MASWALI
- UFAHAMU: (Alama 15)
Soma kifungu kifuatacho kisha ujibu maswali.
Afisa wa ukaguzi wa abiria na mizigo alimrudishia cheti chake cha usafiri na kubofya tarakilishi yake kuashiria kuanza kumhudumia mteja mwingine. Duma alikichukua cheti chake cha usafiri kwa pupa, kana kwamba anamtarajia mtu kuja kukibwakura. Moyo wake ulitweta na kukisukuma kidari chake kikembe nusura kukipasua. Baada ya kukihifadhi cheti hiki ndani ya mfuko wake mdogo wa kusafiria, alichapuka moja kwa moja hadi chumbani ambamo wasafiri hungojea kuiva kwa safari.
Si kwamba Duma ni mwanagenzi wa safari za Ughaibuni. La! Hasha. Amekia vilele vya anga kwa muda wa miaka isiyopungua kumi sasa, tangu alipochukuliwa kijijini mwao alipokuwa na miaka kumi na miwili; mjomba wake anakuja kumtafutia kazi. Kazi aliyopata ilimtia tumbo joto mwanzoni, akataka kutoroka, atokomee kokote kule. Fikiria wewe, ndio sasa umetoka kwenye mbeleko ya mama yako, ubwabwa wa shingo ndio unaanza kukutoka, kisha uje kutoswa kwenye kazi ya kuvuna majani kwenye shamba kubwa la Bwana Mali, majani ambayo unapopata fursa ya kuyatafuna yanakufanya kujihisi kama tiara inayoelea angani! Kisha baadaye upagazwe kazi ya kuyauza majani hayo hayo, pamoja na unga unaohifadhiwa katika vifuko vidogo vya kuvutia, kwenye soko la siri na hata shuleni! Hata hivyo walisema wasemao kwamba papo kwa papo kwamba hukata jiwe, na kinolewacho hupata.
Duma alipata walimu, akafunzwa jinsi ya kuyatumia majani na aina mbalimbali za unga ili kuituliza nadhari ya dhamiri yake ambayo awali ikimsumbua sana. Polepole ule utu na ulimbukeni aliokuwa nao uliyeyuka, akatwaa moyo wa jiwe na kuikumbatia kazi hii kwa dhati ya moyo wake, moyoni akijiambia kuwa hayo ndio majaliwa yake. "Ikiwa hii si utashi wa Mungu, kwa nini akalituma gonjwa kuwaua wazazi wangu, mmoja baada ya mwingine? Kwa nini akawaacha akina ami kunipoka kidogo kilichobakizwa na matibabu ya wazazi wangu? Kwa nini asitume mtu kuja kuniokoa nilipoingizwa kwenye biasharia hii na mjomba Papa?" Duma alijiuliza maswali haya mfululizo. Hatimaye aliihalilisha kazi yake kwa kusema, "Kazi mbi si mchezo mwema."
Dunia alipopata tajiriba ya kutosha kupambana na walinda usalama wenye macho ya kipanga, mwajiri wake hakusita kumtumia kwenye safari za kusafirisha shehena kwenye masoko ya ng'ambo. Mara nyingi aliponea tundu la sindano kutiwa mbaroni. Wakati mwingine mashine za ukaguzi ziliweza kunusa shehena yake, akalazimika kulainisha viganja vya maafisa wakuu forodha. Kila mara alijiambia, "Hii kazi ni hatari, nikipata pesa za kutosha kuufukuza uhawinde nitang'atuka." Hata hivyo, Duma alikuwa tayari alikwisha kuwa sikio la kufa. Alikuwa amedidimia katika ulanguzi wa dawa za kulevya, ulanguzi ambao ulikuwa umemwingia kwenye mishipa jinsi dawa zenyewe zilivyokuwa zimegeuka damu inayosukuma moyo wake. Badala ya kuacha, yeye na mwajiri wake walizua mikakati mipya ya kusafirisha shehena.
