Kiswahili Karatasi ya 2 - 2020 MOKASA JOINT MOCKS EXAMINATION (QUESTIONS AND ANSWERS)

Share via Whatsapp
 1.  Ufahamu (Alama 15)

  Uchumi ni mfumo wa mapato, na matumizi ya watu katika nchi fulani. Uchumi huu huhusisha sekta mbalimbali kama vile utalii, kilimo, sanaa miongoni mwa sekta nyingme muhimu. Ukuaji wa kiuchumi hutegemea mambo kadhaa ili kuzaa matunda. Katika nchi zote ulimwenguni, sera za kisiasa. huamua jinsi uchumi utakavyokua na kunawiri. Kama siasa hazitili maanani sera za ukuaji wa kiuchuini, basi mapato ya nchi hiyo hugubikwa katika wingu kubwa la uchochole.

  Nchini Kenya, kwa mfano, kuna ulinganifu mkubwa kati ya siasa na ukuaji wa kuichumi. Ukuaji wa kiuchumi hutegemea uteuzi wa maafisa wanaosimamia asasi muhimu sana katika usimamizi wa uchumi. Asasi hizi ni kama vile wizara ya fedha, Wizara ya Mipango ya kitaifa na Ruwaza ya 2030, Mamlaka ya Ukusanyaji wa ushuru ( KRA), Benki kuu ya Kenya (CBK). na tume ya kupambana na ufisadi (KACC). Usimamizi wa asasi hizi huwa muhimu sana katika kuamua hatima ya uchumi wa nchi hii.

  Katika mwezi wa Juni kila mwaka, Waziri wa fedha husoma bajeti kwa Wabunge. Katika maelezo yake yaitwayo nakisi ya bajeti hujitokeza. Kabla ya bajeti kuandaliwa Wizara ya Mipango huandaa hati iitwayo Usoroveya wa kiuchurni. Baada ya kusomwa kwa bajeti ni jukumu la Wabunge kupitisha mswada wa kifedha unaohusisha wizara zote au kuutupilla mbali. Jukumu hili linafaa kutekelezwa kufikia tarehe 31 Oktoba ya kila mwaka kulingana na sheria.

  Wakati huo huo, afisa anayejulikana kama Mhasibu Mkuu wa serikali huwa na jukumu la kuchunguza na kutathmini matumizi ya fedha ya Wizara mbalimbali na kutoa ripoti yake kwa kamati ya Uhasibu wa Umma bungeni (PAC). Kamati hii hutoa mapendekezo yake kwa mkuu wa sheria na pia kwa Tume ya kupambana na ufisadi ili haki iweze kutekelezwa mahakamani iwapo dosari za kifedha zimefanyika.

  Benki kuu ya Kenya kupitia kwa Gavana wake huwa na jukumu la kutoa ushauri kwa serikali kuhusu usimamizi wa kifedha, kuchunguza nguvu za shillingi ya Kenya dhidi ya sarafu za kigeni, kutoa sarafu za Kenya kwa umma. na usimamizi wa benki zote nchini miongoni mwa majukumu mengine.

  Kwa upande mwingine, mamlaka ya Ukusanyaji ushuru nchini huwa na jukumu la kuhakikisha kuwa malengo ya ushuru yamefikiwa na pia kuhakikisha kuwa hakuna mtu binafsi au kampuni yoyote inayokwepa kulipa ushuru.

  Iwapo kuna udanganyifu wowote, basi swala hili linafaa kuangaliwa na mahakama zetu na haki kutekelezwa.

  Kwa ujumla, sisi kama wananchi tunafaa kusaidia asasi hizi zote kufikia malengo yake ili tupate ukuaji wa kiuchumi utakaofaidi watu wote. Jambo hili litahakikisha kuwa pengo lililo kati ya walalahai na walalahoi limezibwa. Sisi kama wananchi, tunafaa kuonyesha uzalendo wetu kwa nchi yetu kwa kulipa ushuru inavyotakikana, tukifuata mwito kuwa KULIPA USHURU NI KUJITEGEMEA. Mwisho, tusaidie viongozi wetu katika kuendeleza sera mwafaka za kiuchumi ili nchi yetu ipige hatua kubwa katika ukuaji wa kiuchumi. Iwapo afisa yeyote atatuhumiwa kushiriki katika kashfa yoyote ya kuhujumu nidhamu ya kifedha basi anafaa kukabiliwa vilivyo kisheria bila kujali hadhi yake ya kijamii au kisiasa.

