upya, wakanipa moyo wa ujabari. Fikiria u kigoli, kifua ndio kinaanza kuvuvumka, kisha unaamka usiku kumpata baba yako, ba-ba-ya-ko, kwenye chumba Chako cha malazi. Anakutenda ya kutendwa. Asubuhi huna hata uso wa kumtazamia yeyote, wala kinywa cha kumwambia mamako kuhusu feli uliyotendewa. Na utamwambiaje mja huyu ambaye daima ni mwanamke taa, atakalo baba yeye huliridhia bila swali, na ikitokea kwamba atauliza swali, anakuwa mpokezi wa makonde, vitisho na matusi? Hebu yatie haya kwenye mizani; baada ya mwezi mmoja unaanza kushikwa na kisulisuli, kichefuchefu cha asubuhi nacho kinakuandama. Fikra zako za kitoto zinakutuma kuwaza kuwa ni malaria au homa ya matumbo. Unamwambia mama yako ambaye anaonekana kushtuka kiasi. Mama anapokupeleka hospitali, anapasuliwa mbarika, nawe limbukeni hujui lolote. Mnapofika nyumbani, anakuhoji, nawe hujui kuficha lolote, unamwambia imekuwa mazoea baba yako kukuhujumu kila apatapo nafasi ' "Hili haliwezi kukubalika!Kujipagaza uzazi na ulezi katika umri huu, tena mzazi mwenzio si mwingine, ila baba yako?'Tukio hili la kufadhaisha linatendeka kwa kumdhalilisha mwanamke. Tunaona kuwa mamake Sauna hana uhuru wa kuzungumza kwake, wala kuuliza maswali, na iwapo ameuliza swali, inakuwa ni vita au kichapo kutoka kwa mumewe. Sauna naye anadhalilishwa kwa kubakwa na babake mzazi, wala sio mara moja. Hatimaye anapata mimba ya babake mzazi. Jambo hili linamdhalilisha sana Sauna hivi kwamba heshima yake yote inapotea, na hawezi kuzungumza na mama au baba yake.

14. Umenke

Ni hali amabapo mwanamume hapewi nafasi katika jamii. Mwanamume amedhalilisha katika jamii na nafasi yake haitambuliki.

  1. Katika Riwaya tunapata haya; "Haiwezekani!hili haliwezekani!ltakuwa kama kile kisa cha yule kiongozi wa kiimla wa kike-yule anayesimuliwa katika visakale vya majirani wetu - Kumbuka jinsi katika enzi hiyo ya kiistimari wanaume walivyotumikishwa!si Sisi tuliokuwa tukitifua udongo mashambani huku wanawake kama majeta wanakaa na kututumikisha?" Uk 17;"Fikiria suala la jinsia 'Na usidhani ni jinsia nyingine, ni dada zetu tu. Vyombo wa habari na vikao vya wapigania haki vinapigania elimu ya mtoto wa kike, haja ya kuwainua akina mama kiuchmi, hukumu ya kifo kupitishwa dhidi ya mwanamume, hata mume atakayepatikana na kosa la kumbaka mke wake. Uk 20
  2. "Nakumbuka asubuhi ya pili baada ya mtafaruku kuanza. Nilikuwa sebuleni na wanangu tukitazama runinga. Mara nikaskia; 'Hakuna Amani bila kumheshimu mwanamume. Hatuwezi kukubali haya. Hata mizimu itatucheka!'

15. Sheria

Hizi ni kanuni zinazotungwa na jumuiya fulani kwa mfano bunge au jamii fulani ili kuratibu shughuli za jumuia inayohusika, na adhabu pindi kanuni hizo zikikiukwa.