Safari ya leo ilipoiva, Duma alifanya kama alivyoagizwa na mwajiri wake. Asubuhi na mapema alibugia shehena yake, koo ikakubali kuisafirisha hadi tumboni ambapo uchango wake uliomba kuihifadhi hadi utakapofika wakati wa kuitapika shehena hiyo Ughaibuni. Fungu lililobaki lilitiwa ndani ya begi la kusafiria, katikati ya nguo. Duma alitarajia kwamba atapata jamaa wake wa kawaida kwenye forodha. Akajiambia kwamba hata asipompata huyo jamaa anaweza kuitoa shehena hiyo hiyo kama kafara kwa maafisa wa usalama. Duma alikuwa na bahati ya mtende kumpata huyo jamaa wake, pamoja na afisa wa usalama aliyejuana naye kwa vilemba, akafanikiwa kupitisha shehena zake bila kujua kuwa yake ya arubaini imefika.
Mara tu Duma alipotua kwenye uwanja wa ndege wa Kamata, Polisi wa Kimataifa walimzingira. Mimwero ya kamera za wanahabari ilitishia kuyapofua macho ya mtumwa huyu ambaye alikuwa sharti auwawe kwa kukubali kutumwa. Vikuku viwili vikubwa vilivirembesha viwiko vya mikono yake ambayo aliikabidhi kwa maafisa hawa kama anayekubali kuwajibikia kosa lake. Nchini mwake mwajiri wake alipiga kidoko alipotazama kadhia hii kwenye runinga. Akasema, "Bloody coward! How can he allow himself to be caught?"
- Huku ukitoa mifano mitano, onyesha jinsi haki za binadamu zililivyokiukwa katika kifungu hiki. (alama 5)
- Andika vyanzo vinne vya maovu ya kijamii kwa mujibu wa taarifa. (alama 4)
- "Yaliyompata Duma ni mwiba wa kujichoma." Thibitisha kauli hii kwa kutoa mifano minne. (alama 4)
- Eleza maana ya msamiati ufuatao kulingana na kifungu:(alama 2)
- wenye macho ya kipanga
- zimegeuka damu inayosukuma moyo wake
-
UFUPISHO: (alama 15)
Soma kifungu kifuatacho kisha ujibu maswali.Suala la jamii kujitosheleza wa mahitaji ya chakula na lishe ni jambo ambalo halina budi kushughulikiwa kwa dhati. Chakula ni mojawapo ya mahitaji ya kimsingi ya binadamu na kila mja ana haki kupata chakula, na si chakula tu, bali chakula chenye virutubisho muhimu. Nchi isiyowakimu raia wake kwa chakula ni sawa na ng'ombe aliyeshindwa kumnyonyesha ndama wake.
Kwa muda mrefu, viongozi wamekuwa wakipambana na tatizo la ukosefu wa chakula. Msimu wa kiangazi unapobisha hodi, watu wengi, hasa wale wahitaji, hupukutika kutokana na mng'ato wa njaa. Japo serikali na wafadhili hutuma vyakula vya msaada kwa jamii zilizoathirika zaidi, chakula hiki huwa kama nguo ya kuazima, na bila shaka ya kuazima haikidhi haja.
Mojawapo ya vyanzo vikuu vya uhaba wa chakula ni kiwango cha chini cha uzalishaji na uhifadhi wa chakula chenyewe. Zipo sehemu nyingi nchini ambazo ni kame. Sehemu hizi hukabiliwa na ukosefu wa maji kwani, ama mvua hainyeshi, au inaponyesha haitoshelezi mahitaji ya mimea. Mimea mingi hujikaukia ikiwa michanga ya kudhihaki juhudi za wapanzi. Zipo sehemu katika nchi hii ambazo huenda kwa misimu hata zaidi ya mitano bila kupata zao lolote kutoka mashambani. Hali ikiwa hivi makali ya uhitaji huzidi na wakazi wa sehemu hizi hulazimika kuwa wategemezi kwa majirani na serikali. Wengine wakikosa chakula huazimia kula visivyoliwa. Wanaamwa la mbwa baada ya kukosa la mama.
