Kiswahili Paper 3 Questions and Answers - Kakamega Evaluation Mock Exams 2022

Share via Whatsapp

MASWALI

SEHEMU A: FASIHI SIMULIZI.

  1. LAZIMA.
    Soma kifungu kifuatacho kisha ujibu maswali.
    Hawa wanifuatao wananicha,
    kwa ukoo wangu mtukufu
    kawa jadi yenye majagina
    wa mioyo na vitendo
    wananicha,
    Kwa kuwa wa kwanza kijijini
    kuvishwa taji
    kwa mabuku kubukua
    kwa kuwa jogoo wa kwanza
    kuwika kwenye anga za ilimu
    idhini nikakabidhiwa,
    ya tafiti kuendeleza
    mamlaka nikapewa
    ya kuwaza kwa niaba ya jamii.
    Hawa wanifuatao wananicha
    kwa kuweza
    kuvyaza mikakati
    ya kukabiliana na ulitima walonipagaza
    kwa ndoto zangu za ujana kuzima.
    1. Tambua kipera hiki cha fasihi simulizi. (alama 1)
    2. Kwa kurejelea kifungu hiki taja sababu tatu kwa jibu lako. (alama 3)
    3. Bainisha vipengele viwili vya kimtindo katika kifungu hiki. (alama 2)
    4. Eleza sifa sita bainifu za kipera hiki. (alama 6)
    5. Kipera hiki kinaendelea kudidimia katika jamii yako. Eleza hoja nne utakazotumia kuishawishi jamii yako kukinga hali hii. (alama 4)
    6. Fafanua umuhimu wa kipera hiki katika jamii. (alama 4)
  2. SEHEMU B : RIWAYA.
    A. MATEI: CHOZI LA HERI
    Jibu swali la 2 au la 3.
    “Maisha yangu yalianza kwenda tenge nilipojiunga na kidato cha pili. Unajua hali ya mtafaruku wa kihisia inayowapata vijana…”
    1. Eleza muktadha wa dondoo hili. (alama 4)
    2. Bainisha kipengele kimoja cha kimtindo katika dondoo hili. (alama 2)
    3. Fafanua umuhimu wa nafsineni katika kuijenga riwaya hii. (alama 4)
    4. Kando na nafsineni. Eleza jinsi maisha yalivyowaendea tenge vijana wengine katika riwaya hii. (alama 10)
  3.      
    1. Changanua mtindo katika dondoo hili. (alama 10)
      Maungo yake ambayo daima huwa mepesi yanahisika kuwa mazito kama nanga. Sauna anaingia jikoni na kujifunga kimori, tayari kuanza kuchoma mandazi. Mara moyo unaanza kumwenda mbio na vipapasio vya akili yake kusimama wima. Anajihisi kama anayetarajia kuanza kinyang’anyiro kikali cha upiganaji masumbwi. Kwa mbali anasikia mbisho hafifu langoni. Ghafla uso wake unakumbana ana kwa ana na polisi! Mara anasikia moyo wake ukimuambia, “Yako ya arubaini imefika,”
    2. Riwaya ya chozi la Heri inadhihirisha jinsi migogoro inavyojitokeza katika jamii. Thibitsha ukweli huu. (alama 10)
  4. SEHEMU C: TAMTHILIA
    P. KEA: KIGOGO.
    JIBU SWALI LA 4 AU LA 5.