  1. Uk 20; "Wengine waliokuwa jasiri walidiriki kuingia kwenye maduka ya wafanyabiashara wa kihindi, kiarabu na hata Waafrika wenzao, wakapora walichoweza kabla ya kukutana na mkono mrefu wa utawala "
  2. Uk 82,tunapata kuwa Umulkheri anaenda kwenye kituo cha polisi kupiga ripoti kuhusu kupotea kwa ndugu zake Dick na Mwaliko. Jambo linatuonyesha kuwa kuna sheria ambayo inafuatwa na raia, na pia kwa uwepo wa kituo cha polisi "Mimi ni Umulkheri Lunga. Ninasomea Shule ya Upili ya Mtende. Nimekuja kutoa taarifa kuhusu kupotea kwa ndugu zangu Dick na Mwaliko'alisema Umu huku amemkazia macho askari wa zamu, kwa kuhofia kutosikika "
  3. Uk 22,Wananchi wanaahidiwa kuwa wale ambao walipata mali ya uma kwa njia isiyo halali watapambana na mkono dhabiti wa sheria "Waliogawiwa au kununua mali ya uma kwa njia za udanganyifu watakabiliana na mkono mrefu wa sheria "
  4. Uk 158,Bi. Kangara na Sauna wanatiwa mbaroni kwa kufanya biashara haramu "Polisi walipopashwa habari kuhusu maficho ya Bi. Kangara, walishika tariki moja kwa moja hadi nyumbani kwake ambako waliwatia mbaroni Bi. Kangara na Sauna, mabibi hawa walifikishwa mahakamani na kushtakiwa kwa kosa la ukiukaji wa haki za watoto, wakarambishwa miaka saba gerezani na kazi ngumu "

16. Uongozi mbaya

Haya ni maudhui yanayojitokeza wakati viongozi wanapofanya shughuli zao za uongozi kwa njia isiyofaa. Haya husababisha kuteseka kwa wanajamii au raiya wa kawaida.

  1. Uk 21; "Maeneogatuzi yenu yanahitaji mabarobaro kama nyinyi kulisukuma gurudumu la maendeleo'. Hapa ndipo unashangaa utarudi kwenye shamba lipi na tangu hapo familia yako uliiacha ikiishi kwa msaada wa wale wale waliotoka mbali kule walikotoka, wakapewa maelfu na maelfu ya ekari, wakajenga viwanda na maduka ya biashara, wengine wakalima mashamba makubwa makubwa huku wakidai kuwa ni njia ya kuwahakikishia wenyeji hali ya kujitosheleza kwa chakula. Kumbe wanakuja kutufukarisha Zaidi!Tunapolalamika kashafa za unyakuzi wa hata vikata vidogo tulivyo navyo, tunapozwa roho kwa, tumeunda tume ya kuchunguza kashfa hii. Waliogawiwa au kununua mali ya uma kwa njia za udanganyifu watakabiliana na mkono dhabiti wa sheria; Ni wazi kuwa mwanainchi wa kawaida hadiriki kuziona ripoti za tume hizi au tuseme ripoti hizi huwa wageni wa rafu za makavazi ya kitaifa!" Tunapata kuwa uongozi uliopo ni wa kuwanyanyasa raia wa kawaida ka kunyakua mashamba yao, na kuahidi kuwa kuna tume za kushughulikia mambo hayo, ilhali haziko.

17. Uozo wa maadili ya jamii

Hii ni hali ambapo maadili ya jamii yamepunguka kwa kiasi kikubwa, na hivyo mambo yanayofanywa katika jamii hiyo si ya kukubalika. Tazama mifano michache ifuatayo ya uozo huu.