Hali kadhajika, japo zipo sehemu nyingine ambazo hazina tatizo la ukame, mbinu hasi za kilimo husababisha utoaji wa mavuno haba, hivyo kutojitosheleza kwa chakula. Bila shaka wanapopanda ovyo, wanavuna ovyo. Kuna wakulima ambao hupalilia mmomonyoko wa udongo kwa kulima kandokando ya mito, kupanda zao lile lile katika sehemu ile ile ya ardhi miaka nenda miaka rudi, na kutopanda mimea ambayo hukinga tabaka la juu ya udongo dhidi ya kumomonyelewa na maji au upepo. Matokeo ya haya yanaweza kutabiriwa; udongo wenye rutuba huoshwa na mashamba kutwaa utasa ambao huzidisha kuzalishwa kwa chakula haba. Wakulima wengine hukaidi wito wa kupanda mimea ambayo hustahimili ukame kama vile mibaazi, mihogo, mtama, ulezi na wimbi. Baadhi ya wafugaji hufuga mifugo wengi ambao hushindwa kustahimili kiangazi. Si ajabu kupata kwamba katika baadhi ya maeneo, mizoga ya ng'ombe na hata ngamia imezagaa kote, tanuri la kiangazi linapofanya kazi yake.
Sehemu nyingine zimebarikiwa kwa ukwasi wa chakula. Hata hivyo, baadhi ya wakazi wa sehemu hizi hawana mwao kuhusu umuhimu wa lishe bora. Wapo wanaodhani kuwa chakula ni chakula, bora tumbo lipate haki. Hawa hula vyakula kama vile viazi, mahindi, na wengine nyama bila kujua wanahitaji vyakula vyenye virutubisho muhimu, yaani, wanga, protini, vitamini na madini. Wapo wanaodhani proteni pekee ni nyama. Hawa hula nyama mawio na machweo, matokeo yakiwa kuambulia magonjwa kama vile shinikizo la damu.
Katika kukabiliana na tatizo la uhaba wa chakula, serikali, kupitia wizara husika, imeanzisha miradi ya kuhakikisha kuwa kuna uzalishaji wa chakula kwa kiwango cha kuridhisha. Visima vya maji na mabwabwa yamechimbwa katika sehemu kame ili kunyunyuzia mashamba maji. Baadhi ya wakulima wameanza kupanda mimea ambayo inapevuka na kutoa mazao haraka. Ipo mimea ya kuatika ambayo hutoa matunda baada ya muda mfupi, hivyo kusaidia kupunguza makali wa njaa. Wafugaji wengine wameanzisha miradi ya kufuga kuku wa kututumuliwa. Hawa hukua na kukomaa kwa muda mfupi na huweza kutoa nyama na mayai. Wafugaji wa kuku hawa huweza kuwauza kununua aina nyingine ya vyakula.
Wakulima pia wanahimizwa kutumia njia za kisasa za kuzalisha na kuhifadhi chakula. Chakula kinapohifadhiwa vyema, hata mvua isiponyesha, raia huweza kujitegemea. Ikiwa maghala ya halmashauri ya kuhifadhi chakula nchini hayahifadhi chakula, mara nyingi nchi hulazimika kuagiza chakula kutoka nje kiangazi kinapoajiri. Aidha, chakula kisipohifadhiwa vyema huishia kuharibika na kuhasiri wanaokila, ikawa msiba juu ya mwingine.
