KCSE 2012 Kiswahili Paper 1 with Marking Scheme

Share via Whatsapp
  1. Lazima
    Wewe ni mkuu wa baraza la wnafunzi shuleni mwenu. Kumekuwa na visa vya wanafunzi kukiuka sheria za shule. Andika kumbukumbu za mkutano wa baraza hili uliofanyika kujadili swala hili.
  2. Andika insha kuhusu umuhimu wa vijana katika kuimarisha mshikamano wa kitaifa.
  3. Andika insha inayobainisha maana ya methali: Chombo cha kuzama hakina usukani.
  4. Tunga kisa kinachoanza kwa maneno yafuatayo:
    Nilijaribu kuyafumbua macho yangu yaliyojaa uchovu kutokana na malimbikizo ya usingizi …


MARKING SCHEME

  1. Hii ni kumbukumbu. Mtahiniwa azingatie vipengele viwili vya kimsingi vya utungo wa aina hii; yaani muundo/ sura na yaliyomo/ maudhui.
    1. Sura ya kumbukumbu/ muundo wa kumbukumbu
      1. Kichwa kikuu
        • kichwa hiki kijumuishe:
        • jina la mkutano/ kundi linalokutana
        • mahali pa mkutano
        • siku ya mkutano
        • tarehe ya mkutano
        • saa
      2. Mahudhurio
        1. Waliohudhuria
        2. Waliotuma udhuru
        3. Waliokosa kuhudhuria
        4. Waalikwa/ waliokuwepo ila si wanabaraza kwa mfano, mkuu wa ushauri nasaha (Hii si lazima, ila yaweza kutuzwa kama upekee wa mtahiniwa)
      3. Ajenda
      4. Kufunguliwa kwa mkutano
      5. Kumbukumbu zenyewe ziandikwe kwa utaratibu mwafaka
      6. Kimalizio
    2. Mwili/ Maudhui
      Yaliyomo yashughulikiwe hapa:
      Mtahiniwa ajibu swali alililoulizwa kwa kujadili suala la ukiukaji wa sheria za shule na kupendekeza namna ya kuukomesha.
      Baadhi ya hoja za kuzingatia:
      1. Visa vya ukiukaji wa sheria
        • matumizi mabaya ya dawa
        • matumizi mabaya ya mtandao wa intaneti
        • mahusiano yasiyofaa, kwa mfano, usagaji na ubasha
        • matumizi ya simu tamba(rununu)
        • kutoroka shule
        • kutowaheshimu wakuu
        • baadhi kutozingatia usafi wa mwili na mazingira
        • kuzorota kwa utenda kazi darasani. Kwa mfano baadhi kutofanya mazoezi/ kazi wanayopewa na walimu
        • udanganyifu katika mtihani na majaribio endelevu
        • kuwanyanyasa wanafunzi wenzao
        • kujitenga katika makundi ya kijamii na kiuchumi
      2. Sababu za kukiuka sheria
        • ukosefu wa mawasiliano kati ya wanafunzi na usimamizi wa shule
        • sheria zisizowapa wanafunzi uhuru/ sheria kandamizi
        • uongozi dhalimu
        • ukosefu wa uwajibikaji wa uongozi
        • athari za dawa za kulevya
        • shinikizo la marika
        • matatizo ya wanafunzi kutoshughulikiwa/ wanafunzi kuhisi hawashughulikiwi
        • vielelezo vibaya kutoka kwa wanajamii kuhusu usuluhishaji wa migogoro.
      3. Namna ya kukomesha hali hii
        • wanabaraza kuwa kiungo kati ya wanafunzi na uongozi wa shule
        • kuimarishwa kwa mawasiliano kati ya wanafunzi na walimu/ uongozi wa shule
        • kuimarishwa kwa ushauri marika
        • uongozi kumjali mwanafunzi
        • wanabaraza kufanya mikutano mara kwa mara na wanafunzi ili kuwaelezea sera za shule
        • baraza kushiriki katika vita dhidi ya matumizi ya dawa za kulevya
        • sheria za shule kuchunguzwa upya mara kwa mara ili kubadilisha vipengele ambavyo huenda vikahisika kumnyanyasa mwanafunzi
        • kuwahusisha wanafunzi katika kutoa mapendekezo kuhusu utatuzi wa matatizo yao.