  Maswali
  1. Ipe habari hii kichwa mwafaka (alama 1)
  2. Ukuaji wa kiuchumi nchini Kenya hutegemea nini? (alama 2)
  3. Benki kuu ya Kenya ina majukumu yepi? (alama 4)
  4. Mhasibu mkuu ana dhima ipi serikalini? (alama 2)
  5. Pendekeza hatua tatu za kufufua uchumi kulingana na taarifa (alama 3)
  6. Ni vipi Wakenya wanaweza kuonyesha uzalendo? (alama 1)
  7. Eleza maneno yafuatayo kama yalivyotumika katika ufahamu (alama 2)
   1. hatima
   2. wahalahai
 2. UFUPISHO (alama 15)

  Soma kifungu kifuatacho kisha ujibu maswali

  Inaaminika kuwa majeruhi wengi katika mikasa ya ajali huaga au kuathirika vibaya zaidi kutokana na hali mbaya ya uokoaji. Watu wengi ambao hujitolea kutoa majeruhi baada ya ajali kama za barabarani, maporomoko ya ardhi au nyumba huwa hawang’amui hata chembe jinsi ya kukabiliana na uokoaji. Hatima ya juhudi zao ambazo hulenga kutenda mema ni kuathirika zaidi kwa majeruhi.

  Hali ya uokoaji inaweza kurekebishwa kwa kutoa elimu ya huduma ya kwanza kwa umma. Elimu hii yahitajika na kila Mkenya kwani mikasa ya ajali za barabarani na nyinginezo inaendelea kutokea kila siku.

  Ajali zinapotokea si ajabu kuona makundi ya waokoaji wakibeba majeruhi hobelahobela bila kuzingatia madhara wanayoweza kuwaongezea kutokana na ubebaji wao. Kutojua namna ya kumbeba majeruhi kunaweza kumbabatisha na hata kusababisha kifo.

  Kuna mambo mbalimbali ambayo makundi ya waokoaji yanatakiwa kuzingatia wakati yanatoa huduma ya kuokoa. Kwanza ni muhimu kuchunguza kama kuna hatari yoyote inayoweza ikatokea na kuwatia majeruhi na waokoaji hatarini zaidi. Makundi ya waokoaji yameweza kwa kuliingilia eneo la ajali mbumbumbu kama mzungu wa reli.

  Hatua ya pili ni kutafuta idadi ya majeruhi. Pana uwezekano wa majeruhi kutupwa mbali na eneo la ajali.Vivyo hivyo, kuna majeruhi ambao huweweseka baada ya ajali na kuanza kutembea wasijue wanakoelea. Wengi wao huanguka karibu na eneo la ajali au wakaenda mbali.

  Hatua ya tatu ni kuchunguza kama majeruhi amezimia, moyo unapiga na jinsi anavyopumua. Ili kuhakikisha kuwa majeruhi anapumua, mwokoaji atazame kama kifua kinapanda na kushuka. Hali kadhalika, mwokoaji anaweza kusikiliza au kuguza kifua na kuona kama kuna ishara za kupumua. Iwapo majeruhi anapumua, muokoaji amweke katika hali ambayo itaimarisha kupumua kwake. Anaweza akamlaza chali au kumgeuza kwa pamoja na kichwa chake ili kufungua mkondo wa hewa. Pia mwokoaji ahakikishe hamna chochote kinywani kinachoweza kumsakama. Ikiwa hapumui, mwokoaji anaweza kujaribu kumfanya apumue kwa kupuliza hewa mdomoni mwake.

  Fauka ya hayo, upulizaji wa hewa utahakikisha kuwa damu inazunguka mwilini vizuri.