Ni muhimu kufahamu kuwa jukumu la kupambana na ukosefu wa chakula ni la kila raia. Hali ya kungojea kila mara kulishwa na serikali inatufanya kuwa wategemezi zaidi. Wakulima wadogowadogo ambao huuza vyakula vyao kwa bei ya chini sana mara tu wanapovitoa mashambani wanapaswa kujiasa dhidi ya mazoea haya na kujua kuwa akiba haiozi. Wanaoishi katika sehemu zenye vinamasi wasaidiwe kuzitunza sehemu hizi na kuzitumia kwa njia endelevu. Vijana wahimizwe wawaunge wazee mkono kushughulikia kilimo katika sehemu za mashambani badala ya kuhamia mjini kutafuta kazi za ajira ambazo ni haba. Wanaoishi mjini nao wajifunge nira kutumia nafasi walizo nazo kuendeleza kilimo cha bustani.
- Fupisha ujumbe wa aya tano za kwanza kwa maneno 100 (alama 9,1 ya mtiririko)
- Kwa kurejelea aya tatu za mwisho, eleza njia sita za kukabiliana na uhaba wa chakula. (maneno 85) (alama 6, 1 ya mtiririko)
-
MATUMIZI YA LUGHA: (Alama 40)
- Eleza maana ya silabi. (alama 2)
- Andika neno lenye muundo ufuatao: (alama 1)
irabu + konsonanti + irabu
- Ainisha vitenzi katika sentensi: (alama 3)
Ndege yu taabani, hata hivyo anajaribu kujinasua. - Geuza sentensi ifuatayo kwa kufuata maagizo.(alama 2)
Wachezaji hawakucheza mpira kwa sababu ya mvua.
Anza kwa: Mpira - Andika sentensi ifuatayo katika wakati ujao hali timilifu.
Dobi huwapigia watu nguo pasi. (alama 2) - Andika sentensi ifuatayo upya ukizingatia kinyume cha maneno yaliyopgiwa mstari. (alama 2)
Ubora wa kazi zao ulifichuka baada ya kuanzishwa kwa mradi ule. - Eleza maana ya kirai. (alama 2)
- Ainisha virai vilivyopigiwa mstari. (alama 1)
Zana hizi zimeundwa na mafundi wenye stadi mkubwa.
- Kinga ni hali ya kuzuia madhara fulani. Andika maana nyingine mbili za 'kinga'. (alama 2)
- Changanua sentensi ifuatayo kwa kielelezo cha matawi. (alama 2)
Lililimwa vizuri sana. - Bainisha maana mbili zinazojitokeza katika sentensi ifuatayo: (alama 2)
Wakimbizi walisema kuwa walitamani kurudi kwao mwaka huo. - Eleza maana mbili za sauti ifuatayo: dh. (alama 2)
- Andika sentensi ifuatayo katika umoja. (alama 2)
Hao wenyewe hawakuzingatia mafunzo ya lishe bora. - Tunga sentensi moja kubainisha tofauti ya kimaana kati ya gharama na karama. (alama 2)
- Kanusha sentensi ifuatayo: (alama 2)
Wanafunzi waliingia darasani, wakatoa vitabu wakaanza kusoma. - Tunga sentensi mbili kuonyesha matumizi mawili tofauti ya nukta pacha. (alama 2)
- Tumia nomino ya jamii kuwakilisha maneno yaliyopigiwa mstari. (alama 1)
Nzige wengi sana walivamia na kuharibu mimea. - Onyesha visawe vya maneno yaliyopigiwa mstari. (alama 2)
Washiriki wote walituzwa medali baada ya mchuano huo. - Nomino zifuatazo ziko katika ngeli gani? (alama 1)
- Furaha...
- Nyasi.......
- Uganisha sentensi hizi ukitumia kiunganishi cha kinyume. ( alama 2)
Wananchi walikabiliwa na hatari.
Wananchi waliendelea kuwaokoa majeruhi. - Andika upya sentensi ifuatayo ukianzia kwa yambwa tendwa. (alama 2)
Wafugaji waliwakatia ng'ombe wote majani ya mti huo.