    1. “Ni kiwandani ninakofanyia kazi; Majoka and Majoka ...wamewaua…”
      1. Eleza muktadha wa dondoo hili. (alama 4)
      2. Bainisha vipengele vitatu vya kimtindo katika dondoo hili. (alama 3)
      3. Fafanua sifa mbili za nafsinenewa katika dondoo hili. (alama 2)
    2. Eleza sababu tano za maandamano katika tamthilia ya Kigogo. (alama 5)
    3. Jadili umuhimu wa mandhari ya soko la chapakazi katika kuijenga tamthilia hii. (alama 6)
  5. Fafanua jinsi mwandishi alivyofaulu kutumia mbinu zifuatazo katika kuijenga tamthilia ya Kigogo.
    1. Kinaya. (alama 12)
    2. Jazanda (alama 8)
  6. SEHEMU YA D: HADITHI FUPI
    A.chokocho na D. Kayanda: Tumbo Lisiloshiba na Hadithi Nyingine.
    Jibu swali la 6 au la 7
    Salma Omar Hama: Shiobe inatumaliza’
    1. Changanua mtindo katika dondoo hili. (alama 10)
      Na sisi tunabaki kuwatazama na kusema; Hayatu! Na si kula tu. Kunywa na kunywa tena. Vyakula vyeupe vya rangi. Vitamu, vikali, vichachu. Baridi. Hayatu! lakini mpishi ni nani? Kwa kweli vimepikwaje? Kwa kuni? Makaa? Umeme? si vya kupikwa ni vya kurowekwa hadi vivunde, vioze na kunyunyizwa hata uvundo? Aah! wenye midomo washasema “Usimchunguze bata utashindwa kumla!.
    2. Viongozi ndio wa kulaumiwa katika matumizi mabaya ya mali ya umma. Fafanua kauli hii kwa kurejelea hadithi fupi ya “Shibe Inatumaliza.” (alama 10)
  7. Onyesha namna mwandishi alivyoshughulikia maudhui yaliyo kwenye mabano katika hadithi zifuatazo.
    1. Tulipokutana tena. (ukiukaji wa haki za watoto) (alama 14)
    2. Mtihani wa maisha (Elimu). (alama 6)
  8. SEHEMU E: USHAIRI.
    Soma shairi lifuatalo kisha ujibu maswali.
    Ngakua na mto, ya kuonea
    Ngalisana kito, cha kuchezea
    Kilicho kizito, cha kuelea
    Kikamuenea, akivae.
    Makusudi yangu, Ngaliandaa
    Ngafinyanga chungu, cha mduwaa
    Ngatia vitangu, vinavyong’aa
    Ili ziwe taa, kwa apikae.
    Mkungu wa tano, wa mduwara
    Ulo bora mno, kisha imara
    Ulo na maono, kuwa ni dira
    Kwenye barabara, itindiae
    Ngaomba baraka, kwake Rabana
    Punje za nafaka, kila aina
    Chunguni kuweka, kwa kulingana
    Hajaangu suna, yule alae.
    Ngalifanya bidii, kwenda mwituni
    Sio kutalii, kukata kuni
    Ya miti mitii, huko jikoni
    Isio na kani, ni iwakae.
    Kwa yangu mabega, nikathubutu
    Ngabeba mafiga, yalo matatu
    Bila hata woga, kwenye misitu
    Simba tembo chatu, sinitishie.
    Miti yenye pindi, na jema umbo
    Ngajenga ulindi, mwema wimbombo
    Fundi aso fundi, penye kiwambo
    Moyo wenye tambo, apekechae.
    Singaajiri, ngachimba mimi
    Kisima kizuri, cha chemichemi
    Maji ya fahari, ya uzizimi
    Jua la ukami, siyaishae
    Tamati nafunga, kwa kuishia
    Mato ndo malenga, kanikimbia
    Nahofu kutunga, mabeti mia
    Asije chukia, ayasomae.
    1. Fafanua ujumbe wa shairi hili. (alama 2)
    2. Kwa kurejelea ubeti wa pili, eleza umuhimu wa aina mbili za uhuru wa kishairi alioutumia mshairi. (alama 4)
    3. Andika ubeti wa saba kwa lugha nathari. (alama 2)
    4. Fafanua muundo wa ubeti wa nane (alama 2)
    5. Bainisha mbinu mbili za kimtindo katika shairi hili. (alama 2)
    6. Eleza aina tatu za urudiaji zilizotumiwa katika shairi hili. (alama 3)
    7. Fafanua aina mbili za taswira zinazojitokeza katika shairi hili. (alama 2)
    8. Eleza toni ya shairi hili. (alama 1)
    9. Bainisha nafsineni katika shairi hili. (alama 2)