  1. Ubakaji. Hili ni jambo ambalo limepatikana katika jamii na husababishwa na ukosefu wa maadili mema ya wanajamii. Katika ukurasa wa 25 tunasoma; "Kisha genge hili la mabarobaro watano lilifululiza hadi walipokuwa maskini mabinti zangu wawili, Lime na Mwanaheri. Sikuweza kuvumilia kuona unyama waliotendewa. Nilijaribu kwa jino na ukucha kuwaokoa lakini likawa suala la mume nguvuze!Mahasimu hawa walitekeleza unyama wao na kuniacha bila kunigusa, niuguze majeraha ya moyo " Wasichana hawa wawili walibakwa hadharani huku baba yao akitazama bila uwezo wa kuwasaidia.
  2. Ulanguzi wa dawa za kulevya. Tunapata kuwa Dick anaifanya kazi ya kusafirisha dawa za kulevya kutoka nchi moja hadi nyingine, na hii ni biashara ambayo inafanywa na vijana wengi, na kuwafanya wengine kuingia kwenye mtego ya polisi na kuelekea kutumikia kifungo chao gerezani. Uk 119;120. "Siku hiyo kiwewe kilikuwa kimemkumbatia kwani kazi ya kubeba dafina'kama walivyoiita biashara haramu ambayo kalazimishwa kufanya siku hizo, ilikuwa imewaingiza wengi kwenye nyavu na madema ya polisi, wakatiwa mbaroni "Dick amesafirisha maelfu kwa maelfu ya vifurushi vya dawa hizi. Mwanzoni hakuwa mraibu wa dawa hizi lakini ilibidi ajizoeshe, kwa usalama wake mwenyewe, kwani mara nyingi ilibidi kuzimeza dawa zenyewe ili kwenda kuzitapika kwenye masoko ughaibuni "
  3. Uporaji, wizi na ukatili. Haya ni matendo ya kuchukua mali au milki ya mtu mwingine na kutaka kuimiliki bila idhini na kwa njia ya mabavu. Tunapata kuwa mali ya watu binafsi yanaharibiwa, kwa mfano nyumba na mali yote ya Ridhaa yanateketezwa, wakiwemo watoto wake na mkewe pia. Pia, mali ya wananchi kama mashamba yananyakuliwa na wanaachwa bila chochote. Katika ukurasa wa 25,tunapata kuwa mabarobaro wanavamia watu na kuwafanyia unyama, "Kabla hajajibu lolote, alikuwa amekula mikato miwili ya sime, akazirai kwa uchungu "
  4. Uendelezaji wa biashara haramu. Bi. Kangara walifanya baiashara haramu ya kuwauza watoto na vijana. Uk 157; "Safari yake ilipata mkondo mwingine baada ya polisi kupata fununu kuhusu njama ambazo yeye na Bii Kangara walikuwa wakiendesha. Mabibi hawa walikuwa na mtandao ambao kazi yake ilikuwa kuwauza watoto na vijana "uk 84; "Sauna alikuwa Chui ambaye hakupigwa na mshipa kujifanya mwema kwa waajiri wake ili aaminiwe, naye apate fursa ya kuwaiba watoto na kuwapeleka kwa bibi mmoja ambaye aliwatumia ka biashara ya nipe nikupe, na katika ulaguzi wa dawa za kulevya " Uk 151; "Zao la muungano huu lilikuwa kuzaliwa kwa mwanangu wa pili. Huyu yumo mtaa wa Sinyaa ambako nilikuwa ninaishi baada ya kupigwa putwe na Nyangumi, mkewe wa halali amemrudia. Analelewa na ndugu yake lnabidi hali iwe hivi kwani Sina pesa za kumlipia kijakazi, na vinywa hivi viwili lazima vilishwe. Na usidhani hata kitoto hiki cha pili sikujaribu kukiangamiza. Kwa kweli ukaidi wa kijusi chake ndio mwokozi wacho. Mwishowe nilimwendea daktari ambaye, badala ya kunisaidia, alikilaani kitendo changu na kuniambia kwamba nisimtie katika majaribu " Uk 151;"Hiki kilichonilaza hapa nacho kina roho Zaidi ya saba. Ni kijalaana ambacho nilikiokota katika shughuli za uuzaji pombe. Nadhani mmoja kati ya walevi waliozoea kuja kwenye baa nilimoajiriwa kuuza pombe aliniwahi nishai zikiwa zimenilemea, yakatokea ya kutokea, akaniachia ujira wangu wa kuafriti hiki "
  5. Uavyaji mimba. Tunapata kuwa uavyaji wa mimba ulikuiwa umekidhiri sana, - na hili ni jambo lisilokubalika katika jamii na pia katika maandiko matakatifu. Msichana huyu (Sauna) anapata mimba kiholela na kujaribu awezavyo kuiavya, na mwishowe, baada ya kushindwa kuavya mimba, anaamua kujiua. Katika ukurasa wa shetani' Sauna aliuambia moyo wake, 'Unajua kuwa mmi Sikuumbiwa ujalaana, walimwengu ndio walinifinyanga upya, wakanipa moyo wa ujabari. Fikiria u kigoli, kifua ndio kinaanza kuvuvumka, kasha unaamka usiku kumpata baba yako, ba-ba-ya-ko, kwenye chumba Chako cha malazi. Anakutenda ya kutendwa. Asubuhi huna hata uso wa kumtazamia yeyote, wala kinywa cha kumwambia mamako kuhusu feli Uliyotendewa. Na utamwambiaje mja huyu ambaye daima ni mwanamke taa, atakalo baba yeye hiliridhia bila swali, na ikitokea kwamba atauliza swali, anakuwa mpokezi wa makonde, vitisho na matusi?Hebu yatie haya kwenye mizani; baada ya mwezi mmoja unaanza kushikwa na kisulisuli, - kichefuchefu cha asubuhi nacho kinakuandama fikra zako za kitoto zinakutuma kuwaza kuwa ni malaria au homa ya matumbo. Unammwambia mama yako ambaye anaonekana kushtuka kiasi. Mama anapokupeleka hospitali, anapasuliwa mbarika, nawe limbukeni hujui lolote. Mnapofika nyumbani, anakuhoji, nawe hujui kuficha lolote, unamwambia imekuwa mazoea baba yako kukuhujumu kila apatapo nafasi ' "Hili haliwezi kukubalika!Kujipagaza uzazi na ulezi katika umri huu, tena mzazi mwenzio si mwingine, ila baba yako?"
  6. Mapenzi kati ya baba mlezi na bintiye. Babake Sauna anafanya mapenzi na mwanawe apatapo nafasi, na mwishowe, Sauna anapata mimba. Hili ni jambo ambalo halijakubalika katika jamii na pia ni jambo la kufadhaisha sana na lenye kuleta laana. Mbele ya Mwenyezi Mungu, ni jambo linalofaa pigo kubwa sana na hata mauti. Jambo hili lindhihirisha uozo wa maadili ulioko katika jamii na umefichika sana.
  7. Kutupwa kwa watoto wachanga Katika ukurasa wa 162 tunasoma hapa ameokotwa na binti huyu kwenye jaa la taka, 'alisema askari, 'Huenda akataka kukueleza kadhia yenyewe, 'akaongeza "Asante sana Neema, kwa utu wako, 'akasema mtawa huyu, 'Kitoto hiki kimepata kwao. Hapa, tutakiita Nasibu, Nasibu Immaculata - Najua itatokea familia hitaji itakayokuja kumpanga kama mwanao " Hili linatudhihirishia jinsi jamii imekuwa na mazoea ya kutupa wu ovyo ovyo bila kujali kuwa hao ni binadamu. Haswa wasichana wadogo wanapopata mimba bila ya kujipanga, wakishindwa kuavya mimba, wanaelekea kukitupa kitoto hicho kichanga punde tu baada ya kujifungua.