-
ISIMU JAMII: (Alama 10)
- Umepewa jukumu la kuwazungumzia vijana wenzako kuhusu umuhimu wa uwekezaji. Fafanua sifa tano za lugha utakayotumia. (alama 5)
- Eleza sifa tano za sajili ya kidini. (alama 5)
Mwongozo wa Kusahisha
-
-
- kutengwa na mazingira ya nyumbani
- kudhulimiwa mali na jamaa za wazazi
- ajira ya watoto - Duma kutumikishwa shambani
- kudidimizwa katika ulanguzi wa dawa
- kusababishiwa uraibu wa dawa
- wasiwasi - Duma akiwa mchanga kujazwa wasiwasi / woga
- badala ya mwajiri kumwonea Duma imani, anamshutumu kwa kushikwa
- kuhatarishiwa afya kwa kuhitajika kuzimeza dawa ili kuzisafirisha ughaibuni
- kukatiziwa malezi - anatolewa nyumbani akiwa mchanga / kabla ya ubwabwa wa shingo kumtoka
- kuumbuliwa kwa moyo utu /kufanywa kuwa na moyo mgumu /usugu / ugumu wa moyo
- kusababisha matumizi ya dawa shuleni.
- kumfanya kuwa mvunja sheria / kumhusisha katika ufisadi.5 x 1 = 5
-
- Magonjwa - wazazi wa Duma wanatumia pesa nyingi kwenye matibabu; wanamwacha mnyonge hivyo kuwa windo rahisi la uraibu na ulanguzi wa dawa.
- Uyatima - Duma anakosa walezi hivyo kutoswa kwenye ulanguzi.
- Tamaa - jamaa za Duma wanampoka mali kutokana na tamaa. Duma anaingilia ulanguzi wa dawa kwa sababu ya tamaa.
- Ufisadi - maafisa wa usalama wanapokea hongo na kuendeleza ulanguzi wa dawa zaidi.
- Uraibu wa dawa za kulevya unamfanya Duma kutojidhibiti, anaendelea kuzitumia na kuzilangua kwa kupata nguvu mpya / msukumo.
- Utoto/umri mbichi - unamfanya Duma kuwa windo Jepesi la mjomba Duma.
- Umaskini
- Marafiki/walimu - kumfunza Duma matumizi ya dawa.4 x 1 = 4
-
- Duma anakubali kuziuza dawa shuleni na sokoni.
- Duma anajaribisha kutumia dawa hadi kuwa mraibu sugu.
- Badala ya kuwajibika kubadilika Duma anajiona kuwa mtendwa.
- Anakubali kumeza dawa ili kuzisafirisha.
- Duma anahalalisha matendo yake, hivyo kutoyarekebisha.
- Duma anawahonga polisi aachiliwe, hivyo kudidimia zaidi katika maovu.
- Anashirikiana na mwajiri wake ili kuzua mbinu mpya za kuendeleza uhalifu; anakosa tahadhari na kuishia kukamatwa.
- Hata anapojiwa na wazo la kubadilika hatuoni akilifuatilia; analiahirisha. (ix) Tamaa inamfanya asingatuke kutoka kwenye uhalifu.4 x 1 = 4
Tanbihi
Baadhi ya watahiniwa wanaweza kujadili pande zote mbili wakatoa baadhi ya hoja za kupinga kama vile:- Duma anaingizwa kwenye biashara hii na watu waliomzidi ki-umri - mjomba Papa. (ii) Kupokwa kwa mali kulimfanya kutafuta mbinu za kujikimu.
- Hata hivyo, kwa vile swali linamhitaji kuthibitisha kauli hii, hoja za kuunga zichukue alama zaidi (alama 3), alama ya kupinga iwe moja (1).
-
- Wenye makini / waangalifu / walio macho kupambana na wahalifu
- Ndizo zinazomwendeshea maisha / amekuwa mraibu sugu /ndizo zinazompa msukumo wa kuendelea na uhalifu.