MWONGOZO WA KUSAHIHISHA

  1.      
    1. Majigambo/vivugo. 1x1
    2.        
      1. Kwa ukoo wangu mtukufu, kwa jadi yenye majagina.
      2. Kuwa wa kwanza kijijini kuvishwa taji.
      3. Kuwa jogoo wa kwanza kuwika kwenye anga za ilimu.
      4. Kuweza kuvyaza mikakati ya kukabiliana na ulitima. 3x1
    3.        
      1. Takriri/uradidi- hawa, wanifatao, wananicha.
      2. Inkisari – walonipagaza – walilonipagaza
      3. Lahaja – ilimu
      4. Jazanda/stiara – kuwa jogoo wa kwanza kuwika. 2x1=2
    4.        
      1. Hutungwa na kughanwa na mhusika mwenyewe
      2. Kwa kawaida, hutungwa na kughanwa na wanaume.
      3. Hutolewa kwa nafsi ya kwanza kwa sababu anyejigamba ni mshairi mwenye.
      4. Huwa na usanii mkubwa. Anayehusika hutumia mfanano, sitiari na urudiaji.
      5. Mhusika hujitungia kivugo kufuatia tukio mahusisi katika maisha yake. Mfano kushinda vita, mchezo n.k.
      6. Huwa na matumizi ya chuku. Mhusika hujisifu kupita kiasi.
      7. Mhusika huweza kutaja usuli wake wa kina saba . Anahitajika kutaja na kusifu ukoo wake.
      8. Wahusika mara nyingi huwa walumbi au washairi wanaolewa kwa kina wanayoyasema. 6x1=6.
    5.        
      1. Kuridhisha fani yenyewe kwa vizazi vya sasa na vijavyo.
      2. kuzihifadhii kenye maandishi.
      3. Kuzifunza shuleni.
      4. Kizitamba mara kwa mara.
      5. Kuelimisha jamii kuhusu umuhimu wake.
      6. Kuandaa mashindano ya utambaji wa kipera hiki kutoka kizazi hadi kingine.
      7. kuzihifadhi kwenye video ili kuhifadhi sifa za uwasilishaji kama vile sauti. 4x4=4
    6.        
      1. Hukuza ubunifu. Mtu anavyotunga, majigambo mara kwa mara ndivyo anavyoimarisha uwezo wake wa kubuni mitindo mipya.
      2. Hukuza ufasaha wa lugha. Wahusika wengi huwa walumbi.
      3. Hudumisha utu na utambulisho wa mwanaume katika jamii kupitia mambo mbalimbali mfano vita.
      4. Ni nyenzo ya kufanya watu waheshimiwe. Hudumisha ari ya kufanya wanaume kutaka kuwa mashujaa. 4x1=4
  2.        
    1.        
      1. Msemaji – zahali
        Msemewa/wasemewa- umu, kairu, mwanaheri, chandachema.
        Mahali – kwenye bweni katika shule ya Tangamano.
        Sababu – Ni baada ya zohali kusimuliwa utambaji wa marafiki zake kuhusu hali yao ya maisha ambao ulimchochea na kwatolea wenzake duku duku lake. 3x1=4
      2. Nahau – kwenda tenge. 1x2=2
      3.      
        • Anajenga tabia za wahusika wengine. Mfano babake ni katili.
        • Anajenga ploti. Usimulizi wake unatupa chanzo cha kuondoka nyumbani, kwenda mtaani na hatimaye katika wakfu wa mama Paulina.
        • Kupitia kwake tunaona changamoto zinazowakumba vijana. Anaambulia ujauzito katika umri mdogo na kusitisha masomo yake.
        • Anaonyesha dhiki za familia za mitaani. Yeye na wenzake wanalala kwenye barabara.
        • Anajenga maudhui ya malezi baada ya kupata ujauzito wazazi wake wanamtekeleza na anaamua kuondoka hadi mtawa wa pacha. 4x1