18. Dini

Hii ni imani inayohusiana na kuwepo kwa Kiumbe mwenye nguvu Zaidi kuliko viumbe wengine (Mungu). Haya ni maudhui yaliyojitokeza kwenye kitabu hiki kwa njia zifuatazo;

  1. Katika Uk 31 tunasoma, "Shirika la makazi bora lilikuwa limejitolea kuja kuwajengea wakimbizi nyumba bora. Misikiti na makanisa nayo yalikuwa yamekusanya magunia ya vyakula kuwalisha wahasiriwa wa hali hii ya tandabelua; ...sote tulikaa tukitunga macho barabarani tukisubiri jinsi waumini wanavyoambiwa wasubiri kuja tena kwa Masiya " Pia katika Uk 32 tunasoma kuwa, "Nilikumbuka kifungu kimoja katika sala za waumini(wakati nilipokuwa nikihudhuria ibada),kilichosema, ninawapa Amani mani yangu nawaachia "

19. Ufisadi

Huu ni utumiaji mbaya wa mali ya uma. Pia ni ubadhilifu wa mali ya serikali au chama.

  1. Katika Uk 41 tunapata kuwa kuna tume za kupigana na ufisadi ambazo zinaundwa, na jambo hili ni ishara kuwa kuna ufisadi unaoendelezwa "Je, ni tume ngapi za kuchunguza kashfa za kifisadi ambazo zimeundwa?Hizo si juhudi za kupigana na ufisadi?"
  2. Pia katika uk 13,"Uchukuzi wa milungulu pia ni aina ya ufisadi katika serikali "Wengine walionekana wakitoa milungulu hadharani, wengine wakatishia kuishtaki wizara husika kwa kile walichokiita ukiukaji wa haki za umiliki mali "

20. Demokrasia

Huu ni mfumo wa utawala ambao viongozi wake huchaguliwa kwa njia ya kupiga kura.

  1. Katika ukurasa wa 19 tunasema, "Viongozi wenyewe baada ya kupiga kura, walijikalia makwao, na kuendelea kuwatazama masabaha wao kwenye runinga wakiendelea kuzozana!"

21. Mabadiliko

Hii ni hali ambapo mambo yanaenda kinyume na jinsi yalivyokuwa yakienda mbeleni. Hali ya kufanya mambo inabadilika na kuwa tofauti ya kawaida yake.