-
-
-
- Suala la kujitosheleza kwa mahitaji ya chakula linahitaji kushughulikiwa kwa dharura
- Kila binadamu anahitaji kupata chakula chenye virutubishi.
- Serikali inapambana na tatizo la chakula kwa kutoa misaada
- Wakati wa kiangazi wahitaji hasa hufa kutokana na njaa
- Kiwango cha chini cha uzalishaji na uhifadhi wa chakula husababisha ukosefu wa chakula.
- Ukosefu wa maji huzikumba sehemu kame kutokana na uhaba wa mvua.
- Ukosefu wa mvua huzua hali ya utegemezi.
- Wengine hula hata visivyostahili kuliwa.
- Mbinu hasi za ukulima huathiri utoaji wa mazao.
- Wakulima wengine hupalilia mmomonyoko wa udongo kwa kulima kando ya mito, kulima eneo lilelile na kutopanda mimea inayozuia mmomonyoko wa udongo.
- Baadhi ya wakulima kutopanda mimea inayostahimili ukame
- Wafugaji kufuga mifugo wengi wasiostahimili ukame na kusababisha vifo
- Watu kutojua umuhimu wa lishe bora8 x 1 = 8
mtiririko - 1
Jumla - 9
-
- Serikali imechimba visima na mabwawa katika sehemu kame ili kunyunyizia mashamba maji.
- Wakulima kupanda mimea ya kuatika inayokomaa haraka ili kukabiliana na njaa.
- Kufuga kuku wa kututumuliwa wanaoweza kuuzwa na kununua aina nyingine ya chakula.
- Wakulima kuhimizwa kutumia njia za kisasa za uzalishaji na uhifadhi wa chakula.
- Wakulima wadogowadogo wakome kuuza vyakula vyao kiholela .
- Wanaoishi kwenye vinamasi wavitunze na kuvitumia kwa njia endelevu.
- Vijana washauriwe kushughulikia kilimo mashambani.
- Waishio mijini watumie visehemu wanavyopata kuendeleza kilimo cha bustani. 5 x 1 = 5
mtiririko - 1
Jumla - 6
Au 6 x 1 = 6
-
-
-
- Silabi ni kipashio cha utamkaji ambacho hutamkwa kwa pamoja kama fungu moja la sauti. mf nda - ma ; katika : ndama (alama 2)
Au
Ni sauti moja au zaidi zinazotamkwa kama fungu moja la sauti / kama sauti moja.
Mf. o - a katika oa 2/0 - (alama 2) - afya enda upwa
anza anga igwa
ibra uzwa 1 x 1 = (alama 1)
- Silabi ni kipashio cha utamkaji ambacho hutamkwa kwa pamoja kama fungu moja la sauti. mf nda - ma ; katika : ndama (alama 2)
- yu - kitenzi kishirikishi / kishirikishi kipungufu
anajaribu - kitenzi kisaidizi
kujinasua - kitenzi kikuu3 x 1 = (alama 3) - Mpira haukuchezeka kwa sababu ya mvua nyingi.
au
Mpira haukuchezwa na wachezaji kwa sababu ya mvua nyingi. 2/0 - (alama 2) - Dobi atakuwa amewapigia watu nguo pasi. 2/0 - (alama 2)
- Udhaifu wa kazi zao ulifichuka kabla ya kusitishwa kwa mradi ule.
(Kumalizwa)
(Kukamilishwa)
(Kuhitimishwa)
(Kukomeshwa)( 1/2 x 4 = alama 2) -
- Kirai ni fungu la maneno ambalo hudokeza maana lakini maana hiyo si kamili. au Kirai ni fungu la maneno ambalo huainishwa kwa kuzingatia neno lake kuu. Kwa mfano, nomino ndilo neno kuu la kirai nomino.