    2.      
      1. Umu- Anawapoteza wazazi wake (Lunga na Naomi) na kubaki kuishi kwa hisani ya mkuu wa shule/Hana kwao ambako atakuita nyumbani.
      2. Sauna – Anabakwa na babake wa kambo Bw. Maya, akapata ujauzito na baadaye kulazimishwa kuavya. Baadaye anaondoka nyumbani kwao kutamba na ulimwengu.
        Anahusika katika biashara haramu ya ulaguzi wa watotot na Bi. Kangara na baadaye kutiwa mbaroni.
      3. Hazina- anakosa wazazi wake. Hali hii inamfanya kuishi maisha ya taabu – omba omba karibu na kanisa la mtakatifu Fatima. Anavuta gudi na kutumia mihadarati.
      4. Kairu Pamoja na mamake walifurushwa kwao wasijue wanakokwenda.
        katika msitu wa mamba wanaishi maisha ya taabu. Babake alikataa kumlipia karo na kumfanya mamake kufanya vibarua ili kumtaftia karo.
      5. Mwanaheri- anapata malezi kutoka kwa mzazi mmoja babake. mamake anakufa kwa kunywa dawa (Subira) na kufa.
      6. Chandachema – Hakupata malezi ya wazazi wake, (Fumba na Rehema) na kuishi na nyayake aliyekuwa maskini na baadaye akafa.
        Anaamua kufanya kazi ya kuchuna chai ili apate pesa za kujilipia karo na mahitaji mengine.
      7. Dick – Baada ya kutekwa nyara na Sauna na baadaye kuuzwa kwa Buda, analazimishwa kufanya biashara haramu ya kuuza dawa za kulevya kwa kuhofia maisha yake.
      8. Shamsi – Baada ya kusoma hadi chuo kikuu anakosa kazi/ujira na mwishowe kuingilia ulevi.
      9. Kipanga – Baada aliyemdhania kuwa babake kumkana. Anaingilia ulevi wa Kangaa na kuponea kifo.
      10.    
        • Pete – Wazazi wake wanakosana kwa sababu pete hana mshabaha na babake mwishowe kumfanya kuishi na nyanyake.
        • Mamake hakujali maisha yake, alikosa mahitaji ya kimsingi ya shule.
        • anaozwa kwa buda mmoja mwenyewe wanawake wane akiwa darasa la saba mwishowe kutoweka katika ndoa hiyo. 10x1=10.
  3.      
    1.      
      1. Tashbihi- mazito kama nanga.
      2. Tashhisi – moyo unaanza kwenda mbio/vipapasio vya akili kusimama wima.
      3. Takriri – kama, kama
      4. Mdokezo wa methali – yako ya arubaini imefika
      5. Nidaa – polisi!.
      6. Tawira (Sikivu) – anasikia mbisho hafifu. 5x2=10
    2.        
      1. Kuna mgogoro katika familia ya mzee Mwimo Msubili. Wingi wa vinywa vya kulishwa ulizua uhasama.
      2. Mgogoro wa kijamii unajitokeza baada ya mkoloni kupuuza sera za mwafrika za kumiliki ardhi kibinafsi na kuidhinisha umiliki wa kijamii.
      3. Panatokea mgogoro shuleni wakati ridhaa aliiotwa ‘mfuata mvua” na kutengwa na wengine walimwona kama mwizi.
      4. Ridhaa alijipata katika hali ya mgogoro na nafsi yake. uk.12 miguu yake sasa ilianza kulalamika polepole, parafujo za mwili wake zililegea….baada ya muda wa mvutano wa hisia na mawazo, usingizi ulimwiba.
      5. Kuna mgogoro uliosababishwa na mwanasiasa juu ya nani atakaye kuwa kiongozi wa jamii, kati ya mwnanke na mwanaume.