  Hatua nyingine ni kuchunguza vile amejeruhiwa. Chunguza kama majeraha ni vidonda tu au kuna kuvunjika kwa mfupa na kubainisha ni mfupa upi. Haya yatamwezesha mwokoaji kujua jinsi ya kumbeba majeruhi. Pakiwa na kuvunjika kwa mfupa, ni muhimu kutotumia kiungo kilichovunjika anapobebwa.

  Pia kuchunguza vile majeruhi amejeruhiwa, humwezesha mwokoaji kujua huduma ya dharura atakayoitumia. Majeruhi akiwa anavuja damu sana, ni muhimu kuzuia uvujaji huu. Iwapo ni kidonda kidogo, kinahitaji kufungwa ili kuzuia uambukizaji. Mwokoaji anaweza kutumia kifaa chochote kilicho karibu kutolea huduma hizi. Kwa mfano, anaweza kupasua nguo ya majeruhi ili apate kitambaa cha kusaidia kuzuia kuvuja kwa damu au kumfunga kidonda.

  Hatua inayofuata ni kumhamisha majeruhi toka eneo la ajali hadi hospitalini. Mwokoaji anaweza kuwatumia watu wengine kutafuta msaada. Wanaweza kupiga simu wakitumia nambari za simu za dharura kama zile za polisi, wazimamoto au makundi ya wataalamu wa shughuli za uokoaji. Nambari hii ya simu huwa 999 popote na huwa haina malipo. Wanaopiga simu ni vyema kutoa maelezo ya mahali ambapo ajali imetokea, ama ya ajali na huduma za dharura zinazohitajika.

  Ikiwa makundi ya wataalamu wa uokoaji hayakupatikana, ni jukumu la mwokoaji kuhakikisha majeruhi wamehamishwa na kupelekwa hospitalini. Majeruhi wakiwa wengi ni bora kuanza na wale waliozimia au wenye matatizo ya kupumua kisha kuwaendea wanaovuja damu sana. Baadaye mwokoaji awasaidie waliovunjika mifupa huku akimalizia na wenye majeraha yasiyohatarisha maisha. Ni muhimu kuwabeba majeruhi kwa kutumia machela. Hii hupunguza kuathirika zaidi kwa majeruhi. Iwapo hamna machela karibu, mwokoaji anaweza kuunda moja kwa kutumia vipande viwili vya mbao, blanketi shuka au makoti.

  Ujuzi wa huduma ya kwanza ni mojawapo ya mambo muhimu ambayo kila mtu anapaswa kuwa nayo.

  MASWALI
  1. Fupisha aya tatu za kwanza kwa maneno 50 tu. (Alama 5, utiririko 1)

   Matayarisho
   ........................

   Nakala safi
   .......................
  2. Eleza kwa kutumia maneno 90-100, hatua zinazotakiwa kufuatwa wakati wa uokoaji. (Alama 10, utiririko 1)

   Matayarisho

   Nakala safi

 3. Matumizi ya Lugha (alama 40)
  1. Huku ukizingatia jinsi hewa inavyozuiliwa, ainisha sauti zifuatazo: (alama 2)
   1. /y/ ......
   2. /sh/......
   3. /h/........
   4. /ny/.......
  2. Andika neno lenye muundo ufuatao. (alama 2)
   1. irabu, irabu, irabu ...........
   2. irabu, konsonanti, konsonanti, konsonanti, irabu .......
  3. Ainisha mofimu katika maneno yafuatayo: (alama 2)
   1. mwanao.........
   2. azingatiaye..........
  4. Onyesha aina za vielezi katika sentensi zifuatazo: (alama 2)
   1. Barabara ndefu zaidi ilisakafiwa barabara........
   2. Kiplagat alianza kula alipoambiwa asishike chakula hivi hivi........
  5. Andika sentensi ifuatayo kwa ukubwa. (alama 2)

   Mwanamke huyu alibeba ndoo hizi hadi sokoni......
  6. f) Tunga sentensi yenye muundo ufuatao. (alama 2)