-
- na mafundi - kirai husishi/kirai kihusishi. (alama 2)
- wenye ustadi mkubwa - kirai kivumishi / kirai vumishi (alama 1) 2x1 21 = 1
- Kinga ni jambo au dawa ya kujiepusha na madhara.
Kinga ni kipande cha ukuni chenye moto.
Kukinga ni kutayarisha bindo, mkono au chombo ili kupokea kitu. (1 x 2 = alama 2) -
(8 x 1/4= alama 2) -
- Wakimbizi ndio wanatamani.
- Watu wengine wanatamani.
- Wakimbizi watarudi nyumbani kwa wakimbizi.
- Watu wengine watarudi kwao (hao wengine).
- Watu wengine watarudi kwa wakimbizi.(2 x 1 = alama 2)
- dh + kikwamizwa / kikwaruzo
+ ghuna
+ menoni (2 x 1 = alama 2) - Huyo mwenyewe hakuzingatia funzo la lishe bora.4 x 21 =(alama 2)
- Maana zifuatazo zijitokeze:
Gharama- jumla ya bei ya kufanyia jambo/pesa zinazohitajika kufanya jambo.
- unalopoteza kwa kutozingatia maagizo.
Karama - kipawa kutoka kwa Mungu.2 x 1 (alama 2)
-
- Wanafunzi hawakuingia darasani wala hawakutoa vitabu wakaanza kusoma.
- Wanafunzi hawakuingia darasani, wakatoa vitabu na kuanza kusoma.
- Wanafunzi hawakuingia darasani na hawakutoa vitabu wakaanza kusoma. 2/0 - (alama 2)
- Nukta pacha
- Hutumiwa kutanguliza maneno halisi ya msemaji.
Mwalimu: Nawashauri msome kwa bidii.
Wanafunzi: Tunashukuru. - Hutumiwa kutanguliza maneno yaliyo kwenye orodha.
Alienda sokoni kununua: mapera, machungwa na papai. - Kutenga saa na dakika - saa 8 : 30
- Kutenga shilingi na senti: Shilingi 10:50
- Kutenga sura na mstari, Yohana 8:302x1
- Hutumiwa kutanguliza maneno halisi ya msemaji.
- Wingu la nzige
- Medali - nishani
Mchuano - Kinyang’anyiro, mchezo, mashindano, shindano, pigano. (2 x 1 = alama 2) -
- Furaha - 1 - 1 (alama 1) (ii) Nyasi - U - Z1/ Z1 (alama 1)
Tanbihi
Kuna baadhi ya watahiniwa ambao huenda wakatumia uainishaji wa ngeli unaozingatia viambishi awali vya nomino. Hawa pia watuzwe ipasavyo. Kwa mfano:- Furaha - N - N
- Nyasi - U - N / U - NY / N
- Furaha - 1 - 1 (alama 1) (ii) Nyasi - U - Z1/ Z1 (alama 1)
- Mf
- Wananchi waliendelea kuwaokoa majeruhi licha ya kukabiliwa na hatari.
- Pamoja na hatari iliyowakabili, wananchi waliendelea kuwaokoa majeruhi.
- Minghairi ya kukabiliwa na hatari, wananchi waliendelea kuwaokoa majeruhi.
Mifano mingine: hata baada ya, ilhali, lakini, bali, bighari ya, ila
- Majani ya mti huo yalikatiwa ng’ombe wote na wafugaji.
Yambwa (tendwa) (alama 2)
-
-
- Kaida ambazo zinadhibiti sifa za lugha katika mazungumzo haya ni:
- Mada - uwekezaji
- Umri / uhusiano - anawazungumzia vijana
- Utungo - ni hotuba / mazungumzo ya moja kwa moja / ushauri - nasaha/ mawaidha
- Muktadha - ni muktadha au hali rasmi kwani anatakiwa kutoa mazungumzo hayo.