      6. mgogoro kati ya raia na polisi wakiwa katika harakati zao za kuweka amani. Uk.19 ulio sababisha mamia ya watu kupoteza uhai.
      7. Lily Nyamvula anajikuta katika mgogogoro na nafsi yake, wakati ambapo imani yake inakinzana na kazi ya mumewe kuwa askari .
        Uk.62. 5x2=10
  4.      
    1.      
      1. Msemaji – siti
        Msemewa – sudi
        Mahali – Ni barazani mwa nyumba ya Sudi/katika nyumba ya Sudi alitaka kufahamu sababu ya maandamano ya wafanyakazi katika kiwanda cha Majoka.
        4x1=4
      2. Mdokezo – Majoka …wamewaua
        Taswira (oni) waliokuwa wakindamana.
        Takriri – Majoka. majoka.
        Kuchanganya ndimi – Majoka and majoka. 3x1=3
      3. Sudi
        Mtetezi wa haki – anadai kuwa ni jukumu la viongozi kuhakikisha soko ni safi.
        Mwenye bidii – Anachapa kazi ya kuchonga vinyago kwa bidii.
        Jasiri – anamuambia Kenga kuwa hawezi kuchonga kinyago cha ngao wanavyotaka. (Tathmini majibu ya mwanafunzi – sifa za sudi ni nyingi) 2x1=2
    2.        
      1. Kupanda kwa bei ya chakula katika kioski cha kampuni.
      2. Mazingira chafu. soko la chapakazi ni chafu na ilhali wachuuzi wanalipa kodi ya kusafisha.
      3. Mishahara duni. Walimu, Wauguzi wanashiriki maandamano kulalamikia mazingira duni ya kai pamoja na mishahara duni.
      4. Kufungwa kwa soko la chapalazi. Wachuuzi katika soko hili wanaandamana ili soko lifunguliwe.
      5. Mauaji ya watu bila hatia. Vijana watano ,wachuuzi sokoni wanauliwa bila hatia.
      6. Pesa za kusafisha soko zimefujwa na viongozi na kusababisha soko kutosafishwa.
      7. Wachuuzi kunyimwa haki zao. Wanafungiwa soko na kushindwa kuendelea kufanya biashara zao.
      8. Ukosefu wa ajira kwa vijana. Sudi, Tunu wamesoma hadi chuo kikuu lakini wanakosa kazi ya kufanya.
      9. Ufisadi – matumizi mabaya ya fedha/mali ya umma. mfano pesa za kusafisha soko zinafujwa. 5x1=5
    3.    
      1. Yanajenga sifa za wahusika mbalimbali. Mfano sudi kuwa mwenye bidii. Anafanya kazi ya kuchonga vinyago kwa ustadi.
      2. Yanajenga maudhui mbalimbali. Mfano uchafuzi na mazingira. soko ni chafu, taka, maji machafu yanayopita mtaroni.
      3. Yanaonyesha ukosefu wa uwajibikaji wa viongozi. Kodi inalipwa lakini soko halisafishwi.
      4. Yanajenga mbinu za lugha mfano uk.2 Nidaa Do!, mdokezo uk.3.
      5. Yanajenga ufaafu wa anwani “Kigogo”. Majoka anaamuru kipindi cha mwezi mmoja kusherehekea uhuru.
      6. Yanajenga ploti. Majoka anafunga soko, mkondo wa matukio unabadilika, wanasagamoyo wanaandamana. 6x1=6
  5.      
    1.      
      1. Habari zinazotolewa na mjumbe katika rununu ni za kinaya kuwa wanasagamoyo wasirudishe maendeleo nyuma bali wafurahie. ufanisi. Ukweli ni kuwa hakuna maendeleo
      2. Boza anadai kuwa kulipa kodi ni kujenga nchi na kujitegemea. Ni kinaya kwa vile kodi wanayolipa haitumiki kujenga nchi.
      3. Boza anamwambia Sudi kuwa wanatia doa kwa kila jambo nzuri. Ni kinaya kwa vile hakuna mambo mazuri ambayo majoka ameyafanya. (uk.5)