   KN(RH + RH) + KT(t + V)
  7. Tunga sentensi ukitumia neno alikuwa kama:
   1. kitenzi kishirikishi kikamilifu (alama 1)
   2. kitenzi kisaidizi (alama 1)
  8. Andika sentensi ifuatayo katika usemi wa taarifa: (alama 3)

   Mwanasiasa alisema, “ Mkinipigia kura nitawajengea zahanati kabla mwisho wa mwaka huu.”
  9. Nomino zifuatazo ziko katika ngeli gani? (alama 1)
   1. ufizi ...........
   2. firigisi ...........
  10. Andika sentensi ifuatayo katika wakati ujao hali timilifu. (alama 1)

   Waziri anasoma hotuba yake.
  11. Andika sentensi ifuatayo katika hali kanushi: (alama 1)

   Nzige wengi walikuwa wanavamia maeneo hayo kabla ya serikali kuchukua hatua.
  12. Bainisha kiima na yambwa katika sentensi ifuatayo. (alama 3)
   Mama alimpikia mgeni wetu nyama ya kuku.
  13. Ainisha vishazi katika sentensi ifuatayo. (alama 3)

   Mwalimu aliyetuzwa jana alifundisha shairi lililotungwa na Kezilahabi.
  14. Tunga sentensi moja kutofautisha maana ya daka na taka. (alama 2)
  15. Tunga sentensi mbili kuonyesha matumizi mawili ya kiambishi ka. (alama 2)
  16. Changanua sentensi ifuatayo kwa njia ya mistari. (alama 4)

   Genge la wezi lilituvamia.
  17. Bainisha virai katika sentensi ifuatayo. (alama 3)
   Pikipiki iliyonunuliwa jana iliharibika karibu na mto.
  18. Eleza majukumu ya sentensi ifuatayo: (alama 1)

   Nipe kalamu yangu mara moja!
  19. Andika sentensi ifuatayo upya kwa kubadilisha maneno yaliyopigiwa mstari katika kauli zilizo mabanoni. (alama 2)

   Kazi hii imekuwa (tendea) ngumu sana lakini siwezi kufa (tendeshwa) moyo.
  20. Taja methali inayoafiki maelezo yafuatayo: (alama 1)

   Mtu anayetegemewa katika jamii akiondoka wanaomtegemea huwa mashakani.

 4. ISIMU JAMII (alama 10)

  ‘’Mwenye sikio amesikia. Usiwe kama mimi. Wapurukushe wote wakupotoshao. Fuata ruwaza ya wanaokujali. Kwangu nimejishika sikio baada ya laiti nyingi. Macho yamefumbuka. Usiseme nitazeekea huku. Lengo langu ni kuwahi uzamili na hata uzamifu. Kwani kuitwa profesa ni kosa? Niwafae wengine kimasomaso na kihali’’

  1. Taja na kuthibitisha sajili ya mazungumzo haya. (alama 2)
  2. Tambua mazingira ambamo mazungumzo haya yanatokea. (alama 1)
  3. Eleza sifa zozote saba za lugha zilizotumika kwenye mazungumzo haya. (alama 7)


MWONGOZO WA KUSAHIHISHA 102/2

UFAHAMU

 1. Kuimarisha uchumi                                                                                   (alama 1)
 2. Hutegemea sera za kisiasa hasa katika uteuzi wa maarifa wanaosimamia asasi muhimu sana nchini.
  1. Kutoa ushauri kwa serikali kuhusu usimamizi wa fedha.
  2. Kuchunguza nguvu ya shilingi ya Kenya dhidi ya sarafu za kigeni.
  3. Kutoa sarafu za Kenya kwa umma.
  4. Usimamizi wa benki zote nchini.    (alama 4)
 3.  
  1. Kuchunguza matumizi ya fedha.
  2. Kutathmini matumizi ya fedha ya wizara mbalimbali.
  3. Kutoa ripoti yake kamati ya uhasibu wa umma bungeni.                (alama 2)
 4.  
  1. Kuhakikisha ushuru umelipwa.
  2. Kuziba pengo baina ya walalahai na walalahoi.
  3. Kusaidia viongozi wetu kuendeleza sera mwafaka za kiuchumi.    (alama 3)
 5. Ni vipi Wakenya wanaweza kuonyesha uzalendo?
  Kulipa ushuru inavyotakikana.       (alama 1)
 6.  
  1. Hatima – mwisho/tamati
  2. walalahai-  matajiri/ wenye uwezo mkubwa    (alama 2)