Hoja zifuatazo zizingatiwe:- Lugha rasmi - kuhusu uwekezaji.
- Mtindo wa hotuba / mazungumzo ya moja kwa moja na hadhira / ushauri / mawaidha.
- Msamiati au istilahi za kibiashara - unaohusu uwekezaji, kama vile biashara, hisa, faida, gharama. n.k.
- Anaweza kutumia misimu ya vijana inapostahili ili kujinasibisha zaidi nao / kufanikisha mawasiliano.
- Kuchanganya ndimi, kwa mfano, kutumia Kiingeraza na Kiswahili; au hata sheng kwa kuiwekea mipaka pia.
- Matumizi ya sentensi ndefu-ni hotuba / ushauri.
- Anaweza kuishirikisha hadhira kwa kuiuliza maswali ya balagha, au kuwataka kutoa maoni.
- Lugha elekezi - inayoshauri kuhusu njia chanya za uwekezaji. Hapa matumizi ya kauli au sentensi agizi yatatawala.
- Lugha sanifu / lahaja sanifu itawale kwa vile huu ni utungo rasmi.
- Lugha inayotumia kauli shawishi ili kuwaonyesha umuhimu wa kuwekeza badala ya kutegemea ajira.5 x 1 = 5
-
- Msamiati wa kidini - kwa mfano, Jalali, Mungu, alleluia, amina.
- Lugha chakavu / lugha ya kale, kwa mfano, sama badala ya mbingu.
- Kunukuu vifungu kutoka kwenye msahafu - Biblia au Kurani ili kuwaaminisha waumini.
- Lugha yenye toni kali ya kutisha hasa unapohubiri ili kukashifu tendo hasi.
- Lugha inayohimiza / inayoshawishi kutenda mema
- Matumizi ya mafumbo, kwa mfano mbazi
- Kurudiwa kwa vifungu fulani, kwa mfano Sala ya Bwana, Neema ya Bwana Yesu, amin.
- Matumizi ya kweli kinzani / matumizi ya fantasia. Kusawiri mambo ambayo hayawezekani katika maisha ya kawaida.
- Lugha inayoibusha mhemko / jadhba. Mfano, Amina, Amina
- Majibizano; kwa mfano: “Bwana awe nanyi - awe pia nawe” “Bwana asifiwe - Amina”
- Matumizi ya vihisishi au nidaa kama vile ‘Ee’, - ili kuibua hisia mbalimbali
- Lugha inayojaza matumaini ya maisha mema. Mfano, ‘kabla hujazaliwa nilikujua.’
- Lugha inayomhimiza binadamu kuwa mtegemezi kwa Mungu, k.v. “Msaada wangu unatoka kwa Mungu...”
- Lugha inayoyasawiri maisha ya binadamu kama yanayodhibitiwa na nguvu asizo na uwezo kwazo. Hana lolote la kufanya kuhusiana na maisha yake. Kwa mfano, “Hata ukahuzunika vipi huwezi kuongezea hata pima moja kwenye maisha yako.”
- Kuchanganya ndimi - hasa katika mahubiri.
- Mtumizi ya viziada - lugha kama vile ishara za mikono na uso, na miondoko ya mwili ili kuhuisha uhubiri.
- Lugha ya kushauri au kuelekeza. Kwa mfano, ‘bisheni, nanyi mtafunguliwa.’
- Kutasfidi lugha ili kuondoa aibu. Kwa mfano, ‘kujua mwanamke’, badala ya kujamiiana. 5 x 1 = 5
- Kaida ambazo zinadhibiti sifa za lugha katika mazungumzo haya ni:
Download KCSE 2014 Kiswahili Paper 2 Questions with Marking Scheme.
Tap Here to Download for 50/-
Get on WhatsApp for 50/-
Why download?
- ✔ To read offline at any time.
- ✔ To Print at your convenience
- ✔ Share Easily with Friends / Students