  1. Katika ukurasa wa 10; "Hatua ya mkoloni ya kupuuza sera za Mwafrika za umiliki wa ardhi, na kuamua kujumuisha pamoja ardhi iliyomilikiwa na mtu binafsi, na kuidhinisha umiliki huu kwa hati miliki, ilivuruga mshikamano wa kijamii. Katika sera ya kijadi ya umiliki na matumizi ya ardhi, raiya wote, hata wageni, walikaribishwa na kugawiwa mashamba, hivyo kupata mbinu ya kuyaendeshea maisha. Sera mpya ya umilikaji nafsi wa ardhi ilimaanisha kwamba wale waliokosa pesa za kununulia mashamba wangekosa mahali pa kuishi. Na hata wale waliobahatika kuwa na pesa za kununulia mashamba daima walichukuliwa kama wageni wasiopasa kuaminiwa Tunapata kuwa mfumo uliokuwepo hapo awali wa kumiliki mashamba barani Afrika ulipigwa marufuku na kukawa na mfumo mpya wa umiliki wa mashamba uliohusisha kupewa kwa hati miliki. Haya ni mabadiliko yanayokuja katika jamii.
  2. Katika ukurasa wa 11; "Pengine hata ni mzaha tu. Kesho nitakurudisha shuleni. Nitazungumza na mwalimu ili awaelekeze Zaidi 'Huo ndio uliokuwa mwanzo wa maisha ya heri kwa Ridhaa. Baada ya mwalimu kuzungumza na wanafunzi na kuwasisitizia umuhimu wa kuishi pamoja kwa mshikamano dhihaka na masimangoyaliisha "Kuna mabadiliko yanayofanyika katika shule baada ya mamake Ridhaa kuzungumza na mwalimu wake kuhusu umuhimu wa kuwajuza wa nafunzi ushirikiano na kuishi kwa umoja. Mabadiliko haya yanakuwa ya maana sana kwa Ridhaa kwani elimu yake inaendelea kwa ufasaha na anahitimu hadi chuo kikuu.
  3. Katika ukurasa uo huo wa 11 tunasoma; "Mimi binafsi nimefanya juu chini kuhakikisha kuwa kijiji kizima kimepata maji ya mabomba. Eneo ambalo awali likiitwa Kalahari, sasa limetwaa rangi ya chanikiwiti. Miambakofi, mivule na miti mingine mingi imepandwa. Mvua inanyesha majira baada ya mengine "Haya ni mabadiliko yanayofanyika katika mtaa huu ambao ulikuwa hapo awali umekauka sana lakini baada ya maji ya mabomba kufikishiwa watu, tunapata kuwa kunabadilika na ile hali ya kuwa jangwa inaisha, miti mingi inapandwa na hata mvua nyingi kunyesha.
  4. Katika ukurasa wa 84,"Maisha ya Umu yalichukua mkondo mpya. Siku ile baada ya kuwapigia polisi ripoti, ilibainika kuwa wanuna wake walikuwa wametekwa nyara na Sauna "
  5. Maisha ya Ridhaa pia yanachukua mkondo mpya au kubadilika wakati familia yake inapoangamia kwenye janga la moto, na mali yake yote kuishia hapo. Maisha yaliyokuwa ya furaha pamoja na familia yake yanabadilika na kuwa uchungu mtupu na kilio cha kufiwa na wapenzi wake.
  6. Katika ukurasa wa 40 tunasoma; "Ridhaa: Na nani akasema viongozi waliopo hawajajikuna wajipatapo?Huoni hata wahasiriwa wa magonjwa sugu kama vile iri na hata UKIMWI wana dawa za bei nafuu za kuwawezesha kudhibiti hali hizi?Je, serikali haijaanzisha sera ya elimu bila malipo kwa Shule zote za msingi?Haijagharamia karo za Shule za kutwa katika Shule za upili?kumbuka pia na ule mradi wa kuhakikisha kuwa kila mwanafunzi kuanzia darasa la kwanza ana kipakatalishi chake?Ushaona?Hivi karibuni, nchi inafikia ile vision 2030 hata kabla ya 2030 yenyewe!Je, ni tume ngapi za kuchunguza kashfa za kifisadi ambazo zimeundwa?Hizo si juhudi za kupigana na ufisadi?" Maelezo haya yote yanatuonyesha jinsi taifa limepiga hatua mbele kimaendeleo. Kumekuwa na mabadiliko mengi sana katika serikali na pia hali ya maisha ya raia, bila kusahau elimu.
  7. Katika ukurasa wa 63 tunasoma; "Usicheze na binadamu apatapo nyenzo ya kujiinua!kabla ya miaka miwili kuisha, mahali hapa palikuwa pamepata sura mpya-majumba yenye mapaa ya vigae, misitu ya mihindi na miharage, maduka ya jumla, viduka vya rejareja almuradi kila mtu alijifunga mkaja kutunisha kibindo chake; kufidia alichokuwa amekipoteza hapo awali "Haya ni mabadiliko yanayoendelea katika msitu wa Mamba. Tunaambiwa kuwa msitu huu uligeuka na kuwa nyumbani mwa maelfu ya watu waliogura makwao bila tumaini ya kurudi. Maduka na majumba yanajengwa, na ile hali ya kuwa msitu inabadilika, na mashamba ya watu ndiyo yanayoonekana kwa sasa.
  8. Pia katika ukurasa wa 148 tunasoma; "Maisha yangu yalichukua mkondo mwingine nilipojiunga na darasa la saba. Katika jamii yangu, inaaminika kuwa msichana akishaisha kupashwa tohara, ameingia utu uzimani, hivyo ataipaka familia yake tope ikiwa ataendelea kuozea kwao bila mume "