UFUPISHO

 1. Fupisha aya tatu za kwanza kwa maneno 50 tu. (Alama 5, utiririko 1)
  1. Majeruhi wengi katika mikasa ya ajali huaga au kuathirika vibaya zaidi kutokana na hali mbaya ya uokoaji.
  2. Watu wengi hawang’amui hata chembe jinsi ya kukabiliana na uokoaji.
  3. Hali ya uokoaji inaweza kurekebishwa kwa kutoa elimu ya huduma ya kwanza kwa umma.
  4. Kutojua namna ya kumbeba majeruhi kunaweza kumhatarisha na hata kusababisha kifo.
 2.  Eleza kwa kutumia maneno 90-100, hatua zinazotakiwa kufuatwa wakati wa uokoaji (Alama 10, utiririko 1)
  1. Kwanza ni muhimu kuchunguza kama kuna hatari yoyote inayoweza ikatokea na kuwatia majeruhi na waokoaji hatarini zaidi.
  2. Hatua ya pili ni kutafuta idadi ya majeruhi.
  3. Hatua ya tatu ni kuchunguza kama majeruhi amezimia , moyo unapiga jinsi anavyopumua.
  4. Iwapo majeruhi anapumua, mwokoaji amweke katika hali ambayo itaimarisha kupumua kwake.
  5. Ikiwa hapumui, mwokoaji anaweza kujaribu kumfanya apumue kwa kupuliza hewa mdomoni mwake.
  6. Hatua nyingine ni kuchunguza vile amejeruhiwa – kama majeraha ni vidonda tu au kuna kuvunjika kwa mfupa na kubainisha ni mfupa upi.
  7. Hatua inayofuata ni kumhamisha majeruhi kutoka eneo la ajali hadi hospitalini.
  8. Ni jukumu la mwokoaji kuhakikisha majeruhi wamehamishwa na kupelekwa hospitalini.
  9. Ni bora kuanza na majeruhi waliozimia au wenye matatizo ya kupumua kisha kuwaendea wanaovuja damu sana.
  10. Ujuzi wa huduma ya kwanza ni muhimu kwa kila mtu.

MATUMIZI YA LUGHA

 1. /y/ kiyeyusho                                                              ½ alama
  /sh/ kikwamizo                                                           ½ alama
  /h/ kikwamizo                                                             ½ alama
  /ny/ king’ong’o                                                            ½ alama
 2.  
  1. irabu, irabu, irabu       mf aoa, aua, aue                         alama 1
  2. irabu, konsonanti, konsonanti, konsonanti, irabu mf ombwe, imbwa, umbwa    alama 1
 3.  
  1. Mwanao
   Mw- ngeli
   an – mzizi
   o – umiliki         1/0

  2. azingatiaye
   a- nafsi ya tatu umoja
   zingati – mzizi
   a- kauli tenda
   ye – kirejeshi    1/0
 4.  
  1. Barabara
   zaidi – namna hali
   Barabara – namna hali  alama 1
  2. kifisi – namna mfanano
   hivi hivi – namna vikariri  alama 1
 5.  Janajike hili lilibeba madoo haya hadi sokoni.     2/0
  Mf. Mtoto wa mama ni mrefu.
 6. KN (N + RH) + KT( t + V)
  Mf. Mtoto wa mama ni mrefu. 2/0
 7.  
  1. Kitenzi kishirikishi kikamilifu