          Tanbihi
          1. Sehemu nne kuu za kumbukumbu zijitokeze kama ifuatavyo:
            1. Kichwa/ anwani
            2. Mahudhura/ mahudhurio
              Yaanze kwa walio na cheo, kama vile Mwenyekiti wa Baraza, Katibu wa Baraza
            3. Ajenda
              Ziorodheshwe kwa kufuata kielekezi kifuatacho:
              1. Kufunguliwa kwa mkutano/ wasilisho la mwenyekiti
              2. Kupitia kumbukumbu za mkutano uliotangulia/ kusomwa na kuidhinishwa kwa kumbukumbu za mkutano uliotangulia
              3. Yaliyoibuka/ yaliyotokana na kumbukumbu hizo (baadhi ya hoja zinaweza kujadiliwa hapa). Ubunifu wa mtahiniwa unaweza kuanza kukadiriwa hapa
              4. Ripoti kuhusu shughuli za mwezi (hoja nyingine zijadiliwe pia/ visa vya ukiukaji wa sheria za shule)
              5. Visa vya ukiukaji wa sheria za shule
              6. Mchango wa Baraza katika kukabiliana na visa hivi
              7. Masuala mengineyo/ shughuli nyinginezo
                (mtahiniwa ataibuka na ajenda yake, mradi ihusiane na swali)
            4. Kumbukumbu zenyewe
              Matukio yaandikwe kwa utaratibu wa nambari.
              Kila hoja inayojadiliwa inakiliwe kama suala (kipengele kinachojitegemea). Mifano ifuatayo inaweza kukubaliwa:
              1. Kumb. 1/10/2012: Kusomwa na kuidhinishwa kwa kumbukumbu za
                                            mkutano uliotangulia
              2. Kumb. 2/10/2012: Matumizi mabaya ya dawa
              3. Kumb. 3/10/2012: Ripoti ya matukio ya mwezi uliopita n.k.
            5. Kimalizio
              • Ataje saa za kumalizika kwa mkutano.
              • Nafasi ya sahihi na majina ya mwenyekiti na katibu ionyeshwe
              • Nafasi ya tarehe iandikwe.
          2. Kaida nyingine zote za usahihishaji wa karatasi hii zitumike.
          3. Huenda mtahiniwa asiibuke na visa, sababu na namna ya kusuluhisha. Akadiriwe kulingana na namna anavyojieleza, mradi hoja imekamilika.
  2. Hii ni insha ambayo inamhitaji mtahiniwa kufafanua/ kujadili mawazo yake au mwelekeo wake kuhusu nafasi ya vijana katika utangamano wa kijamii.

    Baadhi ya hoja:
    • Vijana ndio wengi hivyo wanaweza kuwafikia raia wengi.
    • Vijana wanathaminiana na kuaniminiana, kwa hivyo ni rahisi kuwashawishi wenzao kutangamana.
    • Ikiwa vijana watafunzwa maarifa/ mbinu ishi za kukabiliana na matatizo/ changamoto, wataweza kuziwasilisha mbinu hizi kwa wenzao.
    • Ni muhimu vijana kuepuka kutumiwa na viongozi kama vyombo vya kuvulia na kupalilia uhasama miongoni mwa raia.
    • Kwa kuwa kundi la vijana ndilo lenye nishati zaidi, linaweza kutumia nishati hii katika shughuli zinazoleta utangamano kama vile michezo.
    • Vijana wanaweza kujisajili katika vyuo vilivyo katika maeneo mbalimbali nchini ili kutagusana na raia wa makabila tofauti tofauti.
    • Vijana wanastahili/ wanaweza kutumia lugha yao (kwa mfano sheng) kama kiungo cha kuwaunganisha na kueneza hisia za kizalendo.
    • Vijana wanaosajiliwa katika vikosi vya ulinda usalama wanaweza kueneza siasa/ sera ya kudumisha usalama kwa njia ya amani badala ya vita.
    • Vijana wanaweza kukomesha ubaguzi wa kikabila na kinasaba kwa kuhimizana kuchagua viongozi kutoka makabila mbalimbali ili kupalilia mwelekeo wa kitaifa badala ya ule wa kieneo, kikabila au kinasaba.
    • Kushiriki katika shughuli za kiusomi kama vile makongamano kunawawezesha vijana kuja pamoja na kujihisi kama raia wenye maazimio sawa, hivyo kuhimiza mshikamano.
    • Mshikamano unaweza kudumishwa kupitia ndoa za mseto. Kwa vile vijana wengi si wahafidhina, wengine wao wanaoa na kuolewa na wenzi kutoka makabila tofauti. Uhusiano huu unaunga udugu na kupalilia mshikamano.
    • Mradi wa kazi kwa vijana kwa mfano, uliwaleta vijana wa usuli tofauti pamoja.