      4. Wanasagamoyo kusherehekea miaka sitini ya uhuru ni kinaya kwani hakuna cha muhimu kusherehekea.
      5. Majoka kudai kuwa takataka za soko zitaaribu sifa nzuri za jimbo la sagamoyo ni kinaya kwa vile hakuna sifa nzuri Sagamoyo.
      6. Kauli ya Husda kuwa Ashua ni kimada wa Majoka ni kinaya kwa vile Ashua hana nia yoyote na Majoka.
      7. Ni kinaya kwa polisi Sagamoyo kuwatawanya waandamaji. Polisi wanapaswa kulinda na kutetea haki za wananchi.
      8. Majoka kusema kuwa Sagamoyo wanajiweza ni Kinaya. Watu wana njaa. Sagamoyo yenye inapata ufadhili kutoka nje kwa miradi isiyo muhimu.
      9. Ni kinaya Kenga anapomwambia Majoka aache moyo wa huruma, Majoka hana huruma, anapanga mauaji.
      10. Ashua anasema kuwa katika jela kuna amani na amechoshwa na Sudi. Ni kinaya kwani Ashua anapata maumivu akiwa jelani.
      11. Madai ya Ngurumo nikinaya kuwa tangu soko kufungwa Sagamoyo ni pazuri mno. Watu hawana mahali pa kuuzia bidhaa.
      12. Ngurumo kusema kuwa pombe ni starehe ni kinaya kwani watu wanaangamia kutokana na pombe. 6x2=12
        JAZANDA.
    2.      
      1. Husda anamwambia Ashua kuwa hawezi kumtoa bonge kinywani hivhivi. Bonge ni Majoka bwanake Husda kuwa Ashua hawezi kumnyang’anya bwana.
      2. Husda kumwita Majoka, pwagu, pwagu ni mwizi na Majoka amewaibia wanasagamoyo; ananyakua ardhi, anaiba kodi. (uk 27)
      3. Husda anamwambia Ashua kuwa ameshinda kufuga kuku na kanga hatamweza. Kuku ni mumewe sudi, na kanga ni Majoka. (uk.28)
      4. Majoka anasema kuwa hatatumia bomu kuulia mbu. Anamrejelea Tunu kuwa mbu. (uk.35) maanisha kuwa hatatumia nguvu nyingi kumwangamiza.
      5. Siafu huwa wengi na si rahisi kuwamaliza. Siafu ni wanasagamoyo ambao ni wengi kuliko majoka na si rahisi kuwashinda. (uk.52)
      6. Tunu anasema kuwa moto umewaka na utateketea wasipouzima. Mto ni harakati za mapinduzi sagamoyo.
      7. Hashima anamwonya Tunu asijipeleke kwenye pango la joka. Pango la joka anarejelea majoka na watu wake ambao ni katili na wauwaji
      8. Kinyago cha mke mrembo shujaa anachochonga sudi kinaashiria Tunu ambaye ni shujaa wa kweli
      9. Jazanda ya marubani ambao hawaendeshi vyombo vyao vizuri ni viongozi ambao hawaongozi kwa haki.
      10. Chombo anachopanda Majoka kinaenda kinyume badala ya kwenda mbele, majoka hajafanya maendeleo sagamoyo kwa sababu ya ufisadi na tamaa. 8x1=8
  6.      
    1.      
      1. Nidaa – Aah!
      2. Tanakuzi – vitamu, vikali.
      3. Takriri/uradidi- Hayatu! hayatu!
      4. Swali balagha – mpishi ni nani?
      5. Taswira (muonjo) kunywa na kunywa tena. 5x2=10
    2.      
      1. Mzee mambo analipwa mshahara mnono kama mkuu wa wizara zote ilhali kila wizara ina waziri wake.
      2. Ubadilifu unadhihirishwa pale DJ anapolipwa kuwatumbuiza wageni katika sherehe.
      3. Uuzaji wa dawa zilizotolewa katika bohari la kitaifa katika duka la DJ ambayo ni biashara ya mtu binafsi ni ubadhirifu wa mali ya umma.