   Mama alikuwa analala alama 1
  2. Kitenzi kisaidizi
   Mtoto alikuwa analala sebuleni. alama 1
 8. Mwanasiasa alisema kuwa iwapo wangempigia kura angewajengea zahanati kabla mwisho wa mwaka huo.    ½ x 6 = 3
 9. ufizi       U – ZI      ½
  firigisi - I – ZI    ½
 10. Waziri atakuwa amesoma hotuba. alama 1
 11. Nzige wengi hawakuwa wanavamia maeneo hayo kabala serikali kuchukua hatua.  1/0
 12. Kiima – mama
  Mgeni wetu – yambwa tendewa
  Nyama ya kuku – yambwa tendwa   3 x 1
 13. Mwalimu aliyetuzwa jana - kishazi tegemezi     ½ alama
  Alifundisha shairi                   - kishazi huru    alama 1
  Lilotungwa na Kezilahabi   -   kishazi tegemezi    ½ alama
 14. Tathmini jawabu la mwanafunzi
  Daka – shika/kamata
  Taka – uchafu, kusudia/penda   (alama 2)
 15. Ka –amri km. Kaeni chini! Kamwambie aje
  Ka – kitendo kitafanyika wakati ujao, km. Atakayesoma, watakaoshiriki
  Ka – wakati usiodhihirika, km. Waziri kajiuzulu     (alama 2)
 16. Genge la wezi lilituvamia
  S ----     KN + KT
  KN ---- N + KH/KV
  N   ----- Genge
  KH----- H +N /KV ---V + N
  H/V ----   la
  N ----   wezi
  KT -----T
  T -------lilituvamia    ½ X 8 = 4
 17. RN – pikipiki iliyonunuliwa jana
  RT – iliharibika karibu na mto
  RH – karibu na mto   alama 3
 18. Amri     alama 1
 19. Kazi hii imeniwia ngumu sana lakini siwezi kufishwa moyo.   alama 2
 20. Mti mkuu ukigwa wana wa ndege huyumba.   alama 1

ISIMUJAMII

 1. Taja na kuthibitisha sajili ya mazungumzo haya. (alama 2)
  Sajili ya mawaidha/ushauri/ wosia/ nasaha
  Mzungumzaji anamtolea msikilizaji nasaha asifuate mkondo mbaya wa maisha aliyofuata.
 2. Tambua mazingira ambamo mazungumzo haya yanatokea.   (alama 1)
  Shuleni/chuoni/taasisi ya elimu – anaiotoa nasaha hii kwa wenzake akiwa chuoni kwa sababu anasema wasidhani atazeeka huko, lengo ni kupata shahada.
 3. Eleza sifa zozote saba za lugha iliyotumika kwenye mazungumzo haya.   (alama 7)
  1. Lugha iliyojaa matumini-anawania kupata uzamili na uzamifu
  2. Utohozi-profesa-professor
  3. Swali balagha-kwani kuitwa professor ni kosa.
  4. Lugha ya kuonya-mwenye sikio amesikia
  5. Nahau-nimejishika sikio-nimejirekebisha
  6. Lugha sanifu-Kifungu kizima kimetumia lugha ipasavyo
  7. Lugha ya maelezo- wapurukushe wote wakupotoshao fuata ruwaza ya wanaokujali
  8. Msemi-macho yamefumbika-amezinduka
  9. Matumizi ya msamiati wa taaluma ya kiusomi-uzamili,uzamifu na profesa
  10. Matumizi ya sentensi fupi fupi-Usiwe kama mimi.
  11. Lugha inayotumia taswira-anapotolea nasaha anasema usiwe kama mimi picha ya pengine jinsi alivyoathirika anajitokeza akilini.
  12. Lugha imejaa hekima-anasema fuata ruwaza ya wanaokujali(Ushauri anatoa unaongozwa na busara kwa yule hataki msikilizaji ahasirike)
Join our whatsapp group for latest updates

Download Kiswahili Karatasi ya 2 - 2020 MOKASA JOINT MOCKS EXAMINATION (QUESTIONS AND ANSWERS).


Tap Here to Download for 50/-
Why download?

 • ✔ To read offline at any time.
 • ✔ To Print at your convenience
 • ✔ Share Easily with Friends / Students


Get on WhatsApp Download as PDF
.
Subscribe now

access all the content at an affordable rate
or
Buy any individual paper or notes as a pdf via MPESA
and get it sent to you via WhatsApp

 

What does our community say about us?

Join our community on:

 • easyelimu app
 • Telegram
 • facebook page
 • twitter page
 • Pinterest