22. Uharibifu wa mali na mazingira

Assumpta K.Matei amejikita katika maudhui ya uharibifu wa mazingira na pia mali ya watu binafsi.

  1. Katika ukurasa wa 20 tunasoma; "Nchi ya Wahafidhina ilitwaa sura mpya. Misafara kwa misafara ya watu waliohama kwao bila kujua waendako ilizipamba barabara na vichochoro vya Wahafidhina. Mizoga ya watu na wanyama, magofu ya majumba yaliyoteketezwa kwa moto, na viunzi vya mimea iliyonyong'onyezwa na moto ilijikita kila mahali; uharibifu wa mali na mazingira ukashamiri "
  2. Katika ukurasa wa 20 tunapata; "Mara hali ilibadilika, nikaona wote wameyazingira magari barabarani na kuanza kuyawasha moto kana kwamba wanayachoma rtiabiwi ya taka!...Magari yaliwaka moto bila kujali kilichomo ndani " Matukio haya yanatuonyesha jinsi mali ya watu binafsi ilivyoharibiwa na vijana, kwa kuteketezwa moto.

23. Ujaala

Haya ni maudhui ambayo huhusisha mambo yanayofanyika kwa uwezo wake Mwenyezi Mungu. Binadamu hana uwezo wa kuyabadilisha mambo haya, na hayezi kuyaepuka kwa njia yoyote ile. Assumpta K.Matei ametumia maudhui haya katika kazi yake ya fasihi kwa njia hizi;

  1. Katika ukurasa wa 8 tunasoma; "Ridhaa hakuwa mkazi asilia wa msitu wa Heri. Alikuwa 'mfuata mvua',kama walivyoitwa walowezi na wenyeji kindakindaki. Hakupachagua mahali hapa, majaaliwa yalitaka, na majaaliwa yana nguvu!" Ridhaa hakujichagulia kuishi kule, ila alijikuta humo kwa nguvu zake Maulana ambazo haziwezi kuepukika.
  2. Katika ukurasa wa 128 tunasoma; "Hata waliposikia kwa mbali sauti ikitangaza kuwa abiria wanaoabiri ndege Tumaini waanze kuingia, walijua jaala ilikuwa imewakutanisha, kwamba hawatawahi kutengana tena " Haukuwa uwezo wao kukutana, ila tu ni kwa uwezo wake Mungu.

24. Utamaduni

Hizi ni mila, desturi, asili, lmani na itikadi za watu fulani au jamii fulani. Lazima watu hawa ama jamii hii ifuate mila zake, ili kila mmoja atambulike kuwa mmoja kati ya hao watu ama wanajamii.