      Tanbihi
      1. Mtahiniwa anaweza kuchukua mwelekeo wa kuonyesha mambo ambayo vijana wanaweza kufanya ili kuleta mshikamano wa kitaifa. 
      2. Mtahiniwa anaweza pia kuonyesha/kujadili hatua ambazo vijana wamechukua kuleta mshikamano wa kitaifa.
      3. Mtahiniwa anaweza pia kuchanganya mielekeo yote miwili, akataja hoja na kuitolea ufafanuzi kwa kuonyesha hatua ambazo vijana tayari wamechukua kuhusiana na suala hili.
  3. Maana ya methali
    Chombo ambacho kimepangiwa kuzama/ ambacho kina kasoro na kinaweza kuzama, hata kikiendeshwa na nahodha wa aina gani kitazama tu.
    Jambo la kuharibika hata ukalishughulikia vipi litaharibika tu.
    Jambo likiisha kuharibika hata ukajaribu kulirekebisha haitawezekana.
    Ruwaza zifuatazo za masimulizi zinaweza kujitokeza.
    1. Mtahiniwa amsawiri msimulizi/ mhusika ambaye anapuuza jambo hadi pale linapoharibika kisha akaanza kulirekebisha. Msimulizi asidiriki kurekebisha jambo hilo. Kisa kibainishe athari mbaya za kutorekebisha jambo mapema.
    2. Mtahiniwa abainishe hali ambapo licha ya juhudi za mhusika kurekebisha jambo/ kujiimarisha, hafanikiwi. Hapa ni kama jaala inampiga chenga. Mtahiniwa anaweza kuonyesha hiyo ndiyo jaala/ hayo ndiyo majaliwa ya mhusika.
    3. Mtahiniwa anaweza kuandika kisa kinacholenga kuonyesha umuhimu wa kuyarekebisha mambo kabla ya kuharibika kiasi cha kuzidi uwezo wa mhusika kuyarekebisha.

      Tanbihi
      Masharti ya usahihishaji wa insha za methali yazingatiwe.
  4. Mtahiniwa aandike kisa kinachofungamana na mwanzo aliopewa. Hali zifuatazo zinaweza kujitokeza katika kisa:
    • Mhusika/ msimulizi amesafiri kwa siku kadha, na ndio anapata fursa ya kupumzika. Anaamshwa na hawezi kuamka.
    • Msimulizi anaweza kuwa awali alikuwa katika hali ya hatari, pengine kutekwa nyara na sasa ameokolewa, anajaribu kuamka na hawezi.
    • Huenda mhusika/ msimulizi ni muwele hospitalini, anaamshwa na daktari kuhojiwa.
    • Msimulizi anaweza kuwa awali alikabiliwa na mgogoro au changamoto iliyompa wasiwasi na kumkosesha usingizi kwa muda.

      Kwa vyovyote vile, kisa lazima kionyeshe hali ambayo inasababisha kulimbikiza kwa usingizi na uchovu na msukumo au kichocheo cha kuyafumbua macho.

      Tanbihi
      Masharti mengine yote ya utunzaji wa alama katika maswali yote yafuatwe kulingana na kielelezo cha usahihishaji wa insha (mwongozo wa kudumu).
Join our whatsapp group for latest updates

Download KCSE 2012 Kiswahili Paper 1 with Marking Scheme.


Tap Here to Download for 50/-




Why download?

  • ✔ To read offline at any time.
  • ✔ To Print at your convenience
  • ✔ Share Easily with Friends / Students


Get on WhatsApp Download as PDF
.
Subscribe now

access all the content at an affordable rate
or
Buy any individual paper or notes as a pdf via MPESA
and get it sent to you via WhatsApp

 

What does our community say about us?

Join our community on:

  • easyelimu app
  • Telegram
  • facebook page
  • twitter page
  • Pinterest