      4. Dj kupewa kazi ya mipango na mipangilio katika sherehe ilhali kuna mawaziri wawili wanaolipwa mshahara kwa kazi hiyo ni ubadhirifu wa mali ya umma.
      5. Vyakula katika sherehe vinanunuliwa kwa pesa za umma. Pesa hizi zingetumika kuendeleza asasi za kijami..
      6. Viongozi huendeleza ubadhirifu kwa kutumia mali ya serikali yanatumika katika sherehe na kazi za nyumbani kama vile kuleta maji katika sherehe.
      7. Sherehe kubwa za viongozi wa serikali zinatumia mali ya umma. Hivyo basi kuchangia ubadhirifu wa mali katika jamii.
      8. Ubadhirifu unadhihirishwa na viongozi wa serikali wanaochukua watu wa karibu na kuona kuwa wamefaidika kutokana na raslimali za wanajamii bila kuzitolea jasho.
      9. Upeperushaji wa matangazo ya sherehe ya kiongozi binafsi katika vyombo vya habari vya kitaifa siku nzima ni ubadhirifu wa mali ya umma. Pesa zilizotumika zingechangia pakubwa katika kuinua uchumi wa taifa.
      10. Viongozi wa serikali kama vile sasa Mbura wanaamua kujipakulia chakula kupita kiasi katika sherehe za mzee Mambo na jamii yake. Ubadhirifu wa mali ya umma unaonekana ambapo mali yaumma inatumika kuwaajiri mawaziri wawili wenye majukumu sawa katika wizara moja. Kazi hii ingefanywa na waziri mmoja na mshahara wa Waziri wa pili ungechangia katika kuinua sekta nyingine. 10x1=10
  7.      
    1. Tulipokutana Tena.
      1. Bi. Sinai kumnyima Bogoa uhuru wa kucheza na wenzake ila kwa kutoroka.
      2. Bi. Sinai Kumlazimisha Bogoa kwenda kuuza mandazi shuleni badala ya kusoma.
      3. Bogoa kupigwa na Bi Sinai alipopatikana akicheza na watoto wa majirani.
      4. Bi. Sinai kumchoma Bogoa viganja vyake kwa kutumia kijinga cha moto kwa kuyaacha maadazi yaungue.
      5. Bi. Sinai kumpa Bogoa makoko na makombo ya chakula, kulia vyunguni na sufuriani wengine wakila sahanini.
      6. Bi. Sinai kutompa Bogoa hata sekunde moja kuwa na wazazi wake.
      7. Bi. Sinai kumlazimisha Bogoa kufanya kila kitu alichoamrishwa kufanya. Kumenya vitunguu, maji, kuparia samaki, kuchanja kuni.
      8. Babake Bogoa kumtishia kuwa angempiga iwapo angekataa kwenda mjini.
      9. Wazazi wa Bogoa kumtoa nyumbani kwao na kumtelekeza kwa rafiki yao ambaye ni Bi. Sinai.
      10. Wazazi wa Bogoa kumdanganya kuwa akienda mjini anapelekwa shuleni, mavazi mazuri mwishowe hali haiwi hivyo. 7x2=14
    2. MTIHANI WA MAISHA.
      1. Wanafunzi wanaofeli katika mtihani hukata tamaa maishani na hata kutaka kujitoa uhai. Samueli anataka kuchupia bwawani kuepuka fedheha.
      2. Elimu ina gharama. babake Samueli anuza ng’ombe wote kumsomesha mwanawe.
      3. Wanafunzi kufedheheka wanapofeli mtihani wao. Samueli anatamani kuzibadilisha gredi zake duni.
      4. Wanafunzi wa shule za kutwa hulazimika kutembea masafa marefu kwenda shuleni. Samueli anatembea kilomita sita kila asubuhi kwenda shuleni.