  1. Katika ukurasa wa 8 tunasoma; "Unajua zama hizo hali ilivyokuwa!Mzee wenye wake na wana wengi alihesabiwa kuwa mkwasi kwelikweli. Basi wake hawa hawakuchelea kutimiza amri ya maumbile, wakapania kuujaza ulimwengu!" Ulikuwa ni utamaduni wa kiafrika kuoa wanawake wengi, na kuwa na familia kubwa uwezavyo, na kwa hayo, unakuwa mtu wa kuheshimiwa, na kuhesabiwa kati ya wakwasi wa jamii hiyo. Hii ni hali au tendo la watu wawili au zaidi kuungana na kusaidiana katika shughuli aidha za kikazi, ili kuafikia lengo moja sawa.
  2. Katika ukurasa wa 9 tunasoma; "Ilipotokea kwamba kulikuwa na upungufu wa ardhi katika eneo Fulani, watu wangehama na kuishi na watu wa ukoo mwingine. Lilikuwa jambo la kawaida kuwapata watu wakiishi na kulima katika mashamba ya majirani, marafiki na jamaa. Baada ya kuyalima mashamba haya kwa muda, yaliishia kuwa yao. Hawakuhitajika kuyanunua kama wanavyofanya sasa " Tunapata kuona kuwa nyakati za hapo awali, kulikuwa na ushirikiano mkuu katika jamii, na kila mtu aliishi kwa udugu na mwenzake, wakafanya kazi pamoja, wakaishi pamoja, wakalima mashamba pamoja, na hivyo basi, ufanisi ukawa mkubwa sana.

26. Utabaka

Hii ni hali ya kuwa na kundi fulani katika jamii linalotofautiana na kundi lingine katika jamii iyo hiyo, kwa misingi ya kiuchumi, kielimu na kadhalika. Utabaka mara nyingi hujitokeza wakati kunapopatikana matajiri na masikini katika jamii. Pia kuna matabaka ya wasomi, wafanyakazi, wafanya biashara, na kadhalika.

  1. Katika ukurasa wa 14 uliopo ni ule wa hali, mazoea na silika. Hapa tulipo tupamwe na wamwe na walokuwa nacho na wachochole. Unaweza kusema kuna kiasi fulani cha usawa watu husema kuwa binadamu hawawi sawa ila kifoni! Kile ambacho hawajuia ni kwamba hata katika kifo, hamna usawa. Pana tofauti kati ya mandhari wanamofia. Kuna wanaokufa wakipewa na wauguzi katika zahanati za kijiji. Wapo wanaolala maumivu yao yakiwa yamefishwa ganzi kwenye hospitali za kifahari, wakiliwazwa na mashine, kila mmoja akihimiza wenzake kuushikilia kukutu uhai wa mheshimiwa huyu. Hawa wafapo sura zao huwa tulivu; wameziachilia huru roho zao kwa faraja. Huwezi kuzilinganisha nyuso zao na za wanaokufa kwa hamaniko wakizingirwa na jamaa ambao hawana hata hela za kununulia sindano ya kuingiza dawa mwilini!Kuna wale ambao hufia kwenye vitanda vya mwakisu vitongojini baada ya kupiga maji haramu. Hawa husemekana kuwa wamekuwa nzi ambao hufia dondani sio hasara. Hulaumiwa kwa kujitosa katika msiba wa kujiwekia. Tofauti hizi zote unazijua. Unajua pia kuna tofauti hata katika mitindo ya mazishi, viviga vinavyohusishwa na sherehe za mazishi na hata mavazi ya "mwenda zake" na wafiwa. Hata majeneza yenyewe huhitilafiana!" Kuna matabaka mawili yaliyoangaziwa sana hapa, yale ya walala hoi, na walala heri. Matabaka haya mawili yanatofautiana sana kihali, na jinsi ya kufanya mambo yao.

27. Utala

Hii ni hali ya mume mmoja kuwa na wake wengi, au Zaidi ya wawili. Hali hii inapatikana sana katika jamii za waafrika, na mzee huheshimiwa akiwa na familia kubwa Zaidi na wana wengi. Mtala ni mmoja wa wake wengi waliooleka kwa mume mmoja. Assumpta K. Matei anajikita katika maudhui haya kama tunavyo ona kutokana na mifano ifuatayo.

  1. Katika ukurasa wa 7 tunasoma; "Baba yake yasemekana alikuwa na wake kumi na wawili. Unajua zama hizo hali ilivyokuwa!Mzee mwenye wake na wana wengi alihesabiwa kuwa mkwasi kwelikweli "
  2. Katika ukurasa wa 148 tunasoma; "Wajomba zangu hawakuchelea kupokea posa na baadaye mahari kutoka kwa buda mmoja ambaye alinioa kama mke wa nne "
  3. Katika ukurasa wa 151 tunasoma; "Zao la muungano huu lilikuwa kuzaliwa kwa mwanangu wa pili. Huyo yumo mtaa wa Sinyaa ambako nilikuwa ninaishi baada ya kupigwa pute na Nyangumi, mkewe wa halali amemrudia " Kutokana na hali hizi tofauti, tunapata kuona kuwa jambo la wanawake kuoleka kwa bwana mmoja lilikuwa limekithiri sana katika jamii.

28. Malezi

Hii ni hali ya mzazi kumlea mtoto aliyemzaa au hata wa kupanga. Katika riwaya hii, swala la ulezi limejikita sana katika hali tofauti.

  1. Kunao wazazi ambao wanawalea wana wao kwa njia inayofaa,
  2. wengine baada ya kuwazaa wana wao, huwatupa kwenye majaa ya taka ili waage dunia.
  3. Kunao wengine ambao baada ya kujifungua, na kutopata haja ya kuwa na malaika huyo, wanaamua kumtupa langoni la nyumbani mwa watoto wasiokuwa na wazazi ili mwana huyu aweze kutelekezwa na kulelewa huku na wasamaria hawa wema.
  4. Kunao wazazi wengine ambao wanawalea wana wao katika hali ya umaskini, lakini baadae, watoto hawa wanakuwa ndio wa kuwasaidia wazazi wao. ".Lunga ilibidi kuwa baba na mama wa watoto wake, na hilo usilione kama jambo jepesi, Hakuwaacha watoto wake kama alivyofanya mkewe Naomi'
  5. Tunapata kuwa kuna kina mama wengine ambao wanawaachia kina baba watoto ili wawalee. Haya ni malezi mabaya kutokana na wazazi wa kike.


Maswali ya marudio

  1.  
    1. Ujaala ni nini (alama 2).
    2. Kwa kutoa mifano kutokana na riwaya hii, eleza jinsi ujaala umejitokeza katika jamii (alama 10).
  2. Jadili maudhui haya kama yanavyo jitokeza katika riwaya ya Chozi la Heri (alama 20.)
    1. Utamaduni.
    2. Demokrasia.
    3. Mapenzi.
    4. Teknolojia.
  3. Elimu ndiyo nguzo ya maendeleo katika kila jamii. Elimu pia imesababisho mabadiiko mengi katika jamii. Kwa kurejelea riwaya hii, jadifi kauli hii inoyohusiana na elimu (alama 20).
  4. Janga la mauti au kifo limewaadhiri wahusika kadhaa katika riwaya hii. Kwa kurejelea wahusika kadhaa, eleza jinsi mauti yameadhiri kupitishwa kwa maudhui na mwandishi (alama 20).
  5. Thibitisha jinsi maudhui ya ukoloni mkongwe na ukoloni mambo leo yanavyojitokeza katika riwaya hii ya Chozi la Heri (alama 20).
  6. Ufeministi ni hali ya mwanamke kudhalilishwa katika jamii. Kwa kutolea mifano kutoka kwa riwaya hii, eleza jinsi ufeministi ulivyokidhiri katika jamii ya mwafrika (alama 20).
  7. Kama walivyosema waswahili, umoja ni nguvu, utengano udhaifu; tetea kauli hii, huku ukiangazia riwaya ya Chozi is Heri (alama 20.)
  8. Utala ni swala ambalo limejitokeza sana katika jamii za Kiafrika. Kwa kurejelea riwaya ya Chozi la Heri, eleza umuhimu na udhaifu wa utamaduni huu (alama 20).
  9. "Bila shaka hill ni zoo lingine la husuda " Kwa kurejelea riwaya hii, elezea jinsi husuda ilileta balaa kwa wanajamii wa nchi hii ya kiafrika (alama 20).
Join our whatsapp group for latest updates

Download Dhamira na Maudhui Katika Chozi la Heri - Mwongozo wa Chozi la Heri.


Tap Here to Download for 50/-




Why download?

  • ✔ To read offline at any time.
  • ✔ To Print at your convenience
  • ✔ Share Easily with Friends / Students


Get on WhatsApp Download as PDF
.
Subscribe now

access all the content at an affordable rate
or
Buy any individual paper or notes as a pdf via MPESA
and get it sent to you via WhatsApp

 

What does our community say about us?

Join our community on:

  • easyelimu app
  • Telegram
  • facebook page
  • twitter page
  • Pinterest