      5. Wazazi hukasirika watoto wao wanapokosa kufaulu katika mtihani. Babake Samueli anakasirishwa na matokea duni ya mwanawe hata anampa kamba ya kujinyonga.
      6. Elimu pia huathiri uhusiano baina ya wanafunzi. Samueli anashuku uhusiano wake na mpenzi wake iwapo utaendelea kwa sababu yake kuwa na matokeo duni katika mtihani.
      7. Walimu wanakosa kuamini uwezo wa wanafunzi wao. Samueli anajua kuwa mwalimu mkuu hakuamini uwezo wake masomoni. (6x1=6)
  8.      
    1.      
      1. Shairi linazungumzia tatizo la upofu. mf. ngakuwa na mato.
      2. Kwamba mtu aliyepatwa na tatizo la upofu huwa hawezi kufanya mambo ambayo zamani aliyamudu bila tatizo.
        AU.
        Nafsineni inasikitikia hali ya kutomudu kujifanyia mambo kwa sababu ya upofu. 1x2= kutaja 1, kueleza 1
    2. Inkisari – imetumika ili kudumisha ulinganifu wa mizani, mfano: Ngaliandaa- ningaliandaa
      Ngafinyanga – ningalifinyanga
      Ngatia – ningetia
      Tabdila – imetumiwa ili kuleta urari na vina
      Mfano: Mduwaa – mduara
      apikae – apikaye
      vinavyong’aa – vinavyong’aa. 2x2=4 kutaja- 1, sababu 1
    3. Ningetumia miti iliyopinda na yenye umbo zuri kutengenezea kijiti. Ningekipekechea kijiti hiki kwenye tundu la wibombo mwema/mzuri kupekechea moto kwa ufundi mkuu kiwamboni. Ningekua bingwa ningekuwa na moyo shupavu na kupekecha moto/ningekuwa fundi stadi katika upekechaji wa moto. (2x1=1)
    4. Vipande viwili kila mshororo
      1. Mishororo minne
      2. Mshororo wa kwanza una mizani kumi, ilhali wa pili hadi wa nne una mizani kumi na moja. 2x1=2
    5.      
      1. Uradidi – ulo – ubeti 3
        mato – ubeti 1, 9
      2. Tashhisi – mato ndo malenga kanikimbia. 2x1=2
    6.    
      1. Urudiaji wa sauti – ubeti wa 1, a, a,
      2. Urudiaji wa silabi – ubeti wa 1 to, to, to
      3. Urudiaji wa maneno – ulo –ubeti wa 3
      4. urudiaji wa miundo sawa ya mistari
        ngalisana kito, cha kuchezea
        ngalifinyanga chungu cha mduwaa 3x1=3
    7. Taswira mguso – ngafinyanga chungu cha mduwa
      Taswira mwendo – ngafanya bidii, kwenda mwituni
      Taswira hisi – Nahofu kutunza, mahali mia, asije chukia ayasomae. 2x1=2
    8. Toni ya kuhuzunisha/masikito/kuhurumia/majuto
      Nafsineni inakosa/shindwa kufanya mambo mengi
      Maishani kwa sababu ya kukosa macho. 1x1=1
    9. Kipofu/mnyonge – asiye na uwezo wa kumudu/ kujifanyia mambo yake kwa sababu ya upafu. 1x2=2
Join our whatsapp group for latest updates

Download Kiswahili Paper 3 Questions and Answers - Kakamega Evaluation Mock Exams 2022.


Tap Here to Download for 50/-




Why download?

  • ✔ To read offline at any time.
  • ✔ To Print at your convenience
  • ✔ Share Easily with Friends / Students


Get on WhatsApp Download as PDF
.
Subscribe now

access all the content at an affordable rate
or
Buy any individual paper or notes as a pdf via MPESA
and get it sent to you via WhatsApp

 

What does our community